SEHEMU YA 199
Erica alimkabidhi mtoto mama yake, kisha mama yake akamwambia,
“Nenda mwenyewe huko unapotaka kwenda, mjukuu wangu niachie”
Kwakweli pozi lilimuisha gafla Erica maana hakuelew kabisa, ila kwavile alishaita na gari ilibidi atoke tu ili aende.
Wakati anatoka getini ili apande gari, alimkuta Bahati nje ya geti ndio anataka kugonga.
Bahati alimsogelea Erica na kumkumbatia, ila gari nalo lilikuwa nje likimsubiri Erica, alimuangalia Bahati hakujua kwa muda huo amwambie kitu gani, Bahati alimuuliza Erica,
“Vipi mbona uko hivyo?”
“Kuna mahali natakiwa kuwahi”
“Basi twende wote”
“Aaah wewe nisubiri tu hapa”
Erica akasogelea lile gari na kufungua mlango ili aingie, ila Bahati akamshika mkono na kusema,
“Erica, nimeacha kazi zangu zote na nimekuja kwa lengo la kukuona wewe. Kumbuka hata ningekupigia simu yangu usingepokea, ila unataka kuondoka na kuniacha una maana gani? Nimekwambia twende wote hutaki”
“Bahati, nielewe yani kuwa muelewa pale mtu anaposema jamno. Niache niende, kuna mahali nawahi”
“Kwahiyo mimi sio wa muhimu?”
“Sijui kama unanielewa”
Ila kabla Bahati hajamuachia mkono, mara alitoka mama Erica pale nje na kumwambia Erica,
“Eeeeh afadhali bado hujaondoka, mtoto kacharuka mwenzangu”
Yani Erica ndio aliona hapo pamechanganywa maji na mafuta maana mama yake nae kaja kuvuruga tu kama kawaida. Ikabidi ampe Yule dereva pesa ya usumbufu, halafu aingie ndani ambapo Bahati nae alimfata nyuma huku akijiuliza maswali kuhusu mtoto aliyecharuka.
Erica aliingia ndani na kumchukua mtoto kwa mama yake kisha kwenda nae chumbani kumnyonyesha, kwahiyo sebleni alibaki mama Erica na Bahati. Ambapo Bahati alimsalimia vizuri sasa huyu mama, kisha huyu mama alianza kwa kumuomba msamaha,
“Nisamehe mwanangu kwa yaliyopita, yani sikujua nilijua ndio unaniharibia mwanangu hadi tukakupeleka polisi. Nisamehe sana”
“Usijali mama”
“Yani kijana una moyo wewe, nilijua toka siku ile hutokuja tena nyumbani kwangu, ila umekuja jamani una moyo sana. Haya mwenzio huyo ana mtoto”
“Ana mtoto?”
“Ndio, kumbe hujui?”
“Sijui mama”
“Mtoto angekuwa wa Kiswahili tungekuhisi ni wewe ila mtoto ni wa kiarabu sijui kipemba na baba yake hajulikani”
Kiukweli Bahati alijihisi vibaya sana ila hakuweza kujionyesha pale kuwa kajihisi vibaya na hakuweza kumjibu zaidi huyu mama kwani maneno yale yaliujeruwi moyo wake, huku akitamani sana kusikia kutoka kwenye kinywa cha Erica maana bado hakuamini amini kama Erica ana mtoto.
Baada ya kimya kuzidi mama Erica alimuuliza tena Bahati,
“Utakunywa kinywaji gani?”
“Aaah usihangaike mama”
“Hapana sio nisihangaike, hujawahi kunywa chochote hapa nyumbani kwangu, leo nahitaji utie baraka kwa kunywa kitu kwenye nyumba yangu”
“Basi maji mama”
Basi mama Erica alienda kuleta maji na kumpa Bahati ambapo bahati alikunywa maji yale na kuyamaliza kwa muda mfupi tu kwani alihisi kama kuna kitu kimekaa kooni halafu Erica hakutoka chumbani wala nini, ikabidi wakati mama yake anarudisha kikombe aende na kumuita Erica.
Alimkuta kalala pembeni ya mwanaye,
“Yani Erica umeingia kumnyonyesha mtoto na kulala hapo hapo wakati kuna mtu anakusubiri kweli!”
Erica akashtuka na kukumbuka ni kweli Bahati alikuwa akimsubiria ila usingizi ulimpitia alivyokwenda kumyonyesha mtoto kitandani na kuwa na mawazo mengi kuhusu harusi aliyoambiwa ni ya Rahim. Akainuka ili akamsikilize Bahati, alipotoka mama yao alitoka nje na kuwaacha waendelee na maongezi.
Erica hakuongea chochote ila Bahati ndio alianza kuongea,
“Erica kumbe una mtoto? Mbona hukuniambia?”
Erica alikuwa kimya tu, na Bahati aliendelea kuongea
“Ungeniambia mapema Erica, unajua ni jinsi gani nakupenda na sipo tayari kuona ukiaibika. Mamako kaniambia kuwa baba wa mtoto hajulikani ila ungeniambia mapema ingekuwa rahisi kuliweka sawa swala hili. Naweza kuwa baba wa mtoto, haijalishi mtoto huyo anaonekanaje, mama kasema sijui ni mwarabu au mpemba, ninachojua mimi ni kuwa kitanda hakizai haramu, naweza kuwa baba wa mtoto Erica sio sawa kuwa na mawazo kiasi hiko. Yani unapatwa na tatizo unashindwa hata kunishirikisha jamani Erica? Ulihisi nitakataa au?”
Erica alikaa kimya tu ila alikuwa akijiuliza kuwa Bahati ana upendo wa aina gani maana alikuwa ni tofauti na wanaume wote ulimwenguni, alishangaa sana kwani hakujua kama kuna wanaume wenye moyo kama wa Bahati, kwakweli alimshangaa sana na kubaki akimuangalia tu bila ya kumjibu. Bahati aliendelea kuongea,
“Sema neno lolote nielewe Erica, mimi nipo kwaajili yako”
“Nashukuru sana kusikia kuwa bado upo kwaajili yangu, ila kuhusu mtoto haikuwa nafasi nzuri kwa leo kuliongelea hilo swala. Nilitaka nikutafute kwa muda wangu nikueleze ila kwavile umejua sina budi kukwambia, ni kweli nina mtoto na kuhusu swala la baba wa mtoto bado ni kitendawili kwangu. Ila bado nina msimamo wangu ule ule wa tafuta pesa kwa bidii Bahati ili leo na kesho mkeo na watoto wako wafurahie uwepo wako”
“Mke wangu ni wewe na mtoto wangu wa kwanza ni huyo uliyemzaa wewe Erica, nitafanya kazi kwa bidii kweli ili mimi,wewe na mtoto wetu tuishi vizuri. Na kwa hakika kabisa Erica huwezi amini ambayo Mungu katutendea, najua ulishakosea ila hujakosea bado maana hujanikosa mimi. Biashara yetu imekuwa kubwa sana, yani huwezi amini samaki wamekuwa na soko kubwa ambalo sikulitegemea, pia nilikuanzishia biashara ambayo nilisema utaifanya ukimaliza chuo ila sababu unalea acha niendelee tu kuifanya”
“Ni biashara gani?”
“Erica, siwezi kutoka nje ya ufugaji kwahiyo biashara ambayo nilianzisha ni ya kuku wa kienjyeji. Uwiii natamani uone jinsi biashara hiyo ilivyo na neema yani Erica jamani biashara imekuwa kubwa naogopa, na juzi nilikuwa mkoani kuchukua kuku wengine niliagizwa. Na leo nilikuwa nabahatisha tu, ila kwasasa nitakuletea kuku na samaki uwe unakunywa na supu kwaajili ya afya yako na mtoto”
Mara mtoto wa Erica alianza kulia, na Erica akainuka ili akamchukue, Bahati akamwambia,
“Naomba uniletee mwanetu nimuone Erica”
Basi Erica alipotoka ndani alitoka na mtoto, ambapo Bahati alimshika mtoto Yule na alionekana kumfurahia balaa kama mwanae vile.
Bahati hakuondoka mapema kwakina Erica na kuzidi kufanya Erica kukosa muda kabisa hata wa kwenda tena ukumbini kama alivyopanga, basi kwenye mida ya saa mbili na nusu usiku ndipo Bahati alipoaga kuwa anaenda, alimwambia Erica amuitie mama yake ili amuage ambapo Erica alifanya hivyo, wakati mama yake anatoka Erica alienda kumlaza mtoto ndani, kwahiyo mama Erica alivyofika sebleni alimkuta Bahati akijiandaa kuondoka, Bahati akampa mkono wa kwaheri mama Erica ambapo alimwachia na pesa,
“Asante mama, kwaheri. Tutaonana tena”
Mama yake Erica alitabasamu sana na kuendelea kumkaribisha hadi Erica alipotoka na kumsindikiza hadi getini na kumuaga.
Erica alirudi ndani na kumkuta mama yake akiwa ameshika hela mkononi,
“Kheee mama, hela za nini unaenda wapi?”
“Naenda wapi? Nimepewa hela na baba Angel”
“Baba Angel! Sikuelewi mama”
“Si Yule kijana kanipa hela, yani sikujua kama Yule kijana ana moyo wa upendo kiasi hiki”
“Kakupa shilingi ngapi? Mama bhana, sasa Yule kijana kawa baba Angel toka lini?”
“Yule ndio baba Angel mwanangu, ona alivyokaa kumbembeleza mtoto hapa. Yale ile ndio aina ya wanaume wanaotakiwa ulimwenguni. Kanipa elfu hamsini ya pole ya kulea mzazi, nimefurahi sana hata kama mtoto mwarabu ila Yule ndio baba yake”
Erica alimuangalia mama yake ambaye alienda chumbani nay eye akaenda chumbani pia.