Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
- Thread starter
- #501
238
Nilimsindikiza kwa macho hadi alipotoka kabisa na kuelekea kwenye gari lake. Kisha nikasikia mlio wa milango ya gari kufunguka baada ya kubonyeza rimoti, halafu gari likawashwa na kuunguruma taratibu na baadaye mlango wa gari ukafungwa huku geti likifunguliwa na hatimaye gari likatoka na kutokomea barabarani.
Sikuchukua muda mrefu mawazo yangu yakarudi tena kwenye kazi iliyokuwa mbele yangu, kazi ya kutafuta taarifa za Zuena wa Mombasa, kuanzia kwenye mawasiliano yake ya simu hadi kwenye account zake za Tiktok, Facebook na Instagram. Nikazama kwenye kufuatilia kila taarifa aliyoichapisha kwa namna ya kiuchunguzi zaidi. Bado sikuweza kupata jambo lolote lililoonekana kunitia wasiwasi.
Nikiwa bado natafakari hatua zaidi za kuchukua simu yangu ya mkononi ikaanza kuita. Niliitazama nikaona namba ngeni, nikaipokea na kuisikiliza, nikagundua mpigaji alikuwa amekosea namba, nikaikata kwa kuwa haikuwa na kitu cha muhimu.
Sasa nikaamua kujipa mapumziko ili niweze kuendelea na mipango yangu ya safari ya kwenda Mombasa, mapumziko hayo yangekuwa ya muda na ningeuendeleza upelelezi wangu juu ya Rahma baada ya kutoka Mombasa nilikopanga kukaa kwa wiki moja na ushee. Hata hivyo mipango yangu hii haikuwa tuli (static), la! Nilikubaliana na nafsi yangu kuwa ingekuwa inabadilika kutokana na matukio yanavyokwenda, kutokana na mambo yanavyoenenda.
Huko Mombasa nilipanga kufikia katika hoteli ya Serena Beach Resort & Spa, na tayari nilikwisha wasiliana nao na kufanya malipo ya awali mtandaoni na kupewa chumba nambari 204. Nilivutiwa na hoteli ya Serena Beach Resort & Spa kutokana na maelezo niliyoyapata kupitia intaneti.
Ilikuwa hotel kubwa na tulivu zaidi yenye hadhi ya Nyota 4, ikiwa nje kabisa ya Jiji la Mombasa, katika ufukwe wa Bahari ya Hindi. Hoteli hii ilikuwa jirani na Mombasa Marine National Park, na pia ilikuwa rahisi kufika Shimba Hills National Reserve kutokea pale. Hayo ni maeneo ambayo nilipanga kuyatembelea nikiwa Jijini Mombasa.
* * *
Saa 5:15 usiku…
Ulikuwa usiku usio na furaha kwangu kwa mara ya kwanza tangu nimuoe Rehema. Ndiyo, nilikuwa nimelala na Rehema, tukiruhusu miili yetu kustareheshana kama kawaida, mikono ikijifariji kwa kugusa hapa na pale; miguu ikiburudika kwa mguso huo. Hata hivyo, faraja hiyo haikufikia kiwango cha kuzifuta chembechembe zisizoelezeka ambazo zilienea katika fikra zangu.
Sikujua kwa nini nilikuwa na fikra mbaya juu ya Rahma wa Singida! Sikuona kwa nini niendelee kuumizwa kifikra na mtu ambaye hakuwa na rekodi yoyote yenye kutia shaka. Rekodi ya uhalifu. Hata hivyo fikra mbaya juu yake zilishindwa kufutika akilini kwangu kila nilipokumbuka kuwa gari aina ya Range Rover walilokuwa wakitumia lilikuwa na namba za bandia, jambo lililomaanisha kuwa hawakuwa watu wa kuwaamini. Kuhusu Zuena wa Mombasa, ndiyo… alikuwa amenitia mashaka, pengine hata kuliko Rahma wa Singida, lakini hakunisumbua sana akili yangu.
Tukiwa kitandani Rehema alijua fika kuwa kulikuwa na jambo gumu lililonitatiza sana katika kazi yangu mpya na hakuthubutu kuniuliza kuhusu kile kilichonitatiza, alifahamu fika kuhusu utaratibu wa usiri (Compartmentation) kwenye kazi ya ushushushu hakujisumbua kuniuliza kwa kujua nisingeweza kumwambia kwa kuwa kwenye taalumu ya ujasusi kila mtu kwako ni adui na hutakiwi kumwamini yeyote, hata marehemu.
Alionekana kuyasoma mawazo yangu, akanihurumia sana na alijitahidi kufanya kila aliloweza kulifanya kwa dhamira ya kujaribu kunisahaulisha walau kwa muda. Alipoona vitendo vyake havitimizi wajibu alijaribu kutumia maneno, kwa sauti yake laini, iliyopenya katika mwanga hafifu mle chumbani baada ya kuzimwa taa na kisha kuwashwa taa yenye mwanga hafifu wa rangi ya bluu, Rehema aliniambia. “Baby, haya mambo yasikuvuruge, nadhani hakuna asiyejua kama wewe ni shujaa.”
Nilimtazama usoni katika mwanga ule hafifu, nikatabasamu huku mawazo yangu yakihama kutoka kuifikiria kazi yangu ya kumtafuta Rahma wa Singida na kuanza kumfikiria Rehema, ofisa kificho wa Idara ya Usalama wa Taifa. “Kama baba na mama ni mashushushu wasioaminiana sijui mtoto atakuwaje!’ niliwaza na hapo nikajikuta nikicheka.
“Unacheka nini? Ni kweli hakuna asiyejua kama wewe ni shujaa,” Rehema alisema huku akiupitisha mkono wake kwenye nywele zangu na kuanza kuzishikashika kwa namna ya kunitia mdadi.
“Shujaa!” niliuliza kwa sauti iliyokuwa na dalili ya uchovu. “Wanaonifikiria hivyo watakuwa wanakosea sana.”
“Japo sijui ugumu wa task uliyo nayo lakini inanishangaza kuona unavunjika moyo mapema kiasi hiki. Unautia dosari ushujaa wako,” Rehema aliniambia katika hali ya kunisimanga kisha akanikumbatia. Sikusema neno. Kisha kama aliyekumbuka jambo akaniuliza, “Kwa hiyo safari yako ya Mombasa bado ipo?”
“Ipo kama kawaida. Kesho lazima niondoke na nikirudi ndiyo nipite Kilosa nikamwone mtoto halafu niende Tabora kwa wazee,” nilisema kwa sauti tulivu. Kwa taarifa nilizokuwa nazo ni kwamba Zainabu alikuwa na mtoto wa kiume ambaye muda huo alikuwa na miezi minne.
“Jason!” Rehema alisema kwa sauti ya mshangao. Uso wake ulikuwa na dalili zote za mashaka. “Kwani ni lazima uende Mombasa kesho? Ingekuwa ni safari ya kikazi sawa lakini…”
“Lakini nini?” nilimuuliza Rehema bada ya kuona amesita kuongea.
“Nadhani kesho usifanye safari hiyo. Nenda kwanza ukamwone mtoto na kisha wazee upate na baraka zao halafu ndiyo uende safari yako,” Rehema alisisitiza.
“Kwa nini hutaki kesho niondoke?” nilimuuliza Rehema huku nikimtazama usoni kwa umakini.
“Hata sijui! Lakini… nina hisia mbaya,” Rehema alisema kwa kusita sita na kunifanya niangue kicheko.
“Huna sababu ya kuogopa chochote. Hakuna mtu atakayeniteka tena…” nilisema huku nikiwa bado nacheka. Kisha nikaongeza, “Sina njia nyingine zaidi ya kuondoka kesho. Nikiendelea kubaki Tanzania kuna mambo yatazidi kunitatiza akili yangu wakati nahitaji kuipumzisha.”
Rehema hakutia tena neno. Huenda aliamua kukubali yaishe kwa kubaki kimya baada ya kuona nilikuwa nimekusudia kuendelea na safari yangu siku iliyokuwa inafuata. Tayari nilikwisha fungasha vitu vyangu kwenye begi dogo la safari na nilishakata tiketi ya basi la kampuni ya Tahmeed.
Baada ya kitambo kirefu nikamwona Rehema akishusha pumzi na kuniambia kwa sauti ya unyonge, “Sawa, nakutakia safari njema…” kisha akageuka upande mwingine akinipa mgongo.
“Nashukuru, na nyinyi mbaki salama,” nami nilimwambia huku nikipeleka mkono wangu kwenye unywele zake na kuanza kuzipapasa kwa namna ya kuamsha ashki.
“Ila sielewi kwa nini umechagua kusafiri kwa basi hadi Mombasa badala ya usafiri wa ndege!” Rehema alisema kwa sauti tulivu, katika sauti yake kulikuwa na hali ya huruma na unyenyekevu huku masikitiko yakiwa yamejificha nafsini mwake.
“Usijali, mke wangu… nimeamua kutumia basi kama mojawapo ya kufanya utalii usio rasmi kwa sababu nitafanikiwa kuyaona vizuri mandhari ya kupendeza ya nchi yetu. Ila wakati wa kurudi nitapanda ndege,” nilisema huku nikimkumbatia kwa kupitisha mikono yangu kwenye kifua chake. Kisha nikafumba macho yangu nikijaribu kuutafuta usingizi.
* * *
Inaendelea...