SASHA MLINZI WA NAFSI
SEASON 3
Sehemu ya.........56 -57
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047
ILIPOISHIA...
Baada ya polisi kufanya upekuzi kwa zaidi ya dakika 15 ndipo walipogundua kuwa hakukuwa na mtu yeyote kiwandani hapo, walichelewa. Na mbaya zaidi simu ya Inspekta Brandina haikupatikana...
SASA ENDELEA....
Usiku huo msafara wa gari tatu pamoja na lile lililo wabeba Inspekta Brandina pamoja na Tesha uliendelea kuchanja mbuga kwa kasi ukipita katika ya msitu mnene, mwisho waliacha barabara ile ya vumbi inayotoka kule kiwandani na sasa wakaingia katika barabara ya rami wakazidi kusonga mbele kwa kasi kuelekea kusikojulikana. Matumaini ya kuokolewa yalizidi kufifia, hata Inspekta Brandina mwenyewe ambaye awali alikuwa akijiamini sana taratibu akaanza kuingiwa na hofu, hali ilikuwa ni mbaya zaidi kwa mwanadada Tesha aliogopa mno
****
KISIWANI- NDANI YA HIMAYA YA MAGNUS
Baada ya Kareem na kikosi chake kutoka katika kile chumba cha kuhifadhia mizigo kila mmoja alitawanyika kuelekea upande wake katika chumba ambacho alichagua kupumzika usiku huo ndani ya himaya ya Magnus mpaka pale muda wa kuondoka alfajiri na mapema utakapowadia.
Felix yeye alipanda juu kabisa ghorofani katika jengo moja kubwa la kifahari sana, huko ndipo kilipokuwepo chumba chake cha kulala alichokuwa akikitumia siku zote tangu akiwa ni mdogo.
Alifungua mlango na kuingia ndani, kilikuwa ni chumba kikubwa mno kizuri chenye vitanda viwili pamoja mahitaji yote muhimu ndani yake.
Juu ya kitanda kimoja kati ya vile viwili alionekana mwanaume mmoja akiwa amelala. Huyu hakuwa mwingine bali mlinzi na msaidizi wa karibu wa Felix yaani Haron. Ilikuwa ni kawaida ya Felix kuongozana na Haron kila mahali anapokwenda. walikuwa pamoja kila mahali hata ile safari yake ya kwenda nchini Marekani aliongozana na Haron.
Felix aliingia ndani akatembea moja kwa moja akajitupa kitandani pasipo hata kuvua viatu, alikuwa amechoka mno na istoshe kichwa chake kilikuwa kimebeba mawazo rukuki.
"Vipi Felix, kila kitu kipo sawa? Vipi kuhusu Tesha? Mzee kasemaje?" Mara sauti ya Haron ilisikika akiuliza maswali mfululizo wakati huo aliinuka taratibu na kukaa juu kitandani.
Felix alimsikia vizuri sana lakini hakujibu kitu, hakuwa akijisikia kuongea kwa wakati huo.
"... Felix" Haron aliita.
"Unataka nini Haron? unachojali hasa ni nini? Wewe na Baba lenu si moja? au unanipeleleza ili baadae ukamwambie nini nawaza kufanya..." Felix alifoka akainuka na kukaa juu kitandani kama alivyofanya Haron, sasa wakageuka wote wakawa wanatazamana kila mmoja akiwa juu kitandani kwake.
"Hapana mimi siku zote niko upande wako Felix, ni siri zako ngapi nazificha mpaka sasa mzee hajui chochote..?" Alieleza Haron na hapo ndipo Felix akakumbuka jambo lingine aliloelezwa na baba yake Magnus, ni kuhusu siri ya mahusiano ya kimapenzi kati yake na Madam Husnata, hakujua ni vipi Magnus aliweza kuitambua siri hii na kisha kukaa kimya kwa kipindi chote. Felix aliishia kumtazama Haron kwa jicho kali kisha akajitupa kitandani, hakutaka usumbufu wala kuendelea kubishana.
Mpaka sasa kuna mambo mawili makubwa yaliyokuwa yakiitesa akili ya Felix, kwanza kabisa ni kuhusu usalama wa mpenzi wake Tesha ambaye hadi dakika hii hajui alipo na wala hajui ni mazingira gani anapitia kwa wakati huu. Jambo la pili ilikuwa ni kuhusu ile picha ya msichana mrembo aliyonyeshwa na baba yake mda mfupi uliopita, picha ya Sasha binti kutoka ISRA, binti ambaye ndiye muhusika mkuu wa opareshini yao itakayoanza asubuhi. Sura ya Sasha ilikuwa imeganda kwenye ufahamu wa Felix. Kila alipojaribu kujisahaulisha alishindwa. Magnus alifanya makusudi kabisa kuchagua aina ya picha ambayo aliamini itaweza kuamsha tamaa za kiume kwa kijana mwenye lika kama la mwanae Felix. Na kweli alifanikiwa kwa asilimia kubwa kiasi cha kumfanya Felix atamani kuifanya kazi aliyoagizwa na baba yake si tu kwa ajili ya kumsaidia mpenzi wake Tesha hapana bali pia alitamani kukutana uso kwa uso na Sasha binti wa Gu Gamilo kutoka ISRA.
Wakati Felix akiwa katika dimbwi la mawazo ndipo alipokumbuka jambo lingine muhimu. Tangu walipoondoka na Tesha jioni nyumbani kwa Mama David ambaye ni mama yake wa kuigiza huku akimuahidi kuwa wangerudi baada ya muda mfupi lakini hawakurudi.
Alitazama saa kubwa ukutani akabaini ilikuwa ni saa tisa na nusu usiku. Kwa kuwa tayari Felix anazo namba za simu za mama David alitamani kumpigia lakini akasita.
"...ni usiku sana atakuwa amelala! Ila sasa nilimuahidi nitarudi vipi kama akiwa na wasiwasi....mmh! Hapana hawezi kuwa na wasiwasi na mimi kwanza sio mtoto wake!....lakini kama sijarudi na sijamwambia lolote ataona kama nimemdharau....ila ni usiku sana saa kumi kasoro... Hapana nisimpigie....au basi ngoja nipige tu...."
Felix aliwaza na kuwazua mwisho akaamua kumpigia simu Mama David. Simu iliita kwa sekunde chache sana ikapokelewa.
"Ha..hallo..mama" Felix aliongea kwa wasiwasi kidogo, hakutegemea simu kupokelewa haraka kiasi kile ni wazi kuwa hata Mama David naye hakuwa amelala.
"Nini tena usiku huu Feisal?" Mama David alisikika akiuliza swali upande wa pili wa simu hata kabla ya salamu.
Felix alipatwa na kaubaridi ka furaha mara baada ya kusikia ameitwa kwa jina la Feisal. Ilionyesha matumaini makubwa ya yeye kupokelewa na Mama David kama mwanae kamili.
"Aaa! Ni...nilikuwa na wasiwasi sijakutaarifu kama sitorudi nyumbani leo nikaona nikupigie simu, sahamani kwa usumbufu mama"
"Haya sawa" Mama David alijibu kwa kifupi sana kisha akawa anajiandaa kukata simu.
"Aah! Mama samahani uko sawa kweli? sauti yako ni kama...."
"Nikiwa sawa nisipokuwa sawa wewe utanisaidia nini Feisal? Zaidi ya kuniongezea matatizo mnayonipa wewe na watu wako"
"Hapana usiseme hivyo mama. Naweza kukusaidia, najua bado ni mapema sana kuniamini ila nipe nafasi nitafanya kwa nafasi yangu, siwezi kuivunja ahadi niliyokupatia leo Mama" Felix alijieleza akijaribu kuuteka zaidi moyo wa Mama David aweze kumuamini. Wakati wakizungumza hayo Haron hakuwa amelala alikuwa macho akisikiliza kila kitu.
"Ni kuhusu mwanangu David. Hajarudi nyumbani mpaka sasa, Tesha aliniambia kuwa amemuagiza mikoani kikazi lakini moyo wangu unagoma kabisa kuamini, David asingeweza kuondoka bila kuniaga, sio kawaida yake, mbaya zaidi simu yake haipatikani, hata Tesha pia kwa sasa hapatikani. Nakosa amani kabisa nahisi kuna jambo mbaya huenda likawa limetokea, niliwahi kumpoteza mwanangu wa kwanza Feisal kama hivi, sitaki tena ijirudie kwa David..." Alieleza Mama David sauti yake ikionekana kujawa na hali ya wasiwasi.
Kimya kilitawala kwa muda, wakati huo Felix alikumbuka kila kitu kuhusu David, tayari alishafanya mazungumzo na Tesha akamueleza kuwa David alitekwa na watu wasiojulikana. Felix anafahamu vizuri kabisa watu waliomteka David ni watu wanaofanya kazi na baba yake yaani MG family na kwa vyovyote vile Felix alijua wazi kuwa kwa sasa David atakuwa amehifadhiwa kwenye lile bonde pamoja na mateka wengine.
Wakati Mama David akiendelea kutoa maelezo hayo Felix aliinuka taratibu akashuka kitandani akasogea dirishani na kufunua pazia. Sasa akawa anatazama nje kwa uzuri kabisa na kwa kuwa alikuwa juu ghorofani Felix aliweza kuona moja kwa moja hadi kule chini bondeni mahali walipohifadhiwa mateka wa baba yake. Wakati huo sauti ya Mama David iliendelea kusikika simuni akizungumza.
".... Kama utaweza nisaidie kumtafuta mwanangu David popote alipo kisha mrudishe nyumbani mara moja, ongea na Tesha vizuri mulize ni wapi David alikwenda. Kama utamrudisha David salama basi nitayaamini maneno yako na kukupokea kama mwanangu Feisal"
Kimya kilitawala tena kwa muda huku Felix akiyatafakari kiundani maelezo hayo kutoka kwa Mama David, wakati huo macho yake alikuwa ameyaelekeza lilipo lile bonde walipohifadhiwa mateka. Giza lilikuwa nene mno ndani ya bonde lile ingawa kwa mbali sana Felix aliweza kuwaona mateka hao wanaopitia maisha magumu bondeni wakiwa wamewasha moto katika maeneo mbalimbali kusaidia kujikinga na badiri kali bondeni humo. Kwa haraka haraka Felix aliamini David ambaye kwa sasa mama yake anamzungumzia yupo ndani ya bonde hilo pamoja na mateka wengine. Hakujua na wala hakuna aliyejua kuwa kwa sasa David hayuko bondeni bali alishatoka nje kabisa ya bonde hilo na hivi sasa yupo ndani ya chumba kimoja cha mizigo katika himaya hiyo ya Magnus.
"Feisal..unanisikia?" Mama David aliuliza mara baada ya ukimya wa muda mrefu.
****
Mtwara - Nachingwea....
Hiki ni kijiji anachoishi Feisal mwenyewe halisi kaka yake David ambaye inaaminika alishakufa miaka mingi iliyopita na sasa Felix anaishi kwa jina lake huku Mama David naye akiwa mbioni kumkubali kama mwanae.
Usiku huu majira ya kumi kasoro Feisal pia hakuwa amelala, bado kichwani alikuwa anaandamwa na mawazo rukuki kiasi cha kumfanya akose kabisa usingizi. Kwanza alikuwa akiwaza namna atakavyoweza kuyamudu majukumu mapya ya kusoma na kujiunga na kikosi cha zima moto na uokoaji lakini pili Feisal aliwaza ni namna gani ataweza kuifanya kazi ya kumtafuta ndugu yake Boaz mara tu atakapoingia jijini Dar es salaam. Boaz ni ndugu yake asiye wa damu ambaye aliyetekwa na watu wasiojulikana miaka miwili iliyopita. Feisal alikuwa sebuleni huku SASHA na sikujua(mdogo wake Boaz) wao wakiwa wamelala chumbani.
Pamoja na uwezo mkubwa wa kuogelea aliokuwa nao Feisal hadi kufanikiwa kumuokoa binti mrembo Sasha kutoka katika mafuriko ya maji lakini bado Feisal alikuwa na kipaji kingine cha pekee, uchoraji. Feisal alikuwa ni mtaalamu mno wa kuchora, alikuwa na uwezo wa kukikataza kitu au mtu na akamchora kama alivyo.
Hiki ndicho Feisal alikuwa anakifanya usiku huu ikiwa ni katika hatua zake za kwanza kabisa kufanya maandalizi muhimu ya kumtafuta Boaz.
Kama kawaida yake alikusanya vifaa vyake vyote muhimu vya uchoraji tayari kwa kazi. Picha aliyotaka kuichoro usiku huu ilikuwa ya tofuati kiasi, ni picha ya sura ya mtu ambaye aliwahi kumuona mara moja tu katika kipindi chote cha maisha yake, mtu ambaye alikuwa ni mmoja kati ya watu waliohusika na kumteka Boaz miaka miwili iliyopita.
Feisal alituliza akili yake na kuvuta kumbukumbu siku ile ya tukio 21/07/2019 siku ambayo Boaz pamoja na rafiki zake wengine walitekwa nje ya supermarket moja jijini Dar es salaam (MINI SUPERMARKET). Feisal aliikumbuka vizuri sura ya mmoja kati ya wale watekaji, yule ambaye alivua helmet yake kabla ya kuingia ndani ya gari (Felix). Ilikuwa ni kazi ngumu lakini ajabu ni kwamba baada ya masaa mawili hadi inatimia mda huu saa kumi kasoro Feisal alikuwa ameikamilisha kazi yake. Mkononi alikuwa na mchoro wa picha ya mtu anayefanana kwa asilimia kubwa na Felix. Laita kama ungekuwa unamfahamu Felix na kisha ukaitazama picha aliyoichora Feisal usingekuwa na sababu ya kujiuliza mara mbili mbili huyu ni nani. Naam, hiki ni kipaji kingine alichozaliwa nacho mwanaume huyu ambaye kwa sasa anaishi mbali na familia yake huku Mama yake na ndugu zake wengine wakiamini kwamba alishakufa na mbaya zaidi mtu aliyemchora ndio huyo anayeishi kwa jina lake hivi sasa.
Feisal alibaki ametulia kwa muda huku akiwa amekaza macho yake kuitazama picha hiyo aliyoichora.
" Nitakutafuta, nitakupata na lazima unieleze ni wapi uliwapeleka ndugu zangu..." Alisema Feisal huku akiuma meno yake kwa hasira.
****
Ni wakati huo huo ambapo mazungumzo kupitia simu kati ya Felix na Mama David yalikuwa yakiendelea.
"Feisal..unanisikia?" Mama David aliuliza mara baada ya ukimya wa muda mrefu.
"Ndiyo nakusikia mama..."
"Sawa, niahidi basi kama utamrudisha David nyumbani. Najua unazo nguvu za kumtafuta na kumpata" Mama David alizidi kuomba kwa msisitizo.
Felix alitulia kimya huku akiwaza amjibu nini Mama David. Aliamini kuwa David yupo katika lile bonde mbele yake akiwa kama mateka. Kwa dakika kadhaa Felix alijikuta anasahau habari za kazi ngumu wanayotarajia kuifanya asubuhi ya siku hiyo. Kazi ya kwenda Mtwara kumteka Sasha binti kutoka ISRA. Felix hakujua kuwa kwa sasa Sasha yupo mikononi mwa Feisal mtu anayeishi kwa kutumia jina lake na mbaya zaidi Feisal huyo huyo ameichora picha yake na anapanga kumtafuta kwa udi na uvumba ili amueleze ni wapi alipowapeleka ndugu zake mara baada ya kuwateka pale supermarket miaka miwili iliyopita.
Je, nini kitafuata?
Vipi kama Feisal na Felix wakikutana?
Nini itakuwa hatima ya Sasha?
Inspekta Brandina na Tesha wako wapi?
Vipi kuhusu David ndani ya kile chumba?
Na je? Felix atakubaliana na ombi la mama David?
Usikose kufuatilia mfululizo wa simulizi hii nzuri yenye kisa cha kusisimua.
Simulizi na Riwaya Za Saul David bril
Simulizi hii ni Tsh 1000 tu lipia kwa mpesa namba 0756862047 jina Saul au Airtel money namba 0788967317 jina Saul
Kisha njoo WhatsApp namba hzo hzo