MIMI NA MIMI 2
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA ISHIRINI NA TISA
★★★★★★★★★★★★★★★★★★
Siku ikaja mpya. Ijumaa. Eh bwana eh, usiku wa jana JC nilitoka kupewa bonge moja la tetemeko la moyo, baada ya mwanamke niliyempenda kukiri ananipenda, lakini asingeweza kuwa nami kimahusiano. Ilinivunja moyo, hasa kwa kuwa sababu alizotoa kuhalalisha msimamo wake zilikuwa za maana. Nilihisi kushindwa, kwa sababu bado nilitaka nimkamate awe wangu, nimwonyeshe picha kamili ya jinsi ambavyo nilimpenda, lakini hali zikaonekana kupinga hayo. Maneno yake yaliendelea kuzunguka akilini mwangu usiku kucha, yaani nilikuja kupata usingizi kwenye mida ya saa kumi usiku.
Hiyo jana, baada ya wanawake kuondoka hapo kwa bibie, walitumia muda wa kama masaa manne au matano hivi huko kwenye sherehe, na wakaja kurudi ikiwa imeshaingia saa saba usiku. Sikuwa mfatiliaji sana wa mambo ya kitchen party kwa hiyo sikujua huwa zinachukua muda gani, ila naona hiyo ya Doris ilichukua muda mrefu zaidi ya kawaida, ungesema ilikuwa ni send-off yenyewe. Na send-off yenyewe ingefanywa Jumamosi.
Walirudi na kufikia kupumzika, Ankia akiwa amelewa kidogo tu kwa kunywa bia chache, na alinikuta nimejilaza kitandani kwangu kama vile sina habari. Nilikuwa kwenye huzuni na nini, lakini nilimtendea vizuri na kumpeleka akalale tu huko chumbani kwake, kisha ndiyo nikafunga milango na kurudi tena ndani. Sikwenda kwa Miryam tena. Yaani sikuuliza mambo yalikuwaje huko wala nini, ilikuwa ni kurudi tu kitandani na kupambana na hisia zangu.
Kwa hiyo hii leo nimekuja kuamka mida ya saa tatu asubuhi, lakini nikaendelea tu kulala hadi kwenye saa nne. Ankia akaja kunisemesha, na baada ya kunyanyuka, akawa ameona huzuni yangu. Pombe ilikuwa imeshakata kichwani kwake, yaani aliamka vizuri sana na kwa utayari wa kwenda dukani kwake, lakini akaona akae kwanza ili ajue nilikuwa nimehuzunishwa na nini. Yeye kuwa mtu pekee aliyeelewa suala langu na Miryam kwa undani, nikaona nimwelezee tu ukweli wote.
Mwanzoni nilipomwambia kwamba Miryam alikiri kunipenda, Ankia alifurahi na alishangaa sana, na hata kushangaa zaidi kwa nini hilo liwe jambo ambalo lingefanya nikose raha badala ya kunirusha-rusha kwa furaha. Ndiyo nilipomwelewesha yale ambayo Miryam aliyasema baada ya kukiri upendo wake kwangu, Ankia akasikitishwa sana na jambo hilo. Sikujua nifanye nini baada ya hayo, maana nilihisi kama vile mafuta ndani ya gari la ushawishi wangu kumwelekea Miryam yalikuwa yanakaribia kuisha, hilo gari lingesimama tu bila kupenda.
Lakini Ankia akanitia moyo. Akaniambia nisikate tamaa, aliona bado uwezekano wa kumfanya Miryam awe wangu ulikuwepo. Akasema nilihitaji kujua tu jinsi ya kumfanya yule mwanamke aache kuogopa, maana alijua tukiwa wote, mimi ndiyo nitakuwa nguvu yake na kumfanya ajihisi salama. Hivyo ningepaswa kufanya jambo fulani ili Miryam ahisi hivyo.
Nikamwambia sikujua sana nifanye nini tena maana nilikuwa nimeshafanya mengi mno mpaka ingeanza kuonekana ninaigiza, ama namtaka kimaslahi tu, lakini najua ushauri wake ulikuwa sahihi. Mimi mwenyewe sikutaka kukata tamaa hivi hivi tu, ingekuwa ni lazima nijaribu tena kumfanya mwanamke huyo atambue kina cha upendo wangu kwake. Ankia akanitia moyo kuwa ndiyo, nijaribu tena, na hata akasema anajua ningefanikiwa tu. Kama Miryam alikuwa amenipenda tayari, woga ulikuwa kitu gani? Ningepaswa nipigane haswa.
Huo ndiyo ukawa wosia wa mapenzi wa mama mwenye nyumba wangu. Nikamshukuru kwa hilo, naye ndiyo akawa anataka kuondoka sasa kwenda kufungua duka huko Mzinga mida hii ya saa tano. Akaniambia chai ilikuwepo na mkate, nami nikampa shukrani kwa jitihada zake za kirafiki na kumwahidi kumpa zawadi mambo yakienda vyema. Kwa hiyo akaniacha hapo nikiwa nimepata motisha mpya ya kujaribu kumfikia Miryam kwa mara nyingine tena, na zamu hii, ingekuwa ni jaribio la mara ya mwisho.
★★
Kilichofuata ikawa ni kwenda kupiga usafi wa mwili, nikanywa chai, kisha nikavaa vizuri kabisa na kwenda pale kwa wapendwa wangu kuwapa salamu. Wote walikuwepo isipokuwa Miryam na Tesha pekee. Miryam alikuwa kazini, na nikaambiwa Tesha alikuwa ameondoka kwenda kufatilia nafasi fulani ya kazi maeneo ya huko Chamanzi. Shadya na Mariam walinisimulia mambo waliyojionea jana kwenye kitchen party, Mariam akiongea kwa njia chanya, lakini Shadya akipondea sehemu fulani za hafla hiyo, nami nikajitahidi tu kuonyesha utulivu na kuwachangamsha kwa maneno ya hivi ama vile.
Nimekaa nao hapo hadi kwenye mida ya saa saba mchana, ndiyo nikawaaga kwa kusema kuna miadi nafatilia huko Rangi Tatu mara moja, kisha ningerejea ili kuwapa ushirika zaidi. Hawakuwa na neno, na baada ya kuagana nao, nikaenda kwa Ankia tena na kuvaa viatu, kisha nikafunga nyumba na moja kwa moja nikaelekea mpaka Mzinga ili nipande daladala za kwenda huko Rangi Tatu kweli. Njia niliyotumia ilinipitisha dukani kwake Ankia, nami nikaamua kumfata hapo.
Nikamwambia kuwa hapa ndiyo nilielekea huko kazini kwake bibie, nikiwa naenda kufanyia kazi ushauri wake alionipa saa zile. Ankia akafurahi kweli na kusema mchumia juani hulia kitandani, na ni kweli maana kama ningefanikiwa kumkamata yule mwanamke, kitanda kingekoma! Tuliongea kwa utani, lakini alinipa moyo sana wa kwenda kufanikisha hitaji la moyo wangu, nami nikamwacha hapo vizuri na kwenda kuchukua usafiri hatimaye. Kulikuwa na ishu ya daladala kuchelewa mno kufika hapo, na ili kuepuka kuunguzwa na jua, nikaamua kupanda bajaji badala yake.
Vuuu... nikafika Rangi Tatu, nikatembea mpaka Zakhem na kuchukua bajaji tena, kisha ndiyo nikaelekea huko Upendo, Kijichi. Nilikuwa na misisimko, we acha tu! Baada ya maongezi yetu jana, sijui huyo mwanamke angeitikia vipi huu usumbufu wangu wa mara nyingine tena, lakini iwe isiwe, lazima angepaswa kujua tu. Ni yeye tu. Wa moyo wangu tu.
Nikafika hilo eneo, taratibu tu nikasonga mpaka kufikia jengo lake bibie la kikazi, na gari lake lilikuwepo hapo nje. Nilienda nikiwa natarajia kwamba na leo angekuwa peke yake, lakini nilipoingia hapo ndani, nikakuta msaidizi wake akiwa amekaa kwenye meza yake. Tabasamu la furaha likaniponyoka bila kulazimisha.
"Soraya!"
Nikaita hivyo kwa hisia za furaha sana. Kweli ilikuwa ni Soraya, mwanamke mzuri sana ambaye naye nilikuwa nimeshapita naye, na aliokoka janga baya sana la kifo baada ya kuumwa na nyoka mwenye sumu kali ile juzi juzi.
Sikutarajia kabisa kukuta amesharudi kazini mapema namna hii. Alivalia nguo laini ya Punjabi, yenye rangi ya pink, na mamitandio mengi-mengi kuizunguka hadi kufunika kichwa chake. Uso wake wenye tabasamu zuri kunielekea ulipendeza sana, akiwa haonekani kuwa mgonjwa hata kidogo, naye akatabasamu hata zaidi na kunyanyuka kutoka kitini.
Akasema, "JC. Mambo?"
"Ahah... safi. Wee... unaendeleaje?" nikamuuliza hivyo kwa kujali.
"Kama unavyoniona..." akaongea kwa upole.
"Aisee! Nafurahi sana kukuona. Una hakika afya inaruhusu kuanza kazi mapema? Haukuhitaji kupumzika zaidi?" nikamuuliza hivyo.
"Hamna, yaani nilipotoka tu hospitali jana ndiyo nikapumzika, leo nimekuja. Afya iko poa," akasema hivyo.
"Ahaa... vipi hapo?" nikamuuliza hivyo.
Niliuangalia mkono wake, naye akafanya kupandisha nguo yake juu kiasi sehemu hiyo ya mkono. Bado ulikuwa umefungiwa bendeji laini kuzungukia jeraha lake la meno ya nyoka.
Akiwa ananionyeshea, akasema, "Pako sawa. Kunakuwa tu na miwasho ya hapa na pale, ila nimeambiwa baada ya siku kadhaa naweza kuitoa hii... kitakuwa kimeshakauka."
"Yeah, ni sahihi. Jitahidi usipalowanishe pia, sijui hata unaoga vipi..."
"Hahah... naweka mfuko pasiguswe na maji. Usijali JC, niko sawa," akasema hivyo huku akitabasamu, naye akaufunika tena mkono wake.
"Sawa sawa. Angalau," nikamwambia hivyo.
"Vipi kwenu?" akauliza.
"Tuko poa. Na wewe? Familia?"
"Wazima tu."
"Nilisahau kukwambia nilikutana na Arafat siku ile tumekupeleka hospital," nikamwambia.
"Ahah... kumbe mlikutana?" akauliza hivyo kwa aibu.
"Ndiyo. Mumeo ni mtu mzuri. Anakupenda sana," nikamwambia.
"Ndiyo. Nimeshatambua hilo. Na ndiyo maana nimeamua ku... kutulia sasa hivi. Naomba nisamehe kukusumbua sana, eti? Nili... nilikuwa...."
"Usijali Soraya. Usiombe samahani. Nakuelewa," nikamwambia hivyo kwa upole.
Akatabasamu na kusema, "Asante."
Nikatikisa kichwa kama kumtia moyo. Nadhani ikawa imeshaeleweka kwamba jambo lile baina yetu ndiyo lingetakiwa kufikia ukomo, maana hata yeye alionekana kutaka kutulia kwenye ndoa yake kikweli wakati huu kutokana na jinsi ambavyo mume wake alimwonyesha upendo. Siyo mbaya lakini kwamba hatukukutana tena kimwili, angalau tayari alikuwa ameshashiriki na mimi mara mbili. Ilitosha.
"Umekuja kumwona da' Miryam?" akawa ameniuliza hivyo.
Nikatikisa nyusi kukubali.
"Yupo ndani huko. Nenda tu," akasema hivyo.
Nikatabasamu kiasi na kusema, "Je kama hataki kusumbuliwa, utajuaje? Si bora umpe taarifa kwamba ana mgeni?"
"Hamna, sidhani ina shida. Ingia tu, maana we' siyo mgeni rasmi, si mnajuana?" akasema hivyo na kuketi tena.
Nikasema, "Yeah. Asante. Ngoja nimcheki."
"Poa. Karibu," akasema hivyo.
Basi, nikampita Soraya kiroho safi na kuufikia mlango wa ofisi ya bibie, nami nikaamua kufungua tu bila kugonga hodi wala nini. Nikaingia tu hapo mwanzoni na kumkuta Miryam akiwa ameketi kwenye kiti chake cha kibosi kama bosi aliyekuwa yeye, na alikuwa ameegamia mkono wa kiti hicho huku akiushikilia uso wake kwa kiganja chake.
Macho yake mazuri yalielekea hapo mezani ambapo laptop yake ilikuwa imefunguliwa, akionekana kuangalia jambo fulani kwa umakini, na nadhani ilikuwa ni filamu fulani. Alivalia kwa njia nadhifu, blauzi rangi ya maziwa iliyokuwa pana kiasi pamoja na sketi ndefu yenye kubana ya samawati, na nadhani alikuwa amepaka kucha zake ndefu kiasi rangi nyekundu ile ile jana, sema sikuwa nimetambua, na sasa ndiyo nikawa nimeona. Na nywele zake alikuwa amezibana kwa mtindo ule ule niliombania jana.
Nadhani alijua mlango wa ofisi yake ulifunguliwa, lakini hakutazama huku kwa sababu ya kutokuwa na matarajio kwamba ingekuwa ni mgeni. Labda alifikiri ni Soraya. Kwa hiyo ile ameleta macho yake upande wangu hatimaye, kiganja chake kikamtoka usoni na mwili wake kuacha egamio lake, akiniangalia machoni kwa utulivu, lakini kwa kutotarajia. Bila kumsemssha lolote, nikasogea ndani zaidi na kuufunga mlango, halafu nikaelekea mpaka usawa wa meza yake na kusimama huku namwangalia kwa hisia tulivu.
Miryam akaonekana kuishiwa pozi kiasi, siyo kwa njia mbaya, yaani ile kwamba baada ya yeye kukiri jana kuwa alinipenda, halafu akakataa mahusiano pamoja nami, ndiyo nadhani ni kitu kilichomfanya aishiwe raha aliponiona. Akafunika laptop yake na kuendelea kuangalia chini tu, huku akiunganisha viganja vyake hapo mezani.
Nikamwambia, "Miryam, habari za wa...."
"Unataka nini, Jayden?" akanikatisha kwa kuuliza hivyo na sauti yake tamu, akiwa hataki kunitazama usoni.
"Nilitaka tuongee," nikamwambia hivyo kwa sauti tulivu.
"Kuhusu nini?" akauliza.
"Kuhusu mimi na wewe," nikamwambia hivyo.
"Nafikiri niliongea ya kutosha jana. Naomba uongee jambo tofauti, ikiwa halipo, unaweza kwe...."
"Miryam ni wewe tu ndiye uliyeongea jana, naomba nafasi na me ndiyo niongee sasa hivi..." nikamwambia hivyo.
"Najua utakachosema, Jayden. Lakini point yangu itabaki kuwa pale pale. Haitabadilika," akaniambia hivyo na kuniangalia usoni.
"Ni sawa. Haina shida. Lakini nakuomba tu unisikilize," nikamwambia hivyo kwa hisia.
"Ah..." akafanya hivyo na kuangalia pembeni, halafu akanyanyuka kabisa na kujishika kiunoni huku akielekea upande mwingine wa ofisi.
"Sijaja kukulazimisha kwa chochote, Miryam... nilikuelewa. Nahitaji... nataka tu na me unielewe," nikamwambia hivyo kwa sauti tulivu.
Akawa amefikia usawa wa dirisha na kusimama hapo, akiishikanisha mikono yake usawa wa tumbo na kuangalia huko nje kwa njia fulani ya huzuni.
Nikapiga hatua chache kumwelekea, nami nikasimama umbali mfupi kutokea aliposimama yeye na kumwambia, "Nilitafakari yote uliyosema jana. Na... nimeona kwamba uko sahihi kwa mengi, lakini siyo yote. Miryam... hakuna mahusiano yoyote ambayo hayatakuwa na vikwazo, changamoto, matatizo... lazima yatakuwepo. Wakati mwingine unaweza ukajaribu kuyaepuka lakini bado ukaishia kuumia kwa sababu yatakuja kivingine tena. Ndiyo maisha. Huwezi... huwezi sikuzote kukimbia matamanio ya maisha uliyonayo kwa sababu tu unaogopa kuumia, kwa kuwa tu uliwahi kuumia... ingekuwa ni kama watu wote waache kuendesha magari kisa tu wanajua kuna ajali, ni kitu ambacho...."
"Jayden, sitaki unipe madarasa yako. Hizo falsafa peleka huko huko... me... nimeshakwambia nilichokwambia, na itabaki kuwa namna hiyo. Unajisumbua tu," akaniambia hivyo bila kuniangalia.
Nikaangalia chini kwa huzuni kiasi, nami nikamuuliza, "Unakumbuka tulivyokutana mara ya kwanza?"
Akabaki kimya tu na kushusha pumzi taratibu.
"Najua unakumbuka. Nilikuudhi, na ni kitu ambacho kilifanya uumie kwa kipindi kirefu japo hata hukuwa unanifahamu vizuri. Tokea hicho kipindi, nilikuwa nimeshaona namna ambavyo moyo wako ni mwepesi kuumia, lakini ni mkuu sana kwenye kupenda, kwa jinsi tu ulivyowatendea ndugu zako, hata Joshua... na hilo ni jambo lililokufanya uwe imara kusimama kwa ajili yao... licha ya matatizo yote yaliyowapata. Hiyo ni sehemu kubwa sana ya mambo yaliyonifanya nikupende... na nimetamani... kukuonyesha huo upendo kwa sababu najua na wewe unastahili kupata mtu wa kusimama kwa ajili yako pia..." nikamwambia hivyo kwa hisia.
Akawa ametulia tu huku akikaza macho yake kuelekea huko nje.
"Umenifanya nimekuwa imara zaidi Miryam kwa njia ambazo huwezi hata kuelewa, yaani nimesimama huku huu muda wote... ilikuwa kwa ajili yako... na ninataka kuendelea kuwepo kwa ajili yako. Usiache fikira za maumivu na vikwazo zikuzuie kuona jinsi upendo wangu kwako ulivyo mkuu kama moyo wako Miryam... jinsi ambavyo huu upendo utayafunika hayo matatizo yote unayohofia, na kukupa furaha hata nyakati zikiwa ngumu..." nikasema hivyo kwa sauti yenye hisia sana.
Akaibana midomo yake huku macho yakipepeseka huku na kule, nikiona wazi kwamba alikuwa anazizuia hisia zake.
Nikasogea mpaka usawa wa sehemu aliyosimama, nami nikamwambia, "Tumepitia panda shuka nyingi ndani ya hii miezi miwili tokea tulipokutana, na... ijapokuwa ni muda mfupi tu ila... nimeona mengi kuhusu wewe ambayo yakafanya nikupende. Una moyo mzuri Miryam, una... unawajibika, ni mwanamke imara, yaani siwezi kuelezea ni namna gani umenifanya nitamani kuwa mtu bora tena kwa sababu tu ya kukuangalia. Na sasa ninajua nitakuwa bora hata zaidi nikipata nafasi ya kuwa pamoja nawe, siyo kukuangalia tu, ndiyo maana nimeiomba Miryam... nafasi ya kuwa pamoja nawe..."
Akaendelea tu kujikaza na kubaki kimya, akitaka nione kwamba hakujali maneno yangu.
"Yaani Miryam... nime-change sana toka nilipokuja huku, toka nilipokujua, toka nilipotambua hisia zangu kwako... mpaka umenifanya nimejua kubembeleza... ahah... yaani ni kitu ambacho sikuwa nacho kabisa. Naongea tu bila kufikiri kwa sababu kila kitu nachokwambia kinatoka moyoni... na ninakuwa najisikia vizuri sana kwa sababu... ninakuambia wewe. Nime... nimepita sehemu fulani maishani mwangu ambazo zimenivunja vipande-vipande ndani ya moyo wangu, nimejaribu kujifanya kama vile niko sawa kwa muda mrefu, lakini baada ya kukujua... nikatambua nilikuwa nakosea. Si... sikuhitaji kuficha... hisia zangu, yaani... siyo kitu ambacho kingenisaidia. Hivyo vipande ndani yangu vimehitaji kuunganika, ili niwe whole... na nimetambua kwamba ni wewe ndiye unayeweza kuviunganisha. Wewe pekee Miryam..." nikamwambia hivyo kwa hisia sana.
Akaendelea kuwa mtulivu tu.
"Lakini siyo kwamba nitakuwa mbinafsi. Ninakwambia haya ili ujue tu, kwa sababu ndiyo ukweli wangu. Usifikiri kwamba moyo wako ni mzito mno mimi kuweza kuubeba, kwa sababu ni huo huo ndiyo umeniita ili nije kuukumbatia. Haina haja ya kuogopa, vikwazo vipo, hata kama utadondoka Miryam, nitadondoka pamoja nawe pia. Ila sijataka kuingia pendoni mwako ili kuja kukuangusha Miryam, bali kukuonyesha kwamba hauhitaji kuendelea kusimama mwenyewe... kwa sababu Miryam tukisimama pamoja... hakutakuwa na uwezekano wa kuanguka. Nilichokuwa nahitaji ilikuwa ni hiyo nafasi ya kusimama karibu yako, karibu na hisia zako. Nafasi tu Miryam wangu..." nikamwambia hivyo kwa hisia sana.
Akaibana zaidi midomo yake huku uso wake ukikunjamana kwa hisia, na chozi likawa limemtoka.
Nikamshika sehemu ya kiwiko taratibu, halafu nikasogea karibu zaidi na mwili wake kutokea nyuma, nami nikamwambia, "Nakupenda. Naomba tu unipe nafasi ya kukuonyesha hilo Miryam. Tafadhali. Niruhusu niukumbatie moyo wako. Usihisi kwamba kila kitu kitaharibika, nikiwa nawe, sitaruhusu hilo. Please..."
Nilikuwa namsemesha kwa kubembeleza, aisee! Sikufikiria ningekuja kufika huku. Yaani JC kubembeleza mwanamke, ujue nilikuwa nimempenda mno. Miryam akavuta pumzi ndefu na kuishusha taratibu, halafu akajifuta chozi lake upesi na kukishika kiganja changu mkononi mwake. Nikiwa na matarajio mengi hapo, mwanamke huyu akakitoa kiganja changu kwake na kuondoka karibu yangu, naye akaenda zake usawa wa meza na kusimama hapo huku akiinamisha uso wake. Dah!
Nafikiri hilo likawa jibu tosha. Bado aliona uwezekano wa kunipa nafasi kimahusiano ulikuwa mgumu mno, na baada ya kubembeleza huko kote nikawa nimeshindwa kumshawishi kwa mara ya mwisho kabisa. Nilijisikia vibaya mno. Nikafumba macho na kutulia kwa sekunde chache kuiacha hali hiyo iutikise moyo wangu jinsi ilivyotaka, nami ndiyo nikamgeukia na kumtazama kwa hisia sana. Kunipenda alinipenda, lakini alikuwa anaogopa kuingia kwenye bahari ya mapenzi pamoja nami ili tuogelee. Hapa sikuwa na namna tena. Ningepaswa tu nimwachie.
Nikajipa tu utulivu wa kihisia, kisha nikasogea hadi usawa wa sehemu aliyosimama na kumwambia, "Miryam, it's okay. Usijali. Nakuelewa."
Akashusha pumzi kwa njia ya huzuni, huku akigoma kuniangalia usoni.
"Hey... usijisikie vibaya, sawa? Nakuelewa. Na kwa kila kitu, tokea tumejuana, mpaka sasa... naomba tu nikushukuru. Umekuwa sehemu nzuri na bora zaidi kwenye maisha yangu. Sitasahau hilo..." nikamwambia hivyo kwa hisia.
Akafumba macho na machozi kuanza kumtiririka, akijikaza asitoe sauti yoyote. Ah, yaani kulikuwa na hisia nzito hapa! Nilihisi kama vile niko kwenye drama yaani!
Nikamwambia, "Asante. Nakuahidi... sita... sitakutia pressure tena, Miryam. Sitakusumbua tena. Nakuahidi hilo. Nisamehe tu kwa kuwa mbinafsi na nini, lakini... ubaki ukijua kwamba nakupenda sana. Sana Miryam."
Nilimwambia hivyo huku mimi mwenyewe nikilemewa na hisia mpaka machozi kunivizia, naye akawa analia bila kutoa sauti na kujifuta machozi huku na kule.
Nikashindwa hata kujua nifanye nini ili kutoa faraja iliyomfaa yeye kwa wakati huu, na kwa kuwaza labda kumwacha tu ndiyo ingekuwa busara, nikamwambia, "Asante kwa kunisikiliza. Tu-tutaonana baadaye..."
Akaniangalia usoni kwa uchungu sana, kisha akafanya kugeukia upande mwingine kabisa na kufunika pua na mdomo kwa kiganja chake kama anaficha kilio yaani, sijui hata ni nini kilimuuma sana, nami nikaamua tu kumwacha hapo na kuelekea nje hatimaye. Yaani tena nikatoka ofisini kwake na kumpita Soraya hapo alipoketi kama vile sijamwona, nami moja kwa moja nikaelekea mpaka barabarani nikiwa najisikia vibaya mno moyoni. Iliuma wewe!
Yaani nikapanda bajaji na kutulia tu, mtu mwingine angeniangalia angefikiri nilikuwa sawa lakini moyoni nilikuwa naumia mno. Nilikuwa nimemwambia huyo mwanamke kwamba namwelewa, ila nilikuwa nadanganya. Sikumwelewa, yaani sikutaka kumwelewa. Ilikuwa kwa nini anipende halafu asiweze kuwa mwanamke wangu? Pamoja na sababu zote, bado nilijiuliza kwa nini tu hakutaka kukubali niwe mwanaume wake.
Roho iliniuma sana, yaani nilihisi kama vile nimepoteza hazina yenye gharama sana, tena kwa kuiachia mimi mwenyewe. Lakini sikuwa na namna tena. Nilikuwa nimeshambembeleza vya kutosha, alikiri kwamba alinipenda, lakini woga wake ndiyo ukamzuia kunikaribisha jumla ndani ya moyo wake. Alikuwa ameshanifanya zezeta, yaani mpaka mashairi nikawa namwimbia, lakini wapi. Dah! Ambacho kingefuata sasa, ingekuwa kuchukua maamuzi magumu tu, lakini niliyoona yangetufaa sisi sote.
★★
Nimekuja kufika Mzinga ikiwa imeshaingia saa kumi jioni, na wakati natembea kuelekea maskani nikawa nimepita tena usawa wa duka lake Ankia. Akawa ameniona, na mpango wa kwenda hapo tena sikuwa nao lakini nikasimama kwa sababu akawa ameniita ili anisemeshe. Nilikuwa na huzuni wewe, yaani ile amenisogelea tu hapo akawa amehisi kuwa sikuwa sawa kabisa. Kulikuwa na wanawake wengine wamekaa kwenye ubaraza mpana wa vigae sehemu ya duka lake, wakituangalia sana Ankia alipokuwa amesimama kuongea nami.
Mwanamke huyu, baada ya kuniuliza mambo yalikwendaje huko ofisini kwa Miryam, nikaangalia pembeni tu, kukiwa na kitu ndani yangu kilichonichoma sana moyoni kutaka kuisukuma huzuni yangu itoke hapo hapo, na nafikiri akawa ameona hilo. Kwa kuwa sikumjibu, akasema nimsubiri ili twende wote nyumbani kuongea, akionyesha kunijali sana, nami nikatikisa kichwa kukubali na kuanza kuondoka taratibu. Nadhani akawa ameachia mtu hapo asimamie duka kwa niaba yake hadi atakaporejea, kisha akaniwahi na kutembea nami kwa ukaribu.
Sikuongea chochote kile yaani, toka Ankia amejiunga kutembea nami hadi tunafika kwake, aliona ni jinsi gani nilivyokuwa nimetikisika mno moyoni. Nilihisi njaa pia, lakini sikutaka kula. Ile tumefika ndani kwake, nikaketi tu sofani kwa kuegamia na kujishika kichwani, huku simu yangu nikiiweka kwenye mkono wa sofa, nikiwa nahisi kuchoka zaidi kihisia. Yeye pia akakaa pamoja nami kwa ukaribu na kuweka viganja vyake pajani kwangu.
"JC, imekuwaje?" Ankia akauliza hivyo kwa upole.
Nikiwa nimefumba macho tu, nikatikisa kichwa kama kukanusha.
"Kwa hiyo... hiyo ndiyo mara ya mwisho umejaribu kumshawishi na amekataa?" akauliza tena.
Nikatikisa kichwa kukubali na kukaa kwa kuegamiza kiwiko changu kwenye mguu, huku nikitazama pembeni kwa huzuni.
Ankia akasugua bega langu kidogo na kusema, "Pole JC..."
Machozi yakaanza kujaa machoni mwangu, nami nikasema, "Nililiona hili likija. Siyo kwamba nilikuwa naota... au nililitamani. Ila nilijua lingekuja, pamoja na matumaini yote niliyojipa..."
"Unajua sielewi shida anayoona Miryam kwa kweli, ila labda...."
"Hapana, imetosha. Msimamo wake uko pale pale, siwezi kuendelea kumlazimisha..." nikamwambia hivyo kwa hisia.
"Jamani..." akaniambia hivyo kwa huruma.
"Tatizo na me sijui nimekuwaje. Ahah... yaani nali-treat hili suala utadhani ndiyo itakuwa mwisho wa dunia... au utasema nimepawa na ulemavu sasa..."
"JC usiongee hivyo. Kuumia ni kawaida, kumbuka we' ni mwanadamu pia. Hiyo ipo. Mambo hayajaenda kama ulivyotamani, sawa, lakini haimaanishi...."
"Haijalishi, Ankia. Miryam hataki kuwa nami. Hataki. Anaruhusu woga ufunike upendo wake... inabidi tu nimwache kwenye hilo. Na tena me ni mpumbavu, yaani... kweli baada ya yooote niliyofanya, nimechezea wanawake wengine kama vile hisia zao hazina thamani, na Miryam analijua hilo... kweli nilitegemea akubali kuwa pamoja na mtu kama mimi?"
"Unajua hiyo siyo sababu...."
"Inaweza ikawa imechangia, na imekuja kunipiga vibaya usoni kwa sababu ndiyo inanifanya nitambue zaidi na zaidi kwamba simfai. Analijua hilo. Nitamtia aibu..."
"JC..."
"Nitamfedhehesha. Mimi ni mdogo kwake, na nimeshatembea na wanawake wengi, labda anaogopa kivuli cha mapito yangu bado kipo na mimi, na akisema anikubalie.... hhh... Ankia, simfai Miryam. Hata nifanye nini..." nikaongea kwa hisia za kuvunjika moyo.
"Usiongee hayo maneno. Je kama angekuwa amekukubali? Ungesema hivyo?" akaniuliza.
Nikamwangalia usoni kwa hisia.
"Thamani yako anaijua, ndiyo maana amekupenda. Kutokukubali... hiyo ni juu yake yeye, haimaanishi anakuona we' kuwa tatizo. Acha kujilaumu JC..." akaniambia hivyo kwa hisia.
Nikashusha pumzi kwa kufadhaika na kusema, "Najua, Ankia. Najua. Nina... nimeshindwa tu... sijui niwaze nini, yaani... naumia sana yaani... ahh... sijui kwa nini nimekuwa hivi..."
Niliongea huku machozi yakizidi kujaa machoni mwangu, mpaka yakamwagika kabisa na Ankia kuanza kunifuta kwa huruma. Nikavitoa viganja vyake usoni kwangu na kuanza kuyakausha mimi mwenyewe, nisitake suala la kuonewa huruma. Ingesaidia nini?
"Nimekuwa mdhaifu mno..." nikasema hivyo.
"JC..." akaniita kwa upole.
"Miryam amenifanya nimekuwa dhaifu sana Ankia. Sijui ilikuwaje tu yaani mpaka nikampenda huyu mwanamke hivi, lakini... nahitaji tu kumwachia. Seriously yaani, nipite hivi kabisa... na nisiwe namna hii tena. Sitaki tena yaani, ni bora nirudi kuwa jinsi ambavyo nilikuwa mwanzo," nikamwambia.
"Unakata tamaa mapema JC..."
"Unataka nifanye nini sasa?" nikamuuliza hivyo na kumtazama usoni kwa umakini.
Akaniangalia usoni kwa utulivu, kisha akashusha pumzi na kusema, "Unajua JC, unapendeka zaidi ukiwa na furaha ukionyesha unampenda mtu, tokea kwa Mamu mpaka Miryam... umeonyesha utu wako mzuri sana unaokupendezesha zaidi... yaani haufai kuwa kama ulivyokuwa mwanzo. Kabisa. Me naona Miryam amekubadili kwa uzuri, ni bora...."
"Kwa faida ipi, Ankia? Ili nirudi kuhuzunika tena? Haya ndo' mambo niliyokuwaga nakwambia najaribu sana kuepuka... najua yanavyoumiza. Haya, yametimia..." nikaongea kwa uchungu yaani.
"Sasa itakupa faida gani ukianza kuwa jinsi ulivyokuwa mwanzo? Eh? Ndiyo utajisikia vizuri? Utakuwa unamkomoa nani? JC hiyo siyo sahihi, unalijua hilo. Ilikuwaga ngumu mno kwangu kumwacha mume wangu wa kwanza aende... nilimpenda sana. Huzuni ilinitafuna mno, mpaka nikawa siishi kwa utimamu mzuri. Usifikiri sikuelewi, nakuelewa vizuri sana..." akaniambia hivyo.
Nikamwangalia usoni.
"Lakini inapaswa kufikia tu hatua ya wewe ku-move on. Kufanya hayo yote, haitakuwa na faida. Shukuru tu kwamba Miryam amekuwekea kitu kizuri moyoni, kimekung'arisha zaidi... kwa hiyo kutokea hapa ni wewe mwenyewe kusogea mbele zaidi ili uendelee kuwa mtu bora, siyo yule ambaye ulitoka kuwa. Unanielewa JC?" akaongea kwa hisia sana.
Maneno yake yalikuwa ya kweli kabisa. Yalinigusa. Nikahisi faraja kiasi moyoni, maana kiukweli kama siyo Ankia kunitia moyo namna hii, basi huenda ningechukua maamuzi ambayo yangeniumiza tu mwisho wa siku. Hizi ndiyo pindi ambazo mtu unaweza kufanya lolote lile kwa sababu tu ya kuongozwa na hisia, lakini mtu akikutia moyo namna hii ndiyo akili yako inarudi mahali sahihi na kufikiria mambo kwa utimamu unaofaa.
Nikamvuta Ankia na kumkumbatia kwa wororo, yeye pia akirudisha kumbatio langu, kisha nikamwachia na kusema, "Asante Ankia. Umenisaidia sana, hujui tu."
"Najua. Nina busara kuliko unavyodhani, eti ulikuwa unataka kuwa Playboy tena..." akaongea kimasihara.
Nikalazimisha tabasamu na kutazama pembeni tu.
Akasema, "Usijali, tuko pamoja. Haya mambo yapo. Unajua huwezi kushinda kila mechi unayocheza."
"Ni kweli. Tatizo langu ni mechi za kawaida ndo' huwa nashinda, ila ikifika ya kombe lenyewe..." nikasema hivyo na kupiga ulimi kidogo.
"Unamaanisha umeshapitia kitu kama hiki, ndiyo maana ulikuwaga namna ile, eti?" akaniuliza hivyo.
Nikainamisha uso kwa huzuni kiasi.
"Haina haja ya kurudi huko tena. Labda tu Miryam hakuwa fungu lako. Utapata tu mtu mwingine," akaniambia hivyo.
"Dah, Ankia... yaani sidhani nitakuja kupenda mtu mwingine kama hivi. Nampenda sana huyu dada, hajui tu. Yaani mpaka najishangaa sometimes..." nikaongea hivyo kwa hisia.
"Ndo' kama nilivyokwambia, inabidi tu ku-move on. Kwa hiyo utafanya nini sasa hivi?" akaniuliza.
"Labda nikaoge tu kwanza..."
"Sijamaanisha hivyo, kuoga utaoga tu, naongelea... mpango wako. Baada ya Miryam..." akasema hivyo.
Nikatulia kidogo, kisha nikamwambia, "Nafikiri nitaondoka tu."
"Urudi kwenu?"
Nikatikisa kichwa kukubali.
"JC..." akaniita hivyo kwa upole.
"Siharakishi, usijali. Wiki moja ama mbili, ndiyo nitaondoka. Likizo inakaribia kuisha hata hivyo, itakuwa bora tu nikiwa huko tayari kujiweka bize na mambo mengi..." nikasema hivyo kwa uimara.
"Sawa. Ikiwa ndiyo itakufanya ujisikie vzuri..."
"Hamna, sitajisikia vizuri. Lakini kuendelea kukaa tu huku ndiyo... nitajisikia vibaya zaidi, bora kuondoka hata kama bado nitakuwa naumia, lakini hiyo 'zaidi' nitaipunguza-punguza... mhm," nikajaribu kutania kidogo.
Ankia aliniangalia kwa macho yenye huruma yaani, akiwa ameguswa kweli utadhani nilikuwa ndugu yake wa damu labda.
Nikamwambia, "Ngoja tu nikapumzike kidogo, we' rudi dukani. Na usijali, sitajiua... na me najipenda."
Akatabasamu kiasi na kusema, "Utakuwa sawa kweli JC?"
"We' nenda darling, niko poa. Nitatulia tu ndani mpaka ukirudi. Usijali," nikamhakikishia.
Akatikisa kichwa kuonyesha uelewa, nasi kwa pamoja tukasimama.
Ankia akafanya kunikumbatia kidogo tena ili kunipa faraja, nami nikamshukuru na kuanza kuelekea chumbani. Sikatai kwamba alikuwa amenisaidia sana kwa kunitia moyo na nini, lakini bado moyoni nilijihisi vibaya sana. Huzuni ile ya kumwachia Miryam bado ilikuwepo, na isingekuwa rahisi kunitoka mapema sana namna hii, kwa hiyo nikafikiria labda nijilaze kidogo tu kitandani mpaka usingizi unibebe. Mengine ningejuana nayo baadaye.
Wakati ndiyo nimefunga tu mlango na kutaka kukifata kitanda, ukawa umegongwa mara mbili, na Ankia akasikika akiita jina langu. Nikamfungulia na kukuta ameishika simu yangu na kunipatia, akisema niliiacha sofani. Nikamshukuru na kuvuta shavu lake kidogo, naye ndiyo akaniaga kwa mara nyingine tena baada ya kuniambia angewahi kurudi ili tupeane company. Nikafunga mlango tena na kuiweka simu chaji, nami nikaanza kuvua saa na viatu, na ile nataka kuvua T-shirt langu, mlango ukagongwa tena.
Nikatabasamu kiasi maana nahisi Ankia aliona imekuwa ngumu kuniacha kwa sekunde mbili tayari akawa amerudi, nami nikaenda kumfungulia nisikie alichotaka kuniambia. Ile nimefungua mlango, matarajio yangu ya kumwona Ankia yakayeyuka na pigo moja zito kudunda moyoni baada ya kumwona Miryam hapo! Hee!
Nilishangaa. Nikabaki nikimtazama usoni kwa umakini sana, nikiwa najiuliza alifika kivipi hapa ghafla namna hii. Alisimama mbele yangu huku akiniangalia machoni kwa hisia zilizoonyesha mvurugo yaani, nami nikahisi kwamba kulikuwa na tatizo. Aliunganisha viganja vyake usawa wa tumbo, na vidole vyake vilikuwa vinafinyana-finyana kwa njia iliyoonyesha kwamba alikuwa na wasiwasi. Niliingiwa na hisi ya tahadhari maana upesi nikawa nimetambua kuwa alikuwa ndani ya shida fulani, nami nikauachia mlango na kumshika mabegani.
"Miryam... ume... vipi? Kuna tatizo gani?"
Nilimuuliza hivyo kwa sauti yenye kujali sana, naye akainamisha uso wake na kufumba macho.
"Niambie. Kuna nini?" nikamuuliza hivyo tena.
Akaniangalia usoni kwa hisia, naye akasema, "Nisamehe Jayden..."
Nikabaki nikimtazama machoni kwa umakini. Aliongea kwa sauti yake tamu sana, lakini ilijawa na huzuni kuu.
"Sikutaka kukuumiza, ni woga wangu tu ndiyo ulikuwa unanipofusha kweli. Naomba unisamehe..." akaongea hivyo kwa hisia sana.
Mapigo yangu ya moyo yalikuwa yakienda kwa kasi, nikimtazama kwa hisia makini sana kwa sababu ya kuanza kutarajia mengi mno, nami nikayaachia mabega yake na kusema, "Unamaanisha kwamba...."
Machozi yakaanza kujaa machoni mwake, naye akasema, "Sitaki kuwa mwoga tena. Naomba uukumbatie moyo wangu ili nisiogope tena Jayden..."
Ah!
Nilibaki nikimtazama huyu mwanamke machoni utafikiri sikusikia alitoka kusema nini. Yaani... niliyeyuka! Miryam alikuwa ametoka kusema hivyo? Nilihisi kupagawa aisee!
Akalegeza shingo yake taratibu kama kawaida yake, naye akasema, "Nakuomba..."
Nikaachia tabasamu la hisia sana, nikimwangalia kama vile siamini.
Miryam akatabasamu pia kwa hisia huku machozi yakianza kumtoka, naye akanikumbatia hapo hapo na kuning'ang'ania kwa njia iliyoonyesha upendo wenye nguvu sana. Nilihisi kama naota, lakini najua hata mbingu zilielewa hii ilikuwa kitu halisi. Nikarudisha kumbatio la mwanamke huyu taratibu kabisa, nikihisi furaha yenye ukuu usio na kifani moyoni mwangu. Ni furaha ambayo sikuweza kujua upana na urefu wake kwa kweli, yaani sikujali ilikuwaje mpaka huyu mwanamke akaja hapa akiwa amebadili mawazo yake, nilijali tu kwamba mawazo yake yalikuwa yamebadilika.
Nikaangalia hapo sebuleni na kukuta kwamba Ankia bado alikuwepo, akituangalia mimi na Miryam kwa furaha sana, naye akanionyeshea kidole gumba kama kunipa hongera kwa kufanikiwa kumnasa mwanamke huyu. Nikatabasamu kwa hisia sana na kudondosha chozi la furaha, nami nikambana mwanamke wangu vizuri zaidi mwilini nikihisi amani tele moyoni. Ah, aisee! Lilikuwa ni pambano! Kumbe mechi hii sikuwa nimeipoteza, kombe hili hapa sasa nikawa nimekwezwa!
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Pata Full Story WhatsApp au inbox
Whatsapp +255 678 017 280
Karibuni sana 😉