SEHEMU YA 521.
Kila mmoja aliona maneno ya Gong Gyechung yanaleta maana , isingewezekana mgonjwa kuweza kuhimili upasuaji wa moyo na baada ya hapo akafanyiwa tena upasuaji wa kubadilishiwa ini.
“Lakini sijasema kwamba tunakwenda kumfanyia upasuaji wa moyo baada ya upasuuaji wa ini”Aliongea Clark
“Lakini haina utofauti pia na haitatui shida yake”Aliongea Dokta Lee.
“Njia pekee ya kufanikisha hili ni kufanya upasuaji wote kwa pamoja”Aliongea akimaanisha kwamba upasuaji wa kubadilisha moyo na wa kubadilisha ini ufanyike kwa wakati mmoja.
“Unasemaje?”
“Una kichaa?’
“Ni daktari kweli huyu?”
Madaktari kutoka timu ya Lee walionyesha kabisa kutoridhshwa na maamuzi ya dokta Clark.
“Dokta Clark naweza kusema unavuka mipaka yako kama daktari , wewe hujui kwamba kufanyiwa upasuaji wa kubadilishiwa moyo na ini kwa wakati mmoja ni kinyume cha sheria na leseni zetu zinaweza kufungiwa”Aliongea Dokta Lee kwa wasiwasi mkubwa.
“Nisingeongea hivyo kama mngeonyesha mna mpango mwingine wa kumsaidia mgonjwa , nitaendelea na msimamo wangu huo kwani ndio njia pekee ya kumuokoa mgonjwa”
‘Hatuwezi kufanya upasuaji mkubwa wa aina mbili kwa wakati mmoja , hakuna mtu ambaye ashawahi kujaribu kufanya hivyo , ni kama unamuua mgonjwa”
“Kwahio kama hakuna mtu ambaye ashawahi kufanya ndio tuseme kwamba haiwezekani?”
“kwahio unasema unkwenda kufanya huo upasuaji?”aliuliza Dokta Lee
“Dokta Vincent anaweza kufanya upasuaji wa kubadilisha ini wakati huo mimi nikifanya upasuaji wa kubadilisha moyo , Wallen yeye atahusika na ganzi , hauwezi kuwa upasuaji mgumu kama tu kila mmoja atatoa ushirikiano”
Vincent na Wallen licha ya kwamba walikuwa wakimkubali Dokta Clark lakini kwa upasuaji wa aina hio waliona ni jambo ambalo haliwezekani.
“Ujinga, huu ni ujinga”Aliongea Dokta Lee kwa hasira huku akisimama na kisha akawageukia familia ya Park.
“Jamani msimuamini na maneno yake , hakuna daktari yoyote duniani ambaye anaweza kuamini jambo hili kuwezekana”
“Kwanini wewe ndio unaonekana kuwa na wasiwasi , ni jukumu la mgonjwa yeye mwenyewe kufanya maamuzi , unaweza kutoa maoni yako kama una njia mbadala ya kumuokoa mgonjwa , lakini kama huna kaa kimya”Aliongea Clark na kumfanya Dokta Lee kushindwa kuongea neno lingine.
Ni kweli kabisa hakuwa na matibabu mbadala ambayo yangeweza kumuokoa Babu yake Yezi.
“Jamani kwasababu Dokta Clark yeye kashatoa wazo la matibabu ya mgonjwa nafikiri ni vyema kama tutamshirikisha mgonjwa mwenyewe kufanya maamuzi , hata kama upasuaji huu unaenda kinyume na sheria lakini kama mgonjwa atakubali basi hakuna tatizo”Aliongea Gong Gyechung na kufanya familia nzima imwangalie , mpaka hapo ni kama alikuwa akijitoa kwenye kusimamia matibabu ya Babu yake Yezi kutokana na kwamba Dokta Lee mwenyewe ashaonyesha kukaa tamaa , hivyo njia pekee ni kumpasia jukumu Dokta Clark.
“Mkurugezi Gong ni…”
“Dokta Lee najua wasiwasi wako , lakini hata mimi nimeona kwamba umejitahidi kadri ya uwezo wako lakini kama Dokta Clark ana njia nzuri ya kumuokoa mgonjwa basi sina budi kumpa nafasi”Aliongea Gong na kumfanya dokta Lee kumeza mate mengi , huku akionyesha kutoridhishiwa na maamuzi ambayo yamefanyika.
Edna walikuwa ni moja wapo ya watu ambao walikuwa na wasiwasi na aliona matumaini ya kupona kwa babu yake Yezi ni madogo.
“Hubby unafikiri anaweza kupona?”Edna alimuuliza Roma.
“Kwa hali aliokuwa anayo ni ngumu , lakini Clark ameonekana kujiamini sana hivyo siwezi kutabiri nini kinakwenda kutokea baada ya upasuaji”
Baada ya kuhitimisha majadiliano wote walitaka kusikia maamuzi ya mgonjwa mwenyewe kama angekubali kufanyiwa upasuaji wa aina mbili kwa wakati mmoja kama Clark alivyopendekeza.
Kwasababu muda ulikuwa umeenda jambo hilo lilighairishwa mpaka siku inayofata na Yezi alishauriwa kurudi nyumbani licha ya kwamba alikuwa akitaka kukaa hapo hospitalini na babu yake.
Mtu pekee ambaye alibakia alikuwa ni Kim Jip ambaye muda wote alikuwa kimya, ijapokuwa ilikuwa ngumu kujua kile alichokuwa akiwaza lakini kwa Roma aliweza kujua bwana huyo alikuwa kwenye hali ya huzuni kutokana na bosi wake kuugua, lakini hata hivyo hakuna ambaye alijaribu kumuongelesha , kwanza inasemekana hakuwa akiongea kabisa na kuna baadhi ya watu wanaamini alikuwa bubu.
Upande mwingine katika wilaya ya Gangnam gari nyeusi aina ya Benz ilisimama kando ya jengo la Apartment na Najma alionekana akishuaka kutoka kwenye gari hio mara baada ya kufunguliwa gari na Park Jonghyun.
“Asante kwa kunileta nyumbani , muda umeenda sana unaweza kurudi nyumbani mapema sasa”Aliongea Najma mara baaada ya Park Jonghyun kumsindikiza mpaka karibu na mlango wa kuingia kwenye jengo hilo.
Park Jonghyun alionyesha kutaka kumkumbatia lakini Najma alipiga hatua moja kurudi nyuma akimkwepa lakini hata hivyo hakuonyesha kukasirika.
“Vivian naomba niwe mkweli , tokea ulivyonikubalia ombi langu nimejikuta kuwa na ari mpya kweli , lini utakuwa mpenzi wangu rasmi?”Aliuliza , ilionekana licha ya kwamba Najma amemkubalia lakini bado hakuwa akipewa nafasi hata ya kugusa mwili wa mpenzi wake ndio maana anauliza ni lini atakuwa mpenzi wake rasmi.
“Nipe muda , bado hatujafahamiana kwa muda mrefu ndio maana”
“Okey nitasubiri , nitafute muda wowote ukinihitaji na nitakuja mara moja”Aliongea Park Jonghyun kwa upole na kumfanya Najma kutingisha kichwa kuonyesha kuelewa.
“Unapaswa kurudi sasa , kuna baridi”Alibembeleza Najma.
“Okey , uwe na usiku mwema Vivian”Aliongea na kisha alirudi kwenye gari na msaidizi wake alilitoa katika eneo hilo.
Najma aliishia kuangalia mtaa huo uliokuwa kimya kutokana na watu kuwa ndani kwenye nyumba na kujikuta akipumua kwa ahueni mara baada ya kuona Jonghyun amekwisha kuondoka.
Wakati akitaka kuingia ndan, aliweza kusikia jina lake likiitwa na kumfanya kugeuka nyuma.
“Najma..!!!”
Baada ya kugeuka alishangazwa mara baada ya kugundua ni Edna ambaye anakuja upande wake kwa namna ya kukimbia akiwa amevalia kofia ya Hat.
“Edna kwanini upo hapa..?”Aliuliza huku akionyesha wasiwsi na kumfanya Edna kuweka tabasamu la urafiki.
“Naweza kuona unapoishi , tunaweza kuongea pia kwani hatujapata nafasi ya kuongea hata kidogo”Aliongea Edna na kumfanya Najma kusita kidogo lakini aliishia kumkaribisha ndani na wote kwa pamoja wkaingia kwenye lift.
Upande mwingine kwenye gari, Park jonghyun alionekana kuegamia kioo cha gari huku msaidizi wake akiwa ndio dereva , alionekana kama mtu ambaye alikuwa kwenye mawazo .
“Boss , mwalimu Vivian ni mwanamke mweusi ambaye anatokea kwenye familia ya kimasikini kwanini unatumia juhuhdi kubwa kutaka kumpata, kwanini usipange mpango wa kumchezea na kisha ukachana nae?”Aliongea Dereva kwa lugha ya kikorea.
“Watu kama nyie mtaendelea kucheza na wanawake wa kwenye mabaa , upo sahihi Vivian anatokea kwenye familia ya kawaida lakini licha ya yote anakata mwanaume tajiri kama mimi , huoni kwama ni wa kipekee kati ya wanawake wote?”Aliongea na kumfanya Msaidizi wake kumeza mate.
“Upo sahihi boss , hata Miss Yoonhee tu analazimisha umpende licha ya umaarufi wake.”
“Mwanamke kama Vivian ndio pekee ambaye anaweza kuziamsha hisia za mwanaume , kwasasa siwezi kumfanyia chochote hivyo nitaenda nae taratibu na kumfanya akolee na baada ya hapo nitamtumia na kumtupa, nadhani hayo ndio mafanikio makubwa kwangu kama mwanaume”Aliongea Park Jonghyun huku akitoa tabasamu la kifedhuli.
“Kama ninavyokujua boss wangu , huwezi kupoteza muda wako kwa mwanamke mweusi , Bosi naomba ukimalizana nae na sisi angalau tujaribu kumuonja kwani nina shauku ya kuonja mwanamke wa kiafrika”Aliongea
“Wewe mpuuzi usie na kitu.. ila usijali siwezi kuwatupa”Aliongea na muda huo huo simu yake ilianza kuita mfululizo na aliitoa na baada ya kuona anaempigia alikunja ndita na kisha akapokea na kuweka sikioni.
“Nini?”Alionekana kuuliza hivyo na kisha akaendelea kusikiliza na baada ya kukata simu alivuta pumzi.
“Siendi nyumbani muda huu , endesha kuelekea hoteli ya Myeondong”Aliongea akimwamrisha msaidizi wake na gari ilikunja kiona palepale na kuchukua upande mwingine.
****
Edna baada ya kuingia ndani ya Apartment ya Najma alionekana kuvutiwa kutokana na ubunifu wa mwonekano wa ndani.
Alivua kofia yake aina ya hat na kisha akaketi kwenye sofa , huku bado macho yake yakikagua mandhari nzuri ya eneo la sebuleni katika hilo eneo.
“Huu ubunifu wa hapa ndani naweza kusema ni wa viwango, kwa utulivu wa hapa nadhani hupati shida kuishi peke yako”Aliongea na Najma aliishia kutabasamu kidogo na kisha alienda hadi upande wa jikoni kuandaa kikombe cha chai ili kumfanya mgeni wake kupasha mwili joto.
“Hii Sehemu imeandaliwa na babu yake Yezi kwani ni karibu na nyumbani kwake , ili kurahisisha kutimiza majikumu yangu ya kumfundisha Yezi”
“Kama ni hivyo angekupa chumba tu ndani ya lile jumba lake”
“Nadhani ni kwasababu ya sheria zao za kifamilia , isitoshe mimi sio kijakazi au mgeni mpaka kuishi nao”aliongea Najma na Edna alitingisha kichwa kukubaliana nae.
Maongezi yao yalidumu kwa sekunde kadhaa tu na kisha kimya kikatawala.
Edna mara baada ya kunywa kidogo chai aliinua uso wake na kumwangalia Najma kwa kumkagua na kisha akauuvaa ujasiri ili kuongea kile ambacho kimefikisha hapo ndani.
“Najma unatoka kimapenzi na Park Jonghyn?”Aliuliza Edna na kumfanya Najma kushangazwa swali la Edna.
“Ni Roma ndio ambaye amekuagizia kuja kunitembelea ili uniulize hilo swali?”Aliongea Najma na kumfanya Edna kuona amekamatika.
“Sio yeye tu ambae alihitaji kuuliza , hata mimi pia”
“Kwanini?”
“Kwasababu wasiwasi wetu ni kwa Park Jonghyun , unaweza kumuona ni mpole kwa nje lakini ana upande mwingine ambao huujui na unaweza kuumia”
“Kuumia?”Aliongea huku akionyesha kusita sita kutamka vizuri.
“Park Jonghyun alimfanya Yoonhee kuwa mpenzi wake baada ya kudhania kwamba ndio anakwenda kuwa mrithi wa mali za familia , lakini alimwacha baada ya kuona hakuwa chaguo la Park Juan””Aliongea Edna.
“Yoo yonhee ni yeye na mimi ni mimi , sina thamani yoyote katika vita yake ya kugombea urithi , hivyo kwanini nifanane na Yoonhee katika hilo”
“Lakini huoni kutokana na hilo tabia yake sio nzuri kuwa nae katika mahusiano?”Aliuliza Edna,
“Edna na mimi nataka nikuambie kuhusu Roma pia , Mbele ya macho yangu Roma kamnyofoa mtu shingo bila ya kuwa na hatia kabisa , hivyo kwa mantiki hio inamfanya kuwa uuuaji na mhalifu mkubwa, je unadhani hio ni tabia nzuri ya wewe kuendelea nae katika mahusiano?””
“Kwanini unajaribu kumlinganisa Park Jonghyun na Roma , yeye hakufanya hivyo kwa kufurahia , alifanya hivyo kukulinda”
“Lakini na Park Jonghyun alimtumia Yoonhee kama chombo ili kunufaika na urithi , unafikiri kitendo hicho kinamfanya kuwa tofauti na Roma”Edna aijikuta akikosa usemi hakuwaza maongezi yao yangefikia katika hatua hio.
“Najua wasiwasi wenu ni kuona huenda ninaweza kuchezewa na kisha kutupwa kama takakata , lakini Edna hivi hujafikiria kwamba kama hatokuwa ni Park Jonghyun kuna mtu mwingine ambaye anaweza kufanya hivyo, naomba nikose aibu kukuambia hili…….
Naweza nikawa kweli nimezaliwa katika familia ya kimasikini , lakini leo hii nipo hapa nikijaribu kuweka ukaribu na mtoto wa tajiri mkubwa ndani ya taifa hilo la Korea , nadhani yote hayo yananifanya kuwa mwanamke ambaye sijazaliwa kwa ajili ya kuwa wa kawaida, wakati nilipokuwa Dar nilishawahi kutekwa na mwanaume na akataka kunibaka na kama sio Roma yangekuwa mengine leo hii.
Nilikushukuru sana kwa kile ambacho ulifanya kwa kaka yangu , kipindi kile kabla sijapokea msaada wako nilikuwa kwenye hali ya mawazo sana kujua ni kipi naweza kufanya, lakini Edna unavyoniambia Park Jonghyun ni mtu mbaya kwangu , je unadhani ninaweza kujihakikishia mwanaume mwingine ambaye atakuja kwenye maisha yangu atakuwa na tabia nzuri , je unafikiri nikirudi leo Tanzania ninaweza kukutana na mwanaume ambaye anaweza kunipenda kweli?”
Najua dunia sio ya watu wabaya siku zote , lakini najaribu kufikiria kama nisipobahatika itakuaje, lakini katika yote nakuonea sana wivu Edna..”Aliongea kwa muda mrefu.
Edna hakutaka kongea lolote na kumuacha Najma kuongea kila anachojisikia ili kupunguza sumu iliokuwa ndani ya moyo wake.
“Edna unaweza kuja hapa bila ya wasiwasi kwa ajili ya kunionya kwasababu unajua kila kitu kipo chini yako , una uhakika kwamba muda wowote utakapopatwa na tatizo Roma atakuja kukusaidia , unaweza kumkasirikia , kumuudhi vile utakavyo na pia kuorodhesha mahitaji yako nayotaka atimize na atahakikisha anafanya vile unavyotaka , hayo ndio mahusiano niliokuwa nikiyaota mimi , nataka kupata mwanaume ambaye ninaweza kumtegemea , mwanaume ambaye atakuwa upande wangu muda wote , lakini mwisho wa siku wewe sio mimi , sina bahati kama uliokuwa nayo wewe”
“Kwahio kwa kuongea hivyo unamaanisha kwamba bado utaendelea na Park Jonghyun?”Aliuliza Edna.
“Kama mpango wake ni wa kunichezea tu mimi naweza kujuaje , sina kitu kikubwa cha kumpa kama faida ya kuwa na mimi , tayari ashachaguliwa kwenda kusimamia kampuni nje ya nchi , hajawahi kunilazimisha kufanya kitu chochote nje ya ridhaa yangu , hivyo kwanini nimkatae?”Aliongea .
Edna mpaka hapo aliona hana neno la kuongezea kwa msimamo aliokua nao Najma , lakini alijua nini Park Jonghyun anaweza kufanya pale ambapo atachokozwa.
Edna alitaka kumwambia Najma kwamba akipatwa na matatizo Roma atakuwepo kwa ajili yake , lakini aliona si itamaanisha kwamba anamuweka Najma kwenye mikono ya Roma.
“Hivyo Edna chochote unachoweza kusema hapa kwangu ni kama kitanzi tu , kadri unavyovuta ndio kinavyozidi kukaza zaidi na mwisho wa siku kinanyonga kabisa”Aliongea kimafumbo akimaanisha kwamba kadri anavyomshauri ndio anavyozidisha kasi.
“Najma unaonekana umekuwa mwanamke mkubwa sasa mwenye misimamo yako”
“Wanaume siku zote ni wenye kujidanganya , Edna kama sio mwanaume flani ambaye upo nae sasa huenda kwa umri huu ningekuwa na mwanaume”
“Inawezekana kabisa na inaweza kuwa tofauti pia kwani kuna muda wa kila kitu, Najma mimi nimekuja tu kukushauri lakini naona mwenzangu unajua kile ambacho unafanya hivyo siwezi kukuamulia maisha ambayo unayataka , kuna wanawake wengi sana huko nje ambao pia wanataka kuwa na mume wangu lakini siwezi kumruhusu kuwaonea huruma wote wakait mimi mwenyewe nakosa uvumilivu , hivyo Najma kama utapawa na shida nipigie tu simju nitakusiaida hata hivyo sisi tulikuwa marafiki”aliongea Edna na kisha akasimama na kutoka nje na kuingia kwenye lift na ndani ya dakika chache tu alikuwa nje ya jengo hilo na akakunja kulia akiachana na njia inayoelekea moja kwa moja barabarani.
Ilionekana alikuja hapo akiwa na Roma na alikuwa akimsubiri kwani mara baada ya kusogea mita kadhaa kutoka kwenye jengo hilo aliweza kumuona Roma na kumsogelea na kisha walishikana mikono na kuondoka kwa kutembea..
“Vipi mazungumzo yako yameendaje?”aliuliza Roma.
“Najma amesema anajua kile ambacho anakifanya hivyo hatuna haki ya kumuamulia maisha yake anayoyataka”Aliongea na kumfanya Roma atingishe kichwa kwa huzuni.
“Kama atahitaji msaada naomba umsaidie, labda unaweza pia kuongea na babu yake Yezi kama vipi amsaidie kwa namna nyingine na aweze kurudi Marekani au Tanzania , na isitoshe alikuwa ni rafiki yako sioni kama litakuwa tatizo kama utafanya juu chini urafiki wenu kuendelea”Aliongea Roma na Edna alitingisha kichwa na kumwambia asiwaze kuhusu hilo.
Upande mwingine katika familia ya Gong inayopatikana katika eneo la Gangnam , alionekana Gong Gyevung ambaye amekaa kwenye sofa la leather akiongea na simu , mbele yake alikuwa ameketi Gong Woo mtoto wake pamoja na Dokta Lee Eunjeong.
“Moyo ambao CEO Park anauhitaji tayari umekwisha kupatikana , siku ya upasuaji itakapoamualiwa tutaenda kuuchukua katika hospitaloi ya pili na kwa haraka tutaupeleka katika hospitali yetu kwa ajili ya upasuaji”Aliongea Gong Gyechung mara baada ya kumaliza kuongea na simu.
“Sir naomba unisamehe kwa kuuliza , hivi kwelu unataka kumruhusu yule msichana Clark kufanya upasuaji wa Park Juan? Hii si ingekuwa fursa kwetu kutoa msaada mkubwa kwa familia ya Park??”
“Lakini hata hivyo kufanya upasuaji wa viungo viwili kwa wakati mmoja kwa mtu mzee na dhaifu kama Park Juani unahisia asilimia za mafanikio ni ngapi?”aliuliza Gong Gyechung.
“Ni chini ya asilimia ishirini , lakini ukweli ni kwamba ukiunganisha na makosa ya kibinadamu naweza kusema asilimia ya upasuaji huo kufanikiwa ni chini ya asiliamia moja”
“Nadhani mpaka hapo sasa unapaswa kuelewa , kama tutajihusisha katika huu upasuaji huenda lawama zote zikatuangukia sisi kama upasuaji hautoenda vizuri , hivyo njia rahisi ni kumuacha Clark kufanya upasuaji huo na ukishafeli tutambebesha lawama zote za kumuua Park Juan , hivyo sisi kwa upande wetu tunatakiwa kutoa ushirikiano kuhakikisha kwamba viungo vyote vinavyohiajika vianapatkana na kwa ushirikiano wetu familia yao itaona ni nini tumefanya hivyo hata swala la ndoa kuwa rahisi zaidi kuzungumzika”
“Baba yule Yezi ni mrembo haswa naweza kusema anaweza kushindana na wasichana wengi waliozaliwa hapa hapa Korea, nitafurahi sana kama atakuwa mke wangu’aliongea Gong Woo.
“Acha kuwa mjinga , huruhusiwi kumpenda yule mwanamke , tunachokitaka sisi ni urahisi wa kupata mali zao, mara abaada ya Park Juana kufariki akiwa anafanyiwa upasuaji, baada ya hapo itakuwa juu yako kama utampenda au kumtumia na kuachana nae”
“Baba usijali katika hilo, siwezi kumpenda ila napenda awe sehemu ya wanawake wangu na isitoshe ni bikra nataka niwe mwanaume wake wa kwanza kuitoa”Aliongea huku akitabasamu kifedhuli na kumfanya Gong Gyechung kukunja sura lakini palepale waliangaliana na DoktaLee na kisha wakaangusha kicheko.
SEHEMU YA 522.
Siku iliofuata hali ya Park Juan ilionekana kuimarika na alikuwa kwenye hali nzuri ya kuweza kuongea na kila mtu aliemtembelea.
Asubuhi hio wanafamilia karibia wote walifika hospitali hapo kumjulia hali lakini pia kujua hatima ya matibabu yake kwani kama ni moyo wa kupandikizwa ulishapatikana.
Edna na Roma pia walihudhuria asubuhi hio wakiwa wamemsindikiza Yezi, upande wa wanafamilai wengine walikuwepo wote kasoro YoonHee pekee ambaye haikueleweka mpaka muda huo alikuwa wapi tokea akumbwe na janga la kurekodiwa filamu ya ngono na Roma.
Park Juan alifarijika namna ambavyo Yezi mjukuu wake alivyokuwa na wasiwasi juu ya afya yake , lakini pia kwa wakati mmoja alimuonea huruma kwa namna ambavyo alionyesha kuathirika na hali yake , hivyo kitu pekee ambacho alikifanya ni kumtuliza mjukuu wake kwa kumwambia kwamba atakuwa sawa.
Gong Gyechung alieambatana na Dokta Clark na Dokta Lee walifika hapo kwenye wodi ya VIP aliolazwa wakiwa na fomu maalumu za ridhaa(Consent form) na Gong Gyechung ndio alielezea kwa ufupi kuhusu maamuzi ambayo yamefikiwa ili kutatua tatizo lake la kiafya na Park Juan hakuonyesha kukataa kwani alihitaji kupona kwa wakati huo na isitoshe hakukuwa na njia mbadala ambayo inaweza kumponyesha.
“Mr Park hizi ni fomu tatu za ridhaa ambazo zinahitaji sahihi yako ya kwanza ni kwa ajili ya upasuaji, ya pili ni kwa ajili ya kuongezewa damu na ya tatu ni kwa ajili ya Ganzi , baada ya hapo tutaendelea sasa na taratibu ya upasuaji , moyo wa kupandikiza pamoja na Ini vyote vimeshapaikana chini ya usimamizi wa Mr Gong hapa”Aliongea Profesa Clark.
“Naamini mabadiliko haya ya ghafla ya daktari nadhani upasuaji unakwenda kuwa wa hatari?”AliongeaPArk Juan huku akimwangalia Dokta Lee aliekuwa amesimama upande wa kulia na kumfanya Dokta Lee kuona aibu kiume.
“Nadhani ipo hiyo lakini hata hivyo mimi kuongoza upasuaji wako itakugharimu kiasi kikubwa cha pesa, lakini watu matajiri kama nyie ni kiasi cha kawaida sana”Aliongea na kumfanya Park Juan kutabasamu.
“Paundi milioni ishirini sio kiasi kikubwa sana nitatoa”Alijibu
“Hapana Mr Park naomba nikurekebishe , ukweli ni kwamba ni paundi milioni arobaini”Aliongea bila wasiwasi na kuacha watu wote kuwa katika mshangao.
“Unasemaje?”Aliongea Park Jiyeon kwa mshangao.
“Mwanzoni ilikuwa ni milioni ishirini ya kumpandikiza Ini , lakini sasa hivi upasuaji ambao tunakwenda kumfanyia ni wa kupandikiza moyo pia , hivyo gharama lazima ziongezeke mara mbili yake”
“Wewe ni mwizi na huogopi kuiba na jua lote hili”Aliendelea kulalama Park Jiyeon.
“Unaweza kuongea utakavyo lakini siwezi kwenda kinyume na maneno yangu”
“Wewe…”
Ilibidi Park Juan kuingilia akiwapa ishara kwamba kila mmoja anapaswa kutulia ili yeye aongee.
“Nakubali kulipa , paundi milioni arobaini sio mbaya, kwa kujiamini kwako katika kutaja bei licha ya kwamba unachukua Risk naamini unajua nini unakifanya , lakini kabla ya upasuaji nataka kujua ni miaka mingapi naweza kuishi kama upasuaji utafanikiwa?”
“Kwa kawaida kwa mgonjwa ambaye anapandikizwa moyo ana asilimia themanini na tano kuishi mpaka miaka miwili au zaidi lakini kama utakua chini ya uangalizi mkubwa wa afya yako na kukawa asilimia ndogo ya moyo kukukataa(Heart graft rejection) basi utaweza kuishi mpaka miaka kumi au zaidi, lakini CEO Park kama unataka kuongeza urefu wa maisha yako kwanini usiongee na Mr Roma hapa , anazo mbinu zake za kurefusha maisha , kuokoa maisha yako kunaweza kuwa nje ya uwezo wake lakini kudumisha utendaji mzuri wa mwili wako ndio mahali pake”
“Mr Roma!!!?”Aliongea kwa mshangao huku akimgeukia Roma aliekuwa amekea upande wa kushoto kwake.
“CEO , familia yangu kutoka Tanzania tuna mbinu yetu ya siri ambayo hurithishwa vizazi na vizazi, watu wamezoea kuiita kwa majina mengi, kuna wanaoita Ubatizo wa moto mtakatifu unaodumu kwa siku tatu , wengine pia wanaita , Uumbaji uliotukuka wenye nguvu ya Upako ndani yake, mimi napenda kuita vidonge vya mafuta ya upako, Karne moja iliopita mababu zetu waliweza kupata nafasi ya kwenda kutembelea mbinguni na ndio walikoiba mbinu hio ya kurefusha maisha , upasuaji wako ukimalizika nitakupa ofa ya kukuuzia kidonge kimoja ambacho kitakufanya mwili wako kuwa mgumu kama shoka”Aliongea Roma kwa Kikorea na kufanya watu wote kushangazwa namna ambavyo aliongea kwa muda mrefu bila hata ya kuchapia lakini hata hivyo hakuna ambaye aliamini maneno yake.
“Hubby unamaanisha nini kusema una kitu kama hicho , ni lini tukawa na vidonge vya mafuta ya upako wa kurefusha maisha”Aliuliza Edna baada ya kumfinya Roma aache kuongea pumba.
“Ushasahau na wewe kwamba nina vile vidonge vya kijini vya ubora wa chini , kama nikimpatia ameze kimoja kitamfanya mwili wake kuimarika na anaweza kuishi hata miaka nane mbeleni , ni biashara nzuri yenye faida ya haraka kuliko hata ya kwako ya kuendesha kampuni”Aliongea na kumfanya Edna asiongeze neno.
Baada ya mazungumoz ya mengine ya dakika kama kumi na tano , Park Juana alisaini karatasi za ridhaa na kisha akamkabidhi Dokta Clark.
“Thank you for offering me your trust , I give you my word that your faith will be rewarded , the operation will begin at two in the afternoon”Aliongea akimaanisha kwamba anashukuru kwa kumwamini na imani yake itampa faida , na upasuaji wake utaanza siku hio hio saa nane mchana.
“Much appreciated”Alijibu Park Juan.
Clark hakuwa na haja ya kuandaa upasuaji huo kwa muda mrefu kwanni vuingo vyote vya kupandikiza vilishapatikana.
Upande wa wanafamilia wengine walikuwa na wasiwasi mkubwa kwani waliamini kupona kwa Park Juan ni mwanzo wa kutopata urithi, moja wapo ya watu hao alikuwa ni Park Jonghyun.
“Dr Clark babu yangu ataweza kupona kweli?”Aliuliza Park Jonghyun baada ya kufika kwenye korido ya wodi hizo za hadhi ya juu.
“Sijawahi kufeli “Alijibu Clark na kumfanya Dokta Lee ambaye alikuwa karibu kukunja sura huku akiwa kama mtu ambaye anaamini kabisa upasuaji huo hauwezi kufanikiwa kwa namna yoyote ile kutokana na uzoefu wake katika fani hio ya kitabibu.
Hatimae mchana ukawadia na Profesa Clark na wasaidizi wake walikuwa washajiandaa kwa ajili ya upasuaji, Mgonjwa ambaye ni Park Juan babu yake Yezi alishaingizwa na kuweka tayari katika meza ya upasuaji na tayari alikuwa chini ya nusu kaputi..
Upande wa wanafamilia na watu wengine walikuwa katika eneo maalumu ambalo limetengwa kwa ajili ya uona kile ambacho kinafanyika ndani ya chumba cha upasuaji.
Kabla ya upasuaji kuanza Gong Gyechung aliwapa taarifa kwamba operesheni ya moyo unaotakiwa kupandikizwa mgonjwa katika hospitali ya pili ushaanza kufanyika hivyo ungefika hapo ndani ya lisaa limoja ndani ya muda muafaka, kuhusu ini alisema tayari lipo na upasuaji unaweza kuanza.
Clark mara baada ya kuepwa taarifa hio alitingisha kichwa kuelewa na kisha akawageukia manesi na madaktari wasaidizi wake na kuanza kuwakumbushia majukumu yao kwa mara ya tatu.
“Kama nilivyosema Vincent wewe utadili na upandikizaji wa ini na Walleni utakuwa msimamizi mkuu wa Ganzi na mimi nitakuwa nafuatilia kwa ukaribu maendeleo ya upasuaji , nimeeleweka?”Aliuiza na wote walitingisha vichwa kuelewa.
Baada ya maelezo mafupi hatimae upasuaji ulianza rasmi na Dokta Vincent alitumia kisu vizuri kumkata mgonjwa na kutegneneza nafasi ya kuona ndani.
Upande mwingine wa wale watazamaii , alionekana Yezi akiwa na wasiwasi mno kuliko kila mmoja ambaye yupo katika hilo eneo.
‘Raisi Gong kwanini moyo wa kupandikizwa haujafika bado ,si ungekuwepo hapa kabla ya upasuaji kuanza?”
“Miss Yezi moyo unaopaswa kupandikizwa hautakiwi kukaa nje ya binadamu kwa muda mrefu la sivyo utaweza kupoteza utendaji kazi wake , hivyo kuhakikisha uuendelevu wake lazima ufike ndani ya muda na sio mapema sana”
“Naamini pia haitatokea mpishano wa muda?”aliongea Roma.
“Mr Roma kwa heshima zote , mchakato wa moyo na ini kwa ajili ya upandikizwaji upo chini ya familia yetu ya Gong , hivyo hatuwezi kuruhusu jambo kama hilo litokee kwani litaathiri taswira yetu kama familia , hata kama huheshimu nia yetu ya dhati tunaomba utumie akili ya kawaida tu kufikiria hilo”Aliongea Gong Gyechung na Roma aliishia kutingisha mabega tu akimaanisha kwamba anatarajia maneno yake yawe ya kweli.
Upande wa chumba cha upasuaji Clark alikuwa akifanya upasuaji kwa kasi ya ajabu na kufanya manesi kuwa katika mshangao , hata Dokta Lee mwenyewe hakuwa na spidi kama ya Profesa Clark.
Spidi yake ilimfanya Dokta Vincent kuwa katika presha kubwa ya kumaliza haraka upande wake wa kupandikiza ini.
Ni vitendo vya manesi kupitisha vifaaa vilivyoombwa na wengine kufanya usaidizi katika kukata uzi kila baada ya mshono.
“It’s glued , exceeding the aorta into edge of the heart”(“Umeganda ukipitiliza mpaka kwenye Aota kuingia mpaka kwenye kingo za moyo”)Aliongea Clark huku akionyesha mshangao
“Nini!!”Hata Dokta Lee ambaye alikuwa nje aliweza kuona kitu hicho na kumfanya Yezi kujawa na wasiwasi.
“Dokta Lee nini kimetokea?”Aliuliza Yezi.
“Kuokana na upasuaji uliopita, eneo la moyo wake limefungamana na tishu nyingi hivyo kutengeneza ukovu(Adhesion) kuzunguka eneo lote la nje ya moyo , hivyo itachukua muda mpaka kuondoa mgando huo”Aliongea Dokta Lee.
“Na akishindwa kuondoa Adhesion ndani ya muda mpaka moyo haufika hapa , upandikizaji hauwezi kufanikiwa”Alimalizia dokta mwingine aliekuwa pembeni ya Dokta Lee, walikuwepo wengi wakiangalia wakiwemo wanafunzi..
Upande wa ndani ya chumba cha upasuaji Dokta Clark alikuwa akijitahidi kutuliza watu wake ili kuwa katika hali ya kujiamini kuendelea na kazi.
“Utachukua jukumu la kuondoa Adhesion katike eneo lote kuzunguka moyo fanya haraka lakini kuwa makini”Aliongea dokta Clark akimwambia daktari wa kike ambayr ni msaidizi wake na upasuaji uliendelea.
……………………………
“Upandikizaji wa moyo unatakiwa kufanyika ndani ya masaa manne kamili na sasa yamebakia masaa mawili na dakika therethinni , kama itaendelea hivi hata kama moyo wa kupandikizwa kufika , mchakato wa kuupandikiza hauwezi kukamilika ndani ya muda”Aliongea Dokta Lee upande wa nje na kumfanya Yezi kuzidi kujawa na wasiwasi jumlisha machozi yaliokuwa yakimtoka , kijakazi wake Eunjung alikuwa akijaribu kumtuliza kwa kumpiga piga mgongoni.
“Let me handle the inferior Vena Cava , Probe ponted Scissors..”(Ngoja mimi nishughulike na Vena Cava ya upande wa chini , nipe mkasi Probe pointed Scissor)
Baadhi ya wasaidizi walikuwa wakitokwa na jasho sio kitoto lakini muda huo huo wakiwa katika hali ya kuguswa na namna ambavyo Dokta Clark alikuwa na utulivu wa hali ya juu katika kile anachokifanya
Upande wa Dokta Vincent ambaye yeye alikuwa akidili na Ini alikuwa bize kuhakikisha hachanganywi na changamoto zinzoendelea kujitokeza, aliendelea kufanya kazi kwa juhudi kubwa kukamilisha ndani ya muda .
“Kulingana na upandikizaji wa ini , ateri ya ini tayari imeunganishwa ,nitaendelea na ujenzi wa Gallblader, Twezer line forty…”Aliongea Vincenti na kumfanya Clark kumwangalia mwanafunzi wake na kutingisha kichwa kuonyesha kwamba alikuwa akifurahishwa na uwezo wake.
“Utumbo unazidi kupanuka , ongeza dozi ya kutuliza misuli(muscle relaxant), Dr Clark kama hali itaendelea hivi nafasi yetu ya mafanikio inazidi pia kushuka “Aliongea Dokta Vincent.
“Jipe utulivu, unadhani sijafikiria hilo ,kila kitu kimezingatiwa lakini kama daktari hata kama kuna nafasi ndogo sana ya mafanikio hakikisha unatumia hio hio mpaka itoshe na ifanye kazi”Aliongea na kuwafanya wote kuvuta pumzi na kuongeza umakini.
Upande wa wtazamaji Dokta Lee alianza kumkubali Dokta Clark kwa namna ambavyo alikuwa akijiamini.
Muda huo huo Dean(mganga mkuu) wa hospitali hio alionekana kupokea simu na kusikiliza kwa dakika chache na kisha akaipitisha kwenda kwa mkurugenzi Gong Gyechhung.
“Unafanya ujinga gani wewe mpumbavu ,toka haraka eneo la ajali na uje hapa ndani ya muda”Aliongea Gong Gyechung kwa hasira na kisha akakata simu na kufanya watu wote kumgeukia.
‘Kuna kilichotokea?”Aliuliza yule mganga mkuu kwani mtu aliepiga alitaka kuongea moja kwa moja na mkurugenzi.
“Gari ambalo lilikuwa likisarifisha moyo limekutana na ajali njiani hivyo kusababisha msongamano wa magari mrefu”Aliijibu
“Nini!!! … ni zaidi ya masaa mawili sasa kwanini hakuna ambaye ametoa taarifa?”Aliongea Haoming huku akionyesha kuchanganyikiwa.
“Ulisema mwenyewe hakuna tatizo ambalo linaweza kutokea kwanini sasa hivi?””Aliongea Yezi ambaye alikuwa na hofu kuzidi wote mara baada ya kusikia habari hio.
“Damn it , sijali kama unaniamini au lah , lakini hata mimi sikutarajia kama kunaweza kutokea ajali”Aliongea huku akig’ata meno kwa hasira na kufanya watu wote kuwa katika hali ambayo haielezeki.
“Dr Clark gari ambalo linasafirisha moyo limekwama njiani na barabara yote imefungwa , moyo hauwezi kufika ndani ya muda , narudia moyo hauwezi kufika ndani ya muda , hivyo tafadhari fanya mchakato wa kughairisha upandikizaji wa moyo”Aliongea Dokta Lee kwa kupitia Maiki.
Ndani ya Thieta kila mmoja alishitushwa na taarifa hio na kujikatia tamaa kabisa , hata Clark ambaye alikuwa bize alijikuta akisita kuendelea na kuanza kuangalia kila mmoja ambaye yupo hapo ndani.
“Barabara gani ajali hio imetokea?nitaenda kwa haraka na kuchukua moyo na kuuleta hapa ndani ya muda”Sauti nzito ya Kim jip ilisikika
“Ni upande wa kusini katika daraja la Dongjak , nishatuma tayari watu kufaulisha kupitia barabara nyingine”Aliongea Gong Gyechung,
“Hakuna muda wa kutosha kufanya hivo , waambie wakae sehemu walipo na nitawakuta , nitawafuata kwa kutumia Chopa yangu”Aliongea Kim Jip kwa Amri.
Gong Gyechung mpaka hapo alikuwa katika hali ya wasiwasi kutokana na namna wanafamilia hao walivyokuwa wakimwangalia kwa macho ya lawama namna ambavyo anashughulikia swala hilo.
“Ngoja niende mimi , sidhani kama atafika ndani ya muda , baki na Yezi”aliongea Roma akimwambia Edna kwa kutumia liugha ya kiswahili na Edna hakutaka kumzuia na kumwambia aende haraka na Roma alitoka katika hilo eneo bila ya wengine kufahamu anaenda wapi maana amemuaga Edna tu.
Lakini Yezi alijua Roma ambacho anajaribu kufanya , upande wa chumba cha upasuaji mara baada ya Clark kugeuka na kumuona Roma akiondoka hilo eneo , ujasiri ulirudi na kisha kugeukia wasaidizi wake.
“I need you to handle the superior Vena Cava ,in addition to our prior arrangement , Vincent how is progress?”(“Nataka ushughulikie Vena Cava ya upande wa juu kulingana na mpangilio wetu , Vincent vipi maendeleao?”)
“Kwa sasa naingia hatua ya mwisho mwisho ya kufunganisha utumbo ulioachia..”Aliongea na kumfanya Clark kuridhika.
“Dr Clark unahisi moyo utaweza kufika hapa kwa wakati?”Aliuliza Dokta Wallen.
‘Tusiwe na wasiwasi , tunapaswa kumuamini Roma”Aliongea
“Roma!!”
“Yeah , tupo chini ya masaa mawili mpaka kukamilisha , unapoteza muda,..”Aliogea
Upande mwingine katika eneo la hifadhi ya msitu kusini mwa jiji la Seoul karibu na daraja la Donjak Roma aliweza kutokezea katika upande ambao haukuwa ukipita watu.
Ilikuwa ni mchana hivyo Roma hakutaka kufanya vitendo ambavyo vitaibua taharuki.
Roma yeye alikuwa na haraka zaidi kuliko Kim Jip ambaye anatumia Chopa kufika hapo kwa ajili ya kuchukua moyo
Roma mara baada ya kuchunguza hilo eneo na kutoona kitu ambacho alitarajia alitumia uwezo wake wa kijini kuskani eneo zima hususani katika eneo la juu ambalo kulikuwa na msongamano mkubwa wa magari
Palepale aliweza kugundua tatizo lilikuwa nii moja wapo ya gari aina ya fuso lililokuwa katikati ya daraja likivujisha mafuta na kuanza kuwaka moto huku likiwa limekaa mshazari likizuia magari mengine kutoweza kupita.
Roma kwa haraka haraka alijua mpaka magari hayo kuweza kupita yote basi itachukua masaa mawili , eneo lote lilikuwa na ving’ora vya magari ya polisi ambayo yenyewe yaliongeza msongamano zaidi kwa aneo la mbele.
Ilikuwa ngumu hata kwa Kim Jib kufika hapo na Chopa yake halafu kuweza kufahamu ni gari ipi ambayo imebeba moyo.
Roma mara baada ya kukagua magari yote hatimae aliweza kuona gari dogo ambalo halikuwa ambulance lenye maandishi ubavuni kutoka hospitali ambayo moyo unatokea na palepale alipotea kutoka aliposimama na ile anaibukia ni pembeni ya gari hio karibu na mlango wa dereva na kumfanya aanaendesha kushituka.
“Sir Kuna tatizo lolote ?”
“Nimetokea katika ukoo wa Park , moyo wa kupandikiza uko wapi”Aliuliza Roma.
“Moyo gani tena , kuna mwenzako mwingine kafika hapa na kusema ametokea ukoo wa Park na nimempatia moyo tayari”
“Nini? Una uhakika ametokea katika familia ya Park? Jina lake ni nani?”
“ni bwana mdogo hivi kijana , jina lake ameniambia anaitwa Kim Jip”Aliongea yule dereva na kumfanya Roma kushangaa kwani hakutegemea kama Kim Jip anaweza kufika hapo kabla yake wakati alisema anakwenda na chopa.
“Ameelekea upande upi baada ya kumpatia? Na boksi lililobeba moyo huo linafanana vipi?”
“Ameelekea upande ule wa magharibi , ni ndani ya dakika kama mbili zilizopita na boksi ni rangi nyekundu”Aliongea yule dereva huku akiwa kama aliechaganyikiwa.
Roma mpaka hapo alikuwa tayari na majibu yake ambayo alihitaji na bila kuchelewa alikimbia kuelekea upande wa magharibi.
Roma alijiambia haiwezekani Kim Jip kufika hapo kabla yake , hivyo kwa haraka haraka aliamini mtu ambaye amefika hapo na kuchukua moyo alikuwa na mpango wa kumsingizia kim Jip.
Lakini Roma allijiuliza kwanini Kim Jip ndio ambaye amechaguliwa ili hali alikuwa mtu wa kawaida ambaye hata kuongea kwake ni mara chache sana.
Roma akiwa anasafiri kichawi akiendelea kukagua mazingira aliweza kuona kitu cha rangi nyekundu kilichoshikiliwa na mtu na palepale aliweza kuibukia mbele ya yule mtu .
Alikuwa kama Kim Jip mwenyewe kutokana na mwonekano wake na kama ni mtu mwingine wa kawaida angeweza kudanganyika na kuamini kwa asilimia mia mtu huyo aliekuwa mbele yake ni Kim Jip.
Yule mwanaume alionyesha mshutiko mara baada ya kutokewa na mtu mweusi mbele yake.
“Wewe ni nani?”
“Umeshindwa kunijua mimi , hivyo moja kwa moja inakufanya uwe feki”Aliongea Roma na kumfanya Kim Jip feki kurudi hatua moja nyuma.
“Sijali wewe ni nani , hivyo nipishe”Aliongea lakini Roma hakuwa na matamanio ya kundendeleza maongezi wakati anajua kwamba Clark anasubiria moyo huo kufikishwa ndani ya muda , hivyo alimsogelea kwa spidi yule Kim Jip feki na kwa kutumia mkono mmoja alishika lile boksi la rangi nyekundu.
Mwanaume alikasirishwa na kitendo cha Roma na palepale alitoa kisu mfano wa Daga akidhamiriia kumdunga nacho Roma eneo la tumboni.
Roma alikuwa ashategemea hivyo alimuacha afanye kile anachotaka na yeye kuendelea kung’ang’ania boksi.
Mwanaume yule mara baada ya kisu chake kukutana na ngozi ya Roma ni kama kimegonga kwenye jiwe kwani kilishindwa kupita na kumfanya yule mtu kujawa na mshangao pamoja na mashaka akiamini mtu ambaye yuko mbele yake ni shetani alie katika ngozi ya ubinadamu.
Roma mara baada ya kumpokonya lile boksi alimshikilia shingo na kumning’iniza hewani na kuanza kumkagua ili kujua ni mbinu gani aliotumia kubadilisha sura yake na kuiga ya Kim Jip.
Roma mara baada ya kumchunguza alifahamu staili yake ni kama ya Yamata sect lakini hio yenyewe ilikuwa na utofauti hivyo kwa haraka haraka aligundua inatokea katika makundi ya kininja ya baa la Asia upande wa Kusini Mashariki , mbinu yao haikuwa na muunganiko wowote na makundi ya Kijapani.
“Wewe ni nani?”Aliuliza Roma.
“Naitwa Kim Jip , unapata wapi ujasiri wa kuchokoza familia ya Park?”
“Unashindwa kuelewa upo kwenye hali gani si ndio , ukiendelea na ujinga navunja shingo yako?”Aliongea Roma lakini yule mwanaume alionekana kuwa na mafunzo ya hali ya juu kwani hakuonyesha hofu ya aina yoyote ile na palepale wakati Roma akisubiria jibu ghafla tu yule Kim jip feki alianza kutetema na palepale alitoa povu mdomoni.
Ilionekana tayari amekwisha kujiua na kumfanya Roma kushangazwa na ujasiri wake wa kujiua mwenyewe , mpaka hapo alijua watu waliomtuma sio wa kawaida.
Roma mpaka hapo aliona mtu huyo hana thamani tena huyo hivyo alimtupia pembeni na kuondoka hilo eneo kuanza safari ya kruudi hospitalini.
Hakutaka kumkausha kwani aliamini kama polisi wataweza kugundua miati yake basi wangefanya uchunguzi na ukweli ungejulikana .
Ndani ya hospitali ya Chuo ya Seoul watu wote aliokuwa wakiangalia upasuaji walionekana kuwa katika hali ya wasiwasi mno kutokana na kwamba mpaka muda huo hakukuwa na majibu ya kueleweka juu ya wapi moyo wa kupandikiza ulipo.
“Moyo unafika saa ngapi? , kadri muda unavyozidi kwenda utakosa uwezo wake wa kufanya kazi na kufanya upasuaji usifanikiwe”Aliuliza moja wapo wa madaktari wa hospitali hio.
“Kutokana na kuchelewa kwa kuondoa Adhesion kuzunguka moyo , hawawezi kumaliza ndani ya muda , hivyo sidhani kama wanaweza kufanikiwa hata kama moyo utafika ndani ya muda”Aliongea Dokta Lee na kufanya jopo lote la madaktari na wasiokuwa madaktari kuwa katika hali ya kukata tamaa wakiamini kabisa kwamba upasuaji mpaka hapo umekwisha kufeli.
Upande wa Thieta dokta Vincenti ndio kwanza alikuwa akimalizia kukata uzi wa mwisho wa mshono kukamilisha upandikizaji wa ini.
“The Transplant of the liver has completed , Dr Clark my work end here , I yield good faith on you with the rest of the operation”(Upandikizaji wa ini umekamilika , Dokta Clark kazi yangu inaishia hapa, natoa imani njema kwako na upasuaji uliobakia)
“Good work”Alijibu Dpokta Clark na Daktari msaidizi wa Clark alimwangalia dokta Clark.
‘Hatua ya mwisho tutaanza kuondoa Adhesion upande wa ventrikali ya kushoto , Dr Clark sidhani kama tunaweza kumaliza ndani ya muda”Aliongea na kumfanya Dokta Clark kuangalia kidogo moyo na kisha akaweka vifaa chini.
“Adhesion Complete “Aliongea na kufanya wasaidizi wake kushagnaa akimaanisha kwamba uondoaji wa ukovu umekamilika licha ya kwamba haujakamilika.
“Lakini Dokta Clark hatujamaliza kukata ukovu wa upande wa chini?”
“Yupo sahihi Dokta , huwezi kukata tamaa mapema , si ulisema mwenyewe hakuna kukata tamaa?”Aliongea nesi mkubwa.
Upande wa eneo la watazamaji Dokta Lee alionyesha kuwa katika hasira mara baada ya kuona anachokifanya dokta Clark.
“Clark unafanya nini , kama huwezi kukata ukovu wote ndani ya muda huwezi kumaliza upasuaji”alifoka.
“Nini kinatokea , kwanini Dokta Clark kaacha kuendelea?”Aliuliza Yezi kwa wasiwasi.
“Sijui anafanya nini , lakini kama ukovu wa eneo la Ventrikali ya kushoto usopokatwa hakuna uweezekano wa kuvuta moyo nje na ukatoka”
Wakati ndani ya thieta kila mtu akishindwa kuelewa nini anachotaka kufanya Dokta Clark palepale alianza kuongea.
“Mpaka sasa tunapaswa kusubiri kuona kama anaweza kuleta moyo dani ya muda muafaka”Aliongea na kisha palepale aligeukia saa ya mshale iliokuwa ikisikika ndani ya hiko chumba.
Muda huo kila sekunde ilifanya tumbo la kila mmoja kupatwa na joto kali mno na ilikuwa ni kama ile saa ilikuwa ikibipu ndani ya tumbo la kila mmoja.
Dakika tano zilipita na muda huo huo mlango wa chumba cha thieta ulifunguliwa na nesi ambaye alionekana kuwa katika haraka huku mkononi akiwa maeshikilia boksi la rangi nyekundu.
“Dr Clark the heart , The heart is here”Aliongea akisema moyo uko hapa Dokta clark.
Timu yote ilipatwa na ari mpya mara baada ya kuhakikisha ni moyo kweli wakufanyia upandikizaji na kazi ilianza upya.
Upande wa chumba cha watazamaji Roma aliweza kurudi na kwenda kukaa katika sehemu yake na palepale Clark aliekuwa kwenye chumba cha upasuaji aligeuka na kumwangalia Roma kwa macho yaliokuwa yakiongea kitu na Roma alimpa ishara pia na kisha Clark akarudisha macho kwenye kazi yake na akaendelea.
Upande wa Edna alivyoshuhudia namna ambavyo Roma na Clark wanavyoongea kwa ishara alijikuta moyo wake ukifurukuta.
“Mr Roma umefanikiwa vipi kuweza kurudi kwa haraka mpaka ukamzidi hata Kim Jip ambaye ametumia Chopa?”Aliuliza Gong Gyechung.
“Sidhani kama ni tatizo kwangu kurudi kwa haraka wakati muda ulikuwa unapotea”
“Ah.. ni kweli”Aliongea huku akifuta jasho lililokuwa kwenye uso wake huku akipotezea shauku yake.
Upande wa Park Jonghyun alimwangalia Roma huku akionyesha hali ambayo hajaridhishwa kabisa na matendo yake , lakini hata hivyo hakutaka kuonyesha wazi na watu kumsoma mawazo yake.,
Upande wa Dokta Lee na wenzake hawakuwa hata na habari namna gani Roma amefikisha moyo kwa haraka , mawazo yao yote kama madaktari yalikuwa kwa kile ambacho kinaendelea ndani ya chumba cha upasuaji, walijua hata kama moyo umefika hakuna namna ya upandikizaji kumalizika ndani ya muda ilihali hata moyo ulioharibika bado upo ndani ya kifua cha mgonjwa.
“Clark unafikiria nini…??”Aliuliza Dokta Lee ambaye alikuwa kwenye mhemko wa hali ya juu kwa kile ambacho kinaendelea, maana kidogo tu akiona jambo haelewi lazima ainue maiki na kuongea.
“The Transplant will start now ,Proceed with Piggyback propagation heart transplant”Aliongea .
“Wow!”Madaktari wote waliokuwa wakitazama upasuaji huo walishangazwa na maamuzi yake.
Upande wa Dokta Lee mshipa wa damu ulijitengeneza katika uso wake huku jasho likimtoka
“Oh! Huo ndio mpango wake?”
“What is happening, Piggyback what?”Aliuliza Gong Gyechung akiwa hajaelewa chochote , ijapokuwa maneno ya kingerea ameyasikia lakini hajaelewa maana yake katika maswala ya kitabibu.
“Piggyback unafahamika zaidi kama Parellel heart transplant ni njia ambayo nilisoma kwenye vitabu pekee na sijawahi kuona ikifanyika, ni njia ambayo inatumika kupandikiza mgonjwa na mioyo miwili kwa wakati mmoja , lakini kwa anachotaka kufanya Dokta Clark ni kuacha moyo wa Park Juan wenye shida kuendelea kufanya kazi huku akipandikiza moyo mwingine mpya pembeni yake na kuunganisha na mfumo wa mzunguko wa damu ya mwili, faida yake ni kwamba inamfanya mgonjwa kuwa na mioyo miwili kwa wakati mmoja inayofanya kazi , hivyo inasaidia wakati mpya ukizoea mwili na mwingine unaendelea kutoa sapoti ya kufanya kazi na hata huko mbeleni ukifa kabisa basi mpya utaendeleza kazi ya kusukuma damu”Aliongea Doka Lee na kufanya wale wasiokuwa madaktari kushangazwa na maneno yake.
“Nishawahi kusikia aina hii ya upasuaji kufanyika mara moja tu ndani ya Uk , unataka kumaanisha aliefanikisha ni Dokta Clark?”Aliuliza Dean wa hospitali.
“Lakini hata hivyo ili kuweza kufanikisha hilo lazima moyo wa kwanza auachanishe kwanza na mwili ndio aendelee hivyo mafanikio bado ni madogo”Aliongezea Doka Lee na madaktari wengine wote walikubaliana nae na kutaka kuona ni kipi dokta Clark angeweza kufanya kwa hali hio na muda mchache uliobaki.
Najua mnanidai vipande nitaendelea kuvifidia.