HADITHI: BADO NINAISHI (ASHRAFU NDILO JINA LANGU)
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+
SEHEMU YA AROBAINI NA NANE
"Na vijana ambao nilikuwa nahitaji uniletee umekuja nao?"
"Ndiyo mkuu, nimekuja na wanaume wa kazi haswa sita"
"Safi mimi na wewe tutapanga muda mzuri wa kuweza kuonana ila hakikisha kwanza kesho unakutana ana kwa ana na vijana wote wakujue ili ujue kampuni inaendaje kisha nitahitaji ripoti yako"
"Sawa bosi" simu ilikatwa raisi akiwa anatabasamu kwa sababu watu ambao alikuwa anawahitaji sana tayari walikuwa nchini, aliona ni muda mwafaka wa yeye kuanza kuyakamilisha mambo yake kwa ukubwa sana bila kujulikana.
Mwanaume huyo ambaye alikuwa amefika muda mfupi tu uliokuwa umepita, aliitoa simu yake na kuipiga kwa katibu mkuu kiongozi wa Tanzania usiku huo. Aliipokea simu hiyo kwa mara ya kwanza ikiwa ndani ya taifa la Tanzania maana alikuwa amezoea kuipokea ikiwa nje ya nchi.
"Bosi"
"Nipo Tanzania. Kesho waite vijana wote tutakuwa na kikao na mimi nitakuja moja kwa moja wote mnifahamu"
"Sawa bosi japo imekuwa ghafla sana"
"Kuwa ghafla sio shida, nataka uandae majibu kwamba ni kwanini mpaka sasa masuala madogo kama haya umeshindwa kuyaweka sawa mpaka nimelazimika kuja mwenyewe, halafu ulivyo na akili fupi huoni shida raisi wako kuchafuliwa huku unajua kabisa kwamba wewe ndo utakuwa mtu wa kwanza kunyooshewa kidole kitu ambacho kitaifanya kampuni yetu kuweza kuingia kwenye matatizo huku wewe ukinenepa tu na kubadilisha wanawake"
"Naomba unisamehe sana kiongozi, hili nitaliweka sawa nipe nafasi nyingine"
"Maisha hayakupi nafasi nyingi hivyo Gedfrey, maisha haya ni mafupi sana hivyo ukifanya makosa mengi inatakiwa ufundishwe namna sahihi ya kuitumia kila nafasi ambayo unakutana nayo"
"B....." kabla hajajibu simu hiyo ilikatwa, bosi wake ambaye alikuwa anaishia kuwasiliana naye kwenye simu tu alikuwa nchini, kwake ilikuwa ni habari mbaya sana kwa sababu kuna uzembe mkubwa mno ambao ulikuwa umefanyika na yeye ndiye ambaye alikuwa nyuma ya huo uzembe hivyo kukutana na kiongozi huyo moja kwa moja ilikuwa inamletea mazingira magumu sana hasa kwenye kumshawishi ili aweze kumuelewa.
Alihisi kuchanganyikiwa, akaanza kupiga simu kwa vijana wake wote watano ambao ndio walikuwa wanaufanya muunganiko wa kampuni hiyo uweze kuwa mkubwa, aliwapigia wanne na kuwapata taarifa za ujio wa mtu mkubwa zaidi kwenye kampuni wa juu yake, habari ambayo huenda iliwashtua sana wenzake lakini yeye ndiye alishtuka zaidi yao na taarifa zingine ambazo zilimpa sana wasiwasi ni baada ya kusikia kwamba mmoja ya wanaume hao watano hakuwa akipatikana. Ulimboka ndiye mtu ambaye alishindwa kumpata wakati huo ili kumpa taarifa hiyo ili keshoyake asije akakosekana kuwepo.
Kushindwa kumpata mwanaume huyo hewani ilikuwa sababu nzuri kabisa ya kumpigia Justin na kumtaka yeye na vijana wake wakamchukue mtu huyo kama sio kumpatia taarifa kuhusu kikao kikubwa ambacho kingefanyika kesho yake. Justin aliwachukua wanaume wanne jumla wakawa watano ili kuelekea Tabata sehemu ambako alikuwa anaishi mwanaume huyo Ulimboka.
Walitumia dakika arobaini kuweza kufika sehemu hiyo ila walicho kutana nacho kiliwashangaza sana kwani geti la kuingilia ndani lilikuwa wazi. Ndani ya uzio kulikuwa na mijengo minne mikubwa hivyo walianza kuzunguka kila jengo lakini walicho fanikiwa kukutana nacho ni miili ya watu ambayo ilikuwa imeuliwa kikatili sana kila sehemu. Walifanikiwa kuingia kwenye kila nyumba hawakufanikiwa kumkuta mtu wao zaidi ya familia yake mke na watoto wawili ambao walikuwa wamefungiwa chumbani tu. Justin alipiga simu kwa katibu mkuu kiongozi kumpa taarifa hiyo.
"Amechukuliwa"
"Na nani?"
"Hakuna mtu ambaye anaonekana, mke wake anasema alihisi kuna mtu alikuwa nyuma yake kisha hakuelewa kilicho tokea na alipokuja kuzinduka alikuwa yupo chumbani na watoto hakujua nini kilitokea huko nje. Walijaribu kupiga simu mtandao haukuwepo na walifungiwa nje hivyo wakawa hawana cha kufanya"
"Hakuna kamera ili uweze kujua kwamba ni nani alikuwa hapo?"
"Kamera zote zilizimwa, ni wazi mhusika alikuwa anajua alichokuwa anakifanya"
"Namtafuta kijana mmoja serikalini ambaye ni mdukuzi bora sana japo ni mtu wa siri, mumtafute mtoa gazeti la UKWELI WANGU WA SIKU na uhakikishe anapatikana, huyu ndiye atakuwa nyuma ya kila kitu"
"Nimekuelewa bosi nitahakikisha anaingia kwenye mkono wangu"
"Justin do it" aliongea kwa hasira akiwa anaikata simu, wanaume hao waliifungulia familia hiyo na kuondoka nayo hapo ndani huku katibu mkuu kiongozi akionekana wazi kuchanganyikiwa maana kesho yake kulikuwa na kikao kizito sana na alikuwa na mambo mengi ya kujibu lakini wakati huo huo tena akawa amefanya uzembe mwingine wa kupotea kwa mtu wao mmoja ambaye ni Ulimboka, hilo lilikuwa ni jambo jingine kabisa.
SAA MOJA NYUMA.
Ashrafu alikuwa na namba ya nyumba pamoja na sehemu ambayo alikuwa ameelekezwa na Benard Taradadi mmiliki wa benki za TUNAKUWEZESHA jinsi ya kumpata mtoto wa Bruno Josephat ambaye mpaka wakati huo hakuwa anajua kwamba tayari alishakufa kwa kuuawa na raisi ili kumlinda huyo binti yake.
Mwanaume usiku wa manane kabisa jiji likiwa limetulia ndio wakati ambao aliona ni sahihi kuweza kuifanya kazi yake. Nafsi ya huruma ilikuwa imemtoka kwenye moyo wake wakati huo maana aliona anapoteza muda tu kwa mambo ambayo alitakiwa kuyamaliza mapema sana.
Tabata kwa wala bata kama ambavyo huwa wanapaita ndipo alifanikiwa kupatembelea usiku huo akiwa taratibu kwenye gari yake ya Vx nyeusi tii. Mwendo wake haukuwa mkali sana kwa sababu hakutaka kuwashtua watu kabisa hususani wale ambao walikuwa wanakula bata kwenye sehemu za starehe. Aliishia Tabata Kimanga sehemu moja ambayo zilijitenga nyumba kadhaa ambazo zilikuwa zimejengwa kwa ubora mkubwa sana, bila shaka walijitenga watu ambao walikuwa na uwezo wa kumudu vyema milo yao bila wasiwasi.
Alishuka ndani ya gari yake akiwa amevaa nguo nyeusi ambazo zilikuwa zinamfunika kila sehemu mpaka kichwani, ni macho tu ndiyo yalikuwa yanaonekana. Alizunguka nyuma ya jengo la kwanza, akatembea kidogo akiwa makini sana kuangalia namba za nyumba na baada ya muda kidogo alikutana na nyumba ambayo alikuwa anaitaka akiwa anaiangalia kama mita hamsini mbele yake. Aliivuta simu mfukoni na kuibonyeza mara kadhaa ambapo kwenye ile nyumba umeme ulizima ghafla kisha ukawaka tena na wakati unawaka kwa mara ya pili kamera zote zilikuwa zinazima. Mwanaume alivaa gloves mikononi na kusogea getini ambapo aligonga geti kwa nguvu sana kisha akakimbilia upande wa pili ambapo alijivuta juu ya ukuta na kutua ndani nyuma ya jumba moja.
48 NAWEKA NUKTA.