117
Nilikumbuka vyema na picha nzima ya kilichotokea ilikuwa ikipita kichwani kwangu kama niliyekuwa natazama filamu. Nilikumbuka jinsi nilivyokuwa nakunywa pombe kali aina ya Grant’s Whisky kama maji baada ya kunywa Konyagi, Savanna na Heineken.
Muda wote Swedi alikuwa ameketi kwenye sofa lililokuwa jirani akinitazama kwa huzuni. Na baadaye nilianza kuhisi hali yangu ikianza kuwa mbaya kadiri sekunde zilivyokuwa zikiyoyoma na kichwa changu kikiwa kizito mno. Kisha macho yangu yalipoteza nguvu ya kuona na ukungu mwepesi ulitanda kwenye macho yangu…
Hivyo tu! Ni hivyo tu ndivyo nilivyovikumbuka, hakuna kingine isipokuwa kuwa na Swedi pale sebuleni, na kugida pombe kama maji, basi! Nilipojaribu kukumbuka mambo mengine kichwa changu kiligoma kabisa kuyakumbuka!
Amanda alionekana kama aliyekuwa anataka kuniambia kitu lakini alikuwa anasita kusema.
“Swedi yupo wapi?” nilimuuliza Amanda huku nikimwangalia usoni kwa umakini.
“Ameshaondoka baada ya kuhakikisha uko salama. Ulitapika sana na nguo zote zimechafuka,” Amanda aliniambia kwa sauti ya upole huku akinitazama kwa namna ya upendo kama vile mama amtazamaye mwanawe wa pekee.
“Duh! Sasa ilikuwaje wewe ukawa hapa saa hizi wakati haukuwepo?” nilimuuliza Amanda kwa wasiwasi.
“Ni hadithi ndefu kidogo, ni vyema ukapumzika kwanza ili upate nguvu, baadaye tutazungumza,” Amanda aliniambia kwa sauti ya upole katika namna ya kunitia moyo.
“Unajisikiaje kwa sasa?” Amanda aliniuliza huku akijiweka vizuri pale kwenye sofa.
“Najisikia nafuu kidogo ingawa kichwa kinauma sana na ninahisi njaa,” niliongea kwa sauti tulivu huku nikipiga mwayo hafifu.
“Usijali, nimeshaandaa chakula ambacho naamini utakipenda,” Amanda aliniambia huku akinitazama kwa utulivu na kisha akaachia tabasamu. Taratibu akaanza kunikandakanda misuli ya mapajani na kunifanya nijisikie faraja.
Baada ya kitambo fulani cha kunikandakanda aliinuka na kuniacha pale kwenye sofa akaelekea jikoni. Mara tu alipoondoka nilijikuta nikiupisha utulivu kichwani mwangu. Nilipoitazama saa yangu ya mkononi nikagundua kuwa ilikuwa inaelekea kutimia saa 2:20 usiku. Nikajiuliza ilikuwaje Amanda akawepo nyumbani kwangu muda huo baada ya kile kilichokuwa kimetokea kati yetu?
Mimi na Amanda tulikuwa tumehitilafiana baada ya kumkuta na akiwa na mwanamume mwingine mjini Ushirombo, na wakati huo mimi pia nilikuwa na Rehama. Kilichoniudhi zaidi ilikuwa ni baada ya kugundua kuwa mwanamume huyo alikuwa mbioni kumuoa.
Baadaye nikaja kusikia tetesi kuwa Amanda na mwanamume huyo waliingia kwenye mgogoro mkubwa baada ya mwanamume huyo kugundua kuwa Amanda alikuwa bado ananipenda kuliko mwanamume yeyote aliyewahi kukutana naye. Hii ilidhihirika baada ya mkasa ulionipata wa kupigwa risasi kifuani na Jamila siku nilipokuwa nyumbani kwangu na Asia baada ya kutokea mtafaruku kati yetu.
Kipindi chote nilichokuwa nimelazwa hospitali Amanda alikuwa anakuja kuniona na alishinda pale hospitali akisaidiana na Mama na shemeji Emmy, mke wa kaka Eddy, wakinihudumia.
Kitendo cha kuonesha kuwa alikuwa ananipenda sana kilimfanya mwanamume huyo kuingiwa na wivu na kusababisha ugomvi kila siku na ilifikia hatua mwanamume huyo aliamua kuachia ngazi na hivyo Amanda akarudi kwao. Hata hivyo, bado kwangu ilikuwa vigumu sana kumrudisha Amanda moyoni mwangu.
Mara kwa mara Amanda alikuwa analia kila aliponiona nikiwa nimekata tamaa, aliahidi kufanya kila jitihada ili ahakikishe ninapona majeraha ya moyo wangu yaliyosababishwa na mkasa ulionipata hasa kitendo cha kuwa mbali na Rehema. Na kweli mwanzoni alikuwa anafika nyumbani kwangu kila asubuhi, akanifulia nguo, akasafisha nyumba yangu na kunipikia. Alikaa hapo hadi jioni akihakikisha nimekula ndipo alipoondoka kurudi nyumbani kwao Uwanja wa Taifa.
Baadaye alipunguza kuja nyumbani kwangu ingawa alichokuwa anakifanya ni kununua muda kwa kuamini kuwa kidogo kidogo ningeuona umuhimu wake na pengine ningerudisha upendo na hatimaye tungeoana.
Kaka yangu Eddy na rafiki yangu Swedi, kwa nyakati tofauti walinishauri kumuoa Amanda aliyekuwa anaonesha upendo mkubwa kwangu na kumsahau Rehema, lakini bado akili yangu ilishindwa kukubaliana na jambo hilo. Niliamini kuwa nilikuwa nimezaliwa kwa ajili ya Rehema na Rehema alizaliwa kwa ajili yangu. Basi!
“Oh Rehema! Nisamehe mpenzi wangu,” niliwaza huku machozi yakianza kunitoka hasa kila nilipokumbuka vitendo vibaya nilivyomfanyia. Machozi yakazidi kunimwagika usoni mwangu. Majuto ambayo niliyasikia moyoni mwangu kusema kweli yalianza kuniumiza sana.
“Jason, mbona unalia?” sauti ya Amanda ilinishtua sana toka kwenye mawazo yangu, nikayapangusa.
Muda huo Amanda alikuwa amesimama akinitazama kwa umakini baada ya kuweka taratibu trei kubwa iliyosheheni vyakula juu ya meza ndogo ya kioo na kisha akaisogeza mbele yangu, halafu akakaa pembeni yangu huku akinitazama usoni mwangu.
“Jason, unapaswa kuwa jasiri na kujitahidi kusahau, haya nayo yatapita tu,” Amanda aliniambia kwa sauti ya upole huku akiniangalia usoni. Nilibaki kimya nikiwa naangalia chini.
“Jason!” Amanda aliniita huku akinishika mashavu yangu, na kunigeuza uso wangu sehemu alipokaa. Tukatazamana kwa muda pasipo kuzungumza chochote.
“Nimekufahamu kwa muda mrefu sasa na hata hisia zangu nilizikabidhi kwako, sijali kama leo unanichukia au lah, ila ukweli utabaki kuwa nilikupenda, ninakupenda na nitakupenda maisha yangu yote. Kwa nini unakuwa mnyonge kiasi hiki?” Amanda alizungumza kwa sauti ya upole iliyojaa unyonge ndani yake.
“Naomba niache nile,” nilimwambia Amanda huku nikishusha pumzi za ndani kwa ndani kisha nilichukua sahani ili nijipakulie chakula. Sikutaka kumpa nafasi ya kunisaili kwa sababu nisingeweza kuyajibu maswali yake.
“Samahani kama nimekukwaza,” Amanda alisema kwa unyonge huku akishusha pumzi na kuninyang’anya ile sahani.
Kisha alifumba macho yake na kuanza kukiombea kile chakula na alipomaliza kuomba akachukua kijiko kikubwa na kupakua chakula kwenye sahani na kunipa huku akinikaribisha. “Karibu.”
Nilipokea ile sahani na kugundua kuwa alikuwa ameandaa wali wa nazi, mchuzi mzito wa kuku ulioungwa kwa nazi pia. Bakuli la mboga za majani pembeni, na sahani yenye matunda aina ya nanasi, embe na vipande vya tikiti maji vilivyokoza wekundu. Pia kulikuwa na jagi la maji baridi.
Nilishangaa sana maana sikujua Amanda alikiandaa chakula kile muda gani, nilitaka kumuuliza lakini nikasita. Nilianza kula kwa kasi huku nikiwa nimejawa na uchungu mwingi kwenye moyo wangu. Nilikuwa nayakumbuka mambo mengi ambayo nimeyafanya na Rehema, ahadi nyingi ambazo nilipanga na Rehema lakini nikaishia kumlipa ubaya na kumsababishia kulala kitandani akiwa nusu mfu kwa tamaa zangu za kimwili.
Hata hivyo nilijikuta nikishangaa, kwani pamoja na mawazo mengi kuniandama lakini chakula kilikuwa kinashuka vilivyo kooni kwangu kutokana na ustadi wa mapishi. Kwa kweli kilikuwa chakula kitamu sana na Amanda alikuwa msichana fundi wa kupika ingawa akili yangu iliyakubali zaidi mapishi ya Rehema.
Amanda naye alikuwa amejipakulia chakula kwenye sahani yake na kuketi kando yangu, akawa anakula kimya kimya huku akinitupia jicho la wizi. Nilimaliza kula kisha nikashushia na matunda halafu maji. Amanda akanipa kimbaka ili kuondoa masalio ya chakula kwenye meno yangu. Moyoni niliyasifia mapishi ya Amanda ingawa sikumweleza waziwazi.
Hadi muda huo swali moja lilizidi kuitesa akili kwangu, nilikuwa najiuliza ilikuwaje Amanda akawepo nyumbani kwangu muda huo! Au ni Swedi alikuwa amempigia simu? Nilitamani kumuuliza lakini nikasita. Nilichofanya ni kumshukuru kwa chakula kitamu alichonipikia. Nilihisi huenda alifanya hivyo kwa matarajio kuwa pengine angefanikiwa kuuteka tena moyo wangu ingawa haikuwa hivyo, kwani nilimwona kama dada yangu badala ya mpenzi.
Niliiangalia saa yangu nikagundua kuwa ilikuwa imeshatimu saa 3:15 usiku, nikamwambia Amanda kuwa nilihitaji kuwa peke yangu. Ingawa alionesha kusita sana lakini hakuwa na namna ya kufanya kwani sikuhitaji kuwa na mwanamke yeyote ndani ya nyumba yangu wakati huo. Kwa shingo upande Amanda aliinuka ili aondoke.
“Jason!” Amanda aliniita huku akiniangalia usoni.
“Naam!” niliitika huku nikiwa simwangalii usoni.
“Naomba tu uniambie kama kuna jambo lolote baya sana ambalo nimekufanyia!” Amanda aliniuliza huku akionekana mnyonge zaidi.
“Kwa nini?” nilimuuliza huku nikimtazama usoni kwa umakini.
“Nahisi kama vile umekuwa hufurahii uwepo wangu nyumbani kwako, na kila ninachokuongelesha unanijibu kwa mkato tu ukionekana kutawaliwa na hasira! Ni kosa lipi lisilosameheka nililokufanyia?” Amanda aliniuliza huku akijitahidi kuyazuia machozi yaliyoanza kumlenga lenga.
“Wala hujanifanyia jambo lolote baya, ni kwamba mara nyingi nikiwa katika hali ya namna hii huwa sipendi kuzungumza na mtu. Ninapenda kuwa peke yangu,” nilimjibu Amanda huku nikijitahidi kuifanya sauti yangu iwe ya kawaida isiyo ya hasira.
“
Okay! Basi ngoja nikuache… usiku mwema,” Amanda alisema na kuanza kupiga hatua zake taratibu kuelekea mlangoni huku machozi yakianza kumtoka. Sikupenda kumwona akiondoka katika hali ile ya huzuni, ikanibidi nimuwahi.
“Amanda!” nilimwita huku nikipiga hatua kumfuata, akageuka kunitazama huku akifuta machozi. “Naomba unielewe, sijakufukuza nyumbani kwangu na siwezi kukufukuza bali nahitaji kuwa peke yangu kwa muda,” niliongea kwa sauti tulivu baada ya kumfikia na kusimama mbele yake huku nikimtazama machoni.
“Jason, mimi ni mnyonge, najua sina thamani yoyote kwako. Ni kweli nilifanya makosa wakati fulani lakini sistahili kuadhibiwa kiasi hiki. Unajua kabisa nilikukabidhi moyo wangu nikitarajia furaha ila ninachokutana nacho sasa si kile ambacho nilikitegemea,” Amanda alizungumza huku machozi yakimwagika usoni mwake.
Kusema kweli maneno yake yalipenya moja kwa moja hadi moyoni mwangu, taratibu nikamvuta hadi karibu na mwili wangu na kumkumbatia huku nikimfuta machozi kwa vidole vyangu.
“Usihuzunike, nipe muda tu natumaini mambo yatakaa sawa,” nilisema huku nikimwachia.
Tukaangaliana kwa kitambo fulani kila mmoja akiwa kimya, na baada ya kitambo kile Amanda akaachia tabasamu lililoonekana kubeba uchungu ndani yake na kisha akafungua mlango na kuondoka zake. Na mara tu nilipobaki peke yangu mawazo yangu juu ya Rehema yakaibuka upya.
Ukweli ni kwamba niligundua kuwa nilikuwa nampenda Rehema kwa dhati ya moyo wangu. Kumbukumbu juu ya Rehema zilipita akilini kwangu, nilikumbuka nyakati za raha pindi tulipokuwa pamoja, nikakumbuka pia nyakati za mgogoro. Kisha nikazipima nyakati hizo katika mizania kwa lengo la kutafuta uwiano. Raha zilizidi shida kwa uzito usio na hata chembe ya mnuso!
Kwa matokeo hayo nilijiaminisha kuwa; Rehema ndiye alikuwa mwanamke wa maisha yangu.
“Kama alikuwa mwanamke wa maisha yangu, ilikuwaje nikamsaliti na wanawake wengine?” niliwaza. Hata hivyo, jawabu lilikuwa fupi tu, kwamba sikuitambua thamani yake hadi baada ya kumpoteza katika maisha yangu.
* * *
Itaendelea...