Simulizi: Sasha Mlinzi wa Nafsi - 1

Simulizi: Sasha Mlinzi wa Nafsi - 1

Mtunzi wa hii story amefariki au yupo maana ni muda toka trh23!?
 
SASHA MLINZI WA NAFSI
SEASON 3
Sehemu ya........53
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA….
Uso kwa uso Magnus akawa anatazamana na mtoto wake ambaye sura yake alionyesha ni mtu mwenye hasira kali mno. Hali hii iliwashangaza hata wanafunzi wa Magnus wakawa hawaelewi ni nini hasa kinaendelea.

SASA ENDELEA…
Zilipita kama sekunde 30 za kutazamana kati ya Felix na baba yake Magnus, mwisho katika hali ya kushangaza Magnus alitabasamu kisha akawageukia wanafunzi wake na kuzungumza kwa sauti.

“MAPINDUZI YAFANYIKEEEEE……”

“KWA AJILI YA MAISHA BORA YA ISRA NA WATU WAKE….” Waliitika wanafunzi wa Magnus

“Naomba niwatambulishe kwenu kijana wangu, mwanangu wa pekee Felix Magnus, imekuwa bahati sana leo kaja kututembelea katika darasa letu nyakati kama hizi za usiku. Sio jambo la kawaida, mwanangu anayo majukumu mengi niliyompa lakini leo kajibana na hatimae kapata nafasi ya kuja kutuoa, naomba tumkaribishe kwa heshima tafadhali…..”

Wanafunzi wote wa Magnus waliinuka kwa pamoja huku wakimpigia Felix makofi kwa nguvu. Haraka Magnus alipiga hatua na kwenda kumkumbatia kijana wake Felix ambaye hadi dakika hiyo alikuwa katika hali ya kuduwaa akishangazwa na namna baba yake alivyopindisha mada. Si kweli kwamba Felix alikuwa hapo kwa lengo la kuwasalimia wanafunzi wa baba yake la hasha.

Baada ya Magnus kumkumbatia Felix mwanae, alisogeza mdomo wake karibu na sikio la Felix kisha akazungumza kwa sauti ya chini sana.

“Jitahidi kuficha hasira zako mbele ya wanafunzi wangu sitaki utengeneze taharuki yoyote humu, hawa ni watu wangu ambao wananiamini sana kwa hiyo jichunge la sivyo nitamfanya kitu kibaya Tesha.….” Aliongea Magnus huku akimalizia kwa mkwara mzito kisha akazidi kumkumbatia Felix kwa mahaba mazito kama baba wa kijana huyo. Hakuna mwanafunzi yeyote aliyeshtuka au kuhisi kuwa mambo hayakuwa sawa kati ya kijana na baba yake.
****

Upande wa pili nje ya kile kiwanda cha mbolea mambo yalikuwa yamepamba moto. Ni vita kali iliyokuwa ikiendelea kati ya Inspekta Brandina na Joshi Mahende kijana wa Felix. Awali kila mmoja alikuwa akimchukulia poa mwenzake lakini hadi dakika tatu zinakatika tayari kila mmoja alielewa anapambana na mtu asiye wa kawaida.
Inspekta Brandina ambaye amepitia mafunzo maalumu ya kijeshi licha ya mwili wake kuwa mkubwa lakini bado alikuwa ni mwepesi mno. Joshi Mahende naye si haba. Ingawa alijisifia sana na kujiita jeshi la mtu mmoja lakini leo alikutana na kitu cha tofauti.

Joshi Mahende alirusha ngumi na mateke mfululizo na kwa kasi sana lakini bado Inspekta Brandina aliweza kuhimili akikwepa akipangua na kujibu mapigo. Ilifika wakati wakajisahau kabisa kama wako eneo ambalo si salama kwao wote wawili, akili zao zote zikazama katika mpambano huo mkali huku safari hii uvumilivu ukimshinda bwana Joshi Mahende ambaye alichomoa kisu kutoka kiunoni mwake sasa akawa anamshambuli Inspekta Brandina kwa kutumia kisu hicho. Pamoja na hayo yote lakini bado mambo yalikuwa ni magumu kwao wote wawili hasa kwa Inspekta Brandina ambaye mpaka sasa tayari mikono yake ilikuwa imejeruhiwa baada ya kuchomwa na kisu mara kadhaa.

Baada ya mpambano mzito ambao ulidumu kwa zaidi ya dakika saba ghafula Joshi Mahende na Inspekta Brandina walijikuta wanawekwa chini ya ulinzi wakiwa wamezunguukwa na watu tisa wote wakiwa na bunduki mikononi mwao.

Lilikuwa ni tukio la kushtukiza mno yaani kufumba na kufumbua tayari walijikuta wako katikati ya watu wenye silaha, si Inspekta Brandina wala Joshi Mahende aliyetegeme.
Ni wazi walijisahauna mwisho waliweza kuonekana na watu hao ambao walitengeneza mtego wakawanasa kwa urahisi sana. Hawa walikuwa si wengine bali vijana wa Magnus ambao wapo kwenye jukumu zito la kumlinda binti mrembo Tesha. Vijana hao walikuwa ni wengi mno, ni kama Magnus alijua kuwa lolote linaweza kutokea hivyo akaagiza ulinzi uwepo wa kutosha kwani anaijua jeuri ya mtoto wake Felix pengine angeweza kufanya kitu kujaribu kumuokoa mpenzi wake Tesha. Na kweli ndivyo ilivyokuwa, Felix akamuagiza kijana wake wa kazi Joshi Mahende.

“Mikono juu… nasema wote mikono juu, ukijaribu kujitikisa hata kidogo nakumwaga ubongo…” Alitoa amri mmoja wa wale vijana ambaye alionekana kuwa kiongozi wa wengine. Haraka Inspekta Brandina na Joshi Mahende wakatii na kunyoosha mikono yao juu, hawakuwa na ujanja wowote. Wakati huo huo geti kuu la kiwanda hicho likafunguliwa, wakatoka watu wengine wanne nao wakiwa na silaha vilevile.

“Ninyi ni akina nani? Inakuwaje mmetoka kote huko mmekuja kupigania hapa? Mnataka nini?”

Aliuliza yule bwana, Inspekta Brandina na Joshi Mahende wakatazamana hakuna aliyekuwa na uwezo wa kujibu swali lile.

“Wakamateni mkawafungie.…watajibu tu” Alitoa amri na hapo Inspekta Brandina na Joshi Mahende walikamatwa na kuanza kukokotwa kuelekea ndani kiwandani.

Walivuka geti na sasa wakawa wanalielekea jengo moja dogo kati ya majengo mengi yanayounda kiwanda hicho. Inspekta Brandina hakuonekana kuwa na wasiwasi sana aliamini mda si mrefu askari wenzake aliowapa taarifa watafika eneo hilo kutoa msaada.

Wakati wakiukaribia mlango wa lile jengo ghafula kwa kasi sana Joshi Mahende alimgeuza moja kati ya vijana waliokuwa wamemshika akampora silaha akasimama nyuma yake na kumuwekea silaha hiyo kichwani kwa kutumia mkono wake wa kulia na mkono wa kushoto akawa amemkaba kijana huyo shingoni. Lilikuwa ni tukio la haraka sana, ni mtu pekee mwenye mafunzo na uzoefu wa kutosha ndiye angeweza kufanya kile alichokifanya Joshi Mahende ndani ya sekunde zile chache. Tangu akamatwe akili yake ilikuwa ikiwaza ni namna gani atajinasua kutoka kwenye mikono ya watu hao, na ndipo hapo alipopata wazo akawa anasubiri wakati ambao vijana waliomshika watazembea, na wakati ulipofika hapo ndipo Joshi Mahende alipopata mwanya wa kumgeuza kwa nguvu yule kijana, akampora silaha na kisha kumkaba shingoni sawa sawa.

“Rudi nyuma wote, atakae jaribu kusogea karibu basi namuua huyu mwenzenu…” Joshi Mahende alizungumza huku akiwa makini sana, akawa amemuweka yule kijana mbele kama kinga yake kuzuia asije akapigwa risasi.
Taratibu Joshi Mahende akiwa na mateka wake akaanza kurudi nyuma kuelekea getini walipotoka. Wale vijana wengine nao walianza kupiga hatua taratibu kumfuata huku nao wakiwa wamenyoosha silaha zao mbele, hawakujua nini wafanye kuzuia Joshi Mahende asikimbie. Wakawa wanasubiri amri ya mkubwa wao ambaye naye alikuwa katika hali ya bumbuazi, kwa bahati mbaya mtu aliyeshikiliwa na Joshi Mahende alikuwa ni muhimu sana kwake.

Inspekta Brandina ambaye yeye alibaki akilindwa na vijana wawili pekee wenye silaha, hakutaka kufanya lolote akawa anashuhudia tu kwa macho kile kinachoendelea, akili yake kubwa alikuwa akiwaza namna atakavyoweza kumuokoa Tesha akiwa na uhakika yuko mrembo huyo kafungiwa ndani ya jengo moja wapo katika ya majengo mengi ya kiwanda hicho.

Hadi Joshi Mahende na mateka wake wanafika getini bado hakuna kitu kilichofanywa na wale vijana zaidi ya kuendelea kumfuata taratibu.

“Mmoja aje afungue geti hapa….” Joshi Mahende alitoa amri, wale vijana wakawa wanatazamana na mwisho wakageuka kumtazama mkubwa wao, naye pia akawa kimya.

“Nitamuacha mwenzenu akiwa hai kama nitaondoka hapa salama” Joshi Mahende alisisitiza na hatimae amri ikatolewa kijana mmoja akasogea mbele na kufungua geti dogo la katikati.

“Rudi kule na asisogee mtu mwingine” Alisema Joshi Mahende akimuamrisha yule kijana aliyefungua geti akarudi kusimama walipo wenzake. Baada ya hapo Joshi Mahende alitoka nje akiwa na yule mateka wake kisha geti likafungwa.

Wale vijana pamoja na mkubwa wao walibaki wametulia kwa muda wakitii maelezo ya Joshi Mahende kwa ajili ya usalama wa mwenzao. Dakika moja baadae walisikia milio ya risasi mbili zikifyatuliwa mfululizo, hapo uvumilivu uliwashinda wakafungua geti na kutoka nje haraka. Walipofika walimuona mwenzao akigaagaa chini kwa maumivu makali. Alikuwa amepigwa risasi mbili zote katika miguu yake, kulia na kushoto, wakati huo Joshi Mahende hakuwepo tayari alishaondoka kitambo sana.

“Anko, anko P….” Alisema yule kiongozi huku akikimbia kumuwahi mwenzao pale chini, alikuwa ni ndugu kwake na ndiyo maana alitii maelezo yote ya Joshi Mahende kwa ajili ya usalama wa mjomba wake.

“Mnyanyueni mpelekeni ndani….. nitakutafuta wewe mwana haramu nasemajeee…nitakutafuta” Yule bwana alizidi kufuko kwa sauti.
*****

Upande wa pili baada ya ujio wa Felix ilimbidi Magnus ahairishe darasa lake usiku huo, akaondoka na mwanae kwa ajili ya kwenda kuzungumza naye amueleze sababu hasa za yeye kumtaka arejee nyumbani.

Felix na Magnus waliingia katika chumba kimoja kidogo, ingawa kulikuwa na viti lakini hakuna aliyekaa wote wakawa wamesimama wima wakitazamana kwa macho makali mithiri ya mbogo. Wakati huo wote simu ya Felix ilikuwa ikiita mfululizo lakini hakuwa na nafasi ya kuipokea, jambo muhimu kwa wakati huu ilikuwa ni kuongea na baba yake.

Kabla hawajaanza mazungumzo mara yule msaidizi wa kazi wa Magnus alibisha hodi na kuingia, akapitiliza moja kwa moja hadi kwa Magnus akaongea naye kwa sauti ya chini ambayo Felix hakusikia.

“Mkuu kule kiwanda cha mbolea alipoagiza Tesha akahifadhiwe kuna tatizo kidogo, kuna uvamizi umetokea lakini wameweza kuwadhibiti, kwa bahati mbaya pia kuna kijana wetu mmoja kajeruhiwa kwa kupigwa risasi…”

“Vipi kuhusu Tesha ..?”

“Yupo, bado wako naye…”

“Nataka ahamishwe hapo mara moja, sitaki uzembe…”

“Sawa mkuu…” Alijibu kwa unyenyekevu mkubwa wakati wakiendelea na mazungumzo hayo Felix naye alipata mwanya wa kuitazama simu yake, akagundua aliyekuwa akipiga simu wakati wote ni kijana wake wa kazi Joshi Mahende. Lakini pia alikuwa ametuma ujumbe wa maandishi, Felix akaufungua na kuusoma haraka haraka, uliandikwa hivi…

……………Boss sijafanikiwa kumchukua Tesha ulinzi ni mkali sana, mambo hayajakwenda vizuri lakini nakuahidi kumpata haraka sana kabla hakujapambazuka……………

Felix alimaliza kuusoma ujumbe huo kisha akauma meno yake kwa hasira, akainua uso wake kumtazama baba yake Magnus ambaye ni chanzo cha hayo yote, naye wakati huo akawa anamtazama wakatazamana.
Tayari Magnus ameshaagiza Tesha ahamishwe wakati huo Joshi Mahende anamuahidi Felix kwamba atampata Tesha kabla hakujapambazuka, vipi kuhusu Inspekta Brandina? Magnus ataongea nini na mwanae?

ITAENDELEA…
0756862047
 
SASHA MLINZI WA NAFSI
SEASON 3
Sehemu ya.........54
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA….
Tayari Magnus ameshaagiza Tesha ahamishwe kutoka katiika kiwanda cha mbolea wakati huo Joshi Mahende anamuahidi Felix kwamba atampata Tesha kabla hakujapambazuka, vipi kuhusu Inspekta Brandina? Magnus ataongea nini na mwanae?

SASA ENDELEA…

Felix alimaliza kuusoma ujumbe kutoka kwa Joshi Mahende kisha akauma meno yake kwa hasira, akainua uso wake kumtazama baba yake Magnus ambaye ni chanzo cha hayo yote, naye wakati huo akawa anamtazama wakatazamana.

“Yuko wapi Tesha wangu baba?” Aliuliza Felix huku akipiga hatua na kusimama mbele ya baba yake kibabe mno.

“Huwezi kupambana na mimi Felix, nimewahi kuliona jua kabla yako. Bila shaka wewe ndio umewatuma watu kujaribu kumuokoa mpenzi wako si ndiyo? Vipi wameshakupa matokeo ya kilichotokea?” Aliuliza Magnus huku akionekana kutotishwa hata chembe na mikwara ya mwanae ambaye alikuwa amesimama mbele yake akijaribu kujitunisha.

“Nauliza yuko wapi TESHAAAAA….?” Felix aliuliza tena kwa mara ya pili safari hii akipaza sauti zaidi ya mwanzo.

“Ooh! Cool down my Son, unajua leo umeniaibisha sana Felix, vipi unajua hilo…kama umeniaibisha leo?” Aliuliza Magnus na kumkata jicho kali mwanae, Felix akawa kimya, Magnus akaendelea kuzungumza….

“Inawezekanaje mwanadamu wa kawaida kabisa akasimama mbele yako akakuzidi nguvu na kuchukua kitu unachokipenda kutoka kwenye mikono yako. Felix hivi ni kweli ulikuwepo wakati Tesha anatekwa au nimepewa maelezo tofauti?. Kitu ambacho hujui ni kwamba wanadamu ni viumbe dhaifu sana kwetu, ulikuwa na uwezo wa kuwafinyanga wote kwa pamoja kwenye kiganja cha mkono wako kama vile unafinyanga karatasi. Lakini wewe umeshindwa kufanya hivyo umewaacha wakaondoka na Tesha.… hujui chochote kuhusu nguvu kubwa iliyopo ndani yako, hujui chochote kuhusu nguvu tuliyonayo sisi watu kutoka ISRA” Magnus aliongea kwa ukali kiasi, akakatishwa na sauti ya Felix ambaye naye alimjia juu baba yake…

“Nyamaza wewe mzee, stori zako ni hizo hizo kila siku, hujawahi badilika. Nilisha kwambia sitaki kusikia chochote kuhusu hiyo ISRA baba, sitaki kwenda huko. Alafu nashangaa kitu kimoja nikiwa mdogo uliwahi kuniambia watu wa ISRA ni WALINZI WA NAFSI za binadamu si ndiyo? Unakumbuka?. Sasa inakuwaje tena leo unanieleza kitu tofuati, eti naweza kuwafinyanga kama karatasi kivipi yani eeh! nambie basi niamini nini?…Hawa binadamu mnazilinda nafsi zao au mnawafinyanga kama karatasi. Kama ni kulinda nafsi zao vipi kuhusu wale mateka ambao wanashinda uchi kule bondeni, umewaweka wa kazi gani? Tuseme ndio unalinda nafsi zao au ndio unawafinyanga?... Baba binafsi siwezi kukuamini hata kidogo yaani hata chembe ya imani sina kabisa kwako….”

“Felix ungetaka kujua hayo yote ungekaa nyumbani utulie na baba yako nikufunze kila kitu, nikupe siri zote za duniani na siri za ISRA, unazo nguvu lakini huwezi kuzitumia. Tangu ukiwa mdogo ulichangua kukaa mbali na mimi…”

“Ndiyoo… nilifanya maamuzi sahihi kwa sababu mimi sio kama ninyi, mimi siwezi kuwa kama wewe baba, wewe ni muuaji unaroho ya kikatili sijapata kuona” Felix akazidi kufoka.

“Pamoja na kuwa na roho hiyo mbaya unayoisema lakini sijaifikia hata chembe ya roho mbaya waliyonayo watu wa ISRA. Walitufukuza bila huruma na kutunyang’anya kila tulichonacho, huwezi kuhisi maumivu makali niliyopitia mimi baba yako kipindi hicho wewe ulikuwa ni mdogo sana Felix hujui kitu...”

“Basi kama sikuwepo sihusiki, usiniingize kwenye mipango yako baba niache niwe huru…”

“Uhuru gani unaouzungumzia hapo Felix, mkataa kwao ni mtumwa, huko unakokung’ang’ania siku zote sio kwenu ni utumwani, rudi nyumbani kwa baba yako. Hayo maisha yanayokufanya ukimbie kwenu ipo siku yatakugeuka na kukufanya vibaya….”

“Hapana Mzee, niliondoka kwako sio kwa sababu kuna maisha niliyatamani nje hapana, ila ni kwa sababu yako wewe. Siwezi kuishi hapa na kushuhudia mambo ya ajabu unayoyafanya kila kukicha…”

“Unauhakika hiyo ndiyo sababu pekee iliyokutoa hapa Felix?”

“Ndiyo hakuna kingine…”

“Sio kweli, sababu ya wewe kukaa mbali na mimi naijua”

“ipi…?”

“ni tangu siku ulipoonja penzi la mwanadamu ndipo ukaamua kunikimbia baba yako…” Magnus alitoa kauli tata iliyomfanya Felix atoe macho kwa mshangao…

“Unashangaa nini, unafikiri sijui chanzo cha wewe kutoka hapa? Najua kila kitu Felix… yule Madam Husnata ndiye aliyekulaghai tangu ukiwa ni kijana mdogo, ulifanya naye mapenzi, akanogewa, akaanza kukutoa nje ya hichi kisiwa mkawa mnakutaka huko kwa siri, ukawa hutamani tena kurudi huku, akaendelea kukutumia kumaliza hamu zake na wewe bila kujua ukaendelea kumsikiliza na kutumika. Hukuwa unampenda Madam Husnata. Yeye alikupenda kwa sababu ya kitu cha tofauti kilichopo ndani ya mwili wako Felix. Ulikuwa ni kijana mdogo mno tena mno, ungewezaje kumridhisha mama mtu mzima kama yule. Hivi huwa huwazi ni kwa nini? Hujui ni kwa nini Madam Husnata anakung’ang’ania hadi leo licha ya kwamba amejua unampenda sana Tesha? Ni kwa sababu aliona kitu cha tofauti kwako Felix, wewe sio kama wao….”

Maelezo hayo ya Magnus yalimfanya Felix atazame chini kwa aibu, hakuwa anategemea kama baba yake anaijua siri hii, siri ya yeye kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Madam Husnata tangu akiwa ni mdogo. Ni kweli kuwa Madam Husnata ndiye aliyemuonyesha Felix upande wa pili wa dunia akamtoa katika kisiwa cha baba yake na hapo ndipo Felix akajikuta anayatamani maisha haya mapya akatamani kuishi kama waishivyo watu wengine aliowakuta huko. Taratibu Felix akaanza kuikataa mipango ya baba yake Magnus. Kwa msaada wa Madam Husnata Felix akaanza kujitengenezea maisha yake mbali na baba yake, akiwa katika harakati hizo ndipo siku moja akakutana na Tesha akampenda wakapendana bila Madam Husnata kujua. Hii ndiyo sababu Madam Husnata anayo jeuri kubwa mbele ya Felix, hawa ni wapenzi wa muda mrefu sana licha ya Madam Husnata kumzidi umri kwa kiasi kikubwa lakini wala hakujali mama wa watu, alichokuwa anakipata kutoka kwa kijana huyu alikithamini kuliko kitu kingine chochote.

“Sasa kama baba anajua hili tangu mda, kwa nini alikaa kimya? kwa nini ameendelea kufanya kazi na Husnata hadi kumpa cheo kikubwa cha uongozi wa MG Family?” Felix aliwaza akijiuliza maswali ambayo hakuwa na majibu yake. Bado alimuona Magnus kama mtu wa ajabu sana kwake.

“Kama unataka mpenzi wako aendelee kubaki hai basi lazima unisikilize mimi kuanzia sasa…” Magnus aliongea kwa msisitizo. Felix akawa kimya, hakuwa na chaguo lingine zaidi ya kukubali kusikiliza baba yake anataka nini. Awali alimuamini sana kijana wake wa kazi Joshi Mahende lakini mpaka sasa kulikuwa na kila dalili kuwa Joshi Mahende hatofanikiwa kumtoa Tesha mikononi mwa watu wa Magnus usiku huo hivyo ikabidi awe mpole.

Baada ya Magnus kuona sasa Felix yuko tayari kumsikiliza alimuita mlinzi wake mmoja na kumuagiza amuite Kareem. Mmoja kati ya viongozi wakubwa wa kundi lake la kigaidi MG Family. Muda mfupi baadae Kareem akaingia na kusimama pembeni ya Felix. Sasa wakawa tayari kumsikiliza Magnus mzee mwenye mipango mikubwa.

Magnus alipiga hatua kadhaa akasogea karibu na ukuta wa chumba hicho, akafunua pazia lililokuwa mbele yake. Nyuma ya pazia hilo kilionekana kioo kikubwa sana cha runinga, Magnus akaiwasha runinga hiyo kwa kutumia rimoti iliyokuwa tayari mkononi mwake. Picha ya binti mmoja mrembo sana ikajitokeza kwenye kioo cha runinga hiyo. Alikuwa ni binti mrembo mno mwenye sura na umbo la kuvutia. Felix alijikuta anatoa macho kwa mshangao, pengine tangu kuzaliwa kwake hakuwahi kumtia machoni mwanamke mwenye mvuto wa aina hiyo. Ilikuwa ni picha ya Sasha.

Ni kweli kabisa Sasha alikuwa binti wa kipekee sana, kila kitu kwake kilikuwa cha kipekee, kuanzia rangi ya ngozi yake yenye mvuto, macho yake makubwa ambayo akikuangalia utatamani asiache, muonekano wake kuanzia juu hadi chini ulitosha kabisa kumfanya kila mwanaume atakayebahatika kupishana naye asisite kugeuka na kumtazama kwa mara ya pili.
Magnus alitabasamu baada ya kumuona kijana wake akiitazama picha ya Sasha kwa zaidi ya sekunde 60 bila kupepesa macho yake.

“Huyu binti anaitwa Sasha, ni mtoto wa mkuu wa ISRA amefanya makosa siku za hivi karibuni na sasa kafukuzwa na kutupwa nje ya ISRA kama walivyotufanyia sisi miaka mingi iliyopita, hivi ninavyoongea huyu binti yupo mkoani Mtwara. Kwa hiyo basi Felix kesho utaungana pamoja na kikosi cha Kareem na watu wake mtaenda kumtafuta Sasha na kumleta huku kisiwani, hii ndio kazi pekee niliyokuitia hapa, na unalazimika kuifanya pasipo kupinga kwa ajili ya usalama wa mpenzi wako Tesha…” Magnus alieleza, ukimya ulitawala kwa sekunde kadhaa kisha akaendela kuongea…

“Kazi inaweza isiwe nyepesi kama mnavyodhani, huyu ni binti mpendwa wa Mkuu wa ISRA Gu Gamilo nina uhakika hawezi kumuacha mwenyewe lazima atampa ulinzi. Kwa hiyo chukueni kikosi maalumu chenye silaha za kutosha ikiwemo ving’ora kwa tahadhali zaidi…Tumeelewana?”

“Tumeelewa mkuu” Alijibu Kareem lakini Felix akawa kimya.

“Felix mbona hujibu shida nini? Au habari za wewe na Madam Husnata zimekuchanganya, usijali kama utaifanya kazi yangu vizuri sitomfanya kitu Tesha wala sitomgusa Madam Husnata…” Alieleza Magnus huku akipiga hatua kusogea mbele karibu na mwanae Felix, akamshika begani.

Ni wazi kuwa hizi zilikuwa ni jitihada za makusudi za kumuunganisha Felix na Sasha kama ambavyo mzee huyu mwenye kuona mbali aliahidi. Hakukuwa na sababu yoyote ya kumuunganisha Felix kwenye kikosi kinachoenda kumteka Sasha lakini Magnus anafanya hivi kwa makusudi ili kuanza kutengeneza ukaribu kati ya Sasha na Felix. Na tayari alishaanza kuamini mpango wake kufanya kazi baada ya kuyaona macho ya Felix wakati akiitazama picha ya Sasha katika runinga.

JE, NINI KITAFUATA?

ITAENDELEA….
 
SASHA MLINZI WA NAFSI
SEASON 3
Sehemu ya.........55
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA...
Magnus hakukuwa na sababu yoyote ya kumuunganisha Felix kwenye kikosi kinachoenda kumteka Sasha lakini Magnus anafanya hivi kwa makusudi ili kuanza kutengeneza ukaribu kati ya Sasha na Felix. Na tayari alishaanza kuamini mpango wake kufanya kazi baada ya kuyaona macho ya Felix wakati akiitazama picha ya Sasha katika runinga.

SASA ENDELEA...
"Kareem" Magnus aliita

“Nakusikiliza mkuu…”

"Vipi unahitaji kikosi cha watu wangapi ili kuifanya hii kazi..?"

"Aah… saba tu wanatosha mkuu, Felix atakuwa ni wa nane, ninao vijana wengine wapya watatu tayari wamefuzu mafunzo ya kupambana na watu kutoka ISRA nataka niwaunganishe pia wawe sehemu ya kikosi kitakachoenda Mtwara kumteka Sasha" Alieleza Kareem

"Sawa vizuri, kama nilivyoeleza hapo mwanzo kuwa Sasha ni binti anayependwa sana na baba yake Gu Gamilo, licha ya kwamba Sasha hana nguvu zozote kwa sasa lakini lazima Gu Gamilo atamuwekea ulinzi wa kutosha akiwa nje ya ISRA, mnatakiwa muwe makini saana" Magnus aliendelea kusisitiza, Kareem akamuhakikishia kuwa kila kitu kitakwenda sawa na lazima watamleta Sasha mikononi mwake kama alivyo agiza.
Mwisho baada ya mazungumzo hayo muhimu Kareem na Felix walianza kuondoka tayari kwa ajili ya kwenda kupanga mbinu na mikakati ya kuiendesha misheni hiyo. Kabla hawajatoka Kareem alikumbuka jambo akageuka haraka na kumuuliza Magnus.

"Samahani mkuu hawa vijana wapya niliowaleta leo hawana yale mavazi na vifaa maalumu tunavyotumia siku zote kwenye hizi kazi......"

"Unamaanisha helmet…?”

“Ndiyo mkuu lakini sio helmet pekee hata nguo na zile silaha hawana pia” Alieleza Kareem

”Sawa, angalieni kwenye chumba cha mizigo iliyoingia leo na meli kila kitu kipo mle..." Magnus alijibu.
Sasa hatari ilihamia tena kwa kijana David ambaye kama utakumbuka kwa mara ya mwisho David alifungiwa katika chumba chenye mizigo hiyo anayoizungumzia Magnus wakati huu.
Dakika tano baadae Kareem, Felix pamoja na kikosi maalumu kilichoandaliwa kwa kazi hiyo walionekana wakipiga hatua kuelekea katika chumba ilipoifadhiwa mizigo iliyoletwa na meli usiku huo. Huu ulikuwa ni usiku wenye shamra shamra nyingi ndani ya kisiwa cha Magnus.

Katika chumba walichokuwa wakielekea Kareem na timu yake ni chumba hicho hicho ambacho David alikuwemo. Hakuwa ametokea hadi dakika hii tangu pale mlango ulipofungwa kwa nje na yeye akabaki ndani. David aliposikia vishindo vya watu wanakuja haraka alikimbia na kwenda kujifungia tena katika lile lile sanduku alilojificha awali. Sekunde chache baadae alisikia mlango ukifunguliwa na mara akasikia vishindo vya watu ziaidi ya mmoja wakiingia ndani ya chumba hicho. Safari hii David aligeukia upande wa pili wa lile sanduku hivyo hakuweza kuziona sura za watu hao isipokuwa aliweza kuzisikia sauti zao vizuri wakati wakizungumza..

"Kesho asubuhi na mapema tutatoka hapa tukiwa tumeshajiandaa tayari kwa kila kitu, tutarudi kambi kuu ya MG Family na baada ya hapo tutaanza safari kuelekea Mtwara. Kazi yetu ni moja kuhakikisha tunamleta yule mwanamke hapa kwa bosi." Kareem alikuwa akitoa maelezo kwa vijana wake akiwemo Felix, maelezo haya pia David alikuwa aliyasikia kwa uzuri sana. Kareem akaendelea kuzungumza...

".... Kazi inaweza ikawa ni nyepesi lakini pia inaweza ikawa ngumu kama tu tukikutana na maadui kutoka ISRA, nadhani kila mtu hapa anaelewa nikisema maadui kutoka ISRA nakuwa nazungumzia watu gani. Tayari sote tunajua namna ya kupambana nao. Nawakumbusha tu kuwa udhaifu mkubwa wa watu au viumbe kutoka ISRA ni ile sauti ya king'ora inawafanya kukosa nguvu kabisa na hapo tunaweza kuwadhibiti kwa urahisi. Kila mtu anavyo vifaa isipokuwa ninyi watatu pamoja na Felix, ninawapatia sasa hivi...."
Baada ya kusema hivyo Kareem alianza kupekuwa mizigo iliyoletwa usiku huo mmoja baada ya mwingine. Akawa anatoa vifaa muhimu vinavyohitajika. Hofu ikazidi kumjaa David akiamini sasa anakwenda kukamatwa kama tu Kareem atafungua sanduku alilojificha ndani yake.
Mwisho ni kweli Kareem akawa analielekea lile sanduku ambalo ndani yake alikuwamo kijana David, hofu ikazidi kumjaa.

"Kama safari ni kesho kuna ulazima gani wa kutupatia hivyo vitu sasa hivi bwana Kareem, kwa nini tusifanye kesho asubuhi..." Felix alitoa wazo ambalo Kareem hakuwa na pingamizi nalo, akamuheshimu kama mtoto wa bosi.

"sawa tutaondoka hapa saa 12 alfajiri kila mtu atajiandaa kwa wakati wake, muhimu huo mda wote tuwe tayari kuondoka..." Alisema Kareem na wote wakakubaliana hivyo.
Hii ikawa ni bahati kubwa sana kwa David ambaye bado aliendelea kuwa salama salmini ndani ya lile sanduku.
Mwisho Kareem na wenzake wote waliondoka kurudi katika sehemu zao za kupumzika ili asubuhi waamke kuifanya kazi hiyo.
Mlango ulifungwa kwa nje, ni kwa mara nyingine tena David anabaki ndani ya chumba hicho akiwa hana mahala pa kutokea, bado hali ilikuwa ni ngumu sana kwake. Hakujua ni vipi ataweza kutoka nje ya chumba hicho lakini pia kutoka katika himaya ya Magnus pasipo kukamatwa. Aliogopa huenda kilichomtokea rafiki yake Zungu kinaweza kumtokea na yeye pia.

Alifungua lile sanduku akatoka, akasogea hadi mlangoni akajaribu kuutikisa kidogo kuhakikisha kama kweli umefungwa, jibu lilikuwa ni ndiyo, mlango wa chumba cha mizigo ulikuwa umefungwa kwa nje.

"Utatoka tu David, utatoka...." David alijisemea mwenyewe huku akijipiga piga kifuani kujaribu kujifariji.
[emoji294][emoji294][emoji294]

Upande wa pili baada ya Joshi Mahende kufanikiwa kutoka kwenye mikono ya vijana wa Magnus kule katika kiwanda cha mbolea mtihani ulibaki kwa Inspekta Brandina ambaye yeye hakutaka kuleta usumbufu wowote kwa vijana hao lengo ikiwa ni kutambua mahali alipo Tesha.
Ni kweli lengo lake lilitimia baada ya muda mfupi kwani wale vijana walimchukua na baada ya kumnyang’anya kila kitu alichonacho wakamuingiza ndani ya chumba kimoja kipana na chakavu sana. Ni chumba hicho hicho ndicho alichokuwa amehifadhiwa mwanadada Tesha mara baada ya kutekwa.

Tesha akiwa amejikunyata kwenye kona moja ya chumba hicho alishtushwa na sauti ya mlango uliofunguliwa kwa nguvu sana. Haraka alisimama hali akionekana kuwa na wasiwasi mwingi, aliogopa sana akihisi watu hao ambao si wema kwake wanaweza kumfanyia kitu kibaya kama kumuua au laa hata kumbaka. Baada ya Tesha kusimama ndipo hapo aliposhuhudia mwanamke mwingine akisukumwa kwa nguvu kuingizwa ndani ya chumba hicho na baadae mlango ukafungwa tena, alipomtazama vizuri mwanamke huyo Tesha alipigwa na butwaa.

“Afande Brandina..!!”

“Ndiyo ni mimi Tesha, pole…”

“Imekuwaje na wewe wamekuleta hapa…?”

“Nimekuja hapa kukusaidia usijali kila kitu kitakuwa sawa baada ya muda mfupi…”

“Kweli afande… asante sana, asante mno…” Tesha alishukuru huku akisogea na kumkumbatia Inspekta Brandina kwa nguvu, angalau alipata faraja sasa baada ya kutawaliwa na hofu kwa zaidi ya masaa matatu tangu alipotekwa. Kimya kilitawala kwa zaidi ya sekunde 30 wakiwa bado wamekumbatiana. Mwisho Tesha akamuachia Inspekta Brandina na kumuuliza swali.

“Sasa utawezaje kunisaidia? Mbona na wewe wamekufungia humu kama mimi?”

“Usijali Tesha sio mda kuna askari watafika hapa kutusaidia nimesha….” Alisema Inspekta Brandina lakini kabla hajaikamilisha sentesi yake ghafula kwa mara nyingine tena mlango ukafunguliwa kwa nguvu, wakaingia vijana zaidi ya sita wakiwa na siraha mikononi mwao. Bila hata kuuliza waliwakamata Tesha na Inspekta Brandina wakawabeba msobe msobe na kutoka nao hadi nje kabisa ya jengo hilo. Tayari kuna gari (Kenta) lilikuwa likiwasubiri pale nje, Tesha na Inspekta Brandina wakaingizwa ndani ya gari hilo. Hawakujua ni nini hasa kinaendelea lakini baada ya kusikia maneno ya kiongozi wa vijana hao akiwasiliana na mkubwa wake wa kazi ndipo wakaelewa...

“….Sawa bosi hivi ndio tunaanza kuondoka, tunahamisha kila kitu kama ulivyosema….sawa bosi…tuko makini usijali….” Alisema kiongozi huyo.

“Shiiiit! Wanatuhamisha?” Inspekta Brandina alizungumza kwa sauti ya chini huku akikasirishwa na kitendo cha askari wenzake kushindwa kufika mapema kwa wakati.

"Tunafanyaje Afande..." Tesha aliuliza kwa hofu

"Tutajua cha kufanya kuwa mtulivu Tesha" Alijibu Inspekta Brandina akawa anapiga jicho la kuibia akijaribu kuwatazama vijana wa Magnus ambao walikuwa wamesimama na kuwazunguka kila upande huku wengine wakining'inia kwenye bomba za gari hilo.

Dakika 5 baadae msafara wa gari tatu likiwemo lile walilopakizwa Inspekta Brandina na Tesha ulianza safari kuelekea kusikojulikana vijana wakitekeleza agizo maalumu kutoka kwa Magnus ambaye aliwataka wahame mara moja eneo hilo.
Muda mfupi baada ya msafara huo kuondoka ndipo gari za polisi zisizopungua sita zilifika katika kiwanda hicho cha mbolea huku askari wakiwa wamejipanga kikamilifu kukabiliana na waharifu ambao waliamini bado wapo eneo hilo kama walivyotalifiwa na Inspekta Brandina. Baada ya kufanya upekuzi kwa zaidi ya dakika 15 ndipo walipogundua kuwa hakukuwa na mtu yeyote kiwandani hapo, walichelewa. Na mbaya zaidi simu ya Inspekta Brandina haikupatikana.

ITAENDELEA….
Simulizi hii ni Tsh 1000 tu lipia kwa mpesa namba 0756862047 jina Saul au Airtel money namba 0788967317 jina Saul
Kisha njoo WhatsApp namba hzo hzo
 
SASHA MLINZI WA NAFSI
SEASON 3
Sehemu ya.........56 -57
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA...
Baada ya polisi kufanya upekuzi kwa zaidi ya dakika 15 ndipo walipogundua kuwa hakukuwa na mtu yeyote kiwandani hapo, walichelewa. Na mbaya zaidi simu ya Inspekta Brandina haikupatikana...

SASA ENDELEA....
Usiku huo msafara wa gari tatu pamoja na lile lililo wabeba Inspekta Brandina pamoja na Tesha uliendelea kuchanja mbuga kwa kasi ukipita katika ya msitu mnene, mwisho waliacha barabara ile ya vumbi inayotoka kule kiwandani na sasa wakaingia katika barabara ya rami wakazidi kusonga mbele kwa kasi kuelekea kusikojulikana. Matumaini ya kuokolewa yalizidi kufifia, hata Inspekta Brandina mwenyewe ambaye awali alikuwa akijiamini sana taratibu akaanza kuingiwa na hofu, hali ilikuwa ni mbaya zaidi kwa mwanadada Tesha aliogopa mno
****

KISIWANI- NDANI YA HIMAYA YA MAGNUS

Baada ya Kareem na kikosi chake kutoka katika kile chumba cha kuhifadhia mizigo kila mmoja alitawanyika kuelekea upande wake katika chumba ambacho alichagua kupumzika usiku huo ndani ya himaya ya Magnus mpaka pale muda wa kuondoka alfajiri na mapema utakapowadia.

Felix yeye alipanda juu kabisa ghorofani katika jengo moja kubwa la kifahari sana, huko ndipo kilipokuwepo chumba chake cha kulala alichokuwa akikitumia siku zote tangu akiwa ni mdogo.

Alifungua mlango na kuingia ndani, kilikuwa ni chumba kikubwa mno kizuri chenye vitanda viwili pamoja mahitaji yote muhimu ndani yake.
Juu ya kitanda kimoja kati ya vile viwili alionekana mwanaume mmoja akiwa amelala. Huyu hakuwa mwingine bali mlinzi na msaidizi wa karibu wa Felix yaani Haron. Ilikuwa ni kawaida ya Felix kuongozana na Haron kila mahali anapokwenda. walikuwa pamoja kila mahali hata ile safari yake ya kwenda nchini Marekani aliongozana na Haron.

Felix aliingia ndani akatembea moja kwa moja akajitupa kitandani pasipo hata kuvua viatu, alikuwa amechoka mno na istoshe kichwa chake kilikuwa kimebeba mawazo rukuki.

"Vipi Felix, kila kitu kipo sawa? Vipi kuhusu Tesha? Mzee kasemaje?" Mara sauti ya Haron ilisikika akiuliza maswali mfululizo wakati huo aliinuka taratibu na kukaa juu kitandani.

Felix alimsikia vizuri sana lakini hakujibu kitu, hakuwa akijisikia kuongea kwa wakati huo.

"... Felix" Haron aliita.

"Unataka nini Haron? unachojali hasa ni nini? Wewe na Baba lenu si moja? au unanipeleleza ili baadae ukamwambie nini nawaza kufanya..." Felix alifoka akainuka na kukaa juu kitandani kama alivyofanya Haron, sasa wakageuka wote wakawa wanatazamana kila mmoja akiwa juu kitandani kwake.

"Hapana mimi siku zote niko upande wako Felix, ni siri zako ngapi nazificha mpaka sasa mzee hajui chochote..?" Alieleza Haron na hapo ndipo Felix akakumbuka jambo lingine aliloelezwa na baba yake Magnus, ni kuhusu siri ya mahusiano ya kimapenzi kati yake na Madam Husnata, hakujua ni vipi Magnus aliweza kuitambua siri hii na kisha kukaa kimya kwa kipindi chote. Felix aliishia kumtazama Haron kwa jicho kali kisha akajitupa kitandani, hakutaka usumbufu wala kuendelea kubishana.

Mpaka sasa kuna mambo mawili makubwa yaliyokuwa yakiitesa akili ya Felix, kwanza kabisa ni kuhusu usalama wa mpenzi wake Tesha ambaye hadi dakika hii hajui alipo na wala hajui ni mazingira gani anapitia kwa wakati huu. Jambo la pili ilikuwa ni kuhusu ile picha ya msichana mrembo aliyonyeshwa na baba yake mda mfupi uliopita, picha ya Sasha binti kutoka ISRA, binti ambaye ndiye muhusika mkuu wa opareshini yao itakayoanza asubuhi. Sura ya Sasha ilikuwa imeganda kwenye ufahamu wa Felix. Kila alipojaribu kujisahaulisha alishindwa. Magnus alifanya makusudi kabisa kuchagua aina ya picha ambayo aliamini itaweza kuamsha tamaa za kiume kwa kijana mwenye lika kama la mwanae Felix. Na kweli alifanikiwa kwa asilimia kubwa kiasi cha kumfanya Felix atamani kuifanya kazi aliyoagizwa na baba yake si tu kwa ajili ya kumsaidia mpenzi wake Tesha hapana bali pia alitamani kukutana uso kwa uso na Sasha binti wa Gu Gamilo kutoka ISRA.

Wakati Felix akiwa katika dimbwi la mawazo ndipo alipokumbuka jambo lingine muhimu. Tangu walipoondoka na Tesha jioni nyumbani kwa Mama David ambaye ni mama yake wa kuigiza huku akimuahidi kuwa wangerudi baada ya muda mfupi lakini hawakurudi.
Alitazama saa kubwa ukutani akabaini ilikuwa ni saa tisa na nusu usiku. Kwa kuwa tayari Felix anazo namba za simu za mama David alitamani kumpigia lakini akasita.

"...ni usiku sana atakuwa amelala! Ila sasa nilimuahidi nitarudi vipi kama akiwa na wasiwasi....mmh! Hapana hawezi kuwa na wasiwasi na mimi kwanza sio mtoto wake!....lakini kama sijarudi na sijamwambia lolote ataona kama nimemdharau....ila ni usiku sana saa kumi kasoro... Hapana nisimpigie....au basi ngoja nipige tu...."

Felix aliwaza na kuwazua mwisho akaamua kumpigia simu Mama David. Simu iliita kwa sekunde chache sana ikapokelewa.

"Ha..hallo..mama" Felix aliongea kwa wasiwasi kidogo, hakutegemea simu kupokelewa haraka kiasi kile ni wazi kuwa hata Mama David naye hakuwa amelala.

"Nini tena usiku huu Feisal?" Mama David alisikika akiuliza swali upande wa pili wa simu hata kabla ya salamu.
Felix alipatwa na kaubaridi ka furaha mara baada ya kusikia ameitwa kwa jina la Feisal. Ilionyesha matumaini makubwa ya yeye kupokelewa na Mama David kama mwanae kamili.

"Aaa! Ni...nilikuwa na wasiwasi sijakutaarifu kama sitorudi nyumbani leo nikaona nikupigie simu, sahamani kwa usumbufu mama"

"Haya sawa" Mama David alijibu kwa kifupi sana kisha akawa anajiandaa kukata simu.

"Aah! Mama samahani uko sawa kweli? sauti yako ni kama...."

"Nikiwa sawa nisipokuwa sawa wewe utanisaidia nini Feisal? Zaidi ya kuniongezea matatizo mnayonipa wewe na watu wako"

"Hapana usiseme hivyo mama. Naweza kukusaidia, najua bado ni mapema sana kuniamini ila nipe nafasi nitafanya kwa nafasi yangu, siwezi kuivunja ahadi niliyokupatia leo Mama" Felix alijieleza akijaribu kuuteka zaidi moyo wa Mama David aweze kumuamini. Wakati wakizungumza hayo Haron hakuwa amelala alikuwa macho akisikiliza kila kitu.

"Ni kuhusu mwanangu David. Hajarudi nyumbani mpaka sasa, Tesha aliniambia kuwa amemuagiza mikoani kikazi lakini moyo wangu unagoma kabisa kuamini, David asingeweza kuondoka bila kuniaga, sio kawaida yake, mbaya zaidi simu yake haipatikani, hata Tesha pia kwa sasa hapatikani. Nakosa amani kabisa nahisi kuna jambo mbaya huenda likawa limetokea, niliwahi kumpoteza mwanangu wa kwanza Feisal kama hivi, sitaki tena ijirudie kwa David..." Alieleza Mama David sauti yake ikionekana kujawa na hali ya wasiwasi.

Kimya kilitawala kwa muda, wakati huo Felix alikumbuka kila kitu kuhusu David, tayari alishafanya mazungumzo na Tesha akamueleza kuwa David alitekwa na watu wasiojulikana. Felix anafahamu vizuri kabisa watu waliomteka David ni watu wanaofanya kazi na baba yake yaani MG family na kwa vyovyote vile Felix alijua wazi kuwa kwa sasa David atakuwa amehifadhiwa kwenye lile bonde pamoja na mateka wengine.

Wakati Mama David akiendelea kutoa maelezo hayo Felix aliinuka taratibu akashuka kitandani akasogea dirishani na kufunua pazia. Sasa akawa anatazama nje kwa uzuri kabisa na kwa kuwa alikuwa juu ghorofani Felix aliweza kuona moja kwa moja hadi kule chini bondeni mahali walipohifadhiwa mateka wa baba yake. Wakati huo sauti ya Mama David iliendelea kusikika simuni akizungumza.

".... Kama utaweza nisaidie kumtafuta mwanangu David popote alipo kisha mrudishe nyumbani mara moja, ongea na Tesha vizuri mulize ni wapi David alikwenda. Kama utamrudisha David salama basi nitayaamini maneno yako na kukupokea kama mwanangu Feisal"

Kimya kilitawala tena kwa muda huku Felix akiyatafakari kiundani maelezo hayo kutoka kwa Mama David, wakati huo macho yake alikuwa ameyaelekeza lilipo lile bonde walipohifadhiwa mateka. Giza lilikuwa nene mno ndani ya bonde lile ingawa kwa mbali sana Felix aliweza kuwaona mateka hao wanaopitia maisha magumu bondeni wakiwa wamewasha moto katika maeneo mbalimbali kusaidia kujikinga na badiri kali bondeni humo. Kwa haraka haraka Felix aliamini David ambaye kwa sasa mama yake anamzungumzia yupo ndani ya bonde hilo pamoja na mateka wengine. Hakujua na wala hakuna aliyejua kuwa kwa sasa David hayuko bondeni bali alishatoka nje kabisa ya bonde hilo na hivi sasa yupo ndani ya chumba kimoja cha mizigo katika himaya hiyo ya Magnus.

"Feisal..unanisikia?" Mama David aliuliza mara baada ya ukimya wa muda mrefu.
****

Mtwara - Nachingwea....
Hiki ni kijiji anachoishi Feisal mwenyewe halisi kaka yake David ambaye inaaminika alishakufa miaka mingi iliyopita na sasa Felix anaishi kwa jina lake huku Mama David naye akiwa mbioni kumkubali kama mwanae.

Usiku huu majira ya kumi kasoro Feisal pia hakuwa amelala, bado kichwani alikuwa anaandamwa na mawazo rukuki kiasi cha kumfanya akose kabisa usingizi. Kwanza alikuwa akiwaza namna atakavyoweza kuyamudu majukumu mapya ya kusoma na kujiunga na kikosi cha zima moto na uokoaji lakini pili Feisal aliwaza ni namna gani ataweza kuifanya kazi ya kumtafuta ndugu yake Boaz mara tu atakapoingia jijini Dar es salaam. Boaz ni ndugu yake asiye wa damu ambaye aliyetekwa na watu wasiojulikana miaka miwili iliyopita. Feisal alikuwa sebuleni huku SASHA na sikujua(mdogo wake Boaz) wao wakiwa wamelala chumbani.
Pamoja na uwezo mkubwa wa kuogelea aliokuwa nao Feisal hadi kufanikiwa kumuokoa binti mrembo Sasha kutoka katika mafuriko ya maji lakini bado Feisal alikuwa na kipaji kingine cha pekee, uchoraji. Feisal alikuwa ni mtaalamu mno wa kuchora, alikuwa na uwezo wa kukikataza kitu au mtu na akamchora kama alivyo.
Hiki ndicho Feisal alikuwa anakifanya usiku huu ikiwa ni katika hatua zake za kwanza kabisa kufanya maandalizi muhimu ya kumtafuta Boaz.
Kama kawaida yake alikusanya vifaa vyake vyote muhimu vya uchoraji tayari kwa kazi. Picha aliyotaka kuichoro usiku huu ilikuwa ya tofuati kiasi, ni picha ya sura ya mtu ambaye aliwahi kumuona mara moja tu katika kipindi chote cha maisha yake, mtu ambaye alikuwa ni mmoja kati ya watu waliohusika na kumteka Boaz miaka miwili iliyopita.

Feisal alituliza akili yake na kuvuta kumbukumbu siku ile ya tukio 21/07/2019 siku ambayo Boaz pamoja na rafiki zake wengine walitekwa nje ya supermarket moja jijini Dar es salaam (MINI SUPERMARKET). Feisal aliikumbuka vizuri sura ya mmoja kati ya wale watekaji, yule ambaye alivua helmet yake kabla ya kuingia ndani ya gari (Felix). Ilikuwa ni kazi ngumu lakini ajabu ni kwamba baada ya masaa mawili hadi inatimia mda huu saa kumi kasoro Feisal alikuwa ameikamilisha kazi yake. Mkononi alikuwa na mchoro wa picha ya mtu anayefanana kwa asilimia kubwa na Felix. Laita kama ungekuwa unamfahamu Felix na kisha ukaitazama picha aliyoichora Feisal usingekuwa na sababu ya kujiuliza mara mbili mbili huyu ni nani. Naam, hiki ni kipaji kingine alichozaliwa nacho mwanaume huyu ambaye kwa sasa anaishi mbali na familia yake huku Mama yake na ndugu zake wengine wakiamini kwamba alishakufa na mbaya zaidi mtu aliyemchora ndio huyo anayeishi kwa jina lake hivi sasa.

Feisal alibaki ametulia kwa muda huku akiwa amekaza macho yake kuitazama picha hiyo aliyoichora.

" Nitakutafuta, nitakupata na lazima unieleze ni wapi uliwapeleka ndugu zangu..." Alisema Feisal huku akiuma meno yake kwa hasira.
****
Ni wakati huo huo ambapo mazungumzo kupitia simu kati ya Felix na Mama David yalikuwa yakiendelea.

"Feisal..unanisikia?" Mama David aliuliza mara baada ya ukimya wa muda mrefu.

"Ndiyo nakusikia mama..."

"Sawa, niahidi basi kama utamrudisha David nyumbani. Najua unazo nguvu za kumtafuta na kumpata" Mama David alizidi kuomba kwa msisitizo.

Felix alitulia kimya huku akiwaza amjibu nini Mama David. Aliamini kuwa David yupo katika lile bonde mbele yake akiwa kama mateka. Kwa dakika kadhaa Felix alijikuta anasahau habari za kazi ngumu wanayotarajia kuifanya asubuhi ya siku hiyo. Kazi ya kwenda Mtwara kumteka Sasha binti kutoka ISRA. Felix hakujua kuwa kwa sasa Sasha yupo mikononi mwa Feisal mtu anayeishi kwa kutumia jina lake na mbaya zaidi Feisal huyo huyo ameichora picha yake na anapanga kumtafuta kwa udi na uvumba ili amueleze ni wapi alipowapeleka ndugu zake mara baada ya kuwateka pale supermarket miaka miwili iliyopita.

Je, nini kitafuata?
Vipi kama Feisal na Felix wakikutana?
Nini itakuwa hatima ya Sasha?
Inspekta Brandina na Tesha wako wapi?
Vipi kuhusu David ndani ya kile chumba?
Na je? Felix atakubaliana na ombi la mama David?

Usikose kufuatilia mfululizo wa simulizi hii nzuri yenye kisa cha kusisimua.

Simulizi na Riwaya Za Saul David bril

Simulizi hii ni Tsh 1000 tu lipia kwa mpesa namba 0756862047 jina Saul au Airtel money namba 0788967317 jina Saul
Kisha njoo WhatsApp namba hzo hzo
 
Msaada jamani anayejua app nyingine ya kupost simulizi ukiachana na hii forum Facebook, whatsapp na telegram ni app gani naweza tumia maana hapa jamii kuna changamoto post zangu zinafutwa kila baada ya nusu saa
 
Msaada jamani anayejua app nyingine ya kupost simulizi ukiachana na hii forum Facebook, whatsapp na telegram ni app gani naweza tumia maana hapa jamii kuna changamoto post zangu zinafutwa kila baada ya nusu saa
New memba,tayali una malalamiko mkuu.
Mbona umekuja moto.au unataka kuanzisha jukwaa lako nn.
Tutangazie tuu mkuu hakuna shida.
 
Kwahiyo ninyi wa siku nyingi mliishakubali kuwa mazwazwa?
Uzwazwa ni Kwan maono yako mkuu.
Maana Hawa jamaa wanajitahidi kupost vilevile wanatutaarifu kuwa;kwa wale wanaotaka kuisoma yote Basi wafanye malipo.
Na hata malipo yao sio makubwa kivile Basi tu turishazoea vya bule mkuu.
Hata sapoti hatutoi kwao,japo cm zetu hazikose DATA za kuperuzi humu.

Tuwe tunawapa sapoti,maana hizi ni kazi zinazowachukulia pia mda.
Mkuu usipanic,ila jaribu kuwasiliana nao watakutoza hell kiduchu tu na hutojutia hakika.
Tusiwabeze lakini maana wanajitahidi.
 
Back
Top Bottom