HADITHI: BADO NINAISHI (ASHRAFU NDILO JINA LANGU)
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+
SEHEMU YA ISHIRINI NA NANE
“Ni taarifa za mhimu sana ambazo hazitakiwi kulala kabisa”
“Nakupa dakika kumi na tano uwe ofisini hapa”
“Sioni kama ni vizuri tukiongelea ofisini mheshimiwa, kama itakupendeza tukutane nje ya Ikulu”
“Ok. Tukutane Kawe” alitaja eneo hilo kwa sababu halikuwa mbali sana na kule ambako alikuwa anaelekea yeye.
Ndani ya nusu saa tu alikuwa amefika hiyo sehemu ambapo walinzi walishuka kwenye gari na mkurugenzi ambaye naye alikuwa na vijana wake alisogea na kuingia kwenye gari hiyo ambayo alikuwepo raisi.
“Vipi kusumbuana na usiku huu na nimekwambia kuna ratiba zangu binafsi ambazo natakiwa kuzikamilisha. Kuna jambo gani haswa unataka kuniambia”
“Remy ametoroka gerezani”
“Whaaat the f**k”
“Ametoroka asubuhi ya leo”
“Hilo ni jambo ambalo haliwezekani”
“Nimeenda mwenyewe kuhakikisha nimegundua hilo lakini kuna mambo ambayo yanaendelea kule ndiyo yamepelekea jambo hilo litokee”
“Yapi?”
“Bruno Josephat alikuwa kule gerezani”
“Nadhani unanitani sio”
“Hapana mheshimiwa huo ndio uhalisia”
“Bruno anatafuta nini kule na alifungwa kwa ruhusa ya nani?”
“Mkuu wa gereza”
“Luka Gambino?”
“Ndiyo mkuu”
“Hahahah hahahaah hhahaha mpuuzi mkubwa huyu, sababu gani imemfanya afanye hayo yote?”
“Inaonekana kwamba amelipwa pesa nyingi sana”
“Sababu ni ipi hasa mpaka Bruno alipie pesa nyingi kwenda kufungwa?”
“Inaonekana kuna uhusiano mkubwa sana kuwepo kwake kule na Remy kutoroka”
“How?”
“Kabla ya wewe kwenda gerezani kuongea na Remy alikuwa amekutana na Bruno hivyo kuna makubaliano inadaiwa kwamba wameingia na Bruno ndiye amamesaidia Remy kutoroka kule”
“Hizi taarifa wewe umezipatia wapi?”
“Henry alihisi hili jambo mapema nikampa ruhusa ya kulifuatilia hilo hivyo akawa amemuingiza kijana wake mmoja kule gerezani ambaye ndiye amatuletea majibu na taarifa za kutoroka kwa mtu huyo”
“Umefanya maamuzi yapi?”
“Mpaka sasa gereza lipo kwenye usimamizi wangu, Luka Gambino na Bruno wapo kwenye mkono wangu kwa ajili ya mahojiano sema sikuona kama ni ustaarabu kulikamilisha hili bila ruhusa yako”
“Ametoroka gerezani mtu ambaye zimefanyika jitihada kubwa kumpata, mtu ambaye ameua watu wengi sana na kutupotezea pesa nyingi sana halafu kiwepesi tu hawa wajinga wanamtorosha gerezani? Wahoji kwa namna yoyote ile mpaka waseme ukweli wote ambao wanaukumbatia, kesho mimi nitakuja kwa ajili ya kuipata ripoti kwako ila hakikisha hawafi kwa sababu na mimi nitakuwa na mazungumzo nao binafsi hasa Bruno huyu namhitaji sana”
“Sawa bosi”
“Na kuhusu Remy kuna taarifa gani’’
“Muda huu naenda kwenye kikao na vijana wangu, usiku huu huu wanaanza kazi ya kumtafuta”
“Apatikane haraka sana namhitaji, halafu hakuna taarifa zozote zile kuhusiana na hawa wapumbavu ambao wameniharibia sana jina langu kwa hilo gazeti lao la kipumbavu”
“Yote kesho nitakupa majibu kiongozi”
“Nawahitaji hawa watu, unatakiwa kuelewa kile nakwambia kwenye kinywa hiki usiku huu kwamba namaanisha sana”
“Sawa bosi” maelezo yake yalikuwa yametosha hivyo alishuka lakini mheshimiwa raisi alibaki ametulia kwanza maana kila muda ulivyokuwa unazidi kwenda mambo yalikuwa yanazidi kuwa mengi sana. Aliitoa simu yake na kuipiga mahali;
“Kesho nakuhitaji uwepo Tanzania mapema sana” ilikuwa ni amri kisha akaikata simu hiyo na kuamuru vijana wake wamuwahishe kwenda kukutana na mlimbwende Anelia Baton.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kabisa kwenye maisha yake Anelia kuingia sehemu ya kifahari sana kama hiyo, jumba la kifahari la mheshimiwa raisi lilikuwa limepambwa kwa vito vya thamani ambavyo hakuwa na imani kama kuna mahali alipata kuviona, alishangaa jinsi viongozi hao wakubwa wa taita walivyokuwa wanaliingiza taifa kwenye hasara kubwa sana namna hiyo ya kutumia vitu vya gharama huku watoto wakiwa hawana hata viti vya kukalia kwa ajili ya masomo yao.
“Karibu sana malkia, umeipendezesha sana hii nyumba leo” mzee huyo aliongea akiwa anafurahia sana ujio wa mrembo huyo.
“Asante sana mheshimiwa, nimefurahi sana kuweza kupata mwaliko wako ndani ya sehemu nzuri na salama sana kama hii”
“Unajua kuwa raisi ni moja kati ya kazi ngumu sana ambazo watu wengi hawazijui, akili yako inabidi iwe inafanya kazi kwa masaa ishirini na manne kwa sababu maamuzi yako yanakuwa yamebeba hatima ya maisha ya watu wengi sana, ukikosea kidogo tu unawaumiza wengi hivyo kuna muda inakuwa ni vyema ukiwa na sehemu iliyo tulia kama hii kwa ajili ya kutuliza akili”
“Unalo liongea ni sahihi kabisa mheshimiwa lakini sijaelewa lengo hasa la sisi kuweza kukutana hapa”
“Hahaha hahaha Anelia mbona unaniuliza swali la kitoto sana, au unahisi kwamba naweza kukuumiza?”
“Sina maana hiyo mheshimiwa, sio rahisi sana mtu wa kawaida kama mimi kukaribishwa kwa heshima kubwa sana namna hii tena na raisi huenda kuna jambo ambalo labda natakiwa kulifanya na mimi silijui”
“Unapenda kuishi hivyo mpaka siku unakufa Anelia?”
“Hapana mheshimiwa”
“Kweli kwa mwanamke mrembo kama wewe sio vizuri sana kila siku ukawa unapishana na risasi mitaani huko, unatakiwa kupata muda wa kuuweka vyema urembo wako”
“Unamaanisha nini mheshimiwa?”
28 inafika mwisho.