Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

ufukweni mombasa.JPG

249

Muda mfupi uliofuata nilikuwa nimeliacha lile eneo la mapokezi na kushika uelekeo wa upande wa kushoto huku nikiyapeleka macho yangu darini kuzitazama kamera za CCTV zilizofungwa mle ndani ya jengo la hoteli kwa ajili ya usalama. Kuna jambo lilikuwa linanisukuma nilifanye kuhusu zile kamera na hivyo nikapanga kulifanya mara tu nikiingia chumbani kwangu.

Safari hii sikutaka kutumia lifti na hivyo nikaelekea kwenye ngazi. Nilikwenda mbele kidogo kisha nikaingia upande wa kulia na baada ya kuupita mlango mkubwa wa kuelekea sehemu ya maliwato uliokuwa upande wa kulia hatua chache mbele yangu nikaziona ngazi za kuelekea orofa za juu za lile jengo.

Nikapishana na wazungu watatu, wanaume wawili na mwanamke mmoja waliokuwa wakishuka ngazi, wakanisalimia na kushika hamsini zao. Nikaanza kuzikwea zile ngazi haraka haraka huku nikiwa na tahadhari zote, mawazo mengi yaliendelea kupita kichwani mwangu.

Nilipofika katika orofa ya pili nikaanza kutembea taratibu katikati ya ukumbi nikiyatembeza macho yangu upande huu na ule kutazama huku kidole changu cha shahada kikiwa tayari kimetuama vyema kwenye kilimi cha bastola yangu ndani ya mfuko wa suruali yangu. Nilipofika karibu na mlango wa chumbani kwangu nikasimama na kupima hali ya usalama katika eneo lile. Na wakati huo huo nikamwona mhudumu mmoja wa kike akitoka katika chumba cha jirani akiwa amebeba mashuka. Akanisalimia kwa heshima zote na kuendelea na shughuli zake.

Nilimtazama kwa umakini yule mhudumu katika namna ya kumchunguza ili kuhakikisha kuwa hakuwa mtu hatari kwangu au kujua chochote au kama alikuwa anafuatilia nyendo zangu, sikuona kama alitambua chochote. Hadi wakati huo nilijikuta nikiwa simwamini yeyote, hata mtoto mchanga.

* * *



Saa 2:45 asubuhi…

Nilipoingia ndani ya chumba changu ilikuwa imeshatimia saa tatu kasorobo asubuhi, niliingia baada ya kujiridhisha na hali ya usalama ndipo nikaufunga ule mlango nyuma yangu na kusimama katikati ya chumba nikitathmini vizuri mandhari ya mle ndani. Nilizunguka mle ndani kwa utulivu kukipeleleza vizuri kile chumba kabla sijaamua kukikagua katika kila pembe na sehemu niliyodhani ingeweza kutegeshwa kifaa chochote.

Nilipohakikisha kila kitu kiko salama nikachukua Ipad yangu iliyokuwa na programu maalumu ya utambuzi ya TracerMark na kwenda kuketi kwenye sofa huku nikifikiria juu ya hili na lile. Katika safari hiyo ya Mombasa nilikwepa kusafiri na tarakilishi mpakato (laptop) na badala yake nikachukua ile Ipad. Zote zilikuwa na uwezo mkubwa katika kufanya kazi na ziliwekwa programu hiyo ya utambuzi ya TracerMark. Na hata simu yangu aina ya Iphone 13 Pro pia ilikuwa na mfumo huo wa utambuzi.

Nikiwa nimeketi pale kwenye sofa mawazo mengi yakawa yanapita kichwani mwangu. Nilianza kuhisi uchovu mwingi mwilini na hivyo nikainuka na kulifuata jokofu lililokuwemo mle chumbani, nikalifungua na kutoa chupa kubwa ya Grant’s Blended Scotch Whisky na bilauri, kisha nikajimiminia mvinyo na kurudi kuketi pale kwenye sofa.

Kitu cha kwanza nilichofanya baada ya kupiga funda kubwa la mvinyo ni kuifungua bahasha ile na humo ndani nikakuta kijikaratasi kidogo chenye maandishi mekundu ya ujumbe wa vitisho:

Ujumbe wa kifo:

Acha kufuatilia mambo yasiyokuhusu na urudi kwenu Tanzania vinginevyo utakipata unachokitaka. Sikutishi ila nakuonya kwani huelekei kufahamu uzito wa matokeo ya hicho unachokitafuta
.

Ujumbe ule haukuonesha ni wapi ulitoka wala mwandishi wake. Hata hivyo nilifahamu kuwa kama mwanzoni nilidhani ni hisia tu sasa kazi ilikuwa imeanza rasmi. Mambo sasa yalianza kuwa moto kwani ni kama vile nilikuwa nimetupa jiwe kichakani na likawapata watu ambao sasa waliamua kujitokeza rasmi huku wakipiga mayowe ya maumivu.

Kwa kifupi ujumbe ule haukunitisha kabisa ila ulidhihirisha jinsi ambavyo wahusika walivyokuwa waoga kwa sababu kwa mtu yeyote jasiri angeamua kupambana badala ya kuniletea ujumbe wa vitisho ili kunifanya niogope na nisiendelee na harakati zangu za kulifumbua fumbo hilo lenye utata.

Nilikirudisha kile kipande cha karatasi kwenye bahasha yake na kuiweka kando kisha nikaiwasha Ipad yangu na kuingiza code maalumu za kuifanya ifunguke. Halafu nikafungua mfumo maalumu wa utambuzi wa TracerMark na kuanza utundu wangu. Niliingia hapa na kubofya hiki na kile kisha nikaingiza code fulani na muda mfupi uliofuata nikawa nimeshazidukuwa kamera zote za usalama za lile jengo la hoteli huku tabasamu pana likiupamba taratibu uso wangu.

Utundu wangu katika kucheza na mifumo ya kiusalama ulikuwa wa kiwango cha juu. Nilipofanikiwa kuzidukua zile kamera za ulinzi katika jengo nikawa kama niliyeingia kwenye chumba maalumu chenye tarakilishi inayoongoza mfumo mzima wa zile kamera za CCTV, na nilikuwa najua ni wapi ningeweza kuzipata taarifa nilizozihitaji.

Hivyo sikupoteza muda. Nilianza kwa kuzipitia picha zote za video zilizokuwa zimenaswa na kamera ya ukumbi wa orofa ya pili kuelekea kwenye chumba changu ili kuona kama kulikuwa na yeyote aliyejaribu kuingia chumbani kwangu. Picha karibu zote nilizoziona zilikuwa za kawaida nikishuhudia mlolongo wa picha za wateja katika vyumba hivi wakiingia na kutoka kwenye vyumba vyao. Halafu nikajiona wakati nikitoka kuelekea kwenye ukumbi wa chakula.

Muda mfupi tu baada ya kutoka chumbani kwangu ikaja picha ya mwanamke aliyevaa niqab ambaye sasa nilimtambua mara moja kuwa ni Rahma wa Singida akitoka katika chumba cha tatu kutoka kilipokuwa chumba changu na kutupa macho yake mara moja tu kutazama kwenye mlango wa chumba changu kisha akaelekea kwenye lifti.

Dakika moja baadaye akatokea mwanamume mmoja mrefu ambaye sikuweza kumtambua mara moja, alitoka ndani ya chumba kile kile alichotoka Rahma na kutazama kwenye mlango wa chumba changu kwa umakini sana. Alikuwa amevaa sweta jeusi lililounganika na kofia na suruali nyeusi ya dengrizi. Alisimama kwa sekunde chache mlangoni kwake akitazama mlango wangu kama aliyekuwa akijiuliza jambo kuhusu mlango wangu lakini akaghairi na kuelekea kilipo chumba cha lifti. Kisha sikuona chochote cha maana kwenye mlolongo huo wa picha.

Nikahamia kwenye zile kamera mbili za kule nje, mbele ya jengo la hoteli. Hapo nikakutana na picha za lile tukio la kushambuliwa kwa risasi na mtu aliyekuwa ndani ya gari aina ya Toyota Crown jeusi lenye vioo vyeusi visivyoonesha waliomo ndani. Mwili wangu ukanisisimka sana niliposhuhudia tukio lile hasa kitendo cha kuchupa na kujitupa chini kwenye maua huku risasi zikipita sentimita chache kutoka kilipokuwa kichwa changu na kupurura maua. Ilikuwa ni kama nilikuwa natazama filamu ya kusisimua.

Nikaamua kurudisha matukio nyuma zaidi ili nione wale watu walionishambulia walifikaje pale hotelini kabla ya tukio husika. Kwa kupitia kamera hizo nilishuhudia mlolongo wa picha za wafanyakazi na wateja walioingia na kutoka kwenye jengo la hoteli ile pamoja na magari yaliyofika na kuegeshwa eneo la viunga vya maegesho ya magari kwa kwa nyakati tofauti.

Picha karibu zote nilizoziona pale nje ya jengo zilikuwa za kawaida kabisa. Nilipokuwa mbioni kukata tamaa hatimaye nikakiona kile nilichokuwa nikikitarajia. Gari dogo aina ya Toyota Verossa la rangi nyeusi lenye vioo vyeusi visivyomwonesha aliyemo ndani ya gari hilo lilinaswa na kamera zile likiingia na kutafuta maengesho yake nje ya lile jengo la hoteli.

Inaendelea...
 
ufukweni mombasa.JPG

250

Niliitazama kwa umakini ile picha ya video na kuna wakati niliirudisha nyuma ianze upya huku macho yangu yakisafiri taratibu sambamba na tukio lile. Kupitia ile picha ya video sasa nilimwona mdada mmoja mrembo akishuka haraka toka kwenye lile gari aina ya Toyota Verossa jeusi. Nikanakiri namba za gari lile.

Alikuwa mweupe kama ilivyokuwa kwenye maelezo ya yule mfanyakazi wa mapokezi, na alivaa suruali ya jeans ya bluu iliyombana kulionesha vyema umbo lake. Juu alivaa pullneck nyeusi na kichwani alijifunika na mtandio na mweusi huku miwani mikubwa myeusi ikiyafunika macho yake. Miguuni alivaa viatu aina ya Travolta. Alitembea haraka akielekea ndani ya jengo la hoteli huku akiangaza huku na kule kama aliyekuwa anatafuta kitu.

Tukio lile likaufanya moyo wangu upige kite kwa nguvu na koo langu likakauka ghafla. Niliirudisha nyuma ile picha ya video kwa mara ya pili na kuivuta ile sura ya huyo mdada ili kuitazama vizuri sura yake na hapo nikawa nimeridhika na uchunguzi wangu.

Baada ya tukio lile kulikuwa na picha nyingine za video za magari mawili kuingia na moja kutoka huku wafanyakazi wakiwa katika pilika pilika za usafi wa eneo lile zilizonaswa na zile kamera za ile hoteli na zote zile zilikuwa za kawaida tu. Dakika mbili baadaye nikamwona tena yule mdada aliyeshuka kwenye lile gari jeusi aina ya Toyota Verossa akitoka sehemu ya chini ya jengo la ile hoteli na kuelekea moja kwa moja kwenye gari lake ambapo aliingia na kuondoka haraka toka eneo lile.

Wakati gari lile aina ya Toyota Verossa likiondoka lilipishana na gari lingine aina ya Toyota Crown jeusi ambalo pia lilikuwa na vioo vyeusi visivyomruhusu mtu kuona waliomo ndani ya gari, lililokuwa linaingia pale. Mara moja nikalitambua gari hilo kuwa ni lile lililokuwa na watu walionishambulia kwa risasi muda mfupi uliokuwa umepita. Nikanakiri namba za gari.

Lile Toyota Crown jeusi lilipofika katika viunga vya maegesho ya magari pale hotelini likasimama na baada ya takriban dakika mbili mlango wa dereva ukafunguliwa kisha akashuka mwanamume mmoja mrefu mwenye asili ya Kisomali akiwa amevaa mavazi ya gharama, suti nzuri ya kijivu ya pande tatu brand ya Brioni Vanquish ambayo bila shaka ilimgharimu fedha nyingi sana, ambazo zingetosha kabisa kujenga nyumba ya maana Uswahilini. Pia alikuwa amevaa saa ya thamani kubwa aina ya Rolex Submariner.

Alianza kupiga hatua kuelekea ndani ya jengo la hoteli akiwa ameshika funguo za gari akizungusha kwenye kidole chake cha shahada. Mara moja nikamtambua kuwa ni yule mwenye macho kama ya nyoka. Sikuona mtu mwingine kushuka toka ndani ya lile gari na hivyo nikatambua kuwa alikuja peke yake.

Kisha ulifuata tena mlolongo wa picha za wafanyakazi na wateja walioingia na kutoka kwenye jengo la hoteli ile. Na baada ya dakika chache nikamwona tena yule mwanamume mwenye macho kama ya nyoka akitoka sehemu ile ya chini ya jengo la hoteli huku akiongea na simu na kuelekea moja kwa moja kwenye gari lake. Alipofika akaingia ndani ya lile gari na kutulia.

Muda mfupi baadaye mwanamume mwingine mrefu aliyekuwa amevaa sweta jeusi lililounganika na kofia na suruali nyeusi ya dengrizi akatoka sehemu ile ya chini ya jengo la hoteli na kufika hadi pale jirani na lile gari aina ya Toyota Crown jeusi. Nilimtambua kuwa ni yule mwanamume aliyetoka kwenye chumba cha tatu cha orofa ya pili jirani na kilipo chumba changu.

Alikuwa amebeba begi dogo la mgongoni na akasimama huku akitazama huku na kule kama aliyekuwa anatafuta kitu ingawa niliamini alikuwa anataka kuhakikisha kama kulikuwa na mtu aliyekuwa anafuatilia nyendo zake. Aliporidhika kuwa hali ilikuwa shwari akafungua haraka mlango wa nyuma wa lile gari aina ya Toyota Crown jeusi na kuzama ndani.

Nilirudia kuitazama picha ile ya video kwa mara ya pili na kuivuta sura ya yule mwanamume, na hapo nikamtambua kuwa ni Abshir. Sasa nikajua kuwa nilikuwa nimepiga hesabu zangu vizuri, na kujikuta nikitabasamu. Kisha nikaupitisha ulimi wangu kulamba midomo yangu iliyokauka huku nikiendelea kutabasamu.

Baada ya tukio lile kulikuwa na mlolongo mwingine wa picha za wafanyakazi na wateja waliokuwa katika pilika pilika. Sikuona kama zilikuwa muhimu kwangu. Muda wote lile gari aina ya Toyota Crown lilikuwa limeegeshwa pale pale kwenye viunga vya maegesho. Hatimaye zikatokea picha za kile kilichosababisha niamue kuzidukua zile kamera za ulinzi za pale hotelini.

Kwanza nilimwona Rahma akiwa katika mavazi yake ya niqab akitoka sehemu ya chini ya jengo la ile hoteli huku akionekana mwenye wasiwasi. Akaelekea moja kwa moja nje ya eneo lile la uzio wa hoteli akilipita lile gari kana kwamba hakujuana nao. Muda mfupi baadaye nikajiona nikitokea kutoka sehemu ile ya chini ya jengo la hoteli na kuanza kuangaza macho yangu kutazama huku na kule wakati nikimtafuta Rahma.

Nikaendelea kushuhudia mlolongo wa picha za kile kilichoendelea wakati nilipomwona na kuamua kumfuata kule nje ya uzio wa hoteli hadi pale lile gari aina ya Toyota Crown jeusi lenye vioo vyeusi lilivyoanza kutoka na kisha shambulizi kufanyika.

Finally, I got you,” nilijisemea moyoni huku nikiendelea kutabasamu. Sasa nilitambua kuwa ni Abshir ndiye aliyekuwa amenishambulia kwa risasi kutokea ndani ya lile gari aina ya Toyota Crown jeusi lenye vioo vyeusi.

Baada ya hapo kila nilichoweza nilikifanya kwa haraka. Nilifahamu fika kuwa watu waliokuwa wanahusika na kamera zile za usalama katika hoteli hiyo wangeweza kuyaona matukio hayo na hivyo kupatwa na wasiwasi, hivyo nikazipakua zile video na kuzihifadhi kwenye Ipad yangu na kisha kumbukumbu za picha kuanzia pale nilipoonekana nikitoka ndani ya hoteli na kumtafuta Rahma kisha nikamwona na kumfuata hadi pale lile gari aina ya Toyota Crown jeusi lenye vioo vyeusi lilivyoanza kutoka na kisha shambulizi kufanyika niliziondoa kwenye ule mfumo wa kamera za pale hotelini. Na hapo kazi kazi yangu ikawa rahisi, kwani tayari nilishaanza kuupata mwanga wa nani na nani ni adui zangu.

Kisha nilijiegemeza kwenye sofa huku nikiwa nimeridhishwa na uchunguzi wangu, uso wangu ukiendelea kupambwa na tabasamu. Nilikuwa nimepiga hatua kubwa sana na hisia zangu zilinieleza hivyo. Kilichokuwa kinafuata baada ya hapo ni kuziingiza sura za wahusika wote wanne kwenye mfumo wa utambuzi kupitia programu yangu ya TracerMark ili kutafuta taarifa zaidi ambazo zingenisadia kuelewa mambo ambayo sikuwa nayafahamu hadi muda huo. Niliamini kuwa kazi hiyo ingekuwa rahisi zaidi sawa na kuzima mshumaa.

Kingine kilichonifurahisha ni kwamba sasa nilikuwa na uhakika kuwa Zuena wa Mombasa alikuwa na uhusiano na akina Abshir kama ambavyo hisia zangu ziliniambia. Ni hapo kwa Zuena wa Mombasa ndipo ambapo ningeanzia kazi yangu. Hata hivyo, nilifahamu fika sikupaswa kukurupuka kwani ingekuwa sawa na kujitumbukiza kwenye tanuru wakati moto ninauona, sikuwa na shaka kuwa maadui zangu walikuwa wanamsubiri kwa hamu.

“Nitatokea nikiwa tayari…” niliwaza. Nilipoitazama saa yangu ya mkononi nikagundua kuwa robo saa ilikuwa imetoweka tangu ilipotimia saa tatu asubuhi.

Inaendelea...
 
ufukweni mombasa.JPG

251

Taratibu nikaanza kuzama kwenye lindi la mawazo. Nilitambua kuwa mpaka hapo bado nilikuwa nakabiliwa na hatari kubwa. Jaribio lile la kutaka kuniua lilikuwa na maana ya kuninyamazisha na hivyo nilichotakiwa kukifanya ni kuhakikisha nalifumbua fumbo haraka lililonitatiza kuhusu Rahma wa Singida na watu wake, na wakati huohuo nakuwa makini zaidi na nyendo zangu. Na niliapa kuwa nisingemwamini mtu yeyote.

Nilinyanyua bilauri yangu ya Whisky nikapiga tena funda kubwa la mvinyo huku nikisisimkwa mwili wangu.

“Lazima nibaini mambo yao… mapema iwezekanavyo…” niliwaza huku nikiyasaga meno yangu kwa hasira. Hata hivyo, nilijirudi mara moja na kujaribu kuituliza hasira yangu nilipojikumbusha kuwa hadi muda huo ni mimi pekee ndiye niliyekuwa na nafasi ya kuokoa mambo kabla hayajafikia hatua mbaya kwa kuwa nilishapata mwanga.

Nilikunywa tena funda la mvinyo huku nikijitahidi kuifanya akili yangu iwe makini zaidi kabla sijaanza ngwe nyingine ya kuziingiza sura za akina Abshir kwenye mfumo wa utambuzi kwa ajili ya kutafuta taarifa zao.

Nikiwa bado natafakari mara nikahisi kusikia sauti ya mtu akigonga mlango wa chumba changu. Nikayatega masikio yangu vizuri kusikiliza. Nilikuwa sahihi kwani yule mtu aligonga tena na safari hii niliweza kuisikia vizuri ile sauti ya mgongaji, nikawaza mgongaji huyu angekuwa nani? Kwa vyovyote asingeweza kuwa mhudumu wa usafi kwa kuwa muda wa kufanya usafi ulikuwa bado haujafika. Nilitambua kuwa usafi ulikuwa unafanywa kuanzia saa nne asubuhi labda kama kulikuwa na dharula.

Nilipoitupia jicho saa yangu ya mkononi ikanionesha kuwa ilikuwa inaelekea kutimia saa tatu na dakika ishirini na tano ya asubuhi. Mgongaji akagonga tena pale mlangoni na mara hii niliweza kuhisi mgongaji huyu hakuwa mtu wa kawaida, alikuwa mgeni maalumu aliyekusudia kunitembelea, ila sikujua matembezi yake yangekuwa ya heri au shari!

Nikachomoa bastola yangu na kuishika vizuri kisha nikasimama na kuuendea mlango. Kisha nikachungulia kwenye tundu maalumu linalomwonesha mtu aliyesimama nje ya mlango huku bastola yangu ikiwa tayari mkononi. Nikakiona kiuno cha msichana aliyevaa suruali nyeupe ya dengrizi na blauzi ya rangi ya maruni. Nilijiuliza angekuwa nani lakini rangi ya ngozi yake ikanifanya niingiwe na ubaridi, alikuwa mweupe, na hapo taswira ya Zuena wa Mombasa ikajengeka taratibu akilini kwangu.

Hata hivyo sikutaka kuamini kuwa angekuwa Zuena wa Mombasa kwa kuwa nilijua asingewewza kujitokeza kwangu kwa mtindo ule kwa sababu aliamini kuwa sijui kile kilichokuwa kikiendelea. Hata hivyo nikajisemea moyoni kuwa na awe Zuena wa Mombasa au mtu mwingine yeyote nilikuwa tayari kwa lolote, tayari kwa mapambano. Nikajipa ujasiri huku nikijiandaa kwa lolote na kuufungua taratibu mlango wangu huku mkono wangu ulioshika bastola ukiwa mafichoni nyuma ya mlango.

Mlango ulipofunguka macho yangu yakakutana na macho mazuri na machangamfu lakini yaliyokuwa makini mno kuliko macho ya simba jike anayewinda. Yalikuwa macho ya mwanadada aliyesimama mlangoni kwangu akinitazama kwa utulivu huku akitabasamu kabla ya tabasamu lake halijageuka kicheko cha kirafiki.

Alikuwa mwanamke mzuri, tena ni zaidi ya uzuri wa haja. Alikuwa amependeza sana kwa mavazi yake yaliyombana kiasi yakilichora vyema umbo lake refu lenye kiuno chembamba. Kwa uzuri wake angeweza kushiriki mashindano ya urembo wa dunia na akashinda bila upinzani wowote; na angeweza kucheza filamu yoyote ile na akawa kivutio kikubwa. Uso wake mzuri ulijaa ucheshi huku macho yake yakionesha umakini na hekima.

Kichwani alivaa kofia aina ya pama ya rangi ya maruni iliyozifunika nywele zake laini za kishombe, nyusi zake alizitinda vizuri na kuzipaka wanja, kope zake zilikuwa zimerembwa vyema na kuyafanya macho yake yapendeze zaidi, na wakati huo huo kingo za mdomo wake zilikuwa zimekolea rangi ya maruni. Begani alikuwa amening’iniza mkoba mzuri wa rangi nyekundu. Alikuwa ni Leyla Slim Abdullas.

Nilishtuka sana kumwona Leyla pale nje ya mlango wa chumba changu ingawa nilijitahidi kuumeza mshtuko wangu. Mwili wangu ulikuwa kama uliopigwa na shoti mbaya ya umeme na hivyo kuingiwa ganzi na ubaridi fulani wa aina yake ulinitambaa mwilini huku mapigo ya moyo wangu yakibadili mwendo wake na kwenda mbio isivyo kawaida!

“Vipi umeshtuka sana kuniona?” Leyla aliniuliza huku akiniangalia usoni kwa umakini. Macho yake yalikuwa yanacheza cheza kwa msisimko huku yakipepesa taratibu na kuwakawaka kama kioo. Nikakumbuka kuwa hali kama hiyo niliishuhudia siku ya tukio la kutekwa kule ‘Shamba’.

“Kidogo…” nilisema huku nikishindwa kuuficha mshangao wangu na mashaka. Kisha nikachungulia nje na kuyazungusha macho yangu kuangalia eneo lote la ukumbi. Sikumwona mtu mwingine. Eneo lote lilitawaliwa na utulivu.

“Karibu ndani, jasusi,” nilimkaribisha Leyla kwa sauti tulivu ya chini huku nikimpisha pale mlangoni aingie. Akaingia.

Nilimsindikiza kwa macho wakati akipiga hatua zake kwa madaha hadi kwenye sofa na kuketi huku harufu nzuri ya manukato aliyojipulizia ikitamalaki mle ndani na kuleta uhai kwenye pua zangu. Nikashusha pumzi na kuisunda kiunoni bastola yangu halafu nikaurudishia mlango wangu na kuendelea kusimama pale pale mlangoni nikiendelea kumtazama Leyla kwa mshangao.

Nikiwa nimesimama pale kwenye mlangoni nilikuwa najiuliza Leyla aliwezaje kujua kama nilikuwepo pale Serena Beach Resort? Au na yeye alikuwa mmoja wao? Na kama hakuwa mmoja wao basi ni nini kilichokuwa kinaendelea pale? Au lile lilikuwa jini lenye sura ya Leyla? Nikajikuta nikianza kumwogopa.

Kama aliyekuwa akiyasoma mawazo yangu Leyla aliachia tabasamu na kusema kwa sauti yake laini, “Jason, mbona umetahayari sana baada ya kuniona?”

“Sikuutarajia ujio wako…” nilisema huku nikishusha pumzi, ukweli nilishindwa kuuficha mshangao wangu. “Halafu umejuaje kama nipo hapa?”

“Kwani hukutaka nijue?” Leyla aliniuliza huku akikunja sura yake. Sauti yake ilibeba kitu fulani kama hasira au wivu wakati akiongea.

“Sina maana hiyo,” nilimjibu huku nikilazimisha tabasamu na wakati huo huo nikijaribu kuifanya sauti yangu iwe ya kawaida, sauti ya kirafiki.

I’m sorry, I shouldn't have come here without telling you,” (Samahani, sikupaswa kuja hapa bila kukujulisha) Leyla alisema kwa sauti ya upole na kunyanyua mabega yake juu.

It’s okay… karibu sana,” nilisema huku nikihisi koo langu lilizidi kukauka, na hivyo nikachukua bilauri yangu na kujimiminia mvinyo kisha nikapiga funda moja kubwa. Halafu nikaketi kwenye sofa huku nikiwa makini sana nikimtazama Leyla usoni.

Tulikuwa tunatazamana. Sikujua Leyla aliniwazia nini lakini kwa upande wangu nilikuwa bado nashangaa huku maswali lukuki yakizunguka kichwani kwangu na kunivuruga akili yangu. Japokuwa nilipanga kumtafuta kabla ya lile tukio la kukoswa na risasi halijavuruga ratiba zangu zote. Hivyo sikuwa nimefurahishwa na ujio wake pale, ugeni ulioanza kunitia mashaka, kwa sababu sikujua aliwezaje kujua kuwa nipo jijini Mombasa na kwamba nilikuwa nimejichimbia hapo Serena Beach Resort!

Ni kama alikuwa anaendelea kuyasoma mawazo yangu akiguna na kusema, “Samahani, naona hujaridhika na ujio wangu…” kisha aliinuka huku akiitazama saa yake ya mkononi.

Inaendelea...
 
ufukweni mombasa.JPG

252

“Hapana!” nilisema nikiinuka kumzuia asiondoke. “Ujio wako hauna tatizo lolote kwangu, ni vile tu sikukutegemea kabisa ku… dah… hebu keti kwanza…” nilisema kwa kubabaika nikamshika kiuno na kumkumbatia. Nikambusu.

Na hapo nikamwona akilainika. Tukaketi tena. Sasa nikaituliza akili yangu ingawa sikuacha kumtazama usoni katika namna ya kumsoma. “Hebu niambie, Leyla, umejuaje kama nipo hapa?”

“Ni hadithi ndefu kidogo… jambo la msingi ni wewe uelewe tu kuwa nimekuja hapa,” Leyla alisema na kuachia tabasamu. Ndiyo kwanza akazidi kuniweka kwenye wakati mgumu.

Nilianza kujiuliza maswali mengi pasipo kupata majibu na hali ile ikaniacha njia panda. Nikazidi kumtazama Leyla machoni ili niyasome mawazo yake lakini alikuwa mjanja sana. Hakutaka nielewe kilichokuwa kwenye fikra zake. Nilipomkazia macho nikajikuta macho yangu yakigongana na macho laini lakini makini sana yanayobembeleza, macho ambayo si kwamba yalikuwa yanabembeleza tu bali pia yalikuwa yanashawishi na kushurutisha.

“Utakunywa nini mgeni wangu?” nilimuuliza Leyla huku nikiminya midomo yangu.

“Nitakunywa hicho unachokunywa. Ni Grant’s Blended Scotch Whisky, sivyo?” Leyla aliuliza huku akiitazama kwa umakini chupa ya whisky iliyokuwa juu ya meza.

“Ndiyo,” nilijibu huku nikiinuka na kwenda kuchukua bilauri ya pili kisha nikamimina whisky kwenye bilauri hiyo na kumpa Leyla, aliipokea na kunywa taratibu. Kilichonishangaza zaidi ni kwamba alikuwa mkimya sana tofauti na kawaida yake! Aliongea pale tu milipomuuliza swali. Ni kama alikuwa ametingwa na mawazo na alihitaji msaada, au labda alikuwa amechukizwa na jambo fulani.

Nilimfahamu vyema Leyla, alikuwa jasusi aliyebobea kwenye medani za kijasusi na mwenye akili nyepesi sana ya kuweza kupambanua mambo, pia aliweza kucheza na akili ya mtu. Yeye pia kwa kiasi fulani alinifahamu vizuri. Nikiwa bado sielewi aliwezaje kujua kuwa nilikuwepo Jijini Mombasa nikaanza kutatanishwa na hali yake. Nikajiuliza kama alikuwa na tatizo au aliamua tu kucheza na akili yangu baada ya kugundua kuwa nilikuwa sijafurahishwa na ujio wake pale!

Kuwa jasusi ni kuwa mwigizaji. Jasusi mzuri daima ni mwigizaji mzuri sana. Jasusi hubadilika kulingana na mazingira mfano wa maji. Maji yanaleta uhai lakini maji hayo hayo yanaweza kuleta maafa. Maji hayana rangi, huchukua rangi ya mahala yalipo. Ukiyaweka kwenye chombo chekundu huwa mekundu. Ukiyaweka kwenye chombo cheusi huwa meusi. Halikadhalika ukiyaweka kwenye chombo cha bluu huwa ya bluu.

Maji yakiwekwa juani au kwenye moto huchemka, na yakiwekwa kwenye hali ya ubaridi hupoa. Hivyo ndivyo alivyo mpelelezi, hubadilika kulingana na mazingira. Kuna wakati atajitia mwenye huzuni mahala panapohitajika furaha na kinyume chake; mradi dhamira yake ifanikiwe. Naam, uigizaji umo katika damu za wapelelezi wote ulimwenguni, Leyla akiwa ni sehemu yao.

Sasa ustahimilivu ulianza kutoweka ndani yangu. Hata macho yangu yalionesha kwamba akilini mwangu nilikuwa nimeishiwa na uvumilivu juu ya maigizo aliyotaka kuniletea Leyla. Niliamini kuwa hata Leyla mwenyewe aliweza kuyasoma mawazo yangu na hivyo wakati nikiwa katika kutaka kuamua nini nifanye baada ya kuchoshwa na maigizo yake nikamwona akivunja ukimya baada ya kuitazama tena saa yake ya mkononi.

“Jason!” Leyla aliniita kwa sauti ya chini huku akinitazama usoni kwa utulivu.

“Leyla!” nami nilimwita huku nikimkazia macho usoni kwa namna ya kumsaili.

“Kwa nini hukuniambia kama unakuja Mombasa?” Leyla aliniuliza huku akijitahidi kudhibiti donge la hasira ya wivu kooni mwake. Ingawa alijua kuwa nilikuwa nimeoa na nilimpenda sana mke wangu lakini hisia zangu ziliniambia kuwa alikuwa msichana mwenye wivu mkubwa juu yangu.

“Na hii pia ni sehemu ya maigizo yake?” nilijiuliza kisha nikamuuliza kwa utulivu huku usoni nikijitahidi kuumba tabasamu jepesi la kirafiki. “Naomba kwanza uniambie umejuaje kuwa nipo hapa!”

“Nitakwambia kila kitu lakini nataka kwanza kujua kwa nini hukutaka nijue kama upo Mombasa?” Leyla akaniuliza tena kwa utulivu huku akinitazama usoni.

Kabla sijamjibu nilimtazama kwa umakini machoni kuona kama kweli alikuwa anamaanisha. Hata hivyo niliambulia kuyaona macho yale yale mazuri yakionesha upole na hekima na yalikuwa yamebeba tabasamu baridi. Nikashindwa kuelewa nimweke katika fungu gani!

“Sijakwambia kwa sababu nilipanga kukufanyia surprise…” hatimaye nilisema kwa sauti tulivu na kushusha pumzi. Kisha nikaongeza, “Kwa nini nisikwambie wakati nimekuja Mombasa kwa ajili yako? Nimekuja kukutembelea na kukaa na wewe kwa wiki nzima ili tufurahie maisha haya mafupi.”

“Kweli?” Leyla aliuliza kama punguani.

“Sina sababu ya kuongopa,” nilimhakikishia. Kisha nikasisitiza, “Sasa niambie umejuaje kama nipo hapa?”

Kwanza Leyla alishusha pumzi ndefu na kujiweka vizuri pale kwenye sofa kabla hajasema lolote. Kisha akaitazama saa yake ya mkononi na kuangalia darini kwa muda akionekana kama aliyekuwa anatafakari nini cha kusema. Utulivu wake na jinsi alivyokuwa akiitazama saa yake mara kwa mara vilinifanya nianze kuhisi kuwa alikuwa na mpango hasi dhidi yangu na kilichosubiriwa ni muda tu ufike. Mara moja nikalikumbuka tena lile tukio lililotokea kule ‘Shamba’ wakati wa mafunzo hadi nikatekwa na wale makomando.

“Kabla ya yote nakuomba usijisahau kupita kiasi. Wewe ni kachero na kachero siku zote anakuwa makini muda wote kwa kuwa hafahamu nani rafiki na nani adui,” Leyla aliniambia kwa sauti tulivu iliyomaanisha huku akinitulizia macho usoni.

Sikusema neno, nilibaki kimya nikimsikiliza maana hadi muda huo sikuwa nimeelewa nia yake nini zaidi ya kumwona akijaribu kuzungusha zungusha maneno tu, ingawa ni kweli kwenye maisha ya kijasusi umakini muda wote ni jambo muhimu sana. Nikashangaa kuwa japo nilipaswa kuwa makini muda wote lakini ujio wangu hapo Mombasa sikuwa nimeuchukulia kwa umakini unaotakiwa, nilidhani nilikuwa nakuja kupumzisha akili yangu lakini hali ilivyoanza kuonekana ilikuwa tofauti na matarajio yangu.

“Ulipokuwa unashuka kutoka kwenye basi la Tahmeed pale Likoni Ferry nilikuona…” Leyla alisema na kunifanya nishtuke kidogo maana sikulitegemea jambo hilo. “Nilikuwa kwenye mishe mishe zangu nikiwa ndani ya gari langu,” Leyla aliniambia.

Nikavuta kumbukumbu za tukio lile la kushuka toka ndani ya basi la Tahmeed kisha nikaanza kutembea nikisaka teksi.

“Nilishangazwa sana na uwepo wako jijini Mombasa kwa kuwa hukuwa umenitaarifu kama unakuja, ila ulionekana haukuwa makini sana kama ambavyo jasusi anapaswa kuwa! Nilitaka kukuita lakini nikajionya maana sikujua ulikuwa na nani na ulikuwa na misheni gani hapa Mombasa. Nilichofanya ni kuwa makini na nyendo zako. Kisha nikakuona ukiingia ndani ya teksi ya Babu Ali…” Leyla alisema.

“Yule mzee dereva wa teksi anaitwa Babu Ali?” nilimuuliza Leyla.

“Ndiyo, ni dereva maarufu sana hapo Likoni Ferry…” Leyla alisema kisha akaendelea. “Wakati ile teksi ikiondoka toka eneo lile nikaamua kuwafungia mkia huku nikihakikisha hutambui kama nilikuwa nawafuata. Hata hivyo nilitegemnea ungeingiwa na wasiwasi baada ya kuliona gari langu likiwa limewafungia mkia lakini kwa kuwa nia yangu ilikuwa kuhakikisha usalama wako sikuwa na wasiwasi hata kama ungeniona,” Leyla alinyamaza kidogo na kujiweka sawa pale kwenye sofa. Kisha akaendelea.

Inaendelea...
 
ufukweni mombasa.JPG

253

“Nikawafuata hadi hapa Serena Beach Resort na nikakushuhudia ukishuka na kupokewa na wahudumu wa hoteli. Baada ya kuhakikisha kuwa upo salama nikaondoka huku nikisubiri kuona kama ungenipigia simu kunijulisha kuhusu uwepo wako ndani ya jiji letu, lakini haikuwa hivyo hadi sasa.”

Nilimtazama Leyla kwa umakini machoni, nikajikuta nikiyatazama macho ya msichana mweledi, mwerevu, mjanja na mpelelezi aliyekomaa kiupelelezi. Nikapiga funda moja la whisky na nilipoiweka bilauri mezani nikamudu kusema neno moja tu. “Dah!”

Muda wote wakati Leyla akinisimulia mwili wangu ulikuwa unasisimka kwa hofu. Nilianza kujilaumu kwa kutokuwa makini. Nikajiuliza vipi kama ni Zuena wa Mombasa ndiye angekuwa akinifuata kwa nia ya kunidhuru? Kwa vyovyote asingeshindwa kunimaliza kwa kuwa sikuwa makini kabisa.

“Leo kumekucha nikaendelea kusubiria simu yako lakini uvumilivu ukanishinda na hivyo nimeamua kuja mwenyewe nikufanyie surprise. Uzuri hapa hotelini wengi wananifahamu hivyo haikuwa ngumu kupata taarifa zako na kujua upo chumba namba ngapi,” Leyla akahitimisha maelezo yake na kunifanya nihisi kuchoka kabisa.

“Kweli hii ni bonge ya surprise!” nilisema katika hali ya kukata tamaa na hivyo kusababisha kicheko toka kwa Leyla. Nami nikacheka.

“Najua ulipanga kunifanyia surprise badala yake mimi ndo nimeku-surprise,” Leyla alisema kwa utani huku akiendelea kucheka. Tukacheka pamoja na mara kicheko kilipokatika Leyla akaniuliza, “Hujanimbia lengo la ujio wako hapa Mombasa. Sidhani kama ulipanga kuja kunitembelea tu.”

Nilishusha pumzi huku nikitafakari haraka haraka kama nimwambie ukweli juu ya kile nilichokibaini au nimfiche. Sauti fulani ndani yangu ikanisisitiza kumwambia. Nikashusha tena pumzi na kusema, “Ni kweli lengo langu lilikuwa kuja kukutembelea na kupumzisha akili yangu lakini tangu nimefika hapa mambo fulani yenye utata yamejitokeza, na hivyo nahitaji sana msaada wako, Leyla,” nilisema kwa sauti ya chini.

Kisha nilianza kumsimulia Leyla mkasa wote tangu nilipokutana na Rahma wa Singida katika Benki ya NBC Posta jijini Dar es Salaam, nilivyowafuatilia yeye Abshir hadi Lamada Hotel, walivyotoweka kisha akaibuka Zuena wa Mombasa aliyejinadi kuwa mwanamitindo, hadi tukio la kurushiana risasi lililotokea asubuhi ya siku hiyo muda mfupi kabla hajafika hapo Serena Beach Resort.

“Ni dhahiri kuna jambo tusilolijua linaloendelea hapa Kenya. Tunapaswa kuhakikisha tunazijua mbivu na mbichi…” nilimwambia Leyla, ambaye muda wote alikuwa ametulia tuli, hatingishiki, haongei wala hapepesi macho yake.

Kabla sijamwonesha zile picha za video nilizozidukua kutoka kwenye mfumo wa kamera za ulinzi pale hotelini nilimpa asome ule ujumbe wa vitisho nilioukuta pale mapokezi. Leyla aliusoma na kuachia tabasamu lililomaanisha kuwa mtumaji wa ujumbe huo alikuwa mtu mwoga. Kisha nikamwonesha zile picha za video kutoka kwenye kamera za ulinzi za pale hotelini ambazo nilizihifadhi kwenye Ipad yangu.

Leyla alizitazama picha zile kwa umakini na mara kadhaa alionekana kuyarudisha matukio nyuma akijaribu kujiridhisha na kile alichokuwa akikiona, na jinsi alivyoendelea kuzitazama ndivyo uso wake ulivyozidi kukumbukwa na fadhaa. Hadi anamaliza kuzitazama alikuwa ametahayari sana. kilichokuwa kimeshtua zaidi ni kuwaona Zuena wa Mombasa na yule mwanamume mwenye macho kama ya nyoka.

“Miriam!” Leyla alimaka kwa mshangao mkubwa baada ya kuigandisha sura ya Zuena wa Mombasa na kuitazama kwa makini. Kisha kwa sauti ya upole huku akionesha masikitiko akaniambia, “Dah! Jason, kwanza pole sana kwa masaibu yaliyokukuta.”

“Ahsante. Kwa kweli kama si Mungu pengine ungesikia nimekufa,” nilisema huku nikinyanyua bilauri yangu na kunywa mvinyo. “Kwani unamfahamu huyo dada?”

Leyla alibetua kichwa chake kukubali kisha akashusha pumzi ndefu kama aliyetoka kumaliza mashindano ya mbio ndefu. “Yeah… anaitwa Miriam Mutua, ofisa wa Usalama wa Taifa. Kinachonichanganya ni vipi anahusiana na suala hili?”

Nilishusha pumzi za ndani kwa ndani huku nikiitazama vizuri picha ya Miriam Mutua ambaye mimi nilimfahamu kama Zuena wa Mombasa.

“Kwani ni mtu wa aina gani hasa?” nilimuuliza Leyla ili kutaka kumfahamu kiundani Miriam hasa nikikumbuka jinsi ambavyo hisia zangu ziliniambia kuwa hakuwa mtu wa kuaminika na ndiyo maana nilikuwa makini naye sana.

Kwanza Leyla alishusha pumzi za ndani kwa ndani kisha akainamisha uso wake chini huku akikunja sura yake kama aliyekuwa anajaribu kufikiria kwa kina, halafu akainua uso wakie kunitazama. “Ni mtu mcheshi sana, mtiifu na mchapakazi hodari, huwezi hata kumdhania kama anaweza kuwa na mambo kama haya! Mimi ndiye niliyemfundisha mambo mengi jinsi ya kufanya kazi kwani yeye mmoja wa ya vijana ambao hawana miaka mingi katika idara ya ujasusi lakini ameshaonesha uwezo mkubwa katika kazi.”

“Na vipi kuhusu maisha yake nje ya kazi? Anapenda maisha ya juu!” nilimuuliza Leyla huku nikimtazama usoni.

Obviously! Kama msichana wa kileo, anapenda sana maisha fulani classic, you know what I’m saying…” Leyla alinijibu

“Basi sishangai yeye kuwemo kwenye sakata hili…” nilimwambia Leyla. “Najua wapo baadhi ya maofisa wanashirikiana kwa karibu sana na wahaini na wanalipwa mamilioni ya fedha kuvujisha siri za kiusalama. Kwa Miriam kuwa wakala wa mtandao wa kihaini ni jambo la kawaida katika mashirika ya kijasusi duniani.”

“Ni kweli… lakini kingine kinachonishangaza ni kuwepo kwa Abdoulkader Omar hapa Kenya na kuhusika kwenye sakata hili!” Leyla alisema. Nikamdaka juu kwa juu.

“Abdoulkader Omar ndiye nani?” nilimuuliza Leyla kwa shauku.

“Ni huyo mwenye macho kama ya nyoka. Ni mfanyabiashara mkubwa sana ila wengi hapa Kenya hawamfahamu. Ana kampuni inayoitwa Obock Enterprises Limited ambayo inajishugulisha na kujenga viwanda, kusafirisha watalii, kusafirisha bidhaa nje na kuingiza toka nje, na maduka ya kibao kubadili fedha. Ofisi yao kuu ipo Djibouti, na hapa Kenya wana matawi Nairobi na Mombasa.”

“Vipi kuhusu rekodi yake, inatia shaka?” nilimuuliza kwa shauku.

“Mmh! Abdoulkader hana rekodi yoyote chafu, kampuni yake imekuwa inatoa sana misaada hapa Kenya kwa walemavu, akina mama na vijana. Na inasemekana yeye ana undugu na Rais wa Djibouti, Khaleed bin Jamal. Pia kampuni yake ilimsaidia sana Rais wa sasa wa Kenya kushinda uchaguzi,” Leyla alisema na kuongeza, “Hata hivyo bado si sababu ya kumwona hata tatizo kwani naelewa kuwa mfanyabiashara yeyote mkubwa hawezi kukosa makondokando.”

“Basi yote yatajulikana muda si mrefu, ngoja niingize taarifa zake kwenye mfumo maalumu wa utambuzi wa programu ya TracerMark,” nilimwambia Leyla huku nikifungua mfumo huo kisha nikaingiza sura na jina la Abdoulkader Omar.

Baada ya kubonyeza hapa na pale huku nikifungua code hizi na kuingiza code zile hatimaye pale nilipopataka pakafunguka na taarifa za kiintelijensia zilizoandaliwa na mashirika ya kijasusi ya Mosad (Israel) na CIA (Marekani) kumhusu Abdoulkader zikatokea.

Inandelea...
 
ufukweni mombasa.JPG

254

Abdoulkader Omar, raia wa Djibouti na binamu wa Rais wa Djibouti, Khaleed bin Jamal. Abdoulkader Omar ni mfanyabiashara na mkurugenzi mwenza wa kampuni ya Obock Enterprises Ltd. inayojishugulisha na kujenga viwanda, kusafirisha watalii, kusafirisha bidhaa nje na kuingiza toka nje, na maduka ya kibao kubadili fedha. Ofisi yao kuu ipo Djibouti, na hapa Kenya wana matawi Nairobi na Mombasa, kwa Tanzania tawi lao lipo Dar es Salaam, na Kampala nchini Uganda.

Abdoulkader Omar ni mrefu wa futi 6 na inchi 1, ana umri wa miaka 45 na damu yake ni group AB +ve. Ana ndugu wakiume watatu: Abdoulkhareem, Sultan na Kareem na dada yao Shamsa. Ameoa wake wawili: Latifa na Salma, na watoto wanne, watatu kutoka kwa mke mkubwa Latifa, na mmoja kutoka kwa mke mdogo Salma. Ni msomi wa Shahada ya Kwanza ya Biashara za Kimataifa na Lugha aliyoipata toka Chuo Kikuu cha Warwick nchini Uingereza.

Tarifa zikaendelea kudadavua kuwa Abdoulkader Omar amekuwa akikifadhili kwa siri kikundi cha kigaidi cha Al Shabab na anajihusisha na mambo ya utakatishaji wa fedha, ila ndo hagusiki kwa kuwa ana undugu na Rais wa Djibouti, na pia analindwa na wakubwa fulani nchini mwake na hata nchi ya Kenya kwa sababu amekuwa akijificha kwenye mwamvuli wa kufadhili na kuisaidia serikali.

Abdoulkader Omar amekuwa anacheza mchezo wa damu kwa kutumia mkono wa serikali, akishiriki magendo na biashara haramu na vitu hivyo vinamvunisha fedha nyingi mno. Pia amekuwa akishirikiana na magenge ya wauaji, dawa za kulevya, utakatishaji wa fedha na kadhalika na kadhalika nyuma ya pazia. Abdoulkader Omar amekuwa anatumkika kama mkono wa kushoto wa Rais Khaleed bin Jamal wa Djibouti akitumwa kuwamaliza maadui zake. Abdoulkader si tu genge hatari. La hasha! Pia ni jasusi wa kiuchumi na mtu anayehakikisha maslahi na matakwa ya Djibouti na ya Wasomali yanatimia!

Baada ya kupata taarifa za Abdoulkader Omar nikaingiza sura na jina la Abshir kwenye mfumo wa utambuzi wa TraverMark. Baada ya kuhangaika kwa takriban robo saa nikifungua code mbalimbali hatimaye nikawa nimepata maelezo kuhusu mtu huyo.

Abshir ni moja ya majina mengi ambayo huyatumia. Mbali ya majina pia muuaji huyu sura nyingi za bandia kujificha, ni muuaji hatari sana ambaye amebobea katika mauaji iwe ya moto au ya baridi. Muuaji huyu anatoka Jimbo la kujitegemea la Somalia la Puntland lililopo Somalia Kaskazini-Mashariki kwenye ncha ya Pembe ya Afrika, na hutumiwa na mitandao mikubwa ya mauaji japokuwa yeye mwenyewe ana timu yake ya watu wawili wenye weledi mkubwa wa mbinu za kigaidi na mauaji.

Muuaji huyu hajawahi kukamatwa wala kujulikana kwa majina halisi ndiyo maana amepachikwa jina “Soft Assassin” kwa sababu anaua na hapendi kuacha alama yoyote nyuma yake. Sifa kubwa ya muuaji huyu ni kwamba hupenda kutumia silaha aina moja tu, bunduki aina ya 338 Lapua Magnum ambayo huwekwa kiwambo maalumu cha kuzuia sauti ama Sound Suppressor.

Baada ya maelezo hayo kuhusu Abshir zikaja sura mbalimbali zilizoaminika kuwa ni sura zake, na kati ya sura hizo, Leyla aliweza kuitambua sura moja ambayo yeye alimfahamu mtu huyo kwa jina la Mahmood Khaleed kutoka Somalia. Leyla alimtambua kutokana na kuhusika kwake kwenye mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea Septemba 2013 kwenye jengo la Westgate Jijini Nairobi.

“Dah! Hii ishu ni kubwa mno kuliko nilivyotarajia…” nilisema huku nikihisi akili yangu ikishindwa kufanya kazi sawa sawa. “Inagusa mtandao mpana mno ambao una nguvu, yatupasa kuwa waangalifu sana na wakati huo huo tukipanga namna ya kuangusha mipango yao kama Daudi alivyofanya kwa Goliath.”

“Nipo pamoja na wewe katika kila namna, naomba tushirikiane kwenye hili. Wakati wao wanajipanga kivyao na sisi tujipange kivyetu,” Leyla aliniambia katika namna ya kunitia moyo. Kisha akaongeza, “Knowledge is power… ingekuwa ngumu sana kupigana na mtandao kama huu kwa ngumi bila taarifa kama hizi. Lazima uwe na taarifa za kutosha kwanza ili ujue unapiga wapi na kwa nini. Sasa basi kwa kutambua kuwa Abdoulkader Omar ndiye yupo nyuma ya yote haya akimtumia ofisa wa usalama Miriam Mutua inatupa mwanzo mzuri wa kupambana nao.”

Nikiwa nimeituliza akili yangu nilianza kujiuliza kuwa wakati naanza kumfuatilia Rahma wa Singida kule jijini Dar es Salaam hivi nilikuwa nafahamu nini juu ya mtandao huo? Hakuna! Niliwaza kwa uchungu kuwa muda wote nilikuwa nahangaika na Rahma wa Singida wakati kumbe nilikuwa sijui chochote zaidi ya ukweli kuwa nilikuwa najaribu kupambana na watu wenye nguvu zote: kiuchumi, kiulinzi na kiukatili!

“Jason, nakushukuru sana kwa ujio wako hapa Kenya maana umenifungua mengi ambayo sikuwa nayajua. Ni Mungu tu amekuongoza…” Leyla alisema kisha akaongeza, “Siku zote nilikuwa nahangaika kumjua mtu ndani ya idara yetu ya Usalama wa Taifa anayetumiwa kutoa taarifa mbalimbali za kijasusi hapa Mombasa, hatimaye leo nimembaini. Kwa kumtumia Miriam wameweza kufahamu kila kinachoendelea kuhusiana na usalama wa nchi. Kwa hiyo basi Miriam ndiye mshukiwa wetu wa kwanza na atatupa majibu ya maswali yetu na mwanga zaidi kuhusiana na kazi hii.”

“Nakubaliana nawe, Leyla. Tukimpata Miriam tukambana tutakuwa tumepata mwanga wa nini kinaendelea nyuma ya pazia. Naamini hawa watu wana jambo lao wanalotarajia kulitimiza hivi karibuni,” niliafikiana na maneno ya Leyla. Na hapo nikainua bilauri yangu ya mvinyo na kuugugumia mvinyo wote.

Kisha tuliendelea kujadiliana hili na lile na ilipofika saa sita mchana Leyla aliniaga kuwa alikuwa anakwenda ofisini kwa vile alipitia asubuhi na baada ya kikao cha kupashana habari za kiintelijensia (SITREP) akatoka. Aliniambia pia angewasiliana na jamaa zake waliopo ofisi za Mamlaka ya Mapato ya Kenya ili kujua kama namba za yale magari mawili aina ya Toyota Verossa na Toyota Crown ni namba sahihi na si za bandia, na mmiliki ni nani.

Kabla hajaondoka Leyla alinishauri nihame pale Serena Beach Resort kwa muda kwa ajili ya usalama wangu ila nisirudishe chumba ionekane kuwa bado nipo pale kwa ajili ya kuwachanganya adui zangu. Tukakubaliana tuondoke na niende kwenye hoteli nyingine ya kawaida iliyo mbali na eneo lile wakati tukijipanga kwenda nyumbani kwa Miriam jioni ya siku hiyo.

* * *

Endelea kuufuatilia mkasa huu wa kusisimua...
 
Mkuu asante sana askofu natamani niombe jambo ila ntaonekana wafazilaka wapundaka
 
Ila hii story ni tam haswaa... Kwanza haitabiriki
Sisi tumeshazoea ukisoma stori fulan unaweza kutabiria mwishoni itakuaje
Lakini kwa hii movie aseee bwana Bishop Hiluka umetuweza sana naniii
Kunywa ata bia mbili boss
 
Jason kaenda kinyume na miiko ya kazi yake. Kampa faili zima Leyla kuhusu Zuena(Mariam), Rahma wa Singida na Abshir
 
Back
Top Bottom