HADITHI: BADO NINAISHI (ASHRAFU NDILO JINA LANGU)
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+
SEHEMU YA AROBAINI NA NNE
Aliisogelea self ya kuhifadhia silaha yake na kuitoa kisha akaielekeza kwenye sofa moja kubwa ambalo alihisi kulikuwa na mtu kwani kwa ukubwa wake ukiwa nyuma usingeweza kumkuona kabisa mtu ambaye alikuwa mbele yake.
“Clara, sijui nikuite Anelia?” aliisikia sauti nzito ambayo alikuwa anaijua sana kwenye maisha yake. Haikuwa sauti ngeni kabisa kwake hivyo haraka sana alimjua mhusika na mmiliki wa hiyo sauti.
“Unatafuta nini kwangu na umeingiaje hapa Remy?’’
“Hiyo ndiyo salamu?”
“Usijifanye unajali salamu wakati hauna hata muda nazo. Nilipo sikia kwamba kuna mambo unayafanya kihuni nilishangaa sana lakini nilipo sikia umefanikiwa kutoroka kwenye gereza nilishangazwa zaidi na hizo taarifa kwa sababu sikuamini wala kufikiri mtu kama wewe unaweza kuwa zaidi ya vile nilivyokuwa nimekutegemea”
“Ulitamani sana kuniona nikifia gerezani kwa ile miaka sitini niliyo hukumiwa sio? Hilo nalijua, hakuna kitu ulikuwa unajali kuhusu mimi” mwanaume huyo aliongea akiwa anasimama na kuanza kusogea kule alikokuwepo Anelia ambaye alikuwa bado amemnyooshea bastola yake.
“Usisogee nitakuua Remy”
“Najua huwezi kufanya hivyo, hauna huo ujasiri” mwanaume alimjibu akiwa anaendelea kumsogelea taratibu.
“Stoooooop!” aliongea kwa nguvu lakini bado mwanaume aliendelea kumsogelea tu hali ambayo ilimfanya kuruhusu risasi zitoke kuelekea kwa Remy ila aligundua kwamba bastola hiyo haikuwa na risasi, alihisi labda ni presha ilimfanya asifanye hilo jambo kwa usahihi lakini hata baada ya kuikagua na kuziruhusu tena ndipo aligundua kwamba bastola hiyo haikuwa na risasi hata moja.
Mwanaume aliunyoosha mkono wake na kuzimwaga risasi sita sakafuni akiwa ameunyoosha mkono wake.
“Hili nilikuwa nalijua kwamba unahitaji sana kuweza kuniua hasa baada ya kuthibitisha kwamba kila kitu kuhusu mimi na wewe kilikuwa ni maigizo kama wewe mwenyewe ulivyokuwa unaniigizia mwanzo. Sijaja hapa ili kupoteza muda wangu kujadili mapenzi ya uongo ambayo yalikuwepo baina yetu hivyo njoo ukae unisikilize kisha mimi niondoke zangu” alitamka akiwa anasogea kwenye sofa akaketi na kuitoa bastola yake akaiweka mezani hali ambayo ilimfanya Anelia kusita sita sana kusogea kukaa lakini mwanaume huyo aliligundua jambo hilo.
“Kama ningekuwa nahitaji kukuua, ningekuua muda mrefu tu mpaka sasa hata mwili wako ungekuwa umepoa, nina muda mfupi mno wa kukaa hapa” ikamlazimu mwanamke huyo kusogea kwenye sofa akiwa na wasiwasi sana kwenye nyumba yake mwenyewe.
“Wewe ni nani Remy?”
“Unalitaja jina langu halafu unaniuliza mimi ni nani?”
“Najua hili sio jina lako”
“Hahahah hahaha inanishangaza sana, haunijui jina langu wakati bosi wako anayajua majina yangu yote matatu?”
“Whaaaat?”
“Kama kiongozi wako anakutuma kufanya kazi za hatari za kumtafuta mtu kama mimi basi anatakiwa pia kukupatia maelekezo yote ya mhimu kwa sababu wakati mwingine sitakupa nafasi nyingine ya kuishi”
“Unamaanisha kwamba bosi anajua kila kitu kuhusu wewe?”
“Nikisema kila kitu nitakuwa namuonea kwa sababu ni mtu mmoja tu ambaye anajua kila kitu kuhusu mimi kwenye dunia hii kwa watu ambao wapo hai ila bosi wako anajua ukweli wa maisha yangu kwa kiasi kidogo na hata sababu ya msingi ya mimi kufanya haya anaijua, ni kwa sababu tu hataki kukubaliana na ukweli kwamba hawezi kunizuia kukamilisha kile ninakitaka mimi”
“Unahisi kwamba unaweza kufanya lolote kwenye hili taifa sio?”
“Huenda jibu likawa ndio”
“Kwa mkono wangu nitakuua Remy, hii ni ahadi ambayo nimejiwekea kwenye maisha yangu na siwezi kufa kabla sijaitimiza”
“Kila kinywa huwa kinajiwekea ahadi nyingi sana ila ni ngumu sana kuweza kuzitimiza. Labda nikuulize swali rahisi sana, kwangu ulikuja kunipeleleza na sio kwa mapenzi kama ulivyo nidanganya sasa ni sababu gani inayokufanya uhitaji kuniua?”
“Kwahiyo unajifanya haujui Remy?”
“Ningekuwa naijua basi nisingekuuliza”
“Hivi uliwahi hata mara moja kunifikiria kama mwanamke wako kwenye moyo wako?”
“Punguza kuwa mwigizaji, you don’t give a damn about that love, haya yote yanatoka wapi?”
“Hilo unalisema wewe, lakini haujui ni kipi mimi nimekipitia kipindi nipo mwenyewe”
“Wewe ni bora sana kwenye upande wa maigizo na naona umeasha anza tena kuniigizia. Jambo unalotakiwa kulifahamu ni kwamba kila kitu nilikuwa nakijua tokea mwanzo na nilijua kabisa kwa hali yangu lazima wangehitaji kumtumia mwanamke kama wewe. Kukuruhusu wewe kuwa daktari wangu na baadae kuwa mpenzi wangu huo ulikuwa ni mpango wangu mwenyewe kwa sababu mtu ambaye nilikuwa namtaka nilipata taarifa kwamba yupo gerezani na anahitaji msaada ila mtu wa kumsaidia hakuwepo. Ilikuwa ni nafasi yangu bora sana kuweza kukutana na huyo mtu ili niweze kuujua uhalisia wake na umoja wao ambao mimi nimekua nikilala na kuota ndoto mbaya sana nikitamani siku moja kuweza kukutana nao”
“Njia pekee ya mimi kuweza kufika kule gerezani ilikuwa ni kuwa mhalifu ili nikamatwe na makosa makubwa ili nifanikiwe kuingia jela ambako nilifanya matukio ya kutisha yaliyo nipeleka kwenye lile gereza na nimefanikiwa kukutana na huyo mtu tayari hivyo sikuona haja ya kuendelea na maisha ya kuishi gizani kama zamani tena kwa sababu naanza kumpoteza mmoja mmoja. Kwahiyo kama ulijiona mjanja sana kwa kuona umeniingiza mtegoni basi nikupe pole na asante sana kwa kufanikisha kunisaidia mimi kulikamilisha zoezi hili kwa wepesi sana tofauti hata na nilivyokuwa nimetegemea”
“Je mpaka hapo bado unatamani kunifahamu kwamba mimi ni nani Anelia?” mwanamke huyo alikuwa anashangaa namna mwanaume huyo alivyokuwa bingwa kwa kamari ngumu kama hizo kwenye huu ulimwengu.
“Kwahiyo umekuja kuniua?”
“Nimekwambia mapema ningehitaji kukuua kwangu ilikuwa ni kazi rahisi sana hivyo mpaka sasa ungekuwa umekufa ila halijanileta hilo hapa leo. Kuna kitu kimenileta mbali na haya” alikuwa anaonyesha hasira za wazi Anelia ila hakuwa na la kufanya hivyo Ashrafu aliendelea;
“Kwenye haya maisha ya mimi na wewe, hesabia kwamba hatujawahi kukutana, yaani wakati ambao ulikuwepo baina yangu mimi na wewe ufute kwenye kumbukumbu za maisha yako. Usije ukajitokeza tena kwenye njia zangu hata siku moja kwa sababu nitakuua mwenyewe kwa mkono wangu”
44 NAWEKA NUKTA HAPA.