Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
- Thread starter
- #641
272
Kwa dakika kadhaa niliendelea kutulia pale dirishani huku nikiendelea kupiga picha za video kwa kila kilichokuwa kikiendelea pale chini ya lile jengo refu la Alpha Mall, na wakati huo huo nikichunguza kwa umakini kila kitu kwenye jengo lile kana kwamba niliambiwa kuna kitu kingetokea hapo!
Huku nikiendelea kupiga picha za video mara nikayaona magari mawili yakifika pale na kisha yakaegeshwa kando ya lile gari aina ya Toyota Prado TX la rangi ya fedha. Magari hayo yalikuwa ni gari dogo aina ya Toyota Vanguard la rangi nyeusi lililokuwa na namba za binafsi kutokana na utambulisho wa namba zake na Toyota Landcruiser GX V8 jeusi ambalo utambulisho wa namba zake ulionesha kuwa lilikuwa gari la Waziri wa Mambo ya Ndani.
Nikavutiwa zaidi kupiga picha za magari yale, na wakati nikiendelea kupiga picha nikashuhudia kwenye lile gari dogo aina ya Toyota Vanguard jeusi akishuka mwanamume mmoja ambaye ndiye alikuwa akiliendesha gari lile, alikuwa amevaa suti maridadi ya rangi ya kijivu na viatu vyeusi vya Ngozi. Kwa haraka tu niliweza kumtambua, alikuwa Octavian Lister, Ofisa Usalama wa Taifa ambaye alikuwa ni Katibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Nilikuwa nikimfahamu Octavian Lister japokuwa hatukuwa na ukaribu kivile, alikuwa mrefu na umri wake ulikuwa miaka 36, si mnene wala mwembamba lakini aliyeonekana kuwa mkakamavu na mwenye mikono imara iliyojengeka kwa misuli.
Katika lile gari aina ya Toyota Landcruiser GX V8 jeusi la Waziri wa Mambo ya Ndani, nilimshuhudia dereva wa Waziri, mtu mzima, mrefu na maji ya kunde aliyevaa suruali nyeusi ya kitambaa, shati la samawati la mikono mirefu, tai ya rangi ya bendera ya taifa na miwani myeusi ya jua, akishuka haraka kisha akaelekea kwenye mlango wa nyuma na kuufungua, na hapo akashuka mwanamama mmoja nadhifu sana na mrefu kiasi.
Mwanamama huyo alikuwa amevaa vazi zuri la kitambaa cha bazee lililoshonwa na kudariziwa vizuri kwa nyuzi za rangi ya dhahabu na kichwani alikuwa amevaa kilemba kikubwa kama wavaavyo wamama wa Kinaijeria. Nilimtambua vyema mama huyo kuwa ndiye Waziri wa Mambo ya Ndani, Bi Ummi Mrutu.
Mwanamama huyo alikuwa mnene wa wastani na mweupe kwa rangi ya ngozi yake. Hakuwa mwanamke wa kumtazama mara moja tu ukayaondoa macho yako kwake, kwani umbo lake lilisheheni vyema na kunesanesa huku likifanya kila jicho la mwanamume lililomwona kumtazama mara mbilimbili. Alikuwa na umri wa miaka 50 na watu wengi walijiuliza kuwa kama aliweza kuonekana bado mrembo katika umri ule, je, alikuwaje enzi za usichana wake?
Mbali na urembo, kikubwa zaidi kilichokamilisha haiba na mvuto pekee wa mama huyo ilikuwa ni machachari yake. Aliheshimika mno kwa uwezo wake mkubwa wa kusimamia operesheni dhidi ya ufisadi, uhujumu uchumi na nyingine kama hizo zikiwemo za kupambana na majambazi na wauza dawa za kulevya, na aliyafanya hayo akishirikiana na maofisa wa polisi makini wapambanaji kama Derick Mambo, Kamishna wa Taasisi ya kupambana na dawa za kulevya.
Mwanamama Ummi Mrutu alikuwa amefanikiwa mno endapo ungetaka kumlinganisha na mawaziri wa wizara hiyo waliokuwa wamemtangulia kwa kuwa alipenda kuwahamasisha maofisa waliokuwa chini yake kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi, na alitoa ushauri bora kwa viongozi wa juu. Sifa hizo pamoja na nyingine nyingi ndizo zilizofanya akabidhiwe dhamana ya kusimamia wizara hiyo nyeti inayohusika na usalama wa ndani ya nchi, na ngumu kuliko wizara nyingi nchini.
Nikiwa bado napiga picha za video pale dirisha nikamwona Waziri Ummi Mrutu akiongozana na Katibu wake Octavian Lister, wakaingia ndani ya lile jengo la Alpha Mall. Mwanzoni nilidhani labda walikuwa wamefika pale kwa ajili ya manunuzi kwani ndani ya lile jengo kulikuwa na maduka mbalimbali kama duka la nguo maarufu la Kidoti boutique, duka kubwa la samani mbalimbali za ofisini na nyumbani na maduka ya bidhaa nyingine muhimu.
Kwa kumwona Waziri Ummi Mrutu pale shauku yangu ikazidi na kujikuta nikiachana na kupiga picha zilizohusu adha ya usafiri wa daladala katika kile kituo cha daladala cha Makumbusho na kujikuta nikivutiwa kupiga picha katika jengo lile la Alpha Mall, na sasa kamera yangu ilianza kupanda juu taratibu katika ghorofa za lile jengo na kutulia kwenye ghorofa ya kwanza ilipokuwepo supermarket kabla ya kuhamia kwenye vyumba vingine vya ofisi.
Madirisha mengi katika ghorofa ile ya kwanza yalikuwa yamefunikwa kwa mapazia mazito na hivyo vioo vyake viliakisi vizuri taswira ya vitu vya nje na kutomruhusu mtu yeyote kuona mle ndani kwa urahisi. Hata hivyo, katika ghorofa ya pili na ya tatu madirisha yake yalikuwa hayajafunikwa kwa mapazia na hivyo vioo vyake havikuwa vinaakisi kama ilivyokuwa kwa zile ghorofa zingine, na hivyo niliweza kuona kilichokuwa kikiendelea ndani ya vile vyumba.
Niliangalia vizuri katika ile ghorofa ya pili iliyokuwa na mgahawa wa kisasa lakini sikuona chochote cha maana kwani mbali na mgahawa huo kulikuwa na duka kubwa la samani za ofisini na nyumbani. Kamera yangu ikapanda juu zaidi hadi katika ghorofa ya tatu kulikokuwa na vyumba vya ofisi mbalimbali. Na hapo niliweza kuona vifaa vya ofisini kama meza na viti vyake, makabati ya kutunzia nyaraka, rafu za chuma, tarakilishi, mashine za kurudufu, printa pamoja na vitu vingine vidogo vidogo vya kiofisi.
Ndani ya vile vyumba vya ofisi niliweza kuwaona baadhi ya wafanyakazi wakiwa wanaendelea na shughuli zao. Wengine wakiwa wameinamia tarakilishi zao mezani na wengine wakipitia taarifa kwenye majalada ya ofisini. Kila mmoja alikuwa amezama kwenye hamsini zake na hakuna aliyekuwa akitazama pale dirishani ambapo nilikuwa nimesimama nikipiga picha, jambo ambalo lilinipa uhuru zaidi wa kuwapiga picha vizuri.
Wakati nikiendelea kupiga picha huku kamera yangu ikihama taratibu kutoka kwenye dirisha moja na kuhamia kwenye dirisha lingine katika ghorofa ile ya tatu hatimaye macho yangu yakaweka kituo kwenye chumba kimoja cha ofisi kilichokuwa kwenye kona ya kushoto ya ghorofa ile ya tatu ya lile jengo la Alpha Mall baada ya kuwaona watu watatu waliokuwa wameketi kwenye viti wakiwa wamezama kwenye mazungumzo ya kina.
Nilijikuta nikivutiwa mno na kile kilichokuwa kikiendelea humo ndani na kwa msaada wa lenzi kubwa ya kamera yangu yenye kuweza kuchukua vitu vilivyoko mbali, niliona vizuri ndani ya ile ofisi. Niliwatambua vyema wale watu watatu kwa kuwa pazia la dirisha la chumba kile cha ofisi lilikuwa limefunguliwa lote na kuachwa wazi. Watu hao walikuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani Bi Ummi Mrutu, Katibu wa Waziri Octavian Lister na mtu wa tatu alikuwa mpelelezi wa kujitegemea Daniel Kayera.
Huyu Daniel Kayera alikuwa amefungua kampuni binafsi ndani ya jengo lile la Alpha Mall, iliyohusika na upelelezi na iliitwa DanKay Private Detective Agent ili kutafuta ufumbuzi wa kesi tata zilizotingisha nchi zikionekana kuwayumbisha wanasheria na wapelelezi wa serikali. Kwa mfano kesi zilizohusu mauaji ya kutatanisha, ufisadi, uhujumu uchumi na dawa za kulevya.
Endelea...