267
Saa 7:15 mchana…
Nilikuwa nimeketi kwenye benchi nje ya chumba cha mapumziko katika Kituo cha Afya cha Kisimani alichokuwa amepumzishwa Merina tangu alipofikishwa hapo dakika ishirini na tano zilizokuwa zimepita.
Muda wote nilijiinamia kwa huzuni, mambo mengi yalipita kichwani kwangu nikijaribu kuwaza na kuwazua hili na lile pasipo kupata majibu. Nilimhurumia sana Merina kwani nilikuwa nimemwingiza kwenye hatari ambayo hakuitarajia, na hivyo ilitakiwa alindwe kwa gharama yoyote ili asidhuriwe.
Ni mimi niliyekuwa nimeshauri tumpeleke Merina kwenye hospitali yoyote iliyokuwa karibu kwa kuwa nilihisi alihitaji huduma ya haraka, na hivyo tulipofika Kituo cha Afya cha Kisimani kilicho mkabala na mgahawa maarufu wa Acapulco Club & Restaurant gari lililombeba likaingia hapo. Mara tulipomfikisha pale muuguzi aliyekuwa zamu alipomwona akagutuka, “Mungu wangu! Merina!”
“Vipi unamfahamu?” askari mmoja aliyekuwa na cheo cha Sajenti alimwuliza yule muuguzi.
“Ndiyo. Ni jirani yangu,” yule muuguzi alijibu kwa sauti ya mtetemo.
“Mtazameni kama hajaumia ndani kwa ndani,” nilisema wakati wahudumu wa kituo kile cha Afya cha Kisimani walipokuwa wakimbeba kumpeleka kwenye chumba cha daktari. Na baada ya daktari kumchunguza kwa umakini kwa dakika kadhaa alishauri apumzishwe kwenye chumba maalumu cha mapumziko wakati wakichukua vipimo vingine na akatundikiwa nusu lita ya
drip aina ya
Dextrose 5% yaliyowekwa dawa maalumu.
Nikiwa bado nipo pale kwenye benchi nje ya chumba hicho cha mapumziko wakati Merina akiendelea kuhudumiwa mara nikaliona lile gari lingine la Polisi aina ya Nissan Patrol likifika pale kituo cha afya na kumshusha Leyla kisha likaendelea na safari yake.
Wakati Leyla akikaribia pale nilipokuwa nimeketi mlango wa kile chumba cha mapumziko ukafunguliwa na daktari akatoka huku akinitazama kwa namna ambayo ilinichanganya kidogo. Alikuwa daktari mwanamke, mrefu, na alikuwa amevaa mavazi rasmi ya kidaktari na kuning’iniza kifaa cha kupimia mapigo ya moyo shingoni. Nikainuka haraka na kumkabili huku nikiwa na wasiwasi nikitaka kujua hali ya Merina.
“Amezinduka na tumemchunguza hajaumia sana isipokuwa alipatwa na mshtuko tu…” yule daktari aliniambia. Kisha akaongeza, “Unaweza kwenda kumwona.”
Kusikia hivyo moyo wangu ukararuka kwa furaha, na hapo nikaharakisha kuingia mle chumbani huku Leyla akinifuata nyuma.
“Jason!” Merina aliniita kwa furaha aliponiona nikiingia mle chumbani, akainuka bila kujali sindano yenye mrija wa drip aliyochomwa mkononi na kujitupa kwenye kifua changu huku akicheka na kulia wakati huo huo. Nilimkumbatia kwa upendo kisha nikampiga piga mgongoni huku nikimwambia kwa sauti ya upole iliyojaa mahaba, “
It's okay, baby… It's okay!”
Leyla alinitazama kwa namna ambayo ilionesha kuwa alikuwa na wivu juu yangu. Hata hivyo hakufanya chochote. Merina naye alimwona Leyla akashtuka sana na kunitazama machoni akionekana kutaka maelezo. Nikachukua nafasi ile kufanya utambulisho mfupi huku nikimtambulisha Leyla kwa Merina kuwa mtu muhimu aliyesaidia katika kumwokoa yeye Merina baada ya kutekwa na wale watu.
Kisha tuliketi mle chumbani na kuhitaji maelezo toka kwa Merina kuhusu jambo lolote alilolifahamu. Merina alitueleza kuwa siku tatu zilizokuwa zimepita walifika watu wawili pale Serena Beach Resort, walikuwa wageni wa meneja mkuu msaidizi ambaye pia alikuwa meneja matukio.
“Wale wageni walinitia shaka sana tangu nilipowaona mara ya kwanza, walikuwa wanaongea na meneja kwenye eneo la maegesho ya magari lakini hawakuwa wameniona na hivyo nikayasikia maongezi yao,” Merina alisema.
“Walikuwa wanazungumza nini?” nilimuuliza Merina kwa shauku.
“Walikuwa wanazungumza jambo fulani ambalo nahisi lilikuwa la siri na la hatari ambalo lilikuwa limepangwa kufanyika hapa Mombasa katika hoteli ya Bumburi Beach Villa. Sikuweza kusikia vizuri mazungumzo yao lakini miongoni mwa maongezi niliyoyasikia ni kuwa walitaka kumshinikiza Rais aviamuru vikosi vya Kenya vilivyopo Somalia viondoke nchini humo mara moja na kurudi Kenya,” Merina aliweka kituo na kututazama.
Nikaachia tabasamu huku nikibetua kichwa changu kama ishara ya kumhimiza aendelee kuelezea. Leyla pia alifanya vivyo hivyo.
“Niliogopa sana ingawa sikuelewa walipanga kufanya nini, nilitaka nimwambie rafiki yangu mmoja ambaye tunafanya kazi wote pale Serena lakini nikasita sana na kuamua kubaki na siri hiyo moyoni mwangu maana sikuwa namwamini yeyote hadi jana uliponiambia niwe makini kuna watu hatari pale hotelini, nikashawishika kukwamini kidogo, japo bado nilikuwa na mashaka na wewe,” Merina aliniambia.
Kisha Merina alifungua kifungo cha mfuko wa koti la suti yake ya kazini na kutoa bahasha ndogo ya rangi ya kaki.
“Hiyo ni nini?” mimi na Leyla tulijikuta tukimuuliza kwa shauku.
“Bahasha, niliificha baada ya meneja kuidondosha siku hiyo baada ya watu hao kuondoka na kuificha nikidhani kuwa huenda ndani yake kungekuwa na fedha. Hata hivyo nilipoifungua baadaye nikagundua kuwa haikuwa na fedha ila karatasi yenye maelezo ambayo yalinitia uvivu kuyasoma,” Merina alisema na hapo nikaichukua ile bahasha na kuifungua na ndani yake niliiona karatasi nyeupe iliyokunjwa mara tatu, nikaitoa na kuifungua kisha nikaanza kuisoma.
Ilikuwa na maelezo yaliyoandikwa kwa lugha ya kijasusi na hapo nikaelewa kwa nini Merina hakuelewa kilichoandikwa humo. Nilipoyasoma nikashtuka sana.
“Inaeleza nini?” Leyla na Merina walijikuta wakiniuliza kwa pamoja baada ya kuona hali yangu inabadilika baada ya kumaliza kuyasoma maelezo yale kwenye karatasi, nikampa Leyla bila kusema kitu huku nikishusha pumzi ndefu.
Leyla aliisoma ile karatasi na kuonesha kutaharuki sana, “Mungu wangu… ni leo saa kumi jioni?” Leyla aling’aka kwa taharuki baada ya kumaliza kusoma yale maelezo kwenye ile karatasi. “Ni lazima tuzuie tukio hili vinginevyo kutakuwa na umwagaji damu mkubwa na wa kutisha.”
Kisha Leyla alishusha pumzi na kuirudisha ile karatasi ndani ya bahasha na kisha alinipa, nikaitia mfukoni huku nikimkabili Merina.
“Kuna nini?” Merina aliniuliza tena huku uso wake ukiwa umejaa wasiwasi.
“Muda wote ulikuwa umeiweka wapi hii bahasha?” nilimuuliza Merina huku nikimtazama kwa umakini.
“Niliificha na leo asubuhi nikaichukua baada ya wewe kuniomba nikupelelezee pale hotelini kujua nini kinaendelea hasa kwa jambo ambalo ningehisi linatia shaka. Nilitamani sana kukwambia muda ule uliponiambia lakini nikasita. Nikaja kujilaumu baada ya wale wageni wawili waliokuja kunihoji kuhusiana na wewe,” Merina alisema huku uso wake ukiwa umejawa na wasiwasi mwingi. Niliyatafakari maneno ya Merina kisha nikashusha pumzi.
“Kwani kuna nini kimeandikwa humo kwenye hizo karatasi?” Merina akauliza tena baada ya kuona nipo kimya nikiwa nayatafakari maelezo yake.
“Kundi la Al Shabab limepanga kufanya shambulio la kigaidi leo Ijumaa kwenye mkutano wa wafanyabiashara pale Bamburi Beach Villa. Mipango yote ya utekelezaji imeshakamilika na kilichobaki ni utekelezaji tu,” nilimwambia Merina baada ya kufikiria kidogo. Nikamwona akitweta.
Kwenye yale maelezo ilionesha kuwa mipango yote ya kigaidi ilikuwa inaratibiwa na watu watatu, Abdoulkader Omar ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya uratibu wa mkutano huo, Kanali Sultan Jamal aliyekuwa mkuu wa operesheni za ndani wa Usalama wa Taifa nchini Kenya, na Ahmed Kareem, meneja mkuu msaidizi wa Serena Beach Resort. Kanali Sultan Jamal na Ahmed Kareem walikuwa Wakenya wenye asili ya Somalia.
Kilitokea kitambo fulani cha ukimya kisha Leyla alinipa ishara tutoke nje mara moja, na tulipotoka tu akanikabili.
“Jason, narudia tena kusema ahsante sana kwa ujio wako hapa Kenya maana bila wewe sidhani kama haya mambo tungeyajua mapema. Kupitia maelezo hayo nimetambua kwa nini taarifa za kiintelijensia zilikuwa zinawafikia hawa jamaa!” Leyla aliniambia na kushusha pumzi. “Sasa itabidi twende kwa mkuu wangu wa Usalama wa Taifa Kaunti ya Mombasa tukamweleze kila kitu kuhusiana na jambo hili.”
“Huyo mkuu wako unamwamini?” nilimuuliza Leyla huku nikimtazama kwa tuo.
“
Of course! Ni yeye ambaye amekuwa msaada mkubwa sana kwenye operesheni zangu,” Leyla aliniambia.
Sikutaka kubishana naye. Nikatazama saa yangu ya mkononi na kushtuka. Ilikuwa imeshatimia saa saba na dakika hamsini za mchana, hii ilimaanisha kuwa zilibakia saa mbili na dakika kumi tu kabla ya tukio la kigaidi kutokea, na hivyo hatukuwa na muda wa kupoteza. Kila kitu kilipaswa kufanywa chap chap.
* * *
Inaendelea...