SEHEMU YA 200
Angel nae wakati amelala, alitafutwa kwenye simu na Samir ambaye alianza kuongea nae,
“Angel kipenzi, kumbe huwa unaongea na Mussa mara kwa mara?”
“Nitumie ujumbe Samir, kuongea na simu hapa nyumbani ni tatizo kidogo”
Basi Samir akamtumia ujumbe na kumuuliza kuhusu yeye na Mussa,
“Eeeh naomba nieleze mahusiano yako na Mussa”
“Sina mahusiano yoyote na Mussa, ni vile alikosea namba ya simu na tukaanza kuwasiliana na huwa tunawasiliana kawaida tu”
“Mussa hajawahi kukutongoza?”
“Hapana, sijawahi kutongozwa na Mussa kabisa huo ndio ukweli, yani huwa tunawasiliana tu kama marafiki”
“Naona kabisa wazi kuwa penzi langu litaibiwa, Mussa ni ndugu yangu ila simuamini hata kidogo. Naomba Angel uache tabia ya kuwasiliana na Mussa”
“Ila sina mahusiano na Mussa jamani”
“Ila Angel kuna jambo ngoja nikushauri”
“Jambo gani?”
“Kwanini usimwambie mama yako kuwa akupeleke kwenye chuo cha kujifunza kompyuta ili ujifunze funze wakati unasubiria matokeo ya kidato cha nne? Najua huko itakuwa rahisi sana kwa mimi na wewe kuonana mara kwa mara”
“Mmmh wazo zuri, sasa chuo gani?”
“Usijichagulie, mwache mamako akuchagulie mwenyewe, maana ukijichagulia utamfanya akuhisi vibaya, mwache akuchagulie halafu tutajua cha kufanya”
“Sawa, nitaongea nae kuhusu hilo”
“Ila Angel nakuomba acha kuwasiliana na Mussa jamani, mimi ndio namjua Mussa ni ndugu yangu na sio mtu mzuri kwako”
“Nimekuelewa Samir, hakuna tatizo na hata sitawasiliana nae tena”
“Nakupenda sana Angel, yani kumbuka hilo. Muache Mussa kabisa”
Basi Angel na Samir waliongea sana kiasi kwamba Angel alichelewa kulala, kwahiyo alilala saa kumi alfajiri.
Kesho yake kama ambavyo mama Angel alipanga na mumewe, kwanza alimuita Angel na kuanza kuongea nae,
“Angel mwanangu kitu gani unataka kufanya, ni nini kipo katika akili yako kwa muda huu?”
“Mama, kwakweli nimechoka kukaa nyumbani. Mimi nilikuwa napenda labda hata nikasome kozi ya kompyuta”
“Oooh sawa, itabidi basi uende kusoma na Junior”
Hapo kidogo Angel alikaa kimya kwa muda kwani hakufikiria kama mama yake anaweza kutoa wazo la yeye kwenda kusoma na Junior, ila hakuwa na budi zaidi ya kukubali tu,
“Sawa mama,hakuna tatizo”
Basi mama Angel akawaita wote yani watoto wote kwenye nyumba yake maana siku hiyo ilikuwa Ijumaa na wakina Erica waliwahi kutoka shule, akaanza kuongea nao,
“Jamani, nyie watoto nimewaita hapa ili niongee nanyi mambo ya msingi yanayoendelea, kwakweli tabia mbaya kwenye familia yangu sitaki, mambo ya ajabu ajabu kwenye familia yangu sitaki. Junior, mambo ya kumwambia mwanangu Erick aanze kuwa na wanawake sitaki kuyasikia, Angel na Erica kama ambavyo huwa naongea na sasa naongea tena sitaki kusikia wala kuona marafiki zenu wa kiume hapa nyumbani, nilipiga marufuku hata marafiki wa Erick sababu yenu halafu nyie ndio mniletee maajabu ya dunia sitaki huo upuuzi kabisa. Na wewe Erick, fanya kile unachoona sahihi katika maisha sio kile unachoshauriwa na mtu, kwa kifupi stori za ajabu ajabu kwenye nyumba yangu sitaki. Halafu wazo la Angel nalifanyia kazi, kwahiyo Junior jiandae utakuwa ukienda na Angel kwenye chuo cha kompyuta mkajifunze huko. Sasa Junior wewe ndio utakuwa kama mlinzi wa Angel, akipatwa na tatizo lolote ni wewe ndiye utakaye nijibu, nadhani nimemaliza sasa, mmenielewa lakini?”
Wote waliitikia,
“Tumekuelewa mama”
“Haya mwenye swali aniulize, au kama hamna maswali sasa basi muda wote mtakapokuwa na maswali yenu njooni mniulize nami nitawajibu”
Kisha mama yao akainuka na kuondoka zake, basi watoto wakabaki wanaangaliana na Angel ndio akaanza kusema,
“Ila jamani, mbona siku hizi kama mama kawa mkali zaidi? Yani kila kitu anasema hapendi, tatizo ni nini?”
Junior akajibu,
“Itakuwa mumewe hampi utamu vizuri”
Wote waliinuka na kumuacha Junior peke yake kwani ujinga ujinga walioambiwa kuwa wasizungumze basi ndio Junior alikuwa kama anataka kuuanzisha tena.
Ila kama kawaida ya Erica alipoinuka pale alikuwa na yake kichwani tayari na moja kwa moja alienda kwa mama yao na kumueleza swali alilouliza Angel na jinsi Junior alivyosema, kiukweli mama Angel alichukia sana na kuuliza,
“Kwahiyo mkasemaje wengine?”
“Tuliondoka mama”
“Mnaujua utamu nyie? Hivi Junior ana akili gani lakini jamani! Aaaargh mitoto mingine sijui imelelewajwe”
Kisha mama Angel alimuita Junior kwa nguvu sana na Junior akaenda kisha akamnasa vibao vya kutosha na kumuuliza,
“Unaujua utamu wewe? Unazungumzia nini? Mbona una tabia mbaya sana?”
“Nisamehe mamdogo, nisamehe sana nilichokuwa nazungumzia ni kingine kabisa ila sijui wamefikiria nini”
“Haya ulikuwa ukizungumzia nini, yani bila aibu sababu hapewi utamu wa kutosha na mume wake, hivi una nini wewe mtoto? Nitakurudisha kwa mama yako!”
“Nisamehe mamdogo jamani, sikumaanisha hivyo unavyomaanisha. Yani nilikuwa nasema bamdogo hajawahi kukuletea vitu vitamu kama keki”
Mama Angel akamnasa kibao kingine na kumfanya Junior apige na magoti kuomba msamaha, kwani hapo wazo lilikuwa la kurudishwa kwao tu ambapo alikuwa hataki iwe hivyo, basi alipiga magoti na kuendelea kumuomba mamake mdogo msamaha,
“Sasa nenda ukawaambie hao ulikuwa unawaambia huo upuuzi na ukarekebishe hiyo kauli yako, mjinga wewe. Toka hapa”
Basi Junior aliinuka lakini moja kwa moja alihisi mpeleka maneno ni Erica tu, ila ilibidi afanye kama alivyotumwa na kuwaita wote yani Angel, Erick na Erica kisha kuanza kuongea nao,
“Jamani, mmenifikiria vibaya, mimi sikumaanisha utamu wowote zaidi ya utamu wa keki na pipi na juisi, haya Erica mpeleka maneno umemaanisha utamu gani? Unaujua utamu wewe? Jamani katika maisha yangu sijawahi kuona mtu mbea kama wewe Erica, yani hufai hata kidogo, nimetengua kauli yangu jamani, sijamaanisha hivyo, mistake nifukuzwe kwenye nyumba hii, mimi nimependa kuishi hapa, niacheni niishi kwa furaha”
Angel alimuangalia Junior alivyokuwa akiongea halafu alimuangalia Erica kwani mdogo wake kweli alikuwa mbea tena wa kutosha tu, ila walikubaliana pale na kila mmoja kuelekea tena chumbani kwake. Ila kiukweli Junior nae alimchukia Erica, yani katika ile nyumba ni Erick pekee ambaye kidogo alikuwa akikaa kaaa na kuongea mengi na Erica kwani hata Angel alikuwa hapendi kuongea na mdogo wake huyo tena kwa kipindi hiko ambacho ana simu ya magendo ndio kabisa, akaona akiwa anaongea nae mara kwa mara basi atapeleka maneno kwa mama yao.