222
Kisha alisogea akasimama mbele yangu, akanitazama kwa kitambo na kuongea kwa sauti ya chini kama aliyekuwa akininong’oneza. “Afadhali utuambie ukweli, tupo tayari kukubadilishia mtindo endapo huu utaonekana haukufai.”
“Sijui chochote,” niliendelea kusisitiza japo sauti yangu ilikuwa dhaifu.
“Unajua kila kitu, usitudanganye,” Meja Saleh bin Awadh alisema kwa kufoka.
“Ningekuwa najua ningewaambia, au mnadhani nayafurahia haya mateso?!” nilisema kwa sauti ya unyonge iliyokuwa ikitia huruma.
“Nadhani umedhamiria kufa kiume, kufa na siri moyoni… usijali, tunayo njia nyingine itakayokulazimisha kuongea,” Meja Saleh bin Awadh aliniambia huku akiachia tabasamu la kifedhuli. Kisha akaongeza, “Achana na porojo mnazofundishana huko kwenye ujasusi kwamba ukikamatwa hata ukisema ukweli adhabu yako bado itabaki pale pale. Mimi nakuahidi kama utaonesha ushirikiano utaachiwa huru.”
Sikusema kitu bali nilibaki kimya huku nikimtazama kwa hasira kwani nilishachoshwa na maswali yao ambayo nilikwisha kata shauri kuwa kamwe nisingeyajibu hata kama nigelazimika kupoteza uhai wangu. Hata hivyo hali yangu ilikuwa mbaya sana.
Meja Saleh bin Awadh alishusha pumzi ndefu huku akinitazama kwa tabasamu na baadaye tabasamu lake liligeuka kuwa kicheko. Kisha akasema, “Nadhani anahitaji kubadilishiwa burudani.”
Mara nikawaona wale makomando wakinisogelea kwa ukakamavu mkubwa, na kwa haraka sana wakanifungua zile pingu zilizokuwa zimefungwa kwenye mikono na miguu yangu pale kwenye kile kiti cha umeme kilichotumika kunisulubu. Kisha wakanishika miguu yangu na kunivuta wakinishusha kwa nguvu kutoka pale kwenye kile kiti hali iliyonifanya nitue sakafuni kwa matako na kunifanya nisikie maumivu makali sana yaliyosambaa mwili mzima.
Nilijaribu kujitetea lakini ilikuwa kazi bure kwani walianza kunishushia kipigo cha mateke mwilini mwangu na kujikuta nikiishiwa na nguvu na kulala sakafuni kama mfu. Kisha waliporidhika kuwa kile kipigo kilikuwa kimenilegeza kiasi cha kutosha, wakaanza kuniburuza kibabe kuelekea kule kwenye lile tangi kubwa lililojengwa kwa vioo ambalo ndani yake lilikuwa limejazwa maji.
Walinibwaga pale chini jirani na lile tangi la maji. Nikiwa pale chini nikihema kwa nguvu kutokana na kile kipigo, nilimwona Meja Saleh bin Awadh akinisogelea taratibu huku wale makomando wakinizunguka na hapo nikafungwa kamba mikononi.
“Nadhani hutopenda hiki kinachofuata…” Meja Saleh bin Awadh alininong’oneza sikioni, nikamkata kauli.
“Hata uniambie nini, sijui chochote…” wakati nasema hivyo nikakatishwa na kipigo cha mateke ya mgongoni, kabla sijajua nifanye nini mara nikajikuta nikibebwa mzobe mzobe na wale makomando na kurushiwa ndani ya lile tangi la maji. Matukio yote yale yalifanyika kwa haraka sana.
Nikajua sasa walikuwa wamedhamiria kunitesa kwa kunizamisha ndani ya lile tangi la maji kwa kufungulia umeme ulioungwa ndani ya lile tangi la maji ili kunipiga shoti mbaya na ikiwezekana kuniua kabisa. Nilizifahamu mbinu za aina hii za ukatili na utesaji kwa kuwaweka kwenye maji watuhumiwa hasa magaidi, kuwakosesha usingizi, kuwapiga shoti ya umeme na kila aina ya utesaji ili kupata siri kutoka kwao.
“Twambie, au niwaruhusu waendelee na adhabu. Nadhani unajua kitakachokutokea,” Meja Saleh bin Awadh aliniambia huku akinikazia macho.
“Sijui chochote,” nilisema nikiwa nimeshajiandaa kufa. Muda huo nilikuwa nimesimama ndani ya tangi na yale maji yaliishia usawa wa kifua changu.
Nikiwa sijui kilichokuwa kinaendelea ghafla nikapigwa shoti kali ya umeme iliyonitetemesha mwili mzima huku nikihisi ngozi yangu ikiunguzwa na moto wa umeme uliokuwa ukisambaa haraka sana mwilini mwangu. Nikajikuta nikiwa katikati ya maumivu makali sana yasiyoelezeka, nikaanza kutetemeka kama niliyekumbwa na kifafa.
Nilifumbua mdomo wangu kupiga kelele za kumwomba Meja Saleh bin Awadh awaambie makomando wake wasitishe yale mateso lakini sauti yangu haikuweza kutoka, kila nilipopiga kelele niliisikia sauti yangu ikiishia ndani ya akili yangu. Nikaanza kujiona nikipaa angani kwa kasi ya ajabu sana, na nilipofika juu zaidi nikaanza kushuka chini kwa kasi ile ile na kisha nikatumbukia kwenye shimo refu sana lililokuwa na kiza kilichotisha.
Na mara giza zito likatanda kwenye mboni zangu za macho huku taratibu nguvu zikianza kuniishia na mwili wangu ukilegea, mapigo yangu ya moyo nayo yakaanza kudorora, mwishowe nikahisi roho yangu ikifika njia panda. Kisha nikawa kama mtu niliyekuwa umbali mrefu sana angani nikianguka kwa kasi sana kuelekea ardhini nikiwa nimetanguliza kichwa…
* * *
Nilishtuka na kuamka kutoka kwenye usingizi mzito wa kifo baada ya kuhisi mkono wa mtu ukinigusa kwenye paji langu la uso wangu. Niliyafumbua macho yangu taratibu kisha nikageuza shingo yangu kutazama upande ulikotokea ule mkono na kumwona mwanamume mnene na mrefu akiwa amesimama huku akinitazama kwa makini.
Kwa haraka niliweza kugundua kuwa alikuwa na umri wa kati ya miaka 40 na 45, alikuwa Mwarabu na alikuwa na misuli imara ya mikononi iliyotuna kikamilifu. Uso wake ulikuwa mpana na alikuwa amevaa miwani mikubwa iliyoyahifadhi macho yake makubwa. Alivaa suruali ya khaki, shati la samawati na juu yake alivaa koti refu jeupe la kidaktari, shingoni alining’iniza kifaa cha kupimia mapigo ya moyo ambacho kitaalamu kiliitwa
stethoscope.
Kisha niliyazungusha macho yangu haraka haraka na hapo nikagundua kuwa nilikuwa juu ya kitanda cha chuma ndani ya chumba kidogo bila dirisha. Upande wa kushoto wa kile kitanda kulikuwa na meza ya mbao iliyokuwa na beseni dogo la chuma lenye vifaa vyote muhimu vya tiba. Pia kulikuwa na stendi ndefu ya chuma ya kitabibu iliyotundikiwa chupa mbili za dripu, chupa moja ya dripu ya maji na nyingine dripu ya damu.
“Unajisikiaje?” yule daktari aliniuliza baada ya kugundua kuwa nimeamka, hata hivyo sauti yake ilikuwa ya chini kana kwamba hakutaka watu wengine wasikie alichokuwa akiongea.
Kwanza nilibaki kimya nikimtazama kwa umakini, nilijiuliza niko wapi na nini kilikuwa kinaendelea kisha nikashusha pumzi za ndani kwa ndani huku nikimeza mate kuitowesha hofu ndani yangu.
“Hata sielewi ila mwili unaniuma sana,” nilimwambia kwa sauti tulivu huku nikimtazama kwa umakini.
“Usijali, kila kitu kitakuwa sawa,” yule daktari alisema huku akitoa mashine ndogo ya kupimia shinikizo la damu na mapigo ya moyo. “Nahitaji kuangalia mwenendo wa presha na mapigo ya moyo wako…”
Kisha aliifunga ile mashine kwenye mkono wangu wa kushoto halafu akaanza kuipampu kwa muda. Niliyafumba macho yangu huku nikibana pumzi kutokana na ile mashine kuanza kubana kwenye mkono wangu na kusababisha maumivu kidogo. Baada ya kitambo fulani yule daktari alianza kulegeza taratibu kifungo fulani kidogo kilichokuwa pembeni, mara nikasikika sauti ya
‘hisssiii’. Kisha nikamwona akiweka rekodi kwenye faili alilokuwa nalo mkononi.
“Samahani daktari, hivi hapa nipo wapi?” nilimuuliza huku hofu ikinitambaa taratibu.
Yule daktari alinitazama kwa kitambo pasipo kusema neno halafu akashusha pumzi za ndani kwa ndani. Sikuona tashwishwi yoyote usoni kwake. Nikiwa bado nasubiri jibu lake mara nikashuhudia kitasa cha mlango wa kile chumba kikizungushwa taratibu na kisha ule mlango ukasukumwa kwa ndani na kufunguka.
Niligeuza shingo yangu haraka kutazama upande ule nikamwona Meja Saleh bin Awadh akiingia mle chumbani akiwa ameongozana na mtu mwingine ambaye sikumfahamu. Alikuwa kipande cha mtu, amekwenda hewani kisawa sawa. Sikuweza kutambua mara moja asili yake ila hisia zangu zilinitabanaisha kuwa kama hakuwa Mpalestina au Mlebanon basi alitoka Syria. Sura yake ilikuwa ngeni kabisa machoni mwangu na alikuwa amevaa kiraia, suti ya rangi ya samawati, ila nilipomchunguza vizuri kwa jicho la kishushushu nikajiridhisha kuwa yeye pia alikuwa askari komando wa daraja la juu. Alikuwa na sura ya kazi na hakuonekana kuwa rafiki.
Meja Saleh bin Awadh na yule komando Mpalestina, kama nilivyoamua kumwita, wakanitazama kwa umakini pale kitandani huku wakionekana kuridhishwa na maendeleo ya afya yangu. Kisha Meja Saleh bin Awadh akamwambia yule daktari. “Leo itawezekana kumchukua tena kwa mahojiano mafupi?”
“Hali yake bado haijatengamaa vizuri, labda kesho jioni.” yule daktari alijibu huku akinitazama usoni.
“Jana nilikuuliza ukaniambia leo, hivi kweli uko makini na kazi yako, daktari? Kumbuka leo ni siku ya nne tangu awepo hapa na hatuna muda wa kupoteza!” Meja Saleh bin Awadh alisema kwa kufoka.
“Lakini nilisema vile nikitegemea afya yake ingekuwa imeimarika zaidi, hebu mpeni siku moja zaidi…” yule daktari alisema.
“Sikiliza daktari, fanya ufanyavyo tunataka kumhoji mtu huyu leo jioni, hatuna muda na mtu huyu anazo taarifa muhimu sana tunazozihitaji,” Meja Saleh bin Awadh alisisitiza huku akinitazama usoni kwa hasira.
“Sawa, nitajitahidi,” daktari alisema kwa sauti ya kukata tamaa. Kisha kama mtu aliyekumbuka jambo akafungua droo ya meza iliyokuwepo kando ya kile kitanda na kutoa chupa ya chai na bakuli la plastiki.
Halafu aliifungua ile chupa na kumimina uji mwepesi wa mchele kwenye lile bakuli, akanipa. Nililipokea lile bakuli na kuanza kuunywa ule uji wa mchele. Ulikuwa uji wa moto kiasi na mtamu sana kwa kuwa ulitiwa karanga zilizosagwa. Kwa kuwa nilikuwa na njaa niliubugia wote kwa muda mfupi kisha yule daktari akanijazia tena, nao nikaumaliza na kumshangaza kila mtu mle ndani. Muda huo Meja Saleh bin Awadh na yule komando Mpalestina walikuwa wananitazama tu pasipo kusema neno.
“Sasa pumzika, naamini utapata nafuu,” yule daktari alinisisitiza huku akiwatupia jicho wale maofisa, na hapo Meja Saleh bin Awadh akampa ishara kuwa wote waondoke na kuniacha, wakatoka nje ya kile chumba na kufunga mlango wakiniacha peke yangu.
* * *
Endelea...