Simulizi ya kichawi: Makaburi ya wasio na hatia (The Graves of The Innocents)

Simulizi ya kichawi: Makaburi ya wasio na hatia (The Graves of The Innocents)

Sehemu ya kumi--------10


ILIPOISHIA:

“Kuna tukio baya linataka kutokea, kuwa makini,” nilisikia sauti ya baba ikiniongelesha sikioni mwangu, nikageuka huku na kule, baba hakuwepo, nikajua kwa vyovyote lazima alikuwa ameona jambo ndiyo maana akanipa tahadhari, nikajiweka vizuri kitini, nikawa natazama huku na kule.

SASA ENDELEA…

Niliingiza mkono mfukoni na kutoa ile dawa aliyonipa baba, nikaishika ili chochote kikitokea iwe rahisi kufanya kama nilivyoelekezwa. Tukaanza kuteremka kwenye mteremko mrefu, wenye konakona nyingi na makorongo ya kutisha wa Kitonga.

Nilielewa kwa sababu gani eneo hilo lilikuwa maarufu sana, barabara ilikuwa imechomngwa pembezoni mwa milima na mawe makubwa, hali iliyofanya kama upande mmoja kukiwa na ukuta wa mlima basi upande wa pili kuna bonde refu sana.

Yaani kwa kutazama tu urefu wa yale makorongo, nilijikuta nikihisi kizunguzungu, nikawa najiuliza ikitokea dereva akakosea na kupeleka gari kwenye yale makorongo nini kitatokea? Sikupata majibu.

Safari iliendelea, dereva akawa amepunguza sana mwendo, abiria wote ndani ya gari wakiwa kimya kabisa. Nadhani kila mmoja alikuwa na kumbukumbu ya kilichotokea Mlima Nyoka. Ghafla tulishtuka baada ya kuona kuna lori la mafuta, tena likiwa na trela kwa nyuma, likija kwa kasi kubwa nyuma yetu.

Tulishtushwa na kishindo kikubwa kilichosikika nyuma, wote tukageuka na kusimama kwenye siti, tukawa tunatazama nini kinachoendelea? Inavyoonesha, lile lori lilikuwa limepasuka tairi la mbele na kumshinda dereva, sasa likawa linayumba barabara nzima.

Abiria wote walianza kupiga kelele kwenye lile basi, hakuna ambaye alijua nini kitatokea kwa sababu kama lile gari lori lingeendelea kuja kwa mwendo ule, lingeligonga basi letu kwa nyuma na kwa ile kasi yake, maana yake lingeturushia kwenye korongo refu na kutuangukia kwa juu.

Sijui kama kuna mtu angepona, ukizingatia kwamba lilikuwa ni lori la mafuta na lilionesha kuwa na mzigo. Nilichokifanya, kwa haraka nilimnyunyizia ule unga dereva ambaye bado hakuwa akijua afanye nini. Nilipomnyunyizia tu, nilimuona akibadili gia haraka, akaongeza mwendo na kulifanya basi lianze kushuka mteremko ule kwa kasi kubwa.

Kuongeza kasi kwa ghafla kuliwafanya abiria wengine wazidi kuchanganyikiwa, kelele zikazidi ndani ya basi, lile lori nalo likawa linazidi kuja kwa kasi kubwa nyuma yetu.

Wakati dereva akizidi kukanyaga mafuta na kulifanya basi lishuke kwa kasi ya ajabu mteremko ule hatari, ghafla tulishtukia lori jingine likiwa limepaki mbele yetu, dereva na utingo wake wakiwa wamekata matawi ya miti na kusambaza barabarani, ishara kwamba lilikuwa limeharibika.

Kwa kasi ambayo gari tulilopanda lilikuwa likishuka nayo, hata mimi mwenyewe sikuamini kama dereva ataweza kulimudu na kulikweopa lile lori mbele yetu.

Hata hivyo, dereva alitumia kile ambacho wengi huita uwezo binafsi, bila kupunguza mwendo hata kidogo, alizungusha usukani kwa kasi, gari likageuka kama linaenda kugonga jiwe kubwa lililokuwa pemebini ya barabara, kisha akazungusha tena usukani kwa kasi, gari likageuka tena upande wa pili.

Kitendo kile kililifanya basi letu lipenye kwenye uwazi mwembamba uliokuwepo kati ya lile gari lililoharibika na ukuta wa upande wa pili, kufumba na kufumbua likapita pale katikati kwa kasi kubwa na kulipita lile gari bovu, dereva akaanza kupunguza mwendo huku akibadilisha gia.

Sekunde chache baadaye, kilisikika kishindo kikubwa nyuma yetu, lile lori la mafuta lilikuwa limeligonga lile lori jingine bovu kwa nyuma na kulisukuma mita kadhaa kabla ya yote mawili kuangukia kwenye korongo refu, watu wote wakawa hawaamini kilichotokea.

Cha ajabu sasa, wakati watu wote wakitazama kilichotokea kule nyuma, nilishtuka kugundua kwamba kumbe aliyekuwa akiendesha gari hakuwa yule dereva wetu bali baba, macho yakanitoka pima nikiwa siamini ninachokiona. Alipogundua kwamba namtazama, naye alinigeukia na kunitazama kwa sekunde chache, akawa aanendelea kubadili gia huku akifunga breki.

Mbele kidogo kulikuwana uwazi pembeni ya barabara ambao uliwekwa maalum kwa ajili ya magari yanayoharibika njiani, akaendelea kufunga breki na hatimaye, akalisimamisha kabisa basi letu. Wakati watu bado wakiwa bize kushangaa kule nyuma, alifungua mlango wa dereva, akashuka huku akiendelea kunitazama na kunionesha ishara kwamba nisiseme chochote.

Akapotea kwenye upeo wa macho yangu na kuniacha na maswali mengi yasiyo na majibu. Cha ajabu kingine, aliposhuka, pale kwenye siti ya dereva alikuwa amekaa dereva yuleyule, tena akiwa amefunga na mkanda kabisa lakini kama ilivyokuwa mara ya kwanza, naye alionesha kushtuka kama mtu aliyekuwa amelala usingizi mzito. Akageuka huku na kule, macho yangu na yake yakagongana.

‘Kwani kumetokea nini?” aliniuliza kwa sauti ya chini huku akitaka mtu mwingine yeyote asielewe. Nadhani hata yeye alishagundua kwamba kuna mambo yasiyo ya kawaida yalikuwa yakiendelea.

*(Usikose kutembelea Simulizi za Majonzi)

“Ajali, ajali mbaya sana,” nilimjibu huku nikimuonesha kule nyuma tulikotoka ambako moshi mzito mweusi ulikuwa ukifuka kutoka bondeni. Tayari abiria wengi walikuwa wameshashuka kwenye basi na kuanza kurudi kule eneo la tukio. Harakaharaka dereva alifungua mlango na kushuka, na mimi ikabidi nishuke tena safari hii nilipitia pale kwenye mlango wa dereva.

Tukawa tunakimbilia pale eneo la tukio. Trela moja la lile lori la mafuta, lilikuwa limekatika na kuanguka katikati ya barabara kimshazari, jambo lililofanya mawasiliano kati ya pande hizo mbili za barabara yakatike. Hakukuwa na gari ambalo lingeweza kuvuka tena mpaka trela lile liondolewe.

Ajali ilikuwa mbaya kiasi cha kumfanya kila mmoja aliyeshuhudia, ainue mikono yake juu na kumshukuru Mungu kwa sababu kama isingekuwa miujiza iliyotokea, ilibidi basi letu ndiyo ligongwe na kuangukia kule bondeni kisha kuanza kuungua kama ilivyokuwa imetokea.

Tukiwa bado tunaendelea kushangaa kilichotokea, tulishangaa kuona mtu akitoka ndani ya lile lori la mafuta lakini mwili wake wote ukiteketea kwa moto, akawa anajaribu kukimbia lakini hakufika mbali, moto ukamzidi na kumfanya aanguke chini.

Kwa jinsi magari hayo yalivyodondokea chini bondeni, hakuna mtu yeyote ambaye angewahi kwenda kumsaidia yule mtu kwa sababu kwanza eneo lenyewe lilikuwa haliwezi kupitika kirahisi, watu wakawa wanapiga kelele huku tukimshuhudia yule mtu ambaye sijui ndiyo alikuwa dereva au utingo wa gari lililopata ajali akiteketea bila msaada wowote.

Muda mfupi baadaye, magari mengine mengi yalishawasili eneo hilo na kwa sababu barabara ilikuwa imefungwa, yalisimama na kupanga foleni ndefu, abiria na madereva wakawa wanashuka kuja kujionea kilichotokea.

Kila aliyekuwa anaona kilichotokea, alikuwa haamini kabisa. Ilikuwa ajali mbaya mno ambayo kama ingehusisha gari la abiria, sidhani kama kuna mtu yeyote angetoka salama.

Kwa kuwa tulikuwa nyuma ya muda na bado tulikuw ana safari ndefu, ilibidi turudi kwenye basi letu, dereva naye akawa anaonekana kuwa na maswali mengi kuliko majibu.

Japokuwa kwa mara nyingine abiria wote walikuwa wakimsifia kwa jinsi alivyoweza kuepusha ajali ile, mwenyewe alikuwa akijua kutoka ndani ya moyo wake kwamba siyo yeye aliyefanya kazi hiyo na hakuwa akijua chochote kilichotokea.

Tulirudi kwenye basi na baada ya kuhakikisha abiria wote wameingia, dereva aliondoa gari kwa mwendo wa taratibu, gumzo kubwa ndani ya basi likawa ni juu ya ajali hiyo. Wakati watu wakiendelea kujadiliana kuhusu ajali hiyo, mimi bado nilikuwa na maswali mengi mno kuhusu baba.

Bado sikuwa na majibu na hakukuwa na mtu yeyote wa kunijibu zaidi ya baba mwenyewe. Jambo kubwa ambalo lilikuwa likijirudia ndani ya kichwa changu, lilikuwa ni je, kweli baba ni mchawi?

“Unasemaje?” nilisikia sauti ya baba akiniuliza kwa ukali, nikageuka huku na kule lakini baba hakuwepo.

Je, nini kitafuatia?
Ili kutopunguza uhalisia wa matukio haikupaswa kuwa hivi sababu 99.9% ya malori ya mafuta hayashuki kitonga yakiwa na mzigo Bali hupanda yakiwa na mzigo
Screenshot_2023-03-04-07-24-36-25.jpg
 
Sehemu ya 48

ILIPOISHIA:

Nilichopanga kichwani, ni kuchukua maelekezo vizuri kwa yule mtu aliyesema marehemu ni jirani yake kisha kwenda kwanza mpaka eneo la ajali na baada ya hapo, nitakwenda Tumbi kujionea hali ya mgonjwa na hiyo maiti kama nitapata nafasi. Nilikuwa na shauku kubwa ya kujua kila kitu maana moyo wangu ulikuwa na hatia kubwa, hasa kutokana na jinsi taarifa za ajali ile zilivyowaumiza mioyo abiria wengi.

SASA ENDELEA…

Safari iliendelea na hatimaye tukawasili Kibaha, gari liliposimama tu, nilimuwahi yule abiria aliyekuwa akisimulia kuhusu ile ajali, nikamsalimu na kumuomba anielekeze ulipo msiba kwa sababu aliyefariki ni ndugu yangu.

“Ni Mlandizi, ukishuka tu pale kituoni, uliza mtu yeyote eti kwenye msiba wa mtoto aliyekufa kwenye ajali ni wapi? Huwezi kupoteza, mtoto alikuwa anafahamika sana yule kutokana na jinsi alivyokuwa na heshima,” alisema yule abiria, nikamshukuru.

Nilipoachana naye, nilimfuata dereva ili anielekeze sehemu gari lilipopata ajali kwani kuna muda nilimsikia akisema kwamba eneo hilo ni baya sana, ajali huwa zinatokea mara kwa mara. Eneo lenyewe nilikuwa nalifahamu lakini sikujua naweza kufikaje.

“Siyo mbali sana kutoka hapa, hata kwa miguu unaweza kufika, panaitwa machinjioni,” alisema yule dereva, nikamshukuru na kuanza kutembea kuelekea eneo la tukio. Tayari kulishaanza kupambazuka na lile giza la afajiri lilianza kupungua na kumezwa na nuru ya alfajiri.

Kila nilipokuwa napita, wafanyabiashara na wasafiri walikuwa wakizungumzia ajali iliyotokea usiku wa siku hiyo. Kila mtu alikuwa akizungumza lake lakini kama baba alivyoniambia usiku, eneo hilo huwa linatumiwa sana na wachawi, hasa waliopo mafunzoni kama mimi kusababisha ajali.

>>Usiache kutembelea Simulizi za Majonzi

Kila mtu alikuwa anashauri eneo hilo watafutwe waganga waliobobea au wachungaji wakaliombee kwani kulikuwa na nguvu za giza au ‘nyoka chunusi’ anayesababisha ajali. Njiani sikuwa peke yangu, baadhi ya watu nao waliposikia kuhusu ajali hiyo, walitaka kwenda kujionea wenyewe.

Niliongozana na vijana kadhaa, tukawa tunatembea pembeni ya barabara na dakika kadhaa baadaye, tulifika eneo ajali hiyo ilipotokea. Nilipofika eneo hilo, nilishangaa nywele zikianza kusisimka kuliko kawaida huku harufu ya damu ikitawala kwenye pua zangu. Gari lililopata ajali bado lilikuwa eneo la tukio, pembeni ya barabara, yaani kwa jinsi lilivyokuwa limeharibika, kila mmoja alibaki kushika kichwa.

Mjadala uliotawala kwa wote waliokuwa wamefika kushuhudia ajali hiyo, ulikuwa ni nini kilichosababisha ajali hiyo. Kwa sababu kulishapambazuka, niliweza kuliona vizuri eneo hilo, lilikuwa ni tambarare kabisa, hakukuwa na kona wala mteremko, achilia mbali mlima wa kuweza kusababisha ajali mbaya kiasi kile.

Nilitazama kule tulikokuwa tumekaa na baba na baba yake Rahma, ambako baada ya kuuchukua ule mwili wa yule mtoto niliupeleka, nikashangaa kuona kwamba eneo lote lilikuwa jeupe kabisa kiasi kwamba ungeweza kuona umbali wa karibu mita mia tano.

Hakukuwa na miti wala vichaka, eneo lote lilikuwa jeupe kabisa. Nikawa najiuliza pale kwenye migomba tulipokuwa tumekaa ni wapi? Ule mgomba uliokatwa kisha nikapewa ulitoka wapi? Nikahisi labda nimechanganya upande, nikageukia upande wa pili wa barabara, nako kulikuwa kweupe kabisa, nikawa ni kama nimechanganyikiwa.

“Vipi kijana, mbona unaonesha kutotulia? Unatafuta nini?” niligeuka baada ya kusikia sauti hiyo, nikamtazama aliyekuwa akinisemesha. Alikuwa ni mzee mmoja mwenye ndevu nyingi zilizofunika mdomo wote. Mkononi alikuwa na mkongojo na kwa jinsi alivyokuwa amevaa, ilionesha haishi mbali na eneo hilo.

“Aah! Hamna kitu, nashangaa tu jinsi hii ajali ilivyotokea.”

“Mh! Hebu nitazame usoni,” alisema, nikamtazama na yeye akanitazama. Kitendo cha kutazama naye tu, nilihisi ile hirizi niliyoivaa mkononi ikinibana. Maelezo aliyonipa baba, ni kwamba nikiona inanibana ghafla, lazima kutakuwa na mtu eneo hilohilo mwenye nguvu za giza anajaribu kunipima.

Akaniambia nikishaona hali hiyo, haraka sana nizibe kucha ya mkono wa kushoto kwa kutumia kidole gumba cha mkono huohuo, jambo ambalo nililifanya bila yule mzee kunishtukia. Nikashangaa ameanza kupiga chafya mfululizo, tena kwa nguvu. Alipiga chafya kama kumi hivi, kamasi na machozi vikawa vinamtoka kwa wingi, mpaka watu wengine waliokuwa eneo hili wakawa wanamshangaa.

>>Usiache kutembelea Simulizi za Majonzi

“Mtoto mbaya sana wewe, mtazame bichwa lake,” alisema mzee huyo kwa hasira, akawa anaondoka huku akiendelea kunitukana na kupiga chafya.

“Hivi vizee ndiyo vichawi vyenyewe, unakiona kile kibabu kilivyokuwa kinapiga chafya, inaonesha kimenogewa na harufu ya damu,” alisema mmoja kati ya watu waliokuwa eneo lile, wengine wakacheka huku wengine wakiendelea kusikitika.

“Mbona yule mzee anakutukana, kwani umemfanya nini?”

“Mzee gani?”

“Yule aliyekuwa anapiga chafya?” mwanamke mmoja wa makamo aliniuliza, kumbe alikuwa ameshuhudia kila kitu, nikaamua kuvunga maana kuendelea kuzungumza kungefanya watu waanze kunitazama kwa makini, jambo ambalo sikuwa tayari kuona likitokea.

“Mh! Labda umeangalia vibaya, mbona mimi simfahamu na wala sijaongea naye chochote?” nilijibu huku nikigeuka na kumpa mgongo yule mwanamke, nikaona bado ananifuata kwa manenomaneno.

“Itakuwa kuna jambo baya umemfanyia, haiwezekani mzee kama yule aanze tu kukutukana, nataka uniambie, unajua yule ni nani kwangu,” alisema mwanamke huyo huku akizidi kunisogelea mwilini. Kitendo cha kunisogelea tu, nilishtukia ile hirizi ikianza tena kunibana, safari hii kwa nguvu kuliko mwanzo.

Ikabidi nikae chonjo kwa sababu ubanaji wake ulikuwa wa nguvu na baba alishaniambia kwamba ukiona inabana kwa nguvu, ujue upo jirani na mtu mwenye nguvu kubwa ambaye usipokuwa makini anaweza kukudhalilisha mbele za watu.

Haraka niliibana kucha ya kidole kidogo kwa kidole gumba changu na safari hii, nilitumia mikono yote miwili. Kwa mtu asiyejua, angeweza kudhani labda nachezea tu vidole vya mikono yangu kumbe nilikuwa na shughuli nyingine kabisa.

Kitendo hicho kilisababisha mwanamke yule awe ni kama amepandwa na mashetani, akaanza kukimbia huku na kule huku akiongea maneno yasiyoeleweka, akawa anasema kwamba eti pale eneo la tukio pamejaa wachawi na yeye ni miongoni mwa hao wachawi.

Kila mtu alibaki kumshangaa, ikabidi niachie vidole haraka maana kwa jinsi alivyokuwa akiongeaongea huku mara kwa mara akinigeukia na kunitazama kwa macho ya woga, angeweza kunisababishia kizaazaa.

Nilipoachia tu vidole vyangu, alidondoka chini na kuzimia, wanawake wengine wawili ambao inaonesha ni kama alikuja nao, wakawa wanampepea huku wakinitazama kwa macho mabaya. Kwa hali ilivyokuwa, ilibidi tu nianze kuangalia utaratibu wa kuondoka eneo hilo maana hali ilishaanza kuwa tete na sikutaka akizinduka anikute bado nipo eneo hilo.

Nilizugazuga kisha nikajichanganya na watu waliokuwa wakielekea kule upande wa stendi, tayari kulishapambazuka na kijua cha asubuhi kilishachomoza. Kilichonishangaza, ni kugundua kwamba licha ya ajali yenyewe kutokea katika mazingira ya kishirikina, bado kulikuwa na wachawi miongoni mwa watu waliokuwa wakishuhudia kilichotokea.

Nilipanga niende kwanza msibani kisha nikiwa narudi ndiyo nipitie kule Hospitali ya Tumbi kwenda kumwangalia majeruhi wa ajali ile na kama ikiwezekana nikaione na maiti ya huyo mtoto maana ukweli ni kwamba mimi ndiye niliyemchukua kutoka eneo la tukio na sehemu yake nikaweka kipande cha mgomba.

>>Usiache kutembelea Simulizi za Majonzi

Nilikuwa na shauku kubwa sana ya kutaka kujua mambo mengi ambayo kwangu yalikuwa mageni kabisa. Nilipofika stendi, sikuwa na muda wa kupoteza, nilipanda kwenye gari linaloenda Mlandizi ambalo nalo ilikuwa ni lazima lipite pale eneo la ajali.

Safari ilianza, tulipokaribia eneo hilo, nilitoa kichwa nje ili nichungulie tena, nikamuona yule mwanamke aliyekuwa akinichokoza akiwa amekaa kitako chini kuonesha kwamba fahamu zimemrudia, ndugu zake wakawa wanajaribu kumuinua. Nilijikuta nikitabasamu huku moyoni nikijisikia fahari kubwa kuwashikisha adabu waliokuwa wakitaka kunichokoza.

Baada ya muda, gari liliwasili Mlandizi, hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kukanyaga ardhi ya eneo hilo. Niliposhuka, niliwauliza wenyeji mahali kulikokuwa na msiba ambapo bila hiyana walinionesha. Tayari watu wengi walikuwa wamekusanyika nje ya nyumba moja nzuri na ya kisasa, huku wengine wakihangaika kuweka maturubai.

Nilipofika, na mimi nilijifanya ni mwombolezaji wa kawaida tu, nikawasalimia baadhi ya watu kisha nikajichanganya na waombolezaji wengine. Ghafla nilishtuka baada ya kuona kitu ambacho sikukitarajia, nikahisi kijasho chembamba kikianza kunitoka, mara hirizi yangu ikaanza kunibana kwa nguvu, kufumba na kufumbua kamba yake ikakatika, ikadondoka chini!

Je, nini kitafuatia?
 
Sehemu ya 49

ILIPOISHIA:

Nilipofika, na mimi nilijifanya ni mwombolezaji wa kawaida tu, nikawasalimia baadhi ya watu kisha nikajichanganya na waombolezaji wengine. Ghafla nilishtuka baada ya kuona kitu ambacho sikukitarajia, nikahisi kijasho chembamba kikianza kunitoka, mara hirizi yangu ikaanza kunibana kwa nguvu, kufumba na kufumbua kamba yake ikakatika, ikadondoka chini!

SASA ENDELEA…

“Mungu wangu!” nilijikuta nimetamka kwa sauti, hali iliyofanya watu wote washtuke, hata wale ambao hawakuwa wameniona nikiwasili eneo hilo, waligeuka na kunitazama, nikajihisi mwili ukiishiwa nguvu na kunyong’onyea kama nimepigwa na shoti ya umeme.

Sikujua nifanye nini kwa wakati huo, watu wakawa bado wamenikazia macho, kila mtu akiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua mimi ni nani na nini kimetokea mpaka nikashtuka kiasi hicho.

“Wasalimu watu wote kwa heshima kisha wape pole,” nilisikia sauti ya baba masikioni mwangu, ghafla nikajikuta nimepata nguvu na kuwa na imani kubwa kwamba hata iweje, baba ameshajua kinachoendelea kwa hiyo atanisaidia.

“Shikamooni jamani na poleni sana kwa msiba!” nilizungumza kwa kujitutumua huku sauti yangu ikiwa bado na dalili za kutetemeka. Wengine walijibu salamu yangu na wengine walikaa kimya lakini kwa kiasi kikubwa, kitendo cha mimi kuwasalimu, kiliwafanya wengi wanione kama muombolezaji wa kawaida.

Wengine waliendela na mazungumzo yao na wachache walibaki wakinitazama, nikawa natafuta ‘taiming’ ya kuiokota ile hirizi. Kwa harakaharaka niligundua kwamba kulikuwa na zaidi ya watu saba waliokuwa bado wamenikazia macho, nikawa najaribu kuzuga, sikutaka kutazamana na mtu yeyote usoni kwa sababu nilihisi ile hatia niliyokuwa nayo isingeweza kufichika.

Kwa bahati nzuri, nikiwa bado nazugazuga pale nikitafuta namna ya kuiokota ile hirizi pale chini, kulisikika sauti za wanawake wakilia kwa nguvu mara tu baada ya kushuka kwenye gari kwani msiba haukuwa mbali na barabara kuu ya lami ya kuelekea Morogoro.

Watu karibu wote waligeukia kule vile vilio vilikokuwa vinatokea, nikaona huo ndiyo muda pekee wa kufanya kile nilichokusudia. Kwa kasi kubwa niliinama na kuikwapua ile hirizi pale chini kisha nikaisokomeza kwenye mfuko wa suruali. Wakati nikiamini kwamba hakuna mtu aliyeniona, nilishtuka kugundua kwamba wale watu niliokuwa nahisi kwamba wananitazama, wala hawakujishughulisha kuwatazama wale watu waliokuwa wakilia, kumbe bado walikuwa wamenikazia macho na kitendo cha kuikota ile hirizi pale chini, walikishuhudia live bila chenga, kwa mara nyingine nikajikuta nikiishiwa nguvu.

Japokuwa ilikuwa ni asubuhi, nilihisi nikilowa kwapani kwa kijasho chembamba.

“Usipokuwa makini utakiona cha mtema kuni leo, nani aliyekutuma kwenda msibani? Ni mwiko kabisa kwa sheria zetu, bora hata ungeenda makaburini,” sauti ya baba ilisikika tena masikioni mwangu na kuzidi kunipa hofu kubwa ndani ya moyo wangu.

Niligeuka huku na kule, nikagundua kwamba kumbe kulikuwa na watu wengine nyuma yangu waliokuwa bado wakinitazama, nikazidi kuingiwa na hofu. Sikuwa najua natakiwa kufanya nini, nikaamua kuchukua maamuzi magumu.

Kwenye moja kati ya maturubai yaliyokuwa yakiendelea kufungwa, kulikuwa na mshumaa wa rangi ya zambarau ambao tayari ulishawashwa na pembeni yake, kulikuwa na picha kubwa iliyowekwa kwenye fremu ya kioo, sambamba na daftari na kibakuli kilichokuwa na fedha.

Bado watu wengi walikuwa wanawatazama wale waombolezaji waliokuwa wakiendelea kulia kwa uchungu huku wakisaidiwa na wenyeji wao kupelekwa pale msibani, nikatembea kwa hatua za kusuasua mpaka pale kwenye ile picha ya marehemu, nikaitazama.

Kiukweli hakuna siku ambayo nimewahi kujihisi kuwa na hatia kubwa ndani ya moyo wangu kama siku hiyo. Maskini ya Mungu, bado alikuwa binti mdogo kabisa na kwenye picha hiyo alikuwa ameachia tabasamu pana, akionesha kuwa na matumaini mwengi kwenye maisha yake ya baadaye.

Nilijisikia vibaya sana kushiriki kuyakatisha maisha ya msichana yule mdogo asiye na hatia, nikashindwa kujizuia, machozi yakanitoka kwa wingi na kulowanisha uso wangu.

Sikukumbuka tena kama kuna watu walikuwa wakinifuatilia hatua kwa hatua, kwa uchungu niliokuwa nao, niligeuka haraka na kutafuta sehemu ya kujificha kwa sababu huwa sipendi kabisa mtu yeyote ayaone machozi yangu. Kwa kutumia viganja vya mikono yangu nilijiziba usoni, nikasogea mbali kabisa na wale waombolezaji wengine, nikasimama chini ya mwembe uliokuwa jirani, donge kubwa likiwa limeniganda kooni.

“Kijana, wewe ni nani na hapa umefuata nini?” sauti nzito ya mwanaume nisiyemjua ndiyo iliyonizindua kutoka kwenye hali ile, harakaharaka nikajifuta machozi na kugeuka kumtazama.

Alikuwa ni mwanaume wa makamo, mweusi tii, akiwa na macho mekundu sana, huku mishipa mingi ikiwa imesimama kwenye kichwa chake. Kabla ya kumjibu, haraka sana nilimtazama kwenye mikono yake. Cha ajabu, nilimuona akiwa ameweka ile ishara kama ambayo baba alinifundisha, alikuwa ameziba kucha ya kidole chake kidogo kwa dole gumba.

Alipoona nimekazia macho kwenye mkono wake, aliuficha kwa nyuma kisha akarudia tena kuniuliza swali lake.

“Usimjibu chochote, mkazie macho usoni,” nilisikia sauti ya baba, nikafanya kama alivyoniambia. Japokuwa alikuwa na sura ngumu, nilijikakamua kisabuni nakumkazia macho usoni, akashtuka kuona namtazama machoni.

Cha kushangaza, na yeye aliponikazia macho kwa sekunde kadhaa na kurudia tena kuniuliza swali lile, alipoona bado nimekomaa kumtazama machoni, aliachia vile vidole vyake alivyokuwa amevibana, akawa ni kama anababaika machoni maana hakuweza tena kunitazama machoni.

“Usifikiri watu wote hapa ni wajinga, kwa usalama wako ondoka haraka,” alisema kwa sauti ya kukwamakwama lakini sikumjibu chochote zaidi ya kuendelea kumkazia macho, nikamuona akiufyata mkia na kugeuka, akatembea harakaharaka na kwenda kujichanganya na wenzake.

Nikiwa bado namtazama, alipokaa tu niliona wazee wengine kadhaa ambao walikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakinitazama kwa macho ya ukali wakimfuata pale alipokuwa amekaa, wakawa wanazungumza kisha nikaona wote wamegeuka na kunitazama.

“Iweke hiyo hirizi chini ya ulimi na kimbia haraka uwezavyo kuondoka eneo hilo kabla hawajakufikia,” sauti ya baba ilisikika tena masikioni mwangu. Harakahara nikaingiza mkono mfukoni na kuitoa ile hirizi, japokuwa ilikuwa kubwa niliingiza mdomoni na kuibana chini ya ulimi.

Kabla hata sijamaliza kufanya kitendo hicho, nilishtukia lile kundi la wale wazee likija kwa kasi pale chini ya mwembe, nikageuka haraka na kuanza kutimua mbio, sikuwa naijua mitaa ya Mlandizi lakini kwa jinsi baba alivyoongea kwa msisitizo na hali halisi ilivyokuwa, nilijua nikilemaa, kweli nitaadhirika.

Kila mtu alibaki amepigwa na butwaa pale msibani maana ilikuwa ni zaidi ya kituko, nilitimua mbio ambazo sikumbuki kama nimewahi kukimbia maishani mwangu, nikawa nakatiza mitaani huku watu wengine wakishtuka wakidhani labda nilikuwa mwizi, kwa nyuma nikawa nasikia kelele kwa wingi kuonesha kwamba wale watu walikuwa wameniungia tela.

Sikujua nini kitanipata endapo watanitia mikononi na kugundua kwamba mimi ndiye niliyesababisha kifo cha yule mtoto huku mama yake akiwa mahututi, na kusababisha watui wote wawe na huzuni kiasi kile.

Sijisifii lakini ukweli ni kwamba katika suala la mbio, nilikuwa na uwezo mkubwa sana, dakika chache baadaye nikawa nimeshatokomea kwenye mashamba ya mikorosho na minazi, kelele za wale watu waliokuwa wakinifukuza zikiwa bado zinaendelea kusikika, sauti ya baba ikasikika tena masikioni mwangu lakini safari hii, ilikuwa na maelezo ambayo yalinimaliza kabisa nguvu, nikajua mwisho wangu umewadia. Niliujutia sana uamuzi wangu wa kujipeleka mwenyewe kwenye mdomo wa mamba.

Je, nini kitafuatia?
 
Sehemu ya 50


ILIPOISHIA:

Sijisifii lakini ukweli ni kwamba katika suala la mbio, nilikuwa na uwezo mkubwa sana, dakika chache baadaye nikawa nimeshatokomea kwenye mashamba ya mikorosho na minazi, kelele za wale watu waliokuwa wakinifukuza zikiwa bado zinaendelea kusikika, sauti ya baba ikasikika tena masikioni mwangu lakini safari hii, ilikuwa na maelezo ambayo yalinimaliza kabisa nguvu, nikajua mwisho wangu umewadia. Niliujutia sana uamuzi wangu wa kujipeleka mwenyewe kwenye mdomo wa mamba.

SASA ENDELEA…

“Inabidi uvue nguo zote na kukimbia kuelekea upande wa Magharibi mpaka uvuke barabara ya lami kisha kimbia mpaka utakapoukuta mti mkubwa wa mbuyu, uzunguke mara saba kisha fumba macho, usifumbue mpaka nitakapokwambia,” sauti ya baba ilisikika masikioni mwangu.

Yaani nivue nguo zote na kuanza kukimbia nikiwa mtupu? Kibaya zaidi, upande huo wa Magharibi aliokuwa anausema ilikuwa ni kulekule nilikokuwa nakimbia. Kwa lugha nyepesi nilitakiwa kuanza upya kukimbia kurudi kule nilikotoka, safari hii nikiwa mtupu! Ilikuwa ni zaidi ya mtihani.

Kitu pekee nilichokuwa nakihitaji, ilikuwa ni kuokoa na balaa hilo kwani kwa jinsi wale wazee waliokuwa wakinikimbiza walivyokuwa na hasira, kama wangenitia mikononi mwao sijui nini kingetokea. Ilibidi nipige moyo konde, harakaharaka nikavua nguo zote na viatu, nikavikunja na kuvitia kwapani.

Mpaka namaliza, lile kundi lilikuwa limenikaribia sana, kitu pekee ambacho nilikuwa nacho makini, ilikuwa ni kuifunga vizuri ile hirizi yangu mkononi, nikaanza kukimbia kulifuata lile kundi huku nikiwa na hofu kubwa mno moyoni.

Cha ajabu, japokuwa nilikuwa nikikimbia kuelekea kule walikokuwa wanatokea, tena nikiwa mtupu kabisa, ilionesha dhahiri kwamba hakuna aliyekuwa akiniona kwani waliendelea kuangaza macho huku na kule huku wakiendelea kukimbia. Nikawafikia na kupishana nao katika namna ambayo nilikuwa makini kuhakikisha simgusi yeyote wala wao hawanigusi kama baba alivyonieleza.

>> Usiache kutembelea Simulizi za Majonzi kwa hadithi na simulizi kali!

“Hebu simameni kwanza, mbona nywele zinanisisimka hivi?” mmoja kati ya wale wazee. Nadhani yeye alihisi uwepo wangu mahali hapo, wote wakafunga breki na kusimama, wakawa wanatazama huku na kule lakini walishachelewa kwani nilizidi kutimua mbio kama kiberenge.

Nikakwepa kidogo pale kwenye msiba na kupita pembenipembeni kwa kasi kubwa, kizaazaa kikawa kuvuka barabara ya lami. Ikumbukwe kwamba kote huko nilikokuwa napita, japokuwa ilikuwani asubuhi na kulikuwa na watu, ilionesha dhahiri kwamba hakuna aliyekuwa akiniona ingawa mimi nilikuwa nawaona vizuri.

Nilipofika barabarani, kuna pikipiki ilikuwa ikitokea upande wa Morogoro, sikuiona mapema, ile nimeshaingia barabarani ndiyo nikaishtukia ikiwa inakuja kwa kasi kubwa, nikajua kama nisipokuwa makini, inaweza kunigonga na kwa kasi iliyokuw anayo, sijui nini kingetokea.

Nilichokifanya, nilijirusha juu, nikashangaa mwili umekuwa mwepesi sana, nikamruka yule dereva na bodaboda yake lakini kwa bahati mbaya, mguu mmoja nilimgonga kichwani, nikaenda kuangukia ng’ambo ya pili ya barabara na kuinuka haraka, nikataka niendelee kutimua mbio lakini ghafla nilishtushwa na kishindo kizito barabarani.

Ilibidi nijiibe na kugeuza kidogo shingo kwa sababu miongoni mwa masharti niliyoelekezwa na baba, ni mwiko kugeuka nyumaunapokuwa kwenye shughuli zinazotumia nguvu za giza. Nilimshuhudia yule dereva wa bodaboda akiwa ameanguka katikati ya barabara na kujibamiza kwa nguvu.

Nilishtuka sana, nikajua kwa vyovyote mimi ndiyo nimesababisha kwa sababu hata kama yeye hakuwa ameniona, mimi nilimuona na ndiyo maana nilimkwepa lakini kwa bahati mbaya, nikamgonga kichwani. Kilichonitisha zaidi, ni kasi aliyokuwa nayo na uzito wa kishindo chenyewe, nikajua tayari mambo yameshaharibika.

“Mungu wangui, hawezi kupona yule,” nilisikia sauti za mmoja kati ya waombolezaji waliokuwa pale kwenye msiba kwa sababu tukio hilo lilikuwa limetokea mita chache tu pembeni, hasa ukizingatia nilishaeleza kwamba nyumba yenye msiba ilikuwa karibu na barabarani.

Waombolezaji wengi walikimbilia eneo la tukio kujaribu kutoa msaada lakini wengi walisikika wakisema kwa jinsi alivyokula mzinga hawezi kupona. Nilitamani kwenda kushuhudia kilichotokea lakini kwa sababu na mimi nilikuwa na majanga yangu, niliendelea kukimbia. Nilikimbia sana, miba mikali ikinichoma miguuni lakini sikujali.

Mbele kabisa nikauona mbuyu mkubwa kama baba alivyonielekeza, nikaendelea kukimbia mpaka nilipoufikia, nikaanza kukimbia kuuzunguka kutokea upande wa kushoto kuelekea kulia. Nilipofikisha raundi ya saba, nilisikia kizunguzungu kikali, nikadondoka chini kisha nikaona kama giza nene likitanda kwenye upeo wa macho yangu, sikuelewa tena kilichoendelea.

“Wewe Togo, hebu amka,” sauti ya chini ya baba iliyoambatana na teke zito ubavuni ndiyo iliyonizindua kwenye usingizi wa kifo, nikafumbua macho na kushtuka nikiwa nyuma ya nyuma ya akina Rahma, tena nikiwa uchi wa mnyama.

“Vaa nguo haraka, unajifanya mjuaji sana wewe, siku nyingine sikusaidii, pumbavu,” alisema baba huku akiniongezea teke lingine la ubavuni lililosababisha nijisikie maumivu makali.

Niliijizoazoa huku nikijiziba sehemu za mbele kwa mikono yangu, nikaokota nguo zangu zilizokuwa pembeni na kuanza kuvaa huku nikijiuliza nimefikaje nyumbani bila kupata majibu.

“Sijui kwa nini nimeenda kukuandikisha mtu mjinga kama wewe,” alisema baba kwa hasira huku akinishika masikio yangu mawili na kuyavuta kwa nguvu, akiwa ni kama anataka kuninyanyua juu, akanisindikizia na kofi zito lililosababisha nishindwe kujizua, machozi yakawa yananitoka.

Zilikuwa zimepita siku nyingi sana bila baba kunipiga lakini naona siku hiyo nilikuwa nimemuudhi sana, nikawa nahisi kama masikio yangu yananyofoka kwa jinsi alivyoyavuta kwa nguvu, na ule upande alionizabua kofi nao nikawa nahisi kama unawaka moto.

“Chumbani moja kwa moja na ole wako utoke,” alisema baba kwa hasira, nikatembea harakaharaka huku machozi yakinitoka, uso wangu nikiwa nimeuinamisha. Ile naingia tu mlangoni niligongana na Rahma lakini kwa kuwa nilikuwa nalia na akili ilikuwa na mawenge, sikukumbuka hata kumsalimu, nikatembea harakaharaka huku nikichechemea kwani miguu ilikuwa na miba ya kutosha na sikuwa nimepata hata muda wa kuitoa.

Niliingia chumbani na kujilaza kitandani nikiwa bado najiuliza nimefikaje eneo hilo, nikalia kwanza kupunguza hasira zangu kisha nikaanza kutafakari kwa kina mlolongo wa kila kitu kilichotokea. Yaani ndani ya saa chache tu kulikuwa kumetokea matukio mengi mno ya kutisha, ya kuhuzunisha, ya kushangaza na kuchanganya kichwa.

Bado moyo wangu ulikuwa na huzuni kubwa kutokana na hali niliyoiona kule msibani, na japokuwa malengo yangu ya kwenda Hospitali ya Tumbi kuona hiyo maiti ya yule mtoto hayakuwa yamekamilika, bado nilikuwana shauku kubwa ya kutaka kujua kilichotokea. Lakini ni hapo pia nilipokumbuka ile ajali nyingine ya bodaboda niliyoisababisha na pia nikakumbuka kisanga cha dereva wa Bajaj aliyekuwa akipaki jirani na hapo kwa akina Rahma na jinsi nilivyomkomesha asubuhi hiyo. Sikujua kama amesharudi au la na sikujua siku atakaponiona tena atasema nini.

Nikiwa nimezama kwenye dimbwi la mawazo, nilisikia mlango ukifunguliwa, Rahma akaingiza kichwa na kuchungulia ndani, macho yangu na yake yakagongana.

Je, nini kitafuatia?
 
Iweke tuione…..
Jiongeze nenda Google itafute 'Makaburi ya wasio na hatia' utaiona hadi ilipoishia (Sehemu ya 66).

Ilianziaga kule Global publishers kisha ikaletwa humu 2017. Ila haikufikaga mwisho

 
Jiongeze nenda Google itafute 'Makaburi ya wasio na hatia' utaiona hadi ilipoishia.

Ilianziaga kule Global publishers kisha ikaletwa humu 2017. Ila haikufikaga mwisho


Thanks
Kumbe nayo haikuisha. Labda Mwamba ataleta hadi hitimisho
 
Story imetoka kwenye uchawi mpaka kuto.mbana [emoji1787][emoji1787][emoji1787]
 
Mpaka sehemu ya 21 sijui huyu bwana togolani anaumri gani miaka 9 15 au 20
 
Kutoka uganga mpaka uchawi this is the biggest plot twist.. Mpaka hapa sijui nani mbaya episodi ya 34 [emoji23][emoji23][emoji23]
 
Back
Top Bottom