HADITHI: NAFSI ZILIZO TELEKEZWA
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+
UKURASA WA 87
“Unahisi kwamba makamu wa raisi aliwahi kumfanyia jambo lolote lile?”
“Huyu ni mkubwa mwenzako, mimi ndiye natakiwa kukuuliza swali hili wewe na sio wewe kuniuliza mimi hapa” Aaliyah alikuwa anamgusa kwenye mshono ndipo wakakumbuka kuhusu familia.
“Kama angewaua lazima tungeikuta miili yao hapa”
“Hawezi kuua familia ambayo haihusiki hivyo lazima kuna mahali amewafungia ndani ya nyumba humu humu” Aaliya alitoa maoni yake kwa uzoefu wake kwenye hizo kazi.
“Wewe nenda, kachukue ule ushahidi wa video za marejeo uondoke nazo mimi nawasiliana na raisi kumpa taarifa nitawaambia video hizo mhusika ameondoka nazo hivyo hatujazipata ila hakikisha nakutana na huyo bwana mdogo kwa gharama yoyote ile nina mazungumzo naye ya mhimu na maswali mengi kwake. Afanye hivyo kabla mambo hayajawa mabaya zaidi kwani kumuua kiongozi mkubwa kama huyu inaenda kuwa tatizo kubwa huko mbeleni na wanajeshi watasambazwa kila kona pamoja na polisi kumsaka” Aaliyah aliitikia kwa kichwa wakati ambao CDF aliutumia kumpa taarifa raisi ambayo baada ya kupokea taarifa hiyo alichanganyikiwa ndipo akaamua kwenda kwenye bwawa la kuogelea kutuliza akili yake kabla ya kuja kuitwa ili akakutane na Christopher Nyemo.
Aaliyah aliingia kwenye gari ya CDF ambayo ndiyo alitakiwa kuondoka nayo kwa sababu hakutakiwa kukutwa hilo eneo, alikuwa anahema kwa kasi ambayo ilikuwa ni ishara ya wasiwasi. Hakuamini kama mwanaume yule alikuwa mkatili kiasi kile huenda ni kwa sababu hakuwahi kubahatika kumshuhudia akiwa anafanya mauaji kama ambayo aliyafanya hapo, mwili wake ulikuwa ukisisimka vibaya kila alipokuwa anakumbuka kila mwili ambao aliuona. Aliitoa simu yake na kumtafuta mwanaume huyo ambaye aliahidi kumtafuta lakini hakuwa amemtafuta mpaka wakati huo ili na bahati tu alimpatia namba yake binafsi.
Simu iliendelea kuita yeye akiwa anaitoa gari kwa kasi kuelekea njia ya Masaki ambapo alikunja kushoto kwake baada ya hatua kadhaa kuitafuta njia ya Macho Msasani ili aje kutokezea Namanga kisha aingie Moroko aishie alikokuwa anaelekea. Simu iliita mara ya kwanza mpaka ikakata, ikaita mara ya pili ikakata, mara ya tatu ndipo ilipokelewa. Nyuma yake ilisikika sauti nzito ya kiume, alikuwa na uhakika kwamba alikuwa ni Edison.
“Nakusikiliza”
“Kwanini umefanya haya?”
“Mhhhhh nadhani sio biashara yako kujua natakiwa kufanya nini na nini sitakiwi kufanya”
“Jambo ambalo umelifanya ni hatari mno kulivyo unavyo fikiria wewe na hapa kama sio CDF lazima wangeipata sura yako yule ndiye mtu peke ambaye amekubali kufanya kazi na sisi”
“Sisi?”
‘Mimi na wewe kwa sasa tunafanya kazi moja, CDF nimeongea naye, alikuwa mmoja wao lakini amechoka anahitaji kulitumikia taifa lake hivyo amekubali kuwa upande wetu na anahitaji sana kuonana na wewe kwa sababu ana mazungumzo binafsi ya kuongea na wewe”
“Naona umeanza kujichukulia maamuzi yako bibie, nani alikwambia namhitaji mkuu wa majeshi?”
“Edison nisikilize kwa umakini sura yako imeonekana huoni kama ni jambo ambalo litahatarisha maisha yako?”
“Sura imeonekana kwa sababu nilitaka ajue kwamba ni mimi ndiye nimefanya mauaji yale kumuua yule mpuuzi, kwahiyo wewe kuiharibu umeua mipango yangu unatakiwa kuijua mipaka yako sio kuanza kuingilia majukumu ambayo hayakuhusu ukihisi unanifanyia hisani” Aaliyah alibaki anashangaa asiamini kile ambacho alikuwa anakisikia kwenye masikio yake.
“Ulitaka sura yako ionekane? Why?”
“Nataka wajue nini maana ya hofu, nahitaji wajue kwamba ninakuja kwa sababu sina haja ya kujificha tena, wanajua kama aliyekufa sio mimi. Hofu itawafanya watambue walicho kifanya na kuanza kufanya mambo kwa mihemko na wakati wanakuja kukumbuka kutumia akili muda wao utakuwa umeisha”
“Kwanini umemuua makamu wa raisi tena kwa ukatili namna ile mpaka ukaukata ulimi wake?”
“Kwa sababu ule ulimi ndio mara ya mwisho ulitoa kauli ya mke wangu na mwanangu kuuawa. Ni binadamu ambaye sikuwa najua kwamba anahusika na hili mpaka siku ya jana ambapo nilibahika kukutana na mwanaume mmoja ambaye alinipa ukweli niliokuwa naukosa hivyo yule mpuuzi alistahili hili kwa kuhusika na mauaji ya mke wangu na mwanangu ambaye hakuwa amezaliwa bado. Nitakutumia muda na mahali wa kukutana na huyo CDF tena umlete wewe hilo eneo nitakuwa na dakika tano tu za kumsikiliza” simu ilikatwa.
Simu hiyo ilimkutia Edison akiwa ndani ya chumba pekeyake, chumba ambacho kilijaa picha za watu wake wa mhimu kuanzia baba yake mzazi, wale makomando wenzake tisa, Edward Pande mwanaume ambaye alikatisha ndoto zake zote ili kumlea yeye na kumlinda. Pembezoni pia kulikuw a na picha kubwa ya JACK THE LAWYER akiwa ndani ya mahamaka kwenye tabasamu la kusisimua lakini pia picha kubwa zaidi ya zote ilikuwa ni picha ya mkewe Patricia Leonard aliye uawa akiwa na mimba tumboni mwake.
Chini kabisa ya ukuta kulikuwa na picha ya Zulpha Mazipa, mtaani walimjua kama Cersie Mhina lakini ndani ya biashara haramu alifahamika kama Madam Kate. Kwenye picha hiyo alikuwa ameweka alama kubwa ya X kwa rangi nyekundu ikiwa na maana ya kuhesabia kama mwanamke huyo alikuwa ni mfu kwenye maisha yake ila alikuwa anahitaji kukutana naye. Jana yake alifanikiwa kwenda ndani ya karakana ya utengenezaji wa treni maeneo ya Tazara majira ya usiku. Alikutana na Kanaan yule mwanaume ambaye alielekezwa kwamba kama kutakuwa na maelezo ya ziada yalikuwa yanahitajika basi alitakiwa kumtafuta mwanaume huyo ambaye ndiye alimfunulia ukweli wa makamu huyo wa raisi aliyekuwa mwema machoni pa watu kiasi kwamba hata kwenye zile listi za watu wabaya hakuwepo.
Makamu wa raisi alikuwa moja kati ya sehemu mhimu kabisa ya jamii ya LUNATIC SOCIETY na ndiye ambaye alisimamia zoezi zima la kuuawa kwa mkewe. Kanaan alimwelezea kwa undani kuhusu mtu huyo na baadhi ya taarifa ambazo hakuwa nazo Edison kwa sababu kijana huyo aliwahi kufanya kazi kwa ukaribu na Edward Pande ndiyo maana alihakikisha anampatia taarifa hizo nyeti ambazo hakuzilazia damu, haraka alizifanyia maamuzi na kwenda kumuua kiongozi huyo mkubwa wa serikali.
Juu ya meza ndogo ambayo ilikuwa ndani ya chumba hicho uliwekwa upanga ambao bado ulikuwa unavuja damu kwa mbali, ndio ambao aliutumia kwenye ile nyumba akiwa ameupata kutoka kwa Saimon wakati wamemvamia kwenye parking kule na aliipenda mno silaha hiyo kwa sababu ilimfanya kumpitia mtu mara moja tu anamaliza biashara.
“Ni muda wa kukutana na wewe mama” aliongea kwa sauti kali akiuchukua upanga na kuukita kwenye kichwa cha mama yake kwenye ile picha. Zulpha Mazipa alitakiwa kufa kwa namna yoyote ile hata kama alimzaa na kumnyonyesha, uwepo wake duniani ulikuwa na hasara kubwa kwa watu wengi kuliko faida zake.
Alishtuka na kukuta akiwa amefungwa kwenye kiti kwa kutumia nyanya ngumu za umeme. Alijitikisa kwa jazba lakini hakufanikiwa kuchomoka, akaishia kusonya, Ndani kulikuwa na kiza kikali kiasi kwamba hakuwa anaona kile ambacho kilikuwa kinaendelea hapo alipokuwepo. Alijaribu bahati yake kwa mara nyingine kuweza kutunisha misuli yake ili aweze kujitoa hapo ila mwili wake uliishia kwa maumivu makali akaamua kuwa mpole.
Alihisi kuna hatua za watu wawili zikiwa zinakuja upande wa chumba hicho, alikuwa makini kutaka kujua kwamba hatua hizo zilikuwa zinatokea wapi kuelekea hapo alipokuwepo. Taa zenye mwanga mkali ziliwaka ghafla na kumuumiza macho yake ambayo aliyafumba ghafla, baada ya dakika kama mbili aliyafumbua tena ndipo alifanikiwa kuwaona watu hao mbele yake. Edison na Nicola walikuwa wamependezana mno kuwa karibu, aliwakumbuka vyema hao ndio ambao walikuwa wamemteka na mara ya mwisho alizimia bila kuelewa kile ambacho kilikuwa kimeendelea.
UKURASA WA 87 unafika mwisho.