Simulizi: Sasha Mlinzi wa Nafsi - 1

Simulizi: Sasha Mlinzi wa Nafsi - 1

Simulizi nyingine ya SAUL DAVID humu jamii foram
 
SASHA MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya...........42
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA....
"Felix, hadi hapa nilipofikia nimepambana na watu wazito na wakubwa kuliko hata wewe, mwisho wa siku wote niliwasweka gerezani. Acha tuone nani atakuwa na mchezo mzuri kati yangu mimi na wewe." Brandina alijisemea mwenyewe na baada ya hapo akapiga hatua kurudi ofisini kwake.

SASA ENDELEA...

"Afande Afande"
Mara Inspekta Brandina alisikia sauti ya kike ikimuita kutokea nyuma yake, akageuka kutazama. Alikuwa ni mwanadada mrembo Tesha.

"Tesha..!!" Aliita Inspekta Brandina

"Ndiyo ni mimi afande, yuko wapi Felix? Nini kinaendelea?" Alijibu Tesha kisha akauliza maswali mfululizo, wakati huo alikuwa akihema kwa nguvu sana

"Vipi mbona hivyo ulikuwa unakimbia?"

"Ndiyo nimekimbia kuanzia hapo sheri, kuna vijana wamenisababishia ajali kizembe kabisa" Alieleza Tesha asijue kuwa huu ulikuwa ni mpango wa makusudi uliofanywa na MG Family ili kumzuia asifike kituo cha polisi hadi pale watakapo maliza jambo lao.

"Kwa hiyo gari umeliacha wapi..?"

"Nimemwita kijana wangu mmoja anashughulikia taratibu nyingine muhimu, afande mbona hunijibu kuhusu Felix?"

"Felix hayupo hapa, mmepishana sekunde tu. Tumeshamuachia huru"

"Mmemuachia? Vipi kuhusu ile taarifa uliyonipa pale airport, kwa maana hiyo sio kweli Felix hana kosa si ndiyo hivyo afande?"
Brandina alitulia kwa muda kisha akatikisa kichwa chake kukubali.

"Nilijua tu Felix hawazi kufanya hivyo. Ameondoka mda mrefu, unaweza kujua alipoelekea?"

"Hauna namba yake?"

Lilikuwa ni swali gumu kwa Tesha kulijibu kwa sababu baada ya kutengana na Felix hata mawasiliano yalikufa. Ni kweli namba yake ya simu alikuwa nayo lakini Felix hakuwa akipatikana kwa muda mrefu hivyo Tesha akaamini Felix amebadilisha namba ya simu.

"Hauna namba yake?" Brandina alirudia Tena swali lake.

"Aah! Ipo lakini hapatikani , labda kama amewasha simu sasa hivi" Tesha alidanganya huku akizuga na kuchukua simu yake akafanya kama anataka kumpigia Felix

"Teshaa.." Brandina aliita, Tesha akainua uso wake kumtazama

"Usihangaike kumpigia mfuate nyumbani, kaondoka hapa na mama yake"

"Mama yake? yupi?"

"Huwafahamu wazazi wa Felix?" Aliuliza Inspekta Brandina. Hili lilikuwa ni swali la mtego akataka kujua kama watu hawa ni wapenzi basi huenda Tesha akamueleza kitu chochote kitakacho msaidia katika upelelezi wake kuhusu ukweli wa familia ya Felix.

"Mmh! Ukweli siwajui. Afande mimi na Felix hatuna muda mrefu sana kwenye mahusiano, sijui vitu vingi kuhusu yeye" Tesha alijibu akitoa kauli ambayo ilimfanya Brandina asiulize maswali mengine zaidi ni kama alimshtukia.

"Sawa, Felix kaondoka hapa na mama yake, yule mama David ndio mama yake Felix pia"

"Whaat!!"

"Yes! Iko hivyo, walipotezana kwa muda mrefu na leo ndio wamekutana hapa hapa kituoni" Alieleza Brandina.
Hizi zilikuwa ni taarifa ngeni zilizomuacha Tesha kinywa wazi. Eti mama yake David ni mama yake Felix pia .
[emoji294][emoji294][emoji294]

Safari kurudi nyumbani kwa mama David ilikuwa ikiendelea. Garini walikuwepo watu watatu yaani Haron, Felix na mama David. Kulikuwa na hali ya ukimya wa muda mrefu ndani ya gari hilo, kila mmoja alionekana kuwaza lake huku Haron akiwa ndiye dereva.

Hatimaye mama David alivunja ukimya huo.

"Mwanangu yuko wapi...?"

Kimya...

"Hamjanisikia? Nawauliza mwanangu yuko wapi? Tayari nimeshaifanya kazi yenu.." Mama David aliuliza tena safari hii kwa ukali kidogo.

"Mama mwanao yuko salama kuwa mtulivu, subiri tufike nyumbani" Alijibu Haron.
Wakati huo Felix alikuwa kimya kabisa huku akionekana kuwa mbali sana kimawazo. Bado mwanamke mrembo Tesha alikuwa ameganda kwenye ufahamu wa ubongo wake, kila sekunde alikuwa akilikumbuka lile tukio la uwanja wa ndege alipokutana na Tesha kwa mara nyingine baada ya kipindi kirefu kupita.

"No, lazima nimuone Tesha, lazima nimuweke karibu yangu. Nitamlinda mwenyewe dhidi ya baba" Aliwaza Felix

Dakika chache baada walifika nyumbani kwa mama David. Wakakuta tayari Madam Husnata na timu yake walishafika na kusimama nje ya nyumba hiyo wakiwasubiri.

Mara baada ya gari kusimama mama David alikuwa ni wa kwanza kushuka, akawa anapiga hatua ndefu ndefu kuelekea pale aliposimama Husnata.

"Kazi yako imeisha mwanangu yuko wapi?" Mama David aliuliza akiwa na jazba sana. Madam Husnata hakujibu kitu badala yake sauti ya Tatu ilisikika akiita jina la mama kutokea ndani ya nyumba ya Mama David.

Mama David alikimbia haraka kumuwahi binti yake ambaye naye alitoka akikimbia wakakutana katikati na kukumbatiana kwa upendo mkubwa sana. Mama David alishindwa kuyazuia machozi yaliyoanza kumtoka kwa wingi.


"Hi"

"Hi" Felix na Madam Husnata walisalimiana.

"Habari za muda mrefu Felix.."

"Ni nzuri sana"

"Karibu tena Tanzania"

"Asante nimekaribia.."

"Sikujua kama unampenzi anaitwa Tesha, by the way nimekumiss sana" Alisema Husnata, Felix hakijibu kitu akaishia kumtazama tu, ilionekana wazi wawili hawa kuna kitu kinaendelea katikati yao. Ndio sababu Husnata alishtuka akiwa pale ghorofani baada ya Kareem kuzungumza habari za mahusiano ya Felix na Tesha.

Macho na akili ya Felix vyote alikuwa amevielekeza waliko mama David na mwanae Tatu namna walivyokuwa wamekumbatiana kwa upendo mkubwa. Felix alijikuta akili yake inahama na kwenda mbali sana. Siku zote alikuwa akitamani kuishi maisha ya amani na upendo kama wanavyofanya binadamu hawa. Hakuna kitu alikuwa anakichukia kwenye maisha yake kama kuambiwa yeye si binadamu wa kawaida.

Felix alijisahau kabisa, akawa amekaza macho yake kuwatazama Mama David na mwanae Tatu. Husnata naye akawa anamtazama Felix asielewe amepatwa na nini.

"Mmeshaweka kila kitu sawa?" Haron alimuuliza Husnata.

"Yap! Kila kitu kiko vizuri bado tu kuongea na huyu mama aendelee kutunza siri maana nahisi askari wataendelea kuja kumuhoji, hasa yule wanamwita Brandina"

"Sawa, hongereni mmecheza mchezo mzuri sana. Hata mzee Magnus ninaimani atawapongeza sana akisikia"

"Ni kawaida yetu, hakuna kitu kinaweza kuishinda MG Family"

"Nakubali..." Alisema Haron kisha akapiga hatua akasogea karibu na Felix.

"Felix sasa tunaweza kwenda kisiwani kwa Mzee, bila shaka anatusubiri kwa hamu kubwa" Alisema Haron lakini Felix akawa kimya, hakujibu chochote.

"Felix..."

"Hapana siendi kisiwani" Alisema Felix uso wake ukionekana kumaanisha alichokisema. Haron na Husnata wakatoa macho kwa mshangao.

"Unamaana gani Felix"

"Haron, nenda kamwambie baba asante kwa kunitafutia familia, nafikiri ni wakati wangu sasa wa kuishi maisha yangu nikiwa huru, na hii ndio itakuwa familia yangu kuanzia leo" Felix alifafanua huku akiwatazama Mama David na Tatu ambao sasa walikuwa wakipiga hatua kuingia ndani, Felix akaanza kuwafuata nyuma.

"Mnataka nini tena kwangu?" Mama David alifoka mara baada ya Felix kufika pale walipo.

"Nina ombi moja kwako Mama yangu..."

"Nini? Ombi gani?" Aliuliza Mama David, mara Felix akasogea karibu yake na kupiga magoti mbele yake.
Lilikuwa ni tukio lililowaacha kinywa wazi si Haron, si Husnata na hata mama David mwenyewe alishangaa.

"Kwanza kabisa kwa niaba ya wenzangu naomba utusamehe kwa hiki tulichokifanya kwako mama yangu. Lakini pia naomba uniruhusu niwe mwanafamilia wako mama, naomba niichukue nafasi ya marehemu mwanao Feisal. Najua sio rahisi kunielewa lakini tafadhali kwa ruksa yako mama naomba nifanye mwanao niko chini ya miguu yako" Felix aliongea kwa hisia kali.
Ni kweli kabisa alikuwa anamaanisha kile anachokisema. Kwa aina ya maisha aliyokuwa akiishi kijana huyu akifuata sheria kali za baba yake Magnus ambaye alidiriki kumtenga hadi na watu anaowapenda kama vile Tesha, ni kweli kabisa Felix alikuwa na haki ya kuongea maneno kama yale.

"We kijana... Hivi haijatosha tu kwa yote mliyoyafanya kwangu. Mnanitakia nini tena ondokeni...nimesema siwataki...ondoka..ondokaaa" Mama David alipaza sauti huku akivua kandambili yake akaanza kumtandika nayo kijana Felix.

Haraka Haron aliwahi na kwenda kumzuia Mama David aache kufanya kile anachokifanya, ilikuwa ni hatari sana kama Magnus baba wa Felix atazipata habari hizi.

"Sogeaa... " Felix alipaza sauti akainuka ghafula na kusimama katikati ya Haron na mama David. Akawa anamtazama Haron kwa macho makali sana.

"Katu usithubutu tena kuinua mkono wako kumgusa huyu mama, iwe mwanzo na mwisho, nasema iwe mwanzo na mwisho" Felix aliongea kwa jazba huku mdomo wake ukitetemeka, macho yake yakawa yanabadilika na kuwa ya kijani kisha yakarudi tena kwenye hali yake.
Ilikuwa ni kwa mara ya kwanza Haron anamshuhudia Felix akiwa katika hali hiyo, hapo akaamini ni kweli Felix ameamua.

"Felix..." Mara kuna sauti ya kike ilisikika ikiita. Felix na wengine wote wakaelekeza macho yao mahali sauti hiyo imetoka.
Uso kwa uso Felix anagonganisha macho yake na macho ya Tesha.

Je, nini kitafuata?

ITAENDELEA...
 
Hapa mwamba ataonekana katikati ya june 2023. Too sad. By the way hata kama hatulipi na kuna wengine wananunua hii stor! Ipo siku ntainunua huko nije niibwage humu! We jamaa ni mnyanyasaji sana! Sote tuna vipaji vikali! Wewe una cha kutunga na kupost mimi nna cha ku log in jf na kusoma stor! Kila mtu athamini kipaji cha mwenzake ili dunia iwe sehemu salama ya kuishi! Kwa kila mtu! Mwamba una kipaji kasoro hizo mizinguo
 
Hapa mwamba ataonekana katikati ya june 2023. Too sad. By the way hata kama hatulipi na kuna wengine wananunua hii stor! Ipo siku ntainunua huko nije niibwage humu! We jamaa ni mnyanyasaji sana! Sote tuna vipaji vikali! Wewe una cha kutunga na kupost mimi nna cha ku log in jf na kusoma stor! Kila mtu athamini kipaji cha mwenzake ili dunia iwe sehemu salama ya kuishi! Kwa kila mtu! Mwamba una kipaji kasoro hizo mizinguo
Pole sana kaka,,, tutamaliza simulizi wala usijali
 
Hapa mwamba ataonekana katikati ya june 2023. Too sad. By the way hata kama hatulipi na kuna wengine wananunua hii stor! Ipo siku ntainunua huko nije niibwage humu! We jamaa ni mnyanyasaji sana! Sote tuna vipaji vikali! Wewe una cha kutunga na kupost mimi nna cha ku log in jf na kusoma stor! Kila mtu athamini kipaji cha mwenzake ili dunia iwe sehemu salama ya kuishi! Kwa kila mtu! Mwamba una kipaji kasoro hizo mizinguo
Soma hii SIMULIZI yangu nyingine imefika MWISHO kwa mwendo kama huu. Msomaji aliapta anachokitaka na mimi nilipata nachokitaka[emoji120] [emoji116][emoji116]
 
SASHA MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya...........43
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA....
"Felix..." Mara kuna sauti ya kike ilisikika ikiita. Felix na wengine wote wakaelekeza macho yao mahali sauti hiyo imetoka.
Uso kwa uso Felix anagonganisha macho yake na macho ya Tesha

SASA ENDELEA…
“Tesha…..” Felix aliita kwa sauti ya chini akiwa haamini macho yake, ni kwa mara nyingine tena tangu afike kutoka Marekani anakutana na mwanamke huyu mara baada ya kuonana naye kwa mara ya kwanza pale uwanja wa ndege asubuhi ya siku hiyo.

Felix na Tesha walibaki wakitazamana kwa zaidi ya sekunde 30 mwisho walikimbia wote na kwenda kukumbatiana kwa nguvu. Ni wazi wawili hawa walikuwa wamekumbukana kupita maelezo, istoshe walionekana kupendana sana.

“Felix...”

“Tesha...”

“Kwa nini unanifanyia hivi lakini?”

“Nisamehe mama, nisamehe sana…”Alisema Felix huku akiupapasa mgongo wa Tesha taratibu kumtuliza. Tesha hakuweza kuyazuia macho yake yasitoe machozi,alilia sana.

“Tesha usilie tafadhali, unanifanya niumie zaidi” Alisema Felix sura yake ikionekana kubeba uchungu mkubwa. Hakujua ni vipi atajieleza mbele ya mpenzi wake amuelewe. Ni wazi alikuwa amemkosea mno tena mno. Lakini pamoja na hayo yote haikuwa rahisi kwake kuweka wazi ukweli uliomfanya kuanza kumuepuka Tesha ghafula. Alifanya hivyo ili kumlinda dhidi ya baba yake ambaye aliahidi kumuua Tesha kama tu Felix ataendelea kuwa na mahusiano naye. Lakini Felix ataanzia wapi kumueleza Tesha ukweli huo?

Waliendelea kukumbatiana kwa mahaba mazito huku tukio hilo likidumu kwa zaidi ya dakika tano. Wakati huo madam Husnata alionekana kukwera mno na kile kilichokuwa kikiendelea. Mwanadada huyu hatari Kutoka kundi la kigaidi MG Family akawa anamtazama Tesha kwa macho makali mno.

Mama David naye alibaki katika hali ya mshangao asielewe ni vipi Tesha ameweza kufahamiana na Felix mtu anaeishi kwa jina bandia ambalo ni jina la mtoto wake anaeamini amefariki miaka mingi iliyopita. Tayari alishajenga chuki kubwa dhidi ya mtu huyo pamoja na wale wengine wote ambao alishirikiana nao, ikafika hatua hadi wakadiriki kumteka binti yake mdogo Tatu ili tu afanye vile wanavyotaka wao.
Mwisho Felix alimuachia Tesha, akapiga hatua na kusogea karibu na Haron, akaongea kwa sauti ya chini ili mtu mwingine asisikie zaidi ya Haron mwenyewe.

“Sasa unaweza kurudi kisiwani kwa mzee, mimi nitabaki hapa na familia yangu, nitabaki hapa na Tesha pia. Naomba mpelekee hizo taarifa kwa baba kule kisiwani mwambie Felix amemrudia Tesha, sitoogopa tena vitisho vyake. Kama atajaribu kuinua mkono wake na kumgusa huyu mwanamke basi namuhakikishia kwa mikono yangu nitakisambaratisha kile kisiwa chake na kukigeuza majivu”

“lakini Felix….”

“Go and tell him what I have said, Haron sitaki ubishana na wewe. Nikisema nimesema” Felix alisisitiza.

Haron hakuwa na namna nyingine ya kuendelea kupingana na maamuzi ya Felix, alishaona Felix anamaanisha anachokisema. Taratibu akaingia kwenye gari yake na kuondoka. Sasa alisalia Madam Husnata pamoja na walinzi wake.
Mwanadada huyu hatari alipiga hatua kisha akaenda na kusimama mbele ya Felix huku sura yake ikionekana kubeba jambo zito mno. Alipomfikia Felix akataka kusema jambo lakini mara Felix alimuwahi na kuongea…

“Hapa sio mahara pake Husnata, unajua tuna mambo mengi ya kuongea mimi na wewe. Nitakutafuta mwenyewe baadae tafadhali sana”
Husnata alimtazama Felix kwa macho makali kisha akajibu akisema...

“Hakikiasha unafanya hivyo Felix tofauti na hapo unajua nitafanya nini?” Alisema Husnata kisha akageuka na kumtazama Tesha. Hapo aliamini kabisa Felix anaelewa nini kitatokea kama tu hatofanya kama alivyo ahidi. Mwisho Madam Husnata aliondoka akaingia ndani ya gari lake yeye pamoja na walinzi wake wakaondoka. Felix aligeuka akawatazama Mama David na Tesha ambao wakati wote huo walikuwa kimya wakishuhudia mambo yanayoendelea.
Ni mtoto mdogo pekee ndiye angeshindwa kutambua kuwa kuna mambo hayako sawa kwa Felix na watu wake ila si kwa mwanamke anayejitambua kama Tesha. Mpaka sasa tayari alikuwa na maswali zaidi ya 20 kichwani kwake ambayo yote haya yalihitaji ufafanuzi yakinifu kutoka kwa mpenzi wake Felix ambaye sasa alikuwa akielekea pale walipo.
Mama David alitamani kumzuia asije lakini kwa heshima ya Tesha akaamua kumeza mate na kusubiri kuona hatima ya mambo hayo inakuwaje.
****

Upande wa pili katika Mkoani Mtwara wilaya ya masasi kijiji cha Nachingwe katika nyumba anayoishi kijana Feisal hapo ndipo mahali alipomleta Sasha mara baada ya kumuokoa kijijini Nagaga wakati wa mafuriko.
Ni majira ya saa za jioni Sasha alionekana amekaa kwenye kiti kidogo cha miguu mitatu nje ya nyumba hiyo yenye vyumba vitatu pekee. Alikuwa amejifunika kikoi chenye rangi ya kijani huku mbele yake kukiwa na jiko la mkaa, alikuwa kiota moto. Sasha alionekana ni mwenye mawazo sana bado hakujua ni wapi ataanzia kuifanya kazi ambayo alipewa na marehemu Bi Noha tangu akiwa kule kwenye mji wa ajabu ISRA. Sasha alipewa kazi ya kumlinda kijana David ambaye mpaka sasa hakujua anampata vipi, yuko wapi anafanya nini. Pamoja na kwamba Sasha alifukuzwa ISRA na kunyang’anywa nguvu zake lakini bado aliendelea kuishi na kuyaamini maneno ya Bi Noha aliyesema kila kitu kinachotokea kwenye maisha yake ni matokeo ya HATIMA iliyokwisha kupangwa, hivyo ndiyo sababu Sasha hakukata tamaa. Aliamini hata kitendo cha yeye kutupwa nje ya ISRA ilikuwa ni njia ya yeye kukutana na David kwa urahisi ili kuweza kutimiza kazi kubwa ya kuhakikisha anamlinda kijana huyo. Jambo ambalo hakujua ni kwamba mwanaume ambaye amemtoa kutoka kwenye maji ni kaka wa mtu anayemtafuta yaani David.

“Vipi unajisikiaje sasa?”
Sauti hii ya Feisal ndiyo iliyomshtua Sasha kutoka kwenye dimbwi la mawazo

“Angalau nina ahueni kidogo”

“Pole, shika kikombe cha chai angalau upashe mwili joto” Alisema Feisal huku akivuta kiti,akasogea na kukaa pembeni ya Sasha, kisha akampatia kikombe cha chuma kilichochakaa chenye chai ndani yake.
Sasha aliipokea ile chai akaanza kunywa taratibu, wote walikuwa kimya huku wakitazamana kwa macho ya kuibia ibia. Bado Feisal hakuchoka kumtazama mwanamke huyo ambaye alikuwa na uzuri wa asili tena wa ajabu mno, kila alipomtazama alijikuta anavutiwa kumtazama zaidi na zaidi. Mara wakagonganisha macho yao.

“Aah…eee.. vipi bado kumbukumbu zako hazijarejea? Yaani hukumbuki hata kitu kimoja, mfano wapi ni nyumbani kwako, jina la ndugu yako yeyote mmm?”

“Hapana kakangu, sikumbuki kitu chochote mpaka sasa” Alijibu Sasha na wakati akisema hivyo mara ghafula wote walishtushwa na milio mikali ya gari zilizokuwa zinakuja kwa kasi eneo hilo. Waliinuka na kusimama juu huku kila mmoja akiwa haelewi ni nini kinaendelea. Msafara wa gari zaidi ya sita ulionekana ukija kwa kasi kuelekea pale walipo.
Feisal na Sasha walitazamana kila mmoja akimuangalia mwenzake kwa macho ya kuuliza. Hakuna aliyeelewa ni nini kinaendelea.

Je, hawa ni akina nani? Kutoka wapi? Wanataka nini?

ITAENDELEA….
 
Soma hii SIMULIZI yangu nyingine imefika MWISHO kwa mwendo kama huu. Msomaji aliapta anachokitaka na mimi nilipata nachokitaka[emoji120] [emoji116][emoji116]
duu kumbe uliimalizia ngoja niirejelee
 
Simulizi hii ni Tsh 1000 tu lipia kwa mpesa namba 0756862047 jina Saul au Airtel money namba 0788967317 jina Saul
Kisha njoo WhatsApp namba hzo hzo[emoji120]
 
Hivi karibuni.....
0756862047
FB_IMG_1686718423788.jpg
 
SASHA MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya...........44
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA....
Msafara wa gari zaidi ya sita ulionekana ukija kwa kasi kuelekea pale walipo. Feisal na Sasha walitazamana kila mmoja akimuangalia mwenzake kwa macho ya kuuliza. Hakuna aliyeelewa ni nini kinaendelea.

SASA ENDELEA…
Huu ulikuwa ni msafara wa mkuu wa mkowa wa Mtwara mheshimiwa Innocent James Warimbo. Alifika nyumbani anapoishi kijana Feisal ambaye mpaka sasa alikuwa amejizolea umaarufu pasipo yeye mwenyewe kujua. Kile kipande cha video walichokuwa wakirekodi mashuhuda wakati ule wa mafuriko kijijini Nagaga kikimuonyesha Feisal akijitosa majini katika kina kirefu kwa ajili ya kumsaidia mwanamke aliyekuwa mbioni kupoteza maisha kilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii hasa whatsApp na instagram huku wengi wakimsifia Feisal kwa ujasiri mkubwa aliouonyesha. Clip hii iliwafikia hadi viongozi wakubwa serikalini na hapo wakataka kujua ni nini kiliendelea zaidi kwani video ilionyesha mpaka mwisho ambapo Feisal na Yule mwanamke (Sasha) walionekana wakibebwa na yale maji yaendayo kasi sana. Mwisho walipata habari kuwa Yule kijana pamoja na mwanamke huyo walitoka wakiwa salama salmini. Ilikuwa ni habari njema iliyogusa mioyo ya watu wengi. Pamoja na kwamba wengi walipoteza maisha katika dhoruba ile lakini ujasiri aliouonyesha kijana Feisal ulikuwa ni wa kipekee mno. Ndipo hapo Mheshimiwa mkuu wa mkoa Bwana Innocent Warimbo akatamani kuonana na kijana huyo siku hiyo hiyo ya tukio.

Alifika kijijini Nchingwea majira ya saa moja jioni na baadae akaongozwa na watu wanaomfahamu Feisal hadi nyumba anayoishi kijana huyo na kwa bahati nzuri alimkuta. Mkuu wa mkoa alifanya mazungumzo kwa muda na Feisal huku akimsifia sana kwa ujasiri mkubwa aliouonyesha.

“Feisal…” Aliita mkuu wa mkoa

“Naam mzee”

“Nimekuja hapa binafsi na kama muwakirishi wa serikali pia, hata muheshimiwa Rais amependezwa mno kwa hiki ulichokifanya leo na ameagiza tufanye kitu kwa ajili yako. Pamoja na pesa za pongezi tulizokupatia lakini pia tungependa kukuchukua ujiunge na jeshi la zimamoto na uokoaji. Utapewa elimu ya darasani na baadae mafunzo kwa vitendo na kisha moja kwa moja utajiunga na jeshi la polisi kitengo cha uokoajili, hii ni ofa imetolewa na mheshimiwa Rais yeye mwenyewe…sijui unasemaje, Je uko tayari?” Alieleza mkuu wa mkoa na mwisho akauliza swali.
Feisal alitabasamu na kujibu…

“Mheshimiwa ni nani anaweza kupewa ofa kama hiyo alafu akaikataa? Tena kutoka kwa Mheshimiwa Rais, mimi niko tayari…”

“Hahahah inategemeana si unajua kuna kazi nyingine unaweza kuwa unafanya lakini huipendi, mfano mimi nina binti yangu anaitwa Cecillia nilipenda sana awe nesi lakini anaogopa vidonda na damu, nimepambana lakini wapi ikabidi nimruhusu asome anachokita yeye, sasa ni Muhasibu mzuri tu. Haya mambo yapo kwenye maisha si ndiyo hivyo binti?” Alieleza Mkuu wa mkoa kisha akauliza swali na kumtazama Sasha usoni.

“Ni kweli baba” Sasha alijibu, lakini macho ya mkuu wa mkoa hayakubanduka kwenye uso wa mwanamke huyo, alivutiwa kumtazama zaidi.

“Kwa hiyo umesema amepoteza kumbukumbu zake si ndiyo?”

“Ndiyo mzee, nahisi zile purukushani za majini ndiyo zimepelekea yote haya” Alijibu Feisal

“Sawa basi itabidi niondoke naye, nitampeleka hospitali kwa msaada zaidi wa kitaalamu wamsaidie ili kumbukumbu zake zirejee mapema” Alisema mkuu wa mkoa kauli iliyowafanya Sasha na Feisal watazamane lakini mwisho walikubali.

Baada ya maongezi marefu na kijana Feisal pamoja na mwanamke aliyeokolewa Sasha, mwisho mkuu wa mkoa alitoka kuongea na wakazi wa kijiji hicho ambao walikusanyika mara tu baada ya msafara wa mheshimiwa Mkuu wa mkoa kufika eneo hilo. Vyombo mbalimbali vya habari vilikuwa maeneo hayo pia huku vikirekodi na kurusha matangazo ya moja kwa moja juu ya taarifa za mafuriko kijijini Nagaga pamoja na taarifa nyingine muhimu zinazohusiana na tukio hilo.

Mkuu wa mkoa aliongea na wananchi hao zaidi ya dakika tano huku akiweka wazi ofa kubwa ambayo serikali imeitoa kwa kijana Feisal. Kila mmoja alionekana kufurahishwa na maamuzi hayo, ni kweli Feisal alistahili.

“Feisal, mimi siko tayari kuondoka na huyu mzee, nina imani kumbukumbu zangu zitarudi sio mda mrefu” Sasha aliongea kwa sauti ya chini wakati mkuu wa mkoa akiendelea kutoa maelezo namna watakavyo gharamia kila kitu kwa kijana Feisal kumsafirisha hadi Dar es Salaam ambako ndipo kinapatikana chuo walichochakugua kumpatia mafunzo hayo.

Feisal alistaajabu kiasi baada ya Sasha kumwambia kitu ambacho hakutegemea kabisa kukisikia, wakatazamana huku Sasha akiachia tabasamu lililo anza kuutesa moyo wa Feisal taratibu.

“Sawa ngoja amalize kuongea tutaona namna ya kufanya” Alijibu Feisal, ukweli kutoka moyoni mwake hata yeye hakuwa akitamani Sasha aondoke na mheshimiwa mkuu wa mkoa. Tayari alishaanza kutamani kuwa karibu zaidi na binti huyo kutoka mji wa ajabu ISRA.
***

“Felix unawezaje kufanya hivyo, ni kwa muda gani nimekuwa na wewe na hujawahi kunieleza lolote kuhusu wazazi wako. Leo kwenye mazingira kama haya ndio najuana na mama yako mzazi kweli Felix, hapana hukupaswa kunifanyia hivyo” Haya yalikuwa ni maneno ya binti mrembo Tesha akilalamika. Wakati huo Felix na Tesha walikuwa ndani ya nyumba ya Mama David pamoja na Mama David mwenyewe. Ni mara baada ya Madam Husnata pamoja na Haron kuondoka.
Mama David na Felix walitazamani kisha Felix akaanza kueleza historia ile ya uongo akijifanya yeye ni Feisal mtoto wa Mama David aliyepotea kwa mda mrefu huku wengi wakiamini kuwa alishakufa. Ilikuwa ni historia ile ya uongo inayoeleza namna Feisal alivyonusurika kufa baada ya kutumbukia majini na baadae akajikuta anapoteza kumbukumbu pamoja na kupotezana na ndugu zake.

“Ninavyokwambia siku zote sina ndugu nilikuwa namaanisha kweli Tesha, lakini Mungu ni mkubwa sana kupitia changamoto niliyopata leo kukamatwa na polisi kumbe ilikuwa ni njia ya kukutana na mama yangu. Hakika Mungu ni wa ajabu sana” Alieleza Felix huku akimgeukia Mama David ambaye alikuwa ameikunja sura yake, lakini alipotazamwa akalazimisha tabasamu usoni pake. Ni kweli kabisa Mama David alikuwa hakubaliani na kumpokea Felix kama mwanae lakini tayari alishachimbwa mkwara mzito na Madam Husnata kuitunza siri hiyo, istoshe pia wakati ule Felix amepiga magoti na kumuomba sana tena kwa unyenyekevu mkubwa awe sehemu ya familia yake na kisha kumpa onyo zito mwenzake Haron asijaribu kumgusa, hali hii ilianza kumjengea imani kwa kiasi Mama David.

“Msamehe bure mwenzako, hata sio kosa lake. Tumshukuru tu Mungu kwa kutukutanisha tena” Alisema Mama David

“Kwa kuwa mama ndiyo kaongea basi sina budi kukusamehe, sasa sijui nikuite nani Felix au Feisal?”

“Ahahaha! niite vyovyote tu, yote ni majina yangu”

Alijibu Felix, amini usiamini wakati huo huo katika runinga ya mama David zilikuwa zikirushwa habari za shujaa Feisal kutoka kijijini Nachingwea mkoani Mtwara aliyepewa ofa ya kujiunga na jeshi la polisi mara baada ya kufanya tukio moja la kishujaa baada ya kumuokoa mwanamke mmoja kwenye mafuriko makubwa ya maji. Felix hakuona wala Mama David hakuona isipokuwa Tesha ambaye naye hakutilia maanani sana isipokuwa alivutiwa sana na yule mwanamke aliyeokolewa (Sasha) akatamani kama angemtumia katika biashara zake za urembo na mitindo.
Sijui ni nini kingetokea kama Mama David angemuona mwanae halisi Feisal katika runinga ambaye nafasi yake imechukuliwa na Felix mtoto wa Magnus. Na sasa Felix yupo ndani ya nyumba yake Swali ni je, Mama David angemuona Feisal mwanae angemkumbuka? Je, vipi kwa Feisal mwenyewe anakumbuka nini kuhusu ndugu zake? Na sasa amepata ofa ya kuja Dar es salaam jiji ambalo wanaishi ndugu zake, lakini istoshe ni jiji ambalo Felix mtu aliyeishi kwa muda mrefu akilitumia jina lake anapatikana.
*****

Upande wa pili katika kisiwa chenye himaya ya mtu mzito Magnus kiongozi mkuu na mmilikiwa kundi kubwa la kigaidi MG Family mambo yalizidi kusonga taratibu. Sasa mtu huyu alikuwa ndani ya kile chumba cha mateso akijaribu kutumia njia ya ushawishi kama alivyoeleza mwanzo ili kuweza kutambua ni namna gani kijana Zungu aliweza kutoka nje ya lile bonde alilowahifadhi mateka wake akafanikiwa kufika hadi kule barabarani.

Wakati akifanya mazungumzo na Zungu mara kunataarifa zilimfikia msaidizi wake wa kazi kwa njia ya ujumbe wa maandishi na moja kwa moja msaidizi huyo akazifikisha kwa Magnus, akawa anamueleza kwa sauti ya chini.

“Nini? Sasha ameonekana wapi?” Aliuliza Magnus kwa mshangao mkubwa.
“wanasema wamemuona kwenye runinga mkuu…”

“Yuko sehemu gani?”

“Mtwara kijiji kimoja kinaitwa Nchingwea”

“Sawa upesi wasiliana na MG Family wambie namuhitaji huyu binti aletwe hapa kisiwani haraka”

“Sawa mkuu, nawasilaina na Kareem sasa hivi…”

“Sawa, wambie haina haja ya kutumia king’ora, hana nguvu zozote kwa sasa” Magnus alisisitiza.

Je, nini kitafuata?
Sasha atakuwa salama?
Vipi kuhusu David na Dayana kule bondeni?
Nini kitaendelea kati ya Felix na Tesha?
Magnus ataruhusu mahusiano yao yaendelee?
Kuna siri gani kati ya Felix na Madam Husnata?

ITAENDELEA…
 
SASHA MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya...........45 - 46
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA....
“Sawa upesi wasiliana na MG Family wambie namuhitaji huyu binti aletwe hapa kisiwani haraka”

“Sawa mkuu, nawasilaina na Kareem sasa hivi…”

“Sawa, wambie haina haja ya kutumia king’ora, hana nguvu zozote kwa sasa” Magnus alisisitiza.

SASA ENDELEA…
****

Tunarudi ndani ya kisiwa cha Magnus katika bonde alilowahifadhi mateka wake. Maisha yaliendelea kama kawaida, taratibu mateka hao walijikuta wanaanza kulisahau tukio la usiku wa jana pindi wenzao walipojaribu kutoroka na mwisho wakajikuta wanauawa kwa kupigwa risasi na walinzi wa Magnus. Tayari walishaizoea hali hii ya kuona wenzao wanakufa mara kwa mara pale wanapojaribu kutoroka lakini pia wapo wale wanaofariki baada ya kushindwa kukabiliana na maisha magumu ndani ya bonde hilo.

Hali ilikuwa nitofauti kabisa kwa kijana David na binti Dayana ambao wao ndio walijiona kama ni chanzo cha wenzao kuuawa kikatiri usiku wa jana. Wakati wote David alikuwa amekaa na kujiinamia. Hakuwa amekula wala kunywa chochote hadi dakika hiyo. Alimuwaza rafiki yake Zungu ambaye kwa sasa anapitia mateso mazito mno kwa sababu yake.

“Tayari tumeshapata njia, kilichobaki ni kutafuta namna nzuri ya kutoroka hapa kisiwani…” Hatimae David alizungumza baada ya ukimya wa muda mrefu.

“David” Dayana aliita, David akageuka na kumtazama

“…..unajua mimi sikuelewi kabisa”

“Kwanini…?”

“Sikuelewi ani, unauoga ambao sio wa kawaida hivi unakumbuka sababu hasa ya Zungu kuteleza na kuangakua kule juu pangoni ni nini?...wewe ndiyo sababu David, alikuwa anajaribu kukusaidia wewe na baadae akajikuta yeye ndio anaingia kwenye matatizo zaidi. Sasa nashangaa huo ujasiri wa kuongea maneno hayo unaotoa wapi wakati tukiingia kwenye vitendo unakuwa na woga si woga…ani hueleweki” Dayana aliongea maneno ambayo kwa kiasi kikubwa yalimgusa sana David. Ni kweli kabisa alikuwa na aina fulani ya woga kutokana na lile tatizo lake la Acrophobia.

“Dayana ni kweli kabisa unavyosema, lakini sikufanya vile kwa kupenda ninalo tatizo moja kubwa tangu nikiwa mdogo, pamoja na hayo yote haimaaniishi kwamba sitakiwi kupambana, ninayo imani kuwa nitaweza kutoroka hapa ingawa nina hili tatizo”

“Ni tatizo gani David?”
Aliuliza Dayana akitamani kujua zaidi kuhusu tatizo hilo la kiafya linalomsumbua David. Hapo David alimsimulia Dayana kwa kina ni wapi hasa tatizo hili la afya ya kisaikolojia lilianzia yaani siku ile alipomshuhudia kaka yake Feisal pamoja na baba yake Mzee Selemani wakitumbukia majini na mwisho wakapoteza maisha. Ilikuwa ni kisa kizito kilichomsisimua sana Dayana akajikuta anamuonea huruma mno David.

“Kwa hiyo mwili wa kaka yako Feisal haukuwai kuonekana kabisa?”

“Ndiyo, alifia majini na kupotelea huko huko, mwili wake ukawa chakula cha samaki. Kila nikikumbuka hili tukio sio siri huwa naumia sana Dayana. Laiti siku zingekuwa zinarudi nyuma na kutupa nafasi ya kurekebisha makosa yetu basi nisinge thubutu kurudia ule upuuzi wa kumsukuma kaka Feisal ili tu niuwahi mpira. Ona sasa ile dhambi inanitafuna hadi leo. Kifo cha kaka na baba hakijatosha, safari hii tena nampoteza mtu muhimu kama Zungu kwa sababu ya uzembe kama ule ule niliowahi kuufanya miaka ile”

“It’s okay David hutakiwi kujilaumu sana, hata hivyo ulikuwa bado ni mtoto… sio kosa lako kabisa” Alisema Dayana akijaribu kumtuliza David na baadae akatulia.

“Kwa hiyo sasa kama unahilo tatizo la saikolojia tutawezaje kutoroka David?”

“Sio ishu kubwa nina uwezo wa kujizuia na….” Alisema David lakini kabla hajakamilisha sentesi yake mara alisita kuendelea macho yake akia ameyagandisha mbele kumtazama mateka mmoja ambaye alikuwa akipita mbele yao hatua kadhaa kutoka pale walipokuwa. Dayana naye akaelekeza macho yake kuelekea kule anakotazama David. Wote walimuona yule jamaa ambaye usiku wa jana ndiye aliyekuwa akiwashawishi wenzake wapande ngazi wakimbie, lakini ajabu yeye hakupigwa risasi kama wengine. Alioneakna kuwa mzima wa afya tele.

“Huyu fara kwa hiyo yeye hawakumuona au…we jamaa! Oyaa! Oyaa! Wewe…” David alionge mwisho akawa anamwita.

“Anitwa bonge, ita Boaz …” Dayana akamsaidia

“Oyaa Boaziiiiiiii …..” aliita David safari hii kwa sauti kubwa sana yule mtu(Boaz) akasimama na kugeuka.

Alipogonganisha macho na David Boaz akaonekana kuogopa, alikumbuka vizuri usiku wa jana alibishana vikali na David wakati akiwashauri wasitoroke. David akawa anapiga hatua kumfuata, Dayana naye akafuata nyuma.

“Inakuwaje umewapeleka wenzako kwenye kifo alafu wewe umerudi mzima?” Aliuliza David huku akimsogelea Boaz kwa mikwara mizito, hakujali umbo kubwa la mwili wa Boaz.

“mimi pia nimenusurika kufa ndugu yangu angalia” Boaz alijitetea, akageuka na kuwaonyesha eneo la mgongo mahali alipoparazwa na risasi.

“Lakini niliwambia, unaona sasa madhara yake, wenzako wamekufa”

“Hata mimi naona ni heri nife tu maana nishachoka….”

“Kama ni hivyo basi si ungebaki huko juu wakupige risasi na wewe pia”

“Mwanangu unaongea kirahisi sana hivi unajua kwa nini mimi natamani sana kutoka kwenye hichi kisiwa?” Aliuliza Boaz

“Hakuna asiyetamani kutoka kila mtu humu anataka uhuru”

“Lakini mimi ni zaidi ya ninyi wote, unajua kwa nini?”

“Mmnh….”

“Twende tukakae niwasimulie kitu” Alisema Boaz, David na Dayana wakatazamana kisha wakapeana ishara kuwa wakubali tu kumsikiliza Boaz

Walikaa mahali walipozoea kukaa kila siku kisha Boaz akaanza kueleza ni kipi hasa kinachomfanya ahisi yeye ni muhimu zaidi kutoka kuliko mateka wengine wote.

Akaanza kwa kusema…

“mimi ni mzaliwa wa Mtwara wilaya ya masasi, natokea familia ya chini sana kiuchumi, mimi na kaka yangu mmoja ambaye si ndugu yangu wa damu tulikuwa tukifanya kazi kama vibarua katika shughuli za uchimbaji wa madini kwenye migodi ya matajiri kule mtwara. Siku moja alikuja kijana mmoja ambaye ni mtoto wa mmiliki wa mgodi ambao tulikuwa tunafanya kazi siku hiyo. Alikuja kukagua kazi za baba yake jinsi zinavyokwenda. Siku hiyo aliingia ndani zaidi ya mgodi kwa bahati mbaya ikatokea ajali yule kijana akafunikwa na na kifusi. Ilikuwa ni siku ngumu sana kwake lakini mimi na ndugu yangu pamoja na wenzangu wengine wawili tuliweza kupambana na mwisho tukafanikiwa kumtoa yule kijana kwa haraka akakimbizwa hospitali. Baada ya kurudi nyumbani kwao Dar es salaam mzee wake yaani mmiliki wa ule mgodi alitupatia mimi na wenzangu mwaliko maalumu nyumbani kwake ili aweze kutoa shukrani kwa kazi kubwa tuliyoifanya kumokoa kijana wake. Lakini kabla tujaondoka alituuliza kama kuna mtu kati yetu ana akaunti ya benki, hakuna hata mmoja aliyekuwa nayo. Ilibidi mimi nifungue akaunti haraka kabla hatujaondoka, nilifanikiwa na mwisho mimi ndugu yangu na wenzangu wawili tulisafiri hadi jijini Dar es salaam tukafika hadi nyumbani kwa mzee, unajua nini kilitokea? ” Aliuliza Boaz, David na Dayana wakatamani kusikia zaidi.

“….Alituzawaidia pesa nyingi sana na zote zikawekwa kwenye akaunti niliyofungua kule Mtwara, akatutaka tugawane pasu kwa pasu. Aisee yule mzee alijua kutufurahisha, zilikuwa ni pesa nyingi mno. Kila mmoja akaona ameuaga umaskini, lakini kuna kauli inasema ng’ombe wa maskini hazai, ni kweli kabisa. Siku hiyo usiku tukiwa na furaha kubwa tulilewa sana na baadae tukawa tunarudi katika hoteli tuliyopangiwa kupumzika. Nakumbuka tulifika eneo moja lenye supermarket Fulani hivi kubwa MINI supermarket, ndugu yangu akaomba tumsubiri ajisaidie haja ndogo akazunguuka nyuma ya lile jengo. Tukiwa tunamsubiri pale nje ghafula inatokea gari ya hawa jamaa wakatuteka mimi na wenzangu na kutuleta huku, kwa bahati nzuri ndugu yangu yeye hawakumuona. Inauma sana, nimekaa huku kwa miaka mitatu mpaka sasa wenzangu watatu wote walishakufa nimebaki mimi na pesa zetu kwenye akaunti.” Boaz alimaliza kusimulia.

“pole sana Boaz”

“Asante Dayana, unajua kadi yangu ya benki alibaki nayo yule ndugu yangu,ilikuwa kwenye begi lake lakini kinachoniumiza hawezi kuzitoa zile pesa, ni mimi pekee ndio najua namba za siri. Angalau angekuwa anajua hizo namba za siri atoe pesa aendelee kumsaidia Mama na Sikujua ambao wote walikuwa wanatutegemea.”

“Sikujua ndio nani, mkeo?”

“Hapana ni mdogo wangu wa kike, alikatisha masomo yake kwa sababu ya kukosa pesa. Nilimuahidi siku moja nitamtafutia kazi nzuri na atakuwa na maisha mazuri, ni miaka mitatu mpaka sasa sijui hali yake”

“Usijali Boaz kuwa mtulivu, ipo namna ya kutoka hapa lakini inahitaji umakini wa hali ya juu” Alisema David

“Unasema kweli?”

“Ndiyo, nakuhakikishia tutatoka hapa na utakuwa huru, utatoa pesa zako na kumsaidia mdogo wako Sikujua” David aliongea kwa kumaanisha.
****

Usiku huo upande wa pili kijijini Nchingwea mkoani Mtwara, daladala moja ilisimama na akashuka binti mmoja aliyekuwa amevalia gauni la kijivu lililombana. Kichwani alivaa kofia yenye paa la duara iliyolegea. Mkononi alikuwa na mkoba mdogo wenye mikanda mirefu. Alishuka na kuanza kukatiza kwenye mitaa ya kijiji hicho kisicho na umeme. Huyu binti alikuwa ndiye Sikujua mwenyewe mdogo wake Boaz ambaye tumeona stori zake zikisimuliwa kule bondeni. Bonge

“Eeeh! Sikujua nilijua tu lazima utarudi kutoka mjini…” Ilikuwa ni sauti ya dada mmoja rafiki wa Sikujua ambaye walikutana akiwa karibu kufika nyumbani kwao.

“Mambo vipi…” Sikujua akasalimia

“Poa tu za huko town… eeh! Naona kaka yako Feisal kapata zari, kaja kutembelewa na mkuu wa mkoa hadi nyumbani kwenu na amepewa ofa ya kwenda kusoma Dar”

“Najua, tutaonana kesho” Sikujua alijibu kifupi kisha akaondoka zake kuelekea nyumbani.

Alifika na kabla ya kuingia ndani mlango ulifunguliwa ghafula uso kwa uso Sikujua akagonganisha macho yake na macho ya Feisal aliyekuwa anatoka.

IKO HIVI….
Yule ndugu asiye wa damu ambaye Boaz alikuwa akisimulia taarifa zake kule bondeni ni Feisal huyu aliyemuokoa Sasha kwenye mafuriko. Kwa kipindi kirefu Feisal na Boaz wameishi kama mtu na kaka yake mkoani Mtwara, na hawa ndio walioshiriki kumuokoa yule kijana aliyefunikwa na kifusi na baadae wakasafiri hadi Dar es salaam kwa tajiri mmliki wa mgodi ambaye aliwapatia fedha nyingi sana kama shukrani. Siku ile ya utekaji ni Feisal ndiye aliyewaomba wenzake wamsubiri na kisha yeye akazunguuka nyuma ya jengo la MINI supermarket kujisaidia, lakini anaporudi anakutana na tukio la wenzake kutekwa. Ni Feisal ndiye alinusurika kwenye utekaji huo huku kwenye begi lake akibaki na ile kadi ya benki ambayo hajui namba zake za siri mpaka hii leo.

SASA TUENDELEE…

“sikujua?” Feisal aliita kwa mshangao.

“Ndiyo, ni mimi…uko powa Feisal” Alijibu Sikujua, akapiga hatua kuingia ndani. Alipofika sebuleni anakutana na sura ngeni ya binti mzuri na mrembo Sasha. Bado alikuwa ndani ya nyumba hiyo, hakuondoka na msafara wa mkuu wa mkoa kama alivyosema.

“Habari yako dada” Sikujua alisalimia.

“Ni nzuri tu karibu”

“Asante karibu wewe. Mimi hapa ni mwenyeji…”

“Asante nimeshakaribia…”

“Pole kwa maafa yaliyowakuta…..” Alisema Sikujua akionekana tayari anataarifa juu ya kile kilichotokea siku hiyo. Wakati huo bado Feisal alikuwa amesimama pale mlangoni akiwa katika hali ya mshangao, hakutegemea kabisa ujio wa Sikujua usiku huo.

“Sikujua tunaweza kuongea kidogo…” Alisema Feisal

“Yes, bila shaka” Alijibu Sikujua kisha yeye na Feisal wakaongozana kuingia chumbani.

“Kabla ya yote inakuwaje huyu mwanamke bado yuko hapa nyumbani, kwani si umeshamsaidia inatosha?” Sikujua alikuwa ni wakwanza kuanzisha mazungumzo.

“Hilo sio la muhimu kwa sasa, naomba uniambie mama umemuacha wapi, yupo na nini?” Feisal naye akauliza swali badala ya kujibu swali.

“Mama yuko salama usijali”

“Umemuacha na nani usiku huu, mara ya mwisho nakumbuka ulinambia kuwa anaumwa”

“Hali yake sio mbaya sana na tulikuwa wote wakati taarifa zako zinatangazwa kwenye runinga, kafurahi sana kuona umepata bahati kubwa kama hiyo serikalini, hongera Feisal ”

“Asante…”

“Kwa hiyo vipi utaenda Dar?”

“Swali gani hilo unauliza?”

“Hamna nataka tu kujua”

“Nitaenda ndiyo, si umesikia nitajiunga na jeshi la zimamoto na uokoaji”

“Ooh! That’s why nimekuja usiku huu…”

“Una maana gani Sikujua?”

“About your promise Feisal, uliniahidi siku ukirudi Dar utaanza kazi ya kumtafuta kaka yangu Boaz”

“Nakumbuka, siwezi sahau hata siku moja. Iwe walimuua au yuko hai ila tambua lazima nitamtafuta popote alipo na hii ndiyo sababu kubwa nikubali kwenda Dar. Pamoja na kwamba naenda kusoma lakini jukumu langu namba moja litakuwa ni kutafuta Boaz.”

“Nafurahi kusikia hivyo Feisal, niliposikia umepewa ofa kwenda kusoma Dar es salaam sikutaka kupoteza muda nikaona nije haraka nikukumbushe na hili. Nimemkumbuka sana kaka yangu”

“Hata usijali Sikujua, wala hukuwa na haja ya kuja kunikumbusha…”

“Naomba ufanye hivyo Feisal…” Alisema Sikujua wakati huo simu yake ikawa inaita, akatoka nje kuipokea.

Feisal alibaki chumbani amesimama wima akionekana kuzama katika tafakuri nzito, kwa muda alijikuta anazisahau kabisa habari za mwanamke mrembo Sasha pale sebuleni.

Feisal aliinama akavuta sanduku moja chakavu lililokuwa chini ya uvungu wa kitanda, akapekuwa vitu vilivyo ndani yake, mwisho akachukua karatasi moja lililokuwa limekunjwa vizuri, akalikunjua. Ndani ya karatasi hilo kulikuwa na kadi ya benki. Ni ile kadi ya Boaz ambayo akaunti yake inapesa nyingi sana walizopewa na tajiri mmliki wa migodi kama shukrani.

“Nina imani bado uko hai Boaz, nakuja kukutafuta popote ulipo… Nitahakikisha nakurudisha nyumbani na kuwashikisha adabu wale wote waliohusika kukutenga na familia yako” Alisema Feisal, akavuta kumbukumbu zake siku ya tukio la utekaji wa Boaz na wale rafiki zake wengine pale MINI supermarket.

Wakati ule Feisal anarudi kujisaidia haja ndogo ndipo alipokutana na tukio hilo la ndugu zake ambao walikamatwa na watu wa ajabu waliovaa helmet kichwani zenye vioo vya rangi nyekundu. Feisal anakumbuka alijificha na kujibana ukutani kwenye kona ya ukuta akawa anachungulia na kushuhudia rafiki zake wakiingizwa ndani ya gari mmoja baada ya mwingine na kisha wale watekaji wakamaliza na kuingia ndani ya gari pia. Lakini mmoja kati yao alivua helmet yake kabla ya kuingia garini na hapo Feisal akafanikiwa kuiona sura ya mtu huyo.

Kama utakumbuka tukio hili la utekaji pale supermarket ya MINI lilirekodiwa pia na kamera za CCTV na mtu aliyevua helmet alikuwa si mwingine bali Felix mtoto wa Magnus. Pamoja na kwamba kundi la kigaidi MG Family lilifanikiwa kuiiba video ile iliyorekodiwa na kamera za CCTV kwa lengo la kupotea ushahidi lakini kumbe kuna mtu mwingine alikuwepo eneo la tukio na aliweza kuiona sura ya Felix na huyu si mwingine bali Feisal kaka yake David wanaeamini kuwa amekufa.

Katika harakati za kuanza kumtafuta Boaz, Feisal alijua hatua sahihi ya kuanzia ni kumtafuta yule jamaa (Felix) aliyefanikiwa kuiona sura yake siku ya utekaji. Alijua wazi kama atampata Felix basi ataweza kuwapata ndugu na rafiki zake. Lakini jambo ambalo Feisal hakujua ni kwamba kwa sasa Felix ni mtu anayeishi kwa jina na taarifa zake zote baada ya yeye kuaminika kwamba amekufa, na mbaya zaidi hata Mama David ameshinikizwa kumpokea Felix kama mwanae. Lakini vilevile hata Felix na kundi lake hawajui kama Feisal yupo hai na sasa amepata ofa ya kuja jijini Dar es salaam kimasomo.

Ni vita nyingine kati ya Felix na Feisal….
Wakati huo ndiyo kwanza Sasha anajitafuta namna ya kumpata kijana David aliyebeba hatima ya mji wa ajabu ISRA….
Lakini Sasha hajui kama tayari Magnus ameshaagiza watu kuja kumteka na kumpeleka kwenye himaya yake kule kisiwani…..
Felix naye anajitoa ufahamu na kurudisha penzi lake kwa Tesha bila kujali baba yake Magnus atachukua hatua gani…..
Tesha bado yuko gizani hamfahamu ki undani mpenzi wake Felix….
Madam Husnata naye yuko mbioni kuuwasha moto…
Lakini vipi hisia za kimapenzi kati ya Tesha na David ambao tuliona zinaanza kuchipua kati yao Je baada ya ujio wa Felix zitapotea?

Huu ni mwisho wa MSIMU WA PILI (season 2).
Karibu msimu wa tatu kujua zaidi nini kiliendelea katika mfululizo wa mkasa huu wenye matukio ya kusisimua.

MSIMU WA 3 UKO TAYARI NI TSH ELFU 1 TU LIPA KWA MPESA NAMBA 0756862047 KISHA NJOO WHATSAPP NAMBA HIYO HIYO
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

HAKI ZOTE ZIMEHIFADHIWA
 
Simulizi hii ni Tsh 1000 tu lipia kwa mpesa namba 0756862047 jina Saul au Airtel money namba 0788967317 jina Saul
Kisha njoo WhatsApp namba hzo hzo[emoji120]
 
Back
Top Bottom