393
Saa moja baadaye, mnamo saa kumi na mbili na dakika ishirini, mimi na Daniella tulikuwa ndani ya chumba maalumu cha mikutano cha Rais Masinde katika Ikulu ya Dodoma. Rais Masinde alikuwa ameomba kuongea nasi wawili tu ofisini kwake.
Wakati wa maongezi yetu, Rais Masinde aliwaagiza wasaidizi wake kutuandalia vinywaji ambavyo tungevihitaji. Hata hivyo tuliamua kuwa wazalendo kwa kunywa Konyagi. Kila mmoja wetu alikuwa na bilauri ya Konyagi, mvinyo unaozalishwa nchini Tanzania kwa kutumia zabibu za Dodoma. Rais alikuwa anakunywa sharubati ya mchanganyiko wa embe na pasheni.
“Hakika ninyi ni mashujaa ambao nchi ya Tanzania imejaaliwa kuwapata. Nchi hii inapaswa kujivunia watu kama ninyi,” Rais Masinde alisema kwa furaha baada ya wasaidizi wake kutoka na kutuacha peke yetu. “Nimepewa taarifa zenu zote jinsi mlivyohangaika usiku kucha mkikumbana na misukosuko mingi, ninathubutu kusema kuwa ninyi wawili ndiyo mlikuwa mmeushikilia moyo wa nchi hii.”
Hatukumjibu bali tuliinamisha vichwa vyetu kwa heshima kukubali sifa alizotumwagia. Mara Rais Masinde akaonekana kukumbuka jambo.
“Hivi mmepata mahitaji yote?” Rais Masinde alituuliza huku akitutazama kwa umakini.
“Usijali, mhesimiwa Rais, tumepata kila kitu,” niliwahi kusema.
“
Good!” alisema Rais Masinde na kushusha pumzi za ndani kwa ndani. kisha akaongeza, “Natumai mmefuatilia hotuba niliyoitoa jioni hii?”
“Ndiyo mheshimiwa Rais!” mimi na Daniella tulijikuta tukiitikia kwa wakati mmoja na kutazamana.
Halafu nikaongeza, “Hongera sana, mheshimiwa Rais. Hakika umeingia katika historia ya dunia kama Rais shujaa asiyeyumba. Kitendo hiki ulichokifanya leo naamini kila mwananchi huko aliko anakupongeza kwa ushujaa huu. Hakuna aliyetegemea kama ungekuwa na ujasiri mkubwa wa namna hii. Ahsante sana mheshimiwa Rais kwa kuyazingatia maadili ya nchi.”
Rais Masinde alinyanyua bilauri yake ya sharubati na kupiga funda kubwa kisha akafumba macho kwa sekunde kadhaa akiusiklizia ubaridi wa ile sharubati wakati ikishuka kooni kwake. Kisha akasema, “
But… it wasn’t that easy, young man!”
“
I know!” nami nilimjibu pasipo shaka yoyote.
“
Imagine, unatoka kwenye
situation kama yangu halafu unatakiwa utoe hotuba kama ile…” Rais Masinde alisema na kuongeza, “…leo nina furaha kubwa kwani nimefanya jambo ambalo sikutegemea kulifanya. Kwa muda mrefu nilikwisha choshwa kuwa kibaraka wa mataifa makubwa lakini sikuwa na ujasiri wa kuweza kupambana nayo. Nimekuwa Rais kivuli kwa muda mrefu na sitaki kuendelea kuwa kivuli kwa kuwaachia watu wengine wafanye uamuzi juu ya nchi hii…
“Wananchi waliponichagua walikuwa na uhakika mkubwa wa maisha yao kuboreka lakini mpaka leo bado sijaitimiza ahadi hiyo. Nilifanywa kibaraka lakini sasa nimeamua kutoka kuwa kibaraka wa mashetani hawa na kuwa Rais wa Watanzania. Nataka niisafishe nchi. Nataka niondoke madarakani taifa likiwa safi kama lilivyoachwa na waasisi wetu.”
Kufika hapo Rais Masinde alinyamaza na kuigugumia sharubati yote iliyokuwemo katika bilauri yake.
“Mheshimiwa Rais, niseme tu hiki ulichokifanya umedhihirisha wazi kuwa wewe si mtu wa kutaka kutumiwa. Sisi tutakuwa nawe bega kwa bega kuhakikisha unafanikiwa kwenye misheni yako,” Daniella alisema baada ya kupiga funda la Konyagi na kuikita bilauri yake juu ya meza ndogo iliyokuwa mbele yake.
“Ahsante sana, binti… Ninaamini kwa uongozi wa Mungu tutapambana na kulishinda genge hili lenye kutaka kuiharibu dunia. Niseme tu, karibu sehemu kubwa ya watu wanaonizunguka si wazuri kwa kuwa nilipewa maelekezo ya kuwateua, kwa hiyo utaona ni namna gani tulivyo na vita ngumu. Kinachoniumiza moyo ni kuwa wananchi hawajui kuhusu genge hili bali wananifahamu mimi. Nchi ikiyumba lawama zote zitaniangukia…” Rais Masinde alisema kwa huzuni.
Kisha kikakotokea kitambo kifupi cha ukimya kabla Rais Masinde hajavunja ukimya huo. Alikuwa anazungumza kwa huzuni kubwa. “Kingine kibaya zaidi, hata mke wangu Juliana alikuwa upande wao!”
Hatukushangaa sana maana tayari tulikwisha ambiwa kuhusu jambo hili na Askofu Masinde. Ndipo sasa ukafuata wakati ambao Rais Masinde aliamua kutusimulia mambo ambayo, kwa kauli yake mwenyewe, watu wachache sana waliyafahamu.
Alitusimulia jinsi alivyokutana na mwanadada Juliana Isidory Magupa ambaye baba yake alikuwa Mtanzania mwenyeji wa Mwanza lakini mama yake akiwa na asili ya Rwanda.
Wawili hawa walikutana masomoni katika Jimbo la Texas nchini Marekani, wakati yeye Masinde akichukua Shahada ya Pili ya Mawasiliano kwa Umma. Juliana yeye alikuwa anachukua Shahada ya Kwanza ya Sheria.
Huko ndiko uhusiano wao ulipoanzia na baadaye walikuja kufunga ndoa baada ya Albert Masinde kuamua kubakia pale chuoni kufundisha.
Jambo ambalo hakulijua ni kwamba tayari Juliana alikuwa mwanachama wa jamii ya siri ya
Triangle na alikuwa ameshapata mafunzo mbalimbali ya kijasusi, na mojawapo ya masharti aliyokuwa akiyafuata ni kutozaa, ndiyo maana katika ndoa yao hawakubahatika kupata mtoto, ila Albert alikuwa na watoto mapacha aliowapata kabla hajakutana na Juliana.
Wakati Albert Masinde akifundisha chuoni, Juliana alikuwa akizunguka sehemu mbalimbali duniani kama mwanaharakati wa kupagania haki za binadamu na kuna wakati alianza kupata umaarufu mkubwa miongoni mwa wanaharakati duniani.
Baada ya miaka kadhaa ya kufundisha huko Marekani, Juliana alimshawishi Masinde kuingia kwenye siasa na kuahidi kumsaidia kwa kila hali hadi afikie nafasi ya juu ikiwemo kuwa mkuu wa nchi. Jambo hili lilikuwa gumu sana kwa Albert Masinde kwani hakuwahi kufikiria kuwa mwanasiasa na hakujua angeanzaje.
Ndipo Juliana alipoanza kumkutanisha na watu mbalimbali mashuhuri pasipo kumwambia ukweli kuwa walikuwa wakitoka katika jamii ya siri ya Triangle, na watu hao waliahidi kumsaidia Masinde kufikia ndoto hiyo.
Akaacha kazi na kurudi Tanzania ambako aligombea ubunge na kushinda kwa kishindo, kisha Rais wa wakati huo, Kingoba Mgaya, akamteua kuwa Waziri wa Tamisemi na baadaye alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje. Hapo ndipo nyota yake ilipong’ara. Akajulikana kila kona ya nchi.
Miaka mitano baadaye wakati Rais Mgaya akijiandaa kustaafu, katika mchakato wa kumtafuta mrithi wake ndipo jina la Dk. Albert Masinde lilipopenya kimiujiza na hatimaye kuwa mgombea Urais wa Chama tawala.
Sasa wakati akitusimulia, Rais Masinde alikuwa anadhani kuwa huenda zilitumika nguvu za ziada zikiwemo zile za giza katika kumfanya akubali kila kitu alichoambiwa na Juliana na hata kwenye mchakato ndani ya chama.
“Natambua kuna mambo mengi machafu mke wangu aliyafanya ikiwemo kujiingiza katika imani za kishetani. Alikuwa na nguvu za ajabu akifanya mambo ambayo wengine hawawezi kuyafanya, na ilifikia hatua ya kunieleza kuwa hata mimi ningeweza kuwa na uwezo kama ule endapo ningehitaji. Uwezo wa kufanya mambo makubwa kushinda uwezo wa mwanadamu,” Rais Masinde aliongea kwa huzuni.
“
So sorry for that, Mr president. Sikujua kama umepitia mambo magumu namna hiyo,” nilisema kwa huzuni huku nikimtazama Rais Masinde usoni. Niliyahisi maumivu aliyokuwa akiyapitia wakati huo.
“Ni kweli, Jason, nimepitia mambo mengi magumu sana katika kipindi hiki cha urais wangu. Mambo mengine siwezi kuwasimulia… kwa muda mrefu nilitafuta upenyo wa kuniwezesha kuachana na watu hawa lakini nilishindwa. Hili si jambo jepesi. Ni jambo la hatari kubwa kwani hawa jamaa ni watu hatari kama nilivyoeleza lakini pamoja na hatari hiyo sasa nimeamua kupambana nao,” Rais Masinde alisema.
Kisha aliitazama saa iliyotundikwa ukutani mle ofisini kwake na kugutuka kwa mshtuko. Nami niliyapeleka macho yangu kuitazama saa ile, nikagundua kuwa ilishatimia saa moja kamili za jioni. Muda huo Rais alitarajiwa kupumzika.
Mara wasaidizi wake waliingia na kumpa taarifa kuwa muda wa kupumzika ulikwisha fika na kwamba tulipaswa kuondoka na kumwacha rais apumzike. Rais Masinde akainuka na kutupa mkono. Tukaagana na kutoka.
* * *
Endelea...