Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

View attachment 2169944
28

Mrembo wa Shani


Saa 7:20 mchana…

NILILIKUTA basi la Makenga likiwa bado pale pale stendi na hakukuwa na abiria yeyote aliyeongezeka, nikaingia ndani ya basi na kumkuta Eddy akiwa bado ameuchapa usingizi. Niliketi taratibu kwenye kiti changu huku nikiitoa mfukoni ile simu aina ya Tecno Camon 16 Pro niliyoichukua toka kwa yule msichana ambaye sikujua nimwite Tabia au Chausiku. Kisha nilianza kuichunguza kwa umakini.

Na wakati nikiendelea na uchunguzi wangu nilishtushwa na sauti kali ya honi ya gari, nilipoangalia upande ambao sauti hiyo ilitokea nikaliona basi lililokuwa na maandishi ubavuni, STAREHE TRANS, likiingia kwa mbwembwe pale stendi ya mabasi ya sagara mjini Nzega.

Sikujua lile basi lilikuwa linatoka wapi na kuelekea wapi ila nilichoshuhudia ni kundi kubwa la wachuuzi wa biashara ndogondogo wakigombea kuuza bidhaa zao kwa abiria waliokuwemo ndani ya basi hilo, huku wapiga debe na madereva wa teksi na bodaboda wakizongazonga mlangoni kujaribu kupata abiria.

Niliinua mkono wangu wa kushoto wenye saa nikaitazama saa yangu na kushusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani. takriban saa nzima ilikuwa imekatika tangu tuwepo pale stendi ya Nzega tukiwa ndani ya basi la Makenga na bado sikuona dalili yoyote ya kuondoka kuelekea Kahama.

Nikiwa nimeanza kukata tamaa nikamwona mpiga debe aliyetushawishi kukata tiketi katika basi la Makenga akija huku ameongozana na abiria watatu walioshuka toka ndani ya basi la Starehe lililofika pale Nzega muda mfupi.

Mmoja kati ya wale abiria walioongozana na mpiga debe alikuwa mwanamume na abiria wawili walikuwa wanawake. Walipofika pale kwenye gari letu walimkuta kondakta wa basi akiwa amesimama karibu na mlango akiwa tayari kupokea nauli. Macho ya kondakta yalikuwa makali na yaliwatazama abiria wake kwa utulivu huku akitengeneza tabasamu jepesi usoni kwake lililoyafanya meno yake makubwa yaliyopoteza mng’ao wake kutokana na ukungu wa moshi wa sigara kuonekana.

Baada ya kuwafikisha wale abiria yule mpiga debe aliondoka haraka kwenda kuita abiria wengine wa kuja kujaza viti vilivyosalia, na wakati huohuo mabasi mengine yalianza kuondoka taratibu baada ya kujaza abiria.

Bila kupoteza muda yule abiria mwanamume alitoa pochi yake kutoka kwenye mfuko wa nyuma wa suruali na kuifungua kisha akatoa noti mbili ambazo sikujua zilikuwa za thamani gani na kumpatia yule kondakta wa basi kama malipo ya nauli ya watu wawili.

Kondakta alizipokea zile noti kisha alifanya kuzinyanyua juu akizielekeza kwenye mwanga wa jua katika namna ya kuangalia uhalali wake kabla ya kuzihifadhi vyema na kisha aliandika tiketi mbili na kumkabidhi yule abiria mwanamume.

Yule mwanamume alizipokea kisha yeye na mwanamke mmoja, ambaye kwa mwonekano tu alionekana kuwa ni mkewe, walishika vyema mabegi yao madogo ya safari na kuingia ndani ya basi kisha waliongoza moja kwa moja wakanipita na kwenda kuketi kwenye viti vilivyokuwa kule nyuma.

Abiria mmoja, msichana, alibaki palepale chini Jirani na mlango wa kuingilia ndani ya basi akiwa ameegemea gari, alionekana kusita sana na kuna wakati alinyanyua shingo yake kuchungulia mle ndani ya basi huku akiyazungusha macho yake kama aliyekuwa anatafuta kitu kisha alishusha pumzi ndefu akionekana kukata tamaa.

Kondakta wa basi alimkodolea macho yule msichana, macho yake yalijaa matamanio na alionekana kuduwaa kwa muda huku macho yake yakiganda kwenye uso ya yule msichana kisha yalianza kutambaa taratibu kwenye umbo la yule msichana kiasi cha kunifanya nianze kupatwa na mshwawasha na kuvutwa kumtazama vizuri yule msichana ili nione kilichomfanya yule kondakta kuduwaa kiasi kile.

Nilinyanyua kidogo shingo yangu na kumtazama vizuri yule msichana na hapo macho yangu yakaangukia kwenye umbo zuri la yule msichana. Kwa mwonekano wa haraka tu sikushindwa kutambua kuwa alikuwa msichana mrembo wa shani, mwenye macho mazuri na malegevu lakini yaliyokuwa makini sana kuliko hata simba jike anayewinda.

Kwa mlingano wa macho tu, yule msichana alitoa tafsiri ya kuwa na ule uzuri usiomithilika na uwezao kumliwaza, kumpumbaza na hata kumlaza kitandani mwanamume yeyote aliye buheri wa afya.

Moyo wangu ulipiga kite kwa nguvu na hamu ya kutaka kumfahamu zaidi yule msichana iliibuka ndani yangu, nilianza kubabaika kutokana na uzuri wake kwani alikuwa mrembo haswa wa haja kiasi kwamba moyo wangu uliraruka kwa shauku ya kutaka kuwa karibu naye. Nilishindwa kumlaumu yule kondakta kwani nilielewa kwa nini aliduwaa na kusahau majukumu yake kwa muda, ni kwa sababu alikuwa amebabaishwa na uzuri wa yule msichana.

Nilimkodolea macho yule mrembo wa shani huku nikijaribu kuyasanifu mazuri mengi ya yule mrembo aliyejitanashati kikweli kweli mbele ya macho yangu!

Alikuwa ni msichana mrefu ambaye kwa mwonekano tu hakupungua futi 5 na inchi 10, hakuwa mweupe wala mweusi na alikuwa na haiba nzuri ya kuvutia. Alikuwa amevaa suruali ya jump suit ya rangi ya maruni iliyolichora vema umbile lake refu lenye tumbo dogo, nyonga (hips) pana na kiuno chembamba kilichoshikilia mzigo mkubwa wa makalio na minofu ya mapaja yake yaliyonona vyema, na shingoni alivaa kidani cha dhahabu ambacho sikuweza kukitazama kwa makini kwa vile taswira ya matiti yake madogo yaliyotishia kuitoboa ile blauzi ilizivuruga hisia zangu.

Nywele zake nyeusi ndefu na laini alikuwa amezifunika kwa kofia nyekundu ya kapelo. Nyusi zake alikuwa amezitinda vizuri na kuzipaka wanja mwembamba ulioonekana mfano wa mwezi mwandamo, kope zilikuwa zimerembwa vyema na kuyafanya macho yake malegevu yaonekane vizuri na kupendeza.

Alikuwa na midomo yenye maki na kingo pana zilikolezwa kwa rangi nyekundu na vishimo vidogo mashavuni kwake vilionekana na kuongeza ziada nyingine katika utamu wake. Miguuni alivaa raba ngumu za rangi nyekundu na begani alining’iniza mkoba mzuri wa rangi ya nyekundu, ambao kwa mtazamo tu ulionekana kuwa wa thamani kubwa. Mkono wake wa kulia ulikuwa umeshika begi dogo jeusi la safari lililokuwa na magurudumu madogo.

Nikiwa na uhakika kuwa yule msichana alikuwa hafahamu chochote kuwa nilikuwa namtazama hasa kwa kuwa nilikuwa nimevaa miwani myeusi ya jua iliyoyaficha macho yangu, niliendelea na udadisi wangu nikiuajabia uzuri wake usiomithilika huku hisia za upweke zikianza kunitawala.

Nilianza kuomba kimya kimya moyoni ili asighairi safari na aridhie kupanda basi la Makenga kwa sababu alionekana kutopenda kukaa kule kwenye viti vya nyuma, ambavyo hadi wakati huo nafasi ilikuwa imebaki ya abiria wanne tu. Nilisubiri kuona angechukua uamuzi gani kwani nilishavutiwa naye na nilichokisubiri ni namna ya kutengeneza urafiki naye, japokuwa sikujua alikuwa anaelekea wapi.

Nilimtazama kwa namna ya kumchunguza kuanzia unyayoni hadi utosini. Mara nikamwona akinyanyua uso wake kuniangalia na macho yake yalitua na kuweka kituo kwenye uso wangu, na hapo nikamwona akishtuka kidogo. Alinitazama kwa umakini kwa muda akionekana kama aliyekuwa ananifananisha kisha aliachia tabasamu laini la aibu huku akiyakwepesha macho yake na kuangalia kando.

Alipotabasamu ndipo mashavu yake yalipoonesha wazi vishimo vidogo, pembe za midomo yake zikafinya na macho yake yalifanya kuelea uteni. Hali ile ilizidisha hamu yangu ya kutaka kumfahamu zaidi mrembo yule wa shani.

Itaendelea...
Narudi
 
Mmm msaidieni akiwa huko huko kizunguzi kilosa msimiweke karibu huyu simuamini kabisa uyu zai kijiwenongwa
 
Hii riwaya ishakua changamoto mpk unasahau uliishia wapi[emoji119]
Simulizi za Bishop zinataka moyo maana ni nzuri saaaana af hauzi af anatuma anapoamua kuna mda nataka kususa kbs kuisoma af nashindwa...
 
Hii riwaya ishakua changamoto mpk unasahau uliishia wapi[emoji119]
Simulizi za Bishop zinataka moyo maana ni nzuri saaaana af hauzi af anatuma anapoamua kuna mda nataka kususa kbs kuisoma af nashindwa...
Haha! Tuvumiliane wakuu, sometimes natingwa sana na majukumu au nakuwa safarini, tena wakati mwingine kwenye maeneo ambayo hakuna mtandao. Ila tupo pamoja...
 
Mgeni mwema.jpg

205

Simanzi…



Saa 1:30 asubuhi…

BASI la Shabiby lilipiga honi kali za kuashiria kuwa lilikuwa mbioni kuondoka pale kwenye kituo kikuu cha mabasi cha Nanenane, Jijini Dodoma. Honi hizo ziliwafanya wapiga debe wa kituo hicho cha mabasi jijini humo kushangilia na wengine kupiga mbinja kwa fujo.

Zainabu aliyekuwa amekaa kiti cha dirishani alitutazama mimi na Rehema kwa uchungu mkubwa, macho yake yalionesha uchungu mkubwa na machozi yalikuwa yanamlengalenga machoni. Hilo halikunistaajabisha kabisa. Sikustaajabu kwa kuwa niliamini kuwa alikuwa na huzuni ya kumwachia mwanamke mwenzake mwanamume aliyempenda sana.

Kilichonistaajabisha ni baada ya kumwona Rehema naye akilengwalengwa na machozi. Niliwatazama wote wawili, Rehema na Zainabu, nikaona kitu ambacho ilikuwa vigumu sana kwa mtu asiye mdadisi kama mimi kukiona na kukielewa.

Kwa haraka haraka mtu angeweza kusema kuwa kulikuwa na ladha ya upendo wa dhati iliyokuwa inawakilishwa na machozi ya wanawake hao wawili, lakini mimi sikuona kitu kama hicho, niliona kitu cha ziada. Kitu ambacho kila nilipojaribu kukitafakari sikuweza kupata jibu la haraka!

Hatimaye Zainabu alikuwa anarejea kwenye makazi yake mjini Kilosa baada ya kuwa amekaa nasi pale Jijini Dodoma kwa kipindi cha juma moja. Katika muda wote wa juma moja aliokuwa hapo Dodoma alionekana kuwa na furaha kubwa na hakuonesha tofauti yoyote kati yake na Rehema.

Almasi kwa upande wake alikaa pale Dodoma kwa siku moja tu na siku iliyofuata aliondoka kurudi Kilosa. Hata hivyo kwa siku hiyo moja nilikuwa nimepata wasaa mzuri sana wa kuongea naye na kupanga naye mambo mengi mazuri kwa ajili ya future. Kwa ujumla Almasi alikuwa mtu mwenye akili kubwa sana, he was well educated, ingawa hata mara moja hakupenda kugusia kuhusu elimu yake.

Katika siku hiyo moja niligundua kuwa ufahamu wake kuhusu mambo mbalimbali ulikuwa mkubwa mno na alikuwa na uwezo wa kuchambua mambo kiasi cha kunifanya nijione bado natakiwa kurudi shule.

Sasa Zainabu naye alikuwa safarini kurudi Kilosa, na katika safari hiyo, Zainabu alikuwa ameambatana na Grace ambaye alipanga kwenda kukaa Kilosa na Zainabu kwa siku kadhaa. Zainabu sasa alianza kuchukuliwa kama mmoja wa wanafamilia, na kiukweli, familia ilionesha kumkubali. Alikuwa ameambiwa kuwa anaruhusiwa kufika hapo nyumbani kwa Mchungaji Ngelela au kwa ndugu yangu yeyote, wakati wowote.

“Zainabu… ukifika tu naomba unifikishie ujumbe wangu kwa Almasi. Mwambie azingatie sana kile tulichoongea siku alipokuwa anaondoka, na mimi pia nitampigia simu nikifika Kahama,” nilimwambia Zainabu wakati lile basi la Shabiby likianza kuondoka taratibu.

Zainabu aliitikia kwa kichwa huku akifuta machozi yaliyoanza kumtoka na kutiririka mashavuni kwake na kisha tulipungiana mikono ya kwaheri. Mimi na Rehema tulilisindikiza kwa macho lile basi wakati likiondoka hadi pale lilipoingia barabarani na kutoweka kabisa kwenye upeo wa macho yetu.

Nikashusha pumzi ndefu kama niliyemaliza mbio ndefu za marathoni kisha mimi na Rehema tukaangaliana na kukumbatiana. Muda wote Rehema alikuwa mkimya sana na bado aliendelea kulengwalengwa na machozi.

Tulipoachiana tuliongozana hadi kwenye gari lililotuleta, tukaingia na kuondoka kurudi nyumbani kwa Mchungaji Ngelela kwa ajili ya maandalizi ya safari yetu ya kuelekea Kahama siku iliyofuata… safari ya kwenda kuyaanza maisha mapya kama wapenzi tuliohalalishwa yaani wanandoa na pia wazazi wa mtoto Jason Sizya Junior.

Hata hivyo, bado kichwani kwangu kulikuwa swali lililoendelea kunitesa, swali kuwa; hali ile ya upendo na kutokuwepo kwa tofauti yoyote iliyooneshwa na Zainabu kwa Rehema (japo sikuwa na uhakika sana na jambo hilo) ingeendelea kuwepo au ingekuwa ya muda tu? Hadi hapo nilijikuta nikibaki njia panda na nisijue nini cha kufanya.

Huu ni mwisho wa Msimu wa Nne kwenye mfululizo wa Harakati za Jason Sizya. Usikose Msimu wa Tano katika mkasa uitwao “Ufukweni Mombasa”.
 
Dondoo:

Kuanzia msimu wa tano wa Harakati za Jason Sizya stori inabadili kabisa mkondo, utakayoyashuhudia humo yatazidi kukuacha mdomo wazi. Endelea kufuatilia...
 
Dondoo:

Kuanzia msimu wa tano wa Harakati za Jason Sizya stori inabadili kabisa mkondo, utakayoyashuhudia humo yatazidi kukuacha mdomo wazi. Endelea kufuatilia...
kuna mda natamani uuze tusio na subra tujilipue asa hivi ndo nn jmn kimoja tu apo inaitwa tuonane wiki ijayoooooooooooooo wewe ni mtunzi kwelikweli askofu
 
kuna mda natamani uuze tusio na subra tujilipue asa hivi ndo nn jmn kimoja tu apo inaitwa tuonane wiki ijayoooooooooooooo wewe ni mtunzi kwelikweli askofu
Usijali. Shida ni kwamba nina stori nyingi mno nilizoziandika kitambo, hivyo kabla sijaiachia stori yoyote huwa naipitia tena na kurekebisha baadhi ya vitu viendane na hali ya sasa jambo linalonifanya wakati mwingine kuchelewa hasa ukizingatia kuna majukumu mengine yananibana. Hata hivyo ndo maana huwa nikiachia naacha mzigo wa kutosha (isipokuwa leo tu[emoji23][emoji23])...
 
Usijali. Shida ni kwamba nina stori nyingi mno nilizoziandika kitambo, hivyo kabla sijaiachia stori yoyote huwa naipitia tena na kurekebisha baadhi ya vitu viendane na hali ya sasa jambo linalonifanya wakati mwingine kuchelewa hasa ukizingatia kuna majukumu mengine yananibana. Hata hivyo ndo maana huwa nikiachia naacha mzigo wa kutosha (isipokuwa leo tu[emoji23][emoji23])...
Unaonaje ukiuza mkuu wangu?
 
Back
Top Bottom