MIMI NA MIMI 2
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA THELATHINI NA MOJA
★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
Nimekuja kushtuka ikiwa bado ni usiku, na tena nikisema kushtuka namaanisha kushtushwa baada ya kupatwa na njozi isiyo nzuri. Yaani niliota niko mahala fulani pamoja na Miryam, halafu ghafla tukavamiwa na watu waliokuwa wamevalia manguo yaliyochanika-chanika kwa muundo kama wa tambi, huku nyuso zao zikiwa za mafuvu. Walitukamata mimi na Miryam na kuanza kututesa, wakisema maneno "apple pie" kwa njia ya kuimba kwa sauti mbaya kweli, halafu mmoja wao akamchinja Miryam mbele ya macho yangu na kukirusha kichwa chake usoni kwangu.
Yaani uso wa kichwa cha Miryam ulipoufikia uso wangu ndotoni ndiyo nilishtuka kwa kufumbua macho, nikijikuta nimelala chali huku chumba kikiwa na giza bado, nami nikaendelea kutulia hivyo hivyo nikisikilizia namna ambavyo mapigo ya moyo wangu yalitembea kwa kasi. Hofu ilikuwa imenivaa kiasi, maana ndoto za namna hii huwa zinaogopesha kwa sababu zinafanya uhisi vitu kuwa halisi kabisa. Nadhani sijui shauri ya kulala chali, yaani ulikuwa umepita muda sijaota ndoto mbaya, ila sikujihisi amani kabisa kumwota Miryam kwa njia hiyo.
Nikajinyanyua taratibu na kuchukua simu kuangalia muda. Ilikuwa ni saa kumi usiku, ikielekea alfajiri, na hapo yaani usingizi wote ukawa umekata. Hata kama ningesema nijilaze kidogo kusubiri hadi muda niliopangia kuanza kujiandaa ufike, nisingeweza kupata utulivu wa kiakili maana hiyo ndoto iliendelea kunisumbua kichwani ingawa nilijitahidi kuacha kuifikiria. Inawezekana labda niliota tu hivyo bila sababu yoyote, lakini hiyo kitu ilinifanya nihisi kama vile kuna kitu nilikuwa nimesahau kufanya. Ni nini ambacho kingenipa wasiwasi kwamba Miryam angeumia baada ya sisi kuanzisha mahusiano ya kimapenzi hatimaye? Ding, ding, ding... Festo!
Ni kweli kabisa nilikuwa nimeshasahau kuendelea kufatilia ikiwa huyo jamaa alikuwa ameondoka, maana sikuridhishwa na uhakika nilioupata kutoka kwa Miryam mwenyewe na askari Ramadhan aliyesema kwamba jamaa alikimbia nchi. Huenda hiki ndiyo kitu kilichonipa wenge bado, hasa kwa kuwa wakati huu Miryam alikuwa wangu. Kwa njia moja ama nyingine, umakini ulitakiwa kuwa muhimu, yaani sikupaswa kumsahau huyo jamaa. Bertha alikuwa ndani na angekarabatiwa na askari Ramadhan, lakini jamaa alikuwa huru. Huru. Hiyo ilikuwa sababu tosha kwangu kujua kuwa hatari ingeweza kurudi muda wowote ule, hivyo sikupaswa kujisahau sana.
Oh, JC nikiwa na wasiwasi yaani ningewaza lolote lile hata kama hakukuwa na ishu kubwa mno ya kuwaza. Uwezekano wa kwamba Festo angekuwa ameondoka kweli na labda hata kwenda kupata mwanamke mwingine ulikuwepo, lakini ulikuwa ni uwezekano tu, sikujua kama ulikuwa ndiyo uhalisia. Ningepaswa kuwa na uhakika zaidi, kwa hiyo ningeendelea kufatilia nyendo zake kokote ambako angekuwa mpaka nijue kama anastahili kuwekwa pembeni, ili nihakikishe usalama wangu na Miryam pia.
Hivyo ili kuyaondoa mawazo na nini nikawa nimeamua tu kuanza kujiandaa, nikitoa nguo safi kabisa na kunyoosha mkunjo wowote usiotakikana, halafu nikatoka na kwenda kuoga hiyo hiyo saa kumi. Kulikuwa na baridi kali kwa mida hii, na najua mpaka wakati ambao tungeondoka na bibie bado lingekuwepo, hivyo nikaona siyo mbaya nikivaa na koti la ile suti ya kisharobaro ambayo madam Bertha alinipa siku kadhaa nyuma. Kufikiria kulivaa koti hilo kukanifanya nimuwaze, kukiwa na ile nia fulani kwa hisia zangu ya kutaka kujua hali yake akiwa huko ndani, lakini naelewa hiyo isingenisaidia kwa lolote. Kuna vitu tu nilipaswa kuviachia.
Nikaamua tu kutulia na kusubiri mpaka imeingia saa kumi na moja, nami nikaamua kumtumia Miryam ujumbe nikisema nipo tayari, hivyo akiamka na kumaliza kujiandaa anishtue. Lakini ni muda huo bibie akawa amejibu, akiniambia kwamba yaani yeye alikuwa ameshajiandaa mapema mno, na nilikuwa nimemwahi tu kwa kutuma ujumbe maana alitaka kunipigia. Kumbe siyo kwamba tungetakiwa kuamka saa kumi na moja, ila kuondoka saa kumi na moja. Ikiwa ile ndoto isingenishtua, basi alarm ingekuja kuniamsha Miryam akiwa ameshamaliza kuvaa!
Kwa hiyo hapo sote tukawa tumekamilisha maandalizi, yaani yeye alimaliza kuvaa na ndiyo alikuwa anatoka, hivyo na mimi nikavaa viatu vyeupe upesi na kusanuka pia. Nilivalia T-shirt langu jeupe la mikono mirefu pamoja na suruali jeans ya blue, huku koti jeusi-kijivu la suti likinifunika kwa juu. Sikuhitaji kubeba madude mengi, ni simu tu na pesa, pamoja na kadi ya mwaliko wa send-off ya Doris niliyokuwa nimeshalipia, nami nikamwachia ujumbe Ankia wa kumuaga, nikimfahamisha kuwa ninamsindikiza Miryam Morogoro lakini nikamwomba awe makini kutosema hilo kwa yeyote.
Nikatoka ndani hatimaye na kuelekea nje, nikifunga milango na geti kwa uangalifu, kisha nikasimama pembeni usawa wa duka la Fatuma na kumtumia Miryam ujumbe kuuliza alitaka niende kumsubiria kwa wapi maana nilikuwa nje tayari. Akasema nimsubirie hapa hapa nilipokuwa kwa sababu alihofia kutembea peke yake, na hiyo ilipatana na akili. Ikiwa ni saa kumi na moja bado, upande huu wa kitaa ulikuwa na giza, ukimya, na utupu. Mwanamke kama yeye atoke tu na kuanza kutembea mwenyewe ingeweza kuwa hatari, najua hilo halingekuwa na shida kama Tesha angekuwepo angalau.
Hivyo nikasubiria hapo dukani kwa dakika chache, nami nikamwona bibie akitoka mule ndani kwao. Akaja mpaka hapo nje, akifunga geti lao kwa umakini na kisha kurusha funguo huko ndani ya geti, ili mama zake wakiamka waweze kufungua bila tabu. Usalama kwanza. Akaja hadi karibu nami, na alikuwa amevalia gauni refu la kike lililobana, lenye muundo wa kitambaa kama jinsi masweta ya shule yalivyo ingawa siyo nzito, likiwa la rangi ya ugoro na lililochoresha mwili wake vizuri sana.
Alivalia koti la jeans pia lenye rangi ya blue, kufunika kifua ili kuipinga baridi hii ya alfajiri, na miguuni alivalia simple nzuri za rangi ya dhahabu. Nywele zake akiwa amezibana juu ya kichwa chake, alionekana kuwa mrembo sana kwa muda huu, yaani ule upya wa siku kwa alfajiri ulimfanya aonekane mweupeeh kuliko kawaida. Alining'iniza mkoba mweupe wa manyoya mkononi, huku akijikumbatia shauri ya kuhisi baridi. Akanifikia karibu, nami nikauchukua mkoba wake na kisha kumpa kumbatio upesi ili ahisi joto kidogo, na mimi vilevile nihisi lake.
"Umeamka poa?" nikamuuliza hivyo kwa sauti ya chini.
"Yeah. Wewe?" akauliza hivyo kwa sauti tulivu pia.
Nikamwachia na kusema, "Niko fresh. Baridi eh?"
Akatikisa nyusi kukubali.
"Haya, twende. Usije ukaganda," nikamwambia hivyo huku nikisugua mgongo wake kwa kubembeleza.
Mdogo mdogo, mimi na mpenzi wangu tukaianza safari kuelekea barabarani, nikitembea pamoja naye kwa ukaribu huku nampigisha story. Wote tulikuwa na kale kahali ka umakini kwa sababu ya hii kuwa mapema mno, hivyo hakukuwa na utani. Nikawa nimemuuliza ikiwa aliwahi kutumia usafiri wa treni ya mwendokasi kabla, lakini akasema ndiyo ingekuwa mara yake ya kwanza.
Vilevile na mimi pia, hii ingekuwa mara yangu ya kwanza. Najua ujenzi wa huo mradi kwa kipindi hiki ndiyo ulikuwa unaelekea kuifikia Dodoma, na safari za mizunguko kutokea Dar mpaka Moro ndiyo zilikuwa zimeanzishwa, kwa hiyo sote tungeenda kujionea jinsi ambavyo ingekuwa, yaani 'experience' ya mara ya kwanza kuzipanda hizo ishu tungeipitia pamoja. Angalau na nchi yetu ilikuwa inapiga hatua kwenye miundombinu na mambo mengi, ingawa najua hujuma zilikuwa nyingi mno... na zingeendelea.
★★
Basi bwana, mimi na Miryam wangu tukawa tumechukua usafiri wa bodaboda hadi kufikia stendi ya Mbagala Rangi Tatu, nasi tukaelekea huko huku nikiwa nimemshika bibie mkono. Kwa muda huu, eneo hilo lilikuwa na watu, wengi wao wakiwa wanasubiri magari ya kuelekea pande walizotaka kwenda, nasi tukakutana na kizungumkuti cha kuhitaji kusubiri magari ambayo yangekwenda moja kwa moja mpaka Stesheni.
Ingekula muda maana tulisimama karibia dakika kumi na tano bila ya magari hayo kufika, hivyo nikamwambia Miryam tukodi bajaji na kwenda barabara ya kuelekea Makumbusho huko, ili tushukie kwenye kituo fulani ambako daladala za kwenda Stesheni zingepita. Likaonekana kuwa wazo zuri kwake, hivyo tukaamua kuchukua bajaji mmoja wa kutupeleka huko, nayo vruum ikatembea kwa kasi kutuwahisha. Miryam alionekana kuwa na usingizi bado, tangia tumeondoka Rangi Tatu akawa amenilalia tu begani na kufumba macho kwa dakika nyingi, huku mie nikikaza macho mbele na kuendelea kutulia tu.
Tukafika eneo hususa nililotaka na kushukia hapo kwa pamoja, daladala ikaja, nasi tukaendelea na safari kwa mara nyingine tena. Niliwahi kufika maeneo ya Stesheni kipindi fulani lakini sikuwahi kwenda kabisa kwenye stesheni yenyewe, hii mpya ya SGR, kwa hiyo hakukuwa na tabu Miryam wangu kuendelea kunilalia tu begani hadi tulipofika maeneo ya huko. Tulikuwa tunatazamwa sana, na nilipenda. Miryam alistareheka kabisa kuwa kando yangu mbele ya watu wote ambao hatukuwafahamu, na nilitaka ije kuwa namna hiyo kwa wale wote waliojalisha kwetu. Safari yetu ya mapenzi ndiyo ilikuwa inaanza.
Baada ya kufika hilo eneo, tukaelekea mpaka kwenye jengo zuri sana la stesheni hiyo ya treni, na ilikuwa imeshaingia mida ya saa moja kabisa. Tulichelewa, lakini hakukuwa na namna. Yaani hilo jengo, halikuonekana kama jengo la stesheni ya treni, ila kama terminal ya uwanja wa ndege. Lilikuwa zuri, safi, likijengwa kwa vioo vizito kulizunguka, yaani... safi! Ndani sasa ndiyo kulikuwa na utaratibu uliofanya pawe kama airport kabisa, kukiwa na mashine za X-ray za kuchunguza vitu haramu na walinzi maaskari, siyo wale uchwara.
Watu waliofika hapo, yaani walionekana kuwa na yale maisha ya uzungu, pesa, hata kama siyo wote, wengi walijiweka hivyo. Wanawake walivaa kwa kujiachia, mapaja nje nje pamoja na hali kuwa yenye baridi, mionekano ya maana, yaani nilihisi nimeingia sehemu maridadi zaidi kuliko hata nyingine nilizowahi kwenda. Sisemi ilipita zoooote ambazo zilikuwa maridadi, ila nasemea kwa hizi tu zilizohusiana na masuala ya safari ukiondoa majengo ya uwanja wa ndege.
Tukapita ukaguzi, kisha tukapanda hadi ghorofa la pili ili kukata tiketi. Miryam wangu akakaa kusubiri nikate tiketi zetu, nakwambia watu waliopanga foleni fupi fupi wakiwa na zile staarabu za kishua, nami nikapata tiketi hatimaye na kurudi kukaa na bibie. Treni ingefika kwenye mida ya saa tatu, na bila shaka Morogoro tungefika kama siyo saa nne, basi saa tano.
Tukaendelea kutulia tu hapo, mara kwa mara nikiangaliana na Miryam na sote kutabasamu bila sababu yoyote ile, basi tu, ushirika wangu karibu naye ulikuwa mzuri sana. Tukashikana viganja kabisa na kutulia hivyo hivyo, na sikuweza kujizuia kuona namna ambavyo baadhi ya wanawake na wanaume walitutazama sana. Siyo kwamba kusema Miryam ama mimi pekee ndiyo tuliokuwa wenye sura nzuri peke yetu humo, lakini nadhani ni jinsi tu tulivyokuwa tunajiweka ndiyo kuliwavutia. Utulivu, kama hatupo vile.
Nikawa nawatikisia tu vichwa wanaume fulani walionipa salamu kwa njia hiyo, huku nikiepuka kukodolea mwanamke yeyote maana wa kwangu alikuwepo hapo hapo. Na wala hata hakuonekana kujali, alikuwa zake ametulia tu kama hana habari kuwa ningeweza kuibiwa, na hiyo ikanipa hali ya kujiamini zaidi hata kwa yeye ambaye angeweza kuibiwa na wanaume wengine waliomwona kuwa mzuri sana. Nikawa namsemesha mara moja moja tu na kumwonyesha video za ucheshi kwenye simu yangu ili kupisha muda.
Tumekaa hapo mpaka saa mbili na nusu hivi, kweli tangazo la treni kuwadia likatolewa. Tukanyanyuka, pamoja na watu wengine, nasi tukaenda huko na kuingia kwenye siti zetu tulizopewa. Ah, yaani hii treni ilikuwa 'magic.' Ilikuwa nzuri, siti laini, TV ndogo kila mstari wa siti kwa juu, AC za maana, na nadhani hata huduma ya choo ilikuwepo, ila nani angejisaidia kwenye mwendokasi? Natania tu!
Kufikia hii mida jua lilikuwa limeshawaka, kwa hiyo nikawa nimevua koti, huku Miryam akiwa amevaa lake tu. Hakutaka kuongea sana, yaani ile tumefika tu na kukaa, akanilalia begani tena. Nikacheka kidogo tu na kumwambia akae tupige story bwana, lakini bibie akaendelea kulala tu utadhani alikuwa amenunua mto mpya, kwa hiyo nikaona nimwache aenjoy usingizi wake tu. Ndiyo ulikuwa mwanzo wake wa kudeka huo. Nikamwashia na AC, kisha nikaingia mtandaoni kuperuzika.
Saa tatu haikukawia kuingia, na ndiyo treni yetu ikaanzisha mwendo.
★★
Hii safari ilikuwa tulivu sana tofauti na vile nilivyotazamia. Yaani treni ilitembea kama vile iko pale pale. Iliseleleka tu. Sikusikia makelele yoyote, ilikuwa kama niko kwenye ndege. Kukawa na wahudumu wanapita nakwambia, wanatupatia vikeki eti vya kuyeyushia meno, na kwa dakika kama 40 tokea tumeondoka, Miryam alikuwa ameupata usingizi ule wa maana, akilala kwa utulivu bila mifurukuto wala kushtuka hata mara moja. Alikuwa na ule uchovu siyo wa jana au juzi tu, bali wa muda mrefu, na sasa angalau akawa ameutoa kidogo kwa msaada wa bega langu. Na sikuachia kiganja chake yaani.
Nilipenda kumwangalia usoni alipokuwa amesinzia, ile amani aliyonipa nikiiona hapo, na hatimaye baada ya hizo dakika kukata akawa ameamka. Akanitazama usoni kukuta namwangalia tu kwa utulivu, naye akanyanyua kichwa chake na kuegamia siti yake huku akiziba mdomo kupiga mhayo.
"Mambo?" nikamuuliza hivyo kwa sauti ya chini.
Akaniangalia usoni na kusema, "Poa."
"Kalikuwa kamechoka!" nikamwambia hivyo kiutani.
Akatabasamu kizembe.
"Pole. Sema tatizo unapenda kujipa mikazi mingi mno," nikamwambia hivyo.
"Nisipofanya kazi, nitakula nini?" akauliza hivyo huku akiangalia mbele.
"Kazi ya pesa sawa. Kuna ulazima gani wa kufanya hadi kazi za nyumbani?"
Akaniangalia usoni tena.
Nikamtazama pia na kusema, "Nimekuangalia sana. Unatoka kazini na joto kali, unafika tena nyumbani unaliongeza. Kwa nini mwili usichoke mno?"
"Asa' unataka nani afanye? Akina mama? Au Mamu?" akaniuliza hivyo.
"Hamna. Ila... umeshafikiria kutafuta msichana wa kazi?"
"Hapana. Hizo biashara sitaki tena."
"Ulikuwaga naye hapo?"
"Karibia watatu. Tena kabla hata Tesha hajaja, na alipokuja tena. Ni wasumbufu sana..." akasema hivyo.
"Najua. Ila ni kama tu hawajachunguzwa vizuri..."
"Ah, huo muda... hapana. Wawili waliondoka wanalalamika eti Mariam anawachosha, mara sijui shangazi yangu ana roho mbaya... Shadya yaani, na wa mara ya mwisho alikaa miezi miwili, halafu akatoroka akiwa ameniibia elfu hamsini..." akasema hivyo.
"Doh! Kweli..." nikasema hivyo huku natikisa kichwa.
"Sipendi makelele. Angalau sasa hivi mambo siyo mengi mno kama wakati Mamu ameanza kuumwa, so hizi kazi ndogo ndogo nakuwa tu nafanya. Napenda sana kufanya kazi, ikiwa ulikuwa hujui hilo," akaniambia hivyo.
"Najua. Sema... usizidishe sana, bado mrembo, mikazi mingi itafanya ukongoroke..." nikamwambia hivyo kiutani.
Akatabasamu na kusema, "Ndiyo nachotaka."
"We! Ikitokea hiyo nakukimbia," nikamtania.
"Ahah... yaani nakongoroka halafu ndiyo nakung'ang'ania sasa. Hadi kwenu..."
"Ahahahah... itapendeza sana ukija kufika kwetu," nikamwambia hivyo kwa hisia.
Akaniangalia usoni kwa utulivu.
"Nataka mama akujue," nikamwambia hivyo.
Akaweka uso makini huku akitabasamu kiasi.
"Ahah... serious," nikamwambia.
"Mhm... bado mapema," akaniambia hivyo.
"We' unataka iwe lini?"
"Tutajuana tu, lakini Jayden! Ahahah... yaani ndiyo tumeanza jamani, unataka kusema utanipeleka nikamwone mama yako kesho, au?" akauliza hivyo.
"Yeah!" nikamwambia hivyo kwa uhakika.
"Mm?" akafanya hivyo kunipinga.
Nikaanza kuchezesha mabega huku nikiimba, "Me nataka kesho... twende nikupeleke nyumbani..."
Akaangalia pembeni na kutabasamu.
"Me nataka, kesho... twende ukamwone mamaa..." nikamwimbia na kukikaza kiganja chake kiasi.
"Tulia kijana wangu. Kila kitu lazima kiende kwa hatua. Taratibu. Siyo unipate jana, kesho utangaze ndoa," akaniambia hivyo.
"Kibaya ni kipi hapo?" nikamuuliza.
"Hakuna kibaya, ila... nataka tuweke mambo yetu... sawa kabisa. Nataka... familia yangu wakujue kwanza, yaani, tayari wanakujua, ila... wakutambue kama mwanaume wangu... halafu ndiyo unipeleke nimwone mama," akaniambia hivyo
Nikatabasamu kiasi na kusema, "Sawa. Siyo mbaya. Na tunayaweka mambo mengi sawa kwa kudili na hili la Mariam kwanza, uwongo?"
"Eeh, lipite hili... na mengine halafu, tutafanya jambo," akasema hivyo kwa uhakika.
"Mhm... alright. Hao wanaoliangalia huko hilo shamba wanataka nini kwani?" nikamuuliza.
"Kulikuwa kumezuka kama mgogoro, kuna mwenyeji alikuwa anadai sehemu fulani ya shamba letu imeingiliana na lake. Sijui anataka kuliuza? Yaani... anasema kama vile tumeiba sehemu yake..." akanifahamisha.
"Ahaa..."
"Eeeh. Kwa hiyo naenda kusambaratisha hiyo ishu, maana nahisi inaweza ikaja hujuma. Nikienda me mwenyewe kuwathibitishia vipimo vya shamba la Mamu, hawawezi kufanya uchakachuzi, si unajua nikikaa mbali muda mrefu..."
"Eee, hiyo inaweza kutokea," nikamwambia hivyo.
"Yeah. Yaani! Kelele ambazo watu wananipigia kwa sababu tu ya shamba la mdogo wangu, hazikomi. Sijui tu ni kwa nini. Nimemaliza ya Joshua, ikapita. Ikaja ile ya kampuni, waliotaka kunitaifishia hadi nyumba... ukanisaidia ikapita. Sasa hivi tena hii. Yaani hakuna kitu mtu anaweza kufanya akanichanganyia habari kuhusu mali ya mdogo wangu. Naitunza mpaka nihakikishe anakuja kuimiliki yeye mwenyewe," Miryam akaongea hivyo kwa sauti tulivu.
Jambo hilo alilosema likawa limenifanya nikumbuke kitu fulani, nami nikatazama mbele na kushusha pumzi.
Miryam alipoona nimebaki kimya tu, akanyanyua viganja vyetu vilivyoshikana na kuvirudisha mapajani tena, nami nikamwangalia usoni. "Vipi?" akaniuliza hivyo kwa utulivu.
"Safi. Kwani vipi?" nikamuuliza pia.
Akaweka uso wenye udadisi na kusema, "Naona kama mood yako imehama. Kuna kitu unawaza?"
Nikabaki nikimtazama machoni kwa utulivu.
Akaniangalia kwa njia fulani ya uelewa na kusema, "Niambie."
Nikakileta kiganja chake usawa wa kifua changu na kusema, "Kuna kitu nilikuwa bado sijakwambia."
"Mbona serious? Ni kibaya?" akauliza hivyo.
"Siyo kibaya, yaani... ni kuhusu tu kampuni ambayo... yaani, wale watu ambao Joshua alikula lile dili la kuuza kiwanja cha mdogo wako," nikamwambia hivyo.
Akaweka uso wake kiumakini.
"Ni mzee wangu ndiyo alikuwa anakitaka... yaani, yeye ndiyo kichwa cha sehemu ya hiyo kampuni iliyokuwa inadili na hilo suala..." hatimaye nikamwambia.
Miryam akaendelea kuniangalia kwa umakini tu.
"Alikuwa anataka kulinunua shamba la Mamu lakini hakujua kuhusu hizi antics za Joshua... tena, ni dili lililokuwa linasimamiwa na mwakilishi wake," nikamfahamisha.
"Mh! Mbona sielewi?" akaniuliza hivyo.
Nikabaki nikimtazama machoni kwa utulivu.
Akaangalia pembeni kwa ufupi, kisha akaniangalia usoni tena na kusema, "Unamaanisha kwamba... haya yote yaliyotokea juzi juzi yamesababishwa na baba yako wa kufikia... yeye ndiye... alitaka hadi kuuza na nyumba yangu!"
"Miryam, hakuwa anajua kuhusu mambo ya Joshua. Alifanya hilo dili, clean kabisa, kwa hiyo yale yote yalipotokea, akapata hasara... kampuni kwa ujumla... yaani iliporudi hasara lazima kampuni ingehitaji fidia, ndiyo maana. Hayakuwa makosa yake, hata kama asingekuwa mzee wangu, unajua hilo..." nikamwambia hivyo kwa upole.
"Kwa hiyo kumbe ndiyo maana ukatoa ile milioni kumi?" akaniuliza.
Nikabaki kimya tu, nikiendelea kumtazama usoni kwa utulivu.
"Ahah... yaani kutokea mwanzo kumbe ulikuwa.... kwa nini hukuniambia?"
"Haingekuwa na utofauti wowote. Na nilikusaidia siyo kwa sababu tu nilijua hayo, nilikusaidia kwa sababu nilitaka kufanya hivyo. Hayo sasa hivi yameshaisha, nimeona nikwambie tu ukweli kukuelewesha..." nikamsemesha kiupole.
"Mhm... ukweli wa kwamba wewe ni mtoto wa tajiri ambaye utatoa tu milioni kumi na kuzigawa bila kuwaza, kwa kuwa daddy haishiwi eh?" akaongea kikejeli.
"Miryam..." nikamwita hivyo kiupole.
"I'm sorry... nimeshangaa tu. Sikutarajia," akasema hivyo huku akiangalia pembeni kwa huzuni kiasi.
Nikakiweka kiganja chake usawa wa shingo yangu na kusema, "I'm sorry too. Sikukwambia mapema maana mambo yalikuwa mengi, na me mwenyewe nikakuchanganya kwa vingi. Ila nimekuchanganya vizuri mpaka sasa hivi tuko hapa, uwongo?"
Akatabasamu kiasi na kuniangalia.
"Naomba tuyaweke tu hayo pembeni. Sasa hivi tupo kwenye chapter nyingine kabisa..." nikasema hivyo.
Akatikisa kichwa kuonyesha uelewa, naye akasema, "Sawa. Nashukuru kuniambia. Mhm... ndiyo tunaanza kujuana sasa."
"Ahah... ni kweli," nikasema hivyo huku nikitabasamu.
Akatulia kidogo, kisha akauliza, "Kwa hiyo... kwanza, mzee wako anaitwa nani?"
"Frank. Frank Manyanza," nikamjibu.
"Mmm... na ndiyo mwenye hiyo kampuni iliyokuwa interested kununua kiwanja cha Mamu?"
"Siyo kwamba ni yake kabisa, hiyo ni... yaani anahusika nayo kama president, wa hii kampuni, kwa huku Tanzania... yaani ni ya watu wa huko New Zealand, na wameijenga na huku, kwa hiyo..."
"Yeye ndiyo CEO," akasema hivyo.
"Yeah. Wako na level zao."
"Inahusiana na nini?" akauliza.
"Haya masuala ya letting..." nikamwambia.
"Ahaa..."
"Yeah. Ngoja nikuonyeshe. Hilo jengo lipo huko Makumbusho, zuri.... hili hapa..." nikawa nimemwonyesha picha ya jengo hilo kwenye simu yangu.
"Sky Tower. Ni pazuri," akasema hivyo baada ya kusoma hapo kwenye picha.
"Mmm... teranova. Wanatoa space za kufanyia biashara, kupangisha nyumba au vyumba, kumbi za mikutano ama sherehe, za gharama yaani, na.... inahusika na mambo mengi sana, na yeye kwa upande wake huku ndo' anaibeba sasa. Wamepanuka zaidi, ndiyo maana wanataka kusambaza upendo wao kwa mikoa mingine. Nadhani Mwanza, Dodoma, na Arusha labda tayari... ndiyo sababu walitaka na kiwanja cha Mamu ili wajengee mradi wao na huko Moro..." nikamwelezea.
"Okay. That's big..." akasema hivyo.
"Yeah... ana hela huyo! Huwa halali. Nikupe namba zake?" nikamwambia hivyo kiutani.
Miryam akacheka kidogo kwa pumzi na kutikisa kichwa.
"Ahahah... sema nikutoe. Anaweza akakununulia hadi hela huyo. Au hupendi hela?" nikamtania zaidi.
Akasema, "Hebu acha mambo yako bwana. Niambie. Ulisemaga alimuoa mama yako wakati uko form four, si ndiyo?"
"A-ah... yaani... wameanza mahusiano me niko form four, amekuja kumwoa niko form six..." nikamwambia.
"Ahaa... basi nilidhani ulimaanisha amemuoa kipindi uko form four..."
"Hamna..."
"Wanapendana eh? Ndiyo maana anawapenda sana na nyie..."
"Ndiyo, ahah... mzee ameanza kutupenda me na Jasmine kabla hata hajamjua mama. Jasmine ndiyo aliwakutanisha..."
"Ooh... kumbe aliwajua nyie kwanza?"
"Mmm. Kwa mtu wa aina yake, siyo rahisi sana kumpata na kumjua, hana ile socializing ya kawaida. Siyo kwamba anabagua watu lakini, ila kazi zake ndiyo zinamfanya anakuwa... muda mwingi juu zaidi yaani..."
"Kwa hiyo nyie aliwajuaje mpaka akakutana na mama yenu?"
"Kupitia binti yake. Ana mtoto wa kike, mdogo wetu sasa hivi yaani, anaiwa Nuru... niliokoa maisha yake, ndiyo mpaka nikaja kukutana na baba yake..." nikamwambia hivyo.
"Alifanyaje?" akauliza.
"Ah, yaani! Tulikuwa kwenye party fulani kule Malaika, Mwanza... mambo ya vijana na nini si unajua, na Nuru akawepo hapo hiyo siku. Alikuwa mdogo, lakini mambo yake!"
"Ya kikubwa?"
"Aah... alikuwa amepelekwa hapo na jamaa fulani hivi, kwa wakati huo huyo jamaa kama Tesha, ila mambo yake yalikuwa siyo. Nuru alikuwa kwenye miaka kumi na nne, lakini alikuwa ananyweshwa pombe..."
"Wewe..."
"Si na ule ushua na nini, Nuru alikuwa changanyikeni sana, afu' kalikuwa na kiburi enzi hizo! Ila alikuwa na umbo kubwa kubwa, kwa hiyo hata akidanganya ana miaka kumi na nane, watu wanakubali. Sa' kukawa kumetokea ugomvi, huyo jamaa yake kapigana na mtu wakapasuliana chupa, Nuru akachanwa shingoni... pembeni hapa. Sisi tumekuja kusikia commotion hao jamaa wamekimbia, kufika hapo Nuru kalala chini, damu inaruka, anahangaika, halafu sasa... waliokuwepo wakawa wanamwangalia tu... ile ya kipindi kile kwamba hatupaswi kumgusa mpaka watu maalumu waje..." nikamsimulia.
"Ukafanyaje sasa?"
"Ah... unacheza na mimi? Genius," nikamwambia hivyo huku nikimwonyesha ishara kuwa na akili.
"Ahah... niambie sasa..."
"Niliona alikuwa anapata shida kupumua, kwa hiyo nikajaribu kitu ambacho... yaani sikuwa hata na uhakika kama kingefanya kazi. Si nilikuwa nasoma sana, nilijua kuna kitu fulani wanaita cricothyrotomy... neno gumu eh?"
Akatikisa kichwa kukubali.
"Eeh, yaani makeshift, kumfanya mtu kwenye hiyo instance kama mshipa wake umepasuka, trachea ama nini... unatumia bomba dogo kuweka kwenye hilo jeraha, ili aanze kupumulia hapo. Ah, yaani Miryam! Sijui nilikuwaje. Yaani eti nikafanya hivyo. Nikapata kibomba cha... kwanza nilikuwa nafikiri labda mrija wa soda ungeweza kufanya kazi, ahahah... lakini nikatafuta bomba la peni kabisa na kufanya hivyo. Nikamwekea hapo alipokuwa amechanika... yaani nikaingiza ndani, aisee! Nikikumbuka..." nikaongea kwa hisia.
Miryam alikuwa ametulia tu, akiniangalia kwa macho yenye umakini.
"Ndiyo wakaja kumchukua sasa, baadaye... wakampeleka hospitali. Nilikuwa hata sijui kama ingefanikiwa... ila ni Mungu tu. Halafu... baadaye nikagundua kwamba hiyo ishu ni hatari. Ilikuwa bahati ilimwokoa, kama ningemwekea vibaya, me ndiyo ningemuua," nikamwambia hivyo.
Miryam akatikisa kichwa kiasi kwa njia ya kusikitika.
"Haikuwa poa. Ndiyo taarifa zikamfikia baba yake sasa, alikuwa huku wakati huo, na me jina langu likafikishwa kwake. Tulikuja kwenda hospitali na Jasmine kumwona Nuru, yaani... baba yake alitutafuta ndiyo tukapelekwa. Kuanzia hapo ndiyo akaanza kutu-favor mpaka akaja kukutana na mama... imekuwa historia nzuri now," nikamwambia hivyo huku nikiangalia mbele tu.
Nikamtazama hatimaye na kukuta amekaza macho yake mazuri kwangu, kwa njia fulani kama vile anataka kuachia tabasamu.
Nikamuuliza kwa sauti ya chini, "Nini?"
Akatabasamu hatimaye na kusema, "Hamna kitu. Napenda tu kukusikiliza ukiongea."
Nikatabasamu kwa hisia na kumwambia, "Well... nafurahi kujua hilo."
"Inaonekana una mambo mengi sana kwenye maisha yako ambayo nitahitaji kujua... kwa hiyo nitakuwa tayari zaidi kukusikiliza. Ninataka uje uniambie... kila kitu kuhusu wewe," akaniambia hivyo kwa sauti yenye hisia.
Nikatikisa kichwa kukubaliana na hilo, naye akalaza chake begani kwangu tena na kunishikilia kwa njia iliyoonyesha amani.
Kauli yake hapo mwishoni ilikuwa imenifanya niwaze kuhusiana na jambo lingine muhimu zaidi nililopaswa kuja kumwelezea. Juu ya ishu ya mwanangu. Sikuona kwamba lingekuwa gumu mno kwake kumeza, lakini najua nilipaswa kulileta mapema kabisa. Ukitegemea na jinsi ambavyo mambo yalikuwa kwa upande wangu na huyo mtoto ambaye hata sikuwa nimekutana naye bado, mwanamke wangu angetakiwa kuelewa hilo suala kwanza ili nipate wepesi zaidi katika hatua zangu za kushughulika nalo ilivyotakiwa.
★★
Safari ya mwendo wa kasi ikatufikisha Morogoro hatimaye ikiwa imeingia mida ya saa tano asubuhi, nami pamoja na bibie wangu tukatafuta mghahawa mzuri ili kupata chakula kwanza. Jua lilikuwa linawaka kweli kuelekea mida ya saa sita, nasi tulipomaliza kula ndiyo tukachukua taxi ambayo ingetupeleka kule ambako Miryam alidhamiria kwenda. Alikuwa ameshawasiliana na familia yake, hususani Bi Zawadi ambaye alimpigia kujua ikiwa ameshafika. Aliwaacha vizuri huko nyumbani, hata kama ingetokea amechelewa kurejea Dar angekutana nao ukumbini kwenye send-off ya Doris.
Kwa hiyo wapendanao tukapelekwa mpaka kwenye eneo lililojulikana kama Mizani, ikiwa ni barabara iliyoelekea Dodoma, nasi tukaingia ndani ndani zaidi kwenye hizo pande zilizokuwa na maeneo yenye mashamba na viwanja na mapori-pori pia. Niliona kwamba sehemu hizi za huu mkoa zilikuwa zinaendesha ujenzi wa miundombinu mbalimbali, yaani ile iliyokuwa inakuja kwa kasi, kwa sababu viwanja vilikuwa vingi na ni sehemu ambayo ingependeza mno kama hizi harakati zisingekoma.
Tukafika sehemu fulani iliyokuwa na shamba kubwa kweli, likiwa limepandwa mazao ya mbogamboga, mahindi, na viazi nadhani, yaani kwa ile njia isiyo ya kipaumbele sana ingawa yalikuwa mengi. Hili ndiyo lilikuwa shamba la Mariam, na hapo walikuwepo watu kadhaa waliokuwa wakisubiri kwenye kibanda kidogo sehemu za mbele huko, nasi tukaanza kukielekea huku na hao watu wakija kukutana nasi. Walikuwa watano, watatu wakiwa wanawake na wawili wanaume, wote watu wazima, na tulipokaribiana maongezi yakaanza kwa salamu.
Miryam alizungumza nao kwa ustaarabu sana, akitaka kujua yaliyokuwa yanaendelea kufikia sasa. Mwanaume mmoja hapo ndiyo alikuwa akidai kwamba sehemu fulani ya kiwanja chake imeingiliwa, yaani kilipakana na shamba la Mariam, na hawa waliolitunza walikuwa wamepanda mazao mpaka kukiingilia kiwanja chake na kudai sehemu hiyo yote ni yao; yaani kwa niaba ya mmiliki. Alikuwa anataka kukiuza kiwanja chake, na hakutaka iwe mgogoro mkubwa sana kuingiliana na nini, ndiyo sababu alitaka uhakikisho kutoka kwa mmiliki halisi wa hili eneo lingine ili wasije kulaumiana baadaye mengine yakitokea na kusababisha mvurugo.
Ikabidi hadi tupelekwe usawa wa hilo eneo ili tuonyeshwe jambo hilo, naye Miryam ndiyo akaanza kubainisha sasa mambo hakika ya eneo lililokuwa la mdogo wake, karatasi za vipimo na nini, na ikaeleweka kwamba huyo jamaa hakuwa ameibiwa chochote. Alikuwa mbishi haswa, huyo jamaa, yaani hata baada ya kuonyeshwa vipimo na nini akawa anapaisha sauti tu hasa kwa sababu Miryam alitumia heshima kuongea naye akiwa kama mtu mzima. Ikanibidi niingilie kati.
Nikamwambia huyo mzee kwamba ikiwa hakuridhika na uthibitisho aliopewa na Miryam, basi afungue kesi. Tungekuwa tayari kupambana nayo, maana hatukutaka mgogoro wowote wa ardhi na kuanza kukatana mapanga, eti aje tu akate ardhi isiyo yake aiunganishe kwenye ya kwake halafu amuuzie mtu mwingine? Hapana. Kama hakutaka kuamini uthibitisho wa wazi alioletewa na Miryam, basi tungelipeleka hili suala mahakamani, na hapo angekuwa anajisumbua tu maana angrlepoteza wakati, pesa, na labda hata nafasi ya kuuza kiwanja chake.
Miryam pia alikuwa ameshaona kwamba huyo shida yake ilikuwa kuongeza tu upana wa eneo lake ili aliuze kwa gharama ya juu zaidi kwa mnunuzi, kwa hiyo akamwambia aache tamaa, hivi vitu vingekuja kumgharimu maana kama angekuwa mwingine hapo asingekuja kistaarabu. Ni yeye Miryam ndiye aliyekuwa karibu kuibiwa hapo, yaani hilo alilijua, kwa hiyo akamwomba huyo baba aachane na hii kitu kabisa, maana sheria zilikuwepo na alijua haki yake. Ndiyo jamaa akawa mpole.
Maongezi yaliyofuata baada ya hapo yakawa yenye amani kiasi, ikieleweka kwamba hilo eneo jamaa alilosema ni lake lilikuwa ni sehemu ya shamba la Mariam kihalali, kwa hiyo hadithi ikawa imeishia hapo. Ilikuwa ni kusumbuana tu, yaani Miryam kuja huku kote ilikuwa kwa sababu tu waliolitunza eneo la mdogo wake hawakujua kukoromea waliowapandishia sauti, kwa hiyo ilikuwa lazima bibie aje mwenyewe kweli kuweka mambo sawa. Tumekaa hapo mpaka saa nane, ndiyo tukawaacha sasa, na Miryam akiwa amewapatia watunzaji kiasi fulani cha pesa sijui kwa ajili ya nini.
Basi, mission ikawa accomplished, moja kwa moja jambo ambalo lingefuata ingekuwa kurudi kwenye kituo cha stesheni ya treni ili kuwahi kurudi Dar. Kama muda ungekuwa unaruhusu, tungefanya matembezi kidogo, lakini kweli tulihitaji kuwahi huko. Miryam hata hakuwa amejiandaa, katika maana ya kwamba labda aende saluni, ahusike kwa ukaribu na ishu za upendezeshaji wa Doris, yeye mwenyewe kuvaa, yaani alikuwa na rundo la mambo mengi aliyohisi angekosa kutimiza hasa kwa kuwa alihusika kama mwanakamati maalumu kwenye hiyo sherehe, kwa hiyo kujaribu kuwahi lilikuwa suala muhimu sana.
★★
Tukafanikiwa kupata treni ya saa kumi jioni, upesi sana ikatukimbiza kuturudisha Dar na hatimaye kutufikisha huko ikiwa imeshaingia saa kumi na mbili jioni. Miryam alikuwa amewasiliana na Doris kumjulisha kuhusiana na hii hitilafu, kwa hiyo huko wote walielewa kwa nini alikosekana hapa na pale lakini la msingi lilikuwa kwamba angefika tu ukumbini. Yaani hakutaka hata kula tena, akili yote ilikuwa kufika kwenye send-off ya ndugu yake ili kutoa 'support' kwa mwenzake. Nilipenda sana huu utu wake wa kujitahidi mno sikuzote kutanguliza maslahi ya wengine; Mariam kwanza kutokea leo asubuhi, na sasa ingekuwa ni Doris.
Muda ulikuwa unaenda shuta, yaani alikuwa anafikiria kurudi nyumbani, avae vizuri, ndiyo tena tuelekee Kigamboni kwenye ukumbi wa hiyo sherehe haraka, lakini nikamtuliza na kumpa wazo lingine. Nikamwambia twende kwenye moja ya maduka makubwa ya nguo na mitindo pande hizo hizo ili aweze kutengeneza mwonekano wake vizuri kwa ajili ya sherehe, halafu tungeenda huko moja kwa moja. Nikamwambia hata mimi nilikuwa naenda kwenye send-off kama yeye tu, na nilijua tukifanya mizunguko mingi mpaka kurudi nyumbani, tungechelewa, kwa hiyo nikamwomba akubali hilo ili tuokoe muda.
Aliona hilo kuwa wazo zuri, na hata akatania kwa kusema sawa, twende, kwa sababu ya mimi kuwa mtoto wa kishua basi anajua ningegharamikia kila kitu bila kumwaga jasho. Nilifurahi kuwa kwa mara ya kwanza aliridhia mimi kufanya jambo fulani kwa ajili yake bila yeye kuweka migomo kama nilivyokuwa nimemzoea, nasi tukafanya kuelekea kwenye duka moja zuri sana la nguo na mitindo ili tujiweke fresh kabla ya kuelekea sendofuni.
Nikalipia nguo mpya kwa ajili yangu na yeye, yaani yoyote ile ambayo na yeye angechagua, na nikawa nimewaomba wavalishaji wa hapo wamwekee mrembo wangu vito vizuri pia. Mimi nikavaa moja ya yale mashati ya uturuki, la kijivu na lenye mtindo mzuri sana, pamoja suruali nyeusi ya jeans laini pia, na nikanunua na viatu vyeusi (formal) vyenye gharama na kuvitupia, yaani mwonekano rasmi, ungeniona! Nilitokelezea.
Miryam sasa, ndiyo aliniacha kinywa wazi. Alichagua gauni lenye kubana na laini, lenye rangi ya maroon-zambarau na mapambo ya vitu vyenye kuling'arisha, likifunika mkono wake mmoja na mwingine kuuacha wazi. Lilikuwa na mpasuo mrefu mpaka mwanzo wa paja lakini alijitahidi kuusitiri vizuri, na alikuwa amesaidiwa kutengenezewa nywele zake kwa kuzibana nyuma na kuachia mkia wa zilizobaki ulale mbele ya bega lake. Alivalishwa hereni ndefu pia, bangili, na pete nzuri za urembo, huku miguuni akikanyagia viatu vifupi vya kuchuchumia vyenye rangi ya kung'aa ya shaba.
Alitoka na kunifata akiwa ananitazama kwa njia ya subira, ili nimwambie nilichofikiria, nami nikaachia tabasamu hafifu huku nikimtazama kwa hisia sana, halafu nikamtikisia kichwa kuonyesha nimeuelewa mtindo wake. Alipendeza! Ilikuwa kama vile yeye ndiyo alikuwa anaenda kuolewa. Watu wa hapo walituangalia kwa yale macho ya kuinua, yaani tulionwa kuwa kama wateja maalumu sana wakati ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kufika.
Na gharama ya kila kitu ilikuwa ya juu mno mpaka nikatoa kadi yangu ya benki kulipia, na ilifaa maana kuanzia wakati huu, nilikuwa nataka kumwonyesha mwanamke wangu hadhi yake. Ningempa chochote kile yaani ambacho kilimfaa kwa macho yangu, hapa ilikuwa kidogo. Miryam akanishukuru eti kwa kumfanyia kitu kizuri kama hiki, nami nikamwambia asiwaze, ulikuwa ndiyo mwanzo.
Kwa hiyo tulipomaliza kupendezeshwa hapo na kulipia, tukatoka kwa pamoja ikiwa imeshaingia saa moja kuelekea mbili. Tulipendeza, yaani sana! Nguo zetu tulizokuja nazo mwanzoni nilikuwa nimeweka kwenye mfuko kutokea hapo dukani, nami nikakodi usafiri wa Uber utuwahishe huko Kigamboni upesi. Miryam alifahamu kihususa mahali ambapo ukumbi ulikuwepo, maana ilikuwa ndiyo ile ile sehemu waliyofanyia kitchen party ya Doris juzi, hivyo safari ikaanza upesi.
★★
Tumekuja kufika eneo husika la huo ukumbi ikiwa inaenda kuingia saa tatu usiku, yaani send-off ilikuwa imeshaanza. Miryam alikuwa ametafutwa sana na mama zake, Shadya, Tesha, na hata mama yake Doris mwenyewe kuuliza kwa nini alikawia mno, na jibu la haraka ilikuwa ni matatizo ya usafiri. Walimhitaji sana awepo, yeye ndiyo alikuwa kama roho yao pale. Mimi nilikuwa nimeshawasiliana na Ankia, ambaye alisema ametunza sehemu yangu ya kukaa pamoja naye.
Baada ya kushuka sasa, nikamwambia Miryam atangulie huko ndani, maana kwa wakati huu tusingeweza kuingia kwa pamoja ingawa nilitamani sana tufanye hivyo, lakini Miryam akasema hapana, twende pamoja. Nilishangaa kiasi aliposema hivyo, lakini akaniambia haikuwa na shida tukiingia pamoja, ingeonekana tu kwamba tumekutana hapo hapo, siyo lazima ndugu zake wangefikiri tulikuwa pamoja siku nzima. Kwa kuwa aliona hilo kuwa sawa, tukaelekea ndani ya hoteli pamoja.
Ilikuwa ni hoteli kubwa kiasi, magari kadhaa yenye mapambo yakiwa kwa hapo nje, na mziki mnene ukisikika kutokea huko ndani, tukaelekea mpaka malangoni na kukutana na wasimamizi. Walifahamiana na Miryam, hata wakasalimiana vizuri na kumuuliza kulikoni mpaka kuchelewa huko kote. Akaongea nao kifupi tu, na mimi nikiwa nimetulia nikawaonyesha mwaliko wangu, halafu bibie akamwomba mmoja wao achukue mfuko uliokuwa na nguo zetu atutunzie sehemu fulani mpaka baadaye. Ikawa hivyo, na baada ya hapo ndiyo tukaingia sasa.
Ukumbi ulikuwa mzuri, sana, watu wengi wakipendeza na kukaa kwa utulivu MC alipokuwa akiendelea kuweka mambo, nami nikawa nimewaona ndugu zake Miryam kule mbele, wakikaa kwenye meza ndefu na wakiwa wamependeza sana. Miryam pia alikuwa ameshawaona, nasi tukawa tunatembea kwa pamoja tukivuka meza nyingi za watu waliotutazama kwa umakini sana. Miryam angemfikia mtu fulani aliyemfahamu na kusalimiana au kukumbatiana naye, na mimi ningemsubiria tu. Najua kwa baadhi ya watu ingezua swali la ni kwa nini, lakini sikujali. Tuliangaliwa, siyo poa!
Wakati tukiwa tunaelekea mbele zaidi, nikawa nimemwona Ankia, meza moja akiketi na Bobo, mama Chande, Shadya, na watu wengine, nami ndiyo nikamwambia Miryam naelekea hapo. Hakuwa na neno, na familia yake ilikuwa imeshaniona pia, kwa hiyo nikawapungia mkono kwa chini na kutoa ishara kwamba naenda upande mwingine. Ile nimeanza tu kwenda upande wa Ankia, nikamwona Mariam anasimama kutoka kwenye meza ya familia yao na kukutana na Miryam kabla hajawafikia, halafu akasemeshana naye kwa ukaribu huku watu wakiwaangalia.
Mimi nikasonga tu mpaka kwa Ankia, nikapokelewa vizuri hapo, nakwambia hadi Bobo alikuwa amevaa kijentomani mpaka tukachekana kidogo, kisha ndiyo nikaambiwa niagize vinywaji; wahudumu walikuwa wamesimama kila kona. Wakati nataka kufanya hivyo, nikamwona Mariam anakuja upande wetu mpaka akatufikia, halafu akachuchumaa karibu nami na kunishika mapajani kwa mikono yote, asiseme kitu, bali akawa ananiangalia tu.
Nikamwinamia sikioni na kumwambia, "Umependeza Mamu!"
"Asante," akasema hivyo.
"Umekuja kunisalimia?" nikamuuliza.
"A-aah... nimekuja kukuita uje. Njoo ukae na sisi," akaniambia hivyo.
Nikatabasamu kiasi na kusema, "Nafasi yangu ilikuwa huku... huko wanakaa familia. Wakina nyie tu."
"Me nataka uje ukae na sisi, kuna nafasi yako. Ma' mkubwa amesema uje ukae na sisi," akaniambia hivyo.
Nikakaa kisawasawa na kuwaangalia watu wa familia yake kule mbele, nami nikamwona Bi Zawadi akitoa ishara kuwa niende huko. Miryam tayari alikuwa ameshakaa.
Nikamwambia Ankia sikioni, "Nimeitwa kukaa nao hawa, kwa hiyo nawakimbia."
Ankia, akiwa ameshaanza kunywa, akaniambia sikioni pia, "Naona unaelekea kuwa mwanafamilia original."
Nikatabasamu tu na kunyanyuka, na Mariam akanyanyuka pia.
Nikamshika binti mkono na kuanza kwenda huko kwa ndugu zake, yaani tulishikana viganja, na alikuwa akitembea taratibu tu kwa kufuata mwongozo wangu. Najua tulikuwa tukiangaliwa mno, kwa sababu kwa wasiotujua, ilionekana kama vile ukaribu wangu na Mariam ulikuwa wa hali ya juu zaidi, zaidi ya jinsi ambavyo nilimchukulia binti. Mawazo ya namna hiyo najua yalikuwa rahisi sana kuingia kwenye akili za watu, iwe ni nani au nani ambaye ningetembea naye huku nimemshika namna hiyo, hayo mawazo yalikuwepo. Hasa kwa wanawake, walioniona kuwa sukari ya warembo!
Tukafika mezani kwao, hapo akiwepo Bi Jamila, Bi Zawadi, Tesha, mama yake Doris, Dina, wanaume wengine wawili watu wazima, nafikiri mzazi au walezi wa Doris, watoto wadogo watatu, wanawake vijana wawili waliokuwa mapacha, pamoja na Miryam. Mariam akanionyeshea viti ambavyo kilikuwa wazi pembeni yake Miryam, nasi tukaelekea hapo baada ya mi' kushikana mikono na mama wakubwa na kutoa salamu za ishara kwa wengine. Nikakaa katikati ya Miryam na Mariam, huku Tesha akiwa kwa mbele zaidi, nasi tukatoleana ishara za kishkaji na kuanza kuchat bila kuchelewa.
Tesha alikuwa anataka nimwone Happy wake, ambaye alikuwepo hapo ukumbini pia, lakini alikaa sehemu zingine huko nyuma-kati. Bwana, nikafuafa mwongozo wake mpaka nikamwona, na alikuwa mwanamke mzuri, mweupe. Tesha alikuwa anatamani sana kwenda kukaa naye, lakini hapa hakuwa na jinsi. Huyo Happy alipendeza pia, na nilitambua kwamba alimzidi Tesha umri kiasi, kwa hiyo nikamtania kwamba mimi na yeye tulikuwa ligi moja. Sikuwa nimemweka wazi Tesha kwamba tayari nilianzisha uhusiano pamoja na dada yake, kwa hiyo alifikiri mpaka sasa bado namfatilia tu Miryam.
Mariam alipenda sana hivyo mimi kukaa nao, akawa ananisemesha mara kwa mara na mimi kumjibu kirafiki, na nikaona kwamba ndugu zake na Doris waliniangalia mara nyingi sana, upendezi wa mwanzo au husuda yaani, sikujua. Sherehe ikiwa inatembea kwa mbwembwe na nini, mimi nilijiweka kwa njia tulivu tu, lakini kila mara niliposhusha mikono yangu kwa chini, sikuwa natulia. Nilianza kumchokoza Miryam kwa kumbonyeza mguuni kidogo, na mara ya kwanza aliniangalia kama kuona ikiwa nilihitaji kitu fulani, lakini sikumtazama na kuendelea kumbonyeza tu bila kuweka hisia yoyote usoni.
Akawa anakitoa kiganja changu kwake, chini-chini, lakini mimi nikaendelea kumchokoza hivyo hivyo. Mwanzoni alionekana kutopendezwa na hilo, lakini nilipoendelea tu, nikawa naona akijitahidi kuzuia tabasamu lake, nasi tukawa tunafanya kama kuipiganisha mikono yetu chini kwa chini, na mchezo ukaendelea hivyo bila wengine kutambua hadi Doris alipomtafuta bwana harusi na kumpata mpaka ulipofika wasaa wa kukata keki. Shamrashamra na nini, wakaanza kuitana, na hapo nilikuwa nimepiga kinywaji kidogo kisicho cha ulevi, hivyo nikahisi haja ndogo.
Sehemu hiyo ya kula keki ikamalizika baada ya wanafamilia wote wa bwana harusi na Doris kwenda na kulishwa keki, na mimi nikalishwa pia eti kama sehemu muhimu ya hii familia. Doris alikuwa mshkaji sana. Baada tu ya kutoka kula keki, ndiyo nikaamua sasa nielekee kutafuta vyoo ili nishushe haja maana mkojo ulikuwa umekaza kweli. Nikafanikiwa kukipata choo na kutuliza hali, vyoo vikiwa upande ghorofa la juu kutokea ukumbini, na ile nimetoka tu ili nirejee huko, nikawa nimekutana na mwanamke hapo ambaye alisimama kwa kuegamia ukuta wa korido lililotenganisha sehemu iliyoelekea kwenye vyoo vya wanaume na wanawake.
Alikuwa mtu mzima, mwenye mwili mnono haswa. Nilimwangalia vibaya mwanzoni na kutaka kumpita, lakini nilipoona akinitazama moja kwa moja tu kwa umakini ndiyo nikasimama na kugundua kuwa nilimfahamu. Huyu mwanamke ndiye yule niliyekutana naye kule Masai wiki kadhaa nyuma, ambaye alinielewa sana mpaka tukaja kukutana na kutoka kimapenzi kwa siku moja tu, yaani Rukia. Yule mshangazi! Ulikuwa umepita muda sijamwona, na tuliacha kuwasiliana maana nilimpiga chini kwa kutojibu yoyote kati ya jumbe alizojaribu kunitumia baada ya ile siku niliyomtandika hotelini.
Sikuwa nimetarajia kabisa kumwona tena, hasa sehemu hii, ila kwa jinsi alivyokuwa amesimama hapo, ni kama alikuwa akinisubiria. Watu wengine walionekana wakipita huko mbele mbele na wadada kwenda vyooni. Nikaamua kupiga hatua chache na kufika karibu yake huyu mwanamke, naye akatabasamu kiasi na kuniangalia kwa njia yenye upendezi.
"Mambo?" akaniambia hivyo, na sauti yake tulivu ya kimama.
"Fresh, vipi?" nikamwambia hivyo, nikiwa makini.
"Safi. Umependeza..."
"Na wewe pia."
"Asante. Mbona huonekani siku hizi?"
"Nipo. Na wewe?"
"Mhm... na me nipo. Nimekuona wakati unaingia, ulikuwa na yule dada mzuri wa pale mtaani. Ndiyo nyama yako sasa hivi?" akauliza hivyo.
Nikavuta pumzi na kuishusha taratibu, nami nikamwambia, "Ona dada, najua kuna sehemu nimeshatembea na wewe, na...."
Kabla sijamaliza kuongea, akatupita mwanaume mwingine hapo akiwa anaelekea huku chooni.
Nikamwambia Rukia, "Hii siyo sehemu nzuri, tutaongea siku nyingine."
Nikataka kumpita, lakini akasimama mbele yangu na kuuliza, "Lini?"
Nikabaki nikimtazama usoni kwa utulivu. Alionekana kama amechangamshwa na pombe kwa mbali.
"Nimekutafuta mara ngapi hujanijibu? Tokea siku ile ukaniahidi utakuja kuni...."
"Nisikie. Hayo yameshapita, sawa? Ile ishu...." nikasema hivyo na kutoa ishara kwa kiganja kuwa hiyo ishu nimeichinja.
"Basi kumbe we' ni escort tu," akasema hivyo.
"Nini?"
"Hiyo siku ulisema we' siyo kaka poa, nikakuchukulia serious. Kumbe ulikuwa unadanganya. Unatoka tu na wanawake wenye pesa, halafu unahama ukimaliza..." akasema hivyo.
"Hivi wewe... me nilikufata? Si ulikuja kwangu mwenyewe? Nilikuomba hela kwani?" nikamuuliza hivyo.
"Lakini nilipokupa si uliichukua?"
"Oh, kwa hiyo kumbe unataka tu nikurudishie hela zako?"
"Siyo hivyo..."
"Nikumbushe ulinipa shi'ngapi nikupe," nikamwambia hivyo.
"Sitaki unipe hela... hela ninayo."
"Unataka nini sasa?"
"Nakutaka wewe," akasema hivyo.
"Eh, aheh... dada... sahau. Unanielewa? Nikikwambia imeisha, imeisha. Kuna wanaume wengi humo, katafute yeyote akutulize kama unaona mmeo hakupi satisfaction. Mimi siko available tena," nikamwambia.
"Mmm?" akafanya hivyo kikejeli.
"Eeh. Na kama msemo wa Rose Muhando, 'nipishe nipite,'" nikamwambia hivyo.
"Ngojaaa..." akasema hivyo na kunizibia njia tena.
Yule jamaa aliyekuwa ameenda chooni akapita tena, akituangalia mara mbili mbili.
Nikamwambia Rukia, "Sitaki scene dada'angu. Naomba uelewe hilo."
Akatabasamu na kusema, "Scene kama ile uliyomwonyesha Naomi siku ile Masai?"
Nikaweka uso makini.
"Mdogo wangu aliniambia ulimkataa, ukampasulia na chupa. Alikuwa hajui kama nimeshapita na wewe..." akaniambia hivyo.
"Nisikie. Sitaki niwe mkali. Kuna amount ndogo ya heshima niliyonayo kwako dada, sitaki iishe kwa sababu nikiwa mkali nakuwa mbaya. Naomba uelewe kwamba sita...."
Kabla sijamaliza kuongea, Rukia akaweka mkono wake sehemu ya kati kwenye suruali yangu na kuishika mashine yangu ikiwa kwa ndani, halafu akaikamata kwa nguvu pamoja na mipira ya uzazi na kuviminya kwa njia iliyofanya niumie kiasi!
Nilishtuka, na yeye moja kwa moja akanifata mdomoni huku akinisukuma kuuelekea ukuta. Akanibamiza hapo huku akilazimisha denda na mdomo wake ulionuka pombe, yaani eti akitaka kunipa penzi la kibabe, nami nikautoa mkono wake kwa nguvu hapa chini na kuigeuzia nguvu ya limwili lake igeukie ukutani, hivyo nikawa nimemwepuka na kusogea pembeni.
Nikawa nataka nianze kwa kumnyooshea kidole na kumwambia asije kamwe kurudia kunisogelea tena, lakini pale nimeangalia pembeni tu, hapo mbele niliweza kumwona Miryam akiwa amesimama usawa wa njia iliyoelekea kwenye vyoo vya wanawake, akinitazama kwa macho makini sana. Nilichoka!
Nikamwangalia bibie usoni kwa macho yenye wasiwasi, yeye akiwa ananiangalia mimi na Rukia kwa njia iliyoonekana kuwa ya umakini wa kawaida tu, nami nikajifuta mdomo na kuanza kupiga hatua kumfata huko, lakini Miryam akageuka hapo hapo na kuelekea ndani ya vyoo vya wanawake moja kwa moja. Aisss! Hii ingekuwa mbaya, aisee, CV yangu ilikuwa imechafuliwa ghafla sana. Yaani hapo sijui ingekuwaje!
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Pata Full Story WhatsApp au inbox
Whatsapp +255 678 017 280
Karibuni sana