288
Maswali ya Tunu yaliufanya ubongo wangu uchemke kutafuta majibu. Na hapo akili yangu ikafunguka zaidi: nikajiuliza kulikuwa na nini kwenye jengo la Alpha Mall hadi magaidi walenge kulipua hapo badala ya sehemu nyingine? Je, nini lilikuwa lengo lao yaani ni ujumbe gani waliotaka kuutoa kwa serikali kwa kulipua jengo hilo?
Mara nikajiwa na jambo akilini mwangu ambalo mwanzoni sikuwa nimelifikiria kabisa! Kabla sijamwambia chochote Tunu kuhusiana na jambo hilo nilimwomba akitazame upya kile kipande cha video kilichoonesha namna yule mtu aliyefika pale kwenye jengo la Alpha Mall na pikipiki ya magurudumu matatu alivyokuwa akilazimisha kuipachika pikipiki yake katikati ya magari ya Waziri wa Mambo ya Ndani na lile la mpelelezi wa kujitegemea Daniel Kayera.
Magari hayo yalikuwa kwenye maegesho usawa wa dirisha la ofisi ya DanKay Private Detective Agent. Hii ilimaanisha kuwa kama si wote wawili basi mmoja kati ya Waziri Ummi Mrutu au Daniel Kayera ndiye alikuwa mlengwa wa shambulio hilo.
“Sasa tujiulize, ni nani alikuwa
targeted kati ya watu hawa wawili maana kiukweli wote wanao maadui wenye nguvu kutokana na kazi zao na uadilifu wao,” nilisema na hapo Tunu akaafikiana na mimi kuhusu jambo hilo.
Nilisisitiza kuwa maadui wa Waziri Ummi na hata Daniel Kayera kwa vyovyote wasingekuwa watu wa nje bali wa ndani, hivyo tulipaswa kuliangalia jambo hilo kwa uzito mkubwa sana. Sasa kazi ilikuwa ni kutafuta kujua akina nani wangeweza kuwa maadui wa Waziri Ummi Mrutu, na akina nani wangeweza kuwa maadui wa Daniel Kayera. Na kwa nini? Hapo ndipo tulipopaswa kuanzia kazi yetu.
Tulipoanza kumjadili Daniel Kayera tukijaribu kubashiri kama ndiye mlengwa wa bomu hilo, je, nani wangeweza kuwa maadui wake. Na hapo tukabaini kuwa maadui wake ni wale ambao alikuwa akipambana nao kisheria wakati akitafuta haki za wateja wake, kama ilivyokuwa kwenye ile kesi iliyohusu kifo cha Ofisa wa Mashtaka wa Mkoa (RPO) wa Morogoro, Dk Devota Komba, aliyedaiwa kujinyonga kwa kamba ya manila chumbani kwake katika eneo la Forest Hill mjini Morogoro.
Japokuwa kesi ile iliwaibua watu wazito na wafanyabiashara wakubwa wa mjini Morogoro lakini, kwa haraka haraka tu, kila mmoja wetu alibaini kuwa Daniel Kayera asingeweza kuwa
‘target’ ya ugaidi huo kwa kuwa aina ya adui zake wasingeweza kufanya ugaidi wa aina ile, na kama wangehitaji kumuua wasingekuwa na sababu ya kutumia nguvu kubwa namna ile. Hivyo tuliamua kumtoa Daniel Kayera kuwa target ya ugaidi huo. Ila kwa upande wa Waziri Ummi Mrutu, sote tulikubaliana kuwa alikuwa na maadui wakubwa na wenye nguvu.
Lakini bado nilikuwa na shaka, nikamwuliza Tunu, kama shida ya magaidi hao ilikuwa kummaliza Waziri Ummi Mrutu tu kwa nini sasa watumie njia ile ya bomu ambalo liliangamiza watu wengi na kuleta taharuki nchini? Swali hili likazua mjadala mwingine tena… badala ya kupata ufumbuzi sasa tulijikuta tukizidi kutumbukia ndani ya shimo refu lenye kiza kizito…
Ni hapo sasa Tunu aliponiambia kuwa tulihitaji muda zaidi wa kuyatafakari mambo yote hayo ila kwanza tupate nafasi ya kila mmoja wetu kutafakari kwa kina na kuchakata taarifa alizozifahamu kuhusu Waziri Ummi Mrutu… vinginevyo tungeendelea kujiuliza maswali ambayo yangezidi kutuchanganya na tusingepata mwafaka.
“Halafu kwa kukukumbusha tu, kwa nafasi yake kama Waziri wa Mambo ya Ndani aliyesifika sana kwa kusimamia operesheni dhidi ya ufisadi, uhujumu uchumi, wahamiaji haramu, majambazi na wauza dawa za kulevya… Waziri Ummi asingekosa maadui. Amekuwa akipambana na watu wenye nguvu zote: kiuchumi, kiulinzi na kiukatili!” Tunu alisema.
“Dah! ishu nimekuwai kubwa mno kuliko tunavyodhani…” nilisema huku nikihisi akili yangu ikishindwa kufanya kazi sawa sawa. “Kwa vyovyote inagusa mtandao mpana mno ambao upo ndani na nje… namaanisha ndani ya nchi na nje ya nchi; na pia ndani ya serikali na nje ya serikali. Tena ni mtandao wenye nguvu zote kama unavyosema mkuu… si mtandao tu ni genge hatari zaidi ya Mafia.”
Kisha nilimweleza kuhusu mazungumzo yangu na Kamishina Koba hasa aliponiambia kuwa shaka yake ni kwamba kwa aina ya shambulio lilivyotokea inaonekana kabisa kuna mkono wa watu kutoka katika majeshi yetu.
Tunu alishusha pumzi na kunikodolea macho. Nikaongeza, “Kumbuka pia kuwa ni wiki tatu tu zimepita tangu Waziri Ummi atoke kumpoteza kijana wake wa pekee kwa kifo cha kutatanisha.”
“Dah! Sasa ndiyo watumie bomu kumuua Waziri?” Tunu aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Huenda nia yao ilikuwa kujaribu kutupoteza maboya, badala ya kufikiria haya tunayoyajadili sasa tuelekeze macho yetu kwenye vikundi vya kigaidi kama Alshabab au Islamic State,” nilisema na hapo nikamwona Tunu akibetua kichwa chake kuafiki.
“Na kwa kiasi fulani wamefanikiwa maana makao makuu ya Idara Kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, na Jeshi la Wananchi wa Tanzania wameamua kuimarisha ulinzi na usalama katika majengo ya serikali, hospitali, masoko na sehemu maarufu za biashara, mahoteli ya kitalii, stesheni na vituo vya mabasi, shule maarufu hasa za mjini kati, kumbi za starehe, mitaa yenye mikusanyiko ya watu wengi, na madaraja muhimu…” Tunu alinidokeza. Kisha akaongeza.
“Na pia wameazimia kuanzisha operesheni maalumu ya kuwatambua wageni wote walioingia nchini ki halali na ki ujanja ujanja ikiwa sehemu ya uchunguzi wa kuwapata magaidi hao. Tena kazi hii inafanyika kwa kushirikiana na maofisa Uhamiji, Polisi, na kitengo maalumu cha Idara kinachoshughulika na udhibiti wa wageni katika mahoteli.”
Hata hivyo, tulikubaliana kuwa suala la wahamiaji haramu waliokuwa wamejazana nchini lilikuwa tishio kwa usalama wa nchi yetu kwani wangeweza kutumiwa. Na kama si wao basi wangekuwa ni Watanzania wenyewe waliofundishwa na kupewa msaada na wageni walioingia nchini kutoka ughaibuni.
Ni kweli wakati huo kulikuwa na idadi kubwa ya wahamiaji haramu kutoka Rwanda, Burundi, Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Ethiopia. Ongezeko la wageni hawa lilichangiwa kwa kiasi kikubwa na hali ya uhasama nchini Rwanda, na mapigano yasiyokwisha katika nchi za Kongo, Burundi, na Somalia. Wengi wa wahamiaji hawa waliingia nchini kwa njia za panya.
Si hivyo tu pia tulipaswa kuangalia kuhusu ongezeko kubwa la wafanyabiashara na wakazi haramu kutoka India, Pakistani, na nchi nyingine za Asia. Wahamiaji hawa waliingia nchini kwa viza halali kama watalii, au wageni wanaokuja kuwatembelea ndugu zao kwa muda mfupi. Hata hivyo baada ya viza zao kuisha muda wake hawakuondoka nchini bali walijichanganya na watu wa kwao kufanya biashara au kazi za kuajiriwa bila ya kufuata taratibu husika.
Kila tulichokijadili nilikumbuka kukiandika kwenye notebook yangu kwa ajili ya kumbukumbu pindi nikihitaji rejea ya mazungumzo yetu (
reference). Sasa mjadala ulikuwa umechukua sura mpya kabisa. Mambo yalikuwa yanachanganya mno. Hatimaye tulikubaliana kuahirisha mjadala na kupanga muda mwingine mwafaka wa kujadiliana huku tukiyaangalia mambo hayo kwa kina zaidi. Pia tulikumbushana kwenda msibani baadaye jioni huenda huko tungepata mwanga zaidi.
“Ni matumaini yangu kuwa tutapata mwanga mzuri wa namna ya kulimaliza jambo hili mapema. Utanijulisha ukitaka kwenda huko na utanieleza kila utakachokuwa umekifikiria,” Tunu alihitimisha maelezo yake kisha akaitazama saa yake ya mkononi na aliporidhika na mwenendo wa majira yake alinitazama akaachia tabasamu.
Na hapo nikafahamu kuwa tukio lile lilikuwa limeashiria kuwa maongezi yetu mle ndani na Tunu yalikuwa yamefika tamati. Nilikuwa wa kwanza kusimama muda mfupi kabla Tunu hajafanya hivyo na hapo nikafunga mguu wangu na kupiga saluti ya heshima mbele ya mkuu wangu, akaitikia vyema na kunipa mkono wa kuagana.
“Kuwa mwangalifu sana, Jason, kwani yeyote aliyehusika na kitendo hiki haelekei kuwa ni mtu wa kawaida,” Tunu alinionya kwa sauti tulivu huku akinitazama machoni.
“Usijali, mkuu, nitakuwa mwangalifu na nitakufahamisha kila kitu pale itakapobidi,” nilimwambia huku nikiwa bado nimeushika mkono wake, tabasamu langu la kikazi lilikuwa limeumbika vizuri usoni mwangu.
“Nakutakia kazi njema yenye mafanikio,” Tunu aliongea kwa utulivu huku akinipigapiga begani kwa mkono wake na kisha akaachia tabasamu katika namna ya kunitia moyo. Nikatoka kwenda kuendelea na majukumu yangu.
* * *
Endelea kuzifuatilia harakati za Jason Sizya katika mkasa huu wa kusisimua...