HADITHI: BADO NINAISHI (ASHRAFU NDILO JINA LANGU)
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+
SEHEMU YA ISHIRINI
"Nahisi hata wazazi wangu hawakufa kifo cha kawaida, huenda kuna mambo nafichwa hapa hivyo nitamuuliza bosi kwa mara nyingine na kama asiponipa jibu la kueleweka basi kwenye hii kesi ya Remy ndio utakuwa mwanzo wangu wa kuchunguza kilicho tokea. Huu unakuwa mwanzo wangu mpya wa maisha mapya kabisa" alitamka kwa hasira sana akiwa anahitaji kuchunguza hata kifo cha wazazi wake maana machungu aliyo yapitia wakati huo alihisi kabisa kuna mkono wa mtu ulihusika moja kwa moja kwenye hilo. Mapenzi yalikuwa yanaleta kizaa zaa kipya mjini.
GEREZANI
Ulipita muda mrefu sana Remy akiwa kwenye kile chumba ambacho alikuwepo mpaka akawa amepitiwa na usingizi licha ya harufu mbaya ambayo ilikuwa mle ndani. Alikuwa na njaa kali sana kwa sababu ni muda mrefu ulipita bila kugusa chochote kile.
Alishtuka baada ya kumwagiwa maji ya baridi ndipo akakurupuka akiwa na uchovu wa hali ya juu sana. Wanaume wawili walimbeba na kuondoka naye ambapo walimpeleka kwenye chumba kingine ambacho kilikuwa ni kisafi sana tofauti na alichokuwa ametoka na kile ambacho alifikia mara ya kwanza.
Baada ya kufika ndani ya chumba hicho, alikutana na chakula ambacho kilikuwa kipo safi na wakati huo ilikuwa ni majira ya kuelekea jioni pembeni kukiwa na maji ya baridi. Hakuuliza wala kujiuliza mara mbili, kwanza aliyafakamia maji sana maana alikuwa na kiu mpaka midomo ilikuwa imekauka, baada ya kuyapata maji alianza kukishughulikia chakula huku nje wanaume wale wawili wakiwa wanaulinda mlango wake. Baada ya kumaliza kula mwanaume mmoja alitoa vyombo na kuondoka navyo akawa amebakia mmoja ambaye alikuwa amemnyooshea silaha.
Zilisikika hatua za watu zikiwa zinakuja sehemu hiyo hivyo akawa anatamani kujua kwamba ni nani ambaye alikuwa anakuja eneo hilo. Mbele ya nondo za chumba alicho kuwepo aliona sura ya mtu ambaye alimuona kwa mara ya kwanza humo gerezani wakati akiwa anateswa nje. Mtu huyo umri ulikuwa umeenda sana lakini alikuwa amenawiri isivyo kawaida kwa sababu ya maisha safi ambayo alionekana kuwa nayo japo haikuweleweka ni sababu ipi ambayo ilimfanya kuwepo sehemu kama hiyo wakati alionekana kuwa na nguvu sana ndani ya sehemu hiyo na angeweza hata kutoka kama angehitaji.
Wote walikuwa wanaangaliana kwa muda mpaka pale mzee huyo alipo amua kuingia ndani ya chumba hicho akiwataka watu ambao alikuwa amekuja nao ambao nao walikuwa na nguo za kifungwa kubaki nje kisha akawataka wote na mlinzi wasogee mbali kwani alikuwa na mazungumzo nyeti sana na mwanaume huyo ndani ya hicho chumba.
"Maisha ya mtaani ni tofauti sana na sehemu kama hii, sehemu ambayo mwanadamu huthaminiki tena, huku wewe ni sawa na mbwa tu hivyo ukiwa unaleta kiburi sana kwa hawa mabwana hawana hasara kukufanyia unyama wowote ule wala kukupoteza kwa sababu hakuna mtu atahoji wala kuuliza kuhusu wewe kufa au kuwa hai hivyo badala ya kuwaletea kiburi nadhani ungeamua kuishi nao kama wanavyo hitaji tu japo unaweza ukakaa kwa muda mfupi sana hapa ndani kama tutakuwa na mazungumzo mazuri mimi na wewe" mzee huyo aliongea akiwa anakaa mbele ya mwanaume huyo ili wafanya mazungumzo kwa kuonana ana kwa ana.
"Wewe ni nani hasa mpaka unajali mimi kufa au kuishi kwa shida sana ndani ya eneo kama hili?"
"Usiwe na haraka utanifahamu na utajua kwamba ni kwanini nakuhitaji uwe mzima kwa sababu naweza kuwa na matumizi na wewe makubwa sana"
"Nenda kwenye pointi ya msingi, unahitaji nini kwangu?"
"Nimefuatilia faili lako nimevutiwa sana na utendaji wako wa kazi na kwa jinsi unavyo ifanya kazi yako, lakini jambo kubwa zaidi ambalo limenivutia sana kwako ni ujasiri wako ambapo haupo tayari kutumikishwa na mtu yeyote yule na nilikuwa namtafuta sana mtu wa aina yako nahitaji tufanye kazi"
"Ndo tumeonana leo na unahisi unanijua?"
"Yeah, kuna namna watu wa aina yetu macho yetu tu huwa yanazungumza lugha moja hivyo ilikuwa ni rahisi tu kutambua kwamba mimi na wewe tunaweza kufanya kazi kwa pamoja na ikawa kazi kubwa na nzuri pia"
"Mimi sio mtu wa hivyo na wala hakuna kazi yoyote ile ya hatari ambayo naweza kuifanya kwenye maisha yangu"
"Umejuaje kama kazi ni ya hatari?"
"Ingekuwa ni rahisi ungekuwa umeshapata watu wa kuifanya, acha kunifanya mimi ni mtoto mzee"
"Ila hata malipo yake ni makubwa sana"
"Unahisi kwamba nafanya kazi kwa sababu ya malipo?"
"Hautapata pesa tu bali kuna zawadi kubwa sana ambayo inawez ikakufanya upate nafasi ya kuishi kwa mara ya pili"
"Kwamba hicho ni kitisho cha kutaka kuniua?"
"Mimi na wewe hatuna ugomvi wowote ule hivyo sio mimi wa kukuua ila hawa watu ambao wamekuweka hapa, wewe upo hai kwa muda mfupi tu kwa sababu huenda kuna vitu ambavyo wanavihitaji kutoka kwako lakini kiuhalisia ni kwamba wakimalizana na wewe hawawezi kukuacha hai lazima wakuue"
"Kazi yako ni ipi?"
"Hapo sasa tunaongea kiume. Nina binti yangu ametekwa nahitaji ukamkomboe"
"Whaaaaaat?"
"Ukifanikisha hili nakuahidi kukupa pesa yoyote ile ambayo utaihitaji wewe lakini pia wakati unaenda kuifanya kazi hiyo mimi ndiye nahusika kukutoa wewe hapa gerezani na nakuahidi baada ya hapo hautarudi tena hapa. Nitakufutia utambulisho wako wote na unaweza kwenda taifa lolote lile ukaanza maisha yako mapya ambayo hakuna mtu yeyote atajua kwamba uliwahi kuwa hai"
"Mwanao ametekwa na nani?"
"Maelekezo yote utapewa lakini aliye mteka ni mtu ambaye alikuwa ni rafiki yangu hapo zamani"
"Kwanini amteke mtoto wako?"
"Ni stori ndefu sana na ndiyo maana nimeishia kwenye hili gereza. Nikiwa nje nafuatiliwa kila hatua ninayo ikanyaga na kama nikiteleza kidogo tu nikafanya jambo la kijinga basi nampoteza mwanangu kwa sababu watamuua"
"Ndiyo sababu umeogopa kuwatumia watu wako kwa sababu unajua wanafahamika itakuwa ni rahisi kujulikana ukampoteza mwanao?"
"Ndiyo, hii ndiyo sababu kubwa ambayo imenifanya nitafute mtu wa nje ambaye hakuna anaye kufahamu. Hata hapa gerezani nahisi kuna watu wananifuatilia hivyo wanajua nakutana na nani na nafanya nini ila kwa sababu nakula sahani moja na viongozi wa hapa kuna vitu naweza kuvifanya bila kujulikana"
20 inafika mwisho.
Febiani Babuya.