Simulizi: Harakati za maisha

Simulizi: Harakati za maisha

SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA

Tukiwa njiani kuelekea sehemu ambayo sikujua kwani hawakusema,
Simu yangu ndogo iliita, ni simu ambayo inahusika zaidi na ndugu tu.
Kuangalia anayepiga ni mke wangu. Lakini kabla sijapokea niliporwa ile simu na afande huku akiangalia jina la mtu anayepiga Kisha akanirudishia ikiwa imekata. Baada ya kuita kwa mara ya pili, Nilipokea.

Vipi mume wangu kwani imekuwaje tena mbona sielewi, nimesikia unaitwa jambazi? Halafu mnaelekea wapi saizi? Tafadhali naomba nijue ili nije nijue naanzia wapi. aliongea mke wangu huku nikiwa sijamjibu chochote,kisha afande yule akapokonya simu yangu na kukaa nayo.

Hakuna tena kuongea na simu humu acha ujinga usijione kama nani, halafu na wewe Black (akimaanisha Jastini)
hebu lete simu yako na wewe, nyie mpo chini ya ulinzi, acheni u****
aliongea kwa jazba yule afande huku akitukana.
Lakini Jastini hakuwa na simu jambo ambalo hata Mimi nilishangaa, kwanini asiwe na simu?
muda ule mbona niliwasiliana naye?

Oyaa afande Fox eeh, huyu boya hana simu eti, inawezekanaje?
Hebu simamisha gari. afande ambaye hakuwa na silaha aliamrisha yule dereva niliyesikia akiitwa Fox akimtaka asimame.

Hilo ndiyo tatizo lako afande punguza presha, kama hana simu atatuonesha ilipo ngoja tufike Central kwanza, hiyo ni michezo ya kitoto anafanya na kama Kuna mahali kaificha sisi tutajua tu . Yaani nilivyo na hamu naye huyu boya.
aliongea yule dereva anayeendesha gari akiwa anamjibu afande mwenzie.

Baada ya muda fulani tulifika kituo cha kati huku pilika zikiwa nyingi muda ule, askari wote tuliokuja nao walishuka huku tukipokelewa na askari wengine kabisa wenye maneno ya kejeli.

Hebu muone huyu brazamen eti anaangalia saa, au akili yako unajua unarudi eeh,hapa ninyi ni wateja wetu,ukiwa na hotel lazima utake watu waje walale, wale,si ndiyo eeh?
Huko kwenye ma bar wamiliki wanataka wapate faida mara mia zaidi ya walivyowekeza.yaani wateja wajae,so na hizi Selo lazima wateja wajae,eeeh .aliongea kwa kejeli afande fulani mwenye umri uliosogea huku akiwa kavaa miwani yenye kamba ili isianguke.

Dakika zaidi ya kumi tulikuwa pale Kaunda lengo wachukue maelezo na taarifa fulani toka kwetu,yaani mimi na Jax lakini ikawa ni foleni hawa wamekuja kudhamini ndugu zao hawa ni wahalifu wapya wanaletwa yaani fujo zilikuwa nyingi.hatimaye tukapewa nafasi huku moyo ukiniuma sana kwani nilikuwa nafanyiwa uonevu mkubwa sana kiasi cha kuanza kumchukia Jastini lakini pia niliwaza simu yangu maana yule afande alishuka na sikumuona tena.

Baada ya afande kuchukua taarifa akataka kutuweka mahabusu lakini akaambiwa na mwenzake kwamba twende kwenye chumba cha mahojiano moja kwa moja .halafu baada ya hapo tutarudi mahabusu.

Tuliingia kule tukakuta kuna chumba kidogo chenye vifaa vikuukuu , virungu, pasi na vitu vingine ambavyo wanavijua wao.

Karibuni sana jamani,karibu sana bwana Daniel,alinitaja jina yule afande huku nikishtuka lakini nikaona labda ananifahamu,alikuwa ni kijana fulani mdogo tu mwenye mwili mwembamba ambaye mabegani alikuwa si haba,huku nikimpongeza kwa umri wake na vile vyeo hakika alishajipata

Hey bro unaitwa Jastiniiiiii ...... akimalizia kwa kutaja full name,
Mbona unalidhalilisha kabila letu bro eeeh,sisi sifa yetu kwenye hii nchi ni kujazana kwenye majeshi tu na siyo kuwa na sifa kama zako vipi kaka?
Hebu huyu mpelekeni Selo halafu huyu niongee naye kwanza.

Mimi nilitoka nikiwa na askari mmoja ambaye alikuwa mkalimkali sana,lakini badala ya kupelekwa Selo nikaambiwa nirudi mahali ilipo Kaunda,hapa nilikuta watu wameongezeka,huku wakiwemo wanaonijua huku wakishangaa why niwekwe chini ya ulinzi.

Hata baadhi ya askari ninaowajua wale ambao wanawatoa mahabusu kutoka vituo vidogo na kuwaleta pale nao walishangaa kuniona pale huku nikiona aibu na uoga kwani taarifa zangu zikifika ofisini ni neno lingine,watu wenyewe wanasubiri ujikanyage tu halafu uone nafasi yako itakavyojazwa mapema,wapo waliosoma taaluma yangu vyuo vya nchi za nje na hawana kazi au nafasi kama yangu wengi wanasukumiwa site huko,niliwaza huku mapigo ya moyo yakiongezeka.

Dani ndugu yangu vipi tena,ni leo tu nilikuona kwenye gazeti,nikasema alhamdullilah nitampigia simu rafiki yangu ili tutete jambo cha ajabu napiga simu hupokei na mimi hapa kuna jamaa yangu ni dereva nimekuja kumuwekea dhamana siunajua tena ile gari yangu kirikuu yangu huwa napatia hela ya mboga sasa nasikia jamaa aligonga mtu mbaya zaidi ni kwenye zebra sasa ndiyo nafanya marekebisho.japo wamenikamua vibaya ila nashukuru nimefanikiwa , kwani una kosa gani Daniel?
aliniuliza yule jamaa ,lakini kabla sijamjibu yule jamaa.

Nilimuona Jastini akija akiwa na pingu kabisa mikono nyuma,nikaona mambo yameshakuwa mabaya , nikamsaidia kumvua viatu na mkanda kisha wakaondoka naye kwenda zilipo Selo,kisha na mimi nikarudi kwenye kile chumba cha mahojiano huku askari wakiwa wameongezeka nikaanza kupigwa spana.

Tuache siku zote tuongee ya leo,

Daniel, unaweza kutueleza ratiba zako za leo tangu ulivyoamka zilikuwaje, aliniuliza yule afande mdogo mwenye tabasamu muda wote

Nikajieleza ilivyokuwa na namna nilivyorudi kwa kuomba ruhusa ili nije nikutane na Jastini.

Wewe jana ukienda kituo X kwaajili ya kutoa taarifa za kutishiwa na Jastini,iweje utake kumalizana naye wakati taarifa ipo kituoni na ni mtu alitishia maisha yako,kirahisi tu ukataka kupatana naye kwanini?

Ni kwasababu alinitishia akinituhumu kuwa nimemtorosha mkewe,ila leo hii baada ya kusikia yupo nyumbani akiwa na mkewe,nikaona ngoja nikamsikilize.
Nilimjibu

Hivi unawezaje kuwa mwenye imani kiasi hicho huoni kama unajiweka kwenye hatari,kwanini usingetoa taarifa polisi ili yeye aeleze kampataje mkewe mbele ya polisi ambako wewe ulishitaki?
aliuliza

Nadhani hapa afande nilikosea ,ni mazoea yangu mimi na Jastini nilijua hasira zake zitakuwa zimepungua haswa baada ya kumpata mkewe.kiufupi hangenifanya kitu.
Nilijibu.

Aisseee sawa,wewe ni mfanyabiashara wa madini?
aliuliza.

Hapana afande mimi ni mfanyakazi tu,na nina biashara ya (nikitaja jina)

Halafu wewe upo humble sana na mimi nataka niwe humble kama wewe halafu wewe ni Braza wangu kwa muonekano tu,sitaki nikukosee heshima,mbona mwenzio hapa kasema wewe unafanya biashara ya madini tena yote,si lazima uwe na mabilioni hizo hizo hela za mafuta unazopata si faida ya unachofanya?
Sasa kwa kunidanganya unanikosea.
aliongea yule afande kwa sauti ya juu kidogo akinitisha

Ningependa yeye huyo aliyekwambia kuwa nafanya biashara hiyo athibitishe kwasababu hawezi kunisingizia,ataje wapi nanunua na wapi nauzia,si unasema kakuambia huyu Jastini?hayupo mbali aje aseme nimsikie.
niliongea kwa kujikaza kidogo.

Yule afande aliniangalia kwa muda huku akitabasamu, yule askari mwenye silaha yupo pembeni akiwa anaperuzi tu kwenye simu yake huku akicheka kwa vile alivyokuwa anaviona

Hebu washa hiyo taa wewe mwenzangu ni mrefu braza.aliniambia huku nikishangaa taa ipo karibu yake niiwashe mimi halafu hakuna urefu wowote hata yeye angewasha tu.

Ila Daniel wewe sijui upoje kwani kufanya biashara ya madini ni kosa?
Kwani ni madawa ya kulevya hayo hadi ukatae kiasi hicho,tena usichojua ni kwamba kuna matajiri wa Ruby wamekuja hapahapa nchini wanatoka Sri lanka,unajua wananunua bei gani gram moja?haya wewe jicheleweshe tu utashindwa kupata connection.aliongea kwa upole safari hii huku akitengeneza tabasamu rafiki.

Ukweli afande unaongelea jambo nisilojua na sijui linafananaje ungesema mbao sawa ni biashara naifanya na nina leseni na vibali vyote lakini sijui kitu kuhusu madini.niliongea bila wasiwasi.

Sawa ,afande nenda naye huyu kwa afande Fox kwanza alisema nikimalizana naye na yeye ana maswali anataka kumuuliza.Aliongea huku nikizodolewa na baadhi ya maaskari tuliopishana nao kwenye zile korido hata sikujua kwanini wanafanya vile.

Enheee Daniel nilikuwa nakusubiri maana leo shift yangu nimeanzia kwako nafika tu hapa kazini napewa gari niwafuate wewe na jambazi mwenzio,halafu simu nimezima maana mkeo anakera sana yaani.
aliongea afande aitwaye Fox ambaye alikuwa anaendesha gari wakati wametuchukua pale home.

Itaendelea........................
nukta
 
SEHEMU YA THELATHINI NA SABA

Siku inayofuata baada ya kupunguza baadhi ya kazi zangu ofisini , niliamua kupiga simu kwa ndugu yeyote wa Jastini ili tupange namna ya kumsaidia,akili ikaniambia kumpigia simu mkewe ni kujitengenezea mazingira mabaya hasa ukizingatia jamaa yupo jela.

Nikakumbuka nina namba ya mtu ambaye nilikuwa nakwaruzana naye muda mwingi ambaye alidai ni dada yake ambaye hatujawahi kuonana ,kiufupi simfahamu na huenda hata yeye ananifahamu.
Nikampigia huku moyo ukinienda mbio maana nilijua natonesha vidonda vya watu na pia yule mdada sijui mmama hakuwa na lugha nzuri sana anaonekana ni mkali mkali,lakini nikalivaa tu lile jambo nikaweka simu sikioni.

Hello nani mwenzangu!
aliuliza upande wa pili mara baada ya kusalimiana.

Naitwa Daniel,mwezi uliopita ulinipigia kwaajili ya masuala ya ndugu yako Jastini.nilijitambulisha.

Oooh sawa nimekukumbuka,
Unasemaje? au unataka nini ?
aliuliza.

Nimepata taarifa za rafiki yangu Jastini kuwa yule gerezani,kifupi nimesikitika sana ila nina wazo fulani dada yangu.niliongea kwa tahadhari huku nikimsikilizia kwa umakini.

(Huku akitoa kicheko hafifu)
Mdogo wangu yupo jela ndiyo,lakini nikushangae wewe,kwani unataka nini kwetu?
Kwanza ulisema huhusiki na masuala ya Jastini ukidai tukuache na tulikuacha kweli licha ya Jastini kushindwa kukuhusisha moja kwa moja lakini ndugu tunatambua kuwa huenda mna kiapo mlichojipangia kuwa kama mmoja akikamatwa basi msitajane,ni kweli hakukutaja licha ya kupewa kibano kikali ataje wahusika na hakutaka kutaja yeyote.sasa ni biashara gani isiyo na washirika?
Ni kwamba ndugu yangu ni mjinga sana.aliweka kituo.

Samahani mama tunaweza kuonana tuongee kirefu ? niliuliza .

Inawezekana!
Lakini kwani unataka nini kwetu wewe,maana nahofia usalama wangu.aliongea akionesha ni mwenye wasiwasi kidogo.

Kuwa na amani dada ,mimi sina nia mbaya ni kwamba nahitaji tujadili hatima ya rafiki yangu Jastini kuwa usiogope.

Sawa mimi nipo maeneo ya mahakama ya (akiitaja mahakama ilipo)
Najaribu kuonana na watu fulani tujue namna ya kushughulikia haya masuala.alijibu.

Sasa dada kama upo hapo nadhani ni jambo jema kwanini tusionane tupange kabisa,eeeh ndani ya dakika chache nitakuwa hapo . niliongea kwa pupa .

Basi subiri nimalize mambo yangu kisha nitakupigia simu maana kuna mtu namsubiri hapa niongee naye . aliweka kituo.

Mida ya saa saba mchana tulionana yule mama ambaye kiukweli alikuwa ni mtu mzima tofauti na nilivyodhani huku akiwa na wenzake watatu , wanawake watatu akiwemo na yeye na mwanaume mmoja.walikuwa makini sana huku wakinitazama kwa hofu huenda walijua mimi si mtu mwema.

Nilijitambulisha kwa mara nyingine huku tukiingia kwenye mgahawa mmoja hivi,lakini hata mimi nilikuwa makini nao maana ni kama tunawindana.

Naitwa Lydia kama nilivyokuelekeza kwa siku ya kwanza,huyu ni mtoto wangu ,akimuonesha yule mwanaume ambaye ni kama umri tulilingana tu.na hawa ni ndugu wa mke wa jastini.alinitambulisha kwa wale watu huku akiniangalia pasi na kupepesa macho,sijui alijua labda nina manati nitamdhuru!!

Mimi kama nilivyowaeleza mwanzo ni kwamba sihusiki na habari za Jastini na mnavyosema hakunitaka huko kituoni licha ya kupewa mateso ,ni kweli kwakuwa asingeongea uongo kwakuwa sihusiki ila ni kwamba ni rafiki wa karibu,siyo kikazi ama kibiashara bali maisha ndivyo yalivyo.niliongea huku wakionesha wanakubali.

Kwanza bro mimi nikushukuru sana,kwa kuweza kutaka kushirikiana na sisi kumnusuru Jastini ambaye mimi ni mjomba wangu,na tangu mwanzo ,mama yangu na ndugu wote niliwaeleza kuwa wasihangaike kutafuta nani ama nani ,kifupi uncle wangu alishakuwa kwenye matatizo hivyo hakukuwa na haja ya kutaka kuwaumiza na watu wengine tusiokuwa na ushahidi nao.

Lakini kwa kufupisha maelezo ni kwamba Jastini anakabiliwa na kesi kubwa ya kufanya biashara ya nyara za serikali (madini)bila. Vibali huku akitambua kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.hivyo yupo jela kwa shitaka hilo na si vinginevyo.maana wale wadai wake walishamsamehe.alifafanua yule niliyetambulishwa kuwa ni mtoto wa dada yake Jastini.

Kwanza nilipenda maelezo yake lakini pia huenda tabia ya Jastini alikuwa anaijua siku nyingi hivyo hakushtuka hata kusikia mjomba wake yupo lockup . Baada ya hapo nilimuita tuongelee kwenye gari nikiwaacha wale wanawake wanakula.

Kwanza nikushukuru kwa kunifahamisha vizuri maana mama yako alikuwa anaongea kwa vitisho sana kiasi cha kumuogopa .niliongea huku nikijichangamsha.

Sikia bro,mimi Jastini namjua vizuri sana,mimi mwenyewe kashachukua hela zangu nyingi sana huku akijaribu kunishirikisha kwenye biashara zake lakini nikawa nagoma,pia si mimi tu wapo wengi ambao kawatapeli ,huku wengine wakisamehe na wenye madeni makubwa makubwa ndiyo hao wanakuja.hivyo bro usiwe na shaka na mimi ndiye niliyemtuliza mama kuwa asikusumbue kwani nilijua moja kwa moja utakuwa huhusiki maana kwanza mjomba wangu kwenye biashara hiyo yupo kitambo sana,na kilichomfanya arudi nyuma kimaisha ni baada ya kutamani kununua kuliko kuwa mchimbaji.aliongea yule jamaa huku nikifurahi angalau nitapumua maana Dah mwezi mzima hata bia sinywi,zitashukaje na nina mawazo.

Tulibadilishana contacts zetu huku nikiona sasa yule ndiye mtu sahihi ambaye nitaongea naye jambo likaeleweka kuliko wanawake.

Naitwa Pastor Lewis unaweza kusave hivyo ndiyo utanikumbuka vizuri,pia karibu sana kanisani kwetu.aliongea huku akitabasamu.

Kwanza nilimuangaliaaa kisha nikamuuliza.

Kwani wewe ni mchungaji,maana nilikuwa nawaza tukitoka hapa upige hata mbili tatu japo mimi bado niko kazini nisingekunywa.niliongea nikiwa namshangaa maana hakufanania na uchungaji,

Ndugu yangu hakuna jipya chini ya jua ,sisi binadamu ni wakosefu na ipo njia impendezayo mwenyezi Mungu ambayo ukiifuata hutatetereka.hata mjomba wangu nilikuwa namwambia mara kwa mara lakini labda aliniona mpuuzi.kumbuka yanayofanyika yote leo yalishafanyika,na kwanza nikushukuru kwa hicho ulichotaka kunipa ,na nikushauri tu kuwa kwani ukinywa hizo bia bro unapata faida gani? sisemi unakosea ila waweza kunipa faida hata mbili tatu ili nijue.aliweka kituo.

Hapana ni mazoea tu hivi vitu vina faida basi,ni kwamba tulijikuta tunashawishika tu kuvitumia.niliongea kwa aibu fulani hivi maana kutangaza ulevi mbele ya hawa wachungaji huwa sipendi.

Daniel,una jina zuri la nabii mkubwa sana kwa mujibu wa biblia ,okoka sasa hujachelewa ,ukisoma kitabu cha Muinjili Marko,anatuonesha ni jinsi gani tunapaswa tutubu na kuiamini Injili, wakati ni sasa Danieli.
aliweka kituo.kisha nikaenda kuwaaga wale akina mama ambao imani ilirudi tuliagana kwa furaha kisha nikarudi ofisini huku nikiwaza vitu vingi ila tayari nikushukuru kuona wameamini kuwa sihusiki na msala wa ndugu yao.

Nilirudi nyumbani mapema ,kumbuka mwezi mzima na tangu nitoke kule kwa mganga sikuwahi kugusa pombe,kwanza bado sikuwa na imani ya moja kwa moja kuwa matatizo yangu yameisha nilijua naweza kukamatwa muda wowote na maaskari hivyo nikajiweka mbali na vyombo kwa muda ili nijue mbivu na mbichi kwanza.

Nikiwa barabarani katikati ya foleni kuna jamaa alikuwa anauza vitabu vingi sana,na mimi ni mpenzi wa vitabu nikaamua kumuita huku nikichukua kitabu fulani kinachohusu masuala ya uchumi kikiandikwa na mhadhiri fulani wa moja ya chuo kikuu bora Duniani Havard ,nikasema hiki kitanisaidia kuzugazuga ili nisiwe natoka ndani,kwanza mchungaji Lewis kaniongezea kitu pombe siyo ya kuendekeza.

Jifunze,
Elimika
Burudika.

Inaendelea......................
 
SEHEMU YA THELATHINI NA NANE

Nilipekua pekua kurasa za kitabu kile huku nilivutiwa sana na yaliyomo mule nikizidi kukumbuka na kujifunza vitu vingi sana.

Mke wangu naye alirudi toka kwenye mihangaiko yake huku akionekana ni mwenye furaha sana.

Kiukweli mume wangu umebadilika sana kwanza umependeza sana na unavutia,ni wiki ya tatu unakaribia mwezi sasa sioni dalili ya kuwa ulikunywa pombe halafu unawahi sana kurudi,yaani hadi wivu unanijia kwa sasa sitaki hata utoke nje nahisi wanawake wengine watakuchukua.aliongea huku akitabasamu.

Wivu tena ,unakuwaje na wivu saizi badala ya unionee wivu nikiwa sipo au nikichelewa kurudi.niliuliza.

Kuna wivu kwenye maisha ya kawaida kwa mfano mtu akiwa na mafanikio kukuzidi basi unaweza kuwa na wivu kwa kutamani ufike alipo.au hata kama unajua hutokaa ufanane naye lakini hakuna namna .

Halafu kuna wivu wa mapenzi hapa kuna namna nyingi ,yaani hata kama upo kitandani lazima nione kama naibiwa lazima nipapase nijiridhishe.
Na wivu huu hata unipe bahari nzima na meli zote bila uwepo wako ni kazi bure,na huu ni wivu ambao hata anayekuonea wivu naye hajijui.

Halafu kuna wivu kwakuwa unacho na huu ndiyo umetamalaki Duniani kote,mtu anawaza rasilimali zako kupotea anakuonea wivu kwasababu,utafuja pesa na kushindwa kutimiza majukumu yako ,kuhusu wewe nilikuwa sikuonei wivu kwakuwa ulishanitoka kwenye nafsi yangu,wewe mtu gani ukirudi umelewa hatuna muda wa kupiga stori ,hakuna mapenzi,sawa hata kama familia yako unaijali lakini uwepo wako kama hivi mimi ndiyo napenda .tunapata muda wa kuongea kama hivi na nimshukuru Mungu nadhani maombi yangu yamejibiwa.aliweka kituo mke wangu huku siku hiyo utani wa hapa na pale ukitawala mithili ya ndoa mpya yenye siku tatu tangu ifungwe.

Ilikuwa siku ya kipekee yenye furaha ambayo nilijua imetokea na ni ngumu kujirudia kwakuwa hizi kuta za nyumba zetu zingekuwa zinaongea basi zina siri nyingi sana inafikia mtu unajilaumu kwanini nilioa .kinachokufanya uikumbatie ndoa ni familia iliyotengenezwa pamoja na umri,basi unabaki ukivumilia shida.siri ya kata aijuaye kata.

Siku inayofuata nikiwa ofisini kwangu nilipunguza kazi zangu kisha nikachukua kitabu changu nilichonunua jana ili nikipitie pitie ni utaratibu wangu wa siku nyingi vitabu huwa nasomea ofisini kipindi hicho ofisini. hakujafungwa kamera
(Technology sometimes ina madhara)

Mlango uligongwa, huku nikidhani ni Mfanyakazi wa mule ndani nikamwambia asukume ,aliingia jamaa mmoja ni mfanyakazi mwenzangu wa kitambo sana huku akiwa yupo kwenye kampuni ya mtu binafsi ni mtu alichangia sana mimi kufanikiwa,
Ni mtu aliyenizidi vitu vingi ,umri,
Maendeleo,hata tunavyomiliki sikumkaribia hata kidogo.

Vipi mdogo wangu Daniel naona umeyapatia maisha vilivyo,
Hadi unang'aa mtoto wa kiume na hicho hapo nini ,kitabu hee unajisomea home boy ,hebu nipe kwanza (huku nikimpa)

Alikigeuza geuza huku akitabasamu na kukifungua huku akizidi kucheka.

Daniel bwana ,naona kinazungumzia kuhusu kukuza uchumi eeeeh mara sijui Wealth Grow mara sijui increase value sijui nini yaani mambo kibaoooo.

Daniiii bado unaamini mafanikio kwa kusoma hizi propaganda,maisha hafundishwi mtu wala hakuna kanuni .
Ni jambo moja tu heshimu na kuthamini unachokipata huku ukitumia kidogo zaidi ya ulichoingiza full stop .huwezi kufanikiwa kwa kusoma vitabu ingekuwa hivyo asilimia nyingi ya watu wangekuwa matajiri home boy,

Halafu tufanye ni kweli ni mpenzi wa kusoma vitabu ,mbona vinapatikana mtandaoni ,una computer yako,una simu ,bado unatumia mifumo analogia hivi kwanza ulinunua shilingi ngapi? aliuliza.

Elfu ishirini, nilidanganya, ukweli muuzaji alianza elfu kumi then nikanunua kwa elfu saba tu.

Ona Sasa yaani kitabu tu unanunua kumi kumi mbili, na hapo hujalewa maana nakujua Dani usipotumia laki mbili kwa siku kwa matumizi ya kipuuzi bado hujafanikisha malengo yako.

Acha hizo Shabani, kwa maisha gani nitumie pesa yote hiyo kwa mambo yasiyofaa kweli!! kwa kipato gani haswa usije sababisha mtu akavamiwa bure . Niliongea huku nikichukua kitabu changu .

Huwezi jua Dani ni pesa ngapi umetumia , hebu fikiria kwa mfano umeenda bar ya kawaida tu acha huko kwenye gharama , ukanywa bia za elfu ishirini peke yako, ukanunulia na watu wengine pia, hapohapo hujachukua mwanamke (demu) naye atataka hela hapo hapo hela ya Lodge haaaa Dani just imagine home boy mbona pesa inakata hiyo fasta na hubaki na kitu na unavyopenda starehe Dani ndiyo maana huna hela. alizidi kunizodoa huku nikimwangalia tu.

Tatizo Shabani unayaishi maisha kwa sheria na kanuni ngumu sana maisha ni hayahaya hakuna sababu ya kukufanya usijitese sana , hizo hesabu ulizipiga siyo za Kila siku , siku moja moja jipongeze haupo jela shukuru MUNGU,
Haupo hospital mshukuru MUNGU pia. Sasa kwanini ujibanebane?
Mimi siwezi kaka, siwezi aslani , umekuwa bahili yaani kufanya kazi na waarabu wamekufanya uwe bahili sijui kwanini, pombe hunywi, kuswali huswali Sasa sijui upo upande gani.
Nilimjibu huku akitikisa kichwa kwa kunionea huruma eti.

Mpaka Sasa hivi una nyumba ngapi Dani. Aliuliza.

Nyumba za Nini kaka kwani nalala nje? Wewe nakujua ni chizi wa nyumba Tena ulivyo fala, kwa mfano vile vibanda vyako vitatu vya mkoani kama ungeamua zile pesa ukajenga nyumba moja nzuri kubwa ukaifinish vizuri huoni kama ungekuwa mjanja , Sasa zile nazo nyumba kaka , hebu kwanza ongea kilichokuleta. niliongea huku tukipeana tano tukicheka ni mtu ambaye ukitukuta ni kama tunagombana kumbe ndiyo ongea yetu.

Tuache masikhara kaka mimi Nina dili Kuna gari nimekuja nayo ipo hapo nje naiuza . Aliongea huku akiweka uso serious kuonesha ni ishu ya kweli .

Dah chombo gani hicho unasukuma . Niliuliza.

Ipo nje twende ukaione , tusiandikie mate kaka

Tulitoka nje kabisa ya uzio nikaiona brevis mpya ikionekana haijatumika sana , hata ndani Kila kitu kulikuwa freshi , nikaitest huku Kila kitu kikifanya kazi ipasavyo.

Dah Sheby gari umepata wapi hii na kwanini uuze bro?
Niliuliza.

Oyaa wewe tafuta mteja Mimi naenda mkoani nikirudi utanipa pesa yangu .uza bei yoyote lakini niletee pesa yangu
huku akinitajia kile kiasi ambacho inauzwa ilikuwa ni bei ya kawaida kabisa .nikaona huenda pesa ya kulewea nitapata

Au kama wewe unachukua fresh maana wewe Dani huna gari unatembelea mkweche tu Sasa gari zako nazo gari ulizinunua mafungu kwenye mnada nazo gari ,na sidhani kama Zina kiyoyozi, chukua Chuma hiki kikurahisishie mambo yako wewe.

Hebu nipe documents kwanza maana hii inafaa kwa kuhonga. Kuna mademu wanakuwaga na vipini kwenye ulimi, wakiku tight kwenye lile eneo unaweza kutoa gari kwa muda huo hebu lete kadi yake . Niliongea kiutani huku tukicheka .

Kadi tu ipo chukua kwenye begi hilo hebu angalia Kila kitu kuwa na amani hili ni gari langu la jasho langu halafu anatokea Malaya mmoja anajaribu kunidhulumu, Tena na akome. aliongea kwa kujiamini Shabani huku nikigundua Kuna jambo haliko sawa pia kadi ya gari ilikuwa na jina la kike Tena nikigundua ni mkewe . Nikazidi kupata mashaka.

Bro mbona jina ni la wife Mimi nikajua ni lako? niliongea kwa sauti ya chini huku nikimtazama.

Wewe Dani vipi wewe mshamba Nini, Mali za mke wangu ni zangu nilimuoa akiwa Hana kitu Malaya yule halafu namuweka asimamie miradi yangu mwisho wa siku kwenye account sijaona hela ya maana huku akijizawadia gari. Sasa nimemwambia achague moja talaka au abaki na gari, kanipiga hela ndefu sana na hii gari acha niuze niambulie yaani wanawake si watu wa kuwaamini. aliongea huku akizidi kuwa mkali nikagundua hayupo sawa.

Kwa pesa ambayo ningepata kwenye udalali wa ile gari ilikuwa safi ningepata ya kula nyama choma lakini nikagundua mbona kama chombo kina matatizo.lakini watajuana wenyewe chombo naiuza hii

Kumbuka Daniel Nina tamaa sana na hizi hela za bia huwa sisikii la muadhini Wala mnadi swala. Sasa itakuwaje.

Jifunze,
Elimika,
Burudika.

Itaendelea................
 
Back
Top Bottom