HADITHI: BADO NINAISHI (ASHRAFU NDILO JINA LANGU)
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+
SEHEMU YA ISHIRINI NA NNE
"Unamaanisha yule tajiri mfanya biashara?"
"Ndiyo bosi"
"Why?"
"Kimekuwa kitendawili kizito sana ambacho tunatakiwa kukipatia jibu lake"
"Bruno Josephat ameingiaje ndani ya lile gereza?"
"Bado sijajua juu ya hilo bosi"
"Kwahiyo wanatuchezea mchezo hawa wajinga si ndio? Unaweza ukaniambia mtu mmoja amefanikiwa vipi kutoroka kweye gereza kama lile?"
"Kwa hesabu za haraka haraka inaonekana kwamba ametoka wakati walinzi wanatoka alfajiri"
"Taarifa za ulinzi ni siri kubwa sasa inawezekana vipi yeye ajue akiwa na siku chache tu gerezani?"
"Ni wazi kwamba kuna watu waliuza taarifa"
"Natakiwa kukutana na vijana haraka sana huyu mtu atafutwe kwa namna yoyote ile, mimi naenda gerezani huko wakati huu"
"Tunaenda wote bosi" madam alimwangalia msaidizi wake, hakuwa na namna ikamlazimu kukubali kufanya jambo hilo wakati huo walikuwa wametoka nje wakijifanya kama wana maongezi ya biashara kisha wakapanda kwenye gari kuanza kuelekea hiyo sehemu.
Kila hatua chache walizokuwa wanazipiga, kuna gari ilikuwa inaunga msafara wao, hao walikuwa ni walinzi wa mkuu wa usalama ambao walitakiwa kuhakikisha mheshimiwa yupo salama wakati wote mpaka wanaishika njia ya kuelekea huko msafara ulikuwa umekamilika gari sita zikiwa kwenye mwendo mkali sana. Cleopatra Gambo aliitoa simu yake mfukoni na kumpigia mwanadada Anelia Baton;
"Uko wapi?"
"Mheshimiwa raisi amenipigia simu nakutana naye muda huu"
"Baada ya hapo jiandae, tuna tatizo limejitokeza"
"Lipi hilo?"
"Remy ametoroka gerezani"
"Whaaaat?"
"Haya mambo tutayaongea nikirudi, hakikisha raisi haipati habari hii kwanza na kama kuipata basi mimi ndiye natakiwa kumfikishia mwenyewe"
"Sawa bosi"
Wakati huo ambao simu hiyo ilikuwa inamfikia Anelia, ni wakati ambao alikuwa anaingia kwenye mlango wa Ikulu kwenda kukutana na raisi kama mheshimiwa huyo alivyokuwa ameahidi. Alijitambulisha na kukaguliwa kila kitu baada ya kuonekana yupo salama walimruhusu kuingia na kwenda kukutana moja kwa moja na raisi wake.
Mheshimiwa huyo alikuwa amekaa bustanini sehemu ambayo ilikuwa na upepo safi hususani ule ambao ulikuwa unatokea baharini, hiyo ndiyo sehemu ambayo alikuwa anahitaji kufanyia mazungumzo na mwanamke huyo. Hakuwahi kabisa kumuona mrembo huyo hadharani zaidi ya kuzisikia sifa zake nyingi za uchapakazi kutoka kwa mkurugenzi wake, siku hiyo tena mchana kabisa kukiwa hakuna hali ya jua alibahatika kuona sura adimu sana kwenye taifa lake, sura ambayo huenda haikumfanya aamini kwamba kwenye nchi yake kulikuwa na malaika wazuri namna hiyo. Alijikuta anamkadiria mrembo huyo tangu akiwa mbali mpaka alipo mkaribia pale alipokuwepo, Anelia alifika hapo akiwa kwenye vazi bora sana la kike mpaka mheshimiwa alisahau hata kumkaribisha kitu ambacho kilimfanya mlinzi wake kumkumbusha kwamba mwanamke huyo alikuwa amefika tayari na hapo ndipo mheshimiwa alijikohoza na kumkaribisha kiti mwanamke huyo na kumtaka mlinzi wake awapishe.
"Karibu sana, Anelia nani vile?"
"Baton" ni kama kuna kitu kilimfanya ashtuke baada ya kulisikia jina hilo ila alijifanya kwamba hakuna lolote.
"Asante sana mheshimiwa, najihisi mwenye bahati sana kuweza kupata nafasi ya kukaribishwa na wewe sehemu bora zaidi kama hii ambayo kila mtu ana ndoto ya kuja kufika japo mara moja tu kwenye maisha yake yote"
"Usijali kabisa, wewe ni moja kati ya watu mhimu sana kwenye taifa hili hivyo unastahili kabisa kufika ndani ya sehemu kama hii kwa makubwa ambayo unaifanyia nchi hii. Nimepata taarifa zako na sifa zako nyingi sana juu ya kazi nyingi ambazo umezifanya ndani na nje ya nchi hususani hili la kutusaidia kumkamata huyu gaidi ambaye nasikia alikuwa na magenge mengi sana ya kihalifu. Hii inakufanya wewe kuwa mtu sahihi kabisa kupata sifa zangu na kupata zawadi zangu ambazo nitazitoa kwa ajili yako" mheshimiwa alionekana kabisa amemtamani kama sio kumpenda mwanamke huyo maana alianza kubabaika sana akiwa anamuangalia kuanzia chini na Anelia aliligundua hilo hivyo akawa anajiachia sana.
"Anaonekana anapenda sana chini huyu, ngoja nifanye kila ambacho anakitaka ili kama akiingia kwenye anga zangu basi nitamtumia kulipiza kisasi changu na kuutafuta ukweli juu ya kifo cha wazazi wangu ambacho nahisi kuna mikono ya watu fulani lazima ilihusika" Anelia alijiongelea mwenyewe kwenye moyo wake baada ya kuona tamaa za kifisi mbele ya macho ya raisi kisha akamjibu;
"Najisikia fahari sana kupata sifa kwa bosi wa nchi, naahidi nitafanya kila kitu kwa ajili yako na taifa hili mheshimiwa"
"Una uhakika kwamba upo tayari kufanya lolote kwa ajili ya raisi wako?"
"Ndiyo mheshimiwa"
"Safi sana, kwenye maisha yako wewe unahitaji nini labda Anelia?"
"Napenda nchi yangu iwe na amani kwanza kisha ifuate amani ya moyo wangu"
"Moyo wako nafikiri ni jambo la kumtafita mtu wa kuufanya uwe na amani tu"
"Lakini kazi yangu hainiruhusu hilo mheshimiwa"
"Hahahaha inawezekana ni wewe tu kuamua"
"Hii kazi inakufanya usiwe na chaguo"
"Sio kweli, siku zote lazima uwe na chaguo"
"Mimi silioni kwa sababu kila kitu nakifanya kwa kuiweka nchi mbele kwanza kabla hata ya uhai wangu"
"Ni jambo kubwa kufanya hivyo kwa sababu kama taifa tunawahitaji watu wazalendo kama wewe lakini sio sababu ya kukufanya wewe ukose chaguo"
"Huenda upo sahihi mheshimiwa"
"Unahitaji nini kwa kazi nzuri ambayo unaifanya?"
"Sihitaji chochote kile, kwangu kunitambua tu kwamba nafanya kazi nzuri ni jambo kubwa ambalo linanifanya nijivunie sana"
"Unaonaje leo baadae tukikutana kwenye moja ya nyumba zangu zilizopo baharini huko?"
"Kutakuwa na kazi nyingine mheshimiwa?"
24 inafika mwisho.