Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
- Thread starter
- #581
259
Wakati tukifungua milango ya nyuma ya teksi ile na kuzama ndani macho yangu yalikuwa makini kutazama kila mahali katika namna ya kuchunguza kuwa hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa akitufuatilia nyendo zetu. Muda ule ule ile teksi ikaondoka na kuingia barabarani huku yule kijana dereva wa teksi akijitia uchangamfu wa kila namna katika kuhakikisha kuwa ananizoea, nafasi ambayo kamwe sikutaka kumpa.
Muda wote nilikuwa makini kuchunguza kama tungefungiwa mkia na gari nyingine nyuma yetu lakini hilo halikujitokeza hadi tunafika katika mgahawa maarufu wa Acapulco Club & Restaurant uliopo barabara ya Nyali kwa ajili ya kupata chajio (dinner). Ulikuwa mgahawa mzuri wa kisasa wenye huduma zote muhimu kama aina ya vyakula mbalimbali vya watu wa mataifa tofauti na utulivu wa kutosha.
Tulipoingia pale kwenye mgahawa nikagundua kuwa kulikuwa na watu wa daraja la kati na la juu na wengi walikuwa raia wa kutoka nje ya Kenya. Mle kwenye mgahawa tulitafuta meza moja iliyojitenga kwenye kona moja ya mgahawa na kuketi. Sehemu ile tuliyoketi ilituwezesha sote kuona nje ya mgahawa ule kupitia vioo.
Mhudumu mmoja wa mgahawa ule alikuja kutusikiliza nikaagiza ugali na makange na saladi ya mboga za majani. Merina yeye aliagiza chips kuku na saladi ya mboga za majani. Vyakula vile vilipoletwa na mhudumu tukaanza kuvishambulia huku kila mmoja akionekana kuwa na njaa. Tulipomaliza kupata mlo tukaagiza sharubati ya mchangayiko wa embe na pasheni, tukashushia taratibu huku kichwani nikitafakari kuhusu kazi iliyokuwa mbele yangu.
Baada ya kupata chakula pale Acapulco Club & Restaurant tulikodi teksi nyingine iliyotupeleka katika ukumbi wa maraha wa Bamburi Beach Villa uliopo kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi. Tuliingia kwenye ukumbi wa Bamburi Beach Villa mnamo saa tatu na nusu usiku. Ulikuwa ukumbi mkubwa wa kisasa kabisa wenye kila aina ya vionjo vya daraja la kimataifa wenye jukwaa zuri linalotazamana na viti vingi vya kisasa kwa ajili ya kufanyia matamasha ya muziki na mikutano mbalimbali.
Pia kulikuwa na ukumbi mwingine mkubwa kwa ajili ya kujipatia vyakula vya asili na vya kimataifa wenye meza ndefu za kisasa zilizozungukwa na viti vizuri vya sofa vyenye foronya laini na kila ukumbi ulikuwa umejitenga na hivyo kutengeneza mgawanyo mzuri wa starehe tofauti zenye utulivu zinazoweza kufanyika kwa wakati mmoja.
Siku hiyo kulikuwa na onesho maalumu kutoka kwa msanii wa Afrika Mashariki anayetoka nchini Tanzania, Ali Kiba, ambaye alikuwa anasindikizwa na wasanii wengine maarufu kutoka Kenya. Merina alikuwa ameniomba twende Bamburi Beach Villa kwa kuwa, kama ilivyokuwa kwa wakazi wengi wa Mombasa, alikuwa shabiki mkubwa wa Ali Kiba.
Tulipoingia ndani ya ukumbi wa Bamburi Beach Villa tukatafuta sehemu nzuri, kwenye kona, na kuketi ili tuweze kuona vyema onesho. Lakini pia niliichagua sehemu ile kwa sababu za kiusalama ili niweze kumwona kila mtu aliyeingia ukumbini. Wengi tuliowakuta mle ukumbini walikuwa ni watu wa kipato cha kati na cha juu. Alipofika mhudumu niliagiza mvinyo ghali mwekundu aina ya Pinot Noir na Merina akaagiza kinywaji baridi cha Leapfrog cocktail na tulipoletewa tukawa tunakunywa taratibu huku tukifuatilia onesho jukwaani.
Wakati wote nilikuwa makini kuwachunguza watu walioingia na kutoka mle ukumbini, na hata waliokuwa wameketi ili kuona kama kulikuwa na yeyote wa kumtilia shaka.
Hadi inafika saa tano usiku mwanamuziki Ali Kiba alikuwa bado hajapanda jukwaani. Ni muda huo nilipotaka niinuke nielekee maliwato nikajikuta nikisita baada ya macho yangu kuvutiwa kumtazama msichana mmoja mzuri na mweupe ambaye alikuwa amevaa suruali ya bluu ya dengrizi iliyolichora umbo lake la msichana wa Kiafrika mwenye kiuno chembamba kiasi.
Juu alikuwa amevaa blauzi nyepesi nyekundu iliyozionesha vizuri chuchu zake nyeusi zilizotuna na shingoni mkufu unaometameta uliizunguka vizuri shingo yake ndefu na nyembamba huku ukipotelea katikati ya matiti yake. Mkufu huo ulinishtua na kunifanya nimtazame vizuri usoni na kumtambua.
“Miriam!” nilijikuta nikimaka kwa mshangao kwa sauti ya chini. Hata hivyo Merina alinisikia kwani nilimwona akigeuza shingo yake kutazama upande ambao macho yangu yalielekea.
“Usitazame huko, kuna mmoja wa watu wabaya sitaki atushtukie,” nilimwambia Merina, akanielewa haraka na kugeuka haraka kutazama upande mwingine.
Muda huo Miriam alikuwa amesimama akiyatembeza macho yake taratibu kutazama kila meza iliyokuwa mle ndani kama aliyekuwa anamtafuta mtu na wakati alipogeuka upande wetu niliwahi kuinamisha kichwa changu chini kama niliyekuwa natafuta kitu chini ya meza. Merina naye aliinama kutazama chini akidhani labda nilikuwa nimedondosha kitu.
“Kuna kitu umedondosha?” Merina aliniuliza huku akiyakodoa macho yake kutazama pale sakafuni.
“Hapana, yule mtu sitaki anione,” nilimjibu Merina huku nikiwa bado nimeinamisha kichwa changu na wakati huo huo nikimtazama Miriam kwa chati na kumwona akianza kuondoka na kuufuata uelekeo wa mlango wa kutokea, na hapo nikatambua kuwa alikuwa anaondoka. Nyuma yake alikuwa anafuatwa na mwanamume mmoja mrefu aliyevaa suti maridadi nyeusi.
“Mtu gani?” Merina aliniuliza huku akinitazama kwa wasiwasi.
“Ngoja kwanza, n’takwambia…” nilisema huku nikiinua uso wangu na kuangaza macho yangu huku na kule kutazama kama kungekuwa na mtu mwingine ambaye nilikuwa namfahamu au kumtilia shaka. Sikuona. Hata hivyo sikutaka kupoteza hata sekunde, nami nikainuka.
“Samahani, Merina… nakuja ila nakuomba chukua tahadhari, usimwamini mtu yeyote. Na kama sijatokea baada ya saa moja chukua teksi utangulie nyumbani, hakikisha hakuna mtu anayekufuatilia…” nilimwambia Merina kwa maneno ya msisitizo huku nikimpa noti kadhaa ambazo niliamini zingemtosheleza kwa nauli na mambo mengine. Nikamwona akiingiwa na wasiwasi, akataka kupinga wazo langu la kuondoka nimwache lakini hakupata nafasi kwani tayari nilikwisha mshikisha zile fedha na mimi nikaanza kupiga hatua kuelekea nje ya jengo.
Nilipiga hatua kadhaa na kugeuka kumtazama Merina nikamwona akiwa amesimama akiniangalia kwa wasiwasi. Nikaendelea na safari yangu pasipo kujali wasiwasi wake. Nilitembea kwa tahadhari huku nikijaribu kuwachunguza watu wote waliokuwemo mle ukumbini na hata wale niliopisha ili kuona kama kulikuwa na yeyote wa kumtilia shaka. Nilipohakikisha kwamba hakukuwa na wa kumtilia mashaka nikaharakisha kuelekea nje.
Tayari Miriam alikwisha toka nje na sikutaka aniache mbali sana hivyo nilipotoka tu nje nikaangaza macho yangu kutazama huku na kule sikumwona Miriam lakini nikajikuta nikimwona yule mwanamume mrefu ambaye sasa nilimtambua kuwa ni yule aliyekuwa akiendesha gari aina ya Jeep iliyotufungia mkia wakati tunatoka Serena Beach Resort kabla hatujapata ajali iliyosababisha kifo cha dereva wa teksi.
Alikuwa ni mwanamume mwenye asili ya Kisomali na alikuwa anamalizia kuongea na simu kisha akalifuata gari lake aina ya Range Rover jeusi. Nikiwa bado nashangaa nikaliona lile gari aina ya Range Rover likaanza kuyaacha maegesho ya magari ya pale Bamburi Beach Villa kwa mwendo wa taratibu, kisha likaingia barabarani. Mara nikamwona Miriam akiwa amesimama kwa mbele.
Gari lile lilienda kusimama hatua chache pembeni yake na hapo nikaelewa ni nini kilichokuwa kikiendelea mbele yangu. Lile gari liliposimama tu Miriam akafungua mlango wa nyuma na kuingia ndani na hapo safari ikaanza lile gari likiufuata uelekeo wa barabara ya Jomo Kenyatta Beach.
Sikutaka kuzubaa nikaharakisha kuiendea teksi moja iliyokuwa eneo lile na kumkuta dereva wa teksi, mtu mzima mwembaba wa wastani, ana nywele nyingi zilizochanganyika na mvi na ndevu za wastani akiwa tayari kwani alikuwa ameniona tangu nilipokuwa mbali nikiharakisha kuelekea eneo lile.
Nilipoifikia teksi ile nikafungua mlango wa nyumba na kuingia na kabla yule dereva hajaniuliza uelekeo wangu nikamwambia alifuate lile gari aina ya Range Rover jeusi lililoondoka pale kwenye yale maegesho muda mfupi uliokuwa umepita. Dereva yule alinielewa na bila shaka kumbukumbu ya uelekeo wa lile gari ilikuwa bado ipo vizuri kichwani mwake kwani muda ule ule aliingia na kuliwasha gari lake, likagoma kuwaka.
“Oh shit!’ niling’aka kwa hasira, na wakati huo huo yule dereva akawa analalamika, “Aah! Matatizo yameanza tena!”
“Vipi, gari lako bovu?” nilimuuliza huku akili yangu ikiwa inawaza namna nyingine ya kufanya ili niwawahi akina Miriam na yule dereva wake.
“Aaah vijana wa Mombasa wanatumia sana uchawi, hawataki mimi nipate fedha kama wao,” yule dereva alilalamika.
“We mzee acha imani za kishirikina, we sema gari lako bovu!” nilisema kwa hasira huku nikishuka toka ndani ya gari lake. Kisha nikaikimbilia teksi nyingine ambayo dereva wake alikuwa kijana na alikuwa akiniita baada ya kugundua ile teksi niliyotoka imegoma kuwaka.
Niliifikia nikafungua mlango wa nyuma na kuingia. “Una petroli ya kutosha?” nilimuuliza yule dereva wa teksi kwa wasiwasi.
“Kwani we unakwenda mbali?” yule dereva aliniuliza huku akiingia na kuketi kwenye usukani.
“Sijajua…” nilimjibu. “Nataka ulifuate lile gari aina ya Range Rover jeusi lililoondoka maeneo haya muda mfupi uliopita.”
Yule dereva alielewa na muda ule ule akayaacha yale maegesho ya teksi na kuingia barabarani akiufuata ule uelekeo wa lile gari aina ya Range Rover.
“Ni akina nani wale? Au hayanihusu?” yule dereva aliniuliza na hapo hapo akajishtukia mwenyewe. Nikacheka kidogo kumtoa wasiwasi na kusema kwa sauti tulivu, “Ni mchumba wangu yuko na jamaa mwingine, nataka nikafumanie.” Yule dereva hakuuliza tena.
“Ila naomba kuwa mwangalifu sana, sitaki wajue kuwa wanafuatwa,” nilimwonya yule dereva. Akanielewa na wakati huo tukiingia barabara ya Jomo Kenyatta Beach. Dereva akakunja kulia na kuifuata barabara ile na mwendo mfupi baadaye tukaifikia Barabara ya Malindi.
Tulipoingia barabara ya Malindi tukaliona lile gari aina ya Range Rover likiwa linakikaribia kiwanda cha simenti cha Bamburi. Dereva wangu akaongeza mwendo na wakati tukifika pale Bamburi Cement lile Range Rover lilikuwa limechepuka kulia na sasa lilikuwa limeufikia mzunguko wa barabara jirani na ofisi za Azam.
Baada ya hapo sikujua ni barabara zipi tulizokuwa tukizipita zaidi ya kuona dereva akikunja kona moja baada ya nyingine kulifuata lile gari, hata hivyo bado tulikuwa makini kuhakikisha hawagundui kama wanafuatwa.
* * *
Inaendelea...