Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Kwa kweli tunashukuru sana kwa simulizi hii nzuri. Yaani naisoma kwa mtiririko, mfululizo na kwa muunganiko bila kupoteza utamu wake. Hujawa na choyo kwenye kuipost hapa jukwaani. Ubarikiwe sana mkuu
Amina... Endelea kuifuatilia hakika hutojutia muda wako...
 
ufukweni mombasa.JPG

219

Sijui chochote…




SIKUFAHAMU niliamka baada ya muda gani ila nilikuwa bado nipo sakafuni ndani ya kile chumba, na nilikuwa nahisi njaa sana. Niliinuka na kuketi pale chini, na wakati naangaza macho yangu huku na huko nikabaini kuwa kulikuwa na sinia la chakula na chupa kubwa ya maji mbele yangu. Sikujiuliza mara mbili, nililivuta lile sinia nikaanza kukifakamia kile chakula kwa pupa. Sikuwa na uhakika nilikuwa nimekaa siku ngapi pasipo kula maana ile njaa niliyoihisi haikuwa ya siku moja.

Hata majira yenyewe sikuyafahamu kwa kuwa mle ndani taa ilikuwa inawaka na hakukuwa na hata dirisha la kunifanya nione yaliyokuwa yanaendelea kule nje. Nilipomaliza kula nikachukua maji nikanywa na kujilaza tena pale sakafuni huku nikijiuliza kile chakula kililetwa muda gani, maana kilikuwa kimepoa kabisa!

Sasa kumbukumbu zangu zilikuwa zimerudi, niliweza kukumbuka kila kitu, tangu tulivyotoka chuoni Zawyet Sidi Abd el-Ati kwa ndege maalumu hadi kwenye kisiwa ambacho hadi muda huo sikujua ni kisiwa gani zaidi ya kupatambua mahali hapo kama ‘Shamba’, kisha jioni moja mimi na Leyla tulitoka kwenda matembezi, huko akanivisha pete na kisha tukajikuta tumeingia mtegoni!

Kitu cha mwisho kabisa nilichokumbuka ilikuwa ni maumivu ya kitu kama sindano mgongoni kwangu na kisha nikapoteza fahamu. Sikujua Leyla alikuwa amepelekwa wapi na wale watu na walikuwa wanamfanyia nini. Roho iliniuma sana kwa kushindwa kumlinda Leyla, na kama jambo lolote baya lingempata basi nisingejisamehe kabisa maishani mwangu.

Nilijitazama kidoleni nikaiona ile pete aliyonivisha Leyla, ilikuwa inatoa mng’ao wa ajabu mle ndani, na hapo nikajikuta roho ikizidi kunimuma, nilitamani kuinuka nikamtafute Leyla popote alipo. Nilianza kumhurumia sana huku nikiwaza jinsi ya kujiokoa na kisha nianze kumsaka. Mara nikashtuka baada ya kuhisi kitasa cha mlango wa kile chumba kikizungushwa taratibu na kisha ule mlango kufunguliwa kisha ukasukumwa kwa ndani.

Hisia zangu ziliniambia kuwa alikuwa ni yule mtu amerudi tena, pengine safari hii alihitaji kunihoji. Nikageuka taratibu na kuyapeleka macho yangu kutazama kule kwenye mlango huku nikijiandaa kwa lolote ambalo lingetokea.

Ule mlango ulipofunguliwa yule mtu niliyemtarajia akaingia mle ndani, lakini hakuwa peke yake, alikuwa ameongozana na wanaume wengine wawili, warefu na wenye miili iliyojengeka imara. Mmoja wa wale watu alikuwa mweusi kweli kweli, na mwingine alikuwa Mwarabu. Wote wawili walivaa kombati za kijeshi lakini sikujua ni za jeshi la nchi gani kwa kuwa hawakuwa na nembo yoyote ya utambulisho, kichwani walivaa kofia nyekundu za bareti zenye nembo ya chui.

Watu hao walikuwa wamepanda hewani kisawa sawa na namna ya mikono ya magwanda yao ilivyokunjwa niliweza kuiona misuli yao imara ya mikononi. Haraka sikushindwa kugundua kuwa walikuwa ni makomando waliofuzu vizuri katika medani za masuala ya kijeshi. Nikahisi hofu ikinitambaa mwilini na mapigo ya moyo wangu yakaanza kunienda mbio isivyo kawaida.

Nilitamani nikurupuke na kutimua mbio lakini hilo halikuwezekana kwa kuwa muda haukuniruhusu kufanya vile na wale watu walikuwa ni kama tayari wameshanifikia pale sakafuni nilipolala. Kisha wakajigawa katika mtindo wa kunizunguka. Niliinuka na kuketi pale sakafuni huku nikiwatazama kwa umakini.

Mmoja wao, yule mweusi, alikuja kusimama upande wangu wa kushoto, yule Mwarabu akasimama upande wa kulia. Halafu yule bwana aliyekuwa amekuja mwanzo, ambaye kwa mtazamo tu alionekana ndiye kiongozi, akasimama mbele yangu huku akinitazama kwa tabasamu la kifedhuli. Nikiwa nimeshikwa na mshtuko wa hali ya juu, niliendelea kuyatembeza macho yangu taratibu nikizikagua vizuri sura zao wote kisha nikaweka kituo nikimtazama yule kiongozi.

Yeye aliendelea kunitazama kwa tabasamu na alipojiridhisha kuwa nilikuwa nimerudiwa vizuri na fahamu zangu akakohoa kidogo kusafisha koo lake.

“Nadhani sasa tufahamiane, mimi naitwa Meja Saleh bin Awadh,” yule mtu alijitambulisha kwangu kwa kujiamini huku akinipa heshima zote utadhani nilikuwa mkuu wake wa kazi, kisha akanimpa mkono lakini sikuupokea.

“Usijali, mimi si mtu mbaya,” Meja Saleh bin Awadh aliniambia huku akiendelea kutabasamu kifedhuli na mikono yake ameishikamanisha mbele yake.

“Usingekuwa mtu mbaya ungenikamata na kunifungia humu ndani bila kosa lolote?” nilimuuliza Major Saleh bin Awadh kwa utulivu huku nikianza kuhisi fundo la hasira likinikaba kooni.

Alicheka kidogo kabla hajasema, “Sikia, bwana mdogo… ningekuwa mtu mbaya basi sasa hivi ungekuwa mfu. Elewa maisha hayako sawa kama unavyoweza kudhani,” Meja Saleh bin Awadh aliniambia kwa sauti ya utaratibu kana kwamba mzazi akimwonya mwanawe.

Sikusema kitu bali nilitabasamu kidogo kujifariji na kuitowesha hasira iliyokuwa inachemka ndani ya kifua changu. Meja Saleh bin Awadh akaongeza, “Kwanza ulipaswa kushukuru kwa kuwa bado upo hai.”

“Kwani ninyi ni akina nani na kwa nini mmenikamata?” nilimuuliza Meja Saleh bin Awadh huku nikimkazia macho kabla sijayatembeza macho yangu kuwatazama wale wengine. Nikawaona wakinitazama kwa uchu mkubwa kama fisi walioona mzoga.

“Hatupo hapa kwa ajili ya kuulizwa maswali na wewe. Tupo hapa kwa ajili ya kuhitaji taarifa na tutakupatia nafasi ya kuishi endapo utakuwa tayari kusema ukweli,” alidakia kwa sauti ya ukali yule komando mweusi aliyekuwa amesimama upande wangu wa kushoto.

Niligeuka kumtazama sura yake ikanitia mashaka mno. Alikuwa Mwafika halisi ingawa sikujua asili ya nchi yake, na macho yake yalikuwa makubwa na mekundu yenye uchovu lakini yaliyokuwa yanaonya. Uso wake ulikuwa mrefu, na ijapokuwa alikuwa amevaa kofia ya bareti lakini sikushindwa kubaini kuwa alikuwa na upara unaowaka na usiokuwa na unywele hata mmoja. Muda huo alikuwa kakaza sura yake akinitazama utadhani alikuwa akivishwa medani ya heshima na amiri jeshi mkuu.

“Nitasema ukweli upi nisioufahamu?” nilimuuliza yule komando mweusi huku nikitabasamu, nilikuwa najaribu kuwazuga huku nikiipima hali ya mle ndani.

“Kipi usichofahamu? Tunajua unafahamu kila kitu wala usitudanganye,” yule komando mweusi alisema huku akiminya pua yake, alikuwa ananitazama kwa dharau. Macho yake makubwa yalikuwa na kila dalili ya ukatili yakionekana kunionya kuwa nisijaribu kuleta aina yoyote ya ufedhuli.

“Kama mnanilazimisha kufahamu sawa, lakini sijui mnachotaka,” nilisema kwa hasira kisha nikaongeza, “Kwanza nyinyi ni akina nani na hapa nipo wapi?”

“Usijali, muda si mrefu tutafahamiana vizuri,” Meja Saleh bin Awadh aliniambia huku akikenua meno yake.

Kisha aliyahamisha macho yake kutoka kwangu akayatembeza taratibu akimtazama yule komando mweusi mwenye kiherehere aliyekuwa kushoto kwangu pamoja na yule komando mwenzake kisha akayarudisha tena macho yake pale sakafuni nilipoketi na kusema kwa sauti tulivu lakini yenye kumaanisha. “Nitahitaji mtu huyu atapishwe taarifa zote muhimu anazozifahamu kuhusu Shamba, kwa namna yoyote ile.”

“Vipi kama atapoteza maisha?” yule komando Mwafrika aliuliza huku akinitupia jicho kali.

“Anzeni na EXT-1 akijifanya yeye jasusi mbobevu asiyeogopa mateso basi nendeni moja kwa moja kwenye EXT-3. Kumbukeni roho ni mali yake, sisi tunachohitaji ni taarifa zote muhimu,” Meja Saleh bin Awadh alijibu kwa jeuri na kunitia hofu kubwa.

Endelea...
 
ufukweni mombasa.JPG

220

Nilitambua kuwa ‘EXT-1’ maana yake ‘Extreme Torture stage 1’. Hapa mhalifu huwa anapewa adhabu ya kupigwa, kutishia kuwaumiza watu awapendao, kumpiga shoti za kawaida za umeme au kumpiga sehemu zinazomletea maumivu. Kama anachelewa kusema na jambo ni la hatari kidogo ndipo hutumika hatua ya pili, ‘EXT-2’, inayojumuisha kuua mtu mwingine mbele yake ili kumletea woga, kumwingizia waya puani na kuzidi kuusukuma kama haongei, kumwekea kitambaa usoni na kummiminia maji huku ukikibana ili maji yaingie puani na kumfanya asipumue, kumvisha mfuko wa plastiki kufunika uso wake ili ashindwe kuvuta pumzi na kadhalika.

‘EXT-3’ (Extreme Torture stage 3) ni hatua ya mwisho yenye mateso yaliyopitiliza. Kwenye mafunzo ya kijeshi aina hii ya adhabu hupewa gaidi asiyetaka kutaja sehemu ambapo bomu au kitu cha kudhuru watu kipo na kinahatarisha uhai wa watu kwa wakati huo, na ni cha haraka. Adhabu yake huwa ni kumchoma sindano ya maumivu makali, kumchoma mishipa kwa bisibisi, kumchoma kwa moto wa gesi, kumkata vidole au kumng’oa kucha, kumkata sehemu yenye nyama na kuchomeka nyaya zenye shoti ya umeme.

Okay! Basi tuachieni kazi halafu utapata majibu,” yule komando mweusi, mwenye kiherehere, alisema, na hapo nikamshuhudia Meja Saleh bin Awadh akiondoka na kuwaacha wale makomando. Nikahisi mapigo yangu ya moyo yamesimama maana nilijua ambacho kingefuata hapo kilikuwa kinatisha.

Kwa mara nyingine tena nilitamani nikurupuke na kutimua mbio lakini hilo halikuwezekana kwa kuwa mwili ulikuwa umenyong’onyea na bado sikuwa na nguvu sawa sawa za kuweza kupambana na wale watu. Kwa mara ya kwanza nilianza kuhisi woga mkubwa hasa nilipofikiria kitu gani kingefuatia kama wale jamaa wasingefanikiwa kupata taarifa walizozihitaji kutoka kwangu.

Nilianza kuomba kimya kimya na kuikabidhi roho yangu kwa Mungu ili aninusuru na mateso makali ambayo yangenisababishia kupoteza uhai au kupata ulemavu wa kudumu.

Sasa nilianza kuyahisi maumivu hayo hata kabla sijaanza kuteswa, yalikuwa maumivu makali mno yasiyopimika ambayo sijapata kuyahisi katika maisha yangu yote hapa duniani. Mikono yangu ilijaribu kufinya sakafuni kwa hisia zile za maumivu makali na kila nilipofinya sakafu na kusogeza mikono yangu, ile pete niliyozawadiwa na Leyla ilitoa mng’ao na kuwamulika wale makomando.

Kisha nilianza kuhisi kuwa akili yangu ilianza kufanya kazi taratibu sana na hapo nilimwona yule komando mweusi akinijia na kuushika mkono wangu wa kushoto kisha akaigusa ile pete, cha ajabu nilitulia tu na sikuweza hata kutingishika. Nilibaki nimetulia kama mtu aliye katika usingizi mzito nikimwangalia kwa uchungu wakati akiivua ile pete kutoka kwenye kidole changu.

Kisha aliiweka kwenye mfuko wa suruali yake, na hapo nikahisi kama alikuwa amenipora kitu muhimu zaidi maishani mwangu. Niliiona ile pete kama hazina ya moyo wangu yaani kunipora ilikuwa sawa sawa na kuchukua roho yangu. Nilihisi kama moyo wangu ulikuwa unapasuka vipande ndani kwa ndani kwa sababu ile pete ilikuwa imebeba nguvu kubwa ya uhusiano na mawasiliano kati yangu na Leyla. Kupitia ile pete nilimwona Leyla akiwa karibu zaidi na mimi. Sasa baada ya kuipoteza nilihisi hata Leyla angepotea kutoka kwenye maisha yangu. Kuanzia hapo nikajiona kama mtu aliyepoteza matumaini yote.

Sikujua kwa nini nilinyong’onyea kiasi kile baada ya ile pete kuchukuliwa kwani niliamini kuwa ile pete ilikuwa alama ya upendo wangu kwa Leyla, alama ambayo sasa ilikuwa inatoweka na kupotelea katika mikono ya wahalifu, macho yangu yakajaa machozi. Nilifumba macho yangu ili kuepuka kuwapa nafasi wale wahuni ya kunifanyia dhihaka zaidi. Nikabaki nimetulia nikiwa sijui nifanye nini.

“Wewe!” nilimsikia yule komando mweusi mwenye kiherehere akiniita kwa ukali kidogo. Niliyafungua macho yangu lakini sikuitika, nilibaki kimya nikimkodolea macho.

“Unaitwa nani?” aliniuliza tena yule komando lakini bado niliendelea kubaki mkimya.

“Ooh, kumbe wewe ni jeuri! Haitakusaidia kitu, cha muhimu tunataka utuambie taratibu na bila kificho chochote halafu tutakuachia huru uende zako, nini kinaendelea kule Shamba na pia ututajie majina ya walimu wanaofundisha hapo ni akina nani? Basi!” yule komando mweusi alinihoji huku akinikazia macho.

“Sijui chochote kuhusu unachokisema,” niliongea kwa utulivu.

“Naona umejitolea kufa peke yako huku wenzako wakiwa wanastarehe huko Shamba, sivyo?” yule komando aliniuliza kwa sauti iliyonionya kutoongopa kisha akaongeza, “Au unadhani utasifiwa kwa upuuzi wako wa kujifanya unazingatia sana kiapo cha kijasusi kwa kutotoa siri?”

Nilitaka nitoe tusi lakini nikajizuia na kubaki kimya. Yule komando alinitazama kwa kitambo kirefu huku akiruhusu tabasamu pana kuchanua usoni kwake. Lilikuwa tabasamu la dharau.

“Kwa hiyo, hujui nini kinaendelea huko Shamba wala majina ya walimu wako?” yule komando mwingine mwenye asili ya Kiarabu aliingilia kati na kuniuliza baada ya kuona nipo kimya.

“Kwanza shamba gani mnalozungumzia, mbona siwaelewi?” nami niliwauliza nikijifanya sielewi chochote.

“Usijifanye hujui ni nini tunachokiongelea… Labda nikwambie kitu, huna ujanja wowote kwa kuwa hakuna anayeletwa humu na kushikilia misimamo wake kisha akatoka akiwa hai. Sidhani kama utapenda tufike huko!” yule komando mweusi aliniambia huku akinitazama kwa ghadhabu.

“Hata mimi sipendi tufike huko lakini kama sijui chochote mnataka niwadanganye?” niliuliza huku nikijaribu kuinuka.

Na hapo nikashtukia nikitulizwa kwa kofi zito kutoka kwenye kiganja kilichokomaa kwa mazoezi cha yule komando mweusi, na hivyo kunisababishia maumivu makali sana kichwani. Japo kile kilikuwa kipigo cha mara moja tu lakini maumivu yake yalikuwa hayasimuliki!

“Sasa mbona unanipiga wakati nimekwambia sijui chochote?” nilimuuliza yule komandoo kwa hasira huku nikimtazama.

“Hapa bado hujapigwa, nilichofanya ni kukukumbusha tu kuwa unatakiwa kujibu maswali unayoulizwa, usitulazimishe kutumia nguvu kisha ukajuta,” yule komando aliniambia kwa ukali katika namna ya kunionya.

“Sina ninachoweza kuwajibu kwa sababu sijui chochote,” nilijaribu kujitetea, hata hivyo moyoni nilishaanza kuhisi juu ya hatari kubwa iliyokuwa ikininyemelea.

Yule komando Mwarabu alinishika akakisukasuka ovyo kichwa changu na kunipiga piga nyuma ya shingo yangu kwa dhihaka. Kuona vile nikajiinua kwa nguvu nikiwa nimepandwa na hasira. Hilo lilikuwa kosa kubwa sana. Kilichofuatia hapo nilitamani ardhi ipasuke ili niangukie ndani na kupotelea humo.

Kwa kasi ya umeme yule komando mweusi aliruka juu, akajiviringisha hewani, hapo nikajua akitua chini ingekuwa balaa, hivyo nilijiandaa kwa pigo lolote ambalo lingefuata. Haraka nikajibetua na kuyakwepa mapigo ya haraka ya yule komando.

Kuona hivyo, akakusanya nguvu za kutosha kisha kufumba na kufumbua akajibetua na kuuzungusha chini mguu wake wa kulia akinichota ngwala maridadi yenye ufundi wa hali ya juu. Sikutegemea, nilishikwa na taharuki ya aina yake wakati nilipokuwa nikitupwa hewani na kuweweseka kama niliyekuwa nimepagawa na mapepo.

Nilipotua chini nikashtukia napigwa ngumi mfululizo za tumbo zilizonifanya nijipinde huku nikisikia maumivu makali sana yaliyosambaa haraka hadi mgongoni. Kisha nilichapwa pigo baya la kareti mbavuni na maumivu yake yakanifanya niachie mguno mkali wa maumivu, nikayumba ovyo huku nikirudi nyuma lakini kabla sijaanguka yule komando aliruka na kunidaka kisha akaninyanyua juu juu kama kishada kwa nguvu zake zote na kunibwaga chini kama wafanyavyo wanamieleka, akina John Cena.

Endelea...
 
ufukweni mombasa.JPG

221

Hali ile ilinifanya nitue pale sakafuni kwa matako na kufanya maumivu makali yasambae mwili mzima. Nikapiga yowe kali la maumivu huku nikijitahidi kusimama lakini ilikuwa kazi bure. Yule komando, nilibaini kuwa alikuwa komandoo wa daraja la juu, aliniwahi kabla sijasimama sawa sawa akanikwida tena na kuninyanyua juu.

Nilijitahidi kujitetea kwa kila namna lakini bado haikunisaidia kitu, alikuwa na nguvu nyingi zisizo za kawaida! Alinibeba mzegamzega na kunibwaga kama furushi pale sakafuni. Muda wote yule komando mwenzake alikuwa ametulia tuli bila kutingishika akiniangalia huku uso wake ukiwa umepambwa kwa tabasamu pana.

Baada ya kutua pale sakafuni kama furushi nilipiga tena yowe kali huku maumivu makali yakizidi kusambaa mwilini, nikajikuta nikianza kuingiwa na hofu kubwa. Kisha yule komandoo mweusi alinijia kwa mapigo ya mateke ya haraka ambayo nilijitahidi kwa kila namna kuyapangua kwa mikono yangu bila mafanikio.

Nilitaka kuinuka lakini kizunguzungu kikanishika na kunifanya kutapika chakula chote nilichokula, na hapo nikaanza kuishiwa na nguvu, sikuona tena kama kungekuwa na namna nyingine ya kujiokoa kutoka kwenye mikono matata ya yule komando mwenye kiherehere, hivyo niliamua kunyoosha mikono yangu juu kuashiria kwamba nilikuwa nimesalimu amri. Nilikuwa nahema ovyo.

Yule komando hakunisikiliza, alisimama akanitazama kwa makini na aliporidhika kuwa kile kipigo kilikuwa kimenilegeza kiasi cha kutosha, akaninyanyua na kunikalisha kwenye kile kiti cha umeme kilichokuwa kikitumika kuwasulubu watuhumiwa hatari kisha mikono na miguu yangu ikafungwa kwa pingu.

Na hapo nikajua kuwa walipanga kunipa mateso makali kwa kunipiga na shoti ya umeme kwani kuniweka kwenye kiti cha umeme ilikuwa ni adhabu iliyo katika EXT-3 yaani aina ya mtindo wa mateso wenye maumivu makali mno yasiyoelezeka. Sasa niliamini kuwa nisingeweza kutoka salama mle ndani, ni dhahiri kuwa waliamua kuniua, iwe wamepata taarifa walizokuwa wakizihitaji au hawajazipata.

Na hapo nikamkumbuka mke wangu Rehema na mwanangu Jason Sizya Junior. Pia niliwakumbuka wazazi wangu, ndugu zangu na mwisho nikamkumbuka Zainabu. Machozi yakaanza kunilengalenga machoni lakini nikajitahidi kuyafukuza haraka kwani hali hiyo ingenifanya kuwa mnyonge zaidi mbele ya wale watu.

Nilianza kujilaumu kwa nini sikumsikiliza Rehema alipokuwa akinikatalia kusafiri na hatimaye akaangua kilio baada ya kuonekana nilikuwa nimeng’ang’ania kuondoka. Sikujua angekuwa katika hali gani baada ya kupata taarifa kuwa nilikufa nikiwa mafunzoni au nilikuwa nimetoweka na sijulikani nilipo iwapo maiti yangu isingepatikana baada ya kuuawa na kisha kutupwa porini niwe chakula cha fisi!

Pia nilijiuliza, nini kilikuwa kinaendelea kwa wanachuo wenzangu baada ya kubaini mimi na Leyla tulikuwa tumetoweka? Je, walikuwa katika hali gani huko waliko? Huenda walikuwa wametutafuta sana bila mafanikio na sasa walikuwa wamekata tamaa! Vipi kuhusu Leyla. Naye alikuwa anapitia mateso makali kama yangu au alihurumiwa?

Dah! Nilianza kujiona mtu mwenye mkosi mkubwa sana hapa duniani kwani kila jambo nililolianza lilionekana kuishia pabaya au kukumbwa na misukosuko, nikaanza kujilaumu kukubali kuingia kwenye mafunzo ya ujasusi…

Muda huo damu zilikuwa zinanitoka puani na mdomoni huku sehemu ya juu ya jicho langu la kushoto ikiwa imevimba na kuchanika na ilikuwa inavuja damu taratibu. Moyo wangu ulikuwa unakwenda mbio na uliunguruma sana kama uliokuwa ukipambana na kazi isiyo ya kiasi chake. Mwili wangu nao ulikuwa mzito kama uliofungwa na kipande cha chuma na jasho jingi lilikuwa linanitoka sehemu mbalimbali za mwili wangu.

Sasa nilianza kuuona mwisho wangu ulikuwa karibu mno kuliko nilivyofikiria, hata hivyo nilimwomba sana Mungu anipe nguvu za kupambana na aniepushe na kifo kile cha mateso.

“Sasa tueleze, ni nini kinaendelea huko Shamba na tutajie majina ya walimu wako! Vinginevyo nitawasha swichi ya umeme,” yule komando mweusi aliyekuwa akinisulubu aliniambia huku akinitazama usoni kwa ghadhabu.

“Nimekwisha waambia sijui chochote, kama mnataka kuniua nyie niuweni tu,” nilifoka kwa hasira huku nikimeza funda kubwa la mate kuitowesha hasira iliyojaa kifuani mwangu.

Yule komando aliisogelea swichi ya umeme iliyokuwa ukutani jirani na kile kiti na kugeuza shingo yake kunitazama akiwa amekunja uso wake. “Hii ni nafasi yako ya mwisho, tuambie ni nini kinaendelea huko Shamba na walimu wako wanaitwa akina nani?”

“Sijui chochote,” nilisema kwa hasira.

Yule komando aliachia tabasamu la kifedhuli kisha akapeleka mkono wake kwenye ile swichi ya umeme lakini kabla hajaigusa nikasikia sauti ya mtu mwingine ikisema, “Basi usiwashe, naamini sasa yupo tayari kusema ukweli.”

Niligeuka kumtazama mtu aliyesema maneno hayo na kumtambua, alikuwa ni Meja Saleh bin Awadh. Sikujua alikuwa ameingia saa ngapi mle ndani.

“Unajua, hawa jamaa wanataka kukuua lakini sipendi wafanye hivyo, ila kama utaendelea na msimamo wako kwa kweli sitasita kuwaruhusu wafanye hivyo,” Meja Saleh bin Awadh aliongea kwa namna ya kunishi. Lakini bado sikuwa tayari kufungua mdomo wangu na kuwaeleza walichokuwa wanakitaka.

“Wakati mwingine jifunze kuwa na adabu kwani jeuri haitakusaidia kitu hapa,” Meja Saleh bin Awadh alifoka baada ya kuniona nipo kimya.

“Sawa… lakini jibu langu litabaki kuwa lile lile kuwa, sijui chochote,” nilimwambia huku nikiwatazama wote kwa hasira.

“Kumbe wewe jeuri sana, basi Sajenti endelea na kazi yako,” Meja Saleh bin Awadh alimwambia yule komando mweusi.

Muda huo huo nikamwona yule komando mweusi akiibonyeza ile swichi ya umeme pale ukutani, mara nikaanza kupigwa shoti kali ya umeme iliyonitetemesha mwili mzima, nikahisi miale mikali sana ya moto wa umeme ikinishtua kisha ikaanza kutambaa na kusambaa haraka sana mwilini mwangu. Nilijikuta nikiwa katikati ya maumivu makali sana yasiyoelezeka ambayo sijawahi kuyahisi maishani mwangu yakitambaa mwili mzima, mwili wangu wote ulikuwa unatetemeka huku nikitokwa na jasho jingi.

Nilishindwa kuvumilia nikaanza kupiga kelele kama niliyekuwa nimepigiliwa msumali utosini, hali yangu ilianza kuwa mbaya sana.

“Basi mwache!” Meja Saleh bin Awadh alimwambia yule komando, “nadhani sasa yupo tayari kutwambia.”

Muda huo huo yule komando akabonyeza ile swichi ili kuizima, na hapo nikahisi ahueni kidogo, hata hivyo nilijihisi kizunguzungu kikali sana huku nikihisi kutaka kutapika.

Okay, nadhani maswali yetu mawili unayafahamu, tunasubiri majibu yako,” Meja Saleh bin Awadh alisema huku akinikazia macho.

“Sijui chochote,” nilimwabia huku nikimtazama kwa hasira na hapo nikamwona akitabasamu.

“Sajenti, endelea na kazi,” Meja Saleh bin Awadh alimwambia yule komando mweusi, ile swichi ikawashwa tena.

Nilihisi tena miale mikali sana ya moto wa umeme ikinishtua na kuanza kusambaa haraka sana mwilini mwangu, nikapiga yowe kali nikiwasihi waniache na wakati huo nikawa nikiisikia sauti yangu namna ilivyokuwa ikisafiri na kutengeneza mwangwi kwenye kuta za kile chumba.

Niliendelea kupiga yowe huku kile kizunguzungu kichwani kikizidi kuongezeka na hatimaye nikaacha kupiga yowe kwani nilihisi kuishiwa nguvu lakini yule komando hakuonesha kujali kwani alisimama akinitazama tu huku akitabasamu. Yale mateso yaliendelea zaidi hadi pale nilipoonekana kuanza kuishiwa na nguvu ndipo alipoizima ile swichi.

Endelea...
 
ufukweni mombasa.JPG

222

Kisha alisogea akasimama mbele yangu, akanitazama kwa kitambo na kuongea kwa sauti ya chini kama aliyekuwa akininong’oneza. “Afadhali utuambie ukweli, tupo tayari kukubadilishia mtindo endapo huu utaonekana haukufai.”

“Sijui chochote,” niliendelea kusisitiza japo sauti yangu ilikuwa dhaifu.

“Unajua kila kitu, usitudanganye,” Meja Saleh bin Awadh alisema kwa kufoka.

“Ningekuwa najua ningewaambia, au mnadhani nayafurahia haya mateso?!” nilisema kwa sauti ya unyonge iliyokuwa ikitia huruma.

“Nadhani umedhamiria kufa kiume, kufa na siri moyoni… usijali, tunayo njia nyingine itakayokulazimisha kuongea,” Meja Saleh bin Awadh aliniambia huku akiachia tabasamu la kifedhuli. Kisha akaongeza, “Achana na porojo mnazofundishana huko kwenye ujasusi kwamba ukikamatwa hata ukisema ukweli adhabu yako bado itabaki pale pale. Mimi nakuahidi kama utaonesha ushirikiano utaachiwa huru.”

Sikusema kitu bali nilibaki kimya huku nikimtazama kwa hasira kwani nilishachoshwa na maswali yao ambayo nilikwisha kata shauri kuwa kamwe nisingeyajibu hata kama nigelazimika kupoteza uhai wangu. Hata hivyo hali yangu ilikuwa mbaya sana.

Meja Saleh bin Awadh alishusha pumzi ndefu huku akinitazama kwa tabasamu na baadaye tabasamu lake liligeuka kuwa kicheko. Kisha akasema, “Nadhani anahitaji kubadilishiwa burudani.”

Mara nikawaona wale makomando wakinisogelea kwa ukakamavu mkubwa, na kwa haraka sana wakanifungua zile pingu zilizokuwa zimefungwa kwenye mikono na miguu yangu pale kwenye kile kiti cha umeme kilichotumika kunisulubu. Kisha wakanishika miguu yangu na kunivuta wakinishusha kwa nguvu kutoka pale kwenye kile kiti hali iliyonifanya nitue sakafuni kwa matako na kunifanya nisikie maumivu makali sana yaliyosambaa mwili mzima.

Nilijaribu kujitetea lakini ilikuwa kazi bure kwani walianza kunishushia kipigo cha mateke mwilini mwangu na kujikuta nikiishiwa na nguvu na kulala sakafuni kama mfu. Kisha waliporidhika kuwa kile kipigo kilikuwa kimenilegeza kiasi cha kutosha, wakaanza kuniburuza kibabe kuelekea kule kwenye lile tangi kubwa lililojengwa kwa vioo ambalo ndani yake lilikuwa limejazwa maji.

Walinibwaga pale chini jirani na lile tangi la maji. Nikiwa pale chini nikihema kwa nguvu kutokana na kile kipigo, nilimwona Meja Saleh bin Awadh akinisogelea taratibu huku wale makomando wakinizunguka na hapo nikafungwa kamba mikononi.

“Nadhani hutopenda hiki kinachofuata…” Meja Saleh bin Awadh alininong’oneza sikioni, nikamkata kauli.

“Hata uniambie nini, sijui chochote…” wakati nasema hivyo nikakatishwa na kipigo cha mateke ya mgongoni, kabla sijajua nifanye nini mara nikajikuta nikibebwa mzobe mzobe na wale makomando na kurushiwa ndani ya lile tangi la maji. Matukio yote yale yalifanyika kwa haraka sana.

Nikajua sasa walikuwa wamedhamiria kunitesa kwa kunizamisha ndani ya lile tangi la maji kwa kufungulia umeme ulioungwa ndani ya lile tangi la maji ili kunipiga shoti mbaya na ikiwezekana kuniua kabisa. Nilizifahamu mbinu za aina hii za ukatili na utesaji kwa kuwaweka kwenye maji watuhumiwa hasa magaidi, kuwakosesha usingizi, kuwapiga shoti ya umeme na kila aina ya utesaji ili kupata siri kutoka kwao.

“Twambie, au niwaruhusu waendelee na adhabu. Nadhani unajua kitakachokutokea,” Meja Saleh bin Awadh aliniambia huku akinikazia macho.

“Sijui chochote,” nilisema nikiwa nimeshajiandaa kufa. Muda huo nilikuwa nimesimama ndani ya tangi na yale maji yaliishia usawa wa kifua changu.

Nikiwa sijui kilichokuwa kinaendelea ghafla nikapigwa shoti kali ya umeme iliyonitetemesha mwili mzima huku nikihisi ngozi yangu ikiunguzwa na moto wa umeme uliokuwa ukisambaa haraka sana mwilini mwangu. Nikajikuta nikiwa katikati ya maumivu makali sana yasiyoelezeka, nikaanza kutetemeka kama niliyekumbwa na kifafa.

Nilifumbua mdomo wangu kupiga kelele za kumwomba Meja Saleh bin Awadh awaambie makomando wake wasitishe yale mateso lakini sauti yangu haikuweza kutoka, kila nilipopiga kelele niliisikia sauti yangu ikiishia ndani ya akili yangu. Nikaanza kujiona nikipaa angani kwa kasi ya ajabu sana, na nilipofika juu zaidi nikaanza kushuka chini kwa kasi ile ile na kisha nikatumbukia kwenye shimo refu sana lililokuwa na kiza kilichotisha.

Na mara giza zito likatanda kwenye mboni zangu za macho huku taratibu nguvu zikianza kuniishia na mwili wangu ukilegea, mapigo yangu ya moyo nayo yakaanza kudorora, mwishowe nikahisi roho yangu ikifika njia panda. Kisha nikawa kama mtu niliyekuwa umbali mrefu sana angani nikianguka kwa kasi sana kuelekea ardhini nikiwa nimetanguliza kichwa…

* * *



Nilishtuka na kuamka kutoka kwenye usingizi mzito wa kifo baada ya kuhisi mkono wa mtu ukinigusa kwenye paji langu la uso wangu. Niliyafumbua macho yangu taratibu kisha nikageuza shingo yangu kutazama upande ulikotokea ule mkono na kumwona mwanamume mnene na mrefu akiwa amesimama huku akinitazama kwa makini.

Kwa haraka niliweza kugundua kuwa alikuwa na umri wa kati ya miaka 40 na 45, alikuwa Mwarabu na alikuwa na misuli imara ya mikononi iliyotuna kikamilifu. Uso wake ulikuwa mpana na alikuwa amevaa miwani mikubwa iliyoyahifadhi macho yake makubwa. Alivaa suruali ya khaki, shati la samawati na juu yake alivaa koti refu jeupe la kidaktari, shingoni alining’iniza kifaa cha kupimia mapigo ya moyo ambacho kitaalamu kiliitwa stethoscope.

Kisha niliyazungusha macho yangu haraka haraka na hapo nikagundua kuwa nilikuwa juu ya kitanda cha chuma ndani ya chumba kidogo bila dirisha. Upande wa kushoto wa kile kitanda kulikuwa na meza ya mbao iliyokuwa na beseni dogo la chuma lenye vifaa vyote muhimu vya tiba. Pia kulikuwa na stendi ndefu ya chuma ya kitabibu iliyotundikiwa chupa mbili za dripu, chupa moja ya dripu ya maji na nyingine dripu ya damu.

“Unajisikiaje?” yule daktari aliniuliza baada ya kugundua kuwa nimeamka, hata hivyo sauti yake ilikuwa ya chini kana kwamba hakutaka watu wengine wasikie alichokuwa akiongea.

Kwanza nilibaki kimya nikimtazama kwa umakini, nilijiuliza niko wapi na nini kilikuwa kinaendelea kisha nikashusha pumzi za ndani kwa ndani huku nikimeza mate kuitowesha hofu ndani yangu.

“Hata sielewi ila mwili unaniuma sana,” nilimwambia kwa sauti tulivu huku nikimtazama kwa umakini.

“Usijali, kila kitu kitakuwa sawa,” yule daktari alisema huku akitoa mashine ndogo ya kupimia shinikizo la damu na mapigo ya moyo. “Nahitaji kuangalia mwenendo wa presha na mapigo ya moyo wako…”

Kisha aliifunga ile mashine kwenye mkono wangu wa kushoto halafu akaanza kuipampu kwa muda. Niliyafumba macho yangu huku nikibana pumzi kutokana na ile mashine kuanza kubana kwenye mkono wangu na kusababisha maumivu kidogo. Baada ya kitambo fulani yule daktari alianza kulegeza taratibu kifungo fulani kidogo kilichokuwa pembeni, mara nikasikika sauti ya ‘hisssiii’. Kisha nikamwona akiweka rekodi kwenye faili alilokuwa nalo mkononi.

“Samahani daktari, hivi hapa nipo wapi?” nilimuuliza huku hofu ikinitambaa taratibu.

Yule daktari alinitazama kwa kitambo pasipo kusema neno halafu akashusha pumzi za ndani kwa ndani. Sikuona tashwishwi yoyote usoni kwake. Nikiwa bado nasubiri jibu lake mara nikashuhudia kitasa cha mlango wa kile chumba kikizungushwa taratibu na kisha ule mlango ukasukumwa kwa ndani na kufunguka.

Niligeuza shingo yangu haraka kutazama upande ule nikamwona Meja Saleh bin Awadh akiingia mle chumbani akiwa ameongozana na mtu mwingine ambaye sikumfahamu. Alikuwa kipande cha mtu, amekwenda hewani kisawa sawa. Sikuweza kutambua mara moja asili yake ila hisia zangu zilinitabanaisha kuwa kama hakuwa Mpalestina au Mlebanon basi alitoka Syria. Sura yake ilikuwa ngeni kabisa machoni mwangu na alikuwa amevaa kiraia, suti ya rangi ya samawati, ila nilipomchunguza vizuri kwa jicho la kishushushu nikajiridhisha kuwa yeye pia alikuwa askari komando wa daraja la juu. Alikuwa na sura ya kazi na hakuonekana kuwa rafiki.

Meja Saleh bin Awadh na yule komando Mpalestina, kama nilivyoamua kumwita, wakanitazama kwa umakini pale kitandani huku wakionekana kuridhishwa na maendeleo ya afya yangu. Kisha Meja Saleh bin Awadh akamwambia yule daktari. “Leo itawezekana kumchukua tena kwa mahojiano mafupi?”

“Hali yake bado haijatengamaa vizuri, labda kesho jioni.” yule daktari alijibu huku akinitazama usoni.

“Jana nilikuuliza ukaniambia leo, hivi kweli uko makini na kazi yako, daktari? Kumbuka leo ni siku ya nne tangu awepo hapa na hatuna muda wa kupoteza!” Meja Saleh bin Awadh alisema kwa kufoka.

“Lakini nilisema vile nikitegemea afya yake ingekuwa imeimarika zaidi, hebu mpeni siku moja zaidi…” yule daktari alisema.

“Sikiliza daktari, fanya ufanyavyo tunataka kumhoji mtu huyu leo jioni, hatuna muda na mtu huyu anazo taarifa muhimu sana tunazozihitaji,” Meja Saleh bin Awadh alisisitiza huku akinitazama usoni kwa hasira.

“Sawa, nitajitahidi,” daktari alisema kwa sauti ya kukata tamaa. Kisha kama mtu aliyekumbuka jambo akafungua droo ya meza iliyokuwepo kando ya kile kitanda na kutoa chupa ya chai na bakuli la plastiki.

Halafu aliifungua ile chupa na kumimina uji mwepesi wa mchele kwenye lile bakuli, akanipa. Nililipokea lile bakuli na kuanza kuunywa ule uji wa mchele. Ulikuwa uji wa moto kiasi na mtamu sana kwa kuwa ulitiwa karanga zilizosagwa. Kwa kuwa nilikuwa na njaa niliubugia wote kwa muda mfupi kisha yule daktari akanijazia tena, nao nikaumaliza na kumshangaza kila mtu mle ndani. Muda huo Meja Saleh bin Awadh na yule komando Mpalestina walikuwa wananitazama tu pasipo kusema neno.

“Sasa pumzika, naamini utapata nafuu,” yule daktari alinisisitiza huku akiwatupia jicho wale maofisa, na hapo Meja Saleh bin Awadh akampa ishara kuwa wote waondoke na kuniacha, wakatoka nje ya kile chumba na kufunga mlango wakiniacha peke yangu.

* * *

Endelea...
 
Back
Top Bottom