Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
- Thread starter
- #621
270
Niliamua kupiga moyo konde na kujaribu kuupoteza mshtuko mkubwa usoni mwangu kisha nikageuka na kumtazama yule mtu mwenye mavazi yaliyobana huku nikifahamu fika kuwa tayari usalama wangu ulikuwa mashakani na hivyo nilipaswa kuwa makini sana na watu wale.
“Nilidhani sisi ni wamoja, kwani ninyi ni akina nani na mna shida gani na mimi?” niliuliza kwa kujiamini ingawa niligundua kuwa sauti yangu ilikuwa imepwaya. “Au basi, ngoja niondoke.”
“Usijidanganye huendi popote. Tumekuwa tukiisubiri hii bahati kwa muda mrefu na hatuwezi kuichezea tena,” yule mtu mwenye mavazi yaliyobana aliongea huku akiivua miwani yake na hapo nikayaona macho yake na kumtambua. Alikuwa ni yule mwanamume aliyenifuata na gari aina ya Nissan Patrol jeusi asubuhi wakati naelekea Red Brick Restaurant kuonana na Leyla. Nilipoyatazama vizuri macho yake nikagundua kuwa hayakuwa na huruma hata kidogo.
“Tummalize kabla mambo hayajawa mengi,” mmoja wa wale watu alisema huku akiikoki bastola yake kuondoa usalama.
“No! huyu anahitajika akiwa hai, mkuu ana hamu ya kuonana naye akiwa hai,” yule mtu mwenye mavazi yaliyobana alisema. “Hebu mpekue.”
Kisha mmoja wa wale watu akanisogelea ili anifanyie upekuzi. Sikutaka kuendelea kuzubaa kwani nilifahamu fika nini ambacho kingefuatia baada ya pale. Nikaamua kufanya shambulio la ghafla, nikageuka kwa pigo makini nikiruka juu na kuzipiga teke bastola za wale watu wawili waliokuwa nyuma yangu.
Nilipotua chini nikamchota mtama yule mtu mwenye nguo za kubana na kumbwaga chini kama gunia. Alianguka huku akinitukana tusi zito na kunilaani kwa shambulizi lile makini la kushtukiza.
Wakati nakaa sawa mmoja wao hakunipa nafasi ya kujipanga badala yake akawahi kunichapa teke zito la kifuani lililonitupa ukutani na kunisababishia maumivu makali mno. Niliwahi kusimama haraka na kuchomoa bastola yangu kwani sikutaka kupoteza muda. Risasi moja niliyoiruhusu kufanya safari ikasafiri kwa shabaha makini na kukisambaratisha kichwa chake.
Kuona vile mtu mwenye mavazi yaliyobana akaruka juu huku akiachia teke kali, hata hivyo lilikuwa pigo dhaifu kwani niliwahi kulidaka kisha nikamchota mtama mwingine maridadi kupitia mguu wake mmoja uliosalia chini. Pigo lile likamfanya yule mtu atue chini kwa matako na kupiga yowe kali la maumivu huku akiponyokwa tena na tusi zito mdomoni. Alipotaka kuinuka akajikuta akitazamana na mdomo wa bastola yangu mkononi. Hofu iliyomwingia ikamrudisha chini taratibu.
Muda huo huo mlango wa kile chumba ukapigwa kumbo, wote tukashtuka na nilipotazama mlangoni nikawaona Leyla na Dennis Njoroge wakiingia kwa mtindo wa kininja, kwani waliruka juu na kutua katikati ya chumba kama paka huku bastola zao zikiwa mikononi tayari kwa lolote. Ujio wao ukanipa nguvu na hatimaye tukafanikiwa kuwadhibiti wale jamaa wawili. Kisha Leyla akawasiliana na kiongozi wa kikosi kazi Joram Kamau (E01).
Sikuwa na muda wa kupoteza kwani bado sikujua ni wapi alipokuwa Abshir. Rahma wa Singida tayari alikwisha dhibitiwa na Leyla na kukabidhiwa kunakostahili. Nikatoka na kuelekea ukumbini huku nikipishana na Joram Kamau akiwa na makachero wawili. Macho yetu yalipogongana tu nikanyanyua mkono wangu wa kushoto na kugusa upande wa kulia wa ncha ya kola ya shati niliyokuwa nimeivaa kumwashiria kuwa mambo hayakuwa shwari.
Bila kusita naye akanijibu kwa kugusa sikio lake la kushoto kuashiria kuwa hata yeye anaona hivyo. Nikaongeza mwendo na kuwapita nikielekea ukumbi wa mikutano kumtafuta Abshir. Nikakumbuka kutazama saa yangu ya mkononi na kugundua kuwa ilishatimia saa tisa na dakika hamsini na tisa. Ilisalia dakika moja tu mkutano ufunguliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya ambaye alifika kumwakilisha Naibu Rais.
Wakati nikishuka haraka toka kule juu nikamwona mwanamume mmoja aliyevaa suti ya gharama kama za wanausalama akiwa makini sana kutazama huku na kule kama aliyekuwa akitafuta kitu muhimu sana alichokipoteza, uso wake ulijawa na wasiwasi. Nikahisi mwili wangu ukisisimka na vinyweleo vikisimama, haraka nikavaa miwani yangu ili nimpige picha. Muda huo huo yule mwanamume aligeuka kutazama upande wangu na hapo nikawa nimempiga picha vizuri na ile miwani maalumu na kuzisafirisha mpaka kwenye tarakilishi ili kuoanisha sura yake na sura zilizokuwepo, kifaa kile kikambaini kuwa ni Abshir.
Nikamwona Abshir akinitazama kwa hofu katika namna ambayo nilifahamu kabisa kuwa alitaka kuzimia, kwani hakuamini kama nilikuwa hai, tena nikiwa kamili gado.
“Abshir yupo hapa, kila mmoja akae kwa tahadhari sasa!” nilisema kwenye kifaa maalumu kuwapa taarifa watu wangu wa kikosi kazi cha CSSG.
“Copy!” nikajibiwa mara moja.
Haraka nikatoka kasi kuelekea kule alikokuwepo Abshir, wakati huo Abshir alikuwa anapeleka mkono wake kwenye mfuko wa koti na kuchomoa bastola kubwa aina ya Kimber 1911, kisha akaielekeza kwangu akiwa tayari kwa lolote.
Sikujali, nilikusanya nguvu za kutosha nikaruka juu na kujiviringisha kwa kasi kuelekea alipokuwa amesimama na wakati huo huo nikisikia mvumo wa risasi zilizopita karibu yangu. Nikamkumba kwa nguvu. Sote tukapiga mweleka chini kama mizigo huku bastola ikimtoka Abshir na kuangukia kando. Hesabu zangu zikiwa zimeenda vizuri, nilichupa kuiokota ile bastola yake huku Abshir akiendelea kugaagaa pale sakafuni bila ya mafanikio.
“Gaidi! Msaada gaidi!” nilipiga kelele kutoa tahadhari kwa watu mle ukumbini. Nilikuwa nimefanya uamuzi wa kijasiri na wa hatari sana kwa kujitosa kumkabili yule gaidi. Na hapo nikamwona mwenyekiti wa kamati ya uratibu wa mkutano huo, Abdoulkader Omar akitoa amri kwa wanausalama fulani akiwataja kwa majina ili wanikamate. Nikatambua kuwa wao pia walikuwa miongoni mwa mamluki.
Kauli yake ilinitia hasira hasa nilipowashuhudia wanausalama wawili mamluki wakizielekeza bastola zao kwangu, macho yao yaliashiria mauaji. Sikusubiri, nikaruka na kutua kwa kupiga goti moja chini na kufyatua risasi mbili mfululizo zilizowapata wale mamluki kabla hawajafanya chochote. Mmoja risasi ilimpata kwenye kiganja chake cha mkono ulioshika bastola na kukisambaratisha na mwingine risasi ilimpata kwenye bega lake na kumtupa chini kama mzigo huku akipiga kelele za maumivu.
Kisha nikawaruka walinzi waliojaribu kunizuia huku bastola yangu ikiwa mkononi. Wakati nikiwa hewani mmoja wa walinzi akajaribu kunishika mguu na kunikosa, nikaanguka na kubiringika kama tairi, wakati huo huo nikasikia sauti ya Joram Kamau ikiwaamuru wale walinzi waniache nifanye kazi yangu. Nikaweka bastola yangu sawa kumwelekea Abshir kwani muda huo ni mimi tu niliyemwona wapi kasimama.
Abshir aling’amua hatari iliyomkabili, bila shaka alijua kuwa mimi ni bingwa wa shabaha, akajirusha kwenye dirisha la kioo na kukitawanya kioo kile vipande vipande na kuangukia nje. Sikumwacha, nami nikapita hapo hapo na kujikuta nipo nje chini. Nikamwona akikimbilia kwenye maegesho ya magari, nikaachia risasi moja iliyompata kwa nyuma upande wa kushoto wa kifua chake na kutokea mbele. Akaanguka chini akiwa hana uhai.
Nilimfuata na kusimama nikiutazama mwili wake kwa hasira, mara nikasikia sauti ya risasi kutoka ndani ya ule ukumbi wa mikutano. Nikashtuka na kurudi haraka kule ukumbini. Kumbe Joram Kamau na timu yake walikwenda kumweka chini ya ulinzi Abdoulkader Omar. Yeye alishatambua nini kingetokea na hivyo kabla hawajamfikia akachomoa bastola yake na kujipiga risasi kinywani kwa risasi moja tu iliyoufumua ubongo wake, akaanguka chini akiwa maiti.
Huu ni mwisho wa Msimu wa Tano kwenye mfululizo wa Harakati za Jason Sizya. Usikose Msimu wa Sita katika mkasa uitwao “Taharuki”.