SEHEMU YA 294
Roma ilibidi kwanza ambembeleze mrembo Clark kwanza ili kufahamu ni kitu gani kapata kwenye majaribio ya damu yake, lakini licha ya kumbembeleza ,mrembo huyo bado alionekana kuwa na wasiwasi sana.
“Roma niambie , imekuwaje ukalishwa kitu cha ajabu namna hii?”Aliuliza Clark huku akimwangalia kwa macho yenye wasiwasi.
Roma ilibidi aanze kumueleza kila kitu kwanzia sababu ya kuja Japani lakini pia namna ambavyo amekutana na Seventeen feki na kumlisha sumu , mpaka anamaliza stori yake Clark alishangaa na kusikitishwa na jambo hilo
“Roma huyu Seventeen ni muhimu kwako mpaka unashindwa kujua mtego wa wa namna hio, kwanini hutaki kukubaliana na ukweli kwamba alishakufa na huwezi kumuona tena , Roma kwanini hubadiliki?”Aliuliza Clark kwa hasira mno na kwa jinsi alivyo, alionekana kuwa mtu ambaye alikuwa akimjali sana Roma Ramoni na ndio maana alikuwa amekasiika mno , mrembo huyu alikuwa akikumbuka mengi ya nyuma , Roma alikuwa akifanya mambo mengi ya kijinga mara baada tu ya Seventeen kufariki na ndio maana alilalamika na kuona licha ya kwamba tukio la Seventeen kufa lilitokea miaka mingi iliopita , lakini kwa upande wa Roma alionekana kama mtu ambaye hakuwa tayari kukubali ukweli kama Seveteen ashakufa , kuna muda Profesa aliamini uwepo wa Edna utamfanya Roma kumsahau Seventeen , lakini kwa namna ambavyo Roma alikamatika kwenye mtego wa kijinga namna hio aliamini bado Roma alikuwa na kumbukumbu za Seventeen.
“Roma unafikiria nini kitatutokea mara baada ya wewe kufariki, ni maadui wangapi watatuandama siku wakisikia kifo chako , sisi tunaishi kwa amani na maadui zetu wanatuogopa kwa ajili ya uwepo wako , lakini siku wakisikia kifo chako ni Habari nyingine…”Mrembo Clark alionekana kulalamika sana.
Ni kweli kabisa anachoongea Clark ,kwa mfano siku ikatokea Roma akafariki maadui wengi wa familia ya kifalme ya Wales watapata nafasi sasa ya kuwashambulia , kwani siku zote hawakuweza kufanya hivyo kutokana na uwepo wa Hades na jeshhi lake la The Eagles, na ndio maana Clark alikuwa akiogopa sana Roma akipatwa na matatizo na alitaka sana kumlinda , lakini tabia za Roma za kibinafsi za kumfikiria Seventeen mpaka kujiingiza kwenye matatizo zilimuumiza sana moyo wake.
Roma mwenyewe aliona kuna ukweli juu ya maneno ya Clark , kwa mfano sumu ya Polonium ilioingia kwenye mwili wake , kama angetemegea uwezo wa mwili wake tu pasipo kuwa na mbinu za kijini kujiponyesha huenda ingekuwa ni habari nyingine kuhusu yeye.
“Roma Do you know its real possible for you to die?”Aliuliza Clark huku akimwagalia Roma
“Is it very serious?”Aliuliza Roma kwani alikuwa kwenye sintofahamu kwani mrembo huyu badala ya kumueleza hali yake analia.
“Right now ,every single drop of the blood in you body is mixed with countless amount of lethal toxins , including heavy metal and radioactives ones , if all the element in your body combined can be used to develop nuclear bomb”
“Kwasasa damu yako kila tone limechanganyika na kiasi kisichohesabika cha sumu kali ukijumlisha na madini mazito kama elementi ndani ya mwili wako zikaambatanishwa basi zinao uwezo wa kuzalisha bomb la nuklia”Aliongea Jane na kumfanya Roma kutoa macho ni kweli alikuwa akifahamu sumu ya Polonium ni kali sana , lakini hakuamini kama inaweza kuwa na hatari kubwa namna hio.
Radioactives element maana yake ni aina flani ya madini ambayo yanadharisha mionzi mikali sana , mionzi ambayo kama itagusana na mwili wa binadamu athari zake ni kuua seli za mwili , mfano wa madini hayo ni Polonium , Uranium , sasa madini hayo ndio yanayotumika kutegenezea mabomu ya nyuklia.
Sasa ilishangaza sana kwa mwili wa Roma kuweza kuhimili sumu aina ya Polonium.
“Unauhakika kwamba chembe za sumu ambazo zipo kwenye mwili wangu zinaweza kutegeneza bomu?”Aliuliza Roma akiwa katika mshangao wa kutokuamini maneno ya Profesa Clark.
“Unafikiri natania , unahisi nimelia vyote hivi kwasababu uko sawa, nipo hapa mwenyewe nikishangaa umewezaje kuishi Zaidi ya siku mbili ukiwa na sumu mwilini”Aliongea
Roma mpaka hapo aliamini kwamba mbinu ambayo Master Chi aliomfundisha inauwezo mkubwa sana.
“Okey , niambie kama nitaweza kupona?”Aliongea Roma
“Inawezekana kuua dutu zote ambazo zipo kwenye mwili wako , ijapokuwa teknolijia ya sumu ulioingiziwa inatoka ndani ya kundi la Dhoruba nyekundu,lakini siwezi kushindwa kuiyeyusha sumu yote , lakini shida moja ni kwamba ijapokuwa ninaweza kutengeneza ‘Antidote’ lakini mwili wako kwasasa wote unasumu , jambo ambalo linanifanya kuona itakuwa ngumu sana kumaliza sumu yote mwilini”Roma alifikiria kidogo baada ya kusikia maelezo hayo.
“Vipi kama nitatumia uwezo wangu kuikusanya sumu yote mwilini na kuiweka sehemu moja?”Aliongea Roma na kumfanya Clark kushangaa.
“Can you really do it , there is no scientific theories at all that make it possible”Aliongea akimaanisha kwamba hakuna nadharia yoyote ya kisayansi ambayo inawezekana kwa mtu kukusanya sumu mwilini na kuiweka sehemu moja , Profesa Clark alionekana kuwa katika mshangao.
“Ninachokifanya sio kama Sayansi”Aliongea Roma
“Unazungumzia mbinu ya mazingaombwe ambayo uliniambia ulijifunzia Mongolia?”Aliuliza na Roma alitingisha kichwa , kwani katika stori yake hakumueleza Clark kwamba ameshafika levo ya juu kabisa , levo ya kuzaliwa upya, sasa Roma kipindi alipokuwa anaishsi Uingereza ashawahi kumwambia kuwa alikuwa akijifunza mafunzo ya kijini , ambayo yalikuwa yakimsaidia katika uongojjwa wake wa kuwa kichaa , ugonjwa ambao ulikuwa ukisababishwa na Saratani iliokuwa kwenye ubongo wake.
“Kama unaweza kufanya hivyo basi itakuwa rahisi , nitategeneza dawa haraka haraka , wanasayansi wengi ambao wapo ndani ya Dhoruba nyekundu ni wanafunzi wangu”Aliongea Clark.
Unachotakiwa kuelewa ni kwamba Redstorm au Dhoruba nyekundu ipo chini ya Zeros Organisation, lakini sasa misheni nyingi sio kama zilikuwa zikiongozwa na Zeros Organisation moja kwa moja bali ni kupitia kundi hili la Dhoruba Nyekundu , ni kwa mfano uchukulie Marekani kama Zeros halafu C?IA kama Dhoruba nyekundu.
Sasa Zeros ni Secret international Organisation ambayo imeundwa na mataifa makubwa duniani , lakini hio haimaanishi kwamba mataifa mengine madogo hayapo ndani ya Zeros , ukweli ni kwamba mataifa yote yapo ndani ya Zeros lakini sio wahusikaji wa moja kwa moja.
“Naona wanafunzi wako ndio wanataka kuniua?”Aliongea Roma akimwangalia Profesa Clark.
“Unatakiwa ujione kama mtu mwenye bahati , kwani wanasayansi wengi duniani hawaamini katika maswala ya mbinu za kijini unazotumia, mim mwenyewe kuna muda nilijaribu kufanya utafiti juu ya sayansi za kijini lakini mwisho wa siku kichwa kiliniuma kwani mambo mengi yanakosa Nadharia ya kufanyia Practical Experiment.”Aliongea Clark.
Unachotakiwa kuelewa ni kwamba katika ulimwengu wa Sayansi vitu havitokei bahati mbaya , au wanasayansi hawafanyi gunduzi kwa bahati mbaya , kinachokamilisha gunduzi kwa mwanasayansi ni Nadharia(Theories) ambayo ina Thesis ndani yake , Sasa usichanganyikiwe sana katika sayansi kunaanza ‘hypothesis’ halafu ndio inafuatia Nadharia, unaweza kuwa na ‘Thesis’ halafu ukakosa nadharia(Failed Thesis) , lakini huwezi kuwa na nadharia halafu ukakosa ‘Thesis’.
Ijapokuwa Clark hakuwa na uelewa na mbinu za kijini ambazo Roma alikuwa akitumia lakini alizipenda kwani zilikuwa na manufaa makubwa kwa Roma kuliko hasara , kwa mfano Roma kama isingekuwa mbinu hizo angekuwa sio binadamu Zaidi ya kuwa mnyama ambaye mara zote matamanio yake yatakuwa ni kuua pekee yaani asingeweza kuiongoza akili yake.
Roma kabla ya kupitia project LADO saratani yake ilikuwa ikisambaa mwilini kwa kiasi kikubwa sana na kipindi hiko alikuwa na miezi michache sana ya kuishi , lakini mara baada ya kupitia project hio faida kubwa aliopata ni kwaba ile saratasi ilibadilika kutoka malignant(Kansa inayosambaa kwa kasi) Kwenda ‘Benign’(Kansa ambayo haisambai inakuwa kama uvimbe),sasa kutokana na uvimbe huo kuwa katika ubongo inanamfanya muda mwingine kutoweza kujiongoza , Sasa mafunzo ambayo alifundishwa na Master Chi , yalimuongezea uwezo mkubwa sana wa kuongoza akili yake , yaani ilikuwa ni mara chache sana kwa yeye kupitia mabadiliko halafu akashindwa kurudi katikahali ya kawaida.
Roma baada ya kusikia maelezi ya Clark lakini pia namna mrembo huyo alivyokuwa akilia mbele yake , alijikuta pia akianza kumkumbuka mke wake kauzu , alitoa simu yake na kujaribu kupiga Kwenda Tanzania kwa kutumia namba yake iliozoeleka , lakini simu haikuweza kuunganishwa , ikimaanisha kwamba mtandao wa kitanzania haukuwa na huduma ya kupiga simu kimataifa.
Roma baada ya kuachwa na Clark ambaye alienda kutegeneza Dawa ya kumaliza sumu katika mwili wake , aliona awasiliane na Tanya .
“Contact the telecomunication Company immediately , ensure my number will be able to make and receaive call from Tanzania”Aliongea Roma akimpa maelekezo Tanya kwama ahakikisha namba yake inauwezo wa kupokea simu na kupiga ndani ya Japani Kwenda Tanzania.
Tanya upande wa pili ni kama alikuwa amepewa kazi anayoipenda kwani alipokea maagizo hayo kwa furaha kubwa na zilipita nusu saa tu namba ya Roma ilisoma mtandao na palepale alitafuta namba ya mke wake Edna na kupiga Kwenda Tanzania.
Na simu iliita kwa madakika kadhaa na kupokelewa .
SEHEMU YA 295
“Babe Wifey , mnaendeleaje huko Tanzania, nimekumiss sana mke wangu kipenzi”Aliongea Roma , lakini hakukuwa na jibu upande wa pili na kumfanya kutoa simu sikioni na kuangalia kama imekatwa , lakini aligundua simu haijakatwa.
“Wife muda si mrefu nitarudi Tanzania , nipo Hokkaido huku , niambie unataka nikuletee zawadi gani wewe na Lanlan , Unataka pete ya Almasi yanye ukubwa kama jicho , vipi kuhusu mkufu wa dhahabu wa thamani kubwa , vyote hivyo nitanunua nimeingiza pesa ndefu mumeo”Alijiongelesha Roma mwenyewe , lakini hakukuwa na jibu kabisa.
Upande wa Tanzania ilikuwa ni usiku kama wa saa saba za usiku na mrembo Edna alionekana mpaka muda huo hakuwa amelala kabisa, alikuwa na wasiwasi pia kwani zilipita takribani siku mbili tokea Roma atoke Tanzania Kwenda Japani lakini hakupokea hata simu ya kujulishwa kama alifika salama , mwanzoni hakuwa na tatizo , kwani alikuwa akiamini uwezo wa Roma , lakini bado alikuwa na wasiwasi , lakini pia mrembo huyo alikuwa na mawazo , maswala ambayo ameongea na Amiri juu ya dokta Sheba , yalikuwa yakizunguka kwenye kichwa chake , kuna hisia ambazo zilikuwa zikimwambia kwamba kifo cha mama yake hakikuwa cha kuitwa na Mungu bali kilikuwa cha kusababishwa na binadamu.
Ijapokuwa uchugugzi wa Amiri haukuwa umekamilika lakini kifo cha Dokta huyo siku mbili baada ya kuthibitisha kifo cha mama yake kilimfanya kuwa na wasiwasi sana na kuamini kuna jambo ambalo lilikuwa likiendelea ambalo yeye mwenyewe hakuwa akilifahamu , aliamini huenda kisasi ambacho alikuwa akizungumzia mama yake kilikuwa kikihusiana na kifo chake.
Sasa Edna akiwa kwenye wakati mgumu kama huo, ndio alijikuta akiwa na mawazo mno na hata kuanza kumkumbuka Roma , ijapokuwa ni kweli licha ya kwamba hawakua wa kukaa Pamoja mara nyingi , lakini Edna kwenye moyo wake aliona miezi mitano ambayo aliishi na Roma ilikuwa ni kama miaka miwili na aliamini uwepo wake karibu yake ulikuwa ukifaa Zaidi na kumfanya kutokujihisi mpweke.
Sasa baada ya siku nzima kuangalia simu yake huku akimtukana Roma kimoyo moyo kwa kutokumtaarifu kama amefika salama huko Japani , lakini pia kutowajulia hali , alijikuta akiwa na wasiwasi na hasira juu yake , muda wa saa saba hata alipoona simu ya Roma hakutaka kusikiliza pumba zake kabisa , alikuwa na hasira mno na alichokifanya ni kupokea na kuweka simu sikioni pasipo kujibu chochote mpaka pale Roma alipokata simu.
Edna aliamini kutokuongea ilikuwa ni adhabu nzuri kwa Roma , ndio alifurahi kwamba Roma amemkumbuka , lakini wakati huo alikuwa na hasira nae hivyo alimkalia kimya.
Baada ya kusikia sauti ya Roma , alirudi kitandani na kisha aakamwangalia Lanlan aliekuwa amelala Fofo na kumbusu kwenye maji la uso na kisha akajifunika shuka na usingizi ulimchukua dakika kadhaa mbele.
Asubuhi kulivyokucha Edna alimfikishia Blandina juu ya Roma kupiga simu usiku.
“Edna kasema yuko salama , anaendeleaje na kasema anarudi lini?”Aliuliza Blandina mfululizo huku akiwa ameshikilia ‘Cleaner’na alikuwa akisafisha eneo la sebuleni.
“Yuko salama mama , hupaswi kuwa na wasiwasi tena”Aliongea Edna lakini alijikuta akigeuka nyuma mara baada ya kukumbatiwa kwa nyuma na aligundua aliemkubatia alikuwa ni Lanlan aliekuwa akifikicha macho akionesha ndio kwanza anaamka.
“Mama Lanlan ananjaa…”Aliongea Lanlan na kumfanya Edna kutabasamu kwa uchungu , yaani ndio kwanza anaamka na kitu pekee ambacho anaulizia ni chakula hata salamu hakutoa.
“Lanlan msalimie kwanza bibi na unisalimie na mimi ndio nitakuandalia chakula”Aliongea Edna akimfundisha Lanlan.
“Goodmorning Grandma , Goodmorning Mom “Aliongea Lanlan na Blandina alitabasamu na kuitikia salamu ukweli kila alipokuwa akimuona Lanlan alitamani awe mtoto wa damu wa Roma , aliamini angejisikia vizuri kwa Roma kuwa na mtoto wake wa kumzaa ambae asubuhi angemuita bibi.
Upande wa Qian Xi Maisha yake ndani ya familia ya Edna aliyafurahia , rafiki yake mkubwa alikuwani Yezi na moja ya sababu kubwa ya kujiweka karibu na Yezi ni kutokana na kwamba wote walikuwa na asili ya bara moja , yaani Yezi alikuwa ni Mkorea upande wa baba na Mtanzania upande wa Mama.
Yezi licha ya kwamba alikuwa akipata kila kitu ndani ya familia ya Edna , lakini hakubweteka , mrembo huyo alikuwa amepata kazi kwenye moja ya mgahawa wa Kikorea hapohapo Osterbay , hivyo mara nyingi kila akitoka chuo anaunga moja kwa moja kufanya kazi , licha ya kwamba Edna alikuwa na pesa , ila hakupenda kabisa kumuomba na alitamani kushika hela alioitolea jasho yeye mwenyewe, Blandina ambaye alimchukulia Yezi kama mtoto wake hakupenda kabisa kwa Yezi kufanya kazi , lakini pia hakupenda kumuingilia kwani Yezi alikuwa mtu mzima.
Blandina sasa akili yake ilitulia baada ya kupewa taarifa na Edna kama Roma yupo salama , ule wasiwasi aliokuwa nao uliisha na hali ya furaha ilirudi kwa mara nyingine na hilo Edna aliliona na kumfanya hata kumkumbuka mama yake mzazi Rahel.
*******
Ni siku ya tarehe 25 jioni , yaani siku moja kabla ya ndoa ya Amina na Fayezi ndani ya taasisi ya utafifi wa kibaiolojia , Profesa Clark alionyesha kuridhishwa na dawa yake ilivyofanya kazi ndani ya mwili wa Roma , licha ya kwamba ilikuwa jambo la kushangaza kwa Roma kukusanya sumu yote mwilini mwake na kuisukuma mpaka kwenye mikono yake , lakini alijikuta akifaurahi baada ya kuona Roma kapona.
Upande wa Roma baada ya sumu ile kuisha kwenye mwili wake , hatimae aliweza kujisikia hali ambayo hakuwahi kuisiikia hapo kabla , ni kama mwili wake ulikuwa ukipitia mabadiliko ya hali ya juu sana , kwanza kabisa alijihisi kuwa mwepesi mno na alikuwa ni kama mtu ambaye amepoteza kumbukumbu na sasa akili yake ilikuwa ikianza upya kuhifadhi mafaili , alijikuta mara baada ya kunyanyuka kwenye kitanda akitabasamu huku akimwangalia Profesa Clark.
“Kipi kinakufanya kutabasamu?”
“Mwili wangu ni mwepesi sana , sijawahi kujisikia hivi hapo kabla”Aliongea Roma kwa furaha na kujiona sasa ile levo namba tisa ya kuzaliwa upya ndio anaihisi kikwelikweli.
Profesa Clark baada ya kuona Roma ni mwenye furaha , alishindwa kujizuia na kumsogelea Roma na kumbusu kwenye paji la uso huku akiwa ni mwenye hisia kali , kitendo ambacho kilimshangaza Roma , lakini pia kumfanya kuwa na aibu kwa mara ya kwanza kwenye Maisha yake , kwani kitendo cha mwanamke kumbusu kwenye paji la uso haikuwa cha kawaida hata kidogo na yeye ndio alipaswa kumfanyia mwanamke hivyo.
“Mwili wako ushakuwaa sawa kwa sasa”Aliongea Profesa Clark huku akipotezea tukio alilolifanya kwa kuangalia data zilizokuwa zikionekana kwenye Skrini.
“Thank you , you are always the one who can solve my biggest Troubles”
“Asante sana , siku zote umekuwa mtu wa kutatusha matatizo yangu makubwa”Aliongea Roma kwa namna ya shukrani kwa moyo msafi kabisa , ni kweli mrembo Clark alikuwa ni moja ya msaada mkubwa sana kwake, kwa mfano tu tokea jana yake hakulala alikesha ndanni ya maabara akitengeneza dawa ya kumtibu Roma.
Ukweli ni kwamba moja ya sababu ya Profesa Clark kusoma mambo ya biolojia ni kutokana na matatizo ya ubongo aliokuwa nayo Roma , tokea siku ambayo alifahamu kwamba Roma alikuwa na shida , alitumia muda mwingi sana kuangalia namna ya kumsaidia na mrembo huyo alikuwa ameweka nadhiri zake kwa Roma kwamba ipo siku lazima agundue dawa ya kuponya kansa, hivyo kumhudumia Roma ilikuwa ni jambo ambalo alikuwa akilipenda sana , na juu ya yote ni kwamba membo huyo alikuwa akimpenda sana Roma kwa mapenzi ya dhati kabisa tokea alivyokuwa mtoto hakujali kabisa Roma alikuwa akijihusisha kimapenzi na mama yake mzazi , kwake alitii hisia zake na aliamini Roma siku moja atakuwa wake na mpaka umri aliokuwa nao huo wa kuitwa Profesa hakuwahi kuguswa na mwanaume , alikuwa ni kama anamtunzia Roma.
Ukumbuke Roma wakati anamuokoa Catherine kwenye mikono ya maadui zake , Clark alikuwa ni wa umti wa miaka kumi na moja , lakini kutokana na kujaaliwa kwake uwezo mkubwa wa akili Clark alipofikisha umri wa miaka kumi na tano alikuwa ashafanya vitu vikubwa sana katika ulimwengu wa Sayansi , vitu ambavyo wanasayansi wa kawaida wangechukua miaka Zaidi ya arobaini katika ‘Carear’ zao.
“Kama unapenda nipokee sukrani zako , usiwe unafanya mambo ya kijinga na kujiweka katika hali hatarishi, ukumbuke wewe ni Pluto”Aliongea Clark.
“Hilo ni jina tu , lakini mimi pia ni binadamu , tukio la juzi limetokea kwasababu kumbukumbu za Maisha yangu ya nyuma ni za kuumiza sana na siwezi kuzifuta mara moja , hayo ni makosa ya kibinadamu tu , lakini nina uhakika swala hili haliwezi kujitokeza tena”Aliongea Roma.
“Hujaniambia una mpango gani na Kundi la Dhoruba nyekundu Pamoja na Takamagahara na Innova?”
“Kwasasa sina mpango wa kudili nao , nimeaachia vijana wao kwakua nina mpango wangu kichwani , miaka iliopita niliharibu makao makuu yote ya Zeros , lakini mpaka sasa naamini wamejikusanya upya mahali na wanaendeleza ushetani wao , nimeachia vijana wangu waendelee kufatilia taarifa zote za Zeros , siku wakijichanganya sitosita kuua mmoja mmoja nihakikishe nimeondoa mzizi wote”Aliongea Roma kwa ukawaida kabisa
“Umebadilika sana Roma , nimependezwa sana na mabadiliko yako”Aliongea na kisha akaweka baadhi ya mambo yake vizuri na kisha wote kwa Pamoja walitoka kwenye hio maabara , kazi ya Clark ilikuwa ishaisha hata hivyo kwahio kubaki hapo ndani ya maabara ilikuwa ni kama kupoteza muda.
Roma jana usiku wake alikuwa amewapa kazi kundi la Yamata Sect kuangalia nini kinaendelea sehemu ambayo Amina alikuwa amezuiliwa na taarifa zilionyesha kwamba licha ya mrembo huyo kuzuiwa kutotoka , lakini alikuwa akipata huduma zote kama vile malkia na Roma aliona haina haja ya Kwenda haraka , kwanza kabisa mpango wake haukuwa kumuokoa Amina tu , alikuwa na mpango mwingine kichwani , alijiambia kama kilichomleta Japani ni kuzia ndoa ya Amina basi angeagiza vijana wake tu kufanya kazi hio.
Upande mwingine ndani ya hoteli ya hadhi ya nyota tano ndani ya jiji la Otaru Hoteli iliofahamika kwa jina la El-Fadh, anaonekana mheshimiwa kigombola akiwa ndani ya eneo la VIP akiongea na Dodi Fayez.
“Mheshimiwa nadhani kwasasa unaweza kuwa na amani kabisa , nilikuambia kwamba ninao uwezo kumzimisha yule mpumbavu”Aliongea Fayezi kwa lugha ya kingereza na kumfanya mheshimiwa Kigombola asijue nazungumzia nini.
Kigombola alikuwa ndani ya Japani kwa ajili ya kuhudhuria sherehe ya harusi ya Amina na Fayezi , yeye akiwa kama rafiki wa karibu wa Familia ya Tajiri Khalifa hakuwa na mpango wa kukosa kabisa sherehe hio kwani pia alikuwa na mwaliko maalumu.
“Mr Fayezi sijui unachomaanisha “Aliongea Mheshimiwa Kigombola alievalia suti yake huku akiwa ameshikilia Glass ya wine .
Fayezi alitabasamu na kisha alitoa simu yake kampuni ya Apple na kisha akaenda upande wa picha na kumpatia mheshimiwa Kigombola na mheshimiwa alijikuta ni kama mtu ambaye hakuwa akiamini kile alichokuwa akiangalia kwani kwenye simu hio kulikuwa kukionekana picha ya Roma Ramoni akiwa amelala kwenye kitanda cha kusukuma kwa mataili.
“Mheshimiwa nadhani sasa ushaelewa ninachomaanisha”
“Unataka kusema Roma…. no I mean Hades amekufa?”Aliuliza mheshimiwa kwa namna ya kubabaika.
“Ndio amekufa , kama unavyoona picha yake hapo , mtego ambao aliwekewa ilikuwa ni ngumu sana kuukwepa”Aliongea Fayezi kwa furahsa sana na aliminimna Mvinyo kwenye glass zote mbili na kisha akampa ishara mheshimiwa kugongesha ‘Cheers’ kusherehekea.
Mheshimiwa Kigombola licha ya kuangalia picha hizo hakuwa akiamini kabisa maneno ya Fayezi , aliamini huenda mtu aliekuwa kwenye picha sio Roma mwenyewe , maana tokea siku ambayo amepata kusikia mambo ya kisaynasi kutoka kwa Yan Buwen , alikuwa na wasiwasi sana na kila mtu mwenye uwezo wa ajabu , aliamini huenda huko duniani kuna watu wawili wawili , yaani Clone za watu wengi sana na hata yeye mwenyewe alikuwa akitamani kutengeneza kopi yake.
“Hongera sana Fayezi kwa kufanikisha jambo ambalo nilishindwa kulikamilisha , hakika baba yako amekuwa mwenye maamuzi sahihi sana kukurithisha mali za familia”Aliongea Mheshimiwa Kigombola , ukweli hakutaka hata kusikia ni kwa namna gani ambavyo aliweza kumdhibiti Roma.
Baada ya mheshimiwa raisi kuachana na Fayez na yeye kuingia kwenye chumba chake ndani ya hoteli hio ya El Fadhi , alitoa simu yake haraka haraka na kisha akatafuta namba ya mtu Tanzania na ndani ya dakika kadhaa tu simu ilipokelewa.
“Mr Yan Buwen ninayotaarifa ambayo bado haina uthibitisho”Aliongea Mheshimiwa huku akisikiliza kwa umakini kwenye simu yake.
“Ni uzushi gani huo mheshimiwa unataka kuniambia ukiwa Japani?”Ilisikika sauti tulivu upande wa pili.
“Ni juu ya Hades, nimepata taarifa kutoka kwa mtoto wa Khalifa kutoka Dubai kwamba amekufa”Aliongea.
“Hahaha.. Hahahaha” kilisikika kicheko upande wa pili.
“Mr Yan Buwen mbona unacheka”
“Kigombola mimi pekee ndio mwenye nafasi ya kumuua Hades , hakuna binadamu ambaye ataweza kumuua Hades na mtu yoyote mwenye mpango wa kumuua tofauti na mimi mwenyewe ni adui yangu”
“Mr Yan Buwen lakini nimeona picha yake kabisa kwa macho yangu, na ni yeye kabisa”
“Mheshimiwa unaonaje ukiweka akili yako kwenye mpango wetu, wa kupata damu ya Hades tofauti na kuongea mambo yasio na maana usiku wote huu?”Sauti ilisikika upande wa pili na kumfanya mheshimiwa Kigombola kutulia kwa dakika kadhaa na kisha akavuta pumzi na kuzishusha.
“Sawa Mr Yan , naamini maneno yako Zaidi kuliko ya Fayezi , Hades hajafa bado”
“Safi mheshimiwa … mtu pekee ambaye unaweza kumuamini akikuambia kama Hades amekufa ni mimi peke yangu mheshimiwa , wengine wote wanazungumza uzushi , lakini hata hivyo taarifa yako inanifanya nitake kufanya jambo kabla ya Hades hajafufuka ….”
“Unataka kufanya nini?”
“Utapata matokeo mheshimiwa”Aliongea Yan Buwen na kisha akakata simu.