Simulizi: Nini maana ya mapenzi

Simulizi: Nini maana ya mapenzi

SEHEMU YA 176


Walifika hotelini na kuingia kwenye chumba ambacho Erica alimkodia Rahim, kisha kabla ya vyote Rahim alitaka kwenda kuoga kwanza ila Erica alitoka mule ndani na kwenda kuagiza chakula, alipoenda kuagiza chakula aliwasha tena simu yake na kukuta jumbe kama tatu za Babuu akilalamika kuwa mbona simu haipokelewi, Erica aliamua kumtumia ujumbe,
“Mwenzio nimeshikwa na tumbo la kuhara, nimeona unachelewa nikaamua kukodi bajaji. Nipo nyumbani saivi”
“Sasa ile shida yangu ya maongezi na wewe”
“Tutaongea siku nyingine Babuu, mwenzio naugulia tumbo”
“Pole Erica”
Basi aliposoma huo ujumbe, akazima tena simu yake kwani hakutaka iwe wazi akihofia kupigiwa tena na Babuu.
Alirudi chumbani huku akisubiri kile chakula ambacho alimwagizia Rahim, na chakula kilifika kisha yeye na Rahim wakala na kukaa wakifanya maongezi huku Rahim akimtolea zile zawadi ambazo alimuagiza na Erica alizipenda sana kwani zilikuwa za kuvutia, ilipoanza kuingia jioni Erica alimwambia Rahim kuwa anarudi kwao,
“Yani unamaanisha unataka uondoke Erica uniache peke yangu!”
“Sasa Rahim si nishafanya vyote ulivyosema?”
“Ndio umefanya ila leo huondoki hapa, yani tutalala wote kwakweli, huwezi ukaniacha peke yangu niboreke basi haikuwa na maana ya mimi kutokufikia nyumbani kwetu”
“Ila sijaaga nyumbani Rahim!”
“Sio tatizo, piga simu nyumbani kwenu waambie kuna sehemu umeenda kufanya project ili wasiwe na mashaka ila leo huondoki hapa”
Ilibidi Erica awashe simu na kupiga simu kwa mama yake kwani ndio anakuwaga wa kwanza kushikwa na uoga, akamwambia kuwa kuna sehemu ya gafla wamesafiri kimasomo na wamechelewa kurudi kwahiyo kwao ataenda kesho, mama yake aliitikia ila kwa shingo upande tu, ilibidi amuamini hivyo hivyo ingawa ilikuwa ni ngumu sana kuamini kile alichoambiwa na Erica.

Erica hakuwa na namna nyingine zaidi ya kuwa pamoja na Rahim tu kwani alishajitoa kuwa ndiye mpenzi wake, kwahiyo siku hiyo usiku mzima alikuwa pamoja na Rahim.
Palipokucha alikuwa amechoka kwakweli na hakuweza tena kuendelea na chochote zaidi ya kumuomba Rahim arudi kwao tu,
“Nitakuruhusu Erica ila bado sijaridhika”
“Basi naomba nikapumzike kidogo tu nyumbani”
“Mmmh mbona umeanza kunitisha mapema hivyo? Hivi utaweza kweli kuishi kwenye ndoa?”
“Nitaweza ndio”
“Sasa, mume mwenyewe si ndio mimi. Ndoa inahitaji uvumilivu Erica, sasa kama vitu vidogo hivi kuvumilia huwezi vikubwa je?”
“Sio hivyo ila kumbuka nyumbani nimewaambia kuwa narudi leo sasa mama hawezi kunielewa”
“Sikia nikwambie kitu, tutakodi usafiri kwenda kwenu halafu utamuaga mama yako kuwa mnasafiri kimasomo, utajiandaa halafu tutarudi tena hapa hotelini. Hupendi kuwa na mimi Erica?”
“Napenda”
“Sasa kama unapenda mbona unachoka mapema sana?”
Erica hakuwa na jibu zaidi ya kukubaliana na kile alichosema Rahim, kisha kujiandaa na kuondoka nae hadi kwao ambapo Rahim alikaa mahali akimsubiri atoke kwao.
Erica aliingia kwao ila alikuwa na mawazo sana kwani katika maisha yake ya mapenzi yote, siku hiyo alichoka na kuumia halafu mtu ndio anamsubiri bado ila kwavile alikuwa akiiota ndoa ilibidi avumilie tu kwani aliona uvumilivu ndio utamsaidia.
Hakumkuta mama yake ndani, akajiandaa kisha akamuandikia mama yake barua na kumuwekea laki mbili ndani yake kwani ugonjwa wa mama yake ni hela na alishaujua kwahiyo alivyomuwekea hivyo alijua mama yake asingemsumbua tena na angemuamini hiyo safari aliyoenda.
Kisha akatoka na kumpigia simu Rahim ambapo alikodi tena gari na kurudi nae tena hotelini.
Walikaa huko hotelini na Rahim ila baada ya siku tatu uzalendo ukamshinda Erica, ingawa aliandika barua kwa mama yake kuwa ni safari ya wiki ila baada ya siku tatu aliomba tu kurudi kwao,
“Rahim, sidhani kama tunachofanya ni sawa. Maana sie bado hatujaoana”
“Ndio umetambua leo kwamba bado hatujaoana?”
Erica aliitikia tu ila alitamani apate nafasi ya kwenda kupumzika, na kwa wakati huu Rahim alimruhusu kwani alisema kuwa ameridhika kiasi, kisha akamwambia,
“Swala langu linabaki pale pale, usiwe karibu na mama yangu sawa!”
“Sawa”
Kisha ukafanyika mpango wa kurudi nyumbani kwao.
 
SEHEMU YA 177


Kwakweli Erica kilanga cha kumuwaza Rahim kilimuisha kabisa, akaanza kumkumbuka Bahati jinsi alivyokuwa mpole kwake, akakumbuka siku alikutana na bahati kimwili ila alipomwambia amechoka tu Bahati alimsikiliza na kumuacha apumzike ila kwa Rahim imekuwa tofauti maana hakujua neno la nimechoka yani yeye ukisema nimechoka ni kamavile unasema endelea, Erica aliwaza sana ila kwavile maji alishayavulia nguo akajisemea ni sharti ayaoge maana bado kwenye akili yake alimuweka Rahim kama mume wake.
“Kuna wakati pesa ni mbaya sana, nimekuwa mtumwa wa penzi la Rahim sababu ya hele zake ila isingekuwa hela zake wala nisingekuwa mtumwa kiasi hiki. Sijui kitu gani nifanye nisipende hela, ila mimi sina matumizi makubwa ya hela tatizo lipo kwa watu wanaonizunguka. Inabidi nivumilie tu kuhusu Rahim maana ndio mume wangu”
Alikuwa akijisemea tu mwenyewe, muda kidogo Mama yake alimuita na kumuuliza vizuri mahali alipokuwa,
“Erica, toka umeanza chuo sijawahi kukusikia umesafiri kimasomo, eeeh kipindi hiki imekuwaje? Ulisafiri kimasomo kweli?”
“Ndio mama”
“Erica mwanangu, kumbuka kuna mimba. Nahisi sijawahi kukwambia swala hili, hebu kaa chini nikueleze”
Erica alikaa akimsikiliza mama yake sasa,
“Erica, ukipata mimba na kuzaa kabla ya ndoa halafu Yule mwanaume aliyekupa mimba asikuoe yani utayaona maisha kuwa machungu sana mwanangu. Wanaume wengi hawapendi kuoa wanawake wenye watoto yani utajikuta unaolewa na watu wazima sababu ndio wanakubali, kwenye vijana wanaokubali ni wachache sana. Jichunge mwanangu, sitakuwa na furaha kukuozesha kwa mzee pia sitakuwa na furaha kwa mwanangu wewe msomi kuzalia nyumbani. Naomba ujichunge Erica”
“Sawa mama nitajichunga”
Alimuhasa sana maana alitambua akili za vijana huwa zinabadilika kama kinyonga, baada ya hayo alienda chumbani kwake na kulala, kiukweli alikuwa na uchovu sana maana alipokuwa na Rahim hakupata muda wa kupumzika maana Rahim alikuwa kama mtu ambaye yupo kazini.

Kulipokucha alichukua simu yake na kuiwasha, na moja kwa moja akampigia Rahim, kumuuliza kuhusu anavyojisikia na hali yake ikoje, kisha akamuuliza kama ameshaenda nyumbani kwao,
“Erica, mimi sikurudi kwaajili ya kwenda nyumbani kukaa na mama, nilirudi nikiwa na maana yangu kabisa”
“Sasa utakaa hapo hapo hotelini?”
“Ndio, nitakaa hapa hapa, hakuna tatizo. Ukijisikia kuja niambie kwanza”
Erica aliitikia ila ile kauli ya niambie kwanza ilimpa mashaka maana aliwaza kuwa kwanini aambiwe wakati ni jambo la kusema nipo nje, lakini kamwambia aambiwe kwanza, hakutaka kuwa na mashaka nae sana na pia hakutaka kwenda kumtembelea wakati bado anajiuguza maumivu yake ukizingatia hajawahi kuwa na mwanaume kwa kipindi kirefu vile kwahiyo Rahim ni kama mwanaume wake wa kwanza kuwa nae kwa kipindi kirefu.
Kwahiyo kwa kipindi hiko alikuwa akiwasiliana na Rahim kwenye simu tu.
Erica alishukuru jinsi ambavyo Rahim hakumwambia tena kuwa wakutane kwani alijua akikutana nae ni kwenda kuyazoa maumivu mengine.
 
SEHEMU YA 178

Babuu nae hakuacha kumtafuta Erica kwani bado alikuwa na ya kumueleza, ilipita kama mwezi mmoja ambapo Erica alimruhusu Babuu kwenda kwao kuzungumza nae alichotaka kusema, hakumruhusu mapema kwa kuhofia kuwa Rahim anaweza kufika kwao maana kwa mawazo ya Erica alihisi kuwa ni kwa kipindi chochote kile Rahim angepeleka posa kwao, ila mwezi mzima ilikuwa kimya na wala akiongea na Rahim kwenye simu haongelei maswala ya yeye kwenda kujitambulisha kwao. Alihofia kuwa endapo Rahim angemkuta Babuu nyumbani kwa kina Erica ingekuwa mtafaruku mkubwa, ila kwavile Rahim hakuonyesha lengo la kwenda kwakina Erica ndipo Erica alipomruhusu Babuu kwenda kuzungumza nae.
“Ila Erica siku ile hukunifanyia vizuri kwakweli, yani kuniacha kwenye mataa kweli!”
“Nisamehe bure ni tumbo”
“Sasa siku ile ulivyoondoka alikuja ndugu yangu, yani sikutegemea kumuona pale na wala na yeye hakutegemea kuniona. Tulisalimiana nikamuuliza vipi kumbe kama kawaida kwao hawajui kama kaingia nchini, tena safari hii ameniambia anakomesha”
“Anakomesha nini?”
“Yani huyo ndugu yangu ana wanawake wengi huyo ila mamake hajui tu, anamuonaga mtakatifu balaa ila ana wanawake jamani dah! Siku ile yenyewe kuna mwanamke wake mwingine alitaka kunitambulisha, Yule jamaa wanawake wanampenda sababu ya ushombeshombe na wengine wanamuhonga sana pesa kiasi kwamba hela zake anachezeaga tu hazina kazi”
Erica alihisi kama kubanwa na tumbo la kuendesha maana alijihisi vibaya na tumbo kuunguruma, aliomba kidogo udhuru na kwenda chooni huku akiwaza kuwa anayoyasikia kuhusu Rahim ni kweli au ni kitu gani, hakuelewa kwakweli ila alihisi kuchanganyikiwa tu.
Aliporudi alikaa tena na Babuu kumsikiliza hoja zake, ila hakumuuliza alichokuwa akimuitia siku hiyo ila alimuuliza tu kuhusu huyo ndugu yake,
“Kwahiyo huyo ndugu yako ana wanawake wengi wapi? Hapa nchini au?”
“Yani ni hivi, Yule ni shombeshombe basi wanawake wengi wanavutiwa nae, wengine huwa wanamtongoza wenyewe na kumpa pesa kiasi kwamba ana hela nyingi sana Yule. Kwanza babake ana hela sana, kwahiyo babake tu anampaga hela nyingi halafu na wanawake nao wanampa hela balaa, kwahiyo ana wanawake wengi balaa ila ukimuona huwezi kumdhania anaonekana ni mpole balaa ila ni kicheche hafai”
“Babuu naomba uende, mama yangu atarudi muda sio mrefu”
“Ila swala langu bado sijakwambia”
“Utaniambia tu siku nyingine, ila kwasasa naomba uende”
Babuu hakuwa na jinsi zaidi ya kuondoka.
Erica alihisi kuchanganyikiwa kabisa yani akili yake ilikuwa haijisomi kwa muda huo tangu ameambiwa maneno yale na Babuu, alichukua simu na kumpigia Rahim ila iliita sana hadi ilikatika, alikosa raha kwakweli.
Mama yake alirudi na kumkuta katika mazingira ya kutokuwa na furaha, alimuuliza,
“Nini tatizo mwanangu?”
Leo Erica alijikuta akimuuliza mama yake,
“Mapenzi ni nini mama?”
“Kheee swali gani la kuniuliza hilo Erica?”
“Samahani mama”
Kisha akainuka na kuelekea chumbani kwake, kwakweli akili yake haikuwa sawa kabisa kiasi kwwamba hata siku hiyo hakuweza kupatwa na usingizi, alijikuta akishikwa na wivu maradufu yani alitamani hata kufanya kitu asichokielewa ndipo alipotambua nguvu ya wivu vizuri,
“Yani Rahim, umetembea na mimi kumbe una wasichana wengi. Kumbe unanipaga hela unayopewa na wasichana wako, kwanini Rahim umeamua kunifanyia hivi?”
Alilia sana, ila akawaza kitu kimoja je kama ana mimba au ukimwi, maana ameshaambiwa kuwa Rahim ana wasichana wengi, alilia sana kisha akasema kuwa kesho yake ataenda hospitali kupima mimba na ukimwi.
Aliwaza sana, kitendo hiko kilimfanya akose usingizi kabisa.

Kulipokucha Erica aliondoka kwao asubuhi na kwenda hospitali ambapo alienda kupima mimba na ukimwi, majibu yakaletwa,
“Hongera, huna ukimwi ila una mimba”
Alihisi akili yake kuruka kabisa, akikumbuka ahadi yake ya mwisho alisema hatokuja kutoa tena mimba katika maisha yake, ila sasa ana mimba ya mtu ambaye ni muhuni, aliwaza sana na kulia kwa daktari hata daktari mwenyewe alimshangaa akilia,
“Sasa unalia nini wakati watoto ni Baraka kwa Mungu, hivi unajua kuwa kuna watu wanatafuta watoto”
“Tatizo sio mtoto, tatizo ni baba wa mtoto”
“Kwani kuna wanawake wangapi wanalea watoto wao bila baba? Hebu ondoa mawazo mgando kwenye fikra zako. Kwa muda huu unatakiwa kuanza kuandaa mazingira mazuri kwa mtoto ajaye.”
Erica alitoka pale kwa daktari na kuondoka bila hata ya kumuaga, akawaza kuwa mtu wa kwanza kumwambia ni Rahim, kwa vyovyote vile alihisi pengine akimwambia Rahim kuwa ni mjamzito basi hilo swala la kuwa na wanawake wengi litapotea kwa Rahim na ataanza kumfikiria yeye. Akachukua simu yake na kumpigia Rahim ila iliita sana tu kama jana yake na bila ya kupokelewa ila akakumbuka kuwa Rahim aliwahi kumwambia kuwa yupo hotelini kwa mwezi mzima, ikabidi aende pale hotelini.
Alifika chumba alichomkodiaga Rahim na kugonga ila alifunguliwa na mwanamke, akawa anamshangaa Yule mdada gafla akamuona Rahim akiwa amejifunga taulo yani ametoka kuoga.
 
SEHEMU YA 179


Akachukua simu yake na kumpigia Rahim ila iliita sana tu kama jana yake na bila ya kupokelewa ila akakumbuka kuwa Rahim aliwahi kumwambia kuwa yupo hotelini kwa mwezi mzima, ikabidi aende pale hotelini.
Alifika chumba alichomkodiaga Rahim na kugonga ila alifunguliwa na mwanamke, akawa anamshangaa Yule mdada gafla akamuona Rahim akiwa amejifunga taulo yani ametoka kuoga.
Akili ilimruka kabisa Erica na kushindwa hata cha kufanya kwa muda huo huku akitamani hata kukimbia, wakati amegeuka nyuma ili aondoke, alishikwa mkono na Rahim na kuingizwa chumbani, kisha Yule mdada aliyekuwa mule chumbani kwa Rahim alitoka.
Erica alikuwa akilia sana, yani alilia hadi alihisi kuchanganyikiwa ila Rahim alimkalisha chini, kisha kumuacha akilia halafu yeye akivaa nguo. Alipomaliza alimsogelea na kumuangalia tu akilia hadi Erica aliona ni ujinga wa kuendelea kulia, akanyamaza na kumuangalia Rahim kwa hasira sana, ila kabla hajaongea chochote Rahim alimuuliza,
“Sasa kinachokuliza ni nini?”
Erica alimuangalia Rahim na kuongea kwa gadhabu sana,
“Yani bila hata aibu unaniuliza kinachoniliza ni nini!”
“Aibu gani sasa?”
“Hivi Rahim wewe ni mtu wa aina gani? Yani mimi nikutafutie hoteli halafu wewe ulale na wanawake wengine?”
“Kwahiyo hiyo hoteli uliyonitafutia unalipa wewe au nalipa mimi?”
Erica alizidi kupata hasira na kumwambia,
“Hata kama unalipa wewe ndio unifanyie mambo ya ajabu kweli? Ni haki hiyo?”
“Mambo ya ajabu yapi?”
“Hivi unaona ulichofanya ni sawa? Kulala na mwanamke mwingine unaona ni sawa?”
“Erica hebu acha masikhara, wewe ulichoka na nilikwambia kuwa nilirudi kwaajili yako ila ulidai umechoka kwahiyo ulitaka nifanyeje?”
“Yani Rahim ndio unaniambia hivyo kweli? Asante sana”
Erica akainuka, ila Rahim alimshika tena mkono na kumkalisha chini kisha akamwambia,
“Hebu acha mawazo ya kijinga, nilikuwa napima uelewa wako na wivu kama unao. Hivi kweli Yule anagekuwa mwanamke wangu angeondoka? Si angeanza kugombana na wewe? Halafu nianze tu kutafuta wanawake na kulala nao kwenye chumba kile kile ulichonikodia? Si nitakuwa sina akili, kwani hoteli hapa mjini zimeisha Erica? Kama ningekuwa na tabia hiyo basi hata hii hoteli nisingekaa sana, lazima ningetafuta hoteli nyingine ya kwenda kuwa na wanawake wengine”
“Kwahiyo Yule mwanamke ni nani?”
“Hilo ndio swali ulilotakiwa kuniuliza toka mwanzo sio kuanza kujiliza, Yule mwanamke nilimpa nguo zangu akanifulie na aliniletea leo, sasa nikamwambia aniwekee kitandani sababu naoga, nashangaa ndio wakati anatoka sijui wewe ndio umegonga na muda huo nimetoka bafuni. Yani una mawazo ya kijinga Erica jamani! Huamini mama, amini nakupenda sana”
Erica sasa akatabasamu kwani hakuamini kama Rahim angeongea nae kwa uzuri kiasi kile, kisha akamuangalia na kumuuliza,
“Kwahiyo Rahim wewe sio muhuni?”
“Hivi Erica, ningekuwa muhuni ningehangaika nini kukutafuta wewe? Kwanza nani aliyekwambia kama mimi ni muhuni? Sina hizo tabia mimi, nadhani hata mama yangu ashakwambia mengi sana kuhusu mimi, sinaga mambo ya wanawake kabisa. Niambie kipenzi changu maana naona umekuja kunishtukiza leo”
Erica akafungua pochi yake na kutoa yale majibu kuwa yeye ni mjamzito, kwakweli Rahim alonyesha kufurahi sana,
“Wow Erica jamani, umeamua kunibebea mimba! Nimefurahi sana Erica, na mimi nitaitwa baba sasa”
“Ndio, na mimi nitaitwa mama”
“Sawa, nakuomba Erica usitoe mimba yangu. Mwanangu nitamlea”
“Siwezi kutoa, ila uje nyumbani basi ujitambulishe na tufanye maswala ya harusi”
“Sawa, usijali kuhusu hilo, ila kwasasa nataka tena kusafiri. Yani nilitaka nikupigie simu leo kuwa kesho narudi Marekani. Nitakuja safari nyingine na kuja kwenu kujitambulisha na kukamilisha kila kitu”
“Jamani Rahim, sasa itakuwaje? Mama akijua?”
“Usijali, mwambie mama, mume yupo yani sitakawia kurudi Erica si unajua hata kwetu sijafika”
“Sawa Rahim, ila mimba haina siri mama akijua litakuwa balaa, unadhani mama yangu ataelewa nikimwambia kuwa mume yupo? Hatonielewa kwakweli”
“Usijali Erica, baada ya miezi miwili tu narudi. Nitakuja kwenu kukamilisha kila kitu”
Erica hakuwa na namna zaidi ya kumkubalia Rahim tu kuwa kesho yake anasafiri na ataenda kujitambulisha kwao akirudi baada ya miezi miwili ila alijipa moyo kuwa tumbo litakuwa bado kujitokeza. Kisha Rahim akamwambia tena Erica,
“Nakuomba leo tulale wote mpenzi wangu ili kesho unisindikize”
“Mmmh jamani hata nyumbani sijaaga?”
“Kwani na wewe huna njia ya kuaga nyumbani kwenu jamani Erica, nahitaji kumuaga mwanangu, si unajua nasafiri naenda mbali. Naomba tulale wote jamani Erica”
Ilibidi Erica akubali na atafute namna ya kumwambia mamake kwenye simu ili asiwe na wasiwasi.

Kesho yake Erica aliamka na Rahim kwenye ile hoteli kisha kujiandaa kwaajili ya kwenda uwanja wa ndege maana Rahim alisema ndio safari yake imewadia, kisha Rahim alimpa hela Erica na kumwambia,
“Chukua hii milioni moja ikusaidie saidie maana mimba zina mambo mengi sana, unaweza kutamani hiki mara hiki, hii pesa itakusaidia”
“Asante sana Rahim”
Kisha Erica alichukua ile pesa na kuiweka kwenye pochi yake, kisha Rahim alimwambia,
“Erica napenda kukwambia tena uwe mbali na mama yangu, sio saivi una mimba ndio unaenda kumtafuta mama yangu sijui uwe nae karibu. Tafadhali kuwa mbali na mama yangu, atakupa mawazo mama Yule. Mimba hazitaki mawazo Erica, mimba inataka pumziko la moyo. Kuwa mbali na mama yangu, sitaki ndugu yangu yeyote awe karibu na wewe”
“Nimekuelewa Rahim ila kumbuka siku ile ulitaka kunitambulisha kwa ndugu yako”
“Yani Yule nilikutana nae kwa bahati mbaya, akaniuliza kuwa mbona sijasema ujio wangu ndio nikamwambia yupo na shemeji yake yani nikamgelesha tu ngoja nimtambulishe ila siku ile nilishukuru kweli alivyoitwa maana hata mimi nilitaka kumfanyia mchezo pale wa bila kumtambulisha. Ndugu zangu ni wambea wambea sana, ndiomana sipendi kuwa nao karibu. Ila nakusisitiza tena kuwa mbali na mama yangu”
“Nimekuelewa Rahim”
Kisha wakaondoka na kwenda uwanja wa ndege ambapo Erica alimuacha Rahim kaingia uwanjani kisha yeye akarudi nyumbani kwao.
Erica aliingia kwao ila kwa muda huo mama yake hakuwepo kwahiyo alienda kuoga na kulala, alikuwa akishangaa tu mimba ya kipindi hicho imeanza bila makeke ya kutapika au kujihisi kichefuchefu.
 
SEHEMU YA 180

Erica aliamka usiku kwenye mida ya saa mbili na kutoka chumbani kuelekea sebleni ambapo mama yake alikuwa amekaa, akamsalimia,
“Kheee kumbe ulirudi?”
“Ndio nilirudi mama”
“Nilijua na leo utalala huko huko maana siku hizi unajiamulia tu”
“Ila mama si nilikwambia jamani!”
“Erica mwanangu, Erica binti yangu kila siku ninapokusema hapa unaona kama nakuonea ila ipo siku utasema kweli mama alisema. Utanidanganya ila na mimi nilikuwa msichana kabla yako, naelewa kila kitu. Nitakwambia ulikuwa kwa mwanaume ila utabisha, sawa nidanganye tu ila mimi si ndio mama wa kudanganywa! Unasahau kama mama unatakiwa umweke kama rafiki yako na umshirikishe mambo yako ili akushauri zuri na baya, mwanangu hujaolewa bado, unawezaje kwenda kwa mwanaume na kulala nae hadi asubuhi? Unajua wewe si mke, unawezaje kufanya hivyo? Mwanaume wa hivyo atakuoa kweli? Hakuna mwanaume anayetaka kuoa mwanamke asiyetulia, atakuchekelea kuwa ndio vizuri tulale wote hadi asubuhi ila kumbuka si mumeo huyo, ni mpenzi wako, hata kama kakuahidi ndoa, basi subiri ndoa ndio ukakeshe nae kwenye kulala ila sio mwanaume wakuitana sijui baby halafu unalala nae hadi asubuhi”
“Ila sikuwa kwa mwanaume mama”
“Huwezi kukubali ila mimi ni mama naelewa kila kitu na ipo siku utayakumbuka maneno yangu, napenda upate mwanaume mwenye pesa aje kuwa mume wako ila sijasema ukipata mpenzi mwenye pesa basi ujiachie ukalale nae. Sijasema hivyo, hata kama huyo mwanaume awe na pesa kiasi gani ila kitendo cha wewe kwenda kulala kwake hadi asubuhi ni kujishushia heshima. Sio mke wewe, usitake kujifanya unachukua majukumu ya mke kabla hujaingia kwenye ndoa. Yangu ni hayo, utasema mama vipi anaongea sana ila maneno yangu utayakumbuka”
Erica alimtakia mama yake usiku mwema kwani alijua akiendelea kuongea nae pale basi mama yake yatamtoka maneno mengi sana na hakupendezewa nayo sababu yalikuwa yanamchoma.
Alirudi chumbani kwake na kutafakari maneno ya mama yake ila aliona hata akiyatafakari bado hayana suluhisho kwake maana kama mwanaume kashalala nae kwa siku za kutosha tu, na kwa kipindi hiki ana mimba kwahiyo maneno ya mama yake yalikuwa ni msumari wa moto lakini usioweza kumchoma muhusika maana tayari ameshakosea.
“Inabidi mama nisimwambie kama nina mimba hadi pale Rahim atakaporudi na kujitambulisha nyumbani. Natumaini tumbo halitakuwa kubwa”
Alijipa moyo maana alijua ikiwa mama yake atagundua kuwa ana mimba itakuwa ni balaa hilo.

Chuo kilifunguliwa na alianza tena kwenda chuo ila kwa kipindi hiki alikuwa anachoka sana yani ile kwenda chuo na kurudi tena nyumbani kwao ilikuwa ni swala la uchovu sana, ilibidi awasiliane na Rahim amwambie kuwa anapata shida ya kutoka kwao kwenda chuo,
“Kumbe hiko chuo ulichohamia unakaa nyumbani?”
“Ndio, nachoka sana”
“Basi tafuta chumba cha kupanga karibu hapo, nitakutumia hela ya kodi na nyingine ununue kitanda na godoro upate sehemu ya kupumzika ukitoka chuo yani kwenu uende mara moja moja sana”
“Nashukuru sana kwakweli”
Basi Erica alitumiwa hela na Rahim kisha alitafuta chumba kwenye maeneo karibu na chuo na kuweka kitanda na godoro na vitu kadhaa tu vya kumsadia akiwa kwenye chumba kile na kukaa, yani akawa akitoka chuo anarudi kwenye kile chumba ila mama yake alimdanganya kuwa anaishi hosteli, hakutaka kusema amepanga maana mama yake asingependezewa na swala la kusikia kuwa amepanga.
Kwa kipindi hiko alikuwa anaenda tu kwao kwa kuchungulia yani siku hiyo hiyo anaondoka kiasi kwamba mama yake aliuliza ila alidanganya kuwa masomo ya mwishoni yanasumbua sana akili kwahiyo muda mwingi anatumia kusoma.
Kwa kipindi hiko hakutaka kukutana na mtu yeyote wala hakwenda kwa ndugu yake yeyote kiasi kwamba alikuwa akipigiwa simu na shemeji yake James alikuwa akikata kwani hakutaka kabisa kuongea na shemeji yake huyo.
Siku hiyo akiwa anaelekea kwake alisimamishwa na Fetty njiani,
“Erica, mbona siku hizi umebadilika sana?”
“Nimekuwaje kwani?”
“Umenenepa, wakati wewe sio mnene maana mwili wako huwa kawaida tu ila kwasasa umenenepa”
“Pengine sababu nakaribia kumaliza chuo”
“Vipi umewahi kuonana na Derick hivi karibuni?”
“Hapana, kwani imekuwaje?”
“Mwenzangu Derick kumbe kuna wadada wawili hapa chuo kawazalisha halafu hana mpango wa kuwaoa wala nini, hadi nikasema loh na rafiki yangu Erica angeingia mkenge kumbe!”
“Hivi inakuwaje mwanaume anadanganya watu wawili kwa wakati mmoja?”
“Kheee hujui eeeh! Sasa mbona Derick alikuwa anakudanganya wewe wakati ana wanawake wengine? Yani mwanaume akikwambia nakupenda msikilize palepale ila ndio usijiwekee moyoni ukaona unapendwa balaa. Yani wanaume wenzako sijui wana mioyo mingapi maana mmoja anaweza akapenda hata kumi”
“Na wote akawaonyesha upendo sawa?”
“Ndio, mwanaume hashindwi ila nadhani anakuwepo mmoja anayependwa sana. Ila mwenzio unafikiri wanaume nawaamini sana hata siwaamini, usiniona hivi nishatoa mimba hadi sijui kama nitazaa tena, yani wanaume hawa loh! Kwahiyo unaishi wapi siku hizi?”
“Huko chini”
“Basi siku moja nitakuja kukutembelea unapoishi”
“Sawa karibu”
Fetty aliondoka na Erica alienda anapoishi ila sio kwamba maneno aliyoambiwa hayakumuingia hapana, yalimuingia vilivyo kuwa mwanaume mmoja anaweza kuwa na wanawake hata kumi, alijihisi kuwa na wivu sana yani wivu aliokuwa nao kwa Rahim hajawahi kuwa na wivu wa kiasi kile hadi alikuwa akijihisi vibaya, wivu wake kwa Rahim ulimfanya hata akimtafuta hewani asipopatikana ajihisi vibaya sana na kugundua kuwa hisia zake kwa kipindi hiko zinaendeshwa na wivu.
 
SEHEMU YA 181

Fetty alionekana kumfatilia sana Erica na mwisho wa siku akapafahamu Erica alipokuwa akiishi, na alikuwa akienda kumtembelea mara kwa mara ila Erica hakumwambia kama anaujauzito ingawa tumbo liliendelea kuwa mbele,
“Erica kama una mimba!”
“Jamani kwanini?”
“Nikuonavyo tu”
“Hapana sina mimba”
“Ila kuwa na mimba ni swala la kheri Erica, unajua mimba zinatafutwa siku hizi! Mimi mwenyewe nikibeba mimba nazaa tu, umri ushaenda nitajibana bana hadi lini, yani mimba ikijichomekea tu nazaa”
Erica alikuwa akicheka tu ila hakuthubutu kumwambia Fetty kuwa ni mjamzito ingawa dalili zote alikuwa nazo halafu naye Fetty alishamuhisi kuwa Erica ni mjamzito.
Mara zote Erica alizokuwa akiwasiliana na Rahim alikuwa akimuuliza tu kuwa atarudi lini ili aende kujitambulisha nyumbani kwao, ila Rahim alimwambia swala moja tu kuwa ataenda karibuni,
“Unajua Rahim mimba hii inazidi kukua yani hata nyumbani wakijua sijui nitasema nini, utakuja lini Rahim?”
“Erica, usiwe na mashaka. Nitakuja tu yani hata usiwe na wasiwasi”
“Ila lini Rahim nijue siku niwe na uhakika”
“Usijali Erica, nitakuja tu”
“Kumbuka uliniambia baada ya miezi miwili ila hadi leo kweli ni miezi mingapi imepita Rahim? Hata huonekani jamani na husemi lini utakuja”
“Erica usijali mpenzi wangu, nitakuja tu”
Yani jibu la Rahim lilikuwa ni moja tu kuwa nitakuja usijali, wakati kwa upande wa Erica aliona karibia siri itabumbuluka maana kama nyumbani kwao alikuwa akienda na kuondoka ila alijisemea tumbo likizidi sana basi kwao hatokwenda kabisa.
 
SEHEMU YA 182

Mimba ya Erica iliendelea kukua na kipindi hiki walifanya mitihani ya mwisho chuoni kwahiyo wakafuna chuo ili wasubirie majibu nyumbani na baada ya hapo yafanyike mahafali, akaona kwenda kuishi kwao na mimba ishaanza kuwa kubwa ni swala la aibu kwahiyo aliendelea kuishi pale pale huku akimdanganya mama yake kuwa bado chuo hajamaliza.
Ulipita mwezi bila ya Erica kwenda nyumbani kwao, mama yake akawa anamlazimisha kwenye simu kuwa arudi nyumbani,
“Erica mwanangu hebu rudi nyumbani”
“Bado chuo mama”
“Bado nini? Mbona nasikia chuo mshamaliza muda tu”
“Tumeambiwa mpaka tusubiri matokeo”
“Sasa kwanini hayo matokeo usije kuyasubiria nyumbani jamani”
“Hamna mama”
“Hebu niambie ukweli, nini kinakusibu mwanangu?”
“Hamna kitu mama”
“Una mimba Erica?”
Erica akashtuka na kushindwa hata kumjibu mama yake, Yule mama alipoona kimya alimuuliza tena,
“Una mimba Erica?”
Erica bado alikuwa kimya maana alishindwa kumjibu mama yake ingawa ni kwenye simu. Mama yake aliendelea kuongea,
“Erica, kumbuka mimi ni mama yako na unapaswa kuniambia ukweli. Hivi ukinificha mimi utamwambia nani?”
“Sina mimba mama”
“Sasa kwanini hutaki kurudi nyumbani? Erica kama ni mjamzito halafu unanificha utakuwa umetenda kosa kubwa sana, kwanza umenikosea mimi na umemkosea Mungu, unawezaje kupata mimba nje ya ndoa?”
“Sina mimba mama”
“Rudia tu hayo maneno na iwe kweli huna mimba maana ukiwa nayo sijui nitakufanya nini? Erica wewe ni binti yangu wa mwisho, tunahitaji kucheza harusi yako, tusherekee kwa furaha sio uniletee watoto nyumbani kabla ya ndoa. Narudia tena jichunge”
“Nitajichunga mama”
“Sawa, na vipi kuhusu kurudi nyumbani?”
“Nitarudi mama usijali”
Mama yake Erica alimsisitiza sana Erica kuhusu swala la kurudi nyumbani, huku Erica akihofia kuonekana kwao akiwa mjamzito, na yale maneno ya mama yake ndio yalimtisha maradufu hakujua mama yake angemwambia kitu gani pindi akimkuta mjamzito.
 
SEHEMU YA 183

Siku hiyo alikuwa akiwasiliana na Rahim kwenye mtandao wa facebook kama kawaida, alishangaa kukutana na ujumbe wa Tumaini,
“Erica, mambo vipi. Nimekumiss jamani, natamani nikuone. Erick alirudi ila tulikutafuta hewani bila kukupata, na hajapenda kusikia nina ugomvi na wewe. Anataka kuona tukicheka pamoja, alikuja na zawadi zako kaniachia nikupatie, sasa je nije kwenu kukuletea”
Erica alisoma mara mbili mbili ila hakumjibu maana alijua kama akimruhusu atagundua kuhusu mimba yake maana kwa kipindi hiko ndio tumbo lilikuwa limejitokeza haswaa, ila alijipa moyo kuwa hawezi kuonana nae sababu haishi nyumbani kwao.
Akiwa amekaa mule kwenye chumba chake alisikia mlango wake ukigongwa, akainuka na kwenda kufungua, akashtuka sana maana mlangoni alimuona Fetty akiwa ameambatana na mama yake Erica.


Akiwa amekaa mule kwenye chumba chake alisikia mlango wake ukigongwa, akainuka na kwenda kufungua, akashtuka sana maana mlangoni alimuona Fetty akiwa ameambatana na mama yake Erica.
Erica hakujielewa kwa muda huo, ila mama yake naye alipiga yowe kama kapatwa na habari za msiba,
“Yereeeee uwiiiii Mungu wangu, Erica mama umeniabisha. Uwiii ndio msomi wangu wewe!”
Huyu mama ilionyesha kachanganyikiwa kabisa, ikabidi Fetty amuingize ndani kwa Erica kwa kuhofia kujaza watu pale nje.
Erica nae kwa upande wake hakujua ni kitu gani atafanya na mama yake, ila wakati mama yake ndio kaingizwa ndani ili waweze kuzungumza wakiwa ndani, Erica alipiga magoti na kutaka kuanza kumuomba msamaha mama yake ila kabla ya kuongea alianza kulalamika tumbo kumuuma na alionekana kuwa na hali mbaya gafla, ilibidi mama yake aache kulia sasa na kuanza kushughulika kumsaidia mwanae, ambapo Fetty alienda kuchukua gari ya kukodi kisha wakaenda hospitali, Erica aliingizwa kwa daktari.
Mama yake alibaki nje akiwa na mawazo sana juu ya mwanae, aliwaza vitu vingi maana mimba zina mambo mengi sana, akachukua simu yake na kupigia dada zake Erica ambao walishangaa pia kwa lile waliloambiwa na mama yao, kisha baada ya muda mfupi nao walifika hospitali alipopelekwa Erica ila mpaka muda huo bado daktari hakutoa majibu yoyote na kufanya wamkute mama yao kuwa na mawazo sana,
“Mama jamani, punguza presha”
“Yani sielewi hapa watoto wangu, sielewi kabisa”
“kwanza imekuwaje mama? Hebu tueleweshe kwa ufupi, najua Mungu atamsaidia mdogo wetu na atakuwa salama”
“Sikilizeni, nadhani niliwapigia simu nikiwaambia kuhusu mwenendo wa mdogo wenu kuwa nasikia washamaliza chuo ila yeye hataki kurudi nyumbani, ila nyie mkapuuzia wakati haya mambo ilibidi yachukuliwe kwa umakini sana, kwakweli nimeona kimya jamani wiki zinapita tu, miezi inapita tu kimya. Leo nikaamua niende chuoni kwao, Mungu mwema nikakutana na huyu binti chuoni sijui alikuwa anafanya nini ila nikamuuliza na kumwambia kuwa mimi ni mama yake Erica, hakutaka kunipeleka anapoishi Erica ila alinihurumia kwani mimi ni mama na pia napaswa kufahamu anapoishi mwanangu. Sasa tumeenda pale, ile kugonga Erica katoka akiwa na mimba jamani, tena mimba kubwa tu, nyie Erica kanivua nguo jamani”
“Mama jamani, punguza presha. Cha muhimu ni uzima wa Erica sio swala la kukuvua nguo. Kwani wangapi watoto wao wanapataga mimba mama? Ni wengi tu, usiwe na presha kiasi hiko”
“Nyie hamjui tu, hivi mjomba yenu akisikia habari hizi itakuwaje? Yani alikuwa akitolea ada mbuzi jamani? Naomba uzima kwa binti yangu ila kanitia aibu sana, na nitamsema sana”
Wakati wanazungumza akaja daktari na kuwaita ili kuzungumza nao,
“Tumejitahidi na kwasasa huyu mgonjwa wenu yuko sawa, kabakiza wiki chache tu kujifungua, naona kuna mshtuko alipata ndiomana hali imekuwa hivi. Tunampa mapumziko hapa hospitali kwa siku mbili tumuangalie hali yake ila tunaomba hata atakaporudi nyumbani asifanye kazi yoyote kwasasa maana yupo kwenye hatari. Pia asipate kitu chochote cha kumpa mawazo yani mkiwa mnaongea nae msiongee nae habari za kushtua maana presha yake haipo vizuri”
Daktari aliwaelekeza pale namna watakavyoishi na Erica na wao wakaelewa.
Basi daktari alivyoondoka wakajadiliana,
“Mama, kwasasa Erica asisemwe chochote mpaka ajifungue. Bora umwngalie tu maana tutakosa vyote mama yangu tutamkosa Erica na mtoto wake, tuwe wapole tu kwasasa”
“Kheee jamani mimba hizi, kwahiyo siruhusiwi kuuliza hata baba wa mtoto?”
“Mama huwezi jua pengine ni jambo litakalompa stress”
“Jamani, mbona mimba zetu haikuwa hivi!”
“Hiyo ni zamani mama, siku hizi kuna mambo mengi yanaingiliana”
Wakaongea pale na kwenda kumuona Erica sasa.
 
SEHEMU YA 184

Waliongea nae kwa ustaarabu sana kwani kila mmoja alihofia kumpa matatizo Erica, kisha wakaongea nae kuwa akitoka hospitali wamrudishe nyumbani kwahiyo vitu vya kule alikopanga vihamishwe, naye alikubali kwahiyo dada zake walienda kwa lengo la kuhamisha vile vyombo vya Erica na kuvipeleka nyumbani kwao.
Walipelekwa na Yule Yule Fetty kwenye chumba alichopanga Erica, walifika na kuingia ndani, kwakweli walishangaa vitu vilivyokuwepo mule ndani kwa Erica, kisha wakamwambia Yule Fetty akawatafutie usafiri wa kuhamisha vitu vile. Fetty aliondoka na kuwaacha wakishangaa tu,
“Hivi Bite unaelewa mdogo wangu?”
“Hata sielewi dada”
“Yani huyu Erica kapanga lini jamani mpaka kununua vitu vyote hivi!”
“Tena vya gharama”
“Mmmmh nahitaji kumjua huyo mwanaume aliyempa Erica mimba”
“Sio Yule Bahati kweli!”
“Hapana, Yule alikuwa amechoka sana. Sema hata hivyo tutajua mtoto akizaliwa”
Wakapanga panga vitu kisha Fetty akafika na usafiri, wakasaidiana na vijana wa pale kupakia vitu kwenye gari kisha kuanza safari ya kwenda kwao, kwenye safari zote hizo Fetty alikuwepo hadi nyumbani kwakina Erica, usiku ulishaingia sana, ikabidi walivyofika tu asikae sana na kuaga kisha akaondoka zake.
Ndani walibaki mama yao, Bite na Mage, walikuwa wakiongea tu kuhusu vitu alivyonunua mdogo wao,
“Hivi mama, mwanao kapata wapi hela ya kununua vitu vyote hivi?”
“Hata mimi mwenyewe nashangaa, yani sielewi kabisa”
“Mmmh ngoja tumsubiri huyo mumewe lazima atakuwa bonge la bwana”
Ila mama yao leo katika siku zote hakuwa na furaha hata kidogo yani ile misukosuko ya siku hiyo ilimkosesha amani na furaha kabisa, alijikuta akiwaambia wanae,
“Hao bonge la bwana unafikiri ni waoaji? Hivi kuna muoaji kweli hapa? Mwanaume aweze kukununulia kila kitu cha ndani ila ashindwe kuja kwenu kujitambulisha na kukuoa, kutembea na mwanaume tajiri si ufahari ila ufahari pekee ni kupata heshima ya kuwa mke wa mtu Fulani”
Mage akamwambia mama yake,
“Kheee mama kumbe kuna heshima ya kuwa mume wa mtu hata kama huyo mume akiwa masikini!”
“Hebu nitoleeni mambo yenu kwanza leo nimechanganyikiwa”
Wakaona wakiendelea kuongea watamkera mama yao ikabidi wamuage na kupanga kukutana nae tena kesho asubuhi hospitali kumuona Erica, na walifanya hivyo kwa siku zote ambazo Erica alikuwa hospitali.
 
SEHEMU YA 185

Siku hiyo ilikuwa siku ya kutoka Erica hospitali kwahiyo walienda kumchukua na kumrudisha nyumbani kisha alienda moja kwa moja chumbani kwake huku wakimsisitiza asiwaze sana na apate muda wa kutosha wa kupumzika, dada zake waliongea nae maneno mazuri tu kanakwamba hakuna kosa alilolitenda kumbe wanaogopa kuhatarisha maisha ya mdogo wao, kwahiyo walikuwa wanaombea tu ajifungue ili waweze kuongea ya moyoni.
Siku hiyo usiku ndio Erica alipata tena muda wa kushika simu yake maana toka ile siku ya sekeseke hakushika simu kabisa, aliingia kwenye facebook na kukutana na jumbe za Rahim,
“Erica mpenzi, siku ya tatu leo haupo hewani. Tatizo ni nini mama?”
Erica alitabasamu kuona Rahim anaonekana kumjali sana, kile kitendo kilimfanya ajipe matumaini kuwa Rahim anampenda sana na atakuja tu kumuoa,
“Rahim, nilipatwa na matatizo yani leo ndio nimetoka hospitali”
“Usiniambie mimba imetoka Erica!”
“Hapana mimba haijatoka ila nimeambiwa nisifanye kazi ngumu na nisiwe na stress, nimebakiza wiki chache tu kujifungua”
“Erica, tafadhali nakuomba fata ushauri wa madaktari, mwanangu ni muhimu sana huyo. Nakuomba mwanangu asipate madhara yoyote yale Erica, kuwa makini sana maana likitokea baya kwa mwanangu sijui nitakutenda nini, kuwa makini sana na mwanangu”
“Usijali Rahim, kumbuka huyu ni mtoto wetu wa kwanza na tunampenda sana, nipo makini sitaki mawazo ya ajabu ajabu yazingire kichwa changu, ila lini utakuja kunioa?”
“Erica, sidhani kama ni wakati muafaka wa kujadili hilo swala. Sikia, kesho nitakutumia pesa za kufanya maandalizi yako wakati wa kujifungua, kuwa makini na mtoto Erica. Usitembee tembee kwa miguu, uwe unakodi gari, zile hela nakutumia ili unitunzie mwanangu”
“Usijali Rahim”
Erica aliongea kwa uzuri sana na Rahim hata akalala kwa tabasamu na kusahau kabisa kama Rahim huwa anampa ahadi za kuja kesho tu na wala hatokei.
Aliamka asubuhi na kukuta kila kitu akifanyiwa na mama yake tena bila ya kuulizwa chochote sijui kuhusu mwanaume anayehusika sijui kuhusu mambo mambo gani yani hakuna kitu chochote alichoulizwa na ile hali ilimfanya awe katika hali ya kawaida tu na asijione kuwa amekosea sana kubeba ile mimba.
Jumbe za Tumaini kwenye facebook alikuwa akizipotezea tu kanakwamba hazioni kwani hakutaka afanye nae mawasiliano ya kufika kwao maana aliogopa angemuona na ile mimba, halikadhalika hata simu za Babuu alikuwa hazipokei kabisa.
 
SEHEMU YA 186

Siku ilifika ambapo alipatwa na uchungu sana, kisha mama yake kumkimbiza hospitali yani hapo ndio akaelewa kwanini mama kaitwa mama maana sio maumivu yale aliyokuwaga anayapata pindi akienda kutoa mimba, yale yalikuwa cha mtoto maana hapo ndio alisikia yale maumivu yenyewe yenye neno la uchungu wa mwana aujuaye mzazi.
Alijikuta akipiga kelele za maumivu bila ya machozi na aliyaugulia yale maumivu kwa muda hadi akabahatika kujifungua, yani alionyeshwa tu mtoto wako huyu hapa halafu hapo hapo akazimia ilibidi madaktari waanze harakati za kumsaidia Erica.
Mama yake alikuwa nje na alikuwa amechanganyikiwa sana, aliona mwanae akitolewa leba na kupelekwa kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi sana, jamani hapo huyu mama alichanganyikiwa zaidi, maana kwanza ndugu zake wengine hakuwaambia kuhusu matatizo ya Erica halafu maswala kama hayo yasiyoeleweka yalizidi kumpa kichaa yani hakujielewa kabisa, aliwapigia simu wanae hovyo hovyo maana alishawaambia kuwa yupo hospitali nab ado walikuwa hawajafika, na walipofika walimkuta mama yao akiwa na hali mbaya sana yani amechanganyikiwa kabisa,
“Mama sasa, usijage hospitali, bora tuwe tunakuja wenyewe sasa unachanganyikiwa hivyo ndio nini? Si tuulize vizuri madaktari kuliko kuchanganyikiwa hivyo”
Wakaona Erica akitolewa kwenye kile chumba cha wagonjwa wa uangalizi maalum na kupelekwa wodini, ikabidi wamuite daktari ili awaeleze vizuri,
“Mtamuona sasa, msijali ni mzima kabisa. Alichoka sana kusukuma kwahiyo alizimia ila yupo vizuri kwasasa na mtoto yupo vizuri”
“Oooh asante Mungu, kajifungua mtoto gani?”
“Hongereni sana, kajifungua mtoto wa kike”
Wakafurahi pale na kumshukuru sana daktari, kisha wakaomba kwenda kumuona Erica na mtoto, waliruhusiwa maana hospitali ile ilikuwa ni ya binafsi kwahiyo haikuwa na masharti mengi.
Walifurahi sana kumuona Erica na mtoto, waliambiwa kuwa Erica ataruhusiwa kutoka kesho yake ili kuangalia vizuri anavyoendelea.
Walimpa mtori pale anywe ambao alibebewa na Mage, kisha walivyomuaga walipanga kumpelekea chakula kingine badae ambapo walimuacha na juisi na matunda kwanza.
Waliondoka na kwenda moja kwa moja nyumbani ili kujadiliana kwa ufupi tu,
“Jamani tumeletewa mwarabu mama, yani Yule kama sio mwarabu basi mpemba”
“Jamani ni utoto tu akikua atabadilika”
“Wapi? Mtoto wa kiarabu Yule, watoto wa Kiswahili wanajulikana bhana, Yule ni mwarabu kabisa. Hebu mama sema”
“Sina usemi mimi ila alipojidumbukiza mdogo wenu sijui nani atamuopoa, kwenda kuzaa na waarabu kweli? Aaah huyu mtoto kanishinda tabia mimi jamani loh! Huyo baba wa kiarabu atakuja kweli hapa nyumbani? Jamani sijui mimi ila mmenidhalilisha mama yenu”
“Usiseme hivyo mama, ngoja tuandae chakula cha mzazi sie, iwe mtoto wa kiarabu au wa kipemba ndio mtoto wetu tuliyepewa na Mungu”
Kiukweli mama yao alikuwa akiwaza tu aibu atakayoipata kwa ndugu zake maana hakujua hata ataweka wapi sura yake kuwakwepa.
 
SEHEMU YA 187

Erica alitoka hospitali na kurudi nyumbani ambako aliendelea kupewa vyakula vya mzazi na kuhudumiwa kama mzazi anavyohudumiwa, ni kweli ilikuwa inamuuma sana mama yake ila alijikaza na kumuhudumia mwanae hadi alikuwa katika hali ya kawaida tu, Erica alikuwa anafanya kazi ya kumpiga picha mtoto na kumtumia Rahim ambapo Rahim alionyesha kufurahia sana ujio wa mtoto wao huyo,
“Eeeeh tunamuita nani mama?”
“Kwani wewe unapenda tumuite nani?”
“Chagua tu jina wewe mwenyewe, nimekupa nafasi hiyo”
“Napenda nimuite Angel”
“No, aitwe tu Malaika”
“Ila Malaika na Angel si jina moja jamani kasoro lugha tu”
“Ndio, ila itapendeza zaidi akiitwa Malaika”
“Jamani, mi naona nitapendeza zaidi nikiitwa mama Angel”
“Erica, huoni kama akiitwa Malaika itapendeza zaidi?”
“Basi, mimi nitakuwa namuita kwa kingereza halafu wewe unamuita kwa Kiswahili”
“Jamani mama Malaika, unapenda mabishano eeh! Jina mtoto si aitwe moja tu au nimpe jina la mama yangu”
“Nani?”
“Tumuite Mwajuma maana mama yangu anaiitwa Mwajuma”
“Mwajuma? Ndio jina gani hilo? Mama yako si anaitwa Mrs.Peter jamani, hiyo Mwajuma imetoka wapi?”
“Ndio jina lake, Peter ni jina la mumewe”
“Aaah hilo jina silitaki mimi, mwanangu ataitwa Angel tu”
“Sawa nimekubali hakuna tatizo, ataitwa vile unavyopenda wewe”
Erica aliwasiliana na Rahim ila alikuwa na maswali mengi sana kwenye akili yake kuwa mama yake Rahim kumbe anaitwa Mwajuma, yani akawaza vitu vingi sana ikiwa ni pamoja na jambo la dini kuwa lazima yeye na Rahim kutakuwa na utofauti,
“Mungu wangu sasa atanioaje? Ooooh nimeruka mkojo nimekanyaga mavi, si bora na Bahati aliyeniambia ukweli toka mwanzo jamani, mmmh ila hapana huenda Rahim ni mkristo nitamuuliza tu”
Aliwaza bila ya jibu.
 
SEHEMU YA 188


Erica alipomaliza miezi miwili ya uzazi, mama na dada wa Erica walitoka kidogo na kuzungumza kuhusu mtoto wa Erica,
“Jamani wanangu nadhani sasa ni kipindi muafaka cha mimi kumuuliza mdogo wenu kuhusu baba wa mtoto wake au mnasemaje?”
“Ni kweli mama muulize, na hivi mtoto mwenyewe mwarabu sijui baba yake nani?”
“Kanitia aibu mtoto huyu jamani loh! Kazaa mtoto mzuri kweli ila raha ya mtoto awe na baba sio mtoto tunaishi nae hata baba hajulikani, mwezi wa pili huu hatujawahi kumuona baba wa mtoto wala ndugu wa mwanaume. Inamaana huyo mwanaume hana ndugu jamani? Mimi huyu mtoto kanishinda tabia”
“Usilalamike mama, muulize kwanza maana huwezi jua ni kwanini mwanaume hajafika hadi leo”
Wakakubaliana na mama yao pale ili amuulize kisha walipoaga na kuondoka ndipo mama yao alipomuita Erica na kuanza kuongea nae.
“Haya Erica mwanangu, najua sijawahi kukuuliza wala hatujakaa tuongee, niambie huyo baba wa mwanao yuko wapi na atakuja lini hapa nyumbani?”
“Yupo Marekani, na amesema atakuja tu”
“Kwahiyo ni Mmarekani?”
“Hapana, yupo kule kimasomo tu ila ni wa hapahapa”
“Haya, anaitwa nani?”
“Anaitwa Rahim”
“Kheee Rahim? Mwanangu jamani mwanangu wewe, akili yako ikoje jamani? Kumbe ni Mwislamu”
“Ni Mwislamu!”
“Inamaana hujui au? Yani msomi mzima unashindwa kutofautisha dini kwa majina? Wewe wa wapi wewe?”
“Sikujua kama ni Mwislamu mama”
“Haya sasa, wewe na yeye mtafunga ndoa gani? Usije ukaniletea uwehu wa kubadili dini, yani nyie watoto wa kike jamani mpo kama mafungu ya nyanya, mtu akitaka kupika mchuzi haya, akitaka kukatakata kachumbari haya, akitaka kutengeneza chachandu haya. Hivi ulishindwa kuchagua maisha uyatakayo? Unajifanya kushangaa hapa, unashangaa nini sasa?”
Erica alikuwa kimya tu kwani kama hakuelewa elewa vile, mama yake aliendelea kuongea,
“Erica, narudia kukuita Erica, ukithubutu kubadili dini sahau kuwa mimi ni mama yako. Yani utajua mwenyewe utakachofanya na huyo mpemba wako ila ukithubutu kubadili dini Erica, nisahau kabisa. Umenitia aibu wewe mtoto na wala sikutegemea jamani aaah!”
Erica alikosa raha kabisa kwani alizidi kupata picha kuwa amekosea sana kumuamini Rahim na kuacha mahusiano yake yaliyopita, kwa muda huo alimuona Bahati kuwa ndiye mtu pekee aliyekuwa anajieleza kwa ukweli kwake, sasa atafanyeje kuhusu Rahim, alihisi kuchanganyikiwa.
Usiku ulipofika aliwasiliana na Rahim na kuanza kumdadisi kuhusu kuoana yeye na Rahim,
“Halafu Rahim kumbe mimi na wewe tumetofautiana dini?”
“Ndio, kwani ulikuwa hujui”
“Nilikuwa sijui Rahim”
“Kwahiyo ungejua ungenikataa? Mapenzi hayana dini Erica”
“Sawa nakubali mapenzi hayana dini, ila je utanioa kwa ndoa ya aina gani?”
“Upo tayari kubadili dini nikuoe?”
Hilo lilikuwa ni swali la utata kwa Erica na kumfanya achanganyikiwe zaidi.
 
SEHEMU YA 189


Usiku ulipofika aliwasiliana na Rahim na kuanza kumdadisi kuhusu kuoana yeye na Rahim,
“Halafu Rahim kumbe mimi na wewe tumetofautiana dini?”
“Ndio, kwani ulikuwa hujui”
“Nilikuwa sijui Rahim”
“Kwahiyo ungejua ungenikataa? Mapenzi hayana dini Erica”
“Sawa nakubali mapenzi hayana dini, ila je utanioa kwa ndoa ya aina gani?”
“Upo tayari kubadili dini nikuoe?”
Hilo lilikuwa ni swali la utata kwa Erica na kumfanya achanganyikiwe zaidi.
Ila aliamua kumuuliza tena Rahim,
“Hivi hakuna njia nyingine ya mimi na wewe kuoana zaidi ya kubadili dini?”
“Unadhani tunaweza kuoana kwa njia gani?”
“Si kuna ndoa za bomani Rahim!”
“Ndoa za bomani kwangu ni haramu, Erica kubali kubadili dini nikuoe”
“Ngoja nifikirie basi”
“Ila sio swala la kufikiria sana, ni swala tu la kutolea maamuzi. Kama unahitaji kuishi na mimi basi kubali kubadili dini nikuoe”
Kwakweli Erica aliona wazi kabisa ndoto yake ya kuolewa na Rahim imekufa maana Rahim kashasema hawezi kumuoa hadi abadili dini na mama yake kashasema kuwa akibadili dini basi asahau kuwa yeye ni mama yake yani hapo akashikwa na mkanyiko wa mawazo sana.
Alimuangalia mwanae na kuamua kulala tu kwani kwa vyovyote vile Yule atabaki kuwa mtoto wake,
“Angel wangu, niolewe au nisiolewe ila nitakupenda daima”
Alimkumbatia mwanae na kulala.
 
SEHEMU YA 190


Palipokucha kama kawaida alikuwa wa kwanza kuamka maana kipindi hiko mtoto anaamka mapema sana kwahiyo kwa vyovyote vile aliamka na kuanza kumnyonyesha mwanae na kumuweka katika hali ya usafi. Kama kawaida mama yake alifika na kuanza kumuogesha mjukuu wake, alipomaliza alimvalisha kisha Erica alimnyonyesha na mtoto kulala.
Mama Erica alianza tena kuzungumza na binti yake,
“Vipi kuhusu huyo mwanaume wako hujanijibu?”
“Sielewi mama”
“Huelewi nini sasa?”
“Sikujua kama Yule mwanaume ni Mwislamu mama”
“Haya umejua sasa, una mpango gani?”
“Sijui mama, itakuwaje?”
“Yani wewe mtoto tumekusomesha bure tu, ndiomana serikali ilikunyima mkopo maana akili zako walishaziona kuwa hazimo, masikini kaka yangu kajitahidi kwa uwezo wake wote kuhakikisha unasoma halafu leo aje asikie umezaa na mwarabu sijui mpemba halafu upo upo tu hata huelewi cha kufanya”
“Ila mama unanilaumu bure tu, wewe ndio uliyesababisha yote kwenye maisha yangu. Ulisema nichague mwanaume mwenye hela”
“Nilikutuma mimi ukapanue miguu yako kwa huyo mpemba wako? Nilikutuma? Hebu Erica uwe na akili muda mwingine, ndio nilisema utafute mwanaume mwenye hela, je nilisema ukimpata ukalale nae mzae watoto kabla ya ndoa? Mambo mengine ni ya kujiongeza tu, maisha ni wewe mwenyewe unavyoyachagua na sio watu wanavyosema, wewe msomi mzima hujui hili ni zuri au baya? Nilikwambia utafute mwanaume mwenye hela ndio, ila sikuwa na maana mbaya, sikutaka mwanangu upate shida kwenye ndoa yako sababu mimi nishapitia ila sikukwambia ukabebe mimba kabla ya ndoa. Au uliambiwa ukizaa na mwanaume ndio kigezo cha mwanaume huyo kukuoa? Unajua Erica bora hata ungekuwa mkubwa sana ningesema mwanangu kaona umri umeenda kaamua kuzaa, mwanangu ndio kwanza una miaka 23, dah umenitia aibu sana. Haya sasa huyo mpemba ana mpango gani?”
Erica aliona hata aibu kumjibu mama yake kuwa Rahim kamwambia abadili dini maana aliwaza kuwa ataanza njia gani kumueleza hayo wakati kashakatazwa yani alikuwa njiapanda haswaa, kwavile hakumjibu tena mama yake aliamua kuondoka zake kuendelea na kazi zingine maana aliona ni kama kumpigia mbuzi gitaa.
 
Back
Top Bottom