327
Saa 12:35 jioni…
Gari la Luteni Lister liliniteremsha katika Kituo cha Mafuta cha
Lake kilichopo mkabala na
Malaika Beach Club, Kigamboni, dakika ishirini na tano kabla ya muda nilioahidiana na Sajenti Mambo kukutana hapo.
Sajenti Mambo alinipigia simu wakati tukitoka makaburi ya Kinondoni akanisisitiza kuwepo Malaika Beach Club, Kigamboni, saa moja kamili jioni, nami sikuwa tayari kufuata matakwa yake ya kufika kwa muda uliopangwa wa saa moja jioni kana kwamba nilikuwa nakwenda kwenye ibada kanisani. Kati ya mambo ambayo niliyathamini sana katika maisha yangu ya kipelelezi ni tabia ya kutomwamini mtu yeyote na kumshuku kila mtu, hata marehemu.
Mara zote nilijikumbusha kuwa kupanga muda wa kukutana ni kati ya makosa makubwa kwani unaweza kuwa unashirikishwa kupanga muda wa kifo chako mwenyewe. Hivyo, ni vizuri kukifumania kifo wakati kikijiandaa kukuchukua au kukichelewesha kidogo.
Baada ya kushuka toka kwenye gari la Luteni Lister nikaanza kupiga hatua zangu kwa utulivu nikikatisha barabara na kuelekea ng’ambo ya pili ya barabara ilipo Club ya Malaika. Wakati nikitembea na kukatisha katika ile barabara niliishusha vyema kofia ya pama niliyovaa kuufunika uso wangu huku macho yangu yakiwa makini zaidi kuzichunguza sura za watu waliokuwa eneo lile na mijongeo yao.
Mwili wangu ulikuwa bado mchovu mno kutokana na pilika pilika na kukosa mapumziko kwa siku kadhaa tangu lilipotokea tukio la kigaidi kwenye jengo la Alpha Mall, katika eneo la Makumbusho.
Kisha nilianza kukatiza kwenye viunga vya maegesho ya magari vya Malaika Beach Club ili kwenda kwenye mlango wa mbele wa Club. Hata hivyo wakati nikitembea kuelekea kwenye Club ile nikawa nikiyatembeza macho yangu kwa makini kupeleleza mandhari ya eneo lile ili kuona kama nilikuwa nimewekewa mtego wowote.
Niliona magari machache yaliyokuwa yameegeshwa kwenye eneo la maegesho ya magari la Club ile na nilipoyachunguza vizuri magari yale nikagundua kuwa yalikuwa ya watu wenye kipato cha kueleweka, ambao kwa vyovyote walikuwa mle ndani ya Club wakijipatia vinywaji au starehe yoyote iliyokuwa ikipatikana mle.
Kulikuwa na watu wawili watatu waliokuwa wamesimama pale nje ya Club ile wakiwa na mazungumzo. Watu wale waligeuka kidogo kunitazama wakati nilipokuwa nikiwapita kuelekea kwenye mlango wa kuingilia ndani ya ile Club, sikuonesha kuwatilia maanani lakini nilikuwa makini sana kunusa hatari.
Niliingia ndani ya Club na hapo nikajikuta nikikabiliana na macho ya watu waliokuwa wameketi kwa utulivu mle ndani wakiendelea na starehe zao. Walikuwa watu wachache. Niliangaza macho yangu huku na huko katika namna ya kutafuta sehemu nzuri ya kukaa na wakati nikiyatembeza macho yangu nikawa nikiwachunguza pia watu waliokuwa mle ndani. Kwa haraka nikagundua kuwa wengi wao walikuwa Wahindi.
Kisha nilipiga hatua taratibu kutafuta meza na kwenda kujitenga mbali na watu wengine, nikiketi kwenye meza ya peke yangu iliyokuwa pembeni kabisa ya ule ukumbi, karibu kabisa na mawimbi ya bahari, nikifaidi upepo mwanana wa baharini ambao ulikuwa ukinipuliza mwilini, lakini pia ilikuwa sehemu iliyoniwezesha kuona vizuri pande zote, kule baharini na hata mbele ya Club ile ambako magari yalikuwa yakiingilia. Niliketi huku macho yangu yakiwa yanachambua mazingira.
Runinga pana iliyokuwa imetundikwa ukutani mle ukumbini ilikuwa imejikita katika kurusha matangazo ya kandanda la Ulaya. Sikuwa mfuatiliaji mzuri wa mchezo wa kandanda, hivyo wala sikujua ni timu zipi zilizokuwa zinacheza.
Kisha nikamwita mhudumu mmoja na kumwagiza aniletee mvinyo aina ya
Dompo na baada ya dakika mbili mvinyo ukaletwa, nikaanza kunywa taratibu huku nikiusubiria muda mwafaka ambao Sajenti Mambo angefika. Nilikuwa na shauku kubwa ya kumsikia Sajenti Mambo akinieleza kile alichokifahamu huku nikitaraji kuwa mazungumzo yetu yangenipa mwanga zaidi katika kulitatua suala zito lililokuwa likinisumbua. Japokuwa nilijionya kutomwamini mtu yeyote lakini kwa bahati mbaya, sikuwa na jinsi.
Tangu lilipotokea lile tukio la bomu kwenye jengo la Alpha Mall nilijikuta kila hatua niliyoipiga kwenye upelelezi wangu ilifanya kazi ya uchunguzi iwe ngumu na ya hatari zaidi. Hivyo, kuna muda nikajikuta nikiwa mhitaji zaidi wa kichwa chenye kufikiri kwa upeo mpana zaidi katika masuala ya aina hii. Tayari nilishakuwa na vichwa kama Luteni Lister na Pamela, lakini sasa nilihitaji kichwa ambacho kilikuwemo ndani ya mtandao huo hatari na kilijua mambo mengi zaidi yaliyohusu mtandao huu. Kwa mtazamo wangu kichwa cha Sajenti Mambo kilikuwa mwafaka zaidi.
Luteni Lister baada ya kuliegesha gari lake mbali kidogo na eneo lile la Club alirudi na kutafuta meza iliyokuwa mbali na meza yangu, akaketi na kuagiza mvinyo aina ya Dodoma Wine, akiwa pale kwa ajili ya kuhakikisha ninakuwa salama.
Niliendelea kunywa mvinyo wangu taratibu huku nikitafakari hili na lile katika namna ya kubashiri ni kipi alichotaka kuniambia Sajenti Mambo. Nilianza kuyaona mafanikio ya upelelezi wetu kupitia Sajenti Mambo, nikashusha pumzi na kuitazama saa yangu ya mkononi, nikagundua kuwa bado nilisaliwa na dakika tano kabla ya muda tuliokubaliana. Nikamimina mvinyo katika bilauri na kuendelea kunywa taratibu huku nikiyasafirisha macho yangu kutazama nje ya ukumbi ule.
Ni muda huo huo wakati nikitazama kule nje, macho yangu yalipoliona gari aina ya Lexus la rangi ya fedha lililokuwa na vioo vyeusi visivyoonesha ndani likifika pale Club na kuegeshwa kwenye sehemu maalumu ya maegesho ya magari. Mara moja nikalikumbuka gari lile. Lilikuwa ni lile gari nililoliona nyumbani kwangu usiku wa siku iliyokuwa imetangulia. Gari ambalo Sajenti Mambo na Daniella walilitumia kuniletea ujumbe na kumwachia mlinzi wa nyumba yangu.
Sasa macho yangu yakawa makini zaidi kulitazama lile gari ili nione nani angeteremka, na wakati huo huo nikaliona gari lingine aina ya Nissan Patrol jeusi lenye vioo vyeusi visivyomruhusu mtu kuona waliomo ndani likiingia pale Club na kuegeshwa mbali kidogo na lile gari aina ya Lexus la rangi ya fedha.
Nikiwa makini kuyatazama magari yote mawili mara nikamwona mwanamume mmoja akishuka toka kwenye gari lile aina ya Lexus la rangi ya fedha akiwa ameshikilia
briefcase ndogo mkononi. Ingawa macho yake alikuwa ameyafunika kwa miwani myeusi sikushindwa kumtambua mara moja. Alikuwa Sajenti Albert Mambo wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay.
Aliposhuka alitazama huku na kule, huenda alikuwa anahakikisha usalama wa eneo lile, kisha akashika
briefcase yake vizuri mkononi na kuanza kutembea kwa mwendo wa haraka haraka kuelekea kwenye lango la kuingilia Malaika Beach Club.
Ni wakati huo huo kilipotokea kitu kilichonishtua sana, kwani ghafla nilimshuhudia Sajenti Mambo akisombwa hewani na kisha kutupwa chini kama gunia wakati akiwa hatua chache tu kufika mbele ya lango la kuingilia Club. Na hapo nikawashuhudia watu wachache waliokuwa pale nje ya Club na wengine walioliona tukio lile wakishikwa na taharuki, hata hivyo, mimi sikuwa miongoni mwao na badala yake fikra zangu zilijikita katika kuchukua tahadhari.
Endelea...