Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

taharuki..jpg

281

Shaka…




Saa 3:15 usiku…

NILIKUWA nimeketi kwa utulivu mkubwa ofisini kwangu, kwenye kiti changu kikubwa cha kiofisi cha kuzunguka na chenye magurudumu madogo yaliyokiwezesha kusogea huku na kule, mbele ya tarakilishi yangu ya kisasa aina ya IMac Retina 5K ya inchi 27. Ofisi ilikuwa imesafishwa vizuri na vitu kurudishwa mahala pake, kama ilivyokuwa mwanzo, isipokuwa kile kioo kimoja cha dirishani kilichovunjika kutokana na mtikisiko wa bomu kilikuwa kumezibwa, kwa muda, na mbao laini ‘plywood’. Kazi hiyo ilikuwa imefanywa kwa usimamizi wa msaidizi wangu, Winnie.

Muda wote macho yangu ya kazi yalikuwa matulivu lakini kidole changu kimoja cha mkono wa kulia kilikuwa ‘busy’ kikibofya kwenye vifungo vyenye alama za mishale inayoelekeza pande zote; kulia, kushoto, juu na chini katika kicharazio (keyboard) cha tarakilishi yangu, huku mkono wangu wa kushoto ukiwa umeshikilia bilauri ndefu ya mvinyo mwekundu kutoka Dodoma, ‘Dodoma Wine’.

Macho yangu yalikuwa mekundu yanayorembua na yalikuwa machovu kama vile nilikuwa sijapata usingizi kwa juma zima. Nilikuwa mchovu mno kiakili na kimwili, niliyechoshwa na kazi za siku hiyo lakini nilikuwa na hamu ya kuendelea kufanya kazi, kwa kifupi nilikuwa nimechoka lakini nisiyetaka kupumzika hadi kieleweke!

Licha ya hewa safi ya ubaridi iliyokuwa ikisambazwa na kiyoyozi kilichokuwa mle ndani, nilikuwa nimevua shati langu na kubakiwa na singlendi nyeupe huku kifua changu kipana kilichojengeka kwa mazoezi kikionekana kwa wazi. Kijasho chepesi kilikuwa kinanitoka mwilini.

Japokuwa nilikuwa napitia kazi niliyoifanya siku hiyo kwenye tarakilishi yangu lakini muda mwingi masikio yangu yalisikiliza kwa umakini kila habari iliyokuwa ikirushwa katika runinga kubwa ya bapa iliyotundikwa ukutani ndani ya ofisi yangu. Kituo maarufu cha runinga cha Marekani cha CNN kilikuwa kinarusha matangazo kuhusiana na kifo cha Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Bi Ummi Mrutu, katika mlipuko wa bomu ulilotokea Jijini Dar es Salaam na kutekekeza kabisa jengo la Alpha Mall lenye ghorofa zaidi ya kumi.

Ilielezwa pia kuwa mlipuko huo ulisababisha vifo vingine vilivyofikia ishirini na tano kutokana na ripoti ya serikali hadi muda huo vikiwemo vya dereva na Katibu wa Waziri Mrutu, na majeruhi sabini na nane wengi wao ni wale waliokuwa jirani na eneo lile wakigombea kupanda kwenye daladala. Na kwamba Tanzania iliyokuwa maarufu kwa jina la ‘Kisiwa cha Amani’ sasa ilikuwa imeanza kuingia doa.

Matangazo yale ya CNN pia yalikumbusha kwamba hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa nchi ya Tanzania kushambuliwa na magaidi, na tukio la kigaidi la kwanza lilitokea mnamo Agosti 7, 1998 katika ubalozi wa Marekani ambapo watu 11 raia wa Tanzania walipoteza maisha yao, na wengine 85 walijeruhiwa.

Matangazo hayo pia yaligusia uwepo wa chembechembe za kigaidi zilizoanza kuchipuka nchini Tanzania, huku uchunguzi wa awali ukionesha kuwa magaidi waliohusika na shambulio katika jengo hilo la Alpha Mall, kama ilivyokuwa katika shambulizi la kwanza kwenye ubalozi wa Marekani, si wababaishaji bali ni watu wenye uzoefu wa hali ya juu katika kupanga na kutekeleza mashambulizi makubwa ya kigaidi.

Baadhi ya wataalamu wa masuala ya usalama waliohojiwa na kituo cha CNN walibainisha kuwa chembechembe hizo za kigaidi nchini Tanzania zilikuwa zinafanya kazi kwa ushirikiano au maelekezo ya kundi kubwa la kigaidi kama Islamic State, Alshabab n.k.

Mengi yaliyotangazwa na kituo cha CNN pamoja na vituo mbalimbali vya runinga zilikuwa ni habari nilizozifahamu. Nilitamani sana kusikia jambo ambalo sikuwa nalijua na si habari nilizozitarajia. Niliisubiri kwa hamu habari mpya, si kwa ajili ya kuisikia tu bali niliihitaji kwa ajili ya kuongeza jambo lingine zaidi kuhusiana na upelelezi wangu.

Nilikuwa nimetoka kuzungumza na mkuu wangu wa kazi, Bi Tunu Michael kwa njia ya simu na kumdokeza kwa kifupi kuwa nilikuwa na taarifa za awali ambazo zingenifanya kuwabaini waliofanya shambulio lile la kigaidi endapo taasisi ingenipa jukumu la kuifanya kazi hiyo. Nilimwambia kwa kuwa siku hiyo ilikuwa Jumamosi hivyo ningemweleza kwa kirefu siku ya Jumatatu kwenye kikao cha kupashana taarifa za kiitelejensia (Situation Report) kuhusu ya hali ya ulinzi na usalama nchini na kupanga mikakati ya kukamilisha malengo ya kazi zilizokuwa zikitukabili. Akaafikiana na mimi na kuniambia kwamba Taasisi ya SPACE ilikuwa imenipa baraka zote.

Tunu aliniambia kuwa katika majukumu mapya ambayo angetupatia tayari nihesabu kuwa hilo lilikuwa jukumu langu ila alinisisitiza umuhimu wa kukamilisha kazi zangu kwa wakati na kwa kuzingatia maadili na miiko ya idara katika kila hatua ya utendaji kazi.

Muda wote mle ofisini macho yangu yalikuwa katika kioo cha tarakilishi yangu ila masikio yangu yalikuwa makini katika matangazo ya kituo cha runinga cha CNN huku akili yangu ikiwa imechoshwa kusikia kitu ilichokijua kwenye matangazo yote yaliyokuwa yakiendelea.

Kwenye tarakilishi nilikuwa napitia kwa umakini picha za video nilizochukua, zenye urefu wa dakika 45, tangu yale matukio ya abiria wa daladala katika kituo cha daladala cha Makumbusho kukimbia huku na kule, kusukumana na kugombea mlango wa daladala, hadi ulipotokea mlipuko wa bomu ulioliacha jengo la Alpha Mall likiwa kama gofu. Ilikuwa ni kama nilikuwa natazama filamu ya kusisimua ambayo mwisho wake ulisikitisha sana.

Nikiwa naendelea na kazi yangu ya kuzipitia zile picha za video, kuna wakati nililazimika kurudisha nyuma matukio au kuyasimamisha kabisa na kisha niliikuza picha nikiwa makini sana huku macho yangu yakitafuta kitu fulani nilichodhani kinesaidia katika kunipa njia ya kupenyea kwenye upelelezi wangu. nikiwa katika uchunguzi wa zile picha mara nikaona kitu kilichonifanya niikuze zaidi ile picha, nilikuwa nikimwangalia yule mtu mrefu mwenye ndevu nyingi aliyefika katika jengo la Alpha mall akiwa na pikipiki ya magurudumu matatu.

Nilihisi kugundua kitu kwenye sura ya yule mtu, ila kwa muda huo sikujua ni kitu gani nilichokuwa nimekigundua! Hata hivyo niliandika kwenye ‘notebook’ yangu kuhusu hisia zangu za kugundua kitu ambacho sikuwa nimekijua kwenye video, nikanakiri dakika katika video ambayo kitu hicho kipo, na kisha nilibetua kichwa changu kukubaliana na hisia zangu halafu nikanyanyua bilauri yangu ya mvinyo na kunywa fundo kubwa la mvinyo.

Baada ya kuzipitia zile picha za video kwa takriban saa moja na nusu niliridhika na kazi yangu, nikaegemeza kichwa changu kwenye kiti na mawazo mengi yakaanza kupita kichwani kwangu. Niliamua kulifunga lile faili (folder) lililokuwa na zile picha za video kisha nikafungulia faili lingine lililokuwa na picha za mnato nilizozipiga wakati nikisaidia katika zoezi la uokoaji wa majeruhi wa bomu.

Nilikuwa nikizichunguza zile picha moja baada ya nyingine kwa umakini zaidi huku nikiwa nimejiegemeza kwenye kiti changu nikiendelea kuwaza ni namna gani ningefanikisha jambo hilo mara nikakutana na ile picha ya yule mwanamume mfupi ambaye alikuwa akitafuna bubblish, akiwa na macho ya kusinzia, mustachi mpana na uso wake ulikuwa serious.

Endelea...
 
taharuki..jpg

282

Kwa sekunde takriban tatu niliitazama sura ile ambayo niliamini kama si ofisa wa usalama basi ilikuwa ‘sura ya matukio’, nilijaribu kukumbuka ni wapi nilipopata kumwona. Nilikuwa na hakika sura hiyo haikuwa ngeni kwangu. Niliwahi kumwona mtu yule mahali fulani. Wapi? hilo ndilo lililonitatiza wakati huo.

Kisha nilichukua tena notebook yangu na kuandika jambo kuhusiana na yule mtu nikijipa muda wa kufuatilia taarifa zake kwenye mfumo wa utambuzi wa programu ya TracerMark. Kisha nilianza kuyatazama majina yote ya waathirika (victims) wa tukio la bomu niliyokuwa nimeyaandika kwenye kile kijitabu changu nikiyapitia kwa kuanza na wale niliofahamishwa kuwa walikuwa wamekufa, kisha waliokuwa majeruhi na mwisho nikamalizia na wale waliokuwa wamesalimika.

Niliyatazama kwa umakini yale majina ya waliokuwa mahututi na kupelekwa hospitali na majina ya madereva waliowachukua, aina ya magari na namba za magari waliyokuwa wakiyaendesha, na hospitali walizoelekezwa na Polisi kuwapeleka majeruhi hao. Kisha nikayapitia majina ya wale waliokuwa na hali nzuri kiafya kiasi cha kutohitaji matibabu. Nilizitazama anwani za makazi yao na mahali ambapo wangeweza kupatikana endapo wangehitajika.

Sasa nilikuwa na uhakika wa kuongeza jambo kwenye upelelezi wangu nikiwa tayari nimepata pa kuanzia lakini nikiwa bado sijajua nianzeje! Hata hivyo ilikuwa ni heri kwangu kwa kuwa kitendo cha kuheshimu hisia zangu kilikuwa kimenisaidia baada ya kuamua kupiga picha za video mara tu nilipohisi kuvutiwa na zile pilika pilika za abiria waliokuwa wakigombea daladala kabla ya tukio lile la bomu, na hivyo kuambulia mlango wa ziada. Hata hivyo, nilitakiwa kuwa makini sana isijekuwa mlango huo ni wa kuzimu.

Nilianza kutafakari kuhusu kazi iliyokuwepo mbele yangu. Wakati nikifikiria namna ya kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi zaidi pasipo kutanguliza mbele hisia huku nikiwa sitaki kuathiri kazi nyingine, mara nikayakumbuka maongezi yangu na Kamishina Koba.

Kupitia mazungumzo yetu nilikuwa nimeiona nia njema ya Kamishina Koba katika kulishughulikia suala lile la bomu lakini sikujua kwa nini nilisita sana kumweleza chochote kuhusu kile nilichokuwa nikikijua. Sikutaka kumweleza kwa sababu yeye hakuwa mkuu wangu wa kazi lakini pia sikujisikia kumwambia chochote.

Baada ya kutafakari kwa dakika mbili nilihisi kuwa sasa akili yangu haikuwa imetulia. Mawazo yalinipoka umakini. Nilimfikiria yule mwanamume mwenye ovaroli aliyetelekeza pikipiki yake ya magurudumu matatu iliyokuwa na bomu, halafu nikamfikiria Kamishina Koba na mwisho mawazo yakahamia kwa mwanamume mfupi mwenye mustachi mpana. Nilianza kuhisi akili yangu ikichoka zaidi na kushindwa kufanya kazi yake sawa sawa.

Mwishowe niliachana na kazi kwenye tarakilishi, nikasimama na kwenda dirishani nikawa natazama madhari ya nje nikidhani labda ningechangamsha akili yangu. Nilitulia pale dirishani huku nikitafakari, macho yangu yalizunguka kwa namna ya kustaajabioa hali ya utulivu na ukimya uliokuwepo eneo lile kisha nikalitazama anga lilivyojibana na kuwa jeusi. Namna eneo lile lilivyokuwa tulivu ungeweza udhanie kuwa hapo hapakuwa Dar es Salaam.

Nikiwa nayazungusha macho yangu mithili ya mtalii mbugani Serengeti, macho yangu yalihamia kutazama barabarani, niliyatazama kwa umakini magari machache yaliyokuwa yanapita barabarani kama niliyekuwa nayachunguza kwa umakini, mikono yangu nilikuwa nimeiegemeza pale dirishani.

Kisha macho yangu yalihama toka kwenye magari barabarani hadi pale chini ya jengo letu la Makumbusho Plaza. Kuna kitu nilikiona kikanivutia. Mara ya kwanza nilikiona lakini nilikipuuzia. Mara hii ya pili moyo wangu ulipiga kite kwa nguvu na hivyo nikaamua kukitilia maanani. Ilikuwa ni gari la kifahari aina ya Range Rover Velar la rangi nyeupe lenye vioo vyeusi visivyoonesha watu waliomo ndani, lilikuwa limeegeshwa chini ya jengo la Makumbusho Plaza jirani kabisa na pale nilipoegesha gari langu.

Taa za nyuma za gari hilo zilikuwa zinawaka ikionesha kuwa gari lilikuwa halijazimwa na lilikuwa linanguruma, niliweza kulitambua hilo kwa wepesi kwa kutazama bomba lake la kutolea moshi. Utambulisho wa namba zake ulinionesha kuwa zilikuwa namba za binafsi ingawa sikuwa na uhakika kama zilikuwa namba halisi au za bandia.

Nililitazama gari hilo kisha nikijiuliza maswali mepesi kichwani; lilikuwepo hapo kwa muda gani? Lilikuwa linafanya nini hapo? Mbona lilikuwa haliondoki? Lilikuwa linamsubiri nani usiku huo wakati eneo lile hakukuwa na biashara iliyokuwa inaendelea kutokana na tukio la bomu? Nilichukua kamera yangu ili nilipige picha lakini kabla sijafanikiwa kupiga picha nikaliona likiondoka. Nikaishia kulisindikiza kwa macho likiingia mtaa fulani na kuyoyoma kwenye kiza. Nikaamua kurudi kwenye kiti changu. Angalau akili yangu ilikuwa imechangamka kidogo.

Mara mlango wa ofisi yangu ukafunguliwa na Winnie akaingia akiwa amebeba kikombe cha kahawa, kama ilivyokuwa kawaida yake, alikuwa ameniandalia kahawa ya Kiitaliano (cappuccino) na kuniletea mle ofisini kwangu, akakiweka mezani halafu akasimama kando akinitazama kwa umakini.

“Kumbe bado upo? Mi nikajua umeshaondoka!” nilimuuliza Winnie kwa mshangao huku nikiinua mkono wangu na kutazama saa.

“Nilikuwa namalizia editing ya ile stori ya uhamishwaji wa Wamasai huko Ngorongoro,” Winnie alisema huku akiendelea kunitazama kwa umakini, kisha akasema kwa utani huku akiachia tabasamu pana, “Nilikuletea kahawa upunguze uchovu kumbe mwenzangu unajidunga na mvinyo!”

“Usijali, mrembo… wewe endelea kuniombea tu labda siku moja nikaacha kujidunga. Ujue ndiyo maana nakupenda maana unanijali sana,” nilisema huku nami nikiachia tabasamu kisha nikanyanyua bilauri yangu na kunywa fundo moja la mvinyo huku nikiufurahia sana mvinyo huo halafu nikajiweka sawa pale kwenye kiti changu.

“Vipi, umepata kitu chochote kwenye uchunguzi wako?” Winnie aliniuliza huku akiyatuliza macho yake usoni kwangu.

“Hapana, bado sijapata kitu…” nilijibu.

“Ila matumaini yapo?” Winnie akanipachika tena swali lingine.

“Sijajua kwa kweli,” nilisema huku nikimtazama usoni.

“Nenda kapumzike maana siku hii imekuwa ndefu sana kwako na yenye misukosuko,” Winnie aliniambia huku akijisogea pale kwenye tarakilishi na kuziangalia zile picha za mnato nilizozichukua kwenye eneo la tukio.

“Natamani sana nipumzike lakini sina hakika kama nikifika kitandani nitapata usingizi,” nilisema kwa sauti tulivu lakini iliyobeba kiu ya ushindi. Kisha niliinua tena mkono wangu na kuitazama saa yangu ya mkononi. Mishale ya saa hiyo ilinionesha kuwa ilikuwa imeshatimia saa nne na dakika arobaini za usiku.

Winnie alikuwa anazitazama zile picha za mnato kwenye tarakilishi yangu na kuonesha kusikitishwa sana na tukio lile la kigaidi, alianza kuwalaani watu waliofanya tukio lile la kinyama. “Duniani kuna watu wanyama sana!” Winnie aliongea kwa huzuni huku akiendelea kuzitazama zile picha kwa makini.

“Ni wanyama si kidogo!” niliafiki huku nikipiga funda la mvinyo.

“Natamani sana kukusaidia kuifanya kazi hii?” Winnie aliniuliza huku akiniangalia kwa umakini usoni.

“Kazi ipi?” nilimuuliza huku nikiwa na mashaka kidogo.

“Ya kuchunguza nani waliosababisha mlipuko wa bomu kwenye jengo la Alpha Mall,” Winnie alisema huku akiyakwepa macho yangu na kutazama kando. Sauti yake na sura yake vilimaanisha kile alichokuwa akikisema.

Endelea...
 
taharuki..jpg

283

“Mh! Nisingependa kukuingiza katika matatizo, mrembo. Familia yako bado inakutegemea sana,” nilisema kwa sauti tulivu lakini iliyoonesha wazi shaka ndani yake.

“Usijali, boss,” Winnie akanitoa hofu kisha akaongeza, “Najua kujipigania na kutetea uhai wangu. Natamani sana unishirikishe kwenye uchunguzi wa kazi ngumu kama hizi. Nina uhakika naweza kulifumbua fumbo hili na kisha huu ukawa ni ushindi mkubwa zaidi kwetu sote kama kampuni. Au unaonaje, boss?”

Nilishtuka sana kusikia maneno hayo toka kwa Winnie, nikanyanyua uso wangu uliojaa uchovu kumtazama kwa mshangao huku nikiyatafakari sana maneno yake. Winnie alionekana kumaanisha kile alichokisema na huenda alikuwa anajua kitu kuhusiana na mlipuko ule wa bomu ila hakuwa wazi kuniambia.

Kiukweli binti huyu alishaanza kunitia shaka tangu pale alipoingia ofisini kwangu baada ya mlipuko wa bomu huku akionesha kutokuwa na hofu hata baada ya kuniona nikimwelekezea bastola. Sasa nilikuwa njia panda nikitamani kumfahamu zaidi. Yeye ni nani hasa? Ni mmoja wao au ni ofisa kificho wa usalama wa taifa?

Ili nisimkatishe tamaa niliachia tabasamu na kunyanyua bilauri nikaunywa mvinyo wote uliokuwemo kwenye bilauri hiyo kisha nikaikita juu ya meza. “Natamani kukuamini lakini sitaki kukuingiza kwenye kazi za hatari.”

“Lakini, boss… mimi ni mtu makini,” Winnie alisisitiza.

Moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu nilipomtazama Winnie na kugundua kuwa uso wake ulikwishabadilika na kuwa mbali na mzaha. Nilimtazama machoni nikakiona kitu fulani ambacho sikukielewa kwa haraka. Ilikuwa ni zaidi ya uhakika wa jambo alilokuwa akilisema.

“Una uhakika?” nilimuuliza kwa sauti iliyoonesha shaka fulani, bado nilikuwa nimeyatuliza macho yangu usoni kwake katika namna ya kuyasoma mawazo yake.

“Kwa asilimia zote, boss,” Winnie alisema kwa kujiamini. “Nakuhakikishia hutokuja kujutia kwenye hili.”

“Winnie, naomba uniambie ukweli wewe ni nani?” nilimuuliza huku nikimkazia macho.

“Kwa nini?” Winnie aliniuliza huku akiachia kicheko hafifu katika namna ya kuzuga.

“Nataka tu kufahamu, maana si kwa namna unavyojiamini! Hizi ni kazi za watu wenye taaluma ya ujasusi na si vinginevyo, labda uniambie na wewe ni mmoja wao,” nilimwambia kwa sautu tulivu huku nikimtazama usoni.

Winnie aliachia tabasamu huku akiyaondosha macho yake toka usoni kwangu na kutazama kando, alikaa kimya kwa kitambo fulani akionekana kama aliyekuwa akijishauri jambo kisha akanitazama tena huku akishusha pumzi. Nilikwisha gundua kuwa huyu binti hakuwa wa kawaida, alikuwa na jambo zito sana ndani yake ambalo hakupenda kuliweka wazi.

“Winnie!” nilimwita kwa sauti tulivu.

“Abee!” Winnie aliitikia huku akinitazama kwa wasiwasi.

“Wewe ni nani hasa?” nilimuuliza tena huku nikiwa natabasamu.

Winnie alitabasamu kwanza kabla ya kujibu kwa kuuliza, “Mbona unarudia swali hilo, boss! Kwani umeona nini?”

“Kwa sababu wewe si mtaalamu wa graphics na video editting pekee. Wewe ni nani?” nilimuuliza huku sauti yangu nikiifanya iwe ya kawaida.

Winnie aliyakwepa macho yangu na kutazama chini huku akisita sana. Kusita kwake kulinifanya nimtazame kwa namna ya uchunguzi zaidi katika kumsoma ingawa yeye alijitahidi kuyakwepesha macho yake na kutazama pembeni ili yasikutane na yangu na kwa hali ile nikajua kuwa alikuwa akinificha jambo fulani ambalo nisingeweza kumlazimisha aniweke bayana kwa wakati ule.

Hakutaka kusema mambo mengi, aliniambia kuwa hayo mengine ningekuja kuyafahamu kadiri na muda ukifika.

“Kuwa makini sana,” nilimwambia.

“Usijali, boss,” Winnie alinijibu. “Naweza kujitazama vyema.”

Niliachia kicheko hafifu, si kicheko kama ambavyo Winnie alidhani kuwa niliyaona mazungumzo yetu kama kichekesho fulani bali kicheko changu kilimaanisha kuwa nilikuwa nikiyachukulia maongezi yale kwa uzito mkubwa sana. kuliko ambavyo alidhani. Sasa nilipanga kutafuta taarifa zake ili nimfahamu vyema alikuwa mtu wa aina gani.

Jambo ambalo nilikuwa na uhakika nalo ni kwamba Winnie alikuwa mtaalamu mzuri kwenye masuala ya graphics na video editting, utaalamu wake katika masuala hayo ulikuwa wa kiwango cha juu sana, ndiyo maana nilikuwa nimevutiwa naye baada ya kuletwa kwangu na rafiki yangu Maximillian Njamba, Mkurugenzi wa Njamba Economic and Business Consulting (E.A.) Ltd., na hivyo nikamwajiri katika kampuni yangu ili anitengenezee kurasa za gazeti langu la mtandaoni na kuhariri picha za video kabla hatujazirusha. Hilo wala sikuwa na shaka nalo.

Nilimtazama tena Winnie. Chochote ambacho nilitegemea kukiona katika macho ya msichana huyu kilimezwa na tabasamu jembamba. Msichana huyu, machoni mwa mtu yeyote alikuwa wa kawaida kabisa. Kwa kila hali alikuwa msichana wa kawaida… macho yake yalikuwa ya upole ambayo yasingekuwa na uwezo wa kuficha chochote ambacho angependa kuficha bila ya kumshuku. Lakini hilo halikuondoa ule ‘u-Jason Sizya’ katika fikra zangu.

Kwa muda akili yangu ilihangaika kutafuta kauli ya kuongea. Na kama vile mtu aliyefahamu jinsi akili yangu ilivyohangaika kutafuta neno la kusema aliachia tabasamu pana kisha akaniuliza, “Vipi, Jason, kuna kitu unataka kusema?”

Dah! safari hii Winnie aliita Jason na si badala ya boss! Kabla sijasema jambo nikamwona akishtuka kidogo na kuitazama saa yake ya mkononi. “Dah! Huwa sipendi sana kuwa nje na nyumbani nyakati kama hizi. Ngoja nikazime mashine zangu niondoke nyumbani.”

Nilitabasamu huku nami nikiitazama saa yangu. Yalikuwa ni majira ya saa tano na dakika tano za usiku. Kweli muda ulikuwa umeenda. Nilimtazama Winnie na kumuuliza juu ya makazi yake, akaniambia kuwa alikuwa anaishi eneo la Komakoma, Mwananyamala.

“Unaishi na nani?” nilimuuliza. Ajabu ni kwamba kwa kipindi chote cha miezi sita tangu nimfahamu Winnie sikuwahi kujua makazi yake.

“Nipo kwa wazazi,” Winnie alijibu huku akiyakwepa macho yangu.

“Kwa nini unaishi kwa wazazi hadi leo?” nilimuuliza nikitaka kufahamu lakini hakutaka kujibu swali langu. Aliachia tabasamu pasipo kuonesha meno. Mashavu yake yalituna na macho yake kujifinya.

Okay! Basi kazime na mimi hapa nizime kisha nikusogeze hadi home na gari langu kama hutojali,” nilimwambia.

Thank you,” Winnie alisema na kuanza kupiga hatua kuondoka. Alitembea kwa madaha, kwa vyovyote alijua kuwa macho yangu yalikuwa yakimtazama, hivyo alipoufikia mlango akaufungua na kugeuza shingo yake kunitazama, macho yetu yalipogongana aliyaondosha haraka macho yake na kutazama chini huku tabasamu jembamba likijitokeza na kupotelea katika kona moja ya mdomo wake.

* * *

Endelea...
 
taharuki..jpg

284

Saa 5:15 usiku…

Tulijipakia ndani ya gari langu, nikaliwasha na hapo tukaanza safari ya kumpitisha kwake ili na mimi niende nyumbani nikapumzike. Nilikuwa nimechoka lakini akili yangu ilikuwa haitulii ikiwaza hili na lile. Tulipitia barabara ya Mwananyamala na wakati tukiwa njiani nikawa namdadisi kuhusu uhusiano wake na Maximillian Njamba.

“Nilijuana naye kwa miaka mingi kidogo kupitia dada yake anayeitwa Joyce Njamba, ambaye tulisoma darasa moja pale Zanaki. Baadaye nikaja kugundua kuwa ni rafiki wa kaka yangu mkubwa ambaye kwa sasa anaishi Marekani… Max ni mtu mwenye maneno mengi na mcheshi pia hivyo haikuchukua muda kuunda naye urafiki!”

Kwa hiyo sasa nikafahamu kuwa Maximillian alikuwa na mengi ya kunifahamisha kuhusu Winnie. Sikutaka kumchosha binti huyu kwa maswali yangu yasiyokuwa na mwisho. Niliazimia kutafuta taarifa zake kwenye mfumo maalumu wa utambuzi na kama nisingepata taarifa basi ningemuuliza Maximillian.

Baada ya hapo, ikawa kama zamu ya Winnie kuniuliza. Aliniuliza maswali lukuki juu ya hatari ya kazi ya kazi niliyokuwa naifanya ya kuandika habari za uchunguzi hasa ninapofuatilia jambo ambalo lina maslahi ya wakubwa. Na pia akataka kujua kama nilikuwa na taaluma yoyote ya masuala ya kiintelijensia.

Hivyo kwa namna moja ama nyingine sikushtushwa sana na maswali yake. Nilijitahidi kutoonesha hisia zozote usoni, nikazidi kumpumbaza kuwa mimi nilikuwa mwandishi tu nisiye na ‘A’ wala ‘Be’ katika masuala ya kiintelijensia. Nilimwambia kuwa katika kazi yoyote lazima kuwepo na changamoto hivyo ningeendelea kusimamia kile ambacho niliamini kuwa ni kuutafuta ukweli wa mambo.

Tulipofika Mwananyamala A nikaiacha Barabara ya Hospitali na kukata kushoto nikiifuata Barabara ya Mwinjuma, sikwenda mbali Winnie akanisihi nisimamishe gari. “Nimefika!” aliniambia.

Nikashangaa kidogo kwa kuwa hatukuwa tumefika Komakoma. Hata hivyo sikuonesha mshangao wangu bali nilichofanya ni kusimamisha gari langu chini ya miti kando ya Barabara ya Mwinjuma. Mbele yangu nikaliona lile gari la kifahari aina ya Range Rover Velar la rangi nyeupe lenye vioo vyeusi likiwa limeegeshwa kando ya barabara. Nikalikodolea macho nikijaribu kulichunguza nikiwa na mashaka.

Lilikuwa limeegeshwa takriban mita kumi tu mbele yangu. Muda huo Winnie alikuwa ananishukuru na kisha alifungua mlango wa gari na kushuka huku akiniaga. Nikamwitikia huku nikimtazama nikitaka nione alikuwa anaelekea wapi na wakati huo huo nikiendelea kulichunguza lile gari, kwa hali hiyo Winnie akanipotea katika mazingira ambayo sikujua alielekea wapi. Nikashusha pumzi.

Nikiwa bado hapo naendelea kulichunguza lile gari, mara nikamwona mwanamume mmoja akitokea mtaa wa Ruaha na kwenda moja kwa moja kwenye gari hilo, akazunguka upande wa pili na kupanda ndani ya gari hilo. Umbile la mwanamume huyo lilinifanya nimtambue mara moja. Alikuwa ni yule mwanamume mfupi niliyemwona kule Makumbusho kwenye tukio la bomu akitafuna bubblish. Kilichonifanya nimkumbuke ni macho yake ya kusinzia na mustachi wake mpana.

“Tumekutana tena! What a coincidence!” nilisema kana kwamba alikuwa ananisikia.

Sikuondoka. Niliamua kusubiri nione, macho yangu yaliendelea kulitazama lile gari huku mkono wangu ukiwa umeifikia bastola yangu iliyokuwa kiunoni endapo lingetokea lolote la kutishia usalama wangu. Punde nikamwona msichana mmoja mrefu akiwa amesimama kando ya lile gari upande ule aliokuwepo yule mwanamume mfupi mwenye mustachi mpana. Sikujua msichana huyo alitokea wapi.

Alikuwa msichana mweupe mwenye haiba ya kuvutia. Sura yake ilikuwa ndefu na macho makubwa lakini legevu. Pua yake ilikuwa ndefu na mdomo wake ulikuwa na kingo pana na alikuwa na vishimo vidogo mashavuni mwake. Kichwani alikuwa na nywele ndefu za bandia na alizifunika kwa kofia nyeusi ya kapelo.

Alikuwa amevaa fulana nyeupe iliyoyaficha vyema matiti yake yenye ukubwa wa wastani na juu yake alivaa shati la rangi ya bluu la kitambaa cha dengrizi. Kiuno chake kilikuwa chembamba kiasi kilichoizuia suruali yake ya rangi ya bluu ya kitambaa cha dengrizi na miguuni alikuwa amevaa raba nyeusi.

Muda huo alikuwa ameegemeza mikono yake dirishani mwa gari, akasimama hapo kwa muda kidogo akionekana kuongea jambo na waliokuwemo ndani ya lile gari. Kisha kama aliyekuwa akijishauri jambo, alitazama huku na kule halafu akapanda kwenye gari hilo, wakaondoka. Nilibaki pale pale nikilisindikiza hilo gari kwa macho mpaka lilipoyoyoma kisha nami nikatimka zangu.

* * *



Saa 8:15 usiku…

Jina lake kamili ni Winifrida Thomas Kilomoni, ana urefu wa futi 5 na inchi 8, macho meupe na kundi la damu yake ni A +ve. Winifrida alizaliwa Jijini Dar es Salaam miaka ishirini na sita iliyopita akiwa mtoto wa tatu kati ya watoto watano wa familia ya Kapteni Thomas Zabron Kilomoni na Anastazia William Kigula. Baba yake ni mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na mama yake ni mwalimu.

Winifrida alisoma katika Shule ya Msingi Gilman Rutihinda na kisha akaenda Shule ya Sekondari ya Zanaki, zote za jijini Dar es Salaam na baadaye alikwenda Shule ya Wasichana ya Tabora kwa masomo yake ya juu. Baada ya hapo alikwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alikohitimu Shahada ya Kwanza ya Sanaa katika Lugha na Uandishi.

Akiwa Tabora kipaji chake kilionekana na hivyo wakati anajiunga UDSM tayari Idara ya Usalama wa Taifa ilishakuwa na mpango wa kumwingiza katika programu za mafunzo ya usalama, na hivyo alipomaliza tu chuo akachaguliwa kujiunga na programu maalumu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa ajili ya vijana wasomi walioandaliwa kwenda kuchukua mafunzo ya awali ya ushushushu.

Baada ya kumaliza mafunzo ya kijeshi Winifrida alilitumikia Jeshi kwa muda mfupi na kituo chake kilikuwa Lugalo jijini Dar es Salaam kisha akapelekwa katika Chuo cha Usalama wa Taifa (kilichopo nje ya jiji la Dar es Salaam) kwa ajili ya mafunzo yake ya ushushushu, na baadaye alitunukiwa cheti cha mafunzo ya usanifu picha na uhariri wa video kutoka Mohammed Amin Foundation ya jijini Nairobi.

Winifrida ni shushushu na kazi yake kama shushushu, pasipo kujali ni wapi atatumwa, ni kukusanya taarifa nyeti na muhimu kisha kuzituma kwa mkuu wake kwa ajili ya hatua zaidi. Ana mkanda mweusi katika sanaa ya mapigano hasa katika mtindo wa Taekwondo, na zaidi, ni mwepesi mno kwenye kuchambua mambo na kufanya maamuzi yenye tija, akitambua kuwa ‘kabla risasi haijakufikia, inabidi uwe umeshaamua nini cha kufanya’…

Nilimaliza kusoma kusoma taarifa za siri zilizomhusu Winnie kwenye mfumo maalumu wa utambuzi wa programu ya TracerMark. Tangu niliporejea nyumbani usiku sikuweza kupata usingizi, nilikuwa na kazi tatu; kwanza kutafuta taarifa za Winnie. Pili kuchakata taarifa mpya nilizokuwa nimezipata kuhusiana na shambulizi la bomu katika jengo la Alpha Mall.

Na mwisho nilifanya kazi ya kutafuta taarifa kuwahusu watu wawili; yule mwanamume aliyefika pale kwenye jengo la Alpha Mall akiwa na pikipiki ya magurudumu matatu iliyobeba bomu, na yule mwanamume mfupi mwenye mustachi mpana, halafu nikaangalia kama namba za lile gari aina ya Range Rover Velar la rangi nyeupe zilikuwa halisi. Namba za gari zilikuwa halisi na taarifa za yule mwanamume mfupi hazikuwa na shaka japo nafsi yangu ilinitaka kujiridhisha.

Jina lake kamili ni Deogratius Samson Rutashobya, mzaliwa wa Muleba mkoani Kagera. Ana umri wa miaka thelathini na tatu. Deo, kama anavyojulikana kwa kifupi, ni mfupi lakini mkakamavu na mwenye umbo lililojengeka vyema, baada ya kuhitimu elimu ya sekondari kidato cha sita katika Seminari ya Itaga mkoani Tabora alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa masomo ya Sayansi ya Siasa.

Kisha alijiunga na mafunzo ya awali ya ujasusi ambayo aliyapata katika nchi ya Afrika Kusini na baadaye nchini China ambako alihitimu vyema kabla ya kuendelea na masomo ya saikolojia katika Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza.

Tangu ajiunge na Idara ya Usalama wa Taifa, Deogratius alionekana kuwa na uwezo mkubwa sana na mbinu nyingi za kiupelelezi hasa alipokuwa akifanya kazi wilayani Kahama na baadaye chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Mbali na Kiswahili Deogratius anazifahamu lugha tano za kimataifa za Kiingereza, Kifaransa, Kispaniola, Kiitaliano na Kichina, na pia ana uwezo wa kuongea lugha za makabila mbalimbali ya Tanzania. Kwa sasa anafanya kazi kama ofisa kificho.

Sasa nilitambua ni kwa nini nilikuwa na hakika kuwa sura yake haikuwa ngeni kwangu, kumbe niliwahi kumwona wilayani Kahama wakati alipokuwa akifanya kazi huko kama ofisa wa usalama wa taifa chini ya Mkuu wa Usalama wa Taifa (DSO) Wilaya ya Kahama, Mzee Yasin Mzee.

Ila hakukuwa na taarifa zozote kumhusu yule mwanamume mrefu aliyelipua jengo la Alpha Mall.

Mwishowe niliamua kuachana kwanza na kazi hiyo baada ya kuhisi akili yangu ilikuwa imechoka, nikainuka na kulifuata jokofu na kutoa chupa kubwa ya whisky, nikawa nagida mvinyo huku nikielekea chumbani. Niliketi kitandani nikaunywa mvinyo wote kisha nikalala kitandani. Nilijua kabisa bila hivyo nisingeweza kupata usingizi, usingizi ungekuwa mrefu kupitiliza yaani, ningeshtuka kila mara.

* * *

Endelea kufuatilia...
 
taharuki..jpg

285

Saa 5:30 asubuhi…

Ilikuwa Jumapili tulivu iliyojaa simanzi kutokana na tukio la kigaidi lililokuwa limetokea siku moja kabla. Saa tano na nusu asubuhi ilinikuta nikiwa nafika kwenye makazi ya Waziri Ummi Mrutu eneo la Mikocheni B jijini Dar es Salaam, nikiwa natumia pikipiki niliyoiazima kwa Evans Mwinuka, mmoja wa wafanyakazi wangu. Nilitumia pikipiki kwa sababu za kuepuka usumbufu pale ambapo ningelazimika kukimbia huku na kule katika kufuatilia mawindo. Nilikuwa nimebeba kamera yangu kwa ajili ya majukumu yangu kama mwandishi wa habari.

Makazi ya Waziri Ummi yalikuwa ya kuvutia. Nyumba kubwa na nzuri ya kifahari iliyokuwa imezungukwa na miti mizuri ya kivuli na sehemu za wazi zenye bustani nzuri ya maua na nyasi za kijani kibichi zilizokatwa vizuri. Ukuta wa ile nyumba kuizunguka ulikuwa mrefu uliokuwa umefungwa mfumo maalumu wa umeme wa kuzuia wezi juu yake usiomwezesha mtu kuona ndani.

Ilikuwa moja ya majumba makubwa ya kisasa ya watu wenye ukwasi yaliyokuwa yamezungushwa uzio na mageti makubwa yenye vifaa vyote vya usalama vya kuwahakikishia wakazi wake usalama wa hali ya juu. Geti refu jeusi la nyumba hiyo lilikuwa wazi kukaribisha waombolezaji.

“Muuaji hupenda kushiriki misiba ya aliowaua, si ajabu akawepo hapa,” niliwaza wakati nikitembea kuingia ndani ya uzio wa ile nyumba huku nikiyatembeza macho yangu kijanja kuwatazama watu waliokuwepo pale msibani, kila nilipopiga hatua nilihisi nywele zangu zikinisimama na mwili kunisisimka.

Nilitafuta eneo nikasimama kwanza ili nisome mazingira na namna mambo yanavyoenda. Lengo langu hapo lilikuwa kutafuta lolote ambalo lingenisaidia kwenye ung’amuzi wangu juu ya kilichokuwa kikiendelea kumhusu Waziri Ummi. Katika kufanya hivyo nikamwona mwanamume mmoja mrefu aliyekuwa ameketi mahala fulani kwa utulivu sana. Alikuwa amevalia suti nyeusi na kofia ya pama nyeusi, uso wake ulikuwa mrefu na macho yake alikuwa kayaficha kwa miwani myeusi.

Kwenye baraza kubwa ya nyumba hiyo kulikuwa na picha kubwa ya Waziri Ummi iliyopambwa maua na mishuma miwili ilikuwa ikiwaka huku na huku, nikainuka na kuisogelea picha ile, nilisimama pale kimya kwa nukta kadhaa kisha nikasaini kitabu maalumu kilichokuwa hapo kabla sijapiga picha kadhaa. Nilipomaliza nikatoka na kujaribu kuwahoji baadhi ya jamaa wa marehemu mawili matatu huku nikiwapa pole kwa msiba ule.

Muda wote nilikuwa makini sana, nilijua nisingeweza kutoka hapo msibani mtupu, nilitegemea kupata mwanga angalau nikakutana na mtu ambaye ningemtilia shaka. Penye wengi hapakosi jambo kama wasemavyo Waswahili. Nami niliamini hilo na ndiyo maana nilikuwepo hapo.

Katika zunguka zunguka yangu nilimwona bosi wangu Tunu Michael, viongozi kadhaa wa serikali na vyama vya siasa na baadhi ya maofisa usalama waliokuwa wakifuatilia nyendo za waombolezaji, nikaendelea kujifanya natafuta habari huku nikipiga picha, muda wote macho yangu yalikuwa makini kutazamatazama huku na kule, na hatimaye nikapata eneo lililokuwa kijiwe cha stori. Walikuwa wamejikusanya wanaume kadhaa hapo wakiteta. Nami nikajisogeza taratibu mpaka hapo ili nitege sikio.

Kabla sijafanikiwa kusikia lolote nikamwona mwanamke fulani mrefu mweupe akiwa ndani ya hijabu. Nikajikuta nikivutiwa sana kumtazama mwanamke huyo na haikuchukua muda nikamfahamu kuwa ni yule msichana niliyemwona usiku akiwa na mpelelezi Deogratius kule Mwananyamala halafu akapanda kwenye gari aina ya Range Rover Velar la rangi nyeupe na kisha gari hilo likatokomea.

Kwa namna alivyokuwa mtu mwenye wasiwasi nilianza kupata shaka, nikawa makini sana kumfuatilia nikihakikisha macho yangu hayabanduki toka kwa mwanamke huyo, kila alipoenda na kuongea na watu nikawa namtazama. Hata hivyo sikujua kwa nini sikuwa na imani na mwanamke yule! Nilimpiga picha mbili kwa siri ili baadaye nikatafute taarifa zake kwenye mfumo maalumu wa utambuzi.

Haikuchukua muda mrefu nikamwona akiwa anaongea na mwanaume fulani aliyekuwa amenipa mgongo. Mwanaume huyo alikuwa mrefu mwenye mwili uliojengeka na alikuwa amevalia suti nyeusi. Kichwa chake hakikuwa na nywele. Nikiwa najaribu kubashiri angekuwa nani mara yule mwanamume aligeuka na hapo nikamwona vizuri. Nikamkumbuka kuwa ni yule niliyemwona mwanzo wakati naingia akiwa amevaa kofia ya pama na miwani myeusi.

Sasa alikuwa ameivua ile kofia lakini bado alikuwa na miwani iliyoyaficha macho yake. Hata hivyo niliweza kubaini kuwa macho yake yalikuwa yameingia ndani. Nilimtazama kwa umakini mwanaume huyo, hisia zangu zikaniambia kuwa niliwahi kumwona mahala fulani lakini sikukumbuka nilimwona wapi.

Sasa nikajikuta nikipata hamu ya kumfahamu zaidi na pia kujua yeye na yule mwanamke walikuwepo pale kama nani na malengo yao hasa yalikuwa nini! Nilihakikisha siwatoi kwenye mboni za macho yangu. Niliwapiga picha kwa siri huku nikiamua kuwaweka kwenye uangalizi maalumu, kisha nilimtumia ujumbe mfupi Tunu kumtaarifu juu ya shaka yangu kwa watu wale. Tunu alinitaka niwe makini na nyendo zao halafu kama nitagundua chochote basi nimjulishe.

Mara wakanipotea katika mazingira ambayo sikujua walielekea wapi! nikatweta na kuanza kuzunguka huku na kule nikiwatafuta na katika kufanya hivyo nikamwona yule mwanamume akipenya katikati ya magari mengi yaliyokuwa yameegeshwa eneo lile la msibani. Nikaanza kumfuatilia huku nikimtafuta yule mwanamke lakini sikumwona. Kisha yule mtu akaingia kwenye gari moja la kifahari aina ya BMW X6 la rangi nyeusi lililokuwa na vioo vyeusi kisha lile gari likaondoka toka eneo lile.

Nami nikaondoka kuifuata pikipiki niliyokuja nayo huku nikimtumia Tunu ujumbe mwingine kuwa nilikuwa namfuatilia yule mtu, mara lile gari likasimama mbele kidogo na yule mwanamke akapanda, gari likaondoka. Nikapa shaka na hivyo kuzidisha umakini wangu katika kuwafuatilia kwa nyuma nikilipa umbali kidogo lile gari.

Lile gari liliingia Barabara ya Mwai Kibaki kisha likakunja kushoto likielekea maeneo ya Kawe likiwa katika mwendo wa wastani. Baada ya safari fupi hatimaye tukaja kukutana na Barabara ya CocaCola kwa upande wa kushoto. Barabara ya CocaCola ilikuwa ni barabara maarufu eneo lile na yenye msongamano mkubwa wa magari yaliyotoka na kwenda eneo la Mwenge yakipitia eneo la kiwanda cha soda za CocaCola.

Na hapo nikalivuka lile gari na kujifanya nilikuwa na safari zangu, baada ya umbali mfupi nikafika kwenye daraja na kulivuka, nilipochunguza kwenye kioo cha pikipiki cha kutazama nyuma nikaliona gari likija nyuma yangu, mbele kidogo nikayavuka majengo ya Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Mlalakua) upande wa kushoto. Nikapunguza mwendo nikijifanya kutafuta kitu maeneo yale, na hapo lile gari likanipita kisha likalipita lori aina ya Fuso lililokuwa mbele yao.

Nami niliendelea kuwafungia mkia. Baada ya mwendo wa dakika kadhaa tukalivuka jengo la Infortech upande wa kulia halafu tukaufikia mzunguko wa barabara ulioziunganisha barabara za Mwai Kibaki na Old Bagamoyo, eneo la Kawe-Maringo.

Nikaliona lile gari likiuzunguka ule mzunguko na kuziacha barabara za Mwai Kibaki na Old Bagamoyo likaanza kuifuata barabara iliyoelekea Kawe Beach. Nami nikaifuata barabara ile nikiendelea kuwafungia mkia. Nikaliona lile gari likidaka njia nyingine ya kuchepukia na ndani ya muda mfupi likawa limesimama kando ya mtaa ule. Nikawapita na kwenda mbele zaidi nikijifanya nina safafri zangu. Hata hivyo nilishahisi kuwa walifahamu kuwa nilikuwa nawafuatilia.

Hisia zangu ziliniambia kuwa kwa vyovyote walikuwa wanaelekea maeneo ya Mbezi Beach, hivyo nilikwenda kubana sehemu fulani jirani na barabara ya Mwai Kibaki nikiamini kuwa kwa vyovyote wangepita njia ile, hapo nikaiacha ile pikipiki kwa jamaa mmoja niliyemfahamu na kukodi bajaj, nikatulia ndani ya Bajaj nikimtaka dereva wa Bajaj hiyo awe na Subira.

Nilisubirihapo takriban dakika ishirini bila kuliona lile gari likitokea. Nikaanza kupatwa na wasiwasi kuwa huenda waliamua kurudi walikotoka au walipita njia nyingine, nikaanza kukata tamaa na nilipotaka kuondoka nikaliona lile gari likipita barabara ile na kuingia Barabara ya Mwai Kibaki likielekea maeneo ya Mbezi Beach. Nilihisi kuwa sasa waliamini kuwa wapo salama.

Nikamweleza dereva wa Bajaj alifuate gari hilo lakini ahakikishe hawafahamu kama tunawafuata. Yule dereva aliniambia nisiwe na wasiwasi hata kama wangetupotea alifahamu ni wapi walikuwa wanaelekea, kwani alishaliona gari lile mara kadhaa. Niliwaona wakienda hadi walipoyafikia makutano ya barabara ile za Mwai Kibaki na Ally Sykes, wakavuka na baadaye wakaikuta barabara ya Bahari kwa upande wao wa kulia. Dereva akaingia upande ule akiifuata ile barabara iliyopita katikati ya majumba ya kifahari yaliyozungukwa na kuta zenye ulinzi hadi alipokutana na barabara nyingine ya Ufukweni iliyoelekea kushoto, akakunja kuelekea kushoto akiifuata ile barabara.

Baada ya mwendo mfupi dereva alipunguza mwendo na hatimaye akasimamisha gari mbele ya geti kubwa jeusi kwenye kasri la kifahari, nikaweza kuziona namba kwenye ukuta ya jumba hilo. Ilikuwa nyumba namba 89. Dereva akapiga honi mara mbili. Haukupita muda mrefu geti dogo lililokuwa kando ya lile geti kubwa likafunguliwa na askari mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi akachungulia.

Yule mlinzi alipoliona lile gari akafungua geti kubwa. Wakazama ndani na geti kufungwa nyuma yao. Nikaridhika. Ilimradi sasa nilishajua makazi yao, kwangu hii ilikuwa hatua muhimu sana kuelekea kupata majibu ya maswali yangu. Hivyo sikupoteza muda. Nikamwambia dereva tuondoke ila niliapa kurudi tena na kulifanyia jengo hilo upelelezi zaidi ili nijiridhishe juu ya shaka yangu.

* * *

Endelea...
 
taharuki..jpg

286

Kundi la Nge…




Saa 12:00 asubuhi…

JUMATATU nilifika kwenye ofisi za SPACE mapema kuliko kawaida, nikamkuta bosi wangu, Tunu Michael ameshafika na yupo ofisini kwake. Baada ya kusalimiana nilimwelezea kwa kirefu nikianza na namna hisia zangu zilivyonituma kupiga picha za video kuhusu adha ya usafiri wa daladala jijini Dar es Salaam hadi nilivyojikuta nikilipiga picha tukio zima la kigaidi, nikamwonesha kipande cha video cha dakika 15 kuanzia pale yule mtu mwenye ovaroli akiingia na pikipiki ta magurudumu matatu hadi kutokea kwa mlipuko wa bomu. Hadi anamaliza kuitazama video hiyo alikuwa anatweta kwa msisimuko.

Kilikuwa kipande cha video cha dakika kumi na tano tu lakini kilichobeba ushahidi mkubwa mno kuhusu kile ambacho wengi hawakukijua kuhusu tukio lile la kigaidi. Kwa ujumla tukio zima lilivyoonekana lilikuwa kama sinema. Baada ya kutazama video ile nikampa asome taarifa niliyokuwa nimeikusanya hadi muda huo. Tunu aliisoma kwa uamini kisha akainua uso wake kunitazama akiwa haamini. Alibaki kimya kwa takriban dakika tano akinitazama, asijue nini cha kuongea.

“Kuna mtu mwingine yeyote anayefahamu uwepo wa video hii?” hatimaye Tunu aliniuliza na kuvunja ukimya.

“Hapana. Sikutaka mtu yeyote zaidi yako afahamu juu ya suala hili katika hatua ya awali kama hii,” nilimwambia Tunu kisha nikamweleza kuhusu mazungumzo yangu na Kamishina Koba aliyetaka kufahamu kama nilifahamu chochote kuhusiana na tukio lile, na jinsi nilivyopata hisia mbaya dhidi yake na kuamua kumficha taarifa alizozitaka.

Tunu alionekana kupendezwa sana na uamuzi wangu. “Niseme tu kuwa umefanya uamuzi mzuri na wa busara kwa kutokutoa taarifa hizi kwa chombo chochote cha usalama, huwezi kujua yupi ni mtu sahihi na yupi mamluki. Naomba jambo hili lifanyike kwa weledi na usiri wa hali ya juu vinginevyo taasisi yetu inaweza kuonekana haipo makini,” Tunu aliniambia.

Kisha kikatokea kitambo kingine cha ukimya na baada ya ukimya ule Tunu aliniambia kuwa kazi yangu ilikuwa imemfurahisha sana kiasi cha kukosa neno la kusema. Alinisifu sana kwa wepesi wangu wa kung’amua hatari kama ilivyotokea kule jijini Mombasa ambako japo nilikwenda kwa mapumziko lakini niliweza kubaini hatari na kuisaidia nchi hiyo kuepukana na tukio la kigaidi lililokuwa litokee ufukweni mwa jiji hilo la Mombasa.

Vivyo hivyo video ile na taarifa nilizokuwa nimezikusanya ilikuwa hatua kubwa mno ambayo aliamini hakuna kachero yeyote au taasisi yoyote ya ulinzi na usalama waliokuwa wamefikia hata nusu ya hatua ile.

“Uliponiambia utanishirikisha kuhusu jambo hili sikufahamu kama ulikuwa umefanya kazi kubwa namna hii! Hii ni kazi nzuri sana na kwa kweli hukuniangusha. Umeiwakilisha vyema taasisi yetu ya SPACE…” Tunu alisema huku akishindwa kuificha furaha yake, kisha akaongeza, “Nakushukuru sana.”

Maneno yake yalinitia moyo mno. Nikamshukuru kwa kuniamini kiasi hicho. Kisha aliniambia kuwa ili kazi yangu iwe nyepesi baada ya kikao kilichotarajiwa kuanza muda wowote tungekuwa na mjadala wa kina japokuwa makao makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa tayari walishaunda kikosi kazi cha kushughulikia jambo hilo.

“Unajua katika kazi zetu hakuna kuaminiana, huwezi jua pengine mtu unayemshirikisha ni mmoja wa waliofanya tukio, hivyo ni mimi na wewe tu tunaopaswa kujua uwepo wa video hii. Ingawa kutakuwa na majukumu mengine utakayopewa kuyashughulikia lakini hili ndilo liwe kipaumbele hadi tutakapombaini adui popote alipo… kuanzia sasa jambo hili limeshaingia katika utaratibu wa usiri,” Tunu aliniambia.

Ilipofika saa moja na nusu maofisa wote walikuwa wameshafika na tayari tulishaketi kuzunguka meza ya mkutano, tayari kwa kikao cha kupashana taarifa za kiitelijensia kuhusu hali ya ulinzi na usalama nchini na kupanga mikakati ya kukamilisha malengo ya kazi zilizokuwa zikitukabili (situation report - SITREP). Kikao cha asubuhi hii kilikuwa muhimu sana na cha aina yake. Kilikuwa kikao cha kwanza baada ya tukio la kigaidi na kiliwahusisha pia maofisa wengine kutoka nje ya Taasisi ya SPACE.

Kwa maofisa hao wageni hiki kilikuwa kikao chao cha kwanza. Walikuwa maofisa watano, wawili walitoka makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CID); ofisa mmoja alitoka Kikosi cha Siri cha Ulinzi (Secret Service); na maofisa wengine wawili walitoka Idara ya Ujasusi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (Millitary Intelligence - MI).

Miongoni mwa maofisa hao niliweza kuwatambua wawili, Johnson Mwita kutoka Idara ya Ujasusi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Inspekta Dina Hasunga kutoka makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai. Maofisa wageni walipewa nafasi ya kujitambulisha kwa kifupi majina yao na taasisi walizotoka na baada ya hapo Tunu alisema kuwa angetueleza baadaye kuhusu lengo la maofisa hao kuwepo kwenye kikao hicho.

Japo ndiyo kwanza siku ilikuwa inaanza lakini nilihisi mwili wangu ulikuwa umechoka na ukiniuma kutokana na pilika pilika za siku mbili ingawa kazi ngumu, tena ya hatari, ilikuwa bado ikinikabili. Ilikuwa imepita miezi saba tu tangu nilipotoka kwenye hekaheka za kupambana na magaidi wa al-Shabab kule Mombasa nchini Kenya, mapambano ambayo kuna mtu mmoja aliona ni vyema aandike stori aliyoipa jina la “Ufukweni Mombasa”.

Kwa Tunu Michael mambo yalikuwa magumu zaidi, kwani yeye ndiye aliyekuwa Mkuu wa Taasisi ya SPACE, taasisi ambayo kimsingi ndiyo kilikuwa kitengo cha ufundi (Technical Unit) cha Idara ya Usalama wa Taifa. Maofisa ndani ya SPACE tulikuwa ni watu ambao tulipata mafunzo maalumu ya kutumia vyombo vya kisasa vinavyotamba katika sanaa ya ujasusi, na Tunu ndiye aliyekuwa mkuu wetu.

Kazi kubwa ya maofisa wa Taasisi ya SPACE ilikuwa kutoa msaada (support) kwa maofisa walioko katika medani (field) katika kuunganisha nukta zinazopungua kwenye taarifa wanazofuatilia. Kwa kifupi sisi (kama mafundi) ndio tuliopaswa kufanya kazi ya kunasa mawasiliano ya adui, kusikiliza mazungumzo ya simu (phone bugging) na kuchungulia baruapepe (email interception) za watuhumiwa, ndugu na washirika wao. Pia tulitumika kufanya ufuatiliaji (surveillance) wa watuhumiwa, na washirika wao.

Kutokana na wadhifa wake wa ukuu wa taasisi hii, Tunu alikuwa na jukumu la kuwasiliana moja kwa moja na makao makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa na kujibu hoja au kueleza nini taasisi yake imefanya katika kuweka mikakati ya ulinzi na usalama mtandaoni. Hivyo utaona ni namna gani mambo yalikuwa magumu zaidi kwa Tunu.

Kama kawaida Mkuu wa SPACE ndiye aliyefungua kikao (SITREP) kwa kutoa maelezo mafupi kuhusu hali ya usalama nchini. Siku hii agenda ilikuwa moja tu; suala la ugaidi uliotokea katika jengo la Alpha Mall eneo la Makumbusho. Kwa takriban dakika kumi na tano Tunu alitusomea taarifa maalumu iliyotolewa na makao makuu ya Idara ya Ujasusi kuhusu shambulio hilo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Watanzania 32 walikuwa wamepoteza maisha yao, na wengine 95 walikuwa wamejeruhiwa. Wapo waathirika wa bomu hilo walikumbwa na umauti wakiwa ndani ya jengo la Alpha Mall kwa shughuli za kiofisi, shughuli za kibiashara n.k. na wengine walikuwa wapita njia au waliokuwa abiria kwenye magari yaliyoteketea kwa moto baada ya mlipuko.

Endelea...
 
taharuki..jpg

287

Pia ilielezwa kuwa ukiacha idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha yao, kulikuwa na uwezekano kwamba wengine walikuwa bado wamefunikwa kwenye kifusi. Kutokana na kutokuwepo kwa vikosi maalumu vya uokoaji na uhaba wa vifaa vya kisasa, idadi ya vifo ilitarajiwa kuongezeka. Hivyo, msaada wa haraka ulihitajika ili kunusuru maisha ya waathirika hao.

Kufuatia tukio hilo Rais alitembelea eneo la tukio kujionea hali halisi ilivyokuwa na kisha aliwatembelea majeruhi 55 waliokuwa wamelazwa katika hospitali ya Muhimbili, Agha Khan 18 na Mwananyamala 22.

Taarifa hiyo pia iligusia uwepo wa chembe chembe za ugaidi nchini, na Idara ya Ujasusi iliazimia kuelekeza nguvu zake zote katika ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia ili kuvitambua vikundi vya kigaidi, washirika wake, wafadhili wake, na jinsi vinavyofanya kazi. Hadi muda huo hakuna kikundi chochote kilichokuwa kimekiri au kutangaza kwamba kilihusika na shambulio hilo.

Mwisho, Tunu alitwambia kuwa makao makuu ya Idara ya Ujasusi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini walikuwa wameunda kikosi kazi (task force) kilichogawanywa katika makundi matatu: Kundi la kwanza lilijulikana kama “Termite” (Mchwa) na maofisa wake walikuwa na jukumu la kukusanya taarifa za kiusalama katika maeneo waliyopangiwa na kuziwasilisha kwenye task force. Walipaswa kuchunguza na kukusanya alama za vidole, nyayo na vinasaba (DNA) ili kuthibitisha uwepo wa mtuhumiwa katika eneo husika.

Pia walitakiwa kutambua aina ya bomu lililotumika, vifaa na aina ya vilipuzi vilivyotumika kutengeneza bomu, nguvu na uzito wa mlipuko husika, na madhara yaliyosababishwa na bomu, na kukusanya ushahidi ambao ungetumika kumpata mmiliki au dereva wa chombo kilichobeba bomu. Na walikuwa na wajibu wa kufanya uchunguzi wa viungo vya watu waliouawa katika shambulio, na kupambanua kina nani ni waathirika, na nani walikuwa na viashiria vya kuwa wabebaji wa bomu.

Kundi la pili lilijulikana kama “Spider” (Buibui) na maofisa wake walitakiwa kufanya uchunguzi wa haraka wa eneo la tukio kabla halijavurugwa, na kupata maelezo ya mashahidi kabla hawajatoweka. Haya yote yalitakiwa kufanyika kwa umakini ili kuweka msingi wa mashitaka, na kuwezesha upatikanaji wa wahalifu. Kazi nyingine ya msingi ilikuwa kuangalia namna ya kuzuia matukio mengine ya kigaidi kutokea, kwani wajumbe walitambua na kukubaliana kuwa mashambulizi katika jengo la Alpha Mall ungeweza kuwa mwanzo tu wa mashambulio mengi.

Kundi la tatu lilijulikana kama “Scorpion” (Nge), hili lilituhusisha maofisa wa Taasisi ya SPACE ambao ndio tulikuwa na mafunzo maalumu ya kutumia vyombo vya kisasa vinavyotamba katika sanaa ya ujasusi. Ni katika kundi hili ndipo wale maofisa wageni watano kutoka vyombo vingine vya ulinzi na usalama walikuwa wameletwa kuongeza nguvu kwani walikuwa na sifa zilizowafanya kuingizwa kwenye kundi hili. Walikuwa na elimu na uzoefu wa hali ya juu katika kazi za kikachero na waliwahi kushiriki katika operesheni nyingi ngumu za aina hiyo.

Tunu alikuwa bingwa wa kupanga mikakati na kuelekeza namna ya kufanya kazi, alitueleza kwa kirefu kazi tuliyokuwa tunapaswa kuifanya na namna tulivyotakiwa kuifanya. Mengi ya maelezo yake yalirejea ‘Amri ya Kazi’ (Operation Order) tuliyokuwa tumepewa. Kutia uzito maelezo yake, Tunu alianza kwa kusisitiza kwamba kila ofisa aliyekuwepo hapo ndani alikuwa amewekwa kwenye mizani na kuonekana anafaa kwa kila hali.

Ni kweli, licha ya kwamba wenzangu wote walikuwa wana muda mrefu kazini na mimi muda wangu ulikuwa mfupi ndani ya Idara ya Ujasusi lakini nilikuwa miongoni mwa maofisa tuliofuzu vyema mafunzoni na tayari nilishakuwa na uzoefu wa kukutana na mikikimikiki katika kazi ya upelelezi na kukusanya taarifa za kijasusi kwa kutumia watu na vyombo.

Kwa sababu hiyo Tunu alikuwa na uhakika wa kuona kazi ikitendeka kwa weledi na kwa kufuata misingi na kanuni za Idara ya Usalama wa Taifa. Alisisitiza kuwa sisi tuliokuwepo hapo ndio tulikuwa kipimo cha ukamilifu wa uwezo na ufanisi wa Idara ya Usalama wa Taifa.

“Taarifa za kila mtu anayetiliwa shaka pamoja na nyingine zote zifikishwe kwangu kwa utaratibu maalumu ulioelezwa kwenye operation order,” Tunu alitueleza kisha akasema kuwa Taasisi ya SPACE ilikuwa imebahatika kwa kuwa ofisa wake mmoja alikuwepo kwenye eneo la tukio wakati bomu linalipuka na alishiriki vyema katika hatua zote za awali za uokozi na kuchukua taarifa.

Baadhi ya maofisa wakawa na hamu ya kumfahamu ofisa huyo ni nani, na hapo ndipo Tunu aliponiomba kama inawezekana nikieleze kikao mambo niliyoyashuhudia ili kuwapa picha nzuri zaidi.

Kwa kirefu niliwaeleza jinsi mambo yalivyokuwa tangu lilipotokea shambulio na jinsi nilivyoshiriki katika zoezi zima la uokoaji na wakati huo huo nikichukua maelezo ya waathirika, anwani za makazi yao, jamaa zao na mambo mengine. Nilijitahidi kuwapa maelezo ya kina ili kuwapa picha halisi ya mfululizo wa matukio lakini sikugusia kabisa kama nilikuwa nimepiga picha za video iliyomwonesha yule mtu akifika kwenye jengo la Alpha Mall na pikipiki ya magurudumu matatu ambayo ndiyo ilikuwa imebeba bomu. Mambo hayo yalishaingia katika utaratibu wa usiri na hivyo sikupaswa kuyaeleza kwa maofisa wengine.

Baada ya maelezo yangu tuliendelea na kikao, sasa Tunu alitupa muda wa kujadili kama kulikuwa na chochote cha kujadiliana kabla hatujaelekea kwenye majukumu. Mjadala mkubwa ulikuwa katika masuala tuliyoona ni muhimu zaidi kufuatia hali tete iliyokuwepo nchini. Jambo kubwa lilikuwa kutoa ushauri kwa serikali hususan hatua za kuchukua kulinda jina la Tanzania ili tusipoteze mapato yatokanayo na biashara ya utalii na uwekezaji nchini.

Kisha kama ilivyokuwa kawaida yake, siku hiyo Tunu aligawa majukumu mapya kwa maofisa usalama wote wa Taasisi ya SPACE, kisha akasisitiza umuhimu wa kila ofisa kukamilisha kazi zake kwa wakati na kwa kuzingatia maadili na miiko ya Idara katika kila hatua ya utendaji kazi.

Alipomaliza kutoa maagizo ya jumla alitupa nafasi ya kujadili agizo moja moja na pia kuuliza maswali kwa mambo yaliyokuwa hayaeleweki vyema. Baada ya kipindi cha takriban nusu saa za kueleweshana Tunu alimkabidhi kila mmoja wetu hati za maagizo ya kazi aliyotakiwa kuishughulikia kama alivyokuwa ameelekeza.

Hati niliyopewa haikuwa mpya, ilikuwa ni mwendelezo wa kazi niliyokuwa nikiifanya. Tofauti na hati nyingine, hati yangu ilikuwa na maagizo maalumu niliyopaswa kuyafuata ili kufanikisha kazi ngumu na ya hatari iliyokuwa ikiniumiza kichwa kwa zaidi ya wiki mbili.

Kisha aliwataka maofisa wakaendelee na majukumu isipokuwa mimi, niliambiwa nibaki ofisini kwake kwa dakika chache. Tulipobaki wawili Tunu alinitaka tuendelee kuijadili kwa kirefu taarifa niliyokuwa nimempa kuhusiana na mlipuko wa bomu kwenye jengo la Alpha Mall.

Hata hivyo alikuwa na maswali yaliyomtatiza sana, “Ninatatizwa sana…” Tunu alisema, “hivi hawa waliofanya ugaidi huu walikusudia nini hasa? Kwa nini ugaidi ufanywe kwenye jengo la Alpha Mall na si kwenye majengo ya serikali, hospitali kama Muhimbili, majengo ya ubalozi, masoko na sehemu maarufu za biashara, hoteli za kitalii, mitaa yenye mikusanyiko ya watu wengi au kwenye madaraja muhimu kama la Tanzanite na lile la Mwalimu Nyerere?”

Endelea...
 
taharuki..jpg

288

Maswali ya Tunu yaliufanya ubongo wangu uchemke kutafuta majibu. Na hapo akili yangu ikafunguka zaidi: nikajiuliza kulikuwa na nini kwenye jengo la Alpha Mall hadi magaidi walenge kulipua hapo badala ya sehemu nyingine? Je, nini lilikuwa lengo lao yaani ni ujumbe gani waliotaka kuutoa kwa serikali kwa kulipua jengo hilo?

Mara nikajiwa na jambo akilini mwangu ambalo mwanzoni sikuwa nimelifikiria kabisa! Kabla sijamwambia chochote Tunu kuhusiana na jambo hilo nilimwomba akitazame upya kile kipande cha video kilichoonesha namna yule mtu aliyefika pale kwenye jengo la Alpha Mall na pikipiki ya magurudumu matatu alivyokuwa akilazimisha kuipachika pikipiki yake katikati ya magari ya Waziri wa Mambo ya Ndani na lile la mpelelezi wa kujitegemea Daniel Kayera.

Magari hayo yalikuwa kwenye maegesho usawa wa dirisha la ofisi ya DanKay Private Detective Agent. Hii ilimaanisha kuwa kama si wote wawili basi mmoja kati ya Waziri Ummi Mrutu au Daniel Kayera ndiye alikuwa mlengwa wa shambulio hilo.

“Sasa tujiulize, ni nani alikuwa targeted kati ya watu hawa wawili maana kiukweli wote wanao maadui wenye nguvu kutokana na kazi zao na uadilifu wao,” nilisema na hapo Tunu akaafikiana na mimi kuhusu jambo hilo.

Nilisisitiza kuwa maadui wa Waziri Ummi na hata Daniel Kayera kwa vyovyote wasingekuwa watu wa nje bali wa ndani, hivyo tulipaswa kuliangalia jambo hilo kwa uzito mkubwa sana. Sasa kazi ilikuwa ni kutafuta kujua akina nani wangeweza kuwa maadui wa Waziri Ummi Mrutu, na akina nani wangeweza kuwa maadui wa Daniel Kayera. Na kwa nini? Hapo ndipo tulipopaswa kuanzia kazi yetu.

Tulipoanza kumjadili Daniel Kayera tukijaribu kubashiri kama ndiye mlengwa wa bomu hilo, je, nani wangeweza kuwa maadui wake. Na hapo tukabaini kuwa maadui wake ni wale ambao alikuwa akipambana nao kisheria wakati akitafuta haki za wateja wake, kama ilivyokuwa kwenye ile kesi iliyohusu kifo cha Ofisa wa Mashtaka wa Mkoa (RPO) wa Morogoro, Dk Devota Komba, aliyedaiwa kujinyonga kwa kamba ya manila chumbani kwake katika eneo la Forest Hill mjini Morogoro.

Japokuwa kesi ile iliwaibua watu wazito na wafanyabiashara wakubwa wa mjini Morogoro lakini, kwa haraka haraka tu, kila mmoja wetu alibaini kuwa Daniel Kayera asingeweza kuwa ‘target’ ya ugaidi huo kwa kuwa aina ya adui zake wasingeweza kufanya ugaidi wa aina ile, na kama wangehitaji kumuua wasingekuwa na sababu ya kutumia nguvu kubwa namna ile. Hivyo tuliamua kumtoa Daniel Kayera kuwa target ya ugaidi huo. Ila kwa upande wa Waziri Ummi Mrutu, sote tulikubaliana kuwa alikuwa na maadui wakubwa na wenye nguvu.

Lakini bado nilikuwa na shaka, nikamwuliza Tunu, kama shida ya magaidi hao ilikuwa kummaliza Waziri Ummi Mrutu tu kwa nini sasa watumie njia ile ya bomu ambalo liliangamiza watu wengi na kuleta taharuki nchini? Swali hili likazua mjadala mwingine tena… badala ya kupata ufumbuzi sasa tulijikuta tukizidi kutumbukia ndani ya shimo refu lenye kiza kizito…

Ni hapo sasa Tunu aliponiambia kuwa tulihitaji muda zaidi wa kuyatafakari mambo yote hayo ila kwanza tupate nafasi ya kila mmoja wetu kutafakari kwa kina na kuchakata taarifa alizozifahamu kuhusu Waziri Ummi Mrutu… vinginevyo tungeendelea kujiuliza maswali ambayo yangezidi kutuchanganya na tusingepata mwafaka.

“Halafu kwa kukukumbusha tu, kwa nafasi yake kama Waziri wa Mambo ya Ndani aliyesifika sana kwa kusimamia operesheni dhidi ya ufisadi, uhujumu uchumi, wahamiaji haramu, majambazi na wauza dawa za kulevya… Waziri Ummi asingekosa maadui. Amekuwa akipambana na watu wenye nguvu zote: kiuchumi, kiulinzi na kiukatili!” Tunu alisema.

“Dah! ishu nimekuwai kubwa mno kuliko tunavyodhani…” nilisema huku nikihisi akili yangu ikishindwa kufanya kazi sawa sawa. “Kwa vyovyote inagusa mtandao mpana mno ambao upo ndani na nje… namaanisha ndani ya nchi na nje ya nchi; na pia ndani ya serikali na nje ya serikali. Tena ni mtandao wenye nguvu zote kama unavyosema mkuu… si mtandao tu ni genge hatari zaidi ya Mafia.”

Kisha nilimweleza kuhusu mazungumzo yangu na Kamishina Koba hasa aliponiambia kuwa shaka yake ni kwamba kwa aina ya shambulio lilivyotokea inaonekana kabisa kuna mkono wa watu kutoka katika majeshi yetu.

Tunu alishusha pumzi na kunikodolea macho. Nikaongeza, “Kumbuka pia kuwa ni wiki tatu tu zimepita tangu Waziri Ummi atoke kumpoteza kijana wake wa pekee kwa kifo cha kutatanisha.”

“Dah! Sasa ndiyo watumie bomu kumuua Waziri?” Tunu aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.

“Huenda nia yao ilikuwa kujaribu kutupoteza maboya, badala ya kufikiria haya tunayoyajadili sasa tuelekeze macho yetu kwenye vikundi vya kigaidi kama Alshabab au Islamic State,” nilisema na hapo nikamwona Tunu akibetua kichwa chake kuafiki.

“Na kwa kiasi fulani wamefanikiwa maana makao makuu ya Idara Kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, na Jeshi la Wananchi wa Tanzania wameamua kuimarisha ulinzi na usalama katika majengo ya serikali, hospitali, masoko na sehemu maarufu za biashara, mahoteli ya kitalii, stesheni na vituo vya mabasi, shule maarufu hasa za mjini kati, kumbi za starehe, mitaa yenye mikusanyiko ya watu wengi, na madaraja muhimu…” Tunu alinidokeza. Kisha akaongeza.

“Na pia wameazimia kuanzisha operesheni maalumu ya kuwatambua wageni wote walioingia nchini ki halali na ki ujanja ujanja ikiwa sehemu ya uchunguzi wa kuwapata magaidi hao. Tena kazi hii inafanyika kwa kushirikiana na maofisa Uhamiji, Polisi, na kitengo maalumu cha Idara kinachoshughulika na udhibiti wa wageni katika mahoteli.”

Hata hivyo, tulikubaliana kuwa suala la wahamiaji haramu waliokuwa wamejazana nchini lilikuwa tishio kwa usalama wa nchi yetu kwani wangeweza kutumiwa. Na kama si wao basi wangekuwa ni Watanzania wenyewe waliofundishwa na kupewa msaada na wageni walioingia nchini kutoka ughaibuni.

Ni kweli wakati huo kulikuwa na idadi kubwa ya wahamiaji haramu kutoka Rwanda, Burundi, Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Ethiopia. Ongezeko la wageni hawa lilichangiwa kwa kiasi kikubwa na hali ya uhasama nchini Rwanda, na mapigano yasiyokwisha katika nchi za Kongo, Burundi, na Somalia. Wengi wa wahamiaji hawa waliingia nchini kwa njia za panya.

Si hivyo tu pia tulipaswa kuangalia kuhusu ongezeko kubwa la wafanyabiashara na wakazi haramu kutoka India, Pakistani, na nchi nyingine za Asia. Wahamiaji hawa waliingia nchini kwa viza halali kama watalii, au wageni wanaokuja kuwatembelea ndugu zao kwa muda mfupi. Hata hivyo baada ya viza zao kuisha muda wake hawakuondoka nchini bali walijichanganya na watu wa kwao kufanya biashara au kazi za kuajiriwa bila ya kufuata taratibu husika.

Kila tulichokijadili nilikumbuka kukiandika kwenye notebook yangu kwa ajili ya kumbukumbu pindi nikihitaji rejea ya mazungumzo yetu (reference). Sasa mjadala ulikuwa umechukua sura mpya kabisa. Mambo yalikuwa yanachanganya mno. Hatimaye tulikubaliana kuahirisha mjadala na kupanga muda mwingine mwafaka wa kujadiliana huku tukiyaangalia mambo hayo kwa kina zaidi. Pia tulikumbushana kwenda msibani baadaye jioni huenda huko tungepata mwanga zaidi.

“Ni matumaini yangu kuwa tutapata mwanga mzuri wa namna ya kulimaliza jambo hili mapema. Utanijulisha ukitaka kwenda huko na utanieleza kila utakachokuwa umekifikiria,” Tunu alihitimisha maelezo yake kisha akaitazama saa yake ya mkononi na aliporidhika na mwenendo wa majira yake alinitazama akaachia tabasamu.

Na hapo nikafahamu kuwa tukio lile lilikuwa limeashiria kuwa maongezi yetu mle ndani na Tunu yalikuwa yamefika tamati. Nilikuwa wa kwanza kusimama muda mfupi kabla Tunu hajafanya hivyo na hapo nikafunga mguu wangu na kupiga saluti ya heshima mbele ya mkuu wangu, akaitikia vyema na kunipa mkono wa kuagana.

“Kuwa mwangalifu sana, Jason, kwani yeyote aliyehusika na kitendo hiki haelekei kuwa ni mtu wa kawaida,” Tunu alinionya kwa sauti tulivu huku akinitazama machoni.

“Usijali, mkuu, nitakuwa mwangalifu na nitakufahamisha kila kitu pale itakapobidi,” nilimwambia huku nikiwa bado nimeushika mkono wake, tabasamu langu la kikazi lilikuwa limeumbika vizuri usoni mwangu.

“Nakutakia kazi njema yenye mafanikio,” Tunu aliongea kwa utulivu huku akinipigapiga begani kwa mkono wake na kisha akaachia tabasamu katika namna ya kunitia moyo. Nikatoka kwenda kuendelea na majukumu yangu.

* * *

Endelea kuzifuatilia harakati za Jason Sizya katika mkasa huu wa kusisimua...
 
Back
Top Bottom