Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
- Thread starter
- #301
181
Kwa aibu nilianza kufuta mikono yangu iliyochafuka, tukaondoka na kuendelea na safari yetu ya kwenda nyumbani. Safari ilikuwa ya kimya kimya, hakuna aliyemsemesha mwenzake…
Tulipofika nyumbani Zainabu alinitazama machoni huku akionekana kuzuia machozi. Kabla sijamuuliza kulikoni akanikumbatia kwa nguvu na kuanza kunipiga mabusu uso mzima, mihemuko ya mwili wangu ilikuwa karibu kabisa na hisia zangu hivyo nilianza kulipiza mashambulizi, lakini kila nilipokuwa nikimshika Zainabu kuna picha ya msichana mwingine ilikuwa ikinijia. Msichana huyo alikuwa ni yule niliyemwona ndotoni.
Wakati tukiendelea kukumbatiana na kubusiana Zainabu akaniongoza hadi chumbani na kisha kazi ikaanza pale. Nilishangaa sana kwani siku hiyo Zainabu alikuwa mtundu sana kitandani, lakini kila alipojitahidi kunifanyia mambo fulani taswira ya yule msichana wa ndotoni ilikuwa inanijia.
Tuliendelea kusumbuana na kuchokozana hisia zetu na mwishowe tulikutanisha maungo yetu ya uzazi, nilipokuwa katikati ya mchezo wakati Zainabu akiwa juu kuongoza jahazi sura ya yule msichana ilijaa akilini kwangu na kunifanya nishtuke mno.
“Rehema!” nilijikuta nikilitamka jina hilo ambalo sikujua nililitoa wapi, na papo hapo Zainabu akaacha na kunitazama kwa mshangao mkubwa.
“Rehema kafanyaje?” Zainabu aliniuliza kwa mshangao huku akizidi kunikazia macho. Sikumjibu kwa kuwa sikujua namna ya kuelezea.
“Rehema ni nani?” Zainabu aliniuliza huku akinyanyuka vile vile akiwa uchi na kusimama kando, alinitazama kwa namna ambayo sikuweza kupata tafsiri ya haraka. Alikuwa amehuzunika sana.
Nilijivuta pale kitandani na kusimama, nikamsogelea na kutaka kumshika lakini hakuwa tayari kushikwa. Nilibaki nimetumbua macho na yeye hakuwa anaongea zaidi ya kunitazama huku machozi yakimlengalenga.
“Mgeni!” Zainabu aliniita huku akiketi kitandani. Niliitika huku nami nikiketi kitandani kando yake. Zainabu akanitazama kwa muda kisha akayahamisha macho yake na kutazama mbele huku akishusha pumzi, halafu akaongea bila hata kunitazama, “Naogopa sana… sitaki utoke mikononi mwangu.”
Sikusema kitu. Nilibaki kimya kana kwamba sikuwa nimemsikia.
“Umenisikia, Mgeni?” Zainabu aliniuliza huku akigeuza shingo yake kunitazama usoni.
“Nakusikia, Zai,” nilisema kwa sauti tulivu huku nami nikimtazama usoni.
“Niahidi kwamba hautaniacha,” Zainabu alinisihi huku akiendelea kunitazama usoni.
Kidogo nikawa kimya, nilizidi kushangazwa na kauli ya Zainabu. Sikujua alikuwa na nini na kwa nini alitaka nimhakikishie kwamba sitomwacha! Kwani alikuwa ameona nini? Nilibaki nikijiuliza pasipo kupata majibu. Alipoona nipo kimya akanitazama moja kwa moja machoni.
“Mgeni!” Zainabu aliniita tena.
“Zainabu, unajua mazingira yangu yalivyo, sikumbuki chochote na wala siwezi kutabiri kesho yangu,” nilimweleza huku nikimtazama usoni, nikamwona akivunjika kihisia.
“Sijui kwa nini unanisisitiza kuwa nisikuache, kwani umeona nini kwangu kinachoashiria kwamba nataka kukuacha?” nilimsaili Zainabu.
“Nataka tu kujua msimamo wako, nina wasiwasi endapo utarudiwa na kumbukumbu zako unaweza kuniacha,” Zainabu alisema kwa huzuni.
“Siwezi kujua lakini si kama hivyo unavyoweza kudhani,” nilisema na kuongeza, “ila nakuahidi siwezi kwenda mbali na wewe.”
“Unajua ukiniacha ulimwengu utakuwa tofauti kabisa! Ulimwengu utakuwa mkatili sana kwangu kupita kiasi. Sitaweza kuvumilia maisha haya bila wewe… tafadhali usiniache, Mgeni,” Zainabu alisema huku machozi yakizidi kumlengalenga. Kisha alinishika mkono wangu wa kuume kwa nguvu.
Nilishangazwa sana na hali ile, nikamfuta machozi na kumwahidi ningekuwa naye mpaka mwisho kwa kuwa nilikuwa nampenda sana, na sikupenda kumwona akigubikwa na huzuni. Nilimwambia ningefanya kila jambo lililo ndani ya uwezo wangu kuhakikisha anayafurahia maisha, na kwa nguvu zangu zote ningemwadabisha yeyote yule ambaye angemgusa au kumuumiza.
Hata hivyo nilimwona Zainabu akinitazama tu kama ambaye hakuwa akiyaamini yote niliyomwambia.
“Nakuahidi hilo kwa moyo wangu wote, Zai,” nilisisitiza kisha nikambusu kwenye paji la uso.
* * *
Saa 5:30 usiku…
“Una tatizo lolote, Zai? Naona leo kama hauko sawa kabisa!” nilimuuliza Zainabu baada ya kumwona hayuko sawa. Muda mwingi alikuwa mkimya akiwa anafikiria sana.
Muda huo tulikuwa kitandani. Zainabu alikuwa amenilalia kifuani akionekana mwenye mawazo mengi, lakini nilipomuuliza alinyanyuka na kuketi. Hii ilikuwa siku ile ile ambayo mchana wake nilijikuta nikiropoka jina la Rehema.
“Hapana, niko sawa,” Zainabu alinijibu huku akiachia tabasamu kama njia ya kunionesha kuwa yuko sawa. Hata hivyo nilijua kuwa tabasamu lile halikuwa halisi, lilikuwa limeficha huzuni ndani yake.
“Unakumbuka nimekuuliza maswali mangapi?” nilimuuliza huku nikimtazama usoni bila kupepesa macho yangu. Alionekana kuwaza kwa muda na kujibu japo nilimwona akiwa hana uhakika wa jibu.
“Mawili…” alinijibu na hapo akatazama kando kwa muda kisha aliyarudisha macho yake kwangu na kushusha pumzi za ndani kwa ndani na kuniuliza, “Rehema ni nani?”
“Hata simjui, nilijikuta nimeropoka tu,” nilimwambia Zainabu nikiwa nimeshtuka kidogo ingawa nilijitahidi kuumeza mshtuko wangu. Sikujua kumbe Zainabu alikuwa bado ana kinyongo!
Ukweli sikujua jina hilo nililitoa wapi, kwani lilinijia tu wakati tupo mchezoni baada ya sura ya msichana wa ndotoni kunijia akilini.
“Yaani uropoke tu jina la mwanamke pasipo sababu? Sijawahi kuona!” Zainabu alihoji huku akinikazia macho.
Nilihisi kuwa hata ningejielezaje bado nisingeeleweka, nikaanza kumshikashika Zainabu na kumbusu kila sehemu huku mikono yangu nikiipitisha kwenye ikulu yake. Zainabu aliusukuma mkono wangu na kujiondoa toka mikononi mwangu huku akiniambia kuwa hakuwa na hamu ya kufanya chochote. Nikamwacha.
“Najua hata nijieleze vipi huwezi kunielewa, naomba tu huniamini, mpenzi… hakyamungu simjui mwanamke yeyote mwenye jina hilo, lilinitoka tu,” nilijitetea huku nikihisi hatia imenikaba kooni. Zainabu aliendelea kubaki kimya kabisa akinikazia macho.
“Please…” nilimsihi Zainabu, na bila kujua machozi yalianza kunidondoka. Nikamwona Zainabu akiingiwa na huruma.
“Nimekuelewa,” Zainabu alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani. Kisha aliniita jina langu kikamilifu, “Mgeni Mwema!”
“Naam!” nilijikakamua kuitika.
“Naomba nikwambie kitu… kwangu wewe ni mwanaume wa kipekee…” alisema na taratibu akaanza kurudi katika hali yake ya kawaida ya ucheshi. “Sasa nimefikia uamuzi… nahitaji nikuzalie mtoto!”
Sikusema chochote. Nilibaki kimya nikimtumbulia macho. Zainabu akaniomba nisimame kisha akaniambia nimsogelee, nikamsogelea na kumkumbatia.
“Mgeni, umekuwa nguzo kuu katika maisha yangu kuliko mtu yeyote maishani mwangu, umekuwa nuru mpya katika njia yangu. Na zaidi umekuwa mwanaume bora kati ya wanaume wote ninaowajua…” alisema kisha akasita kidogo na kunitazama usoni. Sikuwa na cha kusema zaidi ya kujibu, “ahsante”.
“Lakini kuna muda najikuta najuta kwa nini nimekufahamu, kwa nini umekuja katika maisha yangu,” Zainabu alisema na kushusha pumzi ndefu.
“Kwa nini unasema hivyo?” nilimuuliza huku nikimtazama usoni kwa umakini.
“Hata sijui lakini ukweli nitajiona mpweke sana siku utakapoamua kuniacha,” Zainabu alisema kwa huzuni.
“Mbona leo unaongea sana kuhusu kuachwa, kwani kuna nini umekiona kwangu?” nilimuuliza Zainabu kwa mshangao. Zainabu hakujibu, badala yake aliachia tabasamu lililobeba uchungu.
“Zai, naomba uniambie… una maana gani kusema hivyo? Huniamini?” nilimuuliza tena kwani maneno yake yalinichanganya kidogo.
“Hata sijui kama nakuamini au sikuamini, ila nimesukumwa tu kusema hivyo…” Zainabu alisema na kubetua mabega yake, “unajua ni vigumu kuwa wakili wa moyo wako.”
“Ninaweza kuwa nimekuelewa lakini huenda vile vile sijakuelewa! Kama shaka yako ni jina la Rehema ukweli hata simfahamu. Labda tu uniweke wazi una maana gani kama sivyo nifikiriavyo?" nilimuuliza Zainabu kwani maneno yake ya mafumbo yalizidi kuniweka njia panda.
Hakunijibu bali aliachia tabasamu na kunisogelea halafu akanikumbatia kwa nguvu na kuanza kunipa joto. Sikutaka kumhoji zaidi, nami nilimkumbatia. Muda huo Zainabu alikuwa anatetemeka kwa hisia kali za huba. Na muda mfupi baadaye tulijikuta tukimezwa na ulimwengu wa huba.
Ilikuwa kama tupo kwenye kisiwa cha maraha kilichoandaliwa maalumu kwa ajili yetu. Tukayasahau yote, tukajiona kama tuliozaliwa upya. Hatukuishiwa na hamu hadi tulipohisi kuchoka tukiwa hoi bin taabani, ndipo tukalala.
Haikuchukua muda nikamsikia Zainabu akikoroma taratibu. Lakini kwangu haikuwa hivyo, sikuupata usingizi na mawazo yangu yalikuwa juu ya Rehema. Nilijiuliza huyu Rehema ni nani? Kwa nini anijie akilini wakati nilikuwa simjui? Je, ni yule msichana wa kwenye ndoto?
Sasa mawazo juu ya Rehema yaliendelea kupita kichwani kwangu na kuninyima usingizi huku yakiufanya usiku kuwa mrefu sana kwangu. Niliishia kugaagaa tu pale kitandani.
* * *
Endelea kufuatilia...