SEHEMU YA 57
Joram aliyakazia macho mabadiliko yote hayo katika uso wa Adela. Kisha akamwona Adela akitabasamu kwa namna ya uchungu mkubwa na kusema, “Mpendwa Joram naomba radhi sana kwa hali iliyonikumba. Kwa kweli, umenirejesha katika milki ya hofu na huzuni kwa kule kunikumbusha mkasa ulioko mbele yangu, mkasa wa Nunda. Kwa kweli, nilikuwa nimeanza kusahau yote tangu nilipohisi kukupenda. Niambie tafadhali. Niambie wapi umefikia katika kumjua Nunda. Ni nani?”
Joram alimwendea na kuutua mkono wake juu ya bega lake. Kwa sauti yenye tabasamu akamwambia, “Usijali mpenzi, nitalitimiza jukumu ulilonipa hivi karibuni. Ninachohitaji ni msaada wako tu, kwa jambo dogo. Nataka leo tutoke wote twende zetu pale West Bar, Buguruni, ili nikamilishe uchunguzi wangu.”
“La, siendi huko. Kwa nini niende?” Adela alikana mara moja. Sauti yake haikuwa na mzaha.
Tabasamu la Joram liligeuka kicheko aliposikia jibu hilo. “Tulitazame swali lako hilohilo kwa upande mwingine. Kwa nini usiende?” alimwuliza.
Adela aliduwaa akiwa hana jibu lolote. Badala yake aliyakaza macho yake kumtazama Joram usoni.
“Sijui kwa nini hutaki kwenda hapo. Ungekuwa umetoa mchango wako katika kumtia Nunda mbaroni,” Joram alisema akiutia mkono wake mfukoni na kutoa kitu. “Hata hivyo, bado kuna jambo jingine ambalo unaweza kunisaidia. Hiyo ni picha,” alimpa kitu hicho alichokitoa mfukoni. “Itazame uniambie kama unamfahamu mtu huyo.”
Ilikuwa picha ya marehemu Ukeke Maulana, ilionyesha kikamilifu sura yake. Joram aliiazima toka nyumbani kwake ili aitumie katika shughuli zake.
Adela aliitazama mara moja tu na kisha kumrudishia Joram huku akikunja uso ghafla. “Simjui mtu huyu. Sijapata kumwona tangu nilipozaliwa,” alisema.
“Alaa!” alinong’ona. “Basi umenisaidia sana mpenzi.”
Kikafuata kimya kifupi. Adela akiwa ameduwaa hali Joram akipambana na tabasamu lililohitaji kuumeza uso wake, pambano ambalo liliifanya midomo yake iwe ikichezacheza. Adela alikitibua kimya hicho kwa kuuliza swali lililomshtua Joram, “Unaupenda uzuri Joram?”
“Ndiyo, wa kila kitu, hasa wa mwanamke ambaye kila jicho humtamani.”
“Joram, unaupenda utajiri?”