Simulizi: Nyuma ya mlango wa adui

Simulizi: Nyuma ya mlango wa adui

NYUMA YA MLANGO WA ADUI
SEHEMU YA SITINI NA NANE
MTUNZI : Mbogo EDGAR
WHATSAPP : 0743632247 (KWAMATUMIZI YA OFISI TU)
TULIPOISHIA SEHEMU YA SITINI SABA: Kwa kuweka kumbu kumbu sawa nikwamba, koplo Cheleji pekee ndie aliemuona Deus akiingia kwenye gari, hivyo ndie mwenye kuweza kuitambua sura ya kijana huyo, japo haku fahamu wala kujuwa kuwa kijana yule aliemuona pale kiluvya madukani, akiingia kwenye gari lile BMW jeusi ndie askari aliekuwa anazungumziwa Mitandaoni…..…….ENDELEA……


*******
Naam!!! mambo yalikuwa mengi sana jioni ile, tayari mkuu wa majeshi alishaulizia mara kadhaa, kama askari Deus ameshapatikana ili aweze kuwahakikishia vingozi wa ngazi za juu kama askari huyo alieachishwa jeshi, atarudishwa jeshini na kubadilishiwa adhabu na kuendelea na kazi.


Lakini jibu lilikuwa ni hapana, hakika ili wachanganya viongozi hao wa jeshi la ulinzi, huku kila mmoja akihangaika kwa nafasi yake kusaka mawasiliano ya kijana huyo, ikifikia hatua ya kuwaza kuwa pengine askari huyo amepata taarifa ya kutafutwa kwake na kuamua kuzima simu, pengine hajuwi dhumuni la kumtafuta.


Mpaka giza linaingia, bado Deus Nyati alikuwa hajapatikana, “afande ninawazo, ikiwezekana tuwasiliane na brigedi ya kusini, watoe mtu mmoja aende nyumbani kwa baba yake Deus, nadhani anaweza kupata dondoo ambazo zitafanikisha kumpata huyu askari, sidhani kama anaweza kukaa masaa ishirini na nne bila kuwasiliana na familia yake” alishauri major yule msaidizi wa major general Mbike, “wazo zuri hebu wasiliana na mkuu wa mafunzo wa brigedi ya kusini haraka, mueleze afanye hivyo” alisisitiza general Mbike Kifimbo.********


Deus mida hii ya saa moja na robo, alikuwa anawasha taa za kuashiria au taa elekezi ya upande wa kushoto, kuiacha barabara ya kuelekea moshi na kuifuata ya kuelekea Rombo, hakuna mtu aliewajari, maana walikuwa katika mwendo wa katika mwendo wa kawaida sana, lakini baada ya kutembea mita chache mbele, wakati wanaivuka shule ya sekondari Shauri Tanga, kijana wetu akakanyaga mafuta na mshale ukaanza kutafuta namba yake, muda wote safari ilikuwa kimya, Sheba akimtazama Deus kwa jicho la kutamani kumuongelesha.


“Ni vyema ungekunywa hata soda Deus, hujatia chochote tumboni toka tumeondoka dar” alisema Sheba, huku anatoa soda moja kwenye mfuko na kumpatia Deus, “siyo muhimu kama kukufikisha na mimi niangalie namna ya kugeuka” alisema Deus, “kwa sauti ambayo licha ya kuwa katika utulivu kama ilivyo kawaida yake, lakini ilionyesha wazi ni jinsi gani amechukia kwa tukio la Mombo, “lakini hatukuwa na namna, wange tuuwa wale” alisema Sheba kwa namna ya kujitetea, “lakini sipendi bunduki sheba” alisema Deus kwa sauti kali kidogo, “lakini haipo katika sheria zako, ulichokumbuka ni kufunga mkanda tu” alisema Sheba na yeye kwa kupaza sauti, “sawa ni vyema kama utafunga mdomo wako na kutulia” alisema Deus, ambae alikuwa anapunguza mwendo kuingia kwenye barabara ya vumbi ni kweli Sheba alitulia kimya, macho ameyaelekeza mbele.********


Naam Arusha mjini, lilionekana gari aina ya Subaru Impreza rangi, likikatiza mitaa ya mianzini, na kufika njia panda ya fire iendayo kwa murombo na gari hilo likiwa katika mwendo wa kawaida tofauti na masaa kadhaa yaliyopita, lilipo onekana likikimbia kwa speed kule merelani, liliingia upande wa kushoto na kuelekea moja kwa moja kufuata barabara ya mjini na kwenda kusimama nje ya jengo la Mrina Hotel.


Mlango wa nyuma wa gari ulifunguliwa akashuka mwanaume mmoja mwenye mkadilio wa umri wa miaka arobaini, ambae alitoa noti kumi za elfu kumi kumi na kumpatia dereva wa gari lile, kisha akachukuwa sanduku dogo jeusi, na kuanza kutembea kuelekea ndani ya hotel, akimuacha kijana yule anahesabu fedha alizopewa.


Lakini sasa kitu ambacho kilihitaji umakini wa hali ya juu sana, nikwamba dereva huyu licha ya kuhesabu fedha zake, ambazo hazikuhitajia hata dakika mbili kumaliza kuhesabu, yeye alikuwa anakata jicho la wizi kumtazama mzee huyu, mwenye kuvalia suruali nyeusi ya kitambaa, shati la blue lenye maua ya njano mpauko, aliekuwa anamalizikia kuingia ndani ya jengo hili lililochangamka.


Ile mzee wa watu anapotea tu, hapo hapo yule dereva akatoa simu yake na kubofya kwa haraka, akapiga namba fulani ya simu iliyohifadhiwa kwa jina la Mduma, simu ambayo haikutumia hata sekunde mbili kuita, ikapokelekewa mara moja, “niambie chalii, huyo dingii amemuacha wapi?” ilisikika sauti yenye rafudhi ya watu toka Arusha, kama ilivyo ongewa na mtu toka upande wa pili wa simu, “yupo sehemu mwake kinyama, yaani alivyo fala, nimemjaza akalale mlina na yeye amekubali” alisema yule dereva kwa sauti yenye rafudhi ya watu wa Arusha, kama mwenzie, “haina noma Chalii, ataisoma namba si yupo na mzigo hapo Mlina?” aliuliza upande wapili wa simu, “mazaga yote anayo kaka, fanya faster wachukuwe wana mtimbe hapa eneo, mchukuwe mizigo” alisema yule kijana huku anaweka fedha yake mfukoni na kuondoa gari, “usijari tena ngoja ni mpigie Chao amcheki huyo boya ajuwe anaingia chumba gani” alisema Mduma na kukata simu.*******


Naaam!!! saa moja kamili, kwa saa za mashariki mwa Afrika, ikiwa ni saa kumi na mbili kamili kwa masaa ya Rwanda, Burundi, na Congo, na saa kumi na moja kamili kwa masaa ya kusini kabisa mwa Africa, gari la polisi lenye kikudi kinacho ongozwa na Koplo Ochu, lilikuwa linakatiza maeneo ya Mombo kwa speed kali sana, speed ile ile ya mia moja arobaini kilomita kwa lisaa limoja.


Lakini walipoiacha Mombo na kutembea kilomita kama tatu hivi, wakashangaa kuona vikundi vidogo vidogo vya watu, pamoja na pikipiki, zilitembea kulekea kule wanakoelekea na kila walipozidi kusogea ndivyo walivyozidi kuona watu wanaongezeka, yaani watembea kwa miguu na pikipiki pia, hata waliposogea zaidi wakaanza kuona foleni ya magari, yaliyojazana barabarani, huku mbele zaidi kukionekana moto mkubwa sana, uliokuwa unaendelea kuwaka.


“Kuna nini tena, huu ndio ujinga wa waswahili, wanataka kucheleweshana tu” alisema Koplo Ochu, huku anashuka na kuanza kutumia upolisi wake kuosogeza magari, ili la kwao lipite na alifanikiwa kwa kiasi kikubwa, maana gari lao lilisogea mpaka kufikia karibu kabisa na makutano ya foleni ya kutoka moshi, ambapo palionekana kuna gari linawaka moto, huku askari wa jeshi la polisi wanne wakisaidia na raia kuuzima mto huo, “imekuwaje hii ajali” aliuliza Othman kwa mshangao, “baada ya kusaidia kuzima moto unauliza imekuwaje?” aling’aka polisi mwenye cheo cha Constable, pasipo kugeuza uso wake kumtazama alieuliza, “koplo Othman hapa, nipo safarini naelekea CCP na gari letu hilo hapo, unaweza kujibu swali langu Constable?” alijitambulisha kibabe koplo Ochu, na hapo yule askari akageuza uso wake, kumtazama muulizaji.


Niwazi hata baada ya kumtazama hakumuamini kama ni polisi, kutokana na uvaaji wake, hivyo akatazama kule ambako mwanga wagari ulikuwa unaonekana, ni kweli akaliona gari la polisi, “ni wenzetu hawa inaonyesha wameshambuliwa, jioni hii zilisikika risasi upande huu, wakati tuna jiuliza nini kinaendelea mara ukasikika mlipuko mkubwa na moto ukaonekana, na hivyo kuja mara moja, na kukuta polisi wenzetu wapo hapa chini wamepigwa risasi hakuna hata mmoja mzima na gari linaungua moto, huku mmoja akiwa ndani, mmoja kati ya walio uwawa ni OC CID, miili yao imekimbizwa hospital Tanga mjini” alieleza yule polisi kwa sauti ya masikitiko na simanzi kubwa.


Hapo moja kwa moja koplo Ochu, akahisi jambo, “poleni sana, wacha sisi tuwahi CCP, maana tunatakiwa kureport pale saa kabla ya saa mbili” alisema Ochu huku anarudi ndani ya gari na kumuamuru dereva aondoe gari nao wakapita, huku yule askari anawaongoza, mpaka walipovuka moto na kuendelea na safari yao.


Ina maana huyo mtu ni hatari kiasi hicho, anawezaje kufanya tukio kama ili, kwa muda mfupi kama huu” aliwaza koplo Othman, huku koplo Ochu akitoa simu yake na kupiga kwa Ulenje kumpatia taarifa ile, ili aweze kuthibitisha kama ndio hao aliowaagiza au kuna wengine.******


Yap! saa moja na nusu ya usiku, kaskazini mwa Tanzania mkoa wa Kilimanjaro, pembezoni mwa mpaka wa Tanzania na Kenya, kilomita mbili toka kijiji cha Longai ni kilomita zaidi ya ishirini toka tarakea, baridi ilikuwa inapuliza vyema kabisa, giza lilikuwa limetanda ni vigumu kuona umbali wa mita hamsini, kutokana na giza hilo, kwenye barabara ndogo na nyembemba, lilionekana gari aina ya BMW S 7 jeusi, likiwa linatembea taratibu, likikatiza kwenye eneo hilo, lililozungukwa na miti mirefu ya kupandwa maarufu kama mikaratusi, ni wazi walikuwa wanatarajia kumuona mtu au watu katika maeneo hayo.


Naam wakiwa wanaendelea kusonga mbele kwa mwendo wa kilomita tano kwa saa, mara ghafla wakamuona mtu anatokea pembeni ya barabara, yani kichakani akiwa na bunduki aina AK 47, mkononi mwake na kusimama katikati ya barabara, “khaaaaa! bunduki tena” alisema Deus kwa sauti ya kukwazika huku anakanyaga brake kusimamisha gari na hapo hapo wakaibuka watu wengine wawili mmoja kati yao akiwa ni mwanamke, “hao ni watu wangu” alisema Sheba huku anamtazama Deus, na uso wake umepambwa kwa tabasamu laini, “ok! malipo yangu yaliyobakia” alisema Deus, huku anamtazama Sheba, ambae pia alikuwa anatabasamu, “una uhakika kuwa unahitaji fedha pekee? au kuna kitu zaidi unakihitaji kwa mschana mrembo kama mimi?” aliuliza Sheba, kwa sauti laini na tulivu, “huu sio wakati wa utani, mpaka sasa sijajua narudi vipi mpaka tarakea kilomita ishirini kwa mguu begi la kilo hamsini mgongoni…” alisema Deus na kabla hajamaliza kuongea, akakatishwa na mlio wa simu ya kwenye dash board ya gari, wote wawili wakatazama kwenye kioo cha screen, yenye upana wa sentimeta thelathini kwa kumi na tano..…….ENDELEA kufuatilia mkasa huu wa NYUMA YA MLANGO WA ADUI unao kujia hapa hapa jamii forums
Tukutane baadae tuone je deus katunukiwa na sheba au inakuwaje kuwaje happ wazee 😅😅
 
NYUMA YA MLANGO WA ADUI
SEHEMU YA SITINI NA SABA
MTUNZI : Mbogo EDGAR
WHATSAPP : 0743632247 (KWAMATUMIZI YA OFISI TU)
TULIPOISHIA SEHEMU YA SITINI SITA: Lakini ile wanakaa sawa tu, ghafla mita kama mia moja mbele yao, wakaliona gari la polisi, likiwa kati kati ya barabara limesimama kwa mtindo wa kukatiza barabara, yani kizuwizi huku polisi sita wakiwa wamesimama pembeni ya gari lile na bunduki mikononi mwao zikielekea kule waliko kuwa wanatokea wao, huku mmoja wao akiwa amesimama katika kati ya gari, yani ubavuni mwa gari amenyoosha mkono mmoja juu, ikiwa ni ishara ya kusimamisha gari lao, “washenzi wametupata” alisema Deus, huku anaanza kupunguza mwendo kwa nguvu kwaajili ya kusimama……….ENDELEA….


Wote wawili walitulia kimya, wakishuhudia gari likiendelea kusotesha tairi kwenye lami kwaajili ya kusimama, hata liliposimama, Deus alikuwa amefanya juhudi ya hali ya juu sana kulisimamisha gari lile pasipo kusababisha ajari.


Hapo Deus aliekuwa anawaza namna ya kumuokoa yule mschana, ili amfikishe sehemu aliyokusudiwa na yeye kupata malipo yake maana hakujua habari ya dhahabu ambayo msomaji unaifahamu, aliwatazama wale polisi ambao walikuwa wanalizunguka gari na bunduki zao mikononi, mitutu wameilekezea kwenye gari, “hivi uliwafanya nini hawa washenzi?” aliuliza Deus, kwa sauti ya upole kama vile hakuna kitu cha hatari mbele yao, “Deus, acha kuuliza maswali na ikiwezekana ufanye jambo tuondoke mahali hapa” alisema Sheba, huku anapeleka mkono chini ya seat yake.
Kabla Deus ajajibu kitu, tayari polisi mmoja alisha ufikia mlango wa dereva na kujaribu kufungua kitasa, lakini mlango haukufunguka, maana ulikuwa umefungwa kwa ndani, yule polisi akainua bunduki yake, akinyoosha usawa wa kioo cha mlango wa dereva, Deus akiwa anamtazama kwa umakini mkubwa, akamtazama mdomo wake ambao ulikuwa unatamka maneno ambayo yeye Deus, hakuyasikia, lakini niwazi alikuwa “anasema fungua mlango” hapo Deus, akafungua mkanda wa kiti na kutoa lock za milango, kisha akafungua mlango, ile anatokeza tu! akashikwa ukosi wa tisheti lake na kuvutwa nje, ukweli kutokana na uwezo alionao katika mazoezi, hakuyumba sana.


Lakini ile anakaa sawa, tayari Sheba alikuwa amesha toka ndani ya gari, sabamba na milipuko mfululizo ya risasi za bastora, kutahamaki tayari Sheba alikuwa amesha washusha askari wa nne, na kubakia wawili walio simama mmoja akiwa bila silaha yoyote na mwingine akiwa na SMG, karibu kabisa na Deus, lakini ile anainua tu, Deus akamuwahi haraka na kumpiga ngumi nzito ya kisogo, ambayo ilimpeleka chini kama mzigo na kumzimisha kabisa, huku yule mwingine akikimbilia kwenye gari, ambalo dereva alikuwa ndani yake, anajaribu kuwasha ili wakimbie, lakini kama vile amepungukiwa na akili, sheba akamimina risasi tatu, ambazo moja ilipiga kwenye bega la yule aliekuwa anakimbilia gari, huku moja ilipiga kwenye kioo cha gari, na kwenda kuchimba kwenye ubavu wa dereva, ambae tayari alikuwa amesha liwasha gari na kuingiza gia namba moja, ambapo kwa msukumo ule wa risasi, akajikuta akanakanyaga mafuta hovyo na kusonga mbele kwa fujo likiingia mtaroni na kushindwa kuendelea na safari, huku dereva aliekuwa anaugulia maumivu akiwa anajitaidi kujitoa kwenye gari.


“sipendi bunduki, hivi nani kakuambia utumie silaha muda huu?” aliuliza Deus, kwa sauti ambayo licha ya utulivu na utaratibu wake, lakini bado ilionyesha kuchukizwa na kitendo kile, “yaani watu saba, hii ni hatari sana tutalazimika kuwakimbia zaidi” alisema Deus akimtazama Sheba, ambae alikuwa anaichomeka bunduki yake kiunoni kwenye pindo ya suruali yake usawa wa kati ya makalio, “kwahiyo unadhani wangekuacha hawa, lazima wangetuuwa kisha kuondoka na gari letu” alijibu Sheba, huku anainama na kuokota mja kati ya SMG zilizoangushwa na wale polisi waliouwawa, “mh! kwanini watuuwe, nani kakuambia watatuuwa?, hebu ingia kwenye gari tuondoke hapa, kabla hatujakutwa” alisema Deus, huku anaingia kwenye gari.


Lakini sasa kabla hajafungu mlango akasikia mlipuko wa kwanza wa risasi, ile kutazama mbele yule jamaa aliekuwa anakimbia bila bunduki alikuwa hewani anaenda chini kama mzigo, huku damu nyungi sana zina vuja kichwani, ni wazi ilikuwa risasi iliyompata ilipiga kichwani, “we mwanamke acha upuuzi, huo ni sawa na ujambazi” alisema Deus, huku anashuka toka kwenye gari, macho yake yapo kwa Sheba, ambae alikuwa anaelekeza silaha kwenye gari la polisi, ambako yule dereva polisi, alikuwa anahangaika kushuka huku anaugulia risasi ya tumbo.


Fumba na kumbua, tayari risasi ilikuwa imesha toka kwenye mtutu wa SMG na kugonga kwenye kioo cha nyuma na kufanya kitawanyike, huku zikifuatia risasi nyingine tano mfurulizo, zilizo ambatana na milipuko yenye kelele mfano wa kiwanja cha majaribio ya shabaha, huku gari likiwa ndio ubao wa shabaha, risasi zilichakaza mwili wa yule askari, “sheba, unaniweka katika wakati mgumu, unadhani nitaishi vipi ndani ya nchi niliyo shiriki mauwaji ya wanausalama wake” alifoka Deus, huku anapokonya silaha toka kwa Sheba, “mbona mgumu kuelewa Deus, unadhani ni wanausalama hawa, hawa ni wanyang’anyi tu, wapo hapa kutuibia” alisema Sheba, huku anageuka na kurudi kwenye gari.


Wakati huo huo, yule askari alie pigwa ngumi ya kisogo, ndio alikuwa anazinduka, akanyoosha mkono taratibu kuchukuwa SMG, yake ili awatandike wakina Deus, lakini kwa bahati mbaya au nzuri Sheba akamuona, hapo haraka akachomoa bastora yake toka kiunoni na kumtandika yule jamaa, “pumbavu, ingia kwenye gari haraka” alisema Deus, huku anatupa ile SMG na kuanza kutembea kuelekea kwenye gari, “nakushauri uchome gari moto, ili kupoteza ushaidi” alisema Sheba, ambae sasa alikuwa anaingia ndani ya gari,


Hapo Deus akageuka kulitazama gari la polisi, halafu akamtazama Sheba, ambae pia alikuwa anamtazama, kisha akaanza kuziokota silaha zilizo kuwa zimezagaa pale chini na kuanza kuitupia ndani ya gari akibakiza moja tu.


Alipomaliza akarudi mita chache nyuma, toka lilipo gari la polisi halafu akaiweka SMG usawa wa bega na kulenga tank la mafuta*******


Wakati hayo yanaendelea, nje ya mji wa Mombo, wakati huo huo barabara hiyo hiyo, maeneo ya njia panda ya Sadan, lilionekana gari aina ya land rover diffender, mali ya jeshi la polisi, lenye askari saba nyuma yake, huku wawili yani Dereva na mwenzie mmoja wakiwa mbele, lilionekana liliembea kwa speed ya mia moja hamsini, kuelekea upande wa Mkata.


Ndani ya gari nyuma palionekana SMG nane zikiwa zimewekwa chini, yani kwenye sakafu ya gari lile ambalo lilibeba askari waliovalia nguo za kiraia pasipo kuzingatia unadhifu, wapo waliovaa tisht na jinsi, wapo waliovaa kodrai na shati za kadet, wengine walivalia kaptura za kaki, na makoti mafupi ya baridi, pia wengine walivalia kofia za sueta maarufu kama mzura.


Gari likukuwa linaenda kasi, ni kweli liilikuwa speed, japo kwa kuwa tumezowea speed ya BMW s7, tunaona kama vile gari hili halikuwa katika speed inayo paswa.


Hata walipo karibia Mkata, wakawaona polisi wenzao wakiwa wamesimama pembeni ya barabara pamoja na gari lao, wakionekana katika mshangao fulani, ni wazi muda mchache uliopita, walikuwa wameshuhudia kitu wasicho kitegemea, na wao hawakusimama, walipita na speed yao hiyo hiyo.
Hilo lilikuwa ni kundi la polisi wa Ulenje, walioongozwa na koplo Othman, wenyewe upenda kumwita Ochu, ambae mawazo na akili yake vilikuwa kwenye kulikamata gari aina BMW jeusi, ambalo aliamini kuwa muda wowote wanalifikia, hawakujuwa kuwa lilikuwa kilomita nyingi mbele yao na kila sekunde lilikuwa lina ongeza umbali katiyao.


Tukiachana na hao, tunaenda maeneo ya Msata, mita mia nne toka kwenye round about ya maungio ya barabara ya bagamoyo na chalinze, ambapo tunaweza kuliona gari kama lile la mbele, yani la polisi nalo likiwa na askari saba nyuma wawili mbele, likitembea kwa speed kuelekea upande wa Mkata, nalo pia lilikuwa katika speed kama ya lile la mwanzo, japo lenyewe lilikuwa lina fikia wakati lina vuka mpaka speed mia moja sitini.


Ili lilikuwa ni kundi la koplo Cheleji, ambae pia kama mwenzie akili na mawazo yake, yalikuwa juu ya kufanikisha kulikamata BMW, maana ukiachilia kujenga sifa na kuaminiwa na Ulenje, pia wangejipatia fedha nzuri sana, hawakujari wala kuwaza juu mwisho wa wale waliopo kwenye gari hilo, ambalo ingetakiwa warudi nalo dar, wao walicho jari nikutekeleza kile walicho tumwa, ambacho ni kuwauwa wote watakao kuwepo ndani ya gari na kurudi na gari na mzigo uliopo ndani yake.


Kwa kuweka kumbu kumbu sawa nikwamba, koplo Cheleji pekee ndie aliemuona Deus, akiingia kwenye gari, hivyo ndie mwenye kuweza kuitambua sura ya kijana huyo, japo haku fahamu wala kujuwa kuwa kijana yule aliemuona pale kiluvya madukani, akiingia kwenye gari lile BMW jeusi ndie askari aliekuwa anazungumziwa Mitandaoni…..…….ENDELEA kufuatilia mkasa huu wa NYUMA YA MLANGO WA ADUI unao kujia hapa hapa jamii forums
Salute kwako mkuu
 
Back
Top Bottom