232
Kwa mujibu wa cheo na wadhifa aliokuwa nao Tunu wakati huo ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa, hakuwa miongoni mwa watu wanaoweza kupigiwa simu na DGIS kwa sababu yoyote ile.
Chain of command ilimtenga na wakubwa wa Idara hata alipokuwa katika operesheni nyeti.
Mara zote wakuu wa operesheni hizo ndiyo waliokuwa na nafasi ya kuzungumza na wakurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa kwa niaba yetu wakati sisi tukiwa katika mapambano. Watu wa medani (
field), kama ilivyokuwa kwangu au kwa Tunu wakati huo, kumbukumbu zetu zilibaki katika mafaili na katika vichwa vya wale tulioshirikiana nao katika vita. Basi!
Kisha Tunu alinitaka nimfuate anitembeze kuyaona mazingira ya ofisi za Taasisi ya SPACE na namna kazi zinavyofanywa (
orientation), na kisha angeniruhusu niondoke nikaanze mapumziko yangu, na kwamba nilitakiwa kufikiria ni nchi gani ambayo ningependa kwenda kutembea kwani gharama zote zingelipwa na Idara ya Usalama wa Taifa.
Tuliinuka tukaelekea kwenye mlango mkubwa wa chuma ukiwa umepachikwa bandiko jeupe lililosomeka ‘SPACE’. Pembezoni mwa mlango huo kulikuwa na kifaa cha kuweka
nywila (
password) kabla hujaingia humo. Tunu akabofya hapo mara kadhaa na mara mlango ukafunguka. Tukazama ndani na kupokelewa na maofisa ambao walitukaribisha kwa bashasha.
Wakati Tunu akinitembeza ndani ya ofisi hizo niligundua kuwa kulikuwa na vitengo vikuu kadhaa vikiwemo vya
Accounting,
Surveillance,
Graphics,
Hacking na
Coding. Gloria Tesha ndiye alikuwa akiongoza kitengo cha
Surveillance na alishirikiana na maofisa wengine akiwemo Philip Bundala.
Kisha tuliingia kwenye ofisi za kitengo cha
Graphics, humo nilimkuta Juma Ndekule akikiongoza kitengo hicho, nikashuhudia maofisa mbalimbali wakiwa wamehemewa (
busy) na kazi. Sauti ya vibofyeo vya tarakilishi zao zilikuwa zinagonga gonga na kuacha. Muda wote Ndekule alikuwa mbele akikodolea kioo cha tarakilishi yake.
Halafu kwenye kitengo cha
Hacking alikuwepo Hawa Kiluvya akishirikiana na maofisa wengine watatu. Hata hivyo, Tunu alinikumbusha kuwa Taasisi ya SPACE ilikuwa ni sehemu ya Idara ya Usalama wa Taifa, na hivyo pamoja na kuwa ofisi ya kitengo kimoja ilikuwa kwenye jengo moja na kitengo kingine, maofisa wa vitengo hivyo hawakuruhusiwa kutembeleana ofisini bila ruhusa au sababu za msingi.
Endapo ofisa wa kitengo kimoja angelazimika kwenda katika ofisi ya kitengo kingine, yaani nje ya kituo chake cha kazi, kwa dharula au sababu nyingine yoyote angetakiwa kuomba kibali (
gate pass) cha kumruhusu kufanya hivyo. Ni utaratibu ule ule uitwao
compatimentation ambao uliisaidia Idara nzima ya Usalama wa Taifa kutunza siri, kuendesha operesheni zinazojitegemea, na kuwazuia maadui wa taifa kujipatia taarifa muhimu kwa urahisi (endapo wangepenyeza mtu wao ndani ya idara).
Huo ulikuwa utaratibu wa lazima wa Idara, kuweka kanuni na taratibu hizo ili kulinda nyaraka na siri za Idara, na pia kujenga nidhamu ya maofisa wake na kila ofisa alikuwa anajua kwamba muda wowote katika ajira yake angeweza kufuatiliwa nyendo zake kwa sababu mbalimbali, iwe kwa lengo la kuthibitishwa uwezo na umakini wake ili apandishwe cheo na kupewa madaraka makubwa, au kwa kutiliwa mashaka.
Baada ya kutembezwa kwenye vitengo vyote hatimaye tulirudi tena ofisini kwa Mkuu wa Taasisi ya SPACE, ambapo Tunu alinipatia maelezo muhimu ya kuzingatia niwapo kazini na hata nje ya kazi, kisha akaniomba nifikirie haraka ni wapi ambapo ningependa kwenda kwa mapumziko halafu nimwambie ili aandae utaratibu.
“Nadhani Mombasa patanifaa zaidi,” nilisema pasipo hata kuushirikisha ubongo wangu. Hata hivyo jambo moja lilikuwa wazi akilini mwangu, nilitamani sana kuwa na Leyla kwenye mapumziko yangu.
Tunu alinitazama kwa mshangao kwa kitambo, huenda alihisi kuwa hajanisikia vizuri. “Mombasa?” aliniuliza huku akinikazia macho yaliyojaa mshangao. “Kwa nini isiwe maeneo kama Dubai au hata…”
“Mombasa ndiyo sehemu pekee kwa sasa nadhani itanifaa ku
refresh my mind,” nilimkata kauli nikiongea kwa kujiamini, na hapo Tunu akabetua mdomo wake na kunyanyua juu mabega yake kwa kebehi.
“Mh! Si bure, kuna mtu tayari kishakulisha limbwata huko maana inaelekea akili yako yote ipo Mombasa,” Tunu aliongea huku akiuvuta mdomo wake. Sikujua kama alifanya vile kwa utani au alianza kusumbuliwa na wivu.
“Acha wivu, mkuu,” nilisema na kuangua kicheko hafifu na kumfanya Tunu aachie msonyo wa nguvu.
“Hata kama... hii ni dalili tosha kwamba umeshatekwa,” Tunu alisema huku naye akiangua kicheko hafifu.
“Si bora nitekwe na huyo wa Mombasa kuliko kutekwa na wale makomando wa kule Shamba,” nilisema kwa utani na kumfanya Tunu aangue kicheko kikubwa. Sasa tulijikuta tukizungumza kana kwamba ni washkaji tu waliokuwa kijiweni badala ya ofisa usalama na mkuu wake wa kazi.
“Yaelekea wale makomando wamekunyoosha kweli kweli!” Tunu alisema huku akiendelea kucheka.
“Dah, we acha tu,” nilisema huku nikishusha pumzi za ndani kwa ndani.
Baada ya maelezo machache Tunu aliniruhusu kuondoka ofisini hapo ili nikaendelee na shughuli zangu za kawaida wakati taratibu zingine za kiofisi zikifanywa. Niliinuka nikapiga saluti ya heshima kisha nikamuaga kwa kumpa mkono, halafu nikageuka na kutembea taratibu kuelekea chumba cha katibu muhtasi wake, mahali palipokuwa na mlango wa kutokea ukumbini.
Nikaingia katika ofisi ya katibu muhtasi wa Tunu na wakati nikitaka kumuaga simu iliyokuwa juu ya meza yake ikaanza kuita kwa sauti ya chini. Salha akanyoosha mkono wake wa kushoto kuinyanyua huku akininyooshea mkono wake wa kulia kuniashiria nisubiri kidogo.
“Mkuu amesema usubiri kidogo kuna mtu anakuja kukuona sasa hivi,” Salha alinieleza baada ya kumaliza kuongea na simu hiyo.
“
Okay,” nilimjibu huku nikiketi kwenye kiti kilichokuwa karibu yangu. Sikujua ni mtu gani niliyekuwa nikimsubiri, na alikuwa anataka nini kwangu, au kunieleza jambo gani! Nilichokuwa nafahamu kwa wakati huo ni kwamba nilikuwa nimesharipoti kazini na kupewa mapumziko ya mwezi mmoja kabla ya kuja kuanza kazi rasmi. Hata hivyo, sikuwa na la kufanya ila kusubiri.
Nilikaa hapo kwa takriban dakika kumi hivi ndipo mlango wa ofisi ile ukafunguliwa. Ofisa mmoja, mwanaume mwenye umri usiopungua miaka therathini akaingia ndani. alikuwa amevaa suti nzuri ya kijivu. Baada ya kutusalimia akajitambulisha jina lake, nami nikamfahamisha jina langu.
“Kumbe wewe ndiye Ofisa ninayekutafuta,” yule Ofisa aliniambia huku akinipa mkono kisha akaendelea kuniambia, “Mkuu ameniagiza nikupe hii
OP.” Alisema na kunyoosha mkono wake kunipa bahasha nyeupe iliyokuwa imeandikwa jina langu.
“Ahsante, nashukuru sana,” nilimjibu yule Ofisa huku nikiipokea ile bahasha na kuitumbukiza katika mfuko wa koti langu. Sikuwa na haja ya kujiuliza kilichokuwemo maana aliyenipa alishaniambia kuwa ni OP yaani “
operation fund”. Nilitambua kuwa hilo lilikuwa neno la ki-idara lenye maana ya “fedha za kufanyia kazi”. Ingawa sikuwa nakwenda kufanya kazi lakini mapumziko niliyokuwa nakwenda yalikuwa yanagharamiwa na Idara. Na hivyo bila kupoteza muda nikamuaga katibu muhtasi wa mkuu na kutoka.
Niliitupia jicho saa yangu ya mkononi wakati nikielekea kwenye gari langu, nikagundua kuwa ilikuwa saa tano na nusu asubuhi. Sikuwa na sababu ya kurudi nyumbani muda huo hasa kwa kuwa Rehema hakuwepo nyumbani, na hivyo nikaona nielekee benki.
* * *
Tukutane wakati mwingine. Endelea Kufuatilia simulizi hii hadi mwisho...