Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
- Thread starter
- #441
223
Najua unanisikia…
NILISHTUSHWA toka usingizini na kelele za kitasa cha mlango wa kile chumba kiliponyongwa kwa papara na kisha mlango kusukumwa kwa ndani. Nilikuwa nimepitiwa na usingizi ulionifanya niyasahau yale mateso kwa muda. Niligeuka kutazama kule mlangoni na hapo nikawaona wanaume wanne wakiingia kibabe mle ndani wakiongozwa na yule daktari.
Niliwatambua wale wanaume kuwa ni Meja Saleh bin Awadh, komando mweusi, komando Mwarabu na yule komando Mpalestina.
“Waambie tu ukweli, leo wamepanga kukuua,” yule daktari alininong’oneza sikioni kwa huruma baada ya kunifikia. Taarifa ile ilinifanya niihisi hofu ya kifo ikinitambaa mwilini.
Watu wale hawakunisemesha badala yake walikizunguka haraka kitanda kisha komando mweusi alichomoa sindano za dripu katika mishipa yangu mkononi pasipo kuzingatia utaalamu wa kidaktari na hivyo kunisababishia maumivu makali, hata hivyo yule mtu hakuonekana kujali. Halafu walinishika miguu yangu na kunishusha toka pale kitandani kwa nguvu, nikaanguka kisha wakaniburuta kibabe kuelekea nje ya kile chumba.
Tulipofika nje ya chumba tukaanza kukatisha ukumbi mrefu hadi mwisho kabisa, tukakata kushoto kisha tukaanza kushuka ngazi hadi tulipofika chini tukaingia upande wa kulia. Safari yetu ikaishia sehemu yenye mlango wa chuma upande wa kushoto. Kisha komando Mwarabu akaufungua ule mlango wa chuma. Wakaniingiza humo.
Sikuweza kuona chochote mle ndani kwa vile kulikuwa na giza nene lakini baada ya muda mfupi taa za mle ndani ziliwashwa na hapo nikapata kuyaona vizuri mandhari yale. Kilikuwa chumba kile kile cha mateso. Koo langu likanikauka kwa hofu ya kifo.
Kisha Meja Saleh bin Awadh alinigeukia na kusema, “Nadhani unaelewa fika ni taarifa gani tunazihitaji toka kwako, leo hatutakubembeleza, tueleze ukweli vinginevyo utakufa kifo cha mateso makali.”
“Hata sielewi kwa nini mnaning’ang’aniza niwape majibu kwa kitu ambacho sikijui wala hamjanituma?” nilimwambia Meja Saleh bin Awadh kwa jeuri.
“Endeleeni na kazi,” Meja Saleh bin Awadh aliwaambia wale makomando. Bila kuchelewa makomando wawili walinikamata na kunifunga kamba miguuni na mikononi haraka haraka na baada ya hapo nilijikuta nikibebwa juu juu na kutundikwa kwenye vile vyuma vifupi vilivyokunjwa na kuchongwa mbele yake mfano wa vyuma vya kuning’inizia nyama buchani, nikaning’inia kichwa chini miguu juu.
Kisha yule komando Mpalestina alinisogelea na kunichapa kofi usoni halafu akanifokea huku nikiwa bado nimening’inizwa. “Kama hawa walikuchekea basi mimi sina utani. Hakuna aliyewahi kuingia humu akabaki na siri zake moyoni, hata wewe naamini utasema tu.”
Nilibaki kimya. Yule komando alinitazama kwa ghadhabu kali kisha akashusha pumzi zake na kutazama kando, akakunja sura yake huku akionekana kama aliyekuwa akitafakari jambo fulani. Mara nikamwona akipiga hatua na kwenda kuchukua kibubu chenye gesi kisha aliiwasha ile gesi na kuonekana akijaribu kurekebisha ule moto wa gesi. Baada ya kuweka moto fulani kwenye kile kibubu cha gesi, akanifuata na kuanza kunipitishia usoni bila kunidhuru, nia ilikuwa kunisikilizisha lile joto lililotoka mle kwenye kibubu.
“Nadhani umelisikia joto lake, nakupa sekunde tano tu utuambie vinginevyo joto hili litakwenda kwenye sehemu zako za siri,” yule komando aliongea huku akinitazama kwa hasira.
Nilibaki kimya kwa kuwa muda ule nilikuwa nahisi kizunguzungu kikali, sauti nyembamba mfano wa sauti itokayo kwenye filimbi ilikuwa inalia kwenye masikio yangu na giza zito lilianza kutanda kwenye mboni za macho yangu. Yule komando Mpalestina alinitazama kwa umakini na kusonya.
Bado nilibaki kimya. Hata hivyo niligundua kitu, niligundua kuwa wale jamaa hawakuwa na nia ya kuniua, huenda walitaka kunitumia kama mateka ili kupeleka madai yao sehemu ndiyo maana waliishia kunitisha tu au kunipa mateso waliyoamini kuwa ningeyamudu.
Wakati nikiwaza hayo nikamwona yule komando Mpalestina akiuzima ule moto wa gesi na kukiweka kando kile kibubu cha gesi. Nikiwa nashangaa nikamwona akichukuwa lile betri kubwa la gari lenye kufua umeme ambalo lilikuwa na vishikizo vilivyofungwa mwishoni. Akalisogeza karibu yangu na hapo nikamwona akiijaribu ile nguvu ya betri kwa kuzigusanisha zile nyaya mbili, zikapiga shoti kubwa na kutoa cheche. Akaonekana kufurahi sana.
“Nadhani hii ndo itakufaa zaidi… ila utanisamehe maana sikupenda tufikishane huku, ila kwa vile umetulazimisha kufanya hivi. Hata hivyo muda wa kujiokoa bado upo. Tuambie tunachotaka kusikia halafu tutakuacha,” yule komando Mpalestina aliniambia. Sikumjibu neno kwani hasira ilikuwa imenikaba kooni.
“Luteni, kama hataki kusema mpe dozi,” nilimsikia Meja Saleh bin Awadh akimwambia yule komando Mpalestina.
Na hapo nikajikuta nikianza kuchomwa na zile nyaya kila sehemu mwilini nikilazimishwa kuongea. Mateso yale yaliendelea kwa dakika mbili huku nikihisi maumivu makali mno mwilini, hata hivyo niliendelea kushikilia msimamo wangu wa kutowaeleza chochote. Hakuacha, akaendelea kunipa mateso yale na mengine zaidi kwa muda mrefu na walipoona sielekei kuwaambia chochote cha maana, Meja Saleh bin Awadh akamwambia yule Luteni aniache.
“Naona amedhamiria kufa kiume,” Meja Saleh bin Awadh alimwambia yule Luteni na muda huo huo nikamwona akinisogelea kisha akaanza kunishushia kipigo.
Kilikuwa kipigo hatari sana kwangu, japo tayari nilikuwa nimewiva kwenye mafunzo ya kujihami ya karate lakini sikuwahi kushuhudia kipigo cha aina ile ambapo mtu anapigwa akiwa amefungwa kwa kamba madhubuti na kuning’inizwa kichwa chini miguu juu. Baada ya kama dakika tano hivi nilikuwa nimechakaa vibaya huku uso wangu wote ukiwa umetapakaa kwa damu.
“Naamini sasa upo tayari kutwambia,” nilimsikia Meja Saleh bin Awadh akisema.
Bado niliendelea kushikilia msimamo wangu wa kutowaeleza chochote. Nilishakubali kufa pasipo kutoa siri. Hata hivyo nilipojaribu kufumbua macho yangu kumtazama Meja Saleh bin Awadh nikajikuta nikimwona kama kiumbe cha ajabu kisichoeleweka huku lile eneo nikiliona kama tufe fulani lililokuwa linazunguka angani.
Kisha nilianza kuona giza mbele yangu na kwa mbali niliisikia sauti ya Meja Saleh bin Awadh ikiniambia. “Twambie vinginevyo utakufa kifo kibaya sana.”
Nilijitahidi kukodoa macho yangu lakini nikawa naona giza mbele yangu, na hata nilipotaka kufumbua mdomo wangu ili nimjibu bado sikufanikiwa kwani fahamu zilikuwa mbioni kunitoka. Mwili wangu ulizidiwa na maumivu makali yasiyoelezeka na sasa nilitambua kuwa mwisho wangu ulikuwa umefika. Halafu sikuelewa nini kiliendelea.
* * *
Endelea...