Simulizi ya Kijasusi: Kiguu Na Njia

Simulizi ya Kijasusi: Kiguu Na Njia

SEHEMU YA 126

mfungwa asiye na mikono gerezani humo na kuanza kutumikia kifungo chake cha miaka thelathini. Gereza lilikuwa kubwa, lenye wafungwa tele, hivyo ilinichukua siku tatu nikisikia tu habari za mfungwa huyo bila kumwona kwa macho. Anakulaje? Anaogaje? Anavaaje na kuvua nguo zake? Nilijiuliza. Lakini swali kubwa zaidi lililonisumbua akili yangu ni pale nilipotaka kujua ni kitu gani kilimsibu mpaka akaipoteza mikono yake yote miwili. Kitu gani hasa kilimtokea? Gereza lilijaa simulizi tele juu yake. Mara anakula kwa kutumia miguu yake, mara hapana, anatumia kinywa chake pekee na kadhalika. Mara aliiba, akakatwa mikono, mara hapana, alizaliwa kama alivyo. Nilipokutana naye kwa mara ya kwanza nilishituka sana. Maumbile ya binadamu yana utaratibu wake. Akiwa na viungo vyake vyote binadamu anavutia macho. Akipoteza baadhi ya viungo vyake anatisha. Ndivyo nilivyomwona bwana huyu. Alionekana mrefu kupita kiasi, mwembamba kupita kiasi. Kwa ujumla, alionekana kama mnazi mrefu mweusi, unaotembea na kuzungumza. Uhai mkubwa zaidi katika umbo hili la kutisha ulikuwa katika sauti yake nzito na meno​
yake meupe ambayo yaling’ara sana kila alipozungumza.
Alikuwa akicheka!
Nilimkodolea macho ya mshangao, pale kwenye kundi la watu walioketi nao wakisikiliza simulizi ambazo sina shaka zilisisimua sana, kwani kila mtu alikuwa akimsikiliza kwa makini huku baadhi wakicheka. Alikuwa akitoa kichekesho. “Baba akamwambia mwanaye, ‘Toto jinga sana wewe. Kwa umri wako huo Idd Amin alishakuwa mkuu wa majeshi ya Uganda.’
“Mtoto akamjibu, ‘Na kwa umri wako huo alishakuwa Rais wa Uganda. Wewe mbona bado tarishi?”



Mie pia niliangua kicheko. Mchekeshaji huyo akageuka kunitazama. Akanikazia macho. Mara nikamwona akiachia tabasamu pevu zaidi huku akiinuka kunifuata.
“Petro!”
Aliniita. Sikuelewa. Nikamtolea macho ya mshangao. “Petro, hunikumbuki?”.
Nilitikisa kichwa kukataa. “Humkumbuki Umsolopogaas?” “Umsolopogaas mwenyewe?”
“Naam, Mzulu halisi. Kiboko ya Wajivuni.” “Kwa jina halisi Matayo Butiku?”
“Naam. Mathew Butiku halisi.” “Mang’ana” nilimjibu.
“Mayia.” Alijibu akicheka.
Sijapata kupigwa na mshangao kama ule. Tuliishi na Matayo katika bweni moja tukiwa katika darasa moja kwa takribani miaka minne. Siwezi kusema kuwa alikuwa rafiki yangu, lakini hakupata kuwa adui yangu. Kwa kweli, alikuwa rafiki wa kila mtu. Utundu wake, ucheshi wake na vituko vyake ndani na nje ya darasa vilifanya awe rafiki wa kila mtu, walimu na wanafunzi, jambo ambalo nadhani lilimsaidia sana kushinda mitihani yake, kwani kidogo kichwa chake kilikuwa kizito kuelewa, lakini akawa mwepesi wa kuibia. Hata uifiche vipi kazi yako Matayo atapenyeza jicho lake na kuchopoa jibu. Kipi kilimtokea? Nilijiuliza. Alikuwa kijana aliyekamilika,​
kwa miguu na mikono ambayo haikupata kutulia. Nakumbuka alipenda sana vitabu vya riwaya, hasa zile za mashujaa. Na alipenda kudandia majina ya wahusika wa riwaya hizo. Kuna wakati tulipewa vitabu vya someni bila shida, mara mwenzetu akaanza kujiita ‘Bulicheka, kiboko ya Wagagagigikoko.’





Tukaletewa Safari ya Sindbad. Mara mathayo akawa ‘Baharia Sindbad.’ Muda si mrefu akasoma Alfu lela U lela, akawa ‘Mfalme Harun Radhid wa Baghdad.’ Aliposoma hadithi ya Allan Quatermain, akavutiwa na yule mzee wa Kizulu, akaachana na jina la umbopa alilolipata katika Mashimo ya Mfalme Suleiman na kuwa ‘Umsolopogaas,’ jina ambalo naona amedumu nalo hadi leo. Hata kabati lake la shule aliweka vitu ambavyo vilipigwa marufuku shuleni hapo; panga, kisu, rungu na shoka ambalo aliliita inkoskaaz.

Aliponifikia, Matayo alitaka kunikumbatia. Haikuwa rahisi. Mikono yake iliyokatika juu ya viwiko ilichoweza kufanya ni kunipapasa kidogo tu mgongoni. Ni mimi niliyeweza kumkumbatia kikamilifu.

Tukaachana na kutazamana kwa muda. “Nini kimetukia Matayo?”

Kwa mshangao wangu alicheka tena. “Ni hadithi ndefu,” alijibu na kuongeza. “Tutatafuta muda tukae mahala nikusimulie.” Akasita kumeza mate. “Na wewe kilikutokea nini?”

“Ni hadithi ndefu vilevile,” nilimjibu. “Au ndio ile hirizi?”

“Hirizi gani?”

“Yako. Ile iliyopotea. Unajua iliokotwa ikachomwa moto lakini ikakataa kuungua? Nasikia mapadre wameipeleka Ujerumani kuifanyia utafiti.”

Nikajisingizia kutabasamu. Kichwani niliwaza jambo moja tu: Babyabato hakusema uongo. Hirizi yangu iliokotwa tena!

Wafungwa waliotuzunguka walionyesha kuvutiwa na taarifa hizo. Wakaanza kusogea ili kutusikiliza vizuri zaidi.
 
SEHEMU YA 127

Nikasema, “Itabidi tutafute muda tukae na kusimuliana masaibu yetu kwa kituo.”
“Kuna ubaya gani?” Butiku alijibu.

* * *​
Mkoa wa Mara unapakana na nchi ya Kenya kwa upande wa kaskazini. Mkoa huo ambao unachangia neema ya ziwa Victoria na mikoa ya Mwanza na Kagera, Mashariki umepakana na mkoa wa Serengeti. Mji wa Tarime, alikozaliwa Matayo Butiku, au ‘Umsolopogaas’ kama anavyopenda kujiita, uko mpakani na Kenya. Mji huu ni maarufu kwa pilikapilika nyingi kama ilivyo miji mingine ya mipakani kama Namanga, na Tunduma uko katika wilaya ya Tarime, kando kidogo ya mpakani, Sirari.
Mkoa huo una sifa zote ambazo nchi hii imejaliwa; mvua za kutosha, ziwa lililojaa samaki, ardhi iliyojaa rutuba na mbuga za wanyama kama Ikorongo, Nata na baba lao; Serengeti.
Mara una makabila mengi ya asili na wahamiaji. Ya asili ni Wakurya, Wazanaki, Wajita na Wajaluo ambao pia, kama Wamasai, wana mizizi yao nchini Kenya. Wahamiaji ni pamoja na wahindi, Wanyarwanda, Warundi, Wahangaza na wengineo. Pamoja na sifa tele za neema katika nchi yao, watu wa​
Mara, hasa Wakurya wamerithi maradhi ambayo hadi leo tiba yake haijapata kupatikana; Ubabe. Mauaji na vita vinavyoitwa vya kikabila, ambavyo kwa kweli ni vita baina ya koo ndani ya kabila moja, vimekuwa vikitawala macho na masikio kupitia katika vyombo vya habari. Vijiji, kama Kubitarere, ni miongoni mwa vile ambavyo vimeathirika mara kwa mara na ubabe wa baadhi ya wanajamii wa ama Waachari ama Walyanchoka.



Kisa? Ama hawa wameshukiwa kuiba ng’ombe wa hawa, ama wamevamia shamba la hawa. Vita vitazuka, watu wanapoteza maisha, mashamba yanachomwa, nyumba zinabomolewa na uharibifu mwingine tele usio na kifani. Mara nyingi serikali, kupitia vyombo vyake vya usalama pekee ambayo huingilia vita hivyo na kuituliza. Lakini si kwa muda mrefu.
Ni mirathi hiyo ya hatari ambayo ilimgharimu rafiki yangu Matayo Butiku mikono yake yote miwili na kumpa kilema cha maisha.
Ilikuwaje?
Zilikuwa zimepita siku mbili toka nilipomtia machoni kwa mara ya kwanza akiwa katika hali ile. Tulipata wasaa wa kuzungumza, mimi nikifyeka majani yeye, aliyepangiwa kufyeka pia akipita hapa na pale huku akimwaga gumzo na vichekesho ambavyo nilibaini baadaye kuwa vilimsaidia sana kupatiwa huduma mbalimbali, ikiwa pamoja na kulishwa chakula.
“Tulipoachana pale shuleni mimi niliendelea kwa miaka miwili kabla sijaacha masomo na kurudi nyumbani ambako nilijiunga na shughuli za uvuvi katika ziwa Victoria. Baadaye niliacha kuvua na kuanza biashara ya kupeleka samaki Nairobi na Kampala.
“Unajua sangara hawaishi kuliwa tu?” aliniuliza ghafla. Sikumwelewa. Akafafanua, “Siku hizi sangara ni mali katika kila kiungo chake. Ngozi yake siku hizi ni mali ghafi inayotengeneza pochi murua za akina mama matajiri. Mifupa yake ni malighafi kwa viwanda vya mbolea na madawa. Siku si nyingi hata ile harufu yake itageuzwa manukato ya aina yake. Sangara ni almasi za ziwani.
“Nilipata fedha nyingi sana. Kwa viwango vya pale kijijini





nilikuwa tajiri. Nikajenga nyumba safi na shamba kubwa la miwa. Toka hapo ndipo mambo yalianza kwenda mrama.” Alisita kidogo.

Nikaitumia fursa hiyo kutumbukiza swali, “Ulikuwa hujabahatika kuoa?”

“Nini? Kuoa?” aliuliza huku akiangua kicheko. “Toka niko darasa la nne, wakati tukilala wote pale bwenini, mimi tayari nilikuwa na mke,” alisema.

Nikapigwa na butwaa. “Ulikuawa na mke!” “Naam.”

“Ulioa lini?”

“Sikuoa, niliozeshwa na ukoo wangu. Nilikuwa mtoto pekee wa kiume katika familia yangu. Dada zangu walikuwa kumi na mmoja. Walianza kuolewa. Tulipata ng’ombe wengi sana lakini wazazi hawakuridhika. Walihitaji mjukuu ili awe mrithi wa mali hizo na awapatie watoto wa kiume.”

“Uliwapata?” “Watu gani?”

“Watoto wa kiume.”

Nikamwona Matayo, kwa mara ya kwanza, akipoteza tabasamu na kuonyesha dalili za masikitiko. Nusu dakika tu, mara alirudia sura yake ya kawaida na kunijibu akisema, “Kuoa ni khiari, kuzaa ni majaliwa. Leo hii nina wake watano, hata mmoja hajanipatia mtoto wa kiume!”

Wake watano! Hata hivyo, sikushangaa sana. Matayo alikuwa mtu wa vituko na miujiza siku zote, muujiza wa kwanza ulikuwa ule wa kujiunga na shule akiwa ametuzidi umri wote darasani. Mwujiza wa pili ukiwa ule wa kuja shule na silaha zake zote. Sasa huu wa kwamba wakati wote alikuwa na mke!
 
SEHEMU YA 128

“Hilo linakushangaza?” aliuliza baada ya kuyasoma mawazo yangu. “Kwa hiyo, utashangaa zaidi nikikwambia kuwa hata wakati tuko shule, kila likizo niliingia kwenye vita na kuwashikisha adabu adui zetu?”
Muujiza mwingine!
“Nilipigana sana. Na nilipata sifa tele za ushujaa. Adui zetu waliniogopa kuliko simba kwa njinsi nilivyokuwa hodari wa kupanga mashambulizi na kukwepa mishale na mikuki yao. Kwa kweli, jina la yule mzee wa Kizulu lilinistahili sana. Hadi leo sina mikono bado wananiogopa sana na kila vita niko mstari wa mbele nikiongoza mapambano. Kama nisingekamatwa na kushitakiwa wangenikoma.
“Ilikuwaje?” “Nini?”
“Ilitokea nini Umsolopogaas akaishiwa ujanja na kukatwa mikono?” nilifafanua.
Akacheka. Kisha akasema, “ Naweza kusema ndege mjanja hunaswa na tundu bovu. Nilifanya kosa la kumdharau adui yangu. Mtoto mdogo sana, tena ambaye alikuwa hajapigana vita yoyote. Tulivamia kijiji chao, tukateka mifugo yote. Watu wazima wote walikimbia, mtoto huyu, wa miaka kumi na moja au mbili aliachwa nyuma akilia. Mkononi alikuwa na sime.
“Nilikatazama katoto kale. Ka kiume! Ningeweza kukaua, ningeweza kukavunja shingo. Lakini nikakahurumia. Kwangu mtoto wa kiume alikuwa lulu. Nikakaacha na kugeuka ili niondoke zangu. Mara waa! Mkono wangu wa kulia uliokuwa na sime ukaanguka chini. Maumivu makali yakanishika, lakini hayakunishinda hasira niliyoipata. Nikageuka kwa kasi. Waa! Nilikutana na pigo la pili ambalo lilidondosha mkono wangu



wa pili. Maumivu hayakuwa na kifani. Bila khiari nilianguka na kupoteza fahamu. Nilipozinduka nilijikuta niko hospitali, mikono yangu tayari imekuwa vibutu.
Na nilipopata nafuu nilishtakiwa kwa mauaji na uporaji na kupewa adhabu hii ninayoitumikia.
Ilikuwa taarifa ya kusikitisha sana. Nilimhurumia, sikuwa na uwezo wa kumsaidia. Nikaishia kumpa pole tena. Nadhani nilimhurumia. Lakini kutokana na vitendo vyake mwenyewe na msimamo wake hata baada ya kupoteza mikono nilishindwa kuamini kama kweli ninamhurumia au la.
“Haya na wewe niambie kulikoni hadi ukafika hapa,” alisema. “Si walisema ukijua kupokea ujue na kutoa? Ama ukiwa mroho usiwe mchoyo?” aliongeza.
Yangu yanaelezeka kweli? Nilijiuliza.


M
Kiguu n2a Njia







2
YA ISHIRINI NA MBILI

Hadi

fungwa hana kauli. Mfungwa hana hiari. Mara tu ukishahukumiwa wewe si wewe tena, ni mali ya mtu mwingine. Utafuata matakwa
na hiari yake hadi mwisho wa kifungo chako.
Kwa mtu aliyekuwa na kifungo kirefu kama mimi, mfumo huo wa kanuni za mfungwa uliniathiri mara kwa mara, ingawa wakati mwingine athari hizo zilikuwa faraja kwangu kwa namna moja au nyingine.
Moja ya faraja hizo ni pale nilipobahatika kuwemo katika kundi la wafungwa walioteuliwa kwenda Zanzibar kusaidia kazi ya kuvuna karafuu. Kwa mujibu wa mkuu wa gereza karafuu zilipamba sana na zilikuwa zikielekea kuharibika. Vijana wa jeshi la kujenga uchumi wa huko walikuwa tayari wamepelekwa lakini hawakukidhi mahitaji.
Niliichekelea sana fursa hiyo. Kwanza ingenipa fursa ya kupumua hewa safi ya nje. Hewa asilia ya oksijeni itokayo katika mimea na kusambazwa na upepo badala ya hii tuliyokuwa tukiitumia ambayo sikujua ilitokea wapi. Lakini pia kufikia Zanzibar ilikuwa ndoto yangu ya muda mrefu. Toka nchi hizi zilipoungana na sifa za Karume za mapenzi kwa nchi yake zikiimbwa katika vyombo vya habari azma yangu ya
 
SEHEMU YA 129

kukanyaga ardhi ya nchi hiyo ilikuwa ikiongezeka siku baada ya siku.
Toka wakati ule ningali belubelu bado, mkakati wangu wa kufanya biashara ya chumvi kati ya Zanzibar na Bagamoyo ulipokwama, niliishia kujifariji kwa kusoma na kusikiliza tu, kila kilichozungumza juu ya nchi hiyo. Nilijifunza kuwa ilikuwa moja ya nchi zenye historia pekee duniani. Kwa mfano, wataalamu wa historia wanaamini kuwa miji katika visiwa hivyo ni vya kale kuliko nchi nyingi za dunia. Inaaminika kuwa waanzilishi wa taifa hilo makabila ya Wahadimu na Watumbatu walianza kuishi katika visiwa hivyo, wakitokea katika pwani za Afrika Mashariki miaka 1000 iliyopita. Watu hao waliishi katika vijiji vidogovidogo vya ukoo, bila uongozi wa pamoja jambo lililofanya wakose uwezo wa kutetea haki yao ya umiliki pale walipoanza kuingia katika visiwa hivyo.
Wafanyabiashara toka nchi za Kiarabu hasa Iran na Iraq na Wahindi wanaelezewa kufanya biashara na nchi hiyo miaka nenda rudi. Katika karne ya 11 na 12 baadhi ya wafanyabiashara hao walianza kuifanya Zanzibar makazi yao ya kudumu wengi wao ikiwa pamoja na kuanza kuoana na wenyeji. Matokeo ya ndoa ni kuibuka kwa watawala kama Mwinyi Mkuu au Jumbe miongoni mwa wahadimu au mashaha miongoni mwa Watumbatu. Viongozi hao hawakuwa na nguvu nyingi. Lakini angalau walisaidia kulinda uhalisia katika makabila yao.
Yule naodha machachari wa Kireno, Vasco da Gama, alifika Zanzibar ,waka 1499 na kufungua njia ya wageni wa kutoka Ulaya nchini humo. Mwaka 1505 nchi hiyo ilifanywa koloni la Ureno pale walipoamua kuiteka kabisa.
Mwaka 1698 Zanzibar ikafanywa sehemu ya mali
za Oman, hatua iliyofuatiwa na Sayyid Said bin Sultan al



Busaid ambaye akiwa na umri wa miaka 15, mwaka wa 1806 kuhamishiwa makao yake ya kifalme mjini humo. Baadaye utawala wa pamoja wa Zanzibar na Oman uligawanyika mwaka 1861 baada ya kifo chake, wanawe ambao walikuwa wakigombea madaraka walipofikia uamuzi wa Sayyid Majid bin Said alipochukua madaraka ya na Zanzibar na ndugu yake Sayyid Thuwaini kuwa Sultan wa Oman.
Baada ya hapo historia ya Zanzibar ina mlolongo mrefu wa kugombea au kupokonyana madaraka baina ya Waarabu na Waarabu, Wajerumani kwa Waingereza na hatimaye Waarabu kwa Waingereza. Ni pilikapilika za aina hiyo zilizofanya Zanzibar iingie katika historia kama nchi iliyovunja rekodi kwa kupigana vita fupi kuliko zote duniani. Vita hiyo ilipiganwa kwa dakika 45 tu. Ilikuwa baina ya majeshi ya Uingereza na yale ya Sultan Sayyid Khalid bin Bargash ambaye, alipokonya madaraka na kujitangaza Sultan wa nchi hiyo wakati Waingereza waliamini mtawala halali angekuwa Hamoud bin Mohamed. Waingereza walimwamuru Bargash kuachia madaraka; akakataa. Wakampa muda wa kuondoka huku manowari zao zikiwa baharini tayari kupiga mizinga iwapo angeendelea kukaidi. Muda waliompa ulipokwisha manowari hizo zililipua mizinga ambayo ililiharibu jengo la Beit al Hokum. Majeshi ya bargash yalijaribu kujibu kwa bunduki zao lakini hazikufua dafu. Dakika 45 baadaye Bargash alikimbilia katika ubalozi wa Ujerumani, vita ikasimamishwa na Maoud bin Mohamed akatawazwa kuitawala Zanzibar.
Utawala wa Mwingereza nao ulikoma katika kisiwa hicho mwaka 1963 pale nchi hiyo ilipotoa uhuru na uchaguzi ulipofanyika muungano wa ZNP na ZPPP uliposhinda kwa hila dhidi ya ASP ya wazalendo akina Abeid Aman Karume na kufanya Waarabu waendelee kuwa madarakani. Utawala



huo haukudumu. Mwaka mmoja baadaye, Januari 12, 1964 wazalendo walipindua serikali hiyo na uongozi kuwekwa chini ya Karume.
Hayakuwa mapinduzi rahisi kama mtu unayeweza kufikiria Waarabu wengi wanadaiwa kuuawa, maelfu wengine wakitupwa gerezani. Aidha, Karume alitumia mapinduzi hayo kurejesha hadhi ya mtu mweusi kwa kutoa amri mwanamume kuoa mwanamke yeyote wa Kiarabu au Kihindi anayempenda. Amri chungu ambayo ilipigiwa kelele na baadhi ya nchi duniani, lakini kwa nchi iliyobobea kwa ukandamizaji, ambayo wakati fulani iliaminika kuwa robo tatu ya raia wake walikuwa watumwa wa Waarabu hatua ipi zaidi ingeweza kurejesha usawa na umoja haraka zaidi ya zile ndoa za lazima?
Misuguano ya ndani na vitisho toka nje kwa taifa hilo dogo ilikoma pale nchi hiyo ilipoungana na Tanganyika na kuzaliwa taifa jipya la Tanzania april 12, 1964 ikiwa miezi mitatu tu baada ya mapinduzi.
Hiyo ndiyo Zanzibar ya kale, ambayo kudra za Mungu
ziliniwezesha kuwa safarini kuiendea.
Mfungwa hachagui njia, mfungwa hachagui siku ya safari. Yeye ni mtu wa kukurupushwa tu, kama mifugo. Ndivyo ilivyokuwa kwetu. Fununu za safari zilianza ghafla kwa minong’oni baina ya wafungwa. “Skochi jamani…. Skochi ya Zanzibar…’ zilivuma taarifa hizo katika selo. Nadhani ‘skochi’ ni lugha moja ya zile lugha za kijelajela iliyokuwa na maana ya ‘escort’ kwa kiingereza kwani mfungwa haendi popote bila askari jela wa kuwasindikiza.
Sikujua Kama ningekuwa mmoja wa wateule hao hadi siku ya safari, jina langu lilipoitwa na kuamriwa kupanda karandinga. Tulikuwa kama wafungwa mia hivi na askari kumi wa kutulinda. Safari yetu ilianza asubuhi ya jumatatu
 
SEHEMU YA 130

moja, tukaifuata barabara ya Dar es Salaam. Tulipofika Moshi tulisimama kwa nusu saa, mkuu wa safari aliposhuka kupata kifungua kinywa.
Nilitamani kuuona mji wa Moshi kwa mara nyingine, lakini niliishia kuuchungulia tu kupitia katika nyavu za waya za karandinga letu, hali ya hewa ilikuwa ileile, tamu inayosisimua. Mlima Kilimanjaro uliendelea kuinamia mji, kama unaolinda kwa maovu, kwa utukufu wake. Kitu kilichonivutia zaidi kwa mji wa Moshi ni usafi. Barabara zilikuwa zikimeremeta, majengo yaking’ara kwa rangi. Ilikuwa nadra sana kuona uchafu ukizagaazagaa mitaani kama ilivyo miji mingi niliyopata kuitembelea.
Safari ilipoanza tena nilikuwa tayari nimepata upenyo mzuri wa kuchungulia nje. Barabara safi, ya lami ilikuwa ikiteleza chini ya matairi ya gari letu kwa uhakika kabisa. Tulikuwa tukielekea Mashariki hadi tulipofika Himo ambapo kuna njia panda ya kuelekea Taveta nchini Kenya na ile ya Dar es Salaam ambayo kwa kiais fulani ilielekea Kusini. Tulipita Kifaru, tukaingia Mwanga. Toka hapo niliweza kuliona kwa mbali bwawa la nyumba ya Mungu. Tukateleza hadi Same, Hedaru, Mkomazi, Mombo na baadaye Korogwe ambapo tulipumzishwa katika gereza moja dogo ambalo sikubahatika kufahamu jina lake. Hapo tulipewa chakula na kutakiwa kumaliza haja zetu za kimaumbile, kubwa na ndogo kabla ya kuanza safari.
Tulifika Segerea na kuiacha barabara inayokwenda Tanga hadi Mombasa tukashuka na kuvuka mto Wami hadi Msata. Hapo viongozi wetu wa safari walisimama kwa muda kujadiliana, ama wafuate barabara ile ndogo isiyo na lami ambayo inachepuka hadi Kiwangwa, Kilola na hatimaye Bagamoyo au ile iliyozoeleka, lakini ya mzunguko, ambayo



ingetufikisha Chalinze, Mlandizi na Kibaha kabla ya kuingia Dar es Salaam. Kumbe safari yetu ya Unguja ilikuwa ianze Bagamoyo. Nadhani kwa usalama wao au wetu waliamua kupita njia ndefu ya Dar es Salaam.
Nilishangazwa na wingi wa watu na majengo niliyoyaona hasa kutokea Mlandizi, mara tu baada ya kuvuka mto Ruvu. Nilipopita kwa mara ya kwanza eneo hili lilikuwa pori la kutisha ambalo lilimilikiwa na nguruwe mwitu na ndege wa porini. Sasa lilijaa binadamu na majengo tele. Wakati huo ilikuwa usiku wa saa tatu hivi, lakini taa za umeme toka maeneo mbalimbali, wingi wa magari barabarani na watu tuliwapitia kando ya barabara uliashiria wingi wa watu na pilikapilika nyingine za kibindamu.
Pilikapilika hizo ziliongezeka maradufu mara tulipoingia Mbezi na hatimaye Kimara. Gari letu lilikwenda kwa mwendo wa kinyonga kutokana na msongamano wa magari. Kandokando mwa barabara, kulia na kushoto, nilishangazwa na wingi wa baa za pombe na wateja waliofurika kelele za muziki wa kileo, ambao baadaye niliambiwa kuwa unaitwa Bongo flavour ziliweza kusikika ndani ya gari hiyo kwa uwazi kabisa. Katika baa moja mwanamuziki mmoja alikuwa akicheza kwa nguvu zake zote;
Kuku kapanda baiskeli, Bata kavaa raizoni…
Wimbo huo ulitufikia vizuri kabisa katika gari. Wengi wetu ambao tulizowea nyimbo za akina Marijani Shabani, Wema Abdallah au Mbaraka Mwishehe tuliishia kucheka kwa mapinduzi haya ya kisanaa. Hatukujua kama tunakwenda mbele au tunarudi nyuma katika fani hiyo ya muziki.
Zaidi ya nyimbo kitu kingine kilichotufikia ndani ya
gari hilo ni harufu ya nyama choma. Yale mapande ya nyama,



mishikaki na kuku waliokuwa wakiokwa katika mabaa hayo yalisambaza harufu tamu ambayo ilitutia uroho wa nyama, mboga iliyopatikana kwa nadra sana gerezani.
Tulifika Dar es Salaam yapata saa nne na robo usiku. Ule muujiza nilioutegemea ulijidhihirisha. Dar es Salaam haukuwa mji tena bali jiji. Majumba mengi yaliyopanda juu, watu wakiwa tele mitaani muda wote. Biashara ya baa ilishamiri karibu kila mahala. Nchi hii haina biashara nyingine?
Tulitoka Ubungo na kuelekezwa Mwenge. Gari likageuzwa na kuelekea Kaskazini tulikotokea tukifuata barabara ya Bagamoyo. Kwangu barabara hiyo ilikuwa muujiza mwingine. Tofauti kabisa na ile tuliyoitumia na akina Leakey miaka kadha wa kadha iliyopita hii ilikuwa barabara pana ya lami. Na ilifurika magari muda wote. Lile pori la wakati ule halikuwepo tena. Badala yake mji ulikuwa umemeza kila kitu kiasi cha kufanya kambi ya jeshi la Lugalo, ambayo zamani ilionekana kujengwa porini sasa iwe katikati ya mji wa kiraia, ambao ulisambaa hadi Pwani yake uwe hadi ufukwe wa Kunduchi. Vile vilivyojulikana kama vijiji vya Tegeta, na Bunju sasa ilikuwa sehemu ya jiji la Dar es Salaam ambalo lilibakiza kilometa mbili tu kuungana na mji wa Bagamoyo, Bagamoyo ambako tulifikishwa katika gereza la Kigongoni kusubiri safari ya Zanzibar.
Ulipata kusikia kuwa binadamu ana mkia? Kama ulipata, je ulipata kuona mkia huo? Ni watu wachache sana duniani waliopata kuuona; mimi nikiwa mmoja wao. Bahati au balaa hiyo nilikutana nayo katika gereza hilo ambalo ni maalum kwa kilimo.
Awali sikuyaamini macho yangu pale nilipowaona watu wa ajabu. Miili yao ilikuwa inatisha, ngozi ikiogofya. Fikiria ngozi ya mtu yeyote, uliyopata kuiona maishani mwako, fikiria
 
SEHEMU YA 131


hata mgonjwa wa UKIMWI aliye taabani sana; bado kamwe hutaweza kumfananisha na miili ya baadhi ya wafungwa tuliokutana nao katika gereza hilo. Walinyauka, walisinyaa na kuifanya miili yao ifikie kiwango hicho cha kutisha. Lakini zaidi ya ngozi ya miili hiyo hali ya kukonda ilitisha zaidi. Baadhi yao, waliokuwa taabani zaidi walionekana kama mifupa iliyounganishwa na aina fulani ya ngozi! Ni pale walipovua mashati ndipo nilipoweza kuona mkia wa binadamu!

Mimi pia nilikuwa mfungwa. Lakini hali ya baadhi ya wafungwa hawa ilinifanya nitokwe na machozi! Nilipouliza nini kinatokea wenyeji walininjibu kwa urahisi tu; Luba.

Luba ndio nini?

Ugonjwa. Unatokana na wadudu ambao hushambulia mpunga. Unajua kilimo cha mpunga kilivyo? Inabidi kuingia katika maji au tope. Kwa mfungwa kulazimishwa kuingia katika maji ya tope linalofika hadi shingoni ni jambo la kawaida. Humo ndimo hukutana na wadudu hawa ambao hushambulia mpunga na hivyo wao pia kushambuliwa.

Msemaji alikuwa mfungwa mzoefu. Ilikuwa vigumu kuamini kweli ni mfungwa kwa jinsi alivyokuwa msafi, kiribatumbo kimejitokeza wazi chini ya kifua chake.

“Ni wajinga,” aliongeza. “Wanaingia kichwakichwa katika miji ya watu. Wangeuliza maradhi hayo yasingewapata.”

“Kwa vipi?” Nilimuuliza.

Alikohoa, kabla hajajibu akisema, “Iko namna. Kuna dawa. Wenzao kabla ya kuzama katika tope lile tunajipaka tumbaku. Wadudu hawatusogelei wala kutudhuru.”

“Kwa nini hamkuwaambia hayo mapema?” nilimsaili. “Si nimekwambia wanaingiamiji ya watu kichwakichwa?”

lilikuwa jibu lake.

Kwa mara ya kwanza nilijisikia kumpiga mtu makonde.







Mtu mwenyewe hakuwa mwingine zaidi ya mzee huyu anayezungumzia maisha ya binadamu wenzake kana kwamba anajadili suala la paka. Ili kuepuka kufanya hivyo nilimwacha akiendelea kubwabwaja na kujiunga na wenzangu tuliokuwa nao katika ‘skochi’.

Nilishukuru pale siku mbili baadaye tulipochukuliwa na magari kuelekea pwani ya Bagamoyo, ambako majahazi mawili yalitupeleka Unguja yalitia nanga yakitusubiri.

Kutoka pwani hiyo hadi Zanzibar ilikuwa safari ya kilometa zipatazo 25 tu, lakini kwa wenzangu wengi ilikuwa safari ndefu, ngumu iliyojaa mashaka. Mawimbi na upepo vilifanya wengi wapatwe na ule ugonjwa uitwao ‘homa ya bahari.’ Baadhi walitapika, baadhi wakiwa taabani kana kwamba wanakaribia kukata roho. Askari wawili waliotusindikiza pia walikuwa wakitapika huku wenzao wakiwacheka.

Wakati tunakaribia kutua pwani tulipata burudani tosha toka kwa pomboo, wale viumbe wa baharini ambao mimi huwaita samaki lakini wataalamu uwachukulia kuwa ni wanyama wa majini kwa kuwa wananyonyesha watoto wao kinyume na samaki wengi, kawaida. Viumbe hawa ambao wengi huwaita ‘Dolphins’ walilizingira jahazi letu, mara kwa mara wakichupa angani na kutuchungulia kwa namna ya kusisimua.

Pomboo, ambao nyama yake ni tamu sana ni viumbe wanaofugika na kufundishwa. Nchi kadhaa tayari wamewafundisha michezo mbalimbali kama kushindana, kuruka kwa pamoja kudaka mpira na mambo mengine tele ambayo huvuta watalii. Baadhi ya nchi zilizoendedelea tayari wanawafundisha kubaini mabomu ya kutegwa baharini na hivyo kuepusha madhara.







Kwangu walikuwa burudani tosha na walitusindikiza hadi tulipotia nanga ufukwe wa Zanzibar, mji mkuu wa nchi hii ambayo inadaiwa iko chini kidogo ya usawa wa bahari. Baadhi ya wataalamu wanadai kuwa iko siku nchi hiyo itamezwa na maji na kutoweka katika uso wa dunia. Lakini hiyo ni hadithi nyingine. Yetu ni kwamba mara tulipofika magari ya wafungwa yalikuwa yakitusubiri tayari kutupeleka katika gereza la kiinua mguu ambako tungepumzika kidogo kabla ya kusafirishwa tena hadi Pemba yaliko mashamba mengi zaidi ya karafuu.

Tulilundikwa katika makarandinga, ambapo hayakutofautiana sana na yale ya bara. Yakatiwa moto na kuondoka. Kwa kiu yangu ya kuufahamu mji wa Zanzibar nilifanya kila jitihada kuhakikisha nachungulia nje na kujionea chochote ambacho ningeweza kukiona. Kwa mbali, niliweza kuiona hoteli maarufu ya bwawani ambayo ilijengwa na serikali ya Karume. Wakati tukipita mitaani, eneo la Kichenzani nilishangaa kuona mitaa yote ikiwa imemezwa na majumba marefu sana, takribani mita mia tano kila nyumba. Nyumba hizi ambazo zilikwenda juu kwa gorofa tatu au nne tu zilielekezwa kuwa ilikuwa kazi nyingine ya Karume kwa wananchi wake alipotoa amri akisema, ‘Wazungu wanashindana kujenga nyumba ndefu kwenda juu kwa ajili ya uhaba wa ardhi yao, sisI tutajenga nyumba ndefu kwa upana.’ Matokeo ya kauli hiyo ndiyo nyumba hIzo ambazo zilikuwa mkombozi kwa wananchi ambao wengi wao walikuwa masikini sana baada ya kukandamizwa na wageni miaka nenda rudi.

Katika eneo la darajani nilishangazwa na wingi wa waendesha baiskeli. Katika maneno fulani ilibidi waongozwe na askari wa barabarani kama ilivyo kwa magari. Eneo hilo lina soko kuu, wenyewe wakiliita ‘markiti’ bila shaka jina







hilo lilitokana na neno ‘market’ la Kiingereza. Kilichonivutia zaidi hapo ni mavazi, kanzu nyeupe ndala miguuni na baragashia kichwani vilitawala mavazi ya mwanaume. Kwa wanawake mabaibui yaliyofunika sura gubigubi yalitamalaki na kunikumbusha miji ya Tanga. Utamaduni mwingine niliobahatika kuuona hapa katika muda mfupi ni kitendo cha wanaume wengi zaidi kuwa na makapu kununua mahitaji ya nyumbani. Ilikuwa nadra sana kuwaona wanawake wakifanya manunuzi hayo.

Tuliiacha darajani na kuambaa pembeni mwa mji mkongwe. Macho yangu yalivutiwa na nyumba za kale, ambazo baadhi zilijengwa zaidi ya miaka mia mbili iliyopita lakini bado zinatumiwa na binadamu hadi leo. Ajabu ni kwamba nyumba hizo zilijengwa kwa udongo, mawe na miti migumu kama mikoko ambayo mingi ingali imara hadi
 
leo. Kitu kinachovuta macho zaidi ni katika mji huu mkongwe ni mitaa yake. Nyumba hizo zilijengwa katika hali ya kubanana sana kiasi kwamba mitaa yake haiwezi kuruhusu gari kupita na hata baiskeli na pikipiki zililazimika kupita kwa uangalifu sana. Sura hii ya aina yake ya mji huu mkongwe ni moja ya sababu zilizopelekea shirika la elimu la Umoja wa Mataifa liutangaze kama moja ya maeneo ya kihistoria ambayo yanahitaji kuhifadhiwa.

Katika mwambao huo wa bahari nilifurahi sana kuliona jengo maarufu Beit el Ajaib lililojengwa na Sultani Bargash mwaka 1883. Jengo ambalo lina simulizi tele za kila aina. Kwa mfano inaaminika kuwa chini ya kila nguzo ya jengo hilo alizikwa hai mtumwa mmoja. Juu yake likiwa na mnara wenye saa kubwa pia linadaiwa kuwa la kwanza nchini na pengine Afrika nzima kutumia umeme na lifti.

Kando yake nililitembelea pia jengo jingine lililokuwa







likitumiwa kama ngome kuu ya Waarabu. Jengo hilo lenye ukumbi mkubwa na kuta pana lilipanda juu ambako kuna majengo na matunda maalum ya kutumia wakati wa vita. Hata hivyo sisi tulikuta tayari jengo hilo lina maduka, kumbi za wazi za burudani na biashara mbalimbali za sana.

Zanzinbar haina wanyama wengi kama bara. Inaaminika kuwa nchi hiyo haina tembo hata mmoja. Jambo ambalo linawashangaza sana wataalamu wa masuala ya wanyama pori kwani mwaka 1295, msafiri mmoja aliyeitwa Marco Polo aliitembelea Zanzibar kutoa taarifa ya kuwepo kwa mamia ya tembo na wanyama wengine.

Kama tusingekuwa wafungwa tungeshiriki katika ngoma ya ‘mwaka kongwa’ iliyokuwa ikipigwa wakati tukipita eneo la Makunduchi. Tuliishia kuchungulia dirishani tu na kuona wanaume wanavyotoana jasho kwa ndizi na migomba katika ngoma hiyo maarufu ya kila mwaka.

Zanzibar hiyo! Kwa machache niliyobahatika kuyaona, machache niliyopata kuyasikia na kuyasoma sikushangaa pale macho yagu katika tundu nililokuwa nikitumia kuchungulia nje yalipoweza kuona idadi kubwa ya watalii wa Kizungu wakipita hapa na pale katika mitaa, vichochoro na fukwe ya Zanzibar. Nilipata pia kusoma mahala kuwa takribani wageni wapatao 100,000 hutembelea visiwa vya Zanzibar kila mwaka kwa ajili ya shughuli za kitalii.

Gereza la Kiinua Mguu halikuwa tofauti na magereza mengine niliyopata kuyatembelea. Hadithi ilikuwa ileile, chakula kibovu, mlundikano katika selo, chawa na kunguni wakitawala, maradhi ya kila aina na vifo. Tulilala hapo siku tatu kabla ya kupakiwa katika moja ya zile meli zao ziendazo kasi, ambayo ilitufikisha pemba, katika mji wa Wete. Huko







tulielekezwa katika mashamba ya karafuu kuanza kazi.

Nilikuwa nikiifahamu karufuu kwa ladha tu, baada ya kuila sana katika pilau kule Pangani. Aidha, niliifahamu kwa harufu yake tamu puani toka katika marashi ya akina mama wa mjini wanaojiandaa kutoka. Sikupata kufahamu kuwa zao hilo lilikuwa na maajabu zaidi. Kwa mfano, sikujua kama karafuu ilikuwa tiba pia ambayo mafuta yake yalitumiwa kumchua mtu aliyeteguka viungo pamoja na tiba ya meno kwa mwenye maumivu. Nilishangaa zaidi kusikia kuwa karafuu, kwa baadhi ya watu, waliitumia kama sigara wakichanganya na vitu vingine walivyofahamu wao.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za kihistoria Sultan Sayyid Said aliyeitawala Zanzibar katika karne ya kumi na nane, alipofika kwa mara ya kwanza nchini humo alishangaa kuona mikarafuu miwili mitatu iliyoota hapa na pale kwa bahari tu ikiwa imestawi vizuri. Wakati huo karafuu likiwa zao hadimu kwa kupatikana katika maeneo machache ya Asia, Sultan huyo alipata wazo. Aliamini kuwa zao hilo lingeweza kuupa nguvu za kiuchumi na umaarufu utawala wake. Hivyo, alilima shamba lake binafsi kama mfano, akapanda miche arobaini na tano. Kisha, akatoa amri kila mtu kulima mikarafuu. Amri ambayo alihakikisha inatekelezwa kwa nguvu zake zote. Hadi anafariki Sultani huyo aliacha tayari biashara ya pembe za ndovu na watumwa ikitishiwa kiuchumi na ile ya karafuu.

Mkarafuu unapendeza kwa macho kama ilivyo harufu yake. Ni mti ambao unakuwa katika rangi yake halisi ya kijani kwa mwaka mzima. Mti huu huenda juu kwa mita kumi hadi ishirini. Maua yake ndiyo karafuu yenyewe. Yako katika sura na maumbile mbalimbali. Maua hayo hupitia rangi mbalimbali kama kahawia, kisha kijani na hatimaye wekundu ambao ndio







huwa dalili ya kukomaa na hivyo huvunwa.

Tulifundishwa yote hayo tukiwa katika uvunaji kazi ambayo ilituweka kisiwani humo kwa miezi mitatu.

Pengine kwa ajili ya ugumu wa usafiri toka kisiwani humo, pamoja na ugeni wetu, hatukushindwa sana kama ilivyokuwa bara na Unguja. Tuliruhusiwa kuchanganyika na wenyeji na, hivyo, kujipatia marafiki wengi wa Kipemba. Hata hivyo, tatizo lilikuwa kuelewana. Ilituchukua muda mrefu kukielewa Kiswahili chao ambacho ama kilichanganyika na kiarabu ama kiliathiriwa na makabila ya asili.

Pemba ilikuwa nyuma kimaendeleo ukiilinganisha na Unguja. Pamoja na kuwa mzalishaji mkuu wa zao hilo la karafuu na mazao mengine, bado wananchi wake wengi zaidi waligubikwa na umasikini. Nyumba zao nyingi zilisikitisha kwa kukosa hata milango, mavazi yao yalikatisha tamaa. Watoto na watu wazima kutembea pekupeku bila viatu ilikuwa jambo la kawaida sana.

Karume amejitahidi. Kila alichokifanya Unguja alikifanya pemba pia. Yale majumba yake marefu yalijengwa pia Wete na mkoani. Wanachi waliishi bila malipo. Hoteli kubwa kama ile ya bwawani pia ilijengwa katika kisiwa hiki kwa kiwango kilekile. Bado wananchi
 
wengi walikuwa taabani na nyuso zao zilionyesha kitu kama kutoridhika au kukata tamaa. Pemba kunani jamani? Nilijiuliza. Kwa kweli, pamoja na uhuru tuliokuwa nao miezi mitatu tulioishi huko niliona kama miaka mitatu ya kuishi katika gereza jingine la aina yake.





















YA ISHIRINI NA TATU

Tumaini Lilirorejea



asaibu ya maisha yanaweza kukupangia jambo ambalo hata hukupata kulifikiria. Mfano mzuri ukiwa wangu mwenyewe. Maishani mwangu

sikukusudia kuwa mhalifu wala sikupata kutarajia kamwe kujikuta nikiishi gerezani kama mfungwa. Lakini ufungwa nao una yake. Ufungwa wangu ulianza kugeuka kuwa utalii.

Mawazo hayo niliyapata tuliporejea toka Zanzibar na kupumzishwa wiki mbili kabla ya baadhi yetu kupangiwa safari nyingine. Mara hii safari yetu ilikuwa ya kueleka Kusini, mkoani Mtwara, ambako tuliombwa kusaidia kazi ya kuchimba mtaro wa kupitisha gesi katika eneo fulanifulani ambayo waajiriwa wa kawaida waligoma kwenda kutokana na ugumu wa mazingira. Sisi, watumwa wasio na wenyewe tulipewa amri tu, ‘Skoch’ ya Mtwara kesho.

Sikupata kufikiria kwenda Mtwara hata mara moja katika ndoto zangu za kimaisha. Mtwara kufanya nini? Wana Mtwara wenyewe walikuwa wanaikimbia. Msamiati wa ‘Wamachinga,’ wale wafanyabiashara vijana, ambao huzunguka na bidhaa zao kila mtaa na kila uchochoro wa jiji la Dar es Salaam, ulizaliwa kutokana na vijana wa Mtwara, pale walipoanza kumiminika mjini baada ya kukata tamaa







vijijini. Walikuja kwa mamia, kutwa wakisaga lami na vumbi la Dar, usiku wakilala kwa dhiki katika vichochoro vya Kariakoo, biashara zao maelfu zikilindwa kama roho zao. Taratibu walianza kuwatishia wamiliki wa maduka, wengi wao wakiwa Wahindi, pale wateja wao walipopunguza kuingia madukani na kuishia kwao. Waliwatishia pia maafisa wa kodi kwani kodi toka kwa wenye maduka zilipungua na kumdai Mmachinga ambaye hujui anaishi wapi, duka lake anatembea nalo, haikuwa kazi rahisi.

Wakati huo ‘Wamachinga’ walichukuliwa kama Wamakua na Wamakonde pekee. Hata jina lao lilitokana na kile kijiji cha Mchinga kilicho Pwani ya Bahari ya Hindi, maili chache toka Lindi. Lakini mafanikio yao tayari yamewavuta Wasambaa na biashara zao za matunda toka Tanga, Wagogo na kahawa zao toka Dodoma, Waha na baiskeli zao toka Kigoma na wengineo. Wote wanafanya kazi za kimachinga na wameafiki jina hilo la Wamachinga pamoja na serikali kuwatafutia majina mbalimbali ya kutia matumaini kama ‘Wajasiriamali, ‘ au ‘Wafanyabiashara wasio rasmi.’

Moja ya sababu zilizofanya nisiote ndoto ya kwenda Mtwara ni zile sifa za ugumu wa safari za kwenda huko. Usafiri wa meli haukuwa na uhakika. Ilisikika habari ya meli moja tu, tena ya mizigo, ambayo ungeisubiri kwa mwezi au miezi kabla ya safari. Meli ambayo ilidaiwa kufurika kupita kiasi na hivyo kuhatarisha maisha ya wasafiri mara kwa mara. Enzi hizo kufikiria safari ya barabara ilikuwa wazimu zaidi. Njia ilikuwa ndefu kuliko ilivyostahili kutokana na ubovu. Yalikuwepo maeneo yasiyopitika, magari ya madereva vichwa ngumu yakizama au kukwama kwa zaidi ya wiki katika tope kabla ya kufikia kivuko cha mto Rufiji na matawi yake.







Pengine kama si kizingiti cha barabara hiyo Mtwara ya leo ingeweza kuwa mfano wa aina yake wa utajiri wa Tanzania, kwani neema ya uchumi ilikuwa imeishukia Mtwara mwaka 1948 Waingereza walipouteua mkoa huu na kongwa Dodoma, maalumu kwa ajili ya kilimo cha karanga. Ekari milioni 325 au kilomita za mraba 13,200 zilitarajiwa kulimwa katika kipindi cha miaka sita na hivyo kuilisha Tanganyika Ulaya nzima karanga na mazao yote yatokanayo na karanga.

Mradi huo ulitengewa dola za Marekani milioni 25. Askari wastaafu laki moja na wakazi wengine tele waliojitokeza kufanya kazi hiyo. Hata hivyo, baada ya jitihada za muda mrefu na kupotea kwa dola milioni 49 zaidi ya zilizotarajiwa kazi ilishindikana. Sababu? Ukosefu wa barabara. Reli iliyokuwepo, ambayo ilitarajiwa kutumiwa kwa usafirishaji wa vifaa na mazao ilichukuliwa na mafuriko ya mto Kinyensungwe. Usafirishaji wa vifaa kama matrekta na mbolea kupitia mto Ruvu nao ulikutana na vizingiti tele; tembo, vifaru na viboko walitishia maisha ya wafanyakazi na hivyo wengi kukimbia. Maradhi ya malaria na matumbo kwa ajili ya maji yasioaminika nako kulichangia.

Jambo jingine ambalo lilisababisha mradi huu kushindikana ni mibuyu. Vifaa vidogovidogo vilivyoweza kufika huko havikuwa na uwezo wa kuing’oa mibuyu mikubwa iliyotanda katika baadhi ya maeneo ya shamba. Si hivyo, baadhi ya mibuyu hiyo ilikuwa na maajabu yake. Baadhi ya mibuyu ilishindikana kutokana na wingi wa nyuki waliokuwa wameweka makazi yao humo, ambao waliwatawanya wakulima hao hadi wakashindwa kufanya kazi yao. Mibuyu mingine ilitumiwa na wenyeji kama matambiko, wasingekubali kamwe







ing’olewe. Mbuyu mmoja ulitumiwa kama gereza kwa ajili ya wahalifu. Huu pia usingeng’olewa.

Hayo na mengine tele yalisababisha tani 2000 tu za karanga zipatikane baada ya miaka tele ya majaribio kabla ya bunge la Uingereza halijatamka rasmi kuuachilia mbali mradi huo mwaka 1951. Kupotea kwa tumaini hilo kuliambatana na kusahauliwa kwa Mtwara, na hivyo kuibuka kwa ukimbizi wa vijana wenye nguvu, kwenda mijini kutafuta maisha kwa ‘Umachinga’.

Hivyo, kugunduliwa kwa gesi, kulikofanywa na kampuni ya Artumas Co. katika mkoa huo ilikuwa neema ya pekee kwa Mtwara na wakazi wake. Lilikuwa tumaini lilirorejea kwa Wamachinga.



* * *

Kwa mujibu wa taarifa zisizo rasmi, ambazo kama wafungwa tulizipata toka hapa na pale wakati tukifanya kazi yetu ya kuchimba
 
mitaro ni kwamba gesi hiyo iliyogunduliwa ingeweza kutumiwa na mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kupikia, kuendeshea viwanda na mahitaji yote ya umeme kwa zaidi a miaka 800.

Taarifa hizo ziliongeza kuwa uamuzi wa serikali ulikuwa kuhakikisha wakazi wa Mtwara, ambao kwa mwaka 2002 walikuwa 1,128,523 wote wanapatiwa fursa ya kuitumia nishati hiyo kwanza kabla haijaruhusiwa kwenda kuwahudumia watu wengine.

Gesi hiyo iligunduliwa Mnazibay, ambako tulipelekwa kufanya kazi. Zilikuwepo pia fununu za nishati hiyo kugunduliwa katika sehemu mbalimbali za mikoa hiyo ya kusini.







Kazi ya kuchimba mitaro hiyo haikuwa rahisi. Kulikuwa na ule wa kupitisha bomba la kuileta gesi hadi Dar es Salaam ambako tuliambiwa kuwa viwanda kadhaa kikiwemo kile maarufu cha Simenti, Wazo, tayari vilikuwa kutumia nishati hiyo badala ya umeme wa TANESO uliozolekea. Umeme ambao ulitegemea zaidi maji ya mvua hivyo, licha ya gharama kuwa kubwa miaka yenye mvua haba ulikuwa matatizo kibao kiasi cha kuanzisha msamiati wa aibu ‘mgao wa umeme.’

Tulifanya kazi yetu kikamilifu, siku tulizopangiwa tulirejeshwa Ukonga, siku zangu za kukaa kifungoni zikifikia ukingoni.

Siku moja bado tukiwa huko Mtwara, nilitembelewa na wazo la ajabu. Kuoa! Sijui wazo hilo lilipenyaje katika kichwa changu kilichofura kwa matatizo na migogoro isiyo na kifani. Mfungwa, asiye na mbele wala nyuma, nawezaje kufikiria kuoa?

Mimi wazo hilo lilinitembelea. Chanzo chake hakikuwa zaidi ya Lulu, msichana wa Kimakua ambaye alitembelea gereza tulilokuwemo akiwa amefuatana na maafisa wenzake wa ustawi wa jamii. Walituweka kikao kwa maelezo kuwa wamekuja kuzungumza nasi kuhusu ya maisha ya uraiani kwani wengi wetu vifungo vyetu vilikuwa vikifikia ukingoni.

Walizungumza mengi. Lakini naapa kuwa hakuna aliyekuwa akiwasikiliza. Lulu, akimeremeta kwa ngozi yake laini ya maji ya kunde, sauti yake ya upole na tabasamu lililosindikiza kauli zake alivutia zaidi ya nasaha zao. Wafungwa wengi walionekana hivyo na walinong’onezana hivyo. Hali ambayo ilidhihirisha zaidi pale tulipopewa wasaa wa kuuliza maswali. Mfungwa wa kwanza alielekeza swali lake moja kwa moja kwa Lulu “Samahani dada Lulu, umeolewa?”







Kila mtu alicheka, ikiwa pamoja na Lulu mwenyewe. “Sijaolewa. Unataka kunioa?” alimjibu na kumtupia

swali pia.

“Huyu akuoe? Atakulisha nini?” alidakia mfungwa mwingine na kuongeza. “Kwanza ni mzee. Kisha hajui kusoma wala kuandika. Kama kuna mume hapa ni huyu mdogo wetu,” alisema akielekeza kidole chake kwangu. “Ni msomi, anazungumza Kiingereza kama Kiswahili. Hata humu ndani amekuja kama ajali tu,” aliongeza.

Sikutarajia kauli kama hiyo. Nilishikwa na aibu kuona kila mtu akinitazama. Lulu Kalenje, kama alivyojitambulisha, alitabasamu kabla hajatamka taratibu, “Naona nimeshapata mchumba. Kwani kaka unaitwa nani?” aliniuliza.

“Petro Kionambali.” Nilimjibu

“Unatoka upande upi wa nchi hii?” aliongeza swali jingine.

“Natokea Kigoma.” “Wewe Muha?” “Haswaa.”

Lulu akacheka tena kabla hajasema. “Sioni kama uchumba wetu utadumu. Watu wa Kigoma hamtuwezi kabisa Wamakua. Tuna tofauti kubwa ya kiutamaduni.”

Nilimwelewa haraka. Nilikuwa nimejifunza mawili matatu juu ya mkoa wa Mtwara na makabila yake kadhaa.

Wageni hao walipoona maswali ya kijelajela yakiongezeka badala ya yale waliyoyakusudia waliaga na kuondoka. Wenzangu walitawanyika. Mie nilibakia palepale kwa muda nikitafakari. Wazo la kupenda na kuoa kwa ujumla lilitokea kusikojulika. Lilijikita kwa muda katikati ya ubongo wangu.

Nilitamani kuoa!







Nilitamani kumwoa Lulu!

Nikamfikiria Lulu, mtoto wa Kimakua. Sikupata kuishi Mtwara. Lakini katika maongezi na tafiti zangu vitabuni nilikuwa nafahamu mengi juu ya mila na tamaduni za Wamakuwa na jirani zao Wayao.

Mtwara, ambayo iko kusini mwa Tanganyika, ikiwa imetengana na nchi ya Msumbuji kwa mto Ruvuma inayo makabila mengi. Makubwa kati yake yakiwa Wamakonde na Wamakua ambao waliingia kutokea Msumbiji. Wayao wanaaminika kutokea Malawi. Hizo zikiwa zile enzi za kuhama kabla ya ujio wa watu weupe ambao walifuatiwa na uamuzi wa uroho na uchoyo uliopelekea kuwekeana mipaka baada ya kupora hiki na kile.

Wamakua na Wayao wanapofikia umri wa miaka kumi hadi kumi na mbili lazima wapitie unyago. Jukumu hilo, huendeshwa na wazee wa kike waliobobea katika masuala ya familia.

Wahusika hulazimishwa kutunza siri yoyote watakayo fundishwa au kuonyeshwa katika mafunzo hayo. Miongoni mwa mafunzo hayo ni jinsi ya kujitunza. Wavivu na jeuri hupewa maneno ya kuwatisha ili waachane na tabia hizo na masuala mengine ambayo somo ataona lazima kuyasisitiza.

Mafunzo hayo hufuatiwa na sherehe za mkesha, ngoma aina mbalimbali kama chimakuani, mtotamto, mselemba na nyinginezo hutumbuiza. Sherehe ambazo huambatana na vinywaji hasa pombe ya mtama ambayo huandaliwa maalum kwa shughuli hiyo.

Yote hayo niliyachukulia kama kawaida. Ambacho nilikiona kizito ni ule utamaduni wao wa kumfanya mtoto mali ya mama zaidi ya alivyo kwa baba. Kwa maana nyingine mtoto







anamsikiliza zaidi mjomba. Ujombani ndio kwao zaidi na ndiko anakokulia.

Kwa falsafa yao mama ndiye hasa anayemjua baba wa mtoto na mama ndiye anayekaa na mtoto tumboni kwa miezi tisa na kumnyonyesha kwa miaka miwili. Baada ya hapo ni yeye anayemlisha na kumvisha hadi anapofikia umri wa kuweza kujitegemea. Hali hiyo husababisha Mmakua au Myao anapooa anahama kwao na kwenda ukweni ambako atapewa shamba na kuonyeshwa mahala pa kujenga ‘mdule’ nyumba zao, ambazo hujengwa kwa fito na udongo paa likiwa la nyasi. Huo huwa
 
SEHEMU YA 135

mwanzo wa maisha mapya ya kijana huyo ambaye hata majina ya watoto wake hutolewa na wajomba.

Kwa jinsi nilivyomfahamu baba yangu, mzee Karimanzira Kionambali, sikuiona namna yoyote ambayo angeweza kukubali niingie katika utamaduni wa aina hiyo.

Jingine lililonitisha ni ule utamaduni wao wa kula ‘dagaa changa’ yaani panya. Makabila mengi ya kusini panya ni mlo halali wanaouthamini sana. Unaweza kutengenezewa kitoweo murua, ambacho kitavutia sana, ukala na kushiba bila kujua kuwa unakula panya. Sikuwa tayari kubahatisha hilo pia!

Kwa kheri Lulu! nilivunja uchumba kimoyomoyo. Uchumba ambao hata ulikuwa haujaanza rasmi, mchumba mwenyewe akiwa hata hazifahamu hisia zangu.



* * *

Sitaweza kuisahau tarehe ya kufunguliwa kwangu. Ni tarehe ambayo nimeishi nayo akilini kwa takribani miaka ishirini nikiisubiri kwa hamu. Lakini pale ilipofika na jina langu kutajwa nikiitwa ofisini nilijikuta nikitetemeka kidogo. Wakati wafungwa wenzangu wakinipongeza kwa kutoka







kwangu salama, mimi nilitokwa na machozi. Waliyachukulia kuwa machozi ya furaha. Laiti wangejua!

Nilikabidhiwa vitu vyangu. Suruali mbili, mashati mawili, viatu na kabrasha langu la vitabu. Nililipokea kabrasha hilo harakaharaka na kulikagua. Kitu nilichokuwa na shauku ya kukiona kilikuwepo! Kitabu changu cha benki. Nikakifunua. Akiba yangu ilikuwa kama nilivyoiacha, shilingi 3,500. Nikakitia mfukoni. Nikakabidhiwa tiketi ya treni, daraja la tatu, ambayo ingenifikisha hadi stesheni ya Kigoma. Toka hapo ningejitegemea kufika Kasulu na hatimaye kijijini kwetu.

Nilikuwa mgeni sana Dar es Salaam. Toka nilivyofika kwa muda ule mfupi na akina Leakey sikupata kurudi tena. Sikuwa na wenyeji wala rafiki ambaye angeweza kunipokea. Hivyo, pale lango la gereza lilipofunguliwa nami nikaruhusiwa kutoka sikujua toka hapo ningeelekea upande gani wa dunia.

Kweli Mungu si Athumani. Wakati bado nashangaa hapo nje gari la mkuu wa gereza lilitokea. Aliponiona akaniita. “Hongera,” alisema “Nategemea hutajiingiza tena katika jambo lolote la kinyume cha sheria ambalo linawea kukurejesha hapa.” Baada ya maneno hayo aliutia mkono wake mfukoni na kuuchomoa ukiwa na noti tatu za elfu kumikumi. Shilingi 30,000! Sikuyaamini macho yangu.

“Mbona nyingi sana mzee?” nilimuuliza

“Nyingi?” alijibu akicheka. “Hazikutoshi, lakini zitakusadia.” Akalitia gari lake moto na kuondoka zake hata kabla sijamshukuru kikamilifu.

Kwa maelekezo ya wapita njia nilifika kituo cha mabasi ya mjini wenyewe waliyaita ‘daladala’. Nikauliza basi la kuelekea stesheni ya treni, nikapanda, kondakta, kijana mdogo mweye lugha ya kihuni alikuwa mtu wa kwanza aliyenipa mshangao







wangu wa kwanza. Ni pale aliponiomba nauli nami kumpa moja ya zile noti nilizopewa na mkuu wa jela. Nilihesabu kwa makini chenji alizonipa. Alikata shilingi mia mbili.

“Nauli mia mbili?” nilifoka.

“Kumbe ngapi?” alinijibu kwa swali vilevile. Alinitazama kwa makini. Nywele zangu zilizoanza kuingia mvi ziliashiriwa ovyoovyo. Suruali yangu iliyopauka ilikuwa pana kiunoni, fupi miguuni ikinifanya nionekane kama moja ya vile vikatuni vinavyochorwa magazetini, sura yangu pia, nadhani ilionyesha ugeni na mshangao kwa kila nilichokiona, wingi wa watu wa magari, wingi na ukubwa wa majengo na kadhalika.

“Au umetoka pale mjomba?” Yule kondakta alihoji. “Pale wapi?” nilimuuliza

Pale mtakuja, ukumbi wa wanaume,” alijibu akielekeza mkono maeneo ya gereza.

“Unauliza jibu?” abiria mmoja alidakia.

Sikuwajibu. Hofu niliyokuwanayo juu ya maisha ya uraiani ilianza kunirejea. Shilingi mia mbili kabla sijaingia gerezani ilitosha kumsomesha mtoto wa mwaka mzima. Wakati huohuo kodi ya chumba kwa mpangaji ilikuwa senti ishirini, shati senti kumi. Nauli halali ya basi kama hilo isingezidi senti tano.

Kumetokea nini? Nilijiuliza. Tulipita Tabata, tukaingia barabara ya Mandela na kuifuata hadi Buguruni ambako tulichukua barabara ya Pugu kueleka mjini. Barabara hiyo ikiwa barabara pekee inayoelekea uwanja wa ndege wa Julius Nyerere magari yalikuwa tele barabarani yakishindana kwa kasi. Aidha, barabara hiyo ilikuwa katikati ya viwanda mbalimbali vilivyotapakaa hadi Chang’ombe na Vinginguti, hali iliyozidi kuipa purukushani za aina yake. Mwendo wa kasi







wa magari hayo na majonjo ya dereva wetu utadhani hana roho vilinitia roho mkononi hadi tulipofika kituo cha stesheni ambapo nilishuka.

Mshangao wa pili ulinisubiri nilipofika stesheni. Nilikuta pamefurika watu, wengi wao wakiwa na mizigo tayari kwa safari. Lakini nilipofika dirisha la tiketi kwa nia ya kuithibitisha tiketi yangu niliulizwa swali ambalo sikutarajia.

“Unataka kuondoka lini?” “Leo.”

“Haiwezekani. Nafasi zimejaa. Labda ufanye booking ya siku nyingine.”

“Haya, nipe tiketi ya kesho.” “Kesho hakuna treni.” Sikuelewa. “Kwa nini?”

“Treni ni mara tatu kwa wiki,” alinifafanulia. “Na ratiba yangu hapa inaonyesha kuwa daraja la tatu limejaa hadi baada ya wiki tano hivi.”

Sikuamini kama nilikuwa nimemsikia vizuri. Treni inasafiri kwenda bara mara tatu kwa wiki! Treni hiyohiyo ambayo wasafiri ni wengi kiasi cha kuifanya ijae hadi kwa wiki tano zijazo! Treni hiyohiyo ambayo ilikuwa ikisafiri kila siku na abiria wakichagua kiti cha kukaa!

“Kwani kumetokea nini?” nilimuuliza karani huyo.

Alinitazama kwa macho ya mshangao kana kwamba nina pembe ya faru usoni. Nadhani aliishuku hata akili yangu. Kwani badala ya kunijibu alifunga dirisha lake.

Kijana mmoja aliyekuwa pembeni akifuatilia majibizano yetu alinivuta kando na kuniuliza “Unataka tiketi ya kuondoka leo? Toa kitu kidogo tu utasafiri.”

“Tiketi ninayo.” Nilijibu nikimwonyesha.







“Sasa tatizo lako nini? Treni ikifika panda. Hakuna

atakayekushusha. Mradi uwe tayari kwenda wima.” “Wima! Toka Dar es Salaam hadi kigoma!”
 
Niliamua kuufuata ushauri wa kijana huyo. Bado zilikuwepo saa sita kabla ya treni kufika, masaa mawili kabla ya muda wa kuondoka. Nikaamua kuutumia muda huo kutafuta benki ambayo nilikuwa nimefungua akaunti yangu.

Ilikuwa kazi nyingine ngumu. Mji ukiwa umepanuka sana, majengo mengi yakishindana kwenda angani, huku watu wakiwa tele na pilikapilika kibao ilinichukua muda kabla ya kumpata mtu aliyenielekeza hadi kuifikia benki hiyo.

Afisa niliyeelekezwa kwake alinipokea kwa heshima zote katika chumba chake kidogo chenye hewa safi iliyokuwa ikitoka katika kiyoyozi. Hewa ambayo iliniburudisha sana kutokana na jasho tele lililokuwa likinitoka. Akapokea kitabu changu na kukitazama kwa mshangao kidogo. Nadhani kwa umri wake hakupata kuona aina hiyo ya kitabu, kwani vilishabadilishwa mara nyingi. Hata hivyo, alipoichezea kompyuta yake kwa muda mrefu aliliona jina langu.

“Petro Kionambali sio?” akauliza. “Ndiyo,” nilimjibu kwa matumaini. “Mbona huna pesa?” aliniuliza tena

Sikumwelewa, “Kwa vipi? Mara ya mwisho nilikuwa na elfu tatu.”

“Ni kweli kabisa,” alijibu. “Miaka ipatayo ishirini na mbili akiba yako ilikuwa elfu tatu. Halafu ukapotea. Gharama za kutunza akaunti yako na kushuka kwa thamani ya pesa kumefanya uwe huna pesa kabisa. Kwa kweli, benki inakudai.”

Ulikuwa mshangao wangu wa tatu katika siku yangu ya kwanza uraiani. Nilihisi naishiwa nguvu, miguu na mikono







ikitetemeka. Pamoja na kiyoyozi jasho jembamba lilianza kunitoka. Kwa sauti dhaifu niliuliza, “Unasema? Sijakuelewa… Nilitarajia fedha zangu ziwe zimeongezeka sana. Unajua wakati ule fedha zile zingenitosha kununua magari hata mawili na kujenga nyumba?”

“Ni kweli kabisa,” alinijibu. “Tatizo lilikuwa lako wewe. Benki ikaendelea kukata gharama zake, fedha zikaendelea kushuka thamani. Kibenki elfu tatu ni elfu tatu tu. Ungekuwepo ukazitumia zingezalisha faida. Kwa bahati mbaya ulipotea. Kwani ulikuwa wapi mzee?”

Sikumjibu. Nilijikongoja kuinuka. Nikapepesuka. Nikajikongoja tena kutoka nje ya ofisi hiyo, macho yakiwa hayaoni vizuri, miguu ikiwa haina nguvu.



.























YA ISHIRINI NA NNE

Dar jiji la Raha na Karaha



ar es Salaam niliiona chungu. Watu, majengo, magari na kila nilichokiona mbele yangu kilinitisha na kuniogofya. Ndiyo, mji ulikuwa

mzuri, uking’ara kwa usafi. Barabara zilimeremeta kwa usafi, magari yakipendeza ubora na thamani. Watu pia walipendeza mitaani.

Wengi wao walivaa mavazi ya bei, waliharakisha kwenda hapa na pale huku nyuso zao zikiwa na dalili za matumaini kinyume cha ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Yote hayo niliyaona na yalinivutia, lakini bado Dar es Salaam niliiona chungu. Ilikuwa baada ya lile pigo la mwisho pale benki. Pigo ambalo liliniacha taabani, nusu hai nusu maiti.

Sikujua nilitoka vipi pale benki hadi stesheni ya reli. Sijui ilikuwaje hata nikafika huko bila kugongwa na moja ya magari tele yaliyotapakaa barabarani kama siafu. Mradi nilijikuta mbele ya stesheni, macho yangu yakikodolea macho saa kubwa ya kwenye mnara. Ilionyesha kuwa bado kulikuwa na saa kama tano kabla ya treni kufika! Saa tano, ambazo niliziona kama miaka mitano! Sikuwa na jinsi. Ilibidi niendelee







kusubiri. Kila dakika moja ya kuendelea kusubiri ilinitesa kama msumari wa moto moyoni.

Mara kwa mara, nilitoa zile senti zangu nilizopewa na mkuu wa gereza na kuzihesabu. Nilikuwa nimezipunguza kwa nauli ya daladala. Mia moja nyingine nililazimika kuzitumia kwa huduma ya choo! Nilikuwa na kiu lakini kila bomba nililofungua halikutoa maji. Baadhi ya ‘wamachinga’ walikuwa wakiuza maji ya chupa. Chupa ndogo mia tatu, kubwa mia saba hadi elfu moja. Maji ya kununua? Maji ambayo utoto wangu wote nimeyachezea katika mito, katika maziwa na hata baharini! Niliamua kujikaza kisabuni.

Nilikuwa na njaa vilevile. Lakini sikuthubutu hata kuuliza bei ya chakula. Nilijua ingebomoa zaidi visenti vyangu ambavyo sasa ilikuwa akiba yangu pekee maishani mwangu. Akiba ambayo ilikuwa lazima inifikishe nyumbani kwetu. Nikaamua kuivumilia njaa vilevile, nikifumbia macho watu wanaokula na kuizibia pumzi harufu tamu ya maakuli.

Saa zilikuwa haziendi. Nikaamua kupitisha muda kwa kutembeatembea mitaani. Nilifuata barabara ya Samora. Macho hayana mipaka, yangu yalipenya vioo vya maduka mbalimbali na kushuhudia vitu vilivyofurika madukani. Vifaa vya elekrtroniki, kama televisheni, deki, dvd, projekta na vinginevyo vilikuwa tele katika sura na bei mbalimbali. Nguo, viatu, pochi za kinamama na vinginevyo vilikuwa tele. Duka moja lilibandika bei kwenye bidhaa zake, viatu 120,000/= suti 550,000/= pochi 85,000/=! Sikuelewa. Sikuelewa zaidi pale nilipoona maduka hayo yakiwa yamejaa watu wakinunua vitu hivyo kwa fujo kana kwamba wana viwanda vya kuchapa noti. Macho yangu yalivutwa pia na watu, hasa wasichana.

Mavazi yao yalinitisha. Baadhi walivaa nguo fupi sana,







mapaja wazi, sehemu kubwa ya tumbo nje huku wakitembea hadharani bila wasiwasi wowote. Baadhi ilikuwa vigumu kujua kama walikuwa wasichana au wavulana kwa suruali zao za jeans. Fulana na kofia kwenye vichwa. Kitu kingine kilichonishangaza ni kuona wasichana wengi walivyofanana. Karibu wote walikuwa weupe! Karibu wote walikuwa na nywele za kizungu! Wengi midomo yao iling’ara kwa rangi nyekundu kama ndege! Wengi walinukia manukato makali ambayo siku za nyuma ungeamini kuwa umepishana na jini! Sikuelewa hali hii hadi nilipofikia duka moja lililokuwa likiuza aina mbalimbali za nywele kama nilizoona kwenye vichwa vya akina dada na kila aina ya vipodozi! Kumbe!

Wavulana wengi nao walinikatisha tamaa. Walivaa jeans zao ambazo zilichakaa au kuchakazwa makusudi, sweta au fulana zenye picha za wacheza sinema wa Marekani kama Rambo na
 
schwarznegger, huku wakiwa wamefunika vichwa vyao kwa kofia au vitambaa vyenye nembo za bendere ya Marekani. Baadhi yao walisuka nywele zao, baadhi walivaa hereni! Ilikuwa vigumu kujua kuwa vijana hao walikuwa Watanzania au Wamarekani weusi hadi pale utakapowasikia wakizungumza Kiswahili. Lakini Kiswahili hicho nacho kilikuwa na manjonjo yake. Kwa kweli, kilistahili kuitwa Kiswaengilish kwa jinsi kilivyochanganywa maneno ya Kiingereza na hata ya mitaani ambayo watu kama Shaaban Robert wangefufuka, wangeweza kuangua kilio.

Wakati huo nilikuwa tayari nimeloa chapachapa kwa jasho. Joto la hapa, mara nyingi linatisha. Nilitamani kununua leso kama nilivoona wengine wakifanya lakini sikuthubutu. Shilingi mia tatu za kulipia kitambaa hicho niliziona kama milioni. Nikawa nikitumia kiganja au kiwiko cha mkono walao







kupunguza jasho la usoni ili niweze kuona niendako.

Wingi wa watu lilikuwa tatizo jingine. Mara kwa mara, niligongwa na mtu au kupigwa kikumbo kilichofanya nikaribie kula mweleka. Nilipogeuka kumtazama mtu niliyegongana naye alikwishakwenda zake bila hata kugeuka nyuma. Hiyo ilinifanya nikumbuke kile nilichosoma nikiwa gerezani juu ya kasi ya ongezeko la watu jijini hapa. Kwamba mwaka 1925 mji huu ukiitwa Mzizima ulikuwa na watu 30,000 tu. Leo unatisha.

Nilifika katikati ya mji wa Dar es Salaam. Pale nilipopita miaka mingi iliyopita na kusimama mbele ya sanamu ya yule Mjerumani machachari Bismarck akiwa na bunduki mkononi kaielekeza baharini. Sanamu hiyo haikuwepo tena badala yake ilijengwa sanamu ya askari mweusi kama mkaa, ikiwa na silaha vilevile kuashiria tulivyopigana na kufa kwa vita ambavyo havikuwa vyetu. Niliitazama kwa muda kabla ya kuendelea na safari yangu, taratibu hadi nilipoifikia bustani ya Ikulu. Miti mingi ya asili ilikuwemo kama nilivyoiona mara ya mwisho. Hata hivyo, nilihisi kuwepo kwa aina fulani ya upungufu. Nini kilichopungua? Nilijiuliza. Nikajibiwa na ukimya mkubwa wa eneo hilo. Ni ukimya huo ulionipa jibu. Zile kelele za wanyama na ndege mbalimbali, hasa tausi, hazikuwepo tena. Tausi wale, ambao mara ya mwisho walinivutia sana kwa jinsi walivyoipamba bustani hiyo kwa maringo na ulimbwende, mara kwa mara wakitoa sauti zao nzuri na kuifumua mikia yao iliyoficha kila aina ya rangi hawakuwepo tena. Walienda wapi? Nilijiuliza bila matarajio ya jibu lolote.

Nikashuka kilima cha Ikulu na kufika Pwani ya Magogoni. Kigamboni ilikuwa upande wa pili wa bahari kama nilivyoiacha. Lakini, sasa, badala ya kuvuka kwa mitumbwi ya makasia kulikuwa na chombo maalum ambacho kilipakia







watu, magari, mazao na hata mifugo yao na kuwavusha upande huu au ule. Nilitamani kuvuka katika kupoteza muda. Lakini nilipoambiwa kuwa ningelazimia kulipia, niliachana na mpango huo.

Nikalisogelea soko la mnada wa samaki. Biashara ilikuwa ikiendelea kama kawaida. Kando kidogo, akina mama walioitwa ‘mama ntilie’ walikuwa kazini wakitoa huduma ya chakula kwa haraka na kwa bei nafuu. Wakati huo tayari natetemeka kwa njaa, chango likinguruma kudai chochote, nilishindwa kujizuia zaidi. Nikaingia katika banda la mmoja wao na kuomba wali kwa samaki. Nilikula wali mtamu sana wa nazi ambao sikupata kuula kwa takribani miaka ishirini. Hata kabla sijakitafuna kichwa cha samaki wangu mmoja kunguru tele waliozagaa huko na huko jiji zima alitua ghafla na kukipokonya. Huyoo, akapaa hadi juu ya paa na kuanza kukila huku kunguru wenzake wakimshangilia. Watu wawili watatu walicheka. Mama ntilie wangu akaniongeza mboga, nikaendelea kula nikimlaani kunguru yule.

Nikakumbuka kusoma mahala, ama gazetini ama kitabuni, juu ya tatizo la ndege hao waliozagaa mjini Dar es Salaam, kwamba wameondokea kuwa kero ya kitaifa; wanaiba kila kinachoibika ikiwa pamoja na nyaya za umeme au vifaa vingine vya kiufundi. Kwamba ndege hao waliletwa nchini, kupitia Zanzibar mnamo miaka ya 1900 na wakoloni wa Kiingereza kwa kusudi la kuwafanya wasaidie usafi kutokana na tabia yao ya kula mabaki ya chakula, mizoga na takataka nyinginezo. Lakini hadi kufikia mwaka 1930 walijifanya ndege wa mjini ambao ni nadra sana kuonekana vijijini.

Nikauliza saa. Nilikuwa nimetumia saa moja na robo tu toka nilipoondoka stesheni. Bado nilikuwa na muda wa







kutosha. Nikaamua kutembea tena, safari hii nikielekea Kariakoo. Kinyume na safari yangu ya mwisho mjini hapo sikuona pori wala jani. Kisutu ambayo zama zile nusu yake ilikuwa pori, fisi wakirandaranda kutafuta chochote, sasa ilikuwa sehemu ya mji iliyotapakaa watu na majengo hadi upeo wa macho. Kilabu cha askari wa zamani kilikuwa pale. Lakini sasa kilijengwa jengo bora zaidi la ghorofa likiwa na wapangaji tele wenye shughuli zao. Ukumbi ulikuwa pale lakini haukuwa na pilikapilika zile za zamani. Ama wanachama wengi walikuwa wamekufa kwa umri mkubwa ama wamekata tamaa.

Kariakoo nayo ilikuwa muujiza mwingine. Pengine soko jipya lililojengwa juu ya lililokuwa handaki la kivita enzi za Mjerumani lilikuwa limevuta watu toka kila pembe ya mji na nchi ama Mungu alikuwa amedondoshea neema eneo hilo. Si haki kabisa kusema watu walikuwa wengi, bali walifurika! Mitaa ya Kongo na Msimbazi ilikuwa haipitiki. Kila mmoja akiwa na pilikapilika zake. Nje na ndani ya soko ndiyo ilikuwa kabisa. Kupumua peke yake ilikuwa shida, achilia mbali kutembea.

“Dingi vipi… mbona unashangaashangaa? Ambaa tupite,” kijana mmoja alinifokea baada ya kunipiga kikumbo.

Nikageuka kumtazama.

“Unashangaa nini? Kashangae feri, ambako shilingi inazama meli inaelea. Siyo hapa.”

Aliongeza.

Sikumwelewa kabisa. Nikajikokota kuondoka.
 
Ilikuwa kazi kubwa kujichoropoa toka katika umati huo na kuifuata barabara ya Uhuru hadi stesheni ambako niliamua kukatisha moja kwa moja na kuisubiri treni.

Nilijiunga na wasafiri wenzangu, wengi wao wakiwa na







mizigo na familia zao. Mmoja kati yao, aliyekuwa na mizigo mingi zaidi alikuwa msichana wa Kizungu. Mwembamba, mwenye pua ndefu na sura ya utulivu. Alikuwa peke yake akilinda mizigo yake kwa makini. Hali hiyo ilinifanya mie pia nizikumbuke pesa zangu. Nikatia mkono wangu mfukoni kwa nia ya kuzipapasa.

Mfuko ulikuwa mtupu! Nilishtuka kama niliyeguswa na waya wa umeme. Nikainuka na kukagua kila mfuko wangu. Hamkuwa na kitu. “Nimeibiwa!” nilisema kwa sauti huku nikitetemeka. Msafiri mmoja aliyekuwa akisubiri usafiri kama mimi aliniuliza taratibu, “Umeibiwa nini mzee?”

“Pesa,”” nilimjibu. “Nyingi?”

“Hapana za kutosha lakini. Zilikuwa pesa zangu pekee.”

“Pole sana. Alisema. Umeibiwa hapa?” “Hapana. Bila shaka ni Kariakoo.”

Alinishangaa, “Ulienda Kariakoo? Kule hakufai kabisa.” Nikamkumbuka yule kijana aliyenipiga kumbo na kisha kuniita ‘Dingi’. Nilihisi hatukugongana naye kwa bahati mbaya. Alikusudia. Ni yeye aliyeniibia au kuandaa mazingira ya kuibiwa kwangu. Sasa sina hata shilingi moja. Sina kitu chochote ninachoweza kuuza nipate walao nauli ya kunitoa

Kigoma mjini na kunifikisha Kasulu!

Badala ya kulia niliangua kicheko. Kwa jinsi nilivyovaa, nilivyochakaa kwa jasho na vumbi, nadhani watu waliokuwa wakinitazama walishuku iwapo nilikuwa na akili timamu au la. Sikujali. Niliendelea kucheka, peke yangu. Kilikuwa kicheko cha uchungu, ambacho baadaye kiligeuka kuwa kilio. Nilijificha katika uchochoro mmoja na kuruhusu machozi kunitririka.







Muda wa treni kufika ulikaribia. Kila mmoja alikaa tayari kwa vita ya kuwahi kuingia ndani. Lakini pale mmoja wa makarani wa TRC alipouendea ubao wa matangazo na kuandika kitu kwa chaki kila mtu alipigwa na butwaa. Mimi nilichanganyikiwa zaidi, mara baada ya kuusoma ujumbe ule. Yule mwanamke wa kizungu, ambaye bila shaka hakujua Kiswahili vizuri alinisogelea na kuniuliza kwa Kiswahili chake

kibovu, “Hiyo maana yake gani?”

Nikamfahamisha kwa Kiingereza. “Wanasema leo hakuna treni, hadi kesho.”

Yeye pia alipigwa na butwaa. Akanikazia macho ya mshangao kabla hajauliza tena, “Kwa sababu gani?”

“Sijui. Hawakuandika sababu.” “Na hiyo kesho, ni saa ngapi?” “Hilo pia hawakueleza,” nilimjibu.

Mama wa watu alitazama lundo la mizigo aliyokuwa nayo, akatazama kundi la watu waliokuwa pale, ambalo hakuweza kupambanua nani alikuwa msafiri kweli nani kibaka; akazidi kuchanganyikiwa.

Minong’ono mingi ilikua ikiendelea. Habari zilikuwa zimevuja. Treni ya mizigo ilikuwa imeanguka huko Kilosa na kufunga njia. Jitihada za kuinua na kisha kurekebisha uharibifu uliotokea zisingekamilika hadi kesho yake. Hivyo, hakukuwa na namna ya kuondoka hadi jioni ya kesho, kama tutakuwa na bahati.

Nilimfahamisha hayo yule mama wa Kizungu. Kiasi alielewa. Akanishukuru. Nikamwona akihangaika kutafuta namna ya kuondoka na vitu vyake vingi. Masanduku, maboksi na vikorokoro tele ambavyo hata sikuweza kubuni vina nini ndani. Nikajitolea kumsaidia. Tulibeba mizigo hiyo kwa taabu hadi chini ya mnara wa saa ambapo alizungumza na dreva







mmoja wa teksi, wakakubaliana. Tukapakia vitu hivyo katika gari hilo.

“Wewe je? Utalala wapi?” Aliniuliza wakati akijiandaa kuingia ndani ya gari hilo.

“Nitafanya maarifa.” Nilimjibu

Alinitazama kwa muda kabla hajaifungua pochi yake ndogo na kutoa noti ya shilingi elfu kumi ambayo alinikabidhi. Katika hali ya kawaida nisingeweza kupokea fedha hizo, lakini kwa hali niliyokuwa nayo na shida ingekuwa dhambi kubwa kuzikataa. Nilimshukuru mara mbilimbili, kimoyomoyo nikimshukuru mara elfu na mbili. Ilikuwa kama nimepata milioni kumi!

Nikarudi stesheni. “Maarifa” niliyokusudia kufanya yalikuwa ni kuupitisha usiku hapo stesheni, ikiwezekana nilale juu ya viti vyao vya mbao, kuisubiri kesho. Sikuwa na bahati hiyo. Mara tu nilipopata kiti na kujipumzisha alikuja askari mmoja wa shirika hilo na kututangazia kuondoka hapo mara moja, utadhani tulipenda kuwa hapo. Tulipositasita walianza kutuswaga kama mifugo. Hatukuwa na namna zaidi ya kuinuka na kuondoka.

Niende wapi? Nilijiuliza. Wakati huo usiku ulishaingia, yapata saa mbili hivi. Tukio la mchana kule Kariakoo lilikuwa limenitia hofu kubwa ya kuibiwa tena. Kutembea usiku kucha pia kuliniogopesha. Hatari elfu moja na moja zingeweza kunitokea; ningeweza kupigwa na majambazi kwa kufikiriwa kuwa nina pesa; ningeweza kukamatwa na polisi na kurudishwa jela kwa kosa la uzuluraji. Ningeweza hata kuuawa na walinzi wa mabenki na majumba mengine kwa kisingizio cha kujaribu kuiba; na kadhalika na kadhalika.

Wakati nikijiuliza hayo nilikuwa nikirandaranda mitaani kwa hofu ya kukaa mahala pamoja kwa muda mrefu







na kushukiwa. Nilishangazwa na utulivu wa mji, tofauti kabisa na mchana. Watu wengi walijaa katika vituo vya mabasi wakipigania kurudi makwao, pembeni mwa mji. Katikati ya mji watu wengi niliowaona walikuwa Wahindi. Walipita katika magari yao au kuketi katika sehemu zinazotengenezwa vinywaji na kuku choma wakitumia. Nasikia wao, kwa ajili ya rangi zao na imani ya watu wengi kuwa wana fedha nyingi zaidi ni waoga wa kuishi uswahilini. Wako tayari kuishi mtu na mkewe na mama na na baba na watoto sita katika kijumba chenye chumba na sebule badala ya kwenda kando ya mji ambako wangechanganyika na Waswahili.

Niliacha barabara ya uhuru, nikaifuata ya Bibi Titi. Nikaifikia bustani ya Mnazi mmoja. Nikashangaa kuona kundi la watu, wakubwa kwa wadogo wakiwa humo ndani. Baadhi walikuwa wakipika kwa kuni.
 
Nikawasogelea kwa matumaini ya kupata hifadhi ya kupumzika hadi kesho. Haikuwa. Kumbe hawa walikuwa ombaomba, jamii mpya iiliyokuwa imeibuka na kujengeka nchini. Wakati wazazi walikuwa na tatizo moja au jingine, ama katika viungo ama katika mfumo wa kufikiria, watoto walitumiwa zaidi katika kuomba wapita njia, hasa wenye magari. Watoto hawa hawakuwa na mipango wala matumaini ya kwenda shule. Hivyo, walikuwa wakiandaliwa kuwa ombaomba wazoefu au majambazi sugu wenye hasira na maisha. Zaidi ya kuwakamata mara kwa mara na kuwarejesha vijijini, ambako walikaa siku mbili tatu na kurudi zao mijini, hakuna jitihada kubwa ya dhati iliyofanyika kuondoa tatizo hili linalozidi kuchanua.

Jamii hiyo haikuonyesha dalili za kunitaka katika kundi lao. Hata salamu zangu hazikujibiwa. Badala yake walinong’ona wenyewe kwa wenyewe kabla ya kuanza kutafuta silaha zao, fimbo, mawe na hata upanga. Sikusubiri







kufukuzwa. Nikajiondoa harakaharaka na kuendea kituo cha mabasi kilichokuwa na watu tele.

Naweza kupata wapi sehemu ya kulala? Nilimuuliza mtu mmoja aliyekuwa akisubiri basi.

Alinitazama kwa macho ya dharau, bila shaka akinichukulia kama kibaka aliyekuwa akitafuta namna ya kujichanganya ili baadaye apore chochote kinachoporeka.

Mtu wa pili alinijibu kwa kunielekeza kwa mkono. Nikainua uso wangu. Jengo kubwa lililopaa angani kwa takribani gorofa nane lilikuwa likimeremeta mbele yangu kwa nuru ya rangi mbalimbali toka katika vioo. Maandishi yenye maremborembo yalikuwa yakicheza kwa kuwaka na kuzimika, kila herufi kwa wakati wake na kusomeka, Peacock hotel.

Nikamtazama jamaa yule na kumcheka kimoyomoyo, jambo ambalo hakunielewa. “Kama haikufai,” alisema. “Ziko nyingine tele. Zipo za shilingi 500,000 kwa siku. Ziko za 100,000/= na hata zile za 20,000/=. Ni mfuko wako tu. Unaweza kulala Sheraton, unaweza kulAla Kilimanjaro hotel au ukitaka Holiday Inn. Kama unataka hoteli za ufukweni nenda zAko Kipepeo Kigamboni, nenda Kunduchi au Bahari. Ziko tele…”

Nikabaini kuwa nanidhihaki. Nikasogea na kumnong’oneza karibu kabisa na sikio lake, “Natafuta hoteli za chumba cha shlingi elfu moja au mbili, sio zaidi.”

Akacheka. Kisha akasema, “Hizo pia nyingi tu. Utazipata Manzese kwa mfuga mbwa, Buguruni kwa Bibi Tarabushi au hata Mwananyamala kwa Mama Zakaria. Ukiwa na bahati hata Mapipa utapata.”

“Ni wapi huko?” nilimuuliza. “Panda basi, nitakuonyesha.”

Nilimfuata ndani ya basi. Tukaketi kiti kimoja. Alishajua







kuwa nilikuwa mgeni wa mji. Hivyo, alinipa hadithi moja baada ya nyingine juu ya mji na vitongoji vyake.

“Unajua kwa nini panaitwa Mapipa?” alitaja. “Zamani palikuwa na vibanda vilivyojengwa kwa mapande ya mapipa juu na chini. Mapipa hayo ni yale yaliyotupwa wakati wa ujenzi wa barabara ya Morogoro. Yalikuwa na soko kubwa pale Mapipa.

“Lakini wakati ule Magomeni haikuwa kama hii ya leo. Mitaa yote ilikuwa na lami. Umeme uliwaka kila mtaa. Mifereji ya maji machafu ilikuwa imejengwa na inahudumiwa vizuri. Leo hii kila kitu kimekufa. Maji machafu yanamwagika hadi barabarani. Taa zimekufa, lami imekufa. Hata mabomba hayatoi maji.”

“Nini kilitokea?” nilimuuliza. “Sijui,” alijibu

Pamoja na maelezo yake nilikuwa nikishangazwa pia na ukubwa wa mji wa Dar es Salaam. Toka katikati ya mji hadi tunafika Magomeni isipokuwa jangwani ambako wakati wa masika hufurika maji, sikuona pori. Mji ulikuwa umeungana, nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa. Wakazi walikuwa hawalali. Karibu kila mtaa niliona baa mbili au tatu, zikiwa zimechanganyika na makazi ya watu, makelele ya muziki yalishindana kwa sauti.

“Hivi hakuna biashara nyingine Dar es Salaam?” nilimuuliza mwenyeji wangu huyo.

“Kwa nini?”

“Naona baa kila mahala.”

Pombe ndiyo bidhaa inayotoka kuliko nyingine,” alinijibu. “Maduka mengi ya vitabu yamefungwa. Watu hawanunui isipokuwa kile kilicholazimishwa na Wizara ya Elimu. Maduka ya madawa pia yameanza kukosa wateja. Watu hawana uwezo







wa kununua dawa dukani wala hospitalini. Mtu anaweza kufa hata miguuni mwa daktari, kama hana pesa za dawa hakuna matibabu.”

“Kwa nini?” Nilimuuliza kipumbavu. “Sijui,” alinipa jibu lilelile nililostahili.

Karibu kila kituo cha basi tuliwaona wasichana wadogowadogo waliovalia mavazi yao ya kutisha, wenyewe wakiyaita ya kisasa; wakiwa wamesimama. Hawakupanda basi lolote wala kuonyesha kuwa na haraka yoyote, usiku mwingi kama huo. Niliwatazama kwa mshangao.

Mwenyeji wangu aliusoma mshangao wangu, “Changudoa!” akasema.

“Nini?”

“Wale pale! Wanajiuza. Tunawaita Changudoa,” alifafanua.

“Si nasikia kuna maradhi hatari yanayoitwa UKIMWI?” “Naam,” alinijibu. Tena omba kusikia usiombe kuuona

kwa macho. Lakini kwa wale, UKIMWI ni ajali kazini!” Sikuelewa. Nikanyamaza.

Tulifika Manzese. Tukashuka kituo cha karibu na daraja pekee la angani, lililoikata barabara ya Morogoro toka kulia hadi kushoto kupunguza ajali za barabarani ambazo niliambiwa ziliua waenda kwa miguu kwa wingi kuliko UKIMWI au malaria.

Nilielekezwa kuelekea kushoto. Kona moja, uchochoro; kona ya pili; uchochoro. Mara tukamezwa na kiza kizito. Bila msaada wa nuru hafifu toka katika vyumba vya wakazi wa eneo hilo nadhani hata mwenyeji wangu angeweza kupotea. Nilimfuata katika vichochoro hivyo, vilivyobana na kugubikwa na uchafu mwingi. Mara kwa mara tulikanyaga dimbwi la tope.







Mara mbili tatu tulikurupusha wanyama wadogowadogo ambao mimi nilidhani ni paka lakini mwenyeji wangu akaniambia, panya!

“Mbona wanene vile?” nikauliza.

Wanakula na kushiba. Manzese hii mjomba,” alijibu. Tulizidi kuingia ndani. Mwenyeji wangu alitembea haraka akipenya hapa na kutokea pale. Nilianza kuogopa. Kwanza, nilihisi kuwa hajui tunakokwenda. Pili, nilianza kumshuku kuwa huenda alikusudia
 
SEHEMU YA 140


kunitendea ubaya. Nikatamani kugeuka nirudi nilikotoka. Hata hivyo, hofu ya kupotea na kupatwa na mabaya zaidi ilinizuia. Badala yake nikamuuliza taratibu, “Mbona hatufiki?”

Aligeuka na kunitazama. Aliisoma hofu katika macho yangu. Akacheka. “Hofu ya nini?” aliuliza baadaye. “Hapo ulipo hata laki huna, achilia mbali milioni. Nataka kukusaidia upate mahala pa kulala, kwani unaonekana kuwa unahitaji msaada. Nikikuacha utapigwa na vibaka na kuvuliwa hata nguo ulizovaa.”

Nikamwamini.

Hatimaye tukaifikia nyumba ya wageni aliyoikusudia. Nje ya nyumba hiyo kwenye uchochoro mmoja kulikuwa na watu wanaokunywa pombe, wake kwa waume. Mwenyeji wangu alionekana mwenyeji hapa. Alimwita mmoja wa watumishi wa nyumba hiyo kwa jina, “Rehema! Mpe chumba mjomba wangu. Mchagulie chumba safi. Sawa?”

Rehema, msichana mkubwa mnene, aliyeonekana kalewa aliniashiria kumfuata. Nyumba haikuwa na umeme. Mishumaa miwili, mmoja uliowekwa mlango wa mbele na mwingine mlango wa nyuma ndiyo iliyotuongoza. Niligeuka







ili kumshukuru mwenyeji wangu. Hakuwepo. Alikwishapenya uchochoro mwingine na kuondoka zake. Nikamfuata Rehema. “Unataka chumba che bei gani?” Aliniuliza. “Vipo vya

elfu mbili na elfu na mia tano.” “Nipe cha elfu na mia tano.”

Kilikuwa chumba cha uwani, kidogo sana. Dirisha lilikuwa moja, dogo vilevile. Kitanda chao kilitosha mtu mmoja tu, si zaidi.

“Kinakufaa?”

“Kinafaa sana.” Nilimjibu.

“Ngoja nilete mshumaa. Umeme umekatwa huu mwezi wa tatu. Na kishoka leo kachelewa kuja.”

“Kishoka ndiyo nani?” nikaomba kuelewa.

“Jamaa yetu ambaye huja usiku kuturudishia umeme. Asubuhi sana huja tena kuukata kabla TANESCO hawajapita mitaa hii,” alifafanua.

“Kwani mnadaiwa pesa nyingi?” nilihoji.

“Nyingi sana. Kama milioni tatu na laki sita hivi. Maji yenyewe mwaka wa nne hayajatoka. Lakini bili yao imefika laki tisa na nusu.”

Nikashangaa. Kwa hesabu za haraka haraka nyumba hiyo, yenye vyumba sita pekee na baa ya uchochoroni haikuwa na uwezekano wa kupata walao laki mbili kwa mwezi. Gharama hiyo ya umeme na maji ilitokea wapi? “Mtalipa?” nilimuuliza.

“Nani alipe? Unalipa deni linalolipika. Lisilolipika unaachana nalo,” alinisomesha.

Rehema alipoondoka nilipanda kitandani kwangu kulala. Ndio kwanza nikabaini kuwa godoro lilikuwa kuukuu, pengine halikupata kubadilishwa toka nyumba hiyo ilipojengwa. Mbavu zangu zilikwenda moja kwa moja kukutana na chaga







za mbao. Si hilo tu, dakika mbili tu za kupumzika juu ya kitanda hicho, nilikaribishwa na mbu na kunguni. Wakati mbu wakiuma baada ya kelele zao za vitisho masikioni, kunguni wao walinitesa kwa kufyonza damu yangu kimyakimya na kunisababishia maumivu mengine. Nilifanikiwa kuwaua kunguni wawili watatu. Lakini harufu yao kali na damu nyingi toka kwa wateja wao ilinitia kichefuchefu

Adha ya tatu ilikua ikinisubiri. Joto. Chumba kilichemka kwa joto kama tanuru. Nikainuka na kufungua lile dirisha pekee. Tendo hilo lilileta karaha badala ya faraja. Harufu nzito, ya kutisha iliyoingia chumbani humo toka dirishani ilinifanya niamke na kumwita Rehema. “Harufu hii ya nini?” nilimuuliza. “Hilo dirisha huwa alifunguliwi!” alinionya akilifunga

mara moja. “Kuna mfereji wa maji machafu hapo. Haujazibuliwa leo mwaka wa sita. Kwa hiyo, maji yametuwama uchafu umeoza na kufanya harufu ya kutisha.”

“Kwa nini hauzibuliwi?” “Sijui”

Nikazidi kushangaa. Mambo gani haya ninayoyashuhudia, siku moja tu baada ya kutoka jela. Kama maisha ya uraiani ndiyo haya, malazi ndiyo haya, iko wapi tofauti ya kuishi uraiani na gerezani?

Tofauti kati ya maeneo ya Manzese na katika ya mji pia ilinishangaza sana. Wakati kule kulionekana kama Peponi huku hakukutofautiana sana na Jehanamu. Kama ungetokea moto, uteketeze nyumba moja ni dhahiri kuwa mamia ya nyumba yangeungua na maelfu ya watu kupoteza maisha. Nikaelewa kwa nini yanapozuka maradhi kama kipindupindu na hata UKIMWI hayaondoki kabla ya kuteketeza mamia ya watu katika maeneo kama haya. Huu ndio uhuru tulioupigania na kuupata? Nilijiuliza. Huu ndio Ujamaa niliousikia mara







kwa mara toka gerezani? Au ndio Azimio la Arusha lililopigiwa sana kelele?

Wakati nikiwaza hayo jambo la ajabu likatokea. Umeme uliwaka. Kishoka alikuwa amefika nadhani. Feni chafu lililokuwa darini likapata uhai. Ama liliwafukuza mbu ama waliogopa kelele zake, kwani niliona mbu wakipungua ghafla. Kunguni nao walijificha. Nikapanda kitandani na kujilaza. Usingizi ukanichukua.

Niliamka kesho yake saa tatu. Nilikuwa mgeni peke yangu katika nyumba hiyo. Rehema alikuwa akipita chumba hadi chumba kukusanya shuka kwa ajili ya kuzifua. Alinionyesha bafu ambalo lilikuwa na maji ya ndoo, kipande cha sabuni ya mchi kikiwa pembeni. Nilioga na kujisikia nikiburudika kidogo, hali ambayo ilinifanya nisikie njaa ikianza kulitekenya tena tumbo langu. Niliishtakia kwa Rehema ambaye alinielekeza uchochoro wenye ‘mama ntilie’ pekee eneo hilo. Nilimpata. Nikanywa chai ya shilingi hamsini, chapati mbili za mia na maharage ya mia. Chakula na bei vilinifuraisha sana.

Nikaanza kazi ya kutafuta njia ya kurudi barabarani. Nilielekezwa mara nne na kupotea mara mbili kabla ya kumwuliza bwana mmoja mtanashati ambaye aliniambia nimfuate.

“Ni afadhali kupotea New York, kuliko katika vichochoro vya Manzese. Humu unahitaji akili za ziada kujua njia ya kwenda na kutoka kwako,” alisema kiongozi wangu huyo mpya wa msafara.

“Kwa nini inakuwa hivi?” Nilimuuliza. “Umeshafika mwanza?” Alinijibu kwa swali jingine. “Zamani sana.”

“Fika sasa hivi uone,” alisema “Kule watu wanajenga hata juu ya mawe. Ile mandhari nzuri ya asili imepotea kabisa







kwa ajili ya watu kutafuta makazi ya kuishi. Tatizo unaloliona hapa
 
Back
Top Bottom