SASHA MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya............29
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047
ILIPOISHIA...
Haukupita muda mara walisikia muungurumo wa helikopta iliyokuwa angani ikiwasili kisiwani hapo.
Naam, walikuwa ni MG Family wakiwasili.
SASA ENDELEA...
Mwisho helikopta hiyo ilitua na kugusa ardhi katika kisiwa cha Magnus. Watu wanne walionekana wakishuka mmoja baada ya mwingi. Wanaume watatu na mwanamke mmoja.
Wanaume hawa walivalia suti nadhifu za bei ghali zenye rangi nyeusi na tai nyekundu. Yule wa kike yeye alivaa baibui la njano hijabu nyekundu na miwani mikubwa ya jua. Walishuka na kuanza kutembea kwa madaha wakiingia ndani ya jumba kuu la Magnus kisiwani hapo. Hawa ndio GM Family wenyewe majina yao waliitwa Kareem, Noel, Yuda na Madam Husnata.
IKO HIVI...
Ni miaka mingi imepita tangu siku Magnus alivyofukuzwa na kutupwa nje ya ISRA. Magnus hakutaka kukubali kushindwa aliendelea kupambana kujipanga upya kuhakikisha anarudi ISRA kwa mara nyingine kuendelea pale alipoishia.
Akiwa nje ya ISRA Magnus aliyaanza upya maisha yake, mambo mengi yanatokea hapa katikati na baada ya kipindi kirefu kupita Magnus anaibuka tena akiwa ni mtu mkubwa anayeishi katika kisiwa kimoja mbali na makazi ya wanadamu. Akiwa huko anaendelea jitihada zake akiamini ipo siku lazima atarudi tena ISRA, wala hakujali kuhusu umri wake ambao tayari ulikuwa umemtupa mkono mno.
Moja kati ya mafanikio makubwa aliyoyapata Magnus katika kipindi chote akiwa nje ya ISRA ni kuunda kundi moja kubwa la kigaidi tena lenye nguvu ambalo alilibatiza jina akaliita MG Family yaani familia ya Magnus, MG ikiwa ni kifupisho cha jina lake.
Kwa msaada mkubwa wa Magnus MG Family ikawa ni mtandao mkubwa na maarufu wa kigaidi Afrika mashariki na hata Afrika kwa ujumla. Ukiacha Boko haram ya Nigeria, Al-Shabab ya Somalia, Ansar-al-sharia ya Tunisia MG Family nayo ikawa ni moja ya kundi tishio la kigaidi nchini likajipatia umaarufu ingawa si kwa ukubwa sana.
Hakuna jambo gumu lililopita kwenye mikono ya MG Family likashindwa kupatiwa ufumbuzi. Walikuwa wamejikamilisha kwa kila idara. si kiuchumi wala si kisiasa kote walikuwa vizuri mno. Tayari walishaingiza mikono yao na kuwashika masikio hadi baadhi ya viongozi wakubwa serikalini. Tofauti na makundi mengine ya kigaidi, MG Family wao walifanya matukio yale tu ambayo yanafaida au ni agizo la kiongozi wao mkubwa yaani Magnus. Mfano wale watu wanaovaa helmet zenye vioo vya rangi nyekundu wanaofanya kazi ya kuwateka watu na kuwapeleka katika kisiwa cha Magnus walikuwa wapo chini ya mtandao huo wa MG Family. Ni mara chache sana MG Family walifanya vitu tofauti, na walifanya kwa siri bila Magnus mwenyewe kujua. Katu hakuwaruhusu kuanza kujihusisha na mambo ya kisiasa kama ilivyo ada kwa makundi mengi ya kigaidi.
Jambo ambalo liliendelea kuwa siri na hakuna aliyejua ni kuhusu kiongozi mkuu wa kundi hilo la kigaidi yaani Magnus mwenyewe.
Hawakujua Magnus ni nani anaishi wapi anafanya nini. Siku zote watu waliokuwa chini ya mtandao wa MG Family waliamini viongozi wakubwa ni watu wanne waliokuwa wakiratibu kila kinachoendelea yaani Kareem, Noel, Yuda na Madam Husnata. Hawa walikuwa ni viongozi wakubwa waliowekwa na Magnus, lakini wengi waliamini hawa ndio wamiliki wakuu wa mtandao wa kigaidi MG Family.
[emoji294][emoji294][emoji294]
Baada ya helikopta kutuwa Kareem, Noel, Yuda na Madam Husnata walishuka na kuanza kutembea kwa madaha kuingia ndani ya jumba kuu la Magnus kisiwani hapo.
Walimkuta Magnus amekaa kwenye kiti chake cha heshima akiwasubiri kwa hamu.
Walisimama mbele yake na kuinamisha vichwa vyao kwa heshima kubwa. Magnus aliwatazama kwa zamu mmoja baada ya mwingine kisha akaongea.
"Nafikiri kila mmoja anataarifa ya kile kinachoendelea wakati huu, nataka kujua wakati mwanangu anaingia kwenye vitabu vya polisi wapelelezi na kuanza kutafutwa ninyi mlikuwa wapi?" Hili lilikuwa swali la kwanza kutoka kwa Magnus.
Kimya kilitawala kila mmoja akimtegea mwenzake ajibu, walimuogopa mno Magnus.
"Mkuu, ukweli hatukujua lolote na hata watu wetu hawamfahamu Felix kama...." Noel alijitoa muhanga na kujibu
"Hamkujua lolote?" Magnus alifoka na kusimama. Kareem, Yuda, Noel na Husnata wote wakapiga magoti na kuinamisha vichwa vyao chini, hawakutakiwa kusimama pindi ambapo mkubwa wao Magnus amesimama.
Magnus aliwatazama tena kwa zamu akionekana kuwa na hasira sana.
"Niangalieni" alitoa amri. Wote wakatii na kuinua nyuso zao.
"Mwanangu anafika Tanzania kesho asubuhi, sitaki aguswe hata unywele wake. Sitaki awe na kesi ya aina yoyote, aachwe huru na asifuatiliwe tena"
"Sawa mkuuu.." Waliitikia kwa pamoja.
"Sitovumilia uzembe wa aina yoyote utakao jitokeza" Magnus alisisitiza.
[emoji294][emoji294][emoji294]
Dakika tano baadae vigogo wa MG Family walitoka nje ya jumba la Magnus, kila mmoja akionekana kuwa bize na simu yake, tayari taratibu za kutimiza jukumu walilopewa zilianza papo hapo.
Mwisho waliingia ndani ya helikopta na baadae helikopta hiyo ikaacha ardhi na kupaa angani.
[emoji294][emoji294][emoji294]
David, Zungu na Dayana wakiwa bondeni waliisindikiza helikopta hiyo kwa macho hadi pale ilipopotelea juu mawinguni.
"Next time hii helikopta ndiyo itakayotubeba na kututoa hapa" Aliongea David. Dayana na Zungu wakageuka kwa pamoja kumtazama.
"Unaota au?" Aliuliza Dayana.
"Nimepata wazo" Alisema David
"Kabla hujatuambia hilo wazo lako kuna kitu nataka kuwaeleza" Zungu alidakia.
"Nini?" David na Dayana wakauliza kwa pamoja.
"Nimepata njia ya kutoka hapa moja kwa moja hadi ufukweni mwa bahari"
"Nini? Acha masihara Zungu" Alisema Dayana
"Unamaanisha kweli jamaangu?" David naye kaongeza swali. Zungu alitikisa kichwa akiashiria kumaanisha kile alichokisema kisha kaongea...
"Wakati mvua imeanza kunyesha mimi nilitoka hapa, kawaida kukiwa na mvua walinzi huwa wanatoka na kukaa kwenye vibanda vyao hivyo niliweza kupenya vikwazo vyao vyote kwa urahisi, kwa bahati nzuri leo nimefanikiwa kuona njia ya pango linalopita chini kwa chini na kutokea kwenye ile barabara iliyopita mlimani chini ya ardhi"
"Unamaanishe ile barabara tuliyopita wakati tunaletwa hapa"
"Ndiyo David" Zungu aliitika.
Zilikuwa ni habari njema mno kwa wote watatu, mwisho walikaa na kukubaliana usiku watoke kwa mara nyingine kwenda kuhakiki njia hiyo.
Taratibu matumaini ya kutoka kwenye mateso hayo yalianza kujionyesha japo si kwa asilimia kubwa sana.
[emoji294][emoji294][emoji294]
Upande wa pili...
Dakika 17 pekee baada ya kutoka hospitali zilitosha kabisa kufika nyumbani kwa Mama David. Nyumba ilikuwa imejitenga peke yake maeneo ya uswahilini hatua kama 50 kutoka barabarani. Ilikuwa ni nyumba ya kawaida yenye bati lililochakaa.
"Asante mwanangu, tutashuka tu hapa hapa haina shida..." Alisema Mama David huku akimuomba Tesha amsaidie kufungua mlango wa gari.
Kwa sababu Tesha naye alikuwa na haraka hakutaka kubishana na Mama David aliona ni heri ashukie hapo ili yeye na dereva wake warudi haraka mjini aendelee kufuatilia habari za Ndege aliyopanda mpenzi wake Felix kutoka Marekani.
"Usijali mama, muhimu nimepajua nyumbani nitakuwa nakuja mara kwa mara kukutembelea. Naomba usisahau maelezo ya daktari mama yangu, punguza mawazo, kula chakula kwa wakati na usiache kutumia dawa pia"
"Nashukuru sana mwanangu. Kwa hiyo David atarudi lini?" Aliuliza Mama David mara baada ya kushuka garini pamoja na mwanae tatu.
"David mmm! Nafikiri baada ya siku nne hivi atakuwa amekamilisha kazi yake, ila tutawasiliana kama kukiwa na mabadiliko nitakwambia" Tesha alidanganya mwisho wakaagana na mama David. Lakini kabla Dereva hajaondosha gari Tesha alitupa macho kwa mara nyingine kutazama nyumbani kwa mama David akaona gari tatu za kifahari aina ya Benz-Mercedes zikiwa zimepaki nje ya nyumba hiyo tena zote zilikuwa nyeusi zinafanana.
Hali hii ilimshangaza sana Tesha lakini kwa kuwa alikuwa na haraka hakutaka kulizingatia sana hilo, akamtaka Dereva aondoshe gari, wakaondoka.
Si kwamba hali hiyo ilimshangaza Tesha pekee, hata Mama David naye alibaki kinywa wazi mara baada ya kuziona gari hizo nyumbani kwake. Haikuwa kawaida na vilevile haikuwahi kutokea tangu ahamie kwenye nyumba. Alijipa moyo akawa anapiga hatua kusogea, mkono wake wa kulia alishika mkoba wake mkubwa na mkono wa kushoto alimshika mwanae tatu.
Akiwa amebakiza hatua kama kumi kufika nyumbani kwake mara ghafula mlango wa gari moja ulifunguliwa akashuka mwanaume wa miraba minne aliyepigilia suti nadhifu nyeusi. Mwanaume huyo alisogea nyuma akafungua mlango wa gari kwa heshima kubwa mara akashuka mwanamke mmoja maji ya kunde, mrefu na mnene kiasi. Alivaa baibui la njano hijabu nyekundu na miwani mikubwa ya jua.
Huyu alikuwa ni Madam Husnata kigogo mmoja wapo kutoka kundi la MG Family linalomilikiwa na Magnus.
Ndiyo ni Madam Husnata yule yule ambaye muda mfupi uliopita alikuwa katika kisiwa cha Magnus akiwa na wenzake Kareem Noel na Yuda.
Kwa nini mwanamke huyu yupo nyumbani kwa mama David? Kuna mahusiano gani? Kafuata nini? Kivipi?
Haya ni maswali ambayo hata mimi mtunzi wako yananiacha kinywa wazi.
Usijali majibu ya maswali haya utayapata kwenye mfululizo wa episode zinazofuata KAA MKAO.
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047