Simulizi: Harakati za maisha

nukta
 
SEHEMU YA THELATHINI NA SABA

Siku inayofuata baada ya kupunguza baadhi ya kazi zangu ofisini , niliamua kupiga simu kwa ndugu yeyote wa Jastini ili tupange namna ya kumsaidia,akili ikaniambia kumpigia simu mkewe ni kujitengenezea mazingira mabaya hasa ukizingatia jamaa yupo jela.

Nikakumbuka nina namba ya mtu ambaye nilikuwa nakwaruzana naye muda mwingi ambaye alidai ni dada yake ambaye hatujawahi kuonana ,kiufupi simfahamu na huenda hata yeye ananifahamu.
Nikampigia huku moyo ukinienda mbio maana nilijua natonesha vidonda vya watu na pia yule mdada sijui mmama hakuwa na lugha nzuri sana anaonekana ni mkali mkali,lakini nikalivaa tu lile jambo nikaweka simu sikioni.

Hello nani mwenzangu!
aliuliza upande wa pili mara baada ya kusalimiana.

Naitwa Daniel,mwezi uliopita ulinipigia kwaajili ya masuala ya ndugu yako Jastini.nilijitambulisha.

Oooh sawa nimekukumbuka,
Unasemaje? au unataka nini ?
aliuliza.

Nimepata taarifa za rafiki yangu Jastini kuwa yule gerezani,kifupi nimesikitika sana ila nina wazo fulani dada yangu.niliongea kwa tahadhari huku nikimsikilizia kwa umakini.

(Huku akitoa kicheko hafifu)
Mdogo wangu yupo jela ndiyo,lakini nikushangae wewe,kwani unataka nini kwetu?
Kwanza ulisema huhusiki na masuala ya Jastini ukidai tukuache na tulikuacha kweli licha ya Jastini kushindwa kukuhusisha moja kwa moja lakini ndugu tunatambua kuwa huenda mna kiapo mlichojipangia kuwa kama mmoja akikamatwa basi msitajane,ni kweli hakukutaja licha ya kupewa kibano kikali ataje wahusika na hakutaka kutaja yeyote.sasa ni biashara gani isiyo na washirika?
Ni kwamba ndugu yangu ni mjinga sana.aliweka kituo.

Samahani mama tunaweza kuonana tuongee kirefu ? niliuliza .

Inawezekana!
Lakini kwani unataka nini kwetu wewe,maana nahofia usalama wangu.aliongea akionesha ni mwenye wasiwasi kidogo.

Kuwa na amani dada ,mimi sina nia mbaya ni kwamba nahitaji tujadili hatima ya rafiki yangu Jastini kuwa usiogope.

Sawa mimi nipo maeneo ya mahakama ya (akiitaja mahakama ilipo)
Najaribu kuonana na watu fulani tujue namna ya kushughulikia haya masuala.alijibu.

Sasa dada kama upo hapo nadhani ni jambo jema kwanini tusionane tupange kabisa,eeeh ndani ya dakika chache nitakuwa hapo . niliongea kwa pupa .

Basi subiri nimalize mambo yangu kisha nitakupigia simu maana kuna mtu namsubiri hapa niongee naye . aliweka kituo.

Mida ya saa saba mchana tulionana yule mama ambaye kiukweli alikuwa ni mtu mzima tofauti na nilivyodhani huku akiwa na wenzake watatu , wanawake watatu akiwemo na yeye na mwanaume mmoja.walikuwa makini sana huku wakinitazama kwa hofu huenda walijua mimi si mtu mwema.

Nilijitambulisha kwa mara nyingine huku tukiingia kwenye mgahawa mmoja hivi,lakini hata mimi nilikuwa makini nao maana ni kama tunawindana.

Naitwa Lydia kama nilivyokuelekeza kwa siku ya kwanza,huyu ni mtoto wangu ,akimuonesha yule mwanaume ambaye ni kama umri tulilingana tu.na hawa ni ndugu wa mke wa jastini.alinitambulisha kwa wale watu huku akiniangalia pasi na kupepesa macho,sijui alijua labda nina manati nitamdhuru!!

Mimi kama nilivyowaeleza mwanzo ni kwamba sihusiki na habari za Jastini na mnavyosema hakunitaka huko kituoni licha ya kupewa mateso ,ni kweli kwakuwa asingeongea uongo kwakuwa sihusiki ila ni kwamba ni rafiki wa karibu,siyo kikazi ama kibiashara bali maisha ndivyo yalivyo.niliongea huku wakionesha wanakubali.

Kwanza bro mimi nikushukuru sana,kwa kuweza kutaka kushirikiana na sisi kumnusuru Jastini ambaye mimi ni mjomba wangu,na tangu mwanzo ,mama yangu na ndugu wote niliwaeleza kuwa wasihangaike kutafuta nani ama nani ,kifupi uncle wangu alishakuwa kwenye matatizo hivyo hakukuwa na haja ya kutaka kuwaumiza na watu wengine tusiokuwa na ushahidi nao.

Lakini kwa kufupisha maelezo ni kwamba Jastini anakabiliwa na kesi kubwa ya kufanya biashara ya nyara za serikali (madini)bila. Vibali huku akitambua kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.hivyo yupo jela kwa shitaka hilo na si vinginevyo.maana wale wadai wake walishamsamehe.alifafanua yule niliyetambulishwa kuwa ni mtoto wa dada yake Jastini.

Kwanza nilipenda maelezo yake lakini pia huenda tabia ya Jastini alikuwa anaijua siku nyingi hivyo hakushtuka hata kusikia mjomba wake yupo lockup . Baada ya hapo nilimuita tuongelee kwenye gari nikiwaacha wale wanawake wanakula.

Kwanza nikushukuru kwa kunifahamisha vizuri maana mama yako alikuwa anaongea kwa vitisho sana kiasi cha kumuogopa .niliongea huku nikijichangamsha.

Sikia bro,mimi Jastini namjua vizuri sana,mimi mwenyewe kashachukua hela zangu nyingi sana huku akijaribu kunishirikisha kwenye biashara zake lakini nikawa nagoma,pia si mimi tu wapo wengi ambao kawatapeli ,huku wengine wakisamehe na wenye madeni makubwa makubwa ndiyo hao wanakuja.hivyo bro usiwe na shaka na mimi ndiye niliyemtuliza mama kuwa asikusumbue kwani nilijua moja kwa moja utakuwa huhusiki maana kwanza mjomba wangu kwenye biashara hiyo yupo kitambo sana,na kilichomfanya arudi nyuma kimaisha ni baada ya kutamani kununua kuliko kuwa mchimbaji.aliongea yule jamaa huku nikifurahi angalau nitapumua maana Dah mwezi mzima hata bia sinywi,zitashukaje na nina mawazo.

Tulibadilishana contacts zetu huku nikiona sasa yule ndiye mtu sahihi ambaye nitaongea naye jambo likaeleweka kuliko wanawake.

Naitwa Pastor Lewis unaweza kusave hivyo ndiyo utanikumbuka vizuri,pia karibu sana kanisani kwetu.aliongea huku akitabasamu.

Kwanza nilimuangaliaaa kisha nikamuuliza.

Kwani wewe ni mchungaji,maana nilikuwa nawaza tukitoka hapa upige hata mbili tatu japo mimi bado niko kazini nisingekunywa.niliongea nikiwa namshangaa maana hakufanania na uchungaji,

Ndugu yangu hakuna jipya chini ya jua ,sisi binadamu ni wakosefu na ipo njia impendezayo mwenyezi Mungu ambayo ukiifuata hutatetereka.hata mjomba wangu nilikuwa namwambia mara kwa mara lakini labda aliniona mpuuzi.kumbuka yanayofanyika yote leo yalishafanyika,na kwanza nikushukuru kwa hicho ulichotaka kunipa ,na nikushauri tu kuwa kwani ukinywa hizo bia bro unapata faida gani? sisemi unakosea ila waweza kunipa faida hata mbili tatu ili nijue.aliweka kituo.

Hapana ni mazoea tu hivi vitu vina faida basi,ni kwamba tulijikuta tunashawishika tu kuvitumia.niliongea kwa aibu fulani hivi maana kutangaza ulevi mbele ya hawa wachungaji huwa sipendi.

Daniel,una jina zuri la nabii mkubwa sana kwa mujibu wa biblia ,okoka sasa hujachelewa ,ukisoma kitabu cha Muinjili Marko,anatuonesha ni jinsi gani tunapaswa tutubu na kuiamini Injili, wakati ni sasa Danieli.
aliweka kituo.kisha nikaenda kuwaaga wale akina mama ambao imani ilirudi tuliagana kwa furaha kisha nikarudi ofisini huku nikiwaza vitu vingi ila tayari nikushukuru kuona wameamini kuwa sihusiki na msala wa ndugu yao.

Nilirudi nyumbani mapema ,kumbuka mwezi mzima na tangu nitoke kule kwa mganga sikuwahi kugusa pombe,kwanza bado sikuwa na imani ya moja kwa moja kuwa matatizo yangu yameisha nilijua naweza kukamatwa muda wowote na maaskari hivyo nikajiweka mbali na vyombo kwa muda ili nijue mbivu na mbichi kwanza.

Nikiwa barabarani katikati ya foleni kuna jamaa alikuwa anauza vitabu vingi sana,na mimi ni mpenzi wa vitabu nikaamua kumuita huku nikichukua kitabu fulani kinachohusu masuala ya uchumi kikiandikwa na mhadhiri fulani wa moja ya chuo kikuu bora Duniani Havard ,nikasema hiki kitanisaidia kuzugazuga ili nisiwe natoka ndani,kwanza mchungaji Lewis kaniongezea kitu pombe siyo ya kuendekeza.

Jifunze,
Elimika
Burudika.

Inaendelea......................
 
SEHEMU YA THELATHINI NA NANE

Nilipekua pekua kurasa za kitabu kile huku nilivutiwa sana na yaliyomo mule nikizidi kukumbuka na kujifunza vitu vingi sana.

Mke wangu naye alirudi toka kwenye mihangaiko yake huku akionekana ni mwenye furaha sana.

Kiukweli mume wangu umebadilika sana kwanza umependeza sana na unavutia,ni wiki ya tatu unakaribia mwezi sasa sioni dalili ya kuwa ulikunywa pombe halafu unawahi sana kurudi,yaani hadi wivu unanijia kwa sasa sitaki hata utoke nje nahisi wanawake wengine watakuchukua.aliongea huku akitabasamu.

Wivu tena ,unakuwaje na wivu saizi badala ya unionee wivu nikiwa sipo au nikichelewa kurudi.niliuliza.

Kuna wivu kwenye maisha ya kawaida kwa mfano mtu akiwa na mafanikio kukuzidi basi unaweza kuwa na wivu kwa kutamani ufike alipo.au hata kama unajua hutokaa ufanane naye lakini hakuna namna .

Halafu kuna wivu wa mapenzi hapa kuna namna nyingi ,yaani hata kama upo kitandani lazima nione kama naibiwa lazima nipapase nijiridhishe.
Na wivu huu hata unipe bahari nzima na meli zote bila uwepo wako ni kazi bure,na huu ni wivu ambao hata anayekuonea wivu naye hajijui.

Halafu kuna wivu kwakuwa unacho na huu ndiyo umetamalaki Duniani kote,mtu anawaza rasilimali zako kupotea anakuonea wivu kwasababu,utafuja pesa na kushindwa kutimiza majukumu yako ,kuhusu wewe nilikuwa sikuonei wivu kwakuwa ulishanitoka kwenye nafsi yangu,wewe mtu gani ukirudi umelewa hatuna muda wa kupiga stori ,hakuna mapenzi,sawa hata kama familia yako unaijali lakini uwepo wako kama hivi mimi ndiyo napenda .tunapata muda wa kuongea kama hivi na nimshukuru Mungu nadhani maombi yangu yamejibiwa.aliweka kituo mke wangu huku siku hiyo utani wa hapa na pale ukitawala mithili ya ndoa mpya yenye siku tatu tangu ifungwe.

Ilikuwa siku ya kipekee yenye furaha ambayo nilijua imetokea na ni ngumu kujirudia kwakuwa hizi kuta za nyumba zetu zingekuwa zinaongea basi zina siri nyingi sana inafikia mtu unajilaumu kwanini nilioa .kinachokufanya uikumbatie ndoa ni familia iliyotengenezwa pamoja na umri,basi unabaki ukivumilia shida.siri ya kata aijuaye kata.

Siku inayofuata nikiwa ofisini kwangu nilipunguza kazi zangu kisha nikachukua kitabu changu nilichonunua jana ili nikipitie pitie ni utaratibu wangu wa siku nyingi vitabu huwa nasomea ofisini kipindi hicho ofisini. hakujafungwa kamera
(Technology sometimes ina madhara)

Mlango uligongwa, huku nikidhani ni Mfanyakazi wa mule ndani nikamwambia asukume ,aliingia jamaa mmoja ni mfanyakazi mwenzangu wa kitambo sana huku akiwa yupo kwenye kampuni ya mtu binafsi ni mtu alichangia sana mimi kufanikiwa,
Ni mtu aliyenizidi vitu vingi ,umri,
Maendeleo,hata tunavyomiliki sikumkaribia hata kidogo.

Vipi mdogo wangu Daniel naona umeyapatia maisha vilivyo,
Hadi unang'aa mtoto wa kiume na hicho hapo nini ,kitabu hee unajisomea home boy ,hebu nipe kwanza (huku nikimpa)

Alikigeuza geuza huku akitabasamu na kukifungua huku akizidi kucheka.

Daniel bwana ,naona kinazungumzia kuhusu kukuza uchumi eeeeh mara sijui Wealth Grow mara sijui increase value sijui nini yaani mambo kibaoooo.

Daniiii bado unaamini mafanikio kwa kusoma hizi propaganda,maisha hafundishwi mtu wala hakuna kanuni .
Ni jambo moja tu heshimu na kuthamini unachokipata huku ukitumia kidogo zaidi ya ulichoingiza full stop .huwezi kufanikiwa kwa kusoma vitabu ingekuwa hivyo asilimia nyingi ya watu wangekuwa matajiri home boy,

Halafu tufanye ni kweli ni mpenzi wa kusoma vitabu ,mbona vinapatikana mtandaoni ,una computer yako,una simu ,bado unatumia mifumo analogia hivi kwanza ulinunua shilingi ngapi? aliuliza.

Elfu ishirini, nilidanganya, ukweli muuzaji alianza elfu kumi then nikanunua kwa elfu saba tu.

Ona Sasa yaani kitabu tu unanunua kumi kumi mbili, na hapo hujalewa maana nakujua Dani usipotumia laki mbili kwa siku kwa matumizi ya kipuuzi bado hujafanikisha malengo yako.

Acha hizo Shabani, kwa maisha gani nitumie pesa yote hiyo kwa mambo yasiyofaa kweli!! kwa kipato gani haswa usije sababisha mtu akavamiwa bure . Niliongea huku nikichukua kitabu changu .

Huwezi jua Dani ni pesa ngapi umetumia , hebu fikiria kwa mfano umeenda bar ya kawaida tu acha huko kwenye gharama , ukanywa bia za elfu ishirini peke yako, ukanunulia na watu wengine pia, hapohapo hujachukua mwanamke (demu) naye atataka hela hapo hapo hela ya Lodge haaaa Dani just imagine home boy mbona pesa inakata hiyo fasta na hubaki na kitu na unavyopenda starehe Dani ndiyo maana huna hela. alizidi kunizodoa huku nikimwangalia tu.

Tatizo Shabani unayaishi maisha kwa sheria na kanuni ngumu sana maisha ni hayahaya hakuna sababu ya kukufanya usijitese sana , hizo hesabu ulizipiga siyo za Kila siku , siku moja moja jipongeze haupo jela shukuru MUNGU,
Haupo hospital mshukuru MUNGU pia. Sasa kwanini ujibanebane?
Mimi siwezi kaka, siwezi aslani , umekuwa bahili yaani kufanya kazi na waarabu wamekufanya uwe bahili sijui kwanini, pombe hunywi, kuswali huswali Sasa sijui upo upande gani.
Nilimjibu huku akitikisa kichwa kwa kunionea huruma eti.

Mpaka Sasa hivi una nyumba ngapi Dani. Aliuliza.

Nyumba za Nini kaka kwani nalala nje? Wewe nakujua ni chizi wa nyumba Tena ulivyo fala, kwa mfano vile vibanda vyako vitatu vya mkoani kama ungeamua zile pesa ukajenga nyumba moja nzuri kubwa ukaifinish vizuri huoni kama ungekuwa mjanja , Sasa zile nazo nyumba kaka , hebu kwanza ongea kilichokuleta. niliongea huku tukipeana tano tukicheka ni mtu ambaye ukitukuta ni kama tunagombana kumbe ndiyo ongea yetu.

Tuache masikhara kaka mimi Nina dili Kuna gari nimekuja nayo ipo hapo nje naiuza . Aliongea huku akiweka uso serious kuonesha ni ishu ya kweli .

Dah chombo gani hicho unasukuma . Niliuliza.

Ipo nje twende ukaione , tusiandikie mate kaka

Tulitoka nje kabisa ya uzio nikaiona brevis mpya ikionekana haijatumika sana , hata ndani Kila kitu kulikuwa freshi , nikaitest huku Kila kitu kikifanya kazi ipasavyo.

Dah Sheby gari umepata wapi hii na kwanini uuze bro?
Niliuliza.

Oyaa wewe tafuta mteja Mimi naenda mkoani nikirudi utanipa pesa yangu .uza bei yoyote lakini niletee pesa yangu
huku akinitajia kile kiasi ambacho inauzwa ilikuwa ni bei ya kawaida kabisa .nikaona huenda pesa ya kulewea nitapata

Au kama wewe unachukua fresh maana wewe Dani huna gari unatembelea mkweche tu Sasa gari zako nazo gari ulizinunua mafungu kwenye mnada nazo gari ,na sidhani kama Zina kiyoyozi, chukua Chuma hiki kikurahisishie mambo yako wewe.

Hebu nipe documents kwanza maana hii inafaa kwa kuhonga. Kuna mademu wanakuwaga na vipini kwenye ulimi, wakiku tight kwenye lile eneo unaweza kutoa gari kwa muda huo hebu lete kadi yake . Niliongea kiutani huku tukicheka .

Kadi tu ipo chukua kwenye begi hilo hebu angalia Kila kitu kuwa na amani hili ni gari langu la jasho langu halafu anatokea Malaya mmoja anajaribu kunidhulumu, Tena na akome. aliongea kwa kujiamini Shabani huku nikigundua Kuna jambo haliko sawa pia kadi ya gari ilikuwa na jina la kike Tena nikigundua ni mkewe . Nikazidi kupata mashaka.

Bro mbona jina ni la wife Mimi nikajua ni lako? niliongea kwa sauti ya chini huku nikimtazama.

Wewe Dani vipi wewe mshamba Nini, Mali za mke wangu ni zangu nilimuoa akiwa Hana kitu Malaya yule halafu namuweka asimamie miradi yangu mwisho wa siku kwenye account sijaona hela ya maana huku akijizawadia gari. Sasa nimemwambia achague moja talaka au abaki na gari, kanipiga hela ndefu sana na hii gari acha niuze niambulie yaani wanawake si watu wa kuwaamini. aliongea huku akizidi kuwa mkali nikagundua hayupo sawa.

Kwa pesa ambayo ningepata kwenye udalali wa ile gari ilikuwa safi ningepata ya kula nyama choma lakini nikagundua mbona kama chombo kina matatizo.lakini watajuana wenyewe chombo naiuza hii

Kumbuka Daniel Nina tamaa sana na hizi hela za bia huwa sisikii la muadhini Wala mnadi swala. Sasa itakuwaje.

Jifunze,
Elimika,
Burudika.

Itaendelea................
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…