SEHEMU YA 83
Alifika uwanja wa ndege kwenye saa nne na nusu, yani hakuwa na furaha kabisa, wakati anasonga pale uwanjani akiwa na mawazo akagongana na mtu, alimuangalia na kumuomba msamaha,
“Uwe makini binti, mtoto mdogo hivyo unawaza nini?”
Erica alimuangalia vizuri sasa huyu mtu alikuwa ni mkaka wa kishombeshombe, Erica alikuwa kama akimshangaa hivi, Yule mkaka aliamua kujitambulisha,
“Naitwa Rahim, sijui mwenzangu unaitwa nani?”
“Naitwa Erica”
“Mbona unaonekana kuwa na mawazo sana?”
Erica alikuwa kimya tu akimtazama, Yule mkaka alimwambia Erica,
“Anyway, chukua kadi yangu hii tutawasiliana”
Erica akachukua ile kadi na kuiweka kwenye pochi yake, kisha akaendelea na safari yake halafu Yule mkaka nae akaondoka zake.
Aliposogea mbele alishikwa bega, alipogeuka tu alikutana na Tumaini,
“Kheee Erica unafanya nini tena huku?”
Erica alijiuma uma, alitamani kumwambia ukweli ila alihofia ikabidi amrudishie swali yeye,
“Na wewe unafanya nini huku dada?”
“Mimi nimekuja kumsindikiza mdogo wangu Erick na baba wanaenda South”
“Kumbe mdogo wako kasafiri?”
“Ndio, yani mdogo wangu hadi namuhurumia”
“Kwanini?”
“Ngoja tukae mahali nikusimulie”
Wakaondoka mahali hapo na kutafuta sehemu yenye mgahawa na kukaa kisha kuagiza vinywaji na kuendelea na maongezi, ila kabla hawajaongea kitu chochote simu ya Tumaini iliita na Tumaini aliipokea,
“Tutaongea badae, saivi kuna sehemu nipo mara moja”
Alivyokata akamuangalia Erica na kumwambia,
“Yani huyu msichana king’ang’anizi huyo?”
“Msichana gani?”
“Si Yule Sia nilikwambiaga kuwa ni mchumba wa Erick”
“Kafanyaje tena?”
“Huyu msichana hajielewi hata sijui kwanini anamng’ang’ania hivyo mdogo wangu wakati mdogo wangu mwenyewe yupo kama kachanganyikiwa. Bora aende zake huko labda ajipatie hata mzungu”
Erica akatabasamu kidogo ila kiukweli alikuwa anaumia moyo, akamwambia tena Tumaini,
“Eeeh nieleze sasa”
“Sikia nikwambia, mdogo wangu Yule Erick kuna kipindi alikuwa akiishi na mamake mdogo na kuna shule moja alipelekwa mgeni tu halafu akafanya madudu na kufukuzwa, nilimuuliza mdogo wangu kwanini alifukuzwa shule akasema ni sababu ya msichana Fulani hajawahi kunitajia jina la huyo msichana ila alisema kuwa alimtongoza huyo msichana halafu huyo msichana akamsemea kwa walimu, kitendo kilichofanya Erick achukiwe na kufukuzwa shule ingawa mamake mdogo aliomba sana Erick asamehewe. Nilimuuliza kuwa ni kweli alimpenda huyo msichana huwa ananijibu hadi leo anampenda sana. Unajua sisi wanawake mara nyingine tunasababisha wanaume kuwa na tabia za ajabu ajabu, yani mdogo wangu Erick kawa mlevi, unajua anakunywa Yule balaa, kawa mtu wa wanawake lakini chanzo chote ni huyo dada”
“Kheee jamani masikini yake, je unatamani kumjua huyo mdada?”
“Sitaki hata kumjua maana nitamuumiza nikimjua, kaumiza sana maisha ya mdogo wangu, hili nililosikia sasa ndio balaa”
“Lipi hilo?”
“Nasikia Erick alikutana tena na huyo mdada na mdada akadai kuwa ana mimba yake, ila Erick kamshuhudia kwa macho yake Yule mdada akitoka kwa dokta kutoa mimba yake, yani katoa mimba ya mdogo wangu kumbe Yule mdada ana mwanaume mwingine. Juzi mdogo wangu kapigana na huyo mwanaume balaa, jamani mdogo wangu hajawahi kupigania mapenzi ndio mara yake ya kwanza. Huyo dada ni shetani kwakweli”
“Inasikitisha lakini”
“Kwakweli inasikitisha sana, yani mimi sipendi mwanamke anayetoa mimba simpendi kabisa. Unajua kutoa mimba ni uuwaji! Hivi sisi tungetolewa na wazazi wetu, tungekuwepo leo? Ila mwanamke muuwaji hana hata huruma anatoa mimba kwakweli, nawachukia watoa mimba. Huyo msichana nikimjua nitamraruwa kwakweli”
Erica hakuwa hata na usemi kwani muhusika alikuwa ni yeye tena ilionyesha Tumaini akiongea kwa uchungu sana jinsi gani alivyo na hasira na huyo msichana ambaye ndio yeye,
“Nimemwambia mdogo wangu, huyo msichana hakupendi labda anapenda pesa ulizonazo tu lakini upendo hana. Hivi Yule msichana anajiona kutoa mimba ndio kashinda, anadhani anabaki kuwa binti loh! Hapana hajui tu, anakuwa mama wa marehemu na sio binti tena”
Erica alinyamaza kwani yale maneno yalimgusa vilivyo, na kuuliza tena
“Kwahiyo mdogo wako atarudi lini?”
“Si oleo wala kesho, kwanza hakutakiwa kusafiri ila kwa hali aliyokuwa nayo, baba ameona bora aende nae. Halafu sasa mpaka tupo nae airport bado anajipa imani kuwa huyo msichana atakuja kuongea nae, cha kushangaza hadi wameingia ndani hakuna huyo msichana kuja wala nini. Mdogo wangu anatia huruma kwakweli, ila Erica huku airport ulifata nini?”
“Aaah dada alinipa mzigo kuna mfanyakazi wa hapa nilikuwa nimempelekea, na nimefika muda sana sema nimechelewa tu kuondoka, ningejua mpo hapa hata ningewatafuta. Namuonea huruma mdogo wako, mpe pole sana”
“Yani kuna wakati natamani kumjua huyo mama marehemu na atanitambua kwakweli, atanieleza sababu za kumuumiza moyo kaka yangu na sababu za kumuua aunt yangu”
Erica aliamua kuagana na Tumaini huku akidai kuwa anatakiwa kurudi kwao mapema ila ukweli ni kwamba maneno ya Tumaini yalimuingia vilivyo na moyo kumuuma sana.
Ila Tumaini alimwambia kuwa anahitaji waende wote nyumbani kwao ili akapafahamu anapoishi Erica, hakubisha juu ya hilo na kuamua kuondoka nae.
Walifika nyumbani kwao, kupiga jicho getini alimuona kuna kijana amekaa chini, aliposogea akagundua kuwa ni Bahati, kwakweli Erica alitamani kurudi na Tumaini walipotoka ila kabla hajafanya chochote Bahati aliinua kichwa chake na alipomuona kuwa ni Erica aliinuka na kwenda kumkumbatia huku akilia, ikabidi Erica amuulize,
“Sasa unalilia nini?”
“Nalilia kiumbe changu Erica, namlilia mwanangu”
Erica aligeuka na kumtazama Tumaini kama naye anayasikia yale maneno anayoyasema Bahati.