253
“Nikawafuata hadi hapa Serena Beach Resort na nikakushuhudia ukishuka na kupokewa na wahudumu wa hoteli. Baada ya kuhakikisha kuwa upo salama nikaondoka huku nikisubiri kuona kama ungenipigia simu kunijulisha kuhusu uwepo wako ndani ya jiji letu, lakini haikuwa hivyo hadi sasa.”
Nilimtazama Leyla kwa umakini machoni, nikajikuta nikiyatazama macho ya msichana mweledi, mwerevu, mjanja na mpelelezi aliyekomaa kiupelelezi. Nikapiga funda moja la whisky na nilipoiweka bilauri mezani nikamudu kusema neno moja tu. “Dah!”
Muda wote wakati Leyla akinisimulia mwili wangu ulikuwa unasisimka kwa hofu. Nilianza kujilaumu kwa kutokuwa makini. Nikajiuliza vipi kama ni Zuena wa Mombasa ndiye angekuwa akinifuata kwa nia ya kunidhuru? Kwa vyovyote asingeshindwa kunimaliza kwa kuwa sikuwa makini kabisa.
“Leo kumekucha nikaendelea kusubiria simu yako lakini uvumilivu ukanishinda na hivyo nimeamua kuja mwenyewe nikufanyie
surprise. Uzuri hapa hotelini wengi wananifahamu hivyo haikuwa ngumu kupata taarifa zako na kujua upo chumba namba ngapi,” Leyla akahitimisha maelezo yake na kunifanya nihisi kuchoka kabisa.
“Kweli hii ni bonge ya
surprise!” nilisema katika hali ya kukata tamaa na hivyo kusababisha kicheko toka kwa Leyla. Nami nikacheka.
“Najua ulipanga kunifanyia
surprise badala yake mimi ndo nimeku-
surprise,” Leyla alisema kwa utani huku akiendelea kucheka. Tukacheka pamoja na mara kicheko kilipokatika Leyla akaniuliza, “Hujanimbia lengo la ujio wako hapa Mombasa. Sidhani kama ulipanga kuja kunitembelea tu.”
Nilishusha pumzi huku nikitafakari haraka haraka kama nimwambie ukweli juu ya kile nilichokibaini au nimfiche. Sauti fulani ndani yangu ikanisisitiza kumwambia. Nikashusha tena pumzi na kusema, “Ni kweli lengo langu lilikuwa kuja kukutembelea na kupumzisha akili yangu lakini tangu nimefika hapa mambo fulani yenye utata yamejitokeza, na hivyo nahitaji sana msaada wako, Leyla,” nilisema kwa sauti ya chini.
Kisha nilianza kumsimulia Leyla mkasa wote tangu nilipokutana na Rahma wa Singida katika Benki ya NBC Posta jijini Dar es Salaam, nilivyowafuatilia yeye Abshir hadi Lamada Hotel, walivyotoweka kisha akaibuka Zuena wa Mombasa aliyejinadi kuwa mwanamitindo, hadi tukio la kurushiana risasi lililotokea asubuhi ya siku hiyo muda mfupi kabla hajafika hapo Serena Beach Resort.
“Ni dhahiri kuna jambo tusilolijua linaloendelea hapa Kenya. Tunapaswa kuhakikisha tunazijua mbivu na mbichi…” nilimwambia Leyla, ambaye muda wote alikuwa ametulia tuli, hatingishiki, haongei wala hapepesi macho yake.
Kabla sijamwonesha zile picha za video nilizozidukua kutoka kwenye mfumo wa kamera za ulinzi pale hotelini nilimpa asome ule ujumbe wa vitisho nilioukuta pale mapokezi. Leyla aliusoma na kuachia tabasamu lililomaanisha kuwa mtumaji wa ujumbe huo alikuwa mtu mwoga. Kisha nikamwonesha zile picha za video kutoka kwenye kamera za ulinzi za pale hotelini ambazo nilizihifadhi kwenye Ipad yangu.
Leyla alizitazama picha zile kwa umakini na mara kadhaa alionekana kuyarudisha matukio nyuma akijaribu kujiridhisha na kile alichokuwa akikiona, na jinsi alivyoendelea kuzitazama ndivyo uso wake ulivyozidi kukumbukwa na fadhaa. Hadi anamaliza kuzitazama alikuwa ametahayari sana. kilichokuwa kimeshtua zaidi ni kuwaona Zuena wa Mombasa na yule mwanamume mwenye macho kama ya nyoka.
“Miriam!” Leyla alimaka kwa mshangao mkubwa baada ya kuigandisha sura ya Zuena wa Mombasa na kuitazama kwa makini. Kisha kwa sauti ya upole huku akionesha masikitiko akaniambia, “Dah! Jason, kwanza pole sana kwa masaibu yaliyokukuta.”
“Ahsante. Kwa kweli kama si Mungu pengine ungesikia nimekufa,” nilisema huku nikinyanyua bilauri yangu na kunywa mvinyo. “Kwani unamfahamu huyo dada?”
Leyla alibetua kichwa chake kukubali kisha akashusha pumzi ndefu kama aliyetoka kumaliza mashindano ya mbio ndefu. “
Yeah… anaitwa Miriam Mutua, ofisa wa Usalama wa Taifa. Kinachonichanganya ni vipi anahusiana na suala hili?”
Nilishusha pumzi za ndani kwa ndani huku nikiitazama vizuri picha ya Miriam Mutua ambaye mimi nilimfahamu kama Zuena wa Mombasa.
“Kwani ni mtu wa aina gani hasa?” nilimuuliza Leyla ili kutaka kumfahamu kiundani Miriam hasa nikikumbuka jinsi ambavyo hisia zangu ziliniambia kuwa hakuwa mtu wa kuaminika na ndiyo maana nilikuwa makini naye sana.
Kwanza Leyla alishusha pumzi za ndani kwa ndani kisha akainamisha uso wake chini huku akikunja sura yake kama aliyekuwa anajaribu kufikiria kwa kina, halafu akainua uso wakie kunitazama. “Ni mtu mcheshi sana, mtiifu na mchapakazi hodari, huwezi hata kumdhania kama anaweza kuwa na mambo kama haya! Mimi ndiye niliyemfundisha mambo mengi jinsi ya kufanya kazi kwani yeye mmoja wa ya vijana ambao hawana miaka mingi katika idara ya ujasusi lakini ameshaonesha uwezo mkubwa katika kazi.”
“Na vipi kuhusu maisha yake nje ya kazi? Anapenda maisha ya juu!” nilimuuliza Leyla huku nikimtazama usoni.
“
Obviously! Kama msichana wa kileo, anapenda sana maisha fulani
classic, you know what I’m saying…” Leyla alinijibu
“Basi sishangai yeye kuwemo kwenye sakata hili…” nilimwambia Leyla. “Najua wapo baadhi ya maofisa wanashirikiana kwa karibu sana na wahaini na wanalipwa mamilioni ya fedha kuvujisha siri za kiusalama. Kwa Miriam kuwa wakala wa mtandao wa kihaini ni jambo la kawaida katika mashirika ya kijasusi duniani.”
“Ni kweli… lakini kingine kinachonishangaza ni kuwepo kwa Abdoulkader Omar hapa Kenya na kuhusika kwenye sakata hili!” Leyla alisema. Nikamdaka juu kwa juu.
“Abdoulkader Omar ndiye nani?” nilimuuliza Leyla kwa shauku.
“Ni huyo mwenye macho kama ya nyoka. Ni mfanyabiashara mkubwa sana ila wengi hapa Kenya hawamfahamu. Ana kampuni inayoitwa
Obock Enterprises Limited ambayo inajishugulisha na kujenga viwanda, kusafirisha watalii, kusafirisha bidhaa nje na kuingiza toka nje, na maduka ya kibao kubadili fedha. Ofisi yao kuu ipo Djibouti, na hapa Kenya wana matawi Nairobi na Mombasa.”
“Vipi kuhusu rekodi yake, inatia shaka?” nilimuuliza kwa shauku.
“Mmh! Abdoulkader hana rekodi yoyote chafu, kampuni yake imekuwa inatoa sana misaada hapa Kenya kwa walemavu, akina mama na vijana. Na inasemekana yeye ana undugu na Rais wa Djibouti, Khaleed bin Jamal. Pia kampuni yake ilimsaidia sana Rais wa sasa wa Kenya kushinda uchaguzi,” Leyla alisema na kuongeza, “Hata hivyo bado si sababu ya kumwona hata tatizo kwani naelewa kuwa mfanyabiashara yeyote mkubwa hawezi kukosa makondokando.”
“Basi yote yatajulikana muda si mrefu, ngoja niingize taarifa zake kwenye mfumo maalumu wa utambuzi wa programu ya TracerMark,” nilimwambia Leyla huku nikifungua mfumo huo kisha nikaingiza sura na jina la Abdoulkader Omar.
Baada ya kubonyeza hapa na pale huku nikifungua
code hizi na kuingiza
code zile hatimaye pale nilipopataka pakafunguka na taarifa za kiintelijensia zilizoandaliwa na mashirika ya kijasusi ya Mosad (Israel) na CIA (Marekani) kumhusu Abdoulkader zikatokea.
Inandelea...