Simulizi: Nini maana ya mapenzi

Simulizi: Nini maana ya mapenzi

SEHEMU YA 296

Walifika na kushuka kisha Moses akawaaga na kuondoka zake, Erica aliingia ndani na mwanae na kumkuta mama yake ambapo alianza kumuonyesha zile nguo alizopewa Angel.
“Kweli siku hizi kuna rah asana, yani mtoto anapata nguo za bure tu. Ndiomana umemshikilia huyo mwanaume, aje nyumbani sasa”
Erica akacheka tu kisha akamuuliza mama yake kuhusu dada yake Bite kuwa anaendeleaje,
“Anaendelea vizuri tu, ila unajua shemeji yako ni aibu tele imemshika hataki kurudi kwake”
“Kutokutaka kurudi sio tatizo, ila tatizo ni kuwa analala wapi? Dada aende kazini kwa shemeji jumatatu, na amtishie jambo moja tu kuwa ataondoka na amtishie kuwa akiulizwa atasema ukweli wa kilichomfanya aondoke, mama shemeji atarudi tu nyumbani sidhani kama atataka aumbuke mara mbili”
Mama yake alikubali swala hilo maana aliona ni jambo jema sana, kisha Erica alienda kufanya kazi zake zingine na kumpa mwanae chakula.
Muda wa kulala ulipofika, Erica alienda kulala na mwanae ila kabla hajalala alipigiwa simu na Erick,
“Erica, si nilikwambia uwe unanieleza kila kitu kinachotokea kwako?”
“Ila hakuna kilichotokea”
“Mbona nimesikia leo hadi ulitaka kuondoka dukani sijui sababu ya Tumaini, kwani tatizo ni nini?”
“Hamna tatizo ila sijui ni kwanini hadi leo dada yako hanipendi”
“Erica swala hilo lisikupe shida hata kidogo, yule ni dada yangu na wewe ni mpenzi wangu, nyie wawili mnacheza nafasi tofauti katika maisha yangu sidhani kama kuna sababu ya nyie kuchukiana. Erica, mimi ndio nakupenda wewe, si lazima dada yangu akupende, cha muhimu ni mimi kukupenda wewe. Halafu kingine lile ni duka langu, sio duka la Tumaini lile, naomba uwe huru kabisa unapoenda pale, sawa”
“Sawa nimekuelewa”
“Sitaki tena uwe na simanzi kipenzi changu, nakupenda Erica, sitanii namaanisha nisemayo, nakupenda”
“Asante, nakupenda sana”
Basi akaagana nae na kulala ila alikuwa na furaha sana kwa siku hizo Erica, alihisi kama kaibeba dunia.

Kama kawaida ya siku hii mama yake alijiandaa na kwenda kwenye ibada na kumuacha Erica akiwa mwenyewe, ila leo alipigiwa simu na dada yake Mage na kumsalimia,
“Erica, mdogo wangu kuna habari nimepata nahisi ni ya kweli ila ulinificha kwasababu zako binafsi”
“Habari gani dada?”
“Nasikia umewahi kulala na Derick”
Erica alishtuka kuona ile habari imefika kwa dada yake, akamuuliza kwa uoga,
“Nani amekwambia maneno hayo dada?”
“Dunia haina siri Erica, usidhani ukificha wewe kila mtu ataficha tena habari yote nimeipata”
“Si kweli dada”
“Usitake kupinga wala kukataa Erica, ni Derick mwenyewe kanieleza mambo haya. Erica nilikuuliza kwa kukupenda kabisa maana hiyo ni laana ambayo wewe na Derick mmeifanya”
“Ila Dada, sijui niseme vipi naomba nisamehewe sikujua kama Derick ni ndugu yangu hata hivyo alininywesha pombe. Naomba hii habari isifike kwa mama”
“Kwa mama labda uifikishe mwenyewe, sina huo mpango wa kufikisha habari hii kwa mama, ni aibu na fedheha kwakweli ila mimi kama dada natakiwa nisimamie swala hili maana ni laana kwenye ukoo”
“Sasa tutafanyaje dada?”
“Natakiwa nikawashirikishe kwanza wakina bamdogo na wao wataniambia cha kufanya ila lazima wewe na Derick muwepo, kwakweli mlifanya kitendo cha ajabu sana, ndugu jamani mmmh!”
“Sikujua dada”
“Basi ngojea nitakupigia simu nikishajua cha kufanya, ndiomana nilikuwa nakuuliza mapema kuwa kuna lolote mmefanya mkawa mananikatalia wakati mnajua fika mshaharibu”
Kisha Mage akakata simu, kwakweli Erica alichukia sana kwa Derick kutoa ile siri maana hakutaka ile siri ifichuke maana aliona inamuoinyesha yeye kama mtu mchafu sana wa kutembea hadi na kaka yake.
“Nakuchukia Derick, na wewe George nakuchukia maana ndio chanzo cha kufanya Derick na mimi tuwe karibu maana kunibaka kwako ndio nikapata msaada kwa Derick, jamani sijui hata nifiche wapi aibu hii, kama hadi wakina bamdogo wanaenda kuambiwa ni lazima mama nae atajua tu”
Kiukweli alikosa raha kabisa, hadi mama yake anarudi kanisani bado hakuwa na raha ila alijaribu kujigelesha kwenye macho ya mama yake asionekane kuwa na matatizo.
 
SEHEMU YA 297


Usiku wa siku hiyo alilala tu hata hakutaka kusikiliza simu wala kitu gani, asubuhi alikurupuka na kujiandaa kisha kwenda kazini.
Alipofika na kuanza kazi zake ndipo alipokumbuka kuwa alisahau simu yake nyumbani ila halikuwa tatizo sana kwake hilo alijua akifika tu nyumbani basi ataikuta sema alikuwa tu anawaza kama mwanae ataiona simu hiyo itakuwaje? Akaamua kutoa mawazo hayo na kuendelea na kazi.
Wakati anaendelea na kazi zake, George alimfata leo na kumuomba namba yake ya simu maana ile ya awali haikupatikana,
“George tunafanya kazi sehemu moja ila haina maana kuwa wewe uwe na namba yangu, ni bora tusiwasiliane tu”
“Hivi Erica wewe unawazaga nini? Yani muda wote unawaza kuwa mtu anataka kukutongoza jamani kweli! Nakuomba namba ya simu sio maswala ya mapenzi ila hapa tupo kikazi kuna kuhabarishana mambo mbalimbali ila unagoma kutoa namba yako ya simu. Sikulazimishi ila kuna siku utaona umuhimu wake”
Kisha George aliondoka kuendelea na kazi zake zingine ila ilionyesha kuwa alichukizwa na jibu la Erica kiasi kwamba toka muda huo hadi wanafunga kazi hakumuongelesha tena.
Muda ulifika na Erica akaenda nyumbani kwao, alipofika tu mama yake alianza kumwambia,
“Leo kumbe ulisahau simu, basi mjukuu wangu akaileta. Nimeiweka hapo juu, ikapigwa na kupigwa ila sikuipokea ila kuna mtu alipiga kwenye simu yangu, nikapokea na kumuuliza nani akaniambia ni Erick, sasa mimi nikasema Erick wa wapi? Jamani mwanao alivyonipora ile simu hata sikutarajia”
Erica akacheka sana, mama yake akamuuliza kuwa anacheka nini,
“Yani Angel bhana, akisikia tu Erick anapiga basi anachanganyikiwa”
“Mtoto wako hafai yani kashikilia ile simu kisha akanipa mwenyewe halafu Yule kijana kaniaga tu bila kujieleza, nikahisi ndio yule uliyemuokota na kumpa Angel. Haya mtoto kaanza vipi kumzoea hivyo?”
Erica akamueleza mama yake jinsi Erick anavyopiga simu kila siku akitaka kuongea na Angel na mwisho wa siku kamzoesha,
“Aaah kumbe, huyo Erick ni hatari, ukiona mkaka anavutiwa hivi na mtoto huyo ni mlezi mwema na atafanya mtoto kujisikia furaha kuwa nae. Ila ni tatizo pia maana mwanao hata ukija kumuonyesha baba yake wa ukweli atamkubali tu ila hatompenda kama huyo”
Erica akatabasamu tu na kwenda ndani kwake ila kwa yeye ndio kitu alichokuwa akikitaka, hakutaka Angel awaze tena kuhusu Rahim hata akimtambulisha amuone kawaida tu maana tayari alishaingiwa chuki na Rahim.

Kesho yake alijiandaa na kwenda kazini ila ilikuwa kama kuna chuki ipo kati yake na George maana hapakuwa na mawasiliano mazuri kabisa kati yao, hata hawakuongea tena yani walikuwa wakifanya tu kazi hata Erica akiuliza kitu kwa George hajibiwi vile inavyotakiwa hadi kumfanya asijisikie vizuri kabisa.
Ilikuwa Ijumaa ambapo Erica hata akatamani kwenda kuongea na Yule bosi wao kuhusu tabia ya George maana hakuielewa kabisa, ila kabla hajajipanga kwenda kuongea nae, bosi wake alipiga simu na kumuita ofisini kwake ikabidi Erica aende, akamsalimia na kukaa.
“Erica, nimekuita hapa kukuuliza kuhusu maendeleo ya kazi. Vipi kazi unaionaje?”
“Ni nzuri mama”
“Na George unamuonaje?”
Erica akatamani kusema kuhusu George ila moyo mwongine akaona si jambo jema kumchongea, kwahiyo akajibu kwa upole tu,
“Yupo vizuri, tunashirikiana nae vizuri sana”
“Nilijua tu kuwa lazima mtashirikiana vizuri, kwakweli George ni kijana aliyetulia, mpole na mwerevu yani toka nimeanza kufanya nae kazi hapa najivunia sana uwepo wake. Erica umeolewa?”
Erica akasita kidogo, na kujibu huyu mama,
“Sijaolewa ila nina mchumba”
“Yuko wapi huyo mchumba?”
“Anaishi nje ya nchi”
“Unamuamini?”
“Ndio namuamini”
“Waswahili husema fimbo ya mbali haiui nyoka, sitaki kukuvunja moyo ila huwa sina imani na penzi la mbali. Ningekuwa ni wewe ningeangalia mwanaume mwenye malengo na mimi, na mwanaume mwenye malengo na wewe ni Yule aliyekaribu nawe kwamaana mtaweza kupanga nae chochote kile”
Erica hakuelewa ni kwanini huyu mama ameamua kumueleza haya yote ila hakuweza kumpinga kwa chochote kwani ndio mwenye ofisi kwahiyo akamsikiliza tu. Kisha Yule mama akaendelea kuongea,
“Oooh nimeshasahau kama ni ofisini, sikia Erica naomba kesho tule wote chakula cha mchana muda wa kuondoka tafadhali”
Erica alimuitikia huyu bosi wake kisha akamruhusu kuendelea na kazi, Erica alirudi kwenye kazi zake na kufanya zile kazi. Muda wa kuondoka ulivyofika aliondoka zake na kwena nyumbani.
Kwa siku hizo zote hakukutana tena na Yule dada ambaye alikuwa jirani wa Bahati kwahiyo kwa namna nyingine aliona ni afadhali hakutani nae.
 
SEHEMU YA 298

Alifika kwao na kumsalimia mama yake kisha kwenda chumbani, na baada ya muda tu mama yake alimuita,
“Erica, nasikia shemeji yako alitishiwa kama ulivyosema basi karudi kwake na aibu hatari halafu Bite alichomwambia ni kuja kuomba msamaha, nahisi kesho au keshokutwa watakuja”
“Sawa hakuna shida”
Erica aliitikia na kutaka kurudi tena chumbani kwake ila mama yake akamzuia na kusema,
“Mbona una haraka hivyo wee mtoto, sijamaliza yangu ujue. Haya, huyo Erick anakuja lini? Nataka kujua maana ushauza mtoto”
“Atakuja tu mama”
“Kwa Rahim ulisema hivyo hivyo, atakuja atakuja na siku zikaenda unajua mara nyingine nawaza Yule aliyesema una kimavi usikute kweli mwanangu. Hebu leo muulize huyo Erick wako atakuja lini na unipe jibu, yani leo na kesho nakupa hiyo kazi halafu keshokutwa nitakuuliza tena swala la kuniambia atakuja tu sitaki kulisikia”
“Sawa mama”
Erica alimuitikia mama yake ila alihisi naye anataka kumchanganya tu kwani bado alikuwa na maswali mengi sana kichwani kuwa kwanini Yule mama amsifie George na badae kumuuliza kuhusu mahusiano yake, alijaribu kuwaza bila hata ya jibu ila hakutaka kile anachofikiria kiwe kweli maana alihisi huenda George na Yule mama ni watu wa karibu mno kwahiyo George amemueleza Yule mama kuhusu yeye na Yule mama anatafuta namna ya kumuweka karibu na George,
“Mmmmh ashindwe, simtaki George na sitamtaka kamwe bora nikose kazi ila sio kuwa tena na shetani kama George”
Aliwaza sana na mwishowe akapigiwa simu na Erick kama kawaida ila akaona hapo ni muda mzuri kumuuliza kuhusu alichoulizwa na mama yake,
“Erick, mama anahitaji kujua ni lini utakuja kwetu?”
“Nitakuja tu Erica”
“Ndio utakuja, ila ni lini?”
“Basi ngoja niandae mazingira kwanza, halafu kesho jioni nitakupa jibu kuwa ni lini”
“Halfu kitu kingine Erick, kama umeamua kweli kuwa na mimi naomba hao wanawake zako wote uachane nao.”
“Mbona nishaachana nao Erica”
“Bado hujaachana nao bhana, ukiachana nao nitajua. Waambie wazi watambue ya kwamba kuna unayempenda, nahitaji uachane nao kweli ili niwe na furaha kuwa napendwa na wewe”
“Sawa nitafanya hivyo Erica, nakupenda sana ujue”
“Nakupenda pia ila fanya hivyo nitafurahi sana”
“Furaha yako ndio furaha yangu, vipi mwanetu kalala?”
“Hahaha kalala ndio, si angenipora simu hapa”
“Basi akishtuka akitaka kuongea nami nibipu tu nitapiga”
“Sawa”
Basi Erica akaagana na Erick na kuamua kulala kwa muda huo.

Kesho yake kama kawaida, alijiandaa na kwenda kazini, ila siku hiyo ilikuwa ni siku fupi tofauti na siku zingine.
Alifika na kufanya shughuli zake, muda wa mchana ulivyofika yani karibu na kuondoka Yule mama alimuita Erica na kumkumbushia swala lake la kwenda kula nae chakula cha mchana, kwahiyo alimwambia amsubirie kidogo ambapo Erica alifanya hivyo.
Basi Yule mama alipomaliza alitoka na Erica na kupanda nae kwenye gari yake kisha wakaenda kwenye mgahawa mmoja mzuri sana na kumwambia Erica aagize anachotaka na yeye akaagiza.
Wakiwa wanasubiri chakula Yule mama alianza kuongea kwa kumuuliza Erica,
“Ulisema mchumba wako yupo mbali?”
“Ndio yupo mbali”
“Napenda kukushauri Erica, kuwa na mwanaume anayejielewa. Kwakweli George ni kijana anayejielewa”
Erica akatabasamu tu, kisha huyu mama aliendelea kuongea,
“Nakumbuka nilipokuwa binti kama wewe mapenzi yalinitesa sana sababu tu nilijifanya nachagua wachumba, uwiii yakanitokea puani yani mwanaume niliyezaa nae huwa najuta tu kuwa nilianzaje kuchukua maamuzi ya kuzaa nae. Ipo siku nitakueleza kwa undani zaidi, mimi nilibeba mimba nilikuwa nalia kila siku, nilijisemea nikizaa wa kike nitamfundisha kuwa wanaume ni viumbe wabaya na wenye roho mbaya. Nikasema nikizaa wa kiume basi nitamfundisha mwanangu awe na upendo wa kweli, asimuache mwanamke kulia, ajue kumbembeleza mwanamke maana lile shetani langu hata kubembeleza halijui”
Chakula kililetwa na kabla hawajaanza kula, yule mama alipigiwa simu kwahiyo aliinuka na kwenda kuongea na simu yake, alivyorudi alianza kuongea na Erica kuhusu simu aliyopokea na kusahau mada za nyuma,
“Kumbe mwanangu alikuwa akinipigia simu, jamani mimi nina mtoto mmoja tu kama jicho langu ila mtoto huyu ni pasua kichwa jamani mpaka huwa nahisi kizunguzungu sijui nilikosea wapi kwenye mimba yake”
“Kwanini mama?”
“Unajua alichoniambia? Eti kapata mchumba anataka kuja kumtambulisha kwangu, unajua nimechoka eeeh! Wasichana wengi wanakuja kwangu wakilia kuhusu mwanangu, nasikia uchungu sana kwangu na mimi nimepitia katika hali kama yao, huwa namuuliza mwanangu kwanini yupo vile? Hanijibu na mimi nakosa jibu kwakweli, nilishindwa kukaa nae hadi ilibidi akakae na babake tu labda karithi kutoka kwa babake huo uhuni. Kwakweli sitaki aniletee mwanamke mwingine kunitambulisha, kuna mmoja tu ndio namkubali, akishindwa kuoa huyo basi”
Erica alimuangalia tu huyu mama, kwani bado hakuelewa ni kwanini anamueleza yote hayo.
Wakati Yule mama akiendelea kulalamika kuhusu mwanae, simu yake ikaita tena na kuinuka kwenda kuongea nayo, baada ya kurudi akamwambia Erica,
“Mkwe wangu nimpendaye kanipigia simu, ila analia huyo balaa yani kashalizwa na mwanangu, nimemwambia aje hapa tuongee. Jamani mwanangu sijui kwanini anamliza mtoto huyu wa watu wakati nishamfundisha asimlize mwanamke, sijui amekuwaje jamani”
Kwakweli Erica hakujua kama aongee kitu gani maana alihisi kama ni mada zisizomuhusu vile, alipomaliza kula aliamua kumuaga huyu mama,
“Aaah jamani Erica, hutaki kumuona mkwe wangu?”
“Nitamuona siku nyingine mama”
Basi Yule mama akampa ruhusa ya kuondoka tu bila kinyongo, wakati Erica anatoka kwenye ile hoteli alimuona Sia mlangoni, alishtuka sana akaamua kujibanza ili Sia asimuone basi Sia akapita pale na Erica akaanza kumfatilia nyuma kuwa Sia anaenda wapi, akamuona akienda alipo Yule mama na alipofika alikumbatiana na Yule mama, ndipo akili ikamjia kuwa Yule ni mama Erick.
 
SEHEMU YA 299



Basi Yule mama akampa ruhusa ya kuondoka tu bila kinyongo, wakati Erica anatoka kwenye ile hoteli alimuona Sia mlangoni, alishtuka sana akaamua kujibanza ili Sia asimuone basi Sia akapita pale na Erica akaanza kumfatilia nyuma kuwa Sia anaenda wapi, akamuona akienda alipo Yule mama na alipofika alikumbatiana na Yule mama, ndipo akili ikamjia kuwa Yule ni mama Erick.
Kwakweli Erica aliishiwa raha muda ule, hata furaha hakuwa nayo tena, akaondoka na kuelekea nyumbani kwao.
Alipotoka tu nje ya ile hoteli wakati anatembea akielekea kituoni, hakuangalia mbele, kuna mmama aligongana nae na kujikuta akiangusha vitabu vya Yule mama ambavyo alikuwa amevibeba, aliinama kuviokota huku akimuomba msamaha sana Yule mama, ila Yule mama alimwambia,
“Usijali binti, ila unaonyesha una mawazo sana”
Erica alicheka tu ili kujigelesha swala la kuwa na mawazo, basi Yule mama alimuomba Erica namba ya simu na kusema,
“Mimi ni mwanamaombi, nimeomba namba yako ili niwe nakualika kwenye maombi kanisani kwetu. Hivi nawahi kanisani”
Kwavile Yule mama alijitambulisha kuwa mwanamaombi basi Erica hakusita kutoa namba yake kwa Yule mama kisha alimuaga na kuendelea na safari ya kuelekea kituoni.
Wakati yupo njiani akielekea kupanda daladala, alikutana na Moses njiani ambaye alisimamisha gari na kutaka kumpa lifti,
“Hapana usijali, naenda tu mwenyewe”
“Hapana Erica, yani nikuone hapa njiani nikuache kweli! Unataka nionekanaje mimi, naomba nikupeleke tu, si unaenda kwenu?”
“Ndio”
“Basi, naomba nikupeleke”
Basi Erica hakuona kama ni vyema kuendelea kubishana na Moses pale kwahiyo alipanda ile gari ya Moses na safari ya kuelekea kwao ikaanza.
Ila Moses alimuona Erica kama anainesha hana furaha ilibidi amuulize,
“Mbona unaonekana huna furaha?”
“Hamna nipo kawaida tu”
“Ni muda mfupi nimekuzoea Erica, hapana hivi ulivyo sio kawaida, inaonyesha una tatizo. Haya bhana kama hutaki nilijue”
Erica aliamua kubadilisha mada na kumuuliza,
“Kwani ulikuwa unaenda wapi?”
“Aaah leo niliwahi kutoka ili nimuwahi mke wangu, nimemmiss sana, wiki yote hii nipo busy sina siku ya kupumzika yani kila siku nipo kazini, kwakweli leo nimewahi kutoka na kesho nimemuomba udhuru Erick maana sitafungua duka nahitaji kuwa karibu na mke wangu”
“Sasa kumbe unawahi kwa mkeo, mbona umejitolea kunipeleka mimi nyumbani?”
“Erica, hivi naanzaje kumwambia Erick nilikutana na Erica njiani akielekea nyumbani ila sikumpeleka, naanzaje kusema? Unajua sielewi kipi kipo katikati yenu wewe na Erick ila nahisi mnajuana, mi nikikupeleka ndio nitaenda kwa mke wangu najua hata Erick nikimwambia hivyo atafurahi sana”
Erica akatabasamu tu na kumuuliza tena Moses,
“Inaonyesha unampenda sana mke wako”
“Yani nahisi nampenda kuliko hilo neno na sana, yani nampenda balaa”
“Hukuwahi kuwaza kumsaliti?”
Moses akacheka,
“Erica, huwa nakutana na wasichana warembo kama wewe hivyo ila kwakweli sababu mke wangu nimempa nafasi ya kwanza basi anakuwa ni mrembo kuwazidi wote. Na kwanini umeniuliza hilo swali?”
“Nasikia wanaume hawajatulia na mwanaume hawezi kutulia na mwanamke mmoja yani lazima atatafuta wa pembeni”
“Tatizo watu hutoa jibu kwa mfano wa mtu mmoja tu. Mimi toka nimuoe mke wangu sijawahi kumsaliti hata mara moja na wala sifikirii kumsaliti nampenda sana. Sisi wanaume pia tunapenda, ukiona mwanaume anahangaika na huyu mara Yule ujue hajapata bado Yule wa kwenye roho yake ndiomana anashika huyu mara huyu ili kuangalia je anaweza akamteka akili yake, ila akishampata wa kwake lazima atatulia. Yani mara nyingine sio mambo ya kulaumu sana sijui wanaume hawajatulia sijui nini na nini, watu hawaelewi tu mtu anakuwa hajapata hitaji lake au anayempenda kwa dhati anazingua ndio utakuta anahangaika hangaika ila akimpata wake hadi utashangaa ndio huyu kweli wa kuruka ruka na wanawake”
Erica alitabasamu tu kwani hapo aliweza kuelewa kuwa kwa Erick basi ni yeye ndiye mwenye nafasi kubwa sana, Moses alimuona Erica akitabasamu tu na kumuuliza,
“Vipi mbona furaha tu”
“Nimefurahi, nimependa vile ulivyosema unampenda sana mkeo. Hakika ulimwengu ungekuwa kama unavyosema basi hata magonjwa ya zinaa yasingekuwepo. Tatizo ni moja tu huyo mwenye upendo wa dhati utamjuaje?”
“Inamaana wewe humjui unayempenda kwa dhati? Yani mtu ukimpenda jamani, hata ukisikia jina lake tu unajisikia furaha, unaweza ukakaa halafu labda likatokea jambo unajikuta ukiwaza angekuwepo Fulani hapa yani unajikuta unapenda tu uwepo wake. Ila kama mtu upon aye tu kupeleka siku mbele vyovyote vile unaona sawa, awepo asiwepo unaona sawa, apige simu, asipige unaona sawa yani hata hujali uwepo wake ila unaweza kujigelesha na kujifanya kuwa unamkumbukaga kumbe kiukweli hakuna kitu”
Walifika nyumbani kwakina Erica, kwakweli Erica alimshukuru Moses na alishukuru pia kwa mazungumzo aliyozungumza nae kwa siku hiyo, kisha akamuaga na kuingia ndani.

Aliingia ndani kwao na kumkuta dada yake Bite pamoja na James, inaonyesha walifika kama mama yao alivyosema kuomba msamaha, pia ilionyesha ni muda huo huo ndio wametoka kufika. Baada ya salamu Erica aliambiwa na mama yake akae pale kwani walihitaji wasikie wote msamaha anaouomba James kwa Erica, basi james alianza,
“Erica shemeji yangu, mdogo wangu naomba unisamehe maana nilichokuwa nafanya kwako sio sawa. Ni shetani tu huyu anataka kuharibu undugu wetu, naomba unisamehe sana. Mimi bado ni shemeji yako na mimi bado ni mwanafamilia wenu. Naomba unisamehe Erica”
“Hakuna tatizo, nishakusamehe ilimradi umegundua kosa lako basi nimekusamehe”
“Nashukuru sana, mama naomba nawe unisamehe sana mtoto wako. Nisamehe kwa yote niliyokuwa nasema kuhusu Erica, nisamehe kwa tukio lile, ni shetani tu alinipitia”
“Nilikuwa nakusikiliza kwa makini sana habari za kusema shetani kakupitia, James usisingizie shetani ila ni akili zako mbovu ndio zimekutuma kufanya vile. Mimi sina tatizo, kaa chini na mkeo mlee mtoto wenu, ujinga ujinga wa kuendekeza ngono utakuponza. Mbona mwanangu Bite mzuri tu jamani kwanini unashindwa kuridhika James? Hebu tulia na mwenzio, na kipindi ukimchoka niletee mwenyewe nikae nae.”
“Usifike mbali mama yangu, nisamehe mtoto wako”
“Nishakusamehe na sina tatizo tena. Ila naomba nikuombe jambo moja”
“Jambo gani mama?”
“James, ingawa tumekusamehe na hatuna tatizo na wewe ila tafadhali sana sitaki ukaribu wako tena na Erica maana huyo shetani wako akakupitia tena ukasababisha matatizo kwa wanangu bure. Sitaki tena ukaribu wako na Erica, una shida yoyote kwa Erica niambie mimi nitafikisha ujumbe”
“Sawa mama nimekuelewa”
“Sawa, najua na mkeo mlishaombana msamaha huko mpaka mmefika hapa”
Bite akajibu,
“Ndio mama, nimeshamsamehe”
“Ila sio unasema umeshamsamehe huku bado una kinyongo moyoni, mumeo kakiri mwenyewe hapa ana urafiki na shetani hadi huwa wanapitiana, kwahiyo elewa kabisa sio unaitikia halafu kesho na keshokutwa unaanza sijui mama kimeenda kimerudi sitaki”
“Sawa mama”
Kisha wakainuka na kushikana mikono, na muda ule ule Bite na mumewe waliaga kwani bado James aliona aibu kuendelea kuwa mahali hapo akizingatia mama yao na wakina Bite hajambakisha na kitu, amemwambia ukweli tu.
Walipoondoka, Erica nae alienda chumbani kwake.
 
SEHEMU YA 300


Kwakweli Erica hakuwa na raha kabisa, kuna mambo mengi sana alikuwa akijiuliza bila jibu hata kidogo,
“Hivi hii maana yake nini katika maisha yangu? Nilikuwa na shida haswaa baada ya kuachwa kwenye mataa na George, akatokea msamalia mwema kunisaidia, akaonyesha kunipenda na kunijali huku akitamani hata ningekuwa mtoto wake, msamalia mwema huyo ndio mama wa Rahim, hakutaka hata kusikia kuwa nina mahusiano na mtoto wake kiasi kwamba hata mjukuu wake hana imani naye, kwamaana hiyo mama huyu imani na mimi imemuondoka gafla, haya sasa katokea mama mwingine na kunifuta machozi ya kutokuwa na kazi kwani kanipa kazi ila ndio mama yake Erick, kuna nini katikati yangu jamani! Sidhani kama ni baraka hii ila ni mkosi tu hata sijui nifanyeje, sitamani hata Jumatatu ifike maana akiambiwa kuhusu mimi hivi atanionaje?”
Aliwaza bila ya jibu, ila kwa upande mwingine akakumbuka kuwa kuna mama alikuwa akimuombea msamaha Erick, ila mbona hakuwa huyu bosi kama ndio mama wa Erick? Kwakweli hakuwa na raha kabisa ila alihitaji kuujua ukweli, akaamua kujilaza kidogo.
Mwanae ndio alimuamsha na giza lilishaingia tayari kwahiyo aliamka na kwenda kumuogesha mwanae kisha kumpa chakula, kwakweli yeye hakujihisi hata hamu ya kula kwangu alikuwa anahisi kila kitu ni kibaya kwa upande wake, akatamani kumueleza ukweli Erick ila akawaza kuwa ataanzia wapi, kuna moyo mwingine ukamuambia kuwa lazima aseme ukweli ili Erick ajue kuwa itakuwaje, muda kidogo wakati anatafakari Erick alipiga simu na kama kawaida mwanae alichukua na kuongea nayo kisha kuirudisha kwake, halafu Erica akaanza kuongea na Erick ila alitaka kujua ukweli kwanza kama Yule mwanamke wa ofisini ni mama yake Erick, alianza kumuuliza kwa mitego,
“Hivi Erick, Yule mama aliyekuwa akikuombea msamaha ofisini kipindi kile unafukuzwa shule ndio mama yako mzazi?”
“Hapana, Yule alikuwa mama mdogo, maana mama yangu kuna kipindi aliniacha nalelewa na mamdogo”
Kisha akaona bora amuulize kwanza kuhusu alichomwambia jana ili asikie Erick ana jibu gani hapo,
“Erick, niambie sasa utakuja lini kwetu na utanioa lini?”
“Erica, unaweza kuhisi nakuongopea au ukahisi sina lengo jema na wewe ila si kweli Erica, nakupenda sana na lazima utakuwa mke wangu ila kuna mazingira tu lazima niyaweke sawa kwanza”
“Mazingira gani? Niambie”
“Ngoja nikueleze ukweli Erica, nimemwambia mzee wangu kuhusu swala la mimi kutaka kuoa jamani huyu mzee kanipinga vikali sana akidai kuwa mimi bado ni mtoto mdogo, sasa mimi nina udogo gani jamani? Wanaoa vijana wa miaka ishirini sembuse mimi kweli! Nadhani ni sababu baba yangu hajawahi kuoa maishani mwake, ila akaniambia kitu cha kunishangaza sana, kuwa hivi karibuni na yeye ataoa kwahiyo nimsubirie yeye aoe ndipo na mie nianze na wazo la kuoa. Ilibidi niachane na huyu mzee, nikampigia mama, yani na yeye ni shida tupu. Kuna msichana mmoja anaitwa Sia, huyu msichana anampaga maneno ya sumu sana mama yangu hadi mama kajikuta anampenda huyu msichana na kunichagulia mimi kuwa nimuoe ila mimi simtaki Sia, yani mama nimerumbana nae sana, na jioni katoka kunipigia simu sijui yupo na huyo Sia yani tumegombana tu. Sasa, kwa baba na mama kote sijafika nao muafaka ndiomana nakuwa mgumu sana kusema kuwa ndoa ya mimi na wewe ni lini? Erica, tunaweza kuoana tu ila baraka za wazazi nazo ni muhimu. Naomba nipe muda niliweke sawa jambo hili”
“Mfano wazazi wako wakikazana kuwa hawataki tuoane utafanyaje?”
“Erica nipe muda tafadhali. Nishakwambia kwasasa hakuna kitu cha kunifanya mimi nikuache wewe, nakupenda sana. Wazazi wangu watanielewa tu maana hata wafanyeje bado mimi ni mtoto wao. Nipe muda Erica nakuomba”
Erica alikubali na kuagana nae, baada ya kukata simu aliwaza swala la mama yake Erick, jinsi alivyokuwa akiongea nae na jinsi Sia alivyofika, yani pale picha halisi inakuja ya mama yake Erick ila akawaza kama akimwambia Erick kuwa mama yake ndio bosi wake kazini inaweza ikawa tatizo kubwa maana Yule mama atamjua mapema na pengine kumletea longolongo, akaona bora kama yakimshinda kabisa basi ndio amwambie Erick kuwa huyo mama ndio bosi wake.
Kwa muda huo aliamua kulala ila kabla hajalala kuna ujumbe uliingia kwenye simu yake, akafungua na kusoma akakuta umetumwa na Yule mwanamama aliyesema kuwa ni mwanamaombi, ujumbe ulisema kuwa
“Mkumbuke muumba wako siku za ujana wako”
Akawaza ni kwanini Yule mama amemtumia ujumbe huo kwa muda huo ila hakutaka kufikiria sana akaamua kulala tu.
 
SEHEMU YA 301


Palivyokucha wakati mama yake akijiandaa kwenda kanisani, Erica nae alijiandaa na kumwambia mama yake kuwa siku hiyo ataenda nae kanisani,
“Kheee kwakweli Mungu mkubwa yani leo kwa hiyari yako Erica umekubali kwenda kanisani?”
“Ndio nimekubali mama”
Basi akajiandaa na kumuandaa na mwanae na kwenda kanisani.
Wakati wanatoka kanisani, kuna wamama walisogea wakimuuliza Erica kuwa mtoto wa nani, aliposema ni wake walikuwa wanakataa kabisa maana hawakuwahi kumuona akiwa na mimba,
“Kheee mtoto una siri wewe, kumbe ulibeba mimba hadi ukazaa?”
Mwingine akasema,
“Hata mama yake ni msiri, hata kutudokeza hamna jamani!”
Erica alicheka tu, wakamuangalia mtoto pale hadi kuondoka ana kwenda nyumbani, walipofika nyumbani mama yake alianza kuongea,
“Yani wale wanawake ulisimama nao ni waongo hao hatari, ndiomana nilivyoona wamesimama na wewe tu nikajificha”
“Kheee mama, watu wameokoka halafu wanakuwa waongo?”
“Sikia Erica, uongo ni tabia ya mtu halafu mwingine anasema ameokoka si kweli mbona hata maandiko yamesema sio wote wasemao Bwana Bwana watauona ufalme wa mbingu. Cha msingi ni wewe kushikilia kile unachokiamini, usimuamini mtu sababu kasema ameokoka yani usiamini kabisa, kuwa na imani yako moyoni itakayokuongoza”
“Sawa mama, ila leo nimejisikia afadhali. Sema kuna jambo nataka nikushirikishe mama yangu”
“Jambo gani hilo?”
Erica akawaza sana, na kutokuelewa anaanzaje kuelezea kuhusu mama yake Erick, ila akajaribu kumuuliza swali mama yake,
“Hivi mama mfano unataka kuolewa ila wakwe zako hawakupendi inakuwaje?”
“Mwanangu, hakuna ndoa inayoumiza moyo kama ndoa ya kuchukiwa na wakwe sijui mawifi sijui mashemeji, tena ndoa ya hivyo bora uombee mumeo awe upande wako, ila akiwa upande wa ndugu zake utahisi dunia ikipasuka. Kwanini umeniuliza hivyo?”
“Mama, wakwe zangu hawanipendi?”
“Unawajua? Ushatambulishwa?”
“Bado, ila hawataki hata kunifahamu”
“Mmmh ndio wazazi wa Erick hao?”
“Ndio mama”
“Kheee na mtoto ushauza kwenye ukoo wa watu wasiojielewa kama hao, mmmh ila usipaniki ngoja mwanangu nitaliombea swala hilo”
“Nashukuru mama”
Erica alienda chumbani kwake sasa, alitulia kidogo kuwa kamueleza mama yake ingawa hakumwambia ukweli wote.
Aliamua kulala ila kabla hajalala alisikia simu yake inaita, akaichukua na kuiangalia akakuta ni Dora anampigia, akaamua kuipokea kwani hakujua ni jambo gani limemfanya apige simu usiku huo ukizingatia ni muda tangu aongee nae, alipokea ambapo Dora alianza kwa kumsalimia kisha akamwambia,
“Erica, una mpango gani na Yule baba?”
“Hivi Dora kwanini huelewi? Nishakwambia Yule mzee simtaki tena simtaki kabisa”
“Sikia Erica, Yule mzee anakupenda kweli. Aliniuliza kuwa rafiki yako nimfanyie nini akubali, nikamwambia labda umuoe maana rafiki yangu ni muda mrefu sana anahitaji ndoa. Yule mzee kanihakikishia kuwa hataki kukuchezea, anataka kukuweka ndani kabisa uwe mke wake, na kasema ataifanya familia yako ifurahie utajiri wake. Erica Yule mzee anakupenda”
“Dora usione nimenyamaza nakusikiliza ukadhani nafurahia huo ujinga wako unaozungumza, yani ungejua unanichefua tu. Dora, mimi na wewe urafiki ulishaishha na licha ya hivyo huyo mzee Jimmy mfikishie ujumbe kwamba Erica hata umuhonge dunia hakutaki. Kwaheri”
Erica alikata simu ya Dora, ila hakutaka kufikiria alichokuwa akiongea na Dora badala yake alikuwa akiwaza tu kuhusu Jumatatu kwani aliiona ni mbaya kwake ukizingatia hakujua ni maneno gani Sia kamwambia Yule mama, alikosa raha kabisa kiasi kwamba alilala kwa mang’amung’amu.
 
SEHEMU YA 302

Kulivyokucha, mapema kabisa aliamka na kujiandaa na kwenda kazini, alifika na kuanza kazi zake na kama kawaida alimkuta George ila hakupewa salamu wala nini, ilibidi leo aamue kumsalimia mwenyewe ila George aliitikia kwa sauti ya chini kabisa na kumfanya Erica ajiulize sana kuwa kwanini George anamfanyia vile ila bado halikuwa tatizo hilo kwake kwani hakuwa hata na wazo la kurudiana na George.
Wakati anaendelea na kazi zake, muda kidogo aliitwa na Yule bosi wake ambaye alianza tena kuongea nae kuhusu habari za George,
“Erica, binti yangu sikia, nimekuita hapa ili kukwambia jambo moja. Tangu nimeanza kufanya kazi na George hapa ni miaka imepita na hakuna siku aliyowahi kuniambia kuwa kuna mtu kampenda, kwakweli ni mara ya kwanza George kaniambia kuna mtu kampenda na anataka kumuoa. Erica, kwakweli George anakupenda sana ila kukueleza anashindwa ndiomana kaniambia mimi”
Erica akamjibu huyu mama,
“Mama, ila mimi nina mchumba wangu na ninampenda sana”
“Ila si nishakueleza madhara ya kuwa na mchumba wa mbali Erica!”
Kabla Erica hajampa maelezo mengine, simu ya Yule mama ikaita na akaipokea na kuongea nayo. Alipomaliza akamuangalia Erica na kusema,
“Kwakweli wanawake tunashida jamani ndiomana huwa wanasema tuombee matumbo yetu kabla ya kubeba mimba na kuzaa, jamani mimi sijui nimezaa kituko cha aina gani, hivi mwanangu ni wa kunifanyia hivi kweli?”
Ilibidi Erica aulize,
“Kafanyaje?”
“Jamani, eti kapata mwanamke ila huyo mwanamke ana mtoto kumbe halafu yeye kajimilikisha huyo mtoto na kuchukua majukumu ya mtoto kama yeye ndio baba, yani hapa ndio dadake kanipigia simu alikuwa ananieleza, nimemwambia aje hapa ofisini ili niongee nae vizuri, nahiotaji kumjua huyo shetani aliyevuruga akili ya mwanangu”
Erica akaona hapa ni balaa juu yake hadi alihisi akishikwa na tumbo la kuhara, na kuomba ruhusa mara moja.
Alienda chooni ila hata hakuweza kujisaidia, alihisi tu tumbo likimsokota, alitulia kwa muda hadi tumbo lilipotulia.
Akarudi kwenye ofisi yake ila hakuweza kufanya kazi ya aina yoyote kwani aliona kila anachoshika hakishikiki, wasiwasi wake ni pale Tumaini atakapofika na kumkuta, ikabidi atumie kigezo cha kuumwa na tumbo ili kuomba ruhusa ya kwenda nyumbani.
Alienda kwa bosi wake na kumueleza jinsi tumbo linavyomsumbua,
“Mbona gafla jamani, kwani tangu asubuhi lilikuwa likikusumbua?”
“Hapana, limeanza gafla tu. Huwa nina vidonda vya tumbo, nahisi ndio vimecharuka”
“Aaah pole sana, nenda nyumbani kapumzike ila kuwa makini sana na vyakula unavyokula kuepuka hivyo vidonda”
Erica alimuitikia huyu mama, kisha akainuka na kwenda kuchukua mkoba wake na kutoka.
Wakati anatoka mlango wa nje, sababu alikuwa na harakati akajikuta akigongana kikumbo na mtu, kumuangalia vizuri alikuta ni Tumaini naye akimuangalia pia.
 
SEHEMU YA 303

Wakati anatoka mlango wa nje, sababu alikuwa na harakati akajikuta akigongana kikumbo na mtu, kumuangalia vizuri alikuta ni Tumaini naye akimuangalia pia.
Erica alishtuka na kuwa kama amesizi kwa muda maana ndio huyo huyo alikuwa akikimbia ili asimkute halafu ndio kagongana nae kikumbo, Tumaini alitingisha kichwa na kusema,
“Ama kweli wewe binti ni mchawi, yani hadi ofisini kwa mama yake Erick! Ulikuwa unafata nini huku?”
Kwavile Erica alishavurugwa, aliamua kumjibu tu kwani kwa muda huo alijisemea kuwa liwalo na liwe,
“Hivi wewe Tumaini kwani unanitakia nini mimi? Sio kwa kunifatilia huko”
“Nakutakia nini? Achana na mdogo wangu”
“Unajua wewe una mambo ya Kiswahili sana halafu ndio unasema baba yenu tajiri umelelewa maisha ya kitajiri, na umesoma ila una uswahili mwanzo mwisho. Kufatilia yangu, kwanini muda huo usikae kufatilia ya mumeo atakayekuoa? Kwani wewe huna mchumba? Huna mpenzi? Yani unaacha kupanga mambo na mchumba wako huko, unakazana kila leo kumfatilia Erica, unapata faida gani unapofanya hivyo? Na unasema niachane na mdogo wako, huyo mdogo wako unamtaka wewe au nini?”
Alipoongea hayo alikuwa mbali kabisa anaishia maana alijua kama angekuwa karibu basi Tumaini angemdunda, maana pale Tumaini alionyesha amechukizwa sana kiasi kwamba Erica angekuwa karibu basi angemkomesha.
Erica aliliona jicho la Tumaini linavyomuangalia kwa hasira, hivyo akaamua kusimamisha bodaboda na kupanda kuelekea nayo stendi.

Wakati amepanda daladala, leo alikutana tena na Fetty na kumfurahia sana, ambapo waliongea mengi mengi, Fetty akamuomba wakae mahali waongee na kushauriana mambo mbalimbali, kwavile ilikuwa mapema Erica hakuona tatizo la kukaa na kuongea na Fetty.
Kwahiyo walishuka mahali na kwenda kukaa kwenye mgahawa Fulani wakiongea huku wakipeana ushauri mbalimbali,
“Erica nimefurahi sana kukutana na wewe, kuna mambo yananitatiza akili yangu ila najua nimekutana na wewe utanishauri”
“Yapi hayo?”
“Bhana mwenzio kuna kitu nimefanya, kwakweli sijapenda ila niliamua kufanya maana maji yalinifika shingoni”
“Kitu gani hiko?”
“Nishawahi kukwambia kuhusu baba wa mwanangu, sasa baada ya kunitimua kule na kurudi nyumbani. Watu wakaniambia nisikubali nizunguke zunguke maana sio hali ya kawaida, na mimi nimeangalia kweli sio hali ya kawaida ukizingatia mwanzoni alikuwa akinipenda tu. Nikaamua kwenda kwa mtaalamu”
Erica akaamua asikilize kwa makini sasa,
“Eeeeh!”
“Sasa bhana, mtalaamu Yule kiboko yani anaonyesha kila kitu unaangalia kwenye kioo kama sinema vile. Ni kweli ndugu wa baba wa mwanangu hawakutaka awe na mimi, sasa kuna mwanamke walimtafutia ndugu yao, walichofanya ili ndugu yao aachane na mimi ni kwenda kwa mganga wakachukua dawa. Ila dawa zenye nguvu bhana huwa zinataka muhusika mwenyewe atende kile kitendo kwahiyo Yule mwanamke alipika chakula na kuweka dawa aliyopewa kisha yeye mwenyewe akamtengea Yule bwana chakula kisha Yule bwana akala si ilikuwa kwao bhana, hata kujiuliza kwanini chakula nitengewe na huyu hakuna, kala kile chakula ndio akaanza varangati kwangu hadi kunifukuza. Kwakweli nimesikitika sana Erica, sasa Yule mtaalamu kasema kazi anaiweza, eti nishirikiane nae tutengeneze makombora ya kumrushia Yule mwanaume ili arudi kwangu. Nimemuitikia tu kuwa nitaenda tena, ila nikajifikiria, Yule mwanaume kapewa dawa, na mimi nimpe dawa zingine si ndio mwanzo wa kuwa chizi Yule!”
“Dah! Rafiki yangu Fetty, kwanza nakupongeza kwa kuwa na moyo wa huruma kama huo maana mwisho wa siku mtamchanganya tu huyo mwanaume, mi naamini kuwa dawa huwa zinaisha nguvu, yani kuna siku tu atarudi kuwa na akili zake timamu.”
“Ni kweli Erica, ila ndugu jamani sijui akili zao zikoje yani wanaacha kufatilia mambo yao wanaanza kufatilia mambo ya watu wengine. Yani wanashangaza sana”
Erica akaamua kumueleza pia kuhusu yeye na Bahati, na jinsi alivyoambiwa kuwa Bahati karogwa,
“Tusiandikie mate wakati wino upo, una elfu kumi hapo?”
“Ya nini?”
“Nataka twende kwa huyo mtaalamu na wewe ukaone kila kitu kilichotokea kwa huyo mwanume. Majina yake yote si unayajua?”
“Ndio nayajua, ila Fetty mimi sijawahi kwenda kwa mganga yeyote toka nizaliwe”
“Erica, kwani tunaenda kuua? Tunaenda kupata ukweli tu, twende acha uoga”
“Kwanza mganga mwenyewe yuko wapi?”
“Yupo Kigamboni”
“Mmmmh jamani Fetty, toka kigamboni si nitachelewa sana nyumbani”
“Hivi Erica mbona unachekesha, kuna watu wanakaa chamanzi na wanafanya kazi kigamboni, wanaenda na kurudi kila siku sembuse wewe wa karibu hapo”
“Kigamboni yenyewe sehemu gani?”
“Kigamboni kwa huyo mtaalamu sio pale ni kigamboni kule unaweza hadi kukutana na Mbagala. Kwahiyo tukubaliane tu tuwahi kwenda ili tuwahi kurudi”
“Jamani Fetty”
“Usijali, kutoka nitakusindikiza hadi kwenu”
Basi Fetty akamshawishi shawishi pale mwisho wa siku akakubali na kwenda na Fetty kwa mganga.
 
SEHEMU YA 304

Walifika kwa huyo mganga na kukuta kuna watu wachache tu, kisha walipoisha waliingia wao ili kuangaliziwa matatizo yao, Erica aliamriwa aweke elfu kumi kwenye kimtungi kidogo kisha aliambiwa ataje jina la huyo mtu anayehisi amefanyiwa limbwata ili waone imeanzia wapi. Baada ya hapo, Yule mganga alipaka unga kwenye kioo chake na kuanza kuwaonyesha Erica na Fetty, kwakweli Erica alishangaa sana kwani ilikuwa kama anaangalia sinema.
Aliwaona ndugu wa Bahati na Yule mshenga wakienda kwa mganga kuchukua dawa, na baada ya hapo walimkabidhi dawa Yule binti ila Yule binti kisha alienda nyumbani kwakina Bahati na kumuandalia Bahati chakula ambapo alimtayarishia na kula, kisha Bahati akaonekana amepatwa na usingizi baada ya kile chakula.
Ikaonyesha tena Yule dada alipelekwa tena kwa mganga na baba yake, safari hii akapewa dawa nyingine, ile dawa Yule dada alionekana akiiweka sehemu za siri baada ya hapo akaandaa chakula na kumpelekea Bahati na alionekana anakula kisha alimpa kinywaji ambacho kiliwekwa pia dawa hiyo, alikunywa pia na baada ya hapo ilionekana harusi kisha Yule mganga akafuta ule unga kwenye kile kioo na kikawa tu kioo cha kawaida, kwakweli Erica alishangaa sana kwani hakuwahi kushuhudia mambo kama yale, aliamua kumuuliza Yule mtaalamu,
“Sasa kwanini dawa nyingine ile aliweka sehemu za siri?”
“Sehemu za siri zina nguvu sana, na ukifanyiwa limbwata la sehemu za siri huwa nguvu yake si ya mchezo yani unajikuta ukisahau kila jambo”
“Mmmmh makubwa”
“Inatakiwa tuanze tiba mapema, si unataka arudi kwako”
“Aaah muache tu mpaka dawa zitakapoisha”
Yule mganga akamuangalia Fetty na kumuangalia Erica kisha akasema,
“Wewe Fetty, ya kwako hatujamalizana, huyu rafiki yako naye hatumalizi tunaacha viporo tu kwanini?”
Fetty akajitetea pale,
“Yani sisi babu tulitaka tu kujua ukweli”
“Haya sawa, ukweli mmeshaujua. Ngoja nikuombe kitu kimoja Fetty, kamsubiri nje huyu rafiki yako Erica, halafu wewe Erica ubaki hapa na mimi kuna mambo nataka nikuonyeshe”
Basi fetty akatoka, Erica alibaki mwenyewe na Yule mganga ila alikuwa na wasiwasi sana, Yule mganga alikoroga dawa na kumpa Erica ili anywe, pale pale Erica akakumbuka jinsi limbwata linavyofanya kazi nay eye ana damu ya kupendwa pendwa akaogopa maana inawezekana hata mganga akawa amempenda, hakutaka kumuwekea mashaka ila hakutaka kunywa ile dawa, aligoma kuinywa na kumfanya Yule mganga amuulize kwanini anagoma kunywa,
“Sijaja kwa ugonjwa hapa, kwahiyo sioni sababu ya kunywa dawa”
Yule mganga alimuangalia Erica, na kumpulizia kitu ambapo kwa muda mchache macho ya Erica yalikuwa kama yamepuliziwa pilipili na kumfanya ajifikiche sana, basi Yule mganga akawa anampa ile dawa anywe kuwa ndio pona yake ila bado Erica aligoma, na muda ule ule aliinuka na kutazama kwa shida hadi kutoka nje kwani macho yalikuwa yakimuwasha ila alivyofika nje muwasho uliisha pale pale, hakutaka hata kukaa alimwambia tu Fetty waondoke ikabidi Fetty amfate kwa nyuma, kwakweli Erica alitembea kwa haraka haraka sana, mpaka ilibidi Fetty atembee kwa mwendo kama wa kukimbia, walivyofika stendi Fetty alimuuliza Erica kuwa imekuwaje,
“Unajua Yule mganga alikuwa akinilazimisha ninywe dawa yake, kumbuka Fetty sijaja huku kwa ugonjwa”
“Ila kwanini umegoma kunywa?”
“Fetty, tumetoka kuangalia pale pale limbwata linavyofanya kazi je kama Yule mganga kanitamani je!”
“Hahaha Erica jamani, sasa kwanini Yule mganga akutamani?”
“Hujui tu Fetty, kwakweli niende nyumbani kwasasa, nimechelewa hivi sijui mama nitamueleza vipi?”
Walipopata usafiri basi safari ikaendelea.
 
SEHEMU YA 305

Kwenye mida ya saa tano usiku ndipo Erica aliingia nyumbani kwao, kwakweli mama yake alifoka sana maana hakupendezewa kabisa kuona mwanae kachelewa kufika nyumbani kiasi kile.
“Erica, kweli mpaka muda huu mwanangu”
“Nisamehe mama”
“Sijapenda, yani sijapenda kabisa”
Akataka kumchukua mtoto ili akamlaze chumbani,
“Hebu nenda kaoge huko usinipakie mjukuu wangu unajisi, najua umetoka wapi hadi muda huu kweli? Nenda kaoge huko”
Basi Erica alienda kuoga kisha kumchukua mwanae kwenda nae chumbani, kiuwekili hata hamu ya kula hakuwa nayo kabisa.
Aliamua tu kulala, akiwa katikati ya usingizi, akamuona Yule mganga ndotoni akimwambia,
“Nakupenda sana Erica, nitakufanyia kila kitu utakacho. Nakupenda sana”
Kisha akamuona Yule mganga akimsogelea kama anataka kumbusu hivi, Erica akashtuka huku jasho likimtoka, akaogopa sana hata kulala tena aliogopa na kuanza kukumbuka story za watu kuwa kuna majini mahaba, kwahiyo alijikuta akijawa na mashaka sana kuwa pengine akute majini mahaba.
Alikaa kaa kisha akaamua kulala tena, muda huu aliona kama yupo ka Yule mganga halafu anataka kunywa kile kinywaji, Erica alishtuka na kuita mama yake kwa nguvu, mama yake alifika na kumkuta Erica akihema sana ikabidi amuulize kuwa tatizo ni nini,
“Kuna mtu wa ajabu nikilala ananijia mama yani nakosa hadi usingizi”
Ikabidi mama yake aingie kwenye maombi, na baada ya yale maombi ndipo Erica akalala sasa.

Kulivyokucha, mama yake alienda kumshtua saa mbili asubuhi,
“Kheee wewe huendi kazini? Wewe mwenyewe urudi saa tano za usiku halafu hadi saa hizi hujaenda kazini tatizo ni nini?”
“Nilisahau kuamka mama”
“Haya amka ujiandae”
“Ila mama nishachelewa”
“Aaah sitaki kusikia hizo mada, jiandae uwende kazini utatafuta jinsi ya kumueleza bosi wako ila uende kazini, na kama huendi utoe taarifa sio kama mambo ya shemeji yako James kuwa kila siku ulikuwa unamuomba ruhusa, kumbuka huko ni ofisi mpya”
Basi Erica aliinuka kitandani na kwenda kuoga halafu kujiandaa ili aende kazini, sema kiukweli hakutaka kwenda tena kazini ila akaenda tu sababu ya mama yake.
Basi alifika ofisini kwenye mida ya saa nne kasoro, akaona ni vyema aende kwanza kwa bosi wake kuripoti ili ajue mbivu na mbichi ila cha kushangaza alivyofika kwa bosi wake hakumkuta ofisini, kwahiyo akaamua kwenda kwenye ofisi yao na kumkuta George akiendelea na kazi, akamsalimia kisha George akamuuliza,
“Mbona leo umechelewa sana?”
“Nilishikwa na tumbo la asubuhi yani limeniendesha sana”
“Aaah pole ila mbona upo hivyo?”
“Nipoje?”
“Aaah hamna kitu”
“Na bosi yuko wapi maana nilikuwa nataka nimwambie kuwa kwanini nimechelewa”
“Hivi unadhani huyu mama huwa anafatilia kiasi hiko? Kama kitengo hiki ninayefatilia ni mimi, sema na uzuri ni kuwa leo hajafika ofisini na sijui kwanini hajafika”
“Aaah kumbe”
Basi Erica akaanza kufanya kazi za pale ila alikuwa na mawazo sana kiasi kwamba hakuwa na raha kabisa.
Muda wa kutoka, leo George alimwambia tena swala la kumpa lift Erica ila Erica aligoma kwani bado alikuwa na kumbukumbu ya kitendo cha kipindi kile cha George kutaka kumbaka, sasa akimgeukia humo kwenye gari itakuwaje? Kwahiyo akaona ni vyema akapande daladala tu kama kawaida.
Basi akaondoka na kwenda stendi ya daladala kama kawaida, ila leo kabla hajapanda alihisi kama kuna uwepo wa mtu nyuma yake, akageuka ila hakumuona mtu yeyote, akaamua kusogea eneo lingine bado alijihisi kuna mtu kasimama nyuma yake, ila alipogeuka hakuona mtu tena. Hofu ikamshika na kutamani daladala ifike tu apande maana hakuelewa ni mtu gani anamfatilia, gafla akapigiwa simu na kupokea, Yule aliyempigia alijitambulisha kuwa Yule jirani wa Bahati, kwa hapo akahisi kuwa ni huyo ndio anamfanyia mchezo wa kukaa nyuma yake ila akamsikiliza’
“Erica, ikija daladala hata kama imejaa ingia upande, ukifika nyumbani nipigie nikwambie maana mtu aliyekuwa nyuma yako si mtu mzuri. Usinijibu ila panda daladala iliyojaa akose nafasi”
Erica aliogopa hata kumjibu Yule dada, na kweli daladala ilikuja imejaa maana muda wote alikuwa akisubiri daladala tupu ili akae kwenye siti, ila toka ameambiwa hivyo alipanda daladala iliyojaa na kuondoka zake.
 
SEHEMU YA 306


Alivyofika kwao, alimsalimia mama yake kisha aliingia chumbani kwake kwani alikuwa na hamu sana ya kujua kuwa ni kitu gani Yule mdada anataka kumwambia, akampigia simu na kumsikiliza,
“Ushafika nyumbani?”
“Ndio nimefika”
“Erica, kuna mtu alikuwa akikufatilia ila si mtu mzuri Yule maana alikuwa akitokea na kutoweka”
Erica alishtuka na kumuuliza Yule mwanamke kuwa huyo mtu yukoje, kwa jinsi Yule mwanamke alivyomueleza moja kwa moja Erica alijua ni Yule mganga maana sifa zote za Yule mganga ndio alizoambiwa, kwakweli Erica aliogopa na hakuweza kukaa kimya zaidi akaamua kumueleza ukweli huyu dada jinsi alivyoenda na rafiki yake kwa mganga na jinsi Yule mganga alivyotaka kumpa dawa na yote yaliyomtokea usiku, Yule dada alishtuka sana na kumuuliza vizuri Erica,
“Eeeeh huyo mganga ni wa wapi?”
Ikabidi Erica aanze kumuelekeza vile alivyokwenda na rafiki yake,
“Uwiii Erica umepotea yani umepotea kabisa, bora hata ungeniomba ushauri kwanza. Huyo mganga ni mzuri sana ila ana majini makali sana, yani kama hivyo kashakupenda tayari na ili kumuepuka labda tupate mganga wa zaidi yake. Namfahamu stori zake huyo mganga, kashalala na wadada wengi waliokwenda kwake ilimradi awapende tu, yani yeye hakutongozi usoni ila atakuvutia kwa dawa na ndotoni”
“Naogopa dada, sasa nifanyeje”
“Inatakiwa twende kwa mganga zaidi yake, ila leo ngoja nikufundishe cha kufanya maana atakufata usiku utajikuta tu umelala nae hata ndotoni”
Kwakweli Erica aliogopa sana na kuanza kusikiliza maelezo anayopewa na Yule mdada, kisha alipokata simu akatoka na kumuaga mama yake kuwa anaenda dukani ila alienda kutafuta vitu alivyoambiwa na Yule mwanamke.

Kwakweli mama yake hakumuelewa kabisa na kujiuliza kuwa mwanae ana matatizo gani, maana toka amerudi kazini hakuekeweka kabisa, akajipanga kumuuliza kuwa tatizo ni nini akitoka dukani ila Erica alikawia sana kurudi mwisho wake wakati anarudi alimkuta mama yake amesinzia sebleni na mjukuu wake mikononi.
Erica aliingia chumbani akawasha dawa aliyoambiwa kisha akaenda kuoga, ile harufu ya ile dawa ndio ilimshtua mama yake usingizini na hadi akaanza kutafuta harufu inatokea wapi, wakati huo Erica alitoka kuoga na kurudi chumbani kwake ila aliona kama kuna ujumbe umeingia kwenye simu yake, akachukua na kuuangalia, akaona umetoka kwa Yule mwanamke aliyesema ni mwanamaombi ulisema,
“Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa”
Akashangaa kwanini katumia ujumbe huo na Yule mama, kisha mama yake akamgongea kwa nguvu, Erica akafungua na mama yake akaanza kufoka,
“Umewasha mavitu gani kwenye nyumba yangu?”
Erica alimuangalia tu mama yake, kisha mama yake alichukua maji na kwenda kuzima, ndipo Erica sasa akamwambia mama yake,
“Aaah mama umezima wakati nataka kujifukiza”
“Hivi wewe mtoto una akili kweli? Mambo ya kiganga haya, nieleze sasa umeanza lini kwenda kwa waganga?”
“Mama nisamehe”
“Mjinga wewe, nisamehe ndio nini? Hebu fungua madirisha huko harufu yako itoke hii, kuniletea ujinga kila kukicha kwenye nyumba yangu, hivi una nini lakini Erica jamani? Kwanini unakuwa hivyo, iko wapi elimu yako? Na usomi huo bado unaamini waganga? Wewe mtoto una matatizo gani? Fungua madirisha hayo na uje sebleni unieleze ujinga wa hizo dawa umeutoa wapi uchome kwenye nyumba yangu”
Basi Erica alifungua madirisha ya chumbani kwake na kwend akuzungumza na mama yake, alipofika sebleni alimuona mama yake amechukia sana akitamani hata kumnasa vibao Erica, ila akamuangalia tu na kumtaka aeleze ukweli wote asimfiche jambo lolote.
Ilibidi Erica amueleze kila kitu mama yake kwani akaona hata akificha hatopata faida na ile hali itazidi kumtesa, akamueleza hata jana yake kuwa ndio chanzo cha yeye kushtuka usiku wa manane maana huyo mganga alikuwa akimfatilia kwenye ndoto. Kitu pekee ambacho hakumwambia mama yake ni kuhusu kazini kwake tu, kwakweli yale maelezo mama Erica alionekana kuchukizwa sana na kuanza kusema,
“Unajua nimechukia sana ila sitaki kuongea kwa hasira maana hutonielewa, unajua mara nyingine mtu unafanya vitu ambavyo badae unakuja kujutia. Ujinga wako ungefanya uwe mke wa mganga wewe, badala uje kusema mama kuna hili na lile na lile, nisaidie maombi mama ila wewe miguu inakuwasha moja kwa moja kwa mganga haya unayachukua na kuyachukua, nakwambia utamsahau huyo Erick na yeye atakusahau kwa ujinga wako. Kijana wa watu ana moyo balaa, yani hupatikani kwenye simu sijui upokei ila anapiga na kuongea na Angel yani wewe Erica wewe usipojiangalia utakosa mwana na maji ya moto”
“Nisamehe mama, naomba unisaidie mama yangu yani sielewi”
“Sitaki kuongea sana ila tutasali pamoja na kama usiku ukiona chochote hukielewi basi uniamshe mama yako tuombe sio kesho tena miguu ikuwashe uwende kwa mganga mwingine.”
“Sirudii mama kufanya hivi”
Basi mama yake alienda nae chumbani kwake na kufanya maombi kwa muda kidogo kisha akamwambia akale ndio alale maana hata kula alikuwa hajala, basi Erica alienda kula na kurudi chumbani kwake ili alale.
Tangia jana hakuwasiliana kabisa na Erick sababu hakupata muda wa kumtafuta kutokana na muda aliofika na kulala, jana kumaliza shughuli zote alilala saa sita, na siku hiyo baada ya mambo yote alijiona saa sita ikimgongea na muda huo akataka kulala ila alipigiwa simu, kuangalia ni namba ya Yule mwanamaombi, akapokea na kuanza kuongea nae baada ya salamu,
“Erica, najikuta Napata mzigo juu yako kuwa nikuombee sana. Napata picha kuwa unapitia kwenye magumu sana”
“Kweli kabisa napitia kwenye magumu”
“Basi usiache kuomba, kilichonifanya nikupigie simu usiku huu ni kitu kimoja”
“Kitu gani hiko?”
“Kuna kitu nakiona kipo siku ya kesho, sijui ni kitu gani ila naona kipo kwako. Kama utaweza basi kesho tulia kwenu tu ukifanya ibada na usiende popote”
Basi Erica alimshukuru na kukata simu ila alijifikiria na kusema,
“Mmmmh ndio hawa hawa anaanza nakuombea nakuombea, sijui kesho usitoke kuna kitu kibaya kwako. Yeye kajuaje? Halafu kesho atanitafuta na kutaka sadaka na kusema nimekuzuia sijui nini na nini. Ngoja nilale zangu mie”
Basi akataka kujilaza ila aliamua kufanya maombi kwanza kwa muda mfupi ingawa aliomba na mama yake ila alijiona ana sababu za kufanya maombi,
“Eeeh Mungu nisaidie, mimi ni mwenye dhambi nakukosea sana nisamehe Mungu wangu. Naomba nisianguke kwenye mikono ya wote wanaonihitaji kwa mabaya, Yule mganga asinipate wala yeyote Yule asinipate, naomba nitunze kwaajili ya Erick tu. Amen”
Alimaliza maombi yake ila akajiuliza,
“Hivi maombi ndio yanatakiwa yawe hivi kweli? Lakini sijui kuomba, Mungu atanisaidia tu maana ananijua”
Muda huo aliamua kulala na alilala vizuri tu kwani hakujiwa na ndoto yoyote kama iliyomjia jana yake.
 
SEHEMU YA 307

Kulipokucha ni mama yake alimuamsha kuwa aende kazini maana mama yake hakujua chochote kinachoendelea kwenye kazi juu ya mwanae, kwa upande mwingine Erica alihisi kwamba huenda Yule bosi wake hajaelezwa ukweli na Tumaini maana kama angeelezwa ukweli basi jana yake angemkuta, ila kwavile hakumkuta alihisi ni amani tu kwake na ataendelea kufanya kazi huku kujizuia kuwa Yule mama asimjue.
Alijiandaa vizuri na kwenda kazini, alifika na kwenda ofisini kwao moja kwa moja ila hakumkuta George akashangaa kuwa siku hiyo George kachelewa au vipi ila kuna upande mwingine aliamua kwenda kwa bosi wao yani Yule mama yake Erick, alivyofika mlangoni kabla ya kugonga alitegesha sikio na kusikiliza Yule mama anaongea na nani maana alisikia kama anaongea na mtu, ndipo akagundua kuwa anaongea na George, akategesha vizuri sikio kusikiliza,
“Yani George, kumbe Yule Erica hafai hafai kabisa huwezi amini, nimemuajiri hapa kumbe nimeajiri nyoka wa kumtafuna mwanangu.”
“Kuna lipi kafanya tena”
“Yule msichana kazaa huko, halafu mtoto kamsingizia mwanangu”
“Kumbe ana mtoto Erica”
“Ndio ana mtoto, jana nilienda na Tumaini mahali kwakweli alivyonionyesha vimenisikitisha sana. Sikutegemea kama binti niliyemuona mpole, mtulivu na mcha Mungu kumbe ni shetani wa mashetani, hivi kashafika uniitie? Usimwambie lolote, nitaongea nae mwenyewe”
Erica akaona msala, aliingia kwenye ofisi yao na kuchukua mkoba wake na kutoka, alipita pale mapokezi kama kishada vile yani hakutaka hata kusimama.
Alipotoka nje ya ofisi wakati anatembea akielekea stendi, alishangaa kuna gari ilipaki pembeni yake milango ikafunguliwa na muda huo huo akaingizwa kwenye lile gari yani kilikuwa kitendo cha muda mfupi na kumfanya ashindwe hata kupiga kelele, wakati ameinua sura yake apige kelele alishangaa kumuona Mzee Jimmy ndio yupo ndani ya gari lile.


Alipotoka nje ya ofisi wakati anatembea akielekea stendi, alishangaa kuna gari ilipaki pembeni yake milango ikafunguliwa na muda huo huo akaingizwa kwenye lile gari yani kilikuwa kitendo cha muda mfupi na kumfanya ashindwe hata kupiga kelele, wakati ameinua sura yake apige kelele alishangaa kumuona Mzee Jimmy ndio yupo ndani ya gari lile.
Erica akaona hapo asipotumia akili basi atabakwa, kwahiyo aliamua kuwa mpole ili kuona kama anaweza kuiteka akili yam zee Jimmy, kwakweli hata yeye alimshangaa Erica maana mwanzoni alionyesha kama kutaka kupiga kelele ila gafla alivyomuona mzee Jimmy alitulia tuli, ilibidi mzee Jimmy amuulize,
“Mbona hujafanya purukushani sasa ili nikushushe?”
“Nifanye purukushani za nini sasa? Nitakuwa sina akili, Dora kaniambia kila kitu jinsi unavyonipenda halafu nianze purukushani kweli?”
“Aaaah kwahiyo nawe umeridhia? Mbona Dora alisema umegoma?”
“Niligoma ili nione Dora nae ana lengo gani maana Yule rafiki yangu ana tamaa sana, ila nilipofikia unataka kunioa nilifurahi sana maana hiyo ndio ndoto ya maisha yangu”
“Erica nitakuoa kweli, basi chagua eneo tukafurahi pamoja”
Erica alifikiria kisha akachagua mahali ambapo alijua ni rahisi kwa yeye kuweza kurudi kwao, kisha Yule mzee akaenda nae alipopachagua, kiukweli Erica hakutaka kufanya fujo yoyote maana hakujua huyu mzee kajipanga vipi ukizingatia, nyuma ya lile gari la mzee Jimmy kulikuwa na gari nyingine ndogo ambayo nayo ilienda pale pale kwenye hoteli ambayo Erica aliichagua na walikaa meza ya pembeni kidogo na ile aliyokaa Erica na mzee Jimmy.
Kisha Erica na mzee Jimmy wakaagiza vinywaji huku Erica akiendelea kumuhoji mzee Jimmy ili kuweka uaminifu kwake,
“Kwahiyo utanioa lini?”
“Yani mwaka huu haupiti Erica, utakuwa mke wangu. Ila nina hamu mwenzio, basi twende ukanipe”
“Sawa usijali, tunywe kidogo tupate nguvu na nikakupe kwa staili yoyote unayotaka”
Alikuwa akisema hayo huku akiwaza sana maana hakujua hata afanye kitu gani, muda kidogo akapigiwa simu alipoiangalia aliona ni Yule mwana maombi, ikabidi Erica apokee kwani aliona kama mkosi wa siku hiyo ndio umejengeka,
“Hallow Erica, sehemu uliyokuwepo si salama, ondoka upesi”
Erica akakata ile simu na kumuangalia mzee Jimmy huku sura yake ikionyesha machozi, ikabidi mzee Jimmy amuulize kuwa imekuwaje,
“Mama kanipigia simu eti mwanangu kazidiwa sana, Mungu wangu sijui nitafanyaje mimi!”
“Sasa itabidi apelekwe hospitali, basi twende wote kwenu”
“Tukienda wote mama yangu hatotuelewa kabisa, masikini mwanangu sijui nafanyaje”
“Sikia basi, twende nje pale nikuchukulie tax halafu uende nayo hadi kwenu mchukue mtoto muwaishe hospitali, halafu utanijulisha ni hospitali gani usijali kila kitu nitalipa mimi”
Basi Erica alionekana kuchanganyikiwa kabisa hadi mzee Jimmy alimuhurumia, wakatoka nje na kumchukulia gari ya kukodi ambapo akampa pesa Erica za kumlipa Yule dereva ili kama pesa aliyompa haikutosha maana kuna pesa nyingine alimpa Yule dereva wa gari ya kukodi.
Kisha Erica alipanda kwenye ile gari na dereva alianza safari ya kumpeleka kwao.
 
SEHEMU YA 308


Walivyofika Erica aliingia ndani kwa muda na kuweka mkoba wake, kisha akatoka na kusimama mlangoni akimwambia Yule dereva aondoke tu akamwambia kama mzee Jimmy atamuuliza amwambie kuwa ulikuta gari nyingine inasubiri kunipeleka hospitali, kwavile dereva alishalipwa chake kwahiyo hakuona tatizo kujiondokea tu.
Erica akarudi ndani kwao, hakutaka hata kuongea chochote na mama yake zaidi ya salamu na kwenda chumbani kwake, kakweli hakuamini kama karudi nyumbani akiwa mzima kabisa, ila kwa tukio lile kuna jambo kubwa sana alikuwa kajifunza.
Kwanza alijiuliza, Yule mzee Jimmy ilikuwaje akapita pale nje ya ofisi ya mama Erick? Na alijuaje kama yeye yupo pale? Alijiuliza na kukosa jibu ila alimshukuru Mungu tu kwa kumuokoa maana mpaka muda huo hakuamini kabisa kama alikuwa amepona toka mikononi mwa mzee Jimmy, aliamua kujilaza sasa.
Jioni ndio mama yake akaenda kumuamsha na kumfanya aamke na kwenda kuoga ili kuondoa uchovu, kisha mama yake alimuita na kuongea nae,
“Unajua Erica sijakuelewa tangu umerudi, maana umenisalimia tu ukapitiliza kulala. Tatizo ni nini maana leo umerudi mapema kutoka kazini halafu hukuwa kwenye hali ya kawaida, tatizo ni nini?”
“Ngoja nikwambie ukweli mama yangu”
“Niambie”
Akaanza kumueleza mama yake alivyokutana na Yule mwanamaombi na zile jumbe alizokuwa akimtumia na tangu jana alivyomwambia kuwa asitoke,
“Sasa mimi leo uliponiambia niende kazini nikaamua kwenda tu, sikutaka kusikia yale maswala ya usitoke wala nini maana nilihisi nae pengine ana mambo kama ya waganga wa kienyeji. Ila nilipokuwa kazini, nikatoka nje mara moja gafla nilikamatwa na mtu na kuingizwa kwenye gari, kuangalia mama alikuwa mzee Jimmy yani ilikuwa hatari leo”
“Eeeeh kwahiyo huyo mzee akakubaka?”
“Hapana mama hakunibaka”
“Ila ikawaje?”
Ikabidi amueleze ilivyokuwa hadi akaweza kuondoka mikononi mwa Yule mzee,
“Kwakweli mama leo ingekuwa habari nyingi, maana ningebakwa hivi najiona”
“Wewe mtoto una kilanga, tena una kilanga haswaa, mtu wa watu kaonyeshwa kuwa kuna baya mbele yako na kakwambia usitoke ila wewe mjuaji basi kiguu na njia Yule ukatoka. Ulishindwa nini kuniambia leo mama siendi kazini sababu ya moja mbili na tatu, ningekataa? Yani na ungebakwa ungekuwa umejitakia mwenyewe kwa kilanga chako? Mtoto hujielewi kabisa wewe, kila siku nasema wewe ni bure kabisa, sikukuzaa hivyo Erica hata huwa sielewi hiyo akili mbovu unaitoa wapi”
“Mama jamani”
“Sio mama jamani, tena nahisi huyo mzee ameathirika yani leo ungepata mimba na ukimwi juu. Mshukuru sana huyo aliyekuwa akikuombea maana ulimpa mzigo mzito wa kufanya maombi juu yako, hata hiyo akili ya kumkwepa leo mzee Jimmy ni Mungu tu kakusaidia mjinga wewe. Ulishindwa nini kunieleza jana mama yako? Unahisi ni mazuri maswala haya?”
“Hapana mama ila sijui hata ilikuwaje sikukwambia”
“Hivi na huyo mzee anataka nini kwako mwanangu? Naomba akikutafuta mwambie aje nyumbani, nataka nizungumze nae kama mzazi, hivi anakutakia nini mwanangu jamani? Ujanani ale na nani na uzee aje amfie nani? Kuna watu wengine hawajiheshimu kabisa, anatakiwa kuheshimu hisia zako kuwa humtaki sio kukulazimisha lazimisha”
“Nishamwambia simtaki mama ila namshangaa kwakweli, ila leo dah sijui ingekuwaje jamani hata sielewi”
“Sikia Erica, siku zote nakwambia ila hunielewi nazungumzia nini. Nimekwambia kuwa lisemwalo lipo na kama halipo linakuja, hayo ni maneno ya waswahili ila yana maana sana. Unapopata ujumbe wowote usiupuuzie na kusema kuwa haiwezi kutokea, haitotokea kama utasimama kweli kumuomba Mungu kuwa hilo jambo baya unalikataa lisitokee katika maisha yako. Sio kuomba hujui halafu unajifanya eti hakuna kitu wakati mtu kashakuzuia usitoke”
“Mama sikujua, nilihisi anajisemea tu”
“Hata mtu akiwa anjisemea tu unatakiwa kukemea sio kujifanya hamna kitu. Maneno yanajenga, maneno yanaumba. Mwisho wa siku unaanza kujilaumu kuwa ningejua ningejua, na kumbuka kuwa majuto ni mjukuu, wewe mtoto usinitafutie makubwa ujue, kila kitu uwe unaniambia maana nishaanza kuona kama akili zako mbovu. Umenisikia, kila kitu uwe unaniambia”
“Sawa mama nitakuwa nitakwambia”
“Mficha maradhi kifo humuumbua, na kumbuka kusali tu kwani maombi ndio silaha tosha, mambo yako ya kushawishiwa kwenda kwa mganga sitaki kuyasikia sawa”
“Sawa mama”
Erica alimuitikia mama yake na kwenda kufanya mambo mengine, kisha kumchukua mwanae na kwenda nae chumbani.
Kabla ya kulala leo alipigiwa simu na Erick, kisha akapokea na kumsalimia,
“Kweli Erica jamani mpenzi wangu, siku mbili nzima hakuna kuwasiliana kweli?”
“Nisamehe bure”
“Namba yako kila nikiitafuta siipati jamani, nimekuwa nikimtafuta bibi yake Angel tu ili niongee na Angel, ni haki kweli hiyo unayonifanyia Erica?”
“Nisamehe Erick jamani”
“Au kwavile nimesema hadi nifikirie cha kufanya kuhusu swala la ndoa mimi na wewe ndio ukaamua kunifanyia visa hivi!”
“Erick, ngoja nikwambie ukweli. Kazi ninayofanya inanibana sana kiasi kwamba nakosa muda kabisa hata sielewi labda simu inakuwa imejizima au nini ila narudi nimechoka sana”
“Kama ni hivyo basi hiyo sio kazi inayokufaa, bora ukae nyumbani tutafute kazi nyingine Erica kuliko kazi ya kukufanya hadi usahau majukumu yako. Unafikiri itakuwaje hata tukiishi pamoja yani upon a kazi tu hakuna muda wa familia unafikiri inakuwaje? Naomba tukubaliane Erica, hiyo kazi uache”
Kwavile Erica alihitaji kuacha kazi kutokana na kujua ukweli kuhusu bosi wake, kwahiyo hakuona tatizo la kusema kuwa anaacha hiyo kazi, ila tu hakutaka kumwambia ukweli Erick kama bosi ni mama yake kwani alihisi ni kumchanganya zaidi,
“Erick nimesikia, nakuahidi naacha hiyo kazi”
“Unaacha lini?”
“yani kuanzia leo ndio nimeacha hivyo, kesho sitaenda tena maana nisijenikaenda wakanilazimisha nisiache, bora nisiende tu na kisha waniachishe wenyewe moja kwa moja”
“Sawa sawa, nimefurahi kuona una masikio ya kunisikiliza mumeo ninachotaka. Tutatafuta kazi nyingine na kama nikiona kazi zinakubana sana basi nitakutafutia biashara ya kufanya kwani najua kukaa nyumbani kunabore sana, kuhusu swala la pesa nitakuagizia pale dukani ukachukue, sawa”
“Sawa, asante”
Erica alitabasamu zaidi aliposikia kuhusu swala la pesa kwani kwa yeye pesa ndio inayomfanya atafute kazi na kuhangaika na mambo mbalimbali ila akiwa na uhakika wa kupata pesa basi atajishughulisha na mambo madogo madogo tu, yani hadi anaagana nae kulala alikuwa na furaha sana.
Usiku wa manane kwenye ndoto akajiwa tena na Yule mganga, safari hii alimwambia,
“Haijalishi ni jinsi gani unanikwepa ila lazima nitakupata Erica”
Akawa kawa anamsogelea ili ambusu, Erica alianza kupiga makelele na mama yake alienda chumbani, kisha akamsimulia mama yake kuhusu aliyoyaota, ikabidi mama yake aingie kwenye maombi na baada ya hapo ndipo alilala tena hadi panakucha hakujiwa na ndoto ya Yule mganga kabisa.
 
SEHEMU YA 309


Kulipokucha Erica akaamshwa na mlio wa simu, kuangalia ni Yule mama muombaji, akapokea na kumsalimia kisha aliamua kumueleza kilichomtokea jana,
“Kwakweli simu yako ndio ilinisaidia”
“Ni Mungu ndio kakusaidia Erica, ila unatakiwa kuomba sana. Na jana usiku ni kitu gani kilikupata? Maana nilishangaa nikipata mguso wa kuomba kwaajili yako”
Basi Erica aliamua kumueleza huyu mwanamke kuhusu swala la yeye na rafiki yake kwenda kwa mganga na jinsi huyo mganga anavyomsumbua katika ndoto na jinsi anavyomuamshaga mama yake na kisha kufanya maombi.
“Erica, mshukuru Mungu sana una mama anayemjua Mungu maana kwa mapito yako ungejikuta upo sehemu mbaya sana”
“Kwakweli namshukuru Mungu kwa hili”
“Sasa ngoja tuendelee kumsihi Mungu tujue tatizo ni nini mpaka huyo mganga anaweza kuendelea kuja ndotoni, Mungu ni mwaminifu Erica na atatujulisha tu. Unajua tukijua chanzo inakuwa rahisi sana kuifunga ile namna anayopitia kuja katika ndoto zako. Nitaendelea kukuombea ila na wewe uendelee kujiombea”
“Asante, nashukuru”
Basi akakata simu na kuamua kuamka tu kama kawaida ila siku hii wala mama yake hakumuimiza tena kwenda kazini, ila ile asubuhi alimuuliza tu kuwa inakuwaje na maswala ya kazi,
“Mama nimeona Yule mzee kashapajua pale ninapofanyia kazi atanisumbua sana, nimeamua kuacha kazi tu”
“Aaah mwanangu, unaacha kazi kirahisi kama hivyo sababu ya mjinga mmoja anayekusumbua akili yako. Sikia mwanangu naomba huyo mzee akikutafuta tena mwambie aje nyumbani, nahitaji kuzungumza nae maana sio kitu kizuri huwezi fanya kazi sehemu yoyote ile maana akiijua tu unaanza kuwa na mashaka na maisha yako, nahitaji afike hapa nizungumze nae maana sijapendezewa na tabia yake kabisa. Vipi hajakutafuta?”
“Hajanitafuta mama”
“Sawa, halafu inabidi tuendelee na maombi na wewe usiache kuomba maana ni makubwa sana umeenda kutazoa kwa yule mganga”
“Sawa mama nimekuelewa”
Akaelewana na mama yake pale kisha akaendelea kufanya mambo mengine.
Kwenye mida ya mchana akiwa chumbani kwake alipigiwa simu na dada yake Mage ikabidi apokee na asikie kuwa ana kipi cha kumwambia, baada ya salamu dada yake alianza kumueleza kuhusu alipofikia kwenye swala la yeye kutembea na ndugu yake,
“Erica, tumeongea na baba wadogo nimewaeleza ukweli, wamesema inabidi tukafanye tambiko”
“Tambiko?”
“Ndio tambiko Erica, unajua ili jambo sio la kawaida yani bila tambiko hiyo laana haitofutika”
“Ila dada kwanini tusiende kwenye maombi tu”
“Wewe Erica hebu niondolee kichaa mie, wakati unaenda kulala na Derick mlikumbuka maombi? Hayo unayoyaita maombi, ulikumbuka kuyafanya wakati unaenda kulala na ndugu yako?”
“Jamani dada”
“Sio jamani dada, ujinga wa namna hiyo siwezi kuukubali hata kidogo umesikia? Tunatakiwa tukafanye tambiko, nimejitoa kwaajili ya maisha yako wewe na Erick, kumbuka sihusiki kwa lolote ila ni nyie wawili ndio mmefanya hadi inabidi tukafanye tambiko”
“Lakini dada”
“Hakuna cha lakini, mwenzio nishamwambia na amekubali, ni Jumamosi tutasafiri kwenda kufanya hilo, kwahiyo na wewe ujiandae”
“Ila dada mama amekataza mambo hayo ya waganga”
“Aliyekwambia tambiko ni mambo ya waganga nani? Inamaana kusoma kote huko hujui maswala ya tambiko? Umefanya mambo ya ajabu lazima tufanye tambiko”
“Kwanini tusifanye maombi tu badala ya tambiko?”
“Hivi wewe Erica unajua maombi wewe? Tangu lini ukajua maombi? Ungeyajua maombi ungezaa nje ya ndoa? Ungeyajua maombi ungetembea na ndugu yako? Ungeyajua maombi ungezaa na mtu unayotofautiana nae dini? Maombi huyajui wewe, hebu nitolee balaa na ukizidi kubisha nitamweleza mama kila kitu halafu uone mama atasemaje baada ya kusikia kuwa ulilala na kaka yako”
“Jamani dada usimwambie mama tafadhali”
“Basi jiandae Jumamosi tusafiri tukaivunje hii laana”
“Sasa mama nitamwaga vipi?”
“Ni siku nyingi hatujaenda kuwasalimia baba wadogo, unatakiwa umuage mama kuwa unaenda kuwasalimia baba wadogo ila mmmh hapana mama atagoma maana anaugomvi wake na wale watu. Basi mwambie mama kuwa kuna mahali unaenda na mimi, ili aniulize mimi na nitajua cha kumwambia yani wewe mwambia kuwa hufahamu chochote kuhusu sehemu unayoenda. Jiandae mapema kabisa, tukutane stendi kuu asubuhi na mapema, Jumatatu utakuwa umerudi nyumbani”
“Mtoto je?”
“Mtoto utaenda nae wapi?”
“Ila bado ananyonya dada”
“Huyo mtoto unamnyonyesha uchafu tu, sikia tutakavyoondoka ndio itakuwa njia pekee ya kumuachisha mwanao ziwa maana utakavyorudi atakuwa ashazoea”
“Dada jamani, nilitaka mwanangu afike miaka miwili kwanza ndio nimuachishe”
“Kwani miaka miwili ndio nini?”
“Kliniki wanashauri kuwa ni vizuri kwani mtoto anakuwa na afya”
“Achana na habari za kliniki, mtoto akitembea tu anaachishwa ziwa sembuse huyo Angel anayemaliza maneno. Haya sisemi lingine tena ila jiandae tu Jumamosi kwaajili ya hiyo safari”
“Sawa dada”
Kisha dada yake akakata simu, kwakweli hakuwa na namna ya kufanya zaidi ya kukubali tu kwani hakuwa na namna zaidi ingawa kila akifikiria kuwa baada ya hapo itakuwa mwisho kumnyonyesha mwanae aliumia zaidi maana alipenda aendelee kumnyonyesha mpaka afunge miaka miwili.
Alitoka chumbani na kwenda sebleni ambako alikuwepo mama yake ila kumwambia chochote hakuweza, wakati akiongea nae mengine simu yake iliita na alipoiangalia ilikuwa ni namba ya mzee Jimmy, akasita kidogo na mama yake akamuuliza,
“Mbona unasita wakati simu inaita?”
“Ni mzee Jimmy mama”
“Sikia, pokea na umwambie kuwa aje nyumbani nahitaji kuonana nae, yani mwambie lolote ila aje hapa nionane nae haiwezekani animalizie furaha ya mwanangu kiasi hiki”
Basi Erica alipokea ile simu na kuongea nayo ambapo akamwambia kuhusu swala la kufika nyumbani kwao kwanza kwani mama yake anataka kumuona,
“Aaah mama mkwe anataka kuonana nami?”
“Ndio”
“Anataka tusemezane kitu gani?”
“Sijui, ila anataka kuonana nawe”
“Basi mwambie nitakuja kesho jioni”
“Sawa nitamwambia”
Basi alivyokata simu akampa huo ujumbe mama yake, na kumuuliza,
“Sasa mama, utaongea nae nini?”
“Erica, mimi ni mzazi na ninaumia sana tofauti na wewe unavyodhani. Nahitaji kuongea nae kwani najua kuwa hata yeye ni mzazi, hapa ni nyumbani kwangu nimemuita hapa kwa makusudi kabisa na akili zangu zinachemka”
“Sasa mama kama akifanya kitendo kibaya hapa nyumbani?”
“Hapa ni nyumbani na hata hivyo naamini Mungu atatusimamia katika hili, nahitaji kuongea nae ukweli sio kukukosesha raha na furaha kiasi hiko, kwanini akufanyie hivyo? Mapenzi huwa hayalazimishwi”
“Sawa mama nashukuru kwa upendo wako maana nilishachanganyikiwa juu ya hili swala”
Wakajadiliana pale kuhusu mambo mbalimbali ila hakuthubutu kugusia kuhusu swala la yeye na dada yake kwenda kufanya tambiko kwani alijua akimwambia tu mama yake basi habari yake kuwa alilala na Derick itajulikana na yeye hakutaka ijulikane.
 
SEHEMU YA 310

Usiku ulipofika kama kawaida hakutaka tena kupoteza muda bila kuwasiliana na Erick, aliongea nae na kumpa mtoto aongee nae kisha yeye kuendelea kuongea nae ambapo Erick alimuuliza,
“Kwahiyo leo hukwenda kazini kama tulivyokubaliana jana usiku si eti eeh!”
“Ndio, sikwenda si nilikwambia naacha kwahiyo nimeacha”
“Sawa, sasa unapenda kufanya kazi gani nyingine?”
“Kazi yoyote tu”
“Sawa, kuna mtu nimeongea nae kuhusu maswala ya kazi nadhani atakutafuta Jumamosi ili uongee nae vizuri, najua atakaa na wewe vizuri kazini maana nishamwambia kuwa asikupe kazi za kukuchosha mwili wala akili yako”
“Sawa Erick, nashukuru sana”
“Unajua Erica wewe ndio mke wangu, mimi nakupenda sana wewe yani wewe si sehemu tu ya maisha yangu bali wewe ni maisha yangu”
Kwakweli Erica alikuwa akijihisi rah asana kila alipoongea na Erick kwani Erick alikuwa na maneno matamu sana ya kumvutia, kisha akaagana nae na kulala.
Kama kawaida ya kipindi hiko, alijiwa na Yule mganga kwenye ndoto na akaanza kumwambia,
“Erica, siwezi kukuacha na nitaanza na huyo unayehisi unampenda sana. Kesho usiku ukithubutu tu kuongea nae kwenye simu nammaliza”
Erica akashtuka na kupiga kelele tena, ambapo mama yake alitoka na Erica alimsimulia mama yake alichokiota,
“Mmmmh Napata mashaka sana, unajua tunafanya maombi ya kumtuliza huyo mtu maana baada ya maombi haji tena kwenye ndoto zako ila inabidi tufanye maombi ya kumuondoa kabisa yani asikuone. Kuna kipi chake unacho?”
“Sina chochote chake mama”
“Lazima kipo, haiwezekani akufatilie kiasi hiki Erica, ngoja tuingie kwenye maombi”
Basi mama yake aliomba sana kuhusu swala lile kisha alimwambia mwanae,
“Erica, haya ni mapambano makubwa umeenda kuzoa mambo mwanangu. Habari za waganga nilishakukataza mwanangu, ona sasa. Itabidi nishirikishe na watu wengine wa maombi wanisaidie swala hili maana anachosema huyo mtu unaweza ukahisi ni ndoto ila ndio hali halisi, na wewe unatakiwa ujue kujiombea Erica”
“Sawa mama”
Kisha Erica akalala tena, muda huu alilala vizuri tu hadi panakucha.

Ila alikuwa na mawazo sana kwa siku hii yani hakuwa na raha kabisa kila akikumbuka maneno ya Yule mganga kuwa asithubutu kuongea na simu usiku, yani hakuwa na raha kabisa, aliwaza kwanini Fetty alimpeleka kwa mganga kama Yule? Kwakweli ile siku hakuwa na raha.
Ilikuwa inakaribia jioni, sikmu yake ikaita akaangalia mpigaji akaona ni Fetty, akapokea na kuanza kumueleza kuhusu yale yote anayoyaona kwenye ndoto kuhusu Yule mganga,
“Pole rafiki yangu, mimi pia sikujua tabia ya Yule mganga, ndio nimeambiwa na watu nikaamua nikupigie simu rafiki yangu kama umepona. Nasikia Yule mganga kashalala na wateja wake wengi sana kwa kutumia madawa, kwakweli niliposikia imeniuma nikasema ngoja nikuulize rafiki yangu maana nakumbuka siku ile wakati umetoka haraka kwa mganga uliangusha leso, sasa watu wanasema Yule mganga akipata kitu chako kimoja basin i rahisi sana kukuteka. Nimekumbuka hilo nikaamua kukupigia simu”
“Mmmh sasa tutafanyeje maana ananitishia kwenye ndoto”
“Sikia cha kufanya, kuna mganga mwingine nimeambiwa nasikia wengi waliotendwa na Yule mganga wanaenda kwa huyo mwingine, ni kiboko yeye ana nguvu zaidi”
“Hapana Fetty, sitaki tena kwenda kwa mganga”
“Erica, uliangusha leso unadhani kama aliichukua utapona kweli? Ataendelea kukufatilia kila siku, ujue”
“Ngoja nikamwambie mama, ila swala la kwenda tena kwa mganga hapana aisee”
Erica akakata simu na kwenda kufungua mkoba wake ili kuhakikisha kama kweli aliangusha leso, alifungua mkoba wake na kukuta leso yake ipo, akajiuliza kuwa kama kaangusha leso mbona bado ipo kwenye mkoba? Akaichukua kuiangalia vizuri, akashtuka sana kwani leso ile ilikuwa kipande, yani hapo ndio akapata maswali zaidi kuwa kipande kilichobaki kikuwapi?
Akawa anatoka ili akamueleze mama yake, alivyofika sebleni tu alisikia mtu akigonga, na mama yake aliinuka kwenda kumfungulia kwahiyo yeye alisimama pembeni kuangalia kuwa ni nani, mama yake alivyofungua alishangaa kumuona mzee Jimmy ila hakushangaa zaidi kwavile alimwambia jana kwamba anaitwa na mama yake, ila kilichomshangaza ni kuwa mama yake alinyanyua mkono na kumnasa kibao mzee Jimmy kamavile ni mtu anayemfahamu.
 
SEHEMU YA 311

Akawa anatoka ili akamueleze mama yake, alivyofika sebleni tu alisikia mtu akigonga, na mama yake aliinuka kwenda kumfungulia kwahiyo yeye alisimama pembeni kuangalia kuwa ni nani, mama yake alivyofungua alishangaa kumuona mzee Jimmy ila hakushangaa zaidi kwavile alimwambia jana kwamba anaitwa na mama yake, ila kilichomshangaza ni kuwa mama yake alinyanyua mkono na kumnasa kibao mzee Jimmy kamavile ni mtu anayemfahamu.
Kisha mama Erica aliwaka na kusema,
“Haya kilichokuleta kwangu ni nini wewe firauni mkubwa? Unataka nini nyumbani kwangu, shetani kama wewe?”
Erica akasogea kwa mama yake na kumwambia mama yake kuwa Yule ndiye mzee Jimmy ila mama yake ndio alizidi kuongea,
“Kheee kumbe ndiomana umekazana kutaka watoto maana watu wazima wote ushamaliza, hivi wewe mwanaume unataka nini kwa walimwengu wewe? Unadhani nasahau ujinga uliotaka kunifanyia, nikiwa na mtoto mdogo huyu huyu ambaye leo unamtaka, shetani mkubwa wewe. Tena umkome mwanangu, ondoka hapa shetani wewe, sikujua jina lako kumbe unaitwa Jimmy, ondoka kwangu upesi shetani wewe na mwanangu umkome, ukiendelea nasema mambo yako yote unayofanyiaga watu, tamaa tu. Hivi watu wazima wameisha? Utaacha lini umalaya wewe? Si ufate watu wazima wenzio, mwanangu mkome mzee wewe, na uondoke kwangu sitaki hata kuongea nawe”
Mzee Jimmy hakusema neno zaidi kwani alionyesha kushikwa na aibu sana kwahiyo alitoka moja kwa moja hadi nje ya geti na kupanda gari lake na kuondoka zake, ila mama Erica aliendelea kuongea hadi Yule mzee alipokuwa ametoka nje bado mama Erica alikuwa akiongea,
“Huna akili hata kidogo wewe mzee, yani maisha yako uhangaike huko balaa halafu uje kuhangaisha na watoto wetu tena, muone vile. Muache mwanangu kama alivyo”
Kisha Yule mama aliingia tena sebleni na kufunga mlango huku akiongea kwa hasira sana na kulaani vikali kitendo cha Yule mzee kuonekana mahali pale.
Ikabidi Erica asogee kwa mama yake na kumuuliza kwa makini kuwa vipi anafahamiana na huyo mzee,
“Mama, kumbe unafahamiana na Mzee Jimmy? Umemfahamu vipi?”
“Yule mzee ni mbwa tena mbwa koko, yani mzee yule hafai ni malaya hatari, kumbe bado anaendelea na tabia yake loh! Unajua sikumjua kuwa ni yeye ulipokuwa unasema mzee Jimmy mzee Jimmy wala sikuwa na wazo kuwa ni yeye maana sikumjua jina lake ila tulimuita kiwembe tu kipindi hiko maana anakata huku na huku”
“Eeeeh mama”
“Yani mzee huyu ni malaya tena malaya koko yani hafai kabisa, ngoja nikueleze nilivyomfahamu huyu mbwa huyu, si uniona mama yako huwa natembea kama nachechemea eeh!”
“Ndio mama”
“Basi chanzo ni huyu mbwa”
“Kheee kumbe! Ilikuwaje?”
“Kipindi cha nyuma kama unavyonijua mama yako napenda kujishughulisha basi ndio hivyo tulikuwa na chama chetu tunakopa huko benki halafu msimamizi alikuwa huyu mzee, jina la kiwembe lilianza pale ambapo alitembea na dada mtu na mdogo mtu ndio watu wakamuita kiwembe kuwa anakata kata tu, sasa kumbe ukitaka mkopo haraka lazima ulale nae ndio upate yani hiyo ndio ilikuwa tabia yako. Sikutaka hata kukutana nae yani nilikuwa namuona ona tu hata sikutaka mazoea nae, kipindi hiko wewe mdogo nakubeba mgongoni, siku hiyo zamu yangu ya kupata mkopo ilifika nimeenda akaanza kuniletea habari zake kuwa lazima nilale nae ndio anipe mkopo, nikamwambia ila mimi nimefata taratibu zinavyosema wala sitaki kwa njia za panya ndiomana sijaharakisha kupata, ila akasisitiza kuwa lazima nilale nae ndio nipewe mkopo nikamgomea kwakweli. Sasa siku hiyo akaniambia kuwa niende ofisini kwake nikasaini makaratasi ya mkopo, basi nikajibeba na mwanangu hadi ofisini kwa bahati nzuri mwanangu nilikuwa nimekubeba kwa mbele maana ingekuwa mgongoni basi saivi nadhani usingekuwepo kwenye macho yangu, nikaingia mule ofisini ili nisaini namsikia mshushe mtoto nikagoma, akasema leo lazima ulale na mimi ndio usaini hizi karatasi, nikagoma kuwa kama ndio hivyo basi, weee Yule mbaba hakukubali akaanza kunilazimisha kuwa nishushe mtoto, nikawa nimegoma tukaanza kupambana yani alinisukuma vibaya nikaanguka chini kwa mgongo hivi dah nilihisi viungo vyangu vimekatika, namshukuru Mungu ulikuwa mbele kwahiyo nilianguka ila nilichokumbuka ni kukushikilia mwanangu bila kujali maumivu ninayopata pale chini, baba asiye na huruma Yule akaainama na kutaka kuanza kunivua nguo, nikapiga kelele ila wapi kelele zangu hazikugonga mwamba, ila ikawa bahati tu kwani muda ule ule kuna watu walikuja na kugonga kwenye ofisi yake, ndipo aliponiachia na kuruhusu wale watu waingie huku akijifanya kuwa ananipa huduma ya kwanza eti nilianguka, yani sina hamu nae, nilitoka nachechemea na kurudi kwangu kumbe kulikuwa na maumivu ya ndani kwa ndani juu yangu, kumbuka hatukuwa vizuri kipesa kipindi hiko. Nilitaka nikafungue kesi kuhusu huyu kiwembe ila watu wakanishauri kuwa itanishinda maana huyu pesa anayo na mimi sina hela kwahiyo kesi itanishinda tu, nilikuja kwenda hospitali wakati tatizo limeshakuwa kubwa na mpka leo nachechemea mwanangu sababu yake. Toka hapo nikaona kuwa sisi wanyonge hatuna mtetezi maana kama nikifungua kesi basi mwenye pesa atanishinda, mtetezi pekee wa wanyonge ni Mungu tu, ndipo nilipoamua kuokoka ili niwe nashtaki kwa Mungu”
Erica alikuwa akilengwa lengwa na machozi kwa maelezo hayo ya mama yake, na akaona kweli ana haki ya kumzaba kibao mzee Jimmy, kwa stahili hiyo hafai kabisa, alimuhurumia mama yake kwani ni kweli alikuwaga akichechemea kwenye kutembea, siku zote hakujua chanzo cha mama yake kuchechemea kumbe ilikuwa ni yeye mwenyewe,
“Pole mama, Mungu atakusaidia mama yangu”
“Mungu ameshanisaidia mwanangu na anaendelea kunisaidia, si jambo jema kuona Yule Yule mtu aliyetaka kunibaka mimi ndio atake kumbaka na mwanangu kweli?? Mara nyingine huwa nahisi yeye alitia kama mkosi kwako mwanangu hata unapata maswahibu mbalimbali katika maisha yako, yani namchukia Yule halafu leo nimuone nimchekee, weee haipo hiyo kwakweli”
Erica alizidi kumpa pole mama yake kwani aliweza kujua kwa undani zaidi ubaya wa mzee Jimmy na kumfanya hata asishangae kuona katembea na Dora nab ado anahitaji kutembea na yeye, kwakweli alikuwa akishangaa sana huku akiendelea kuongea mambo mbalimbali na mama yake.
 
Back
Top Bottom