HADITHI: NAFSI ZILIZO TELEKEZWA
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+
UKURASA WA 96
NYUMBANI KWA EDISON
Edison bado alikuwa anaishi paipokuwa nyumbani kwa JACK THE LAWYER, alijua sehemu hiyo ilikuwa salama kwa sababu mhusika alikuwa amekufa hivyo kwake ikawa salama zaidi kuigeuza sehemu hiyo kuwa makazi yake rasmi. Usiku huo ambao aliondoka kwa ajili ya kwenda kuonana na CDF alimuacha Nicola pekeyake, kuna namna alikuwa anamjali binti huyo kiasi kwamba hakupenda kutembea naye kwenye maeneo ya hatari ukizingatia Jack alimwelekeza mapema kwamba alitakiwa kumlinda kwa namna na gharama yoyote ambayo ingekuja mbele yake hivyo alihakikisha analitimiza hilo.
Lakini ni usiku huo huo ambao aliamini kwamba Nicola alikuwa kwenye hatari kubwa kitu ambacho kilikuwa cha kweli kabisa. Damasi akiwa kwenye hali mbaya ya maumivu makali akiendelea kuvuja damu, alimleta Yohani mpaka kwenye eneo hilo ambapo alipaki gari yake nje ya hilo jengo. Aliangalia kila kona kama kulikuwa na mtu wa karibu, muda ulikuwa umekwenda hivyo aliihisi amani mbele yake, alirudi nyuma kidogo akadunda kwenye tairi ya gari akafanikiwa kuudaka ukuta wa juu kabisa. Alijivuta kwa nguvu na kusimama hao juu akiwa amepishana kidogo na nyanya za umeme ambazo zilipitishwa juu ya hilo geti.
Alihesabu mara mbili akanirusha kwa sarakasi mpaka ndani ambapo alitua kama paka bila kutoa kishindo. Alitazama buti lake, liliungua sehemu ndogo ambayo iligusa kwenye zile nyaya hivyo hata yeye angefanya ujinga basi angepata athari ya kukutana na adha ya umeme. Ndani kulikuwa kumetulia, mazingira yake yalikuwa safi ishara ya kwamba mtu ambaye alikuwa anaishi ndani ya eneo hilo alikuwa ana uhakika wa kula vizuri, maisha ya mawazo ya pesa hayakuwa sehemu yake.
Ndani ya sehemu ambayo alijiridhisha kwamba ilikuwa ni sebule aliona kuna mwanga, maana yake mwenyeji wake lazima alikuwa hapo sebuleni, alitabasamu kwa hasira akiwa anasogelea ule mlango ambao ulikuwa mbele yake. Bila kupoteza muda aliukita ule mlango na buti zito akaingia nao ndani, mwenyeji ni kama hakutarajia kuweza kukutana na hali kama hiyo hata hivyo hakuwa mzembe, alikirusha kisu ambacho kilikuwa kwenye mkono wake, Yohani alikikwepa kwa kuinamia pembeni kikaenda kukita kwenye ukuta na kudondoka chini.
Mbele yake alikuwa amesimama Nicola akiwa kwenye kipensi kifupi na kicloptop kilicho mchora vyema umbo lake. Mezani kulikuwa na matunda hivyo bila shaka ilikuwa ni ishara kwamba alikuwa akikitumia kile kisu chake kuweza kukatia yale matunda ambayo alikuwa akiyashughulikia pale mezani.
“Sikutegemea kukutana na wewe mazingira kama haya tena ukiwa umestarehe namna hii ukisubiri kuliwa baada ya kutufanyia usaliti. Binti ni mpuuzi wewe”
“Damasi kakuleta hapa sio?”
“Hakuwa na chaguo lingine nadhani hata wewe umewahi kusikia simulizi zangu kadhaa na ndicho ambacho kitakukuta hata wewe. Tufupishe maelezo bwana ako yuko wapi?”
“Ningekuwa mimi ndo wewe ningeondoka asije akanipata sehemu yoyote ile hapa duniani kuendelea kukaa kwako na kujileta hili eneo unajipunguzia nafasi ya kuendelea kuwa hai”
“Kwa maneno hayo ina maana hayupo. Kwahiyo nitapata vitu viwili kutoka kwako, mzigo wetu lakini pia huyo bwana ako najua atakutafuta tu kwa namna yoyote ile hivyo atalazimika kuja ninapo hitaji mimi ukiwa mkononi mwangu, zoezi langu linaenda kuwa rahisi kwa kuua ndege wawili kwa wakati mmoja” Yohani hakuwa mtu wa utani, maneno aliyo yaongea alikuwa anamaanisha mno, hawakuwa mbali kwa walipokuwa wamesimama. Kujiachia kwake Nicola kulimfanya asiwe na silaha yoyote ya maana ukiacha hicho kisu ambacho kiliishia kukita ukutani, maana yake alitakiwa kuyatetea maisha yake kwa mikono yake miwili.
Aliisukuma meza ambayo ilikuwa mbele yake kuelekea kwa YohanI, meza hiyo ilizunguka kwa kuviringika kwani ilisukumwa kwa nguvu. Nicola alikuwa anakuja tena akiwa peku mguuni kwake, meza hiyo ilipasuliwa kwa mguu Nicola akawa amefika, alirusha mguu wake ukakita kwenye shingo ya Yohani ambaye aliyumba mpaka ukutani ambapo aliutumia mguu wake kumpa balansi. Nicola alizunguka kwa mahesabu yaliyo enda sawa, mguu wake ukakita kwenye uso wa Yohani kwa mara nyingine, aliishia kuyumbisha uso wake na kurudi kusimama kama mwanzo.
Ngumi ambayo ilikuwa inakuja aliiona, alibonyea kwa nyuma kidogo ikaishia kumpapasa kwenye nguvu yake, alijivuta kusogea mbele kwa nguvu ambapo alimkita Nocola na kiganja cha shingo, alipata maumivu makali kwa kuyumba yumba kurudi nyuma, jitu hilo halikuwa na huruma kabisa. Yohani alikanyaga kwenye sofa lililo msaidia kudunda, alitua kwenye bega la Nocola ambaye alifanikiwa kuudaka mguu mmoja mwingine ulimkita kwenye kifua akadondokea kwenye kabati ambalo alilipasua.
Alisimama ghafla akiwa anarusha moja ya kioo ambacho kilipasuka, kioo kile kilikuja kwa spidi Yohani akapishana nacho baada ya kufanikiwa kukikwepa, alikidaka kwa mkono wake, kilimchana ila hakujali wakati huo alikuwa amesha anza kujongea kuelekea alipokuwepo Nicola. Nicola alikuwa anafanya kazi ya kukwepa tu kwa sababu alianza kuzidiwa nguvu na Yohani, alikutana na kiwiko cha mkono wa kulia aliyumbia kushoto ambako Yohani alitumia nafasi hiyo kile kioo kukizungushia nyuma akakidaka na mkono wake wa kushoto kisha akakizamisha kwenye mbavu ya mwanamke huyo.
Maumivu aliyasikilizia vizuri, alipiga kelele za maumivu, Aliongezwa ngumi yenye kilo kadhaa hilo eneo akadondokea ukutani. Mwanaume huyo hakuwa na roho ya kibinadamu kabisa, licha ya Nicola kuwa hai pale chini bado alimfuta na kumuongeza buti la uso lililo mzoa mpaka ukutani ambako alijibamiza vibaya mpaka akapoteza fahamu. Yohani aliangalia kwa umakini sebule hiyo, akawa anazitupa taratibu hatua zake kuelekea zilipo ngazi za kuelekea juu ila alisita baada ya kusikia kelele za kishindo nje. Alimbeba Nicola na kutoka naye nje ambapo mara hii alifungua geti na kutoka nje ambako alimkuta Damasi akipambana kuweza kutoka ndani ya gari ile ili aweze kulikimbia dubwana hilo.
Harakati zake zilimsaidia kufanikiwa kutua chini ya gari ila hakuwa na uwezo wa kwenda popote kwa sababu miguu haikuwa ikifanya kazi kabisa, mguu mmoja ulikuwa umevunjwa na mwingine ulikuwa umepigwa risasi za kutosha. Alimrushia Nicola kwenye buti kisha akamrejea Damasi ambaye hali yake ilikuwa mbaya kiasi kwamba hata kujivuta alikuwa anashindwa, alimbeba mwanaume yule mgongoni akaangalia kila sehemu ndupo aligundua kwamba juu ya geti kulikuwa na vyumba vikali ambavyo vilitokezea. Alisogea akamrushia Damasi kwa juu sana kicha akalishikilia lile geti kuelekea ule uelekeo ambao alimrushia Damasi, alifikia kwenye hivyo vyuma ambavyo vilimtoboa toboa mgongo wake, alimuacha akiwa anahangaika hapo akawasha gari akatoweka Joel John waweza kumuita Joh au Yohani Mawenge.
Dakika kumi baadae ndio muda ambao Edison alikuwa anaingia ndani ya hilo eneo, gari yake ilikuwa kwenye mwendokasi lakini hakujali, alishika breki ghafla hata kabla ya gari kusimama vizuri aliruka kukimbilia ndani. Alisita baada ya kulikaribia geti kubwa ambalo lilikuwa mbele yake, kwa sababu chini palitapakaa damu, mwili wake ulimsisimka huku akizidisha hofu ndani ya moyo wake ndipo akaamua kuyainua macho yake juu.
Alikuwa anaomba isije kuwa ni Nicola ndiye alifanyiwa vile, aliona mtu ametundikwa mithili ya mtu ambaye alikuwa amebanikwa akisubiri moto ukolee. Alikuwa ni Damasi ndiye ambaye aliuawa kikatili juu ya geti hilo. Alihema kwa nguvu na kukimbilia ndani, hakukuwa na dalili za uwepo wa mtu zaidi ya mlango kuvunjika lakini pia vitu kuvurugwa ndani, alijua kabisa Nicola alikuwa ametekwa tayari. Alisogea kwenye chumba cha kuongozea kamera kuona matukio ambayo yalitokea hapo, aliangalia kwa umakini akaishia kusikitika tu kwa sababu jambo hilo ulikuwa ni uzembe wake kumruhusu Damasi kuondoka kirahisi hapo, mara mia angemtoa akiwa amemfumba macho ili asione kwamba alikuwa wapi.
Aliitoa ile maiti kwa sababu watu wangeiona ingekuwa kesi nyingine hiyo kwa mapolisi, alisafisha kila kitu na kuangalia saa yake ya mkononi, ilikuwa inasoma saa nane. Aliitoa ile simu ambayo aliichukua kwa Aaliyah, alipiga ile namba ambayo ilidaiwa kuwa ya raisi, iliita mara moja tu na kupokelewa.
“Tukutane kituo cha mwendokasi gerezani saa kumi kasoro, sitaki kumkuta mlinzi yeyote pale nadhani patafaa kwa ajili ya mazungumzo ya mimi na wewe” hakusubiri jibu upande wa pili aliikata hiyo simu na kuipasua chini. Alitoka akalifunga geti kisha akaingia kwenye gari yake na kutoka hapo kwa kasi kama kuna ugomvi ambao aliuingia na watu kadhaa na alihitaji kuwawahi.
UKURASA WA 96 unafika mwisho.