Simulizi ya Kijasusi: Salamu Kutoka Kuzimu

Simulizi ya Kijasusi: Salamu Kutoka Kuzimu

SEHEMU YA 19

wako. Tazama usivyo na raha. Mtu yeyote anayekufahamu akitokea hapa atadhani uko kizimbani ukisubiri hukumu ya kifo, badala ya kustarehe. Kwa nini?".

Joram aligeuka kumtazama huku akimtengenezea tabasamu jepesi. Kama kawaida, macho yake yaliona kile ambacho yamezoea kuona katika umbo la msichana huyo. Umbo lenye urefu wa kadri, unene wa kadri na sura ambayo ilioana vizuri na umbo hilo. Sura ambayo ilisisimua moyo wa kila mwanaume aliyepata kumtupia macho Neema. Kadhalika, mavazi ya Neema yalikuwa ya kupendeza na yaliliafiki umbo lake. Lilikuwa gauni la kitambaa chepesi ambacho ni dhahiri kilitokea nje ya Afrika Mashariki. Si hayo tu yaliyomfanya Joram ampende Neema na kumthamini binti huyo. Macho ya mwanadada huyu yalikuwa na uzuri wa pekee, uzuri wa kubembelezabembeleza, uzuri wa kishujaa. Yalikuwa na nuru. Si nuru wa "mapenzi" bali nuru ya ujasiri.

Ujasiri huo ndio aliouhusudu Joram. Na ni kwa ajili ya kuuthamini ndipo mara kwa mara akawa akimshinda nguvu shetani wake ambaye alikuwa akitamani kumtia mweleka kwa kumnong'oneza akisema: "Sikia Joram Neema ni binti mzuri sana... na anakupenda sana... Kwa nini usisahau walao kwa siku moja awe mwenzi wako kikazi akastarehe naye kitandani?... Hujui... Utakuwa usiku mzuri kuliko usiku wowote mwingine..." Hayo Joram aliyapuuza na kuendelea kumwona Neema kama mpenzi wake wa dhati.

Mawazo hayo yalimjia tena Joram. Wakati huo, badala ya kumjibu Neema
 
SEHEMU YA 20

swali lake, alitabasamu tena, kisha akavuta sigara kwa utulivu. Tayari kusahau yote.

"Tazama!" Neema alilalamika. "Bado hata unashindwa hata kunijibu! Wamekuloga nini kaka yangu? Kwa kweli sijaiona siku yoyote ambayo uko kwenye starehe isipokuwa hapo tu unapokuwa vitani ukipambana na mikasa ya kutatanisha huku maisha yako yakiwa hatarini. Sijasahau niliposoma katika gazeti la Kiongozi jinsi ulivyokuwa ukicheka mbele ya bastola ya kumwuaji yule hatari katika tukio lililoitwa Lazima Ufe... kule Arusha".

Tabasamu la Joram likageuka kicheko, "Mimi nilidhani kwamba wewe unanielewa vizuri zaidi mpenzi", alisema. "Tatizo langu ni watu kutokunielewa. Hapa nilipo, kimya kama nilivyo, nina furaha na nimestarehe kabisa. Lakini watu watadhani sina raha. Niwapo mbele ya bastola huwa sicheki bali nimechukia sana. Tabasamu langu huwa ni moja ya silaha zangu kwa ajili ya kumlegeza adui. Kwa kweli silaha hiyo naipenda zaidi ya bastola. Kwani humfanya adui ashindwe kuitumia bastola yake.

"Huwa huna hofu?".

"Sijui hofu ni kitu cha aina gani kwa kweli. Labda itabidi nimpate daktari mzuri anipime na kuona kama ninazo chembechembe za kitu hicho kinachoitwa hofu katika moyo wangu. Nadhani hili kwangu ni lazima..."

Neema akaangua kicheko. "U kiumbe wa ajabu sana Joram. Unaona sasa ulivyochangamka baada ya kuanza mazungumzo ya vifo na mauaji? Nadhani kifo chako kitakuwa cha kusikitisha sana".

"Ni afadhali kuliko kufia juu ya kitanda Muhimbili, tena baada ya kuugua miezi kadha wa kadha".
 
SEHEMU YA 21


Wakati mazungumzo hayo yakiendelea, macho ya Joram yakauacha uso wa Neema na kumtazama mtu ambaye alikuwa ameingia ghafla katika baa hiyo. Pamoja na kuingia kama watu wengine, akiwa katika mavazi ya kawaida, suti nyeusi, macho yake yalimvutia Joram. Macho yake yakaonyesha dalili ya wasiwasi na tahayari. Joram hakuona kama wasiwasi huo ulikuwa wa kuwahi pombe. Hilo alilidhihilisha kutokana na macho hayo yalivyotembea huku na huko ndani ya baa. Yalipokutana na macho ya Joram, yalizidi kupatwa na hofu kubwa. Kisha mtu huyo akageuka ba kutoka nje. Mara kilio kikali kikasikika kutoka nje. Ilikuwa sauti ya msichana, akilia kwa uchungu.

"Mwanamke malaya, anapokula pesa za watu wahuni hupelekwa gizani ambako hufanyiwa unyama", lilikuwa jibu la Joram.

"Umejuaje kuwa ni mwanamke malaya Joram?", Neema alihoji. Wakati huo watu walikuwa wakitoka ndani ya baa kwenda nje kutazama. "Anaweza kuwa mke wa mtu aliyekamatwa na kuletwa huku kwa ajili ya kutendewa unyama, twende tukaone".

"Hatuna muda huo..."

"Twende Joram". Wakati huo Neema alikuwa wima akimvuta Joram. "Twende tafadhali..." Ikamlazimu Joram kukubali. Umati wa watu ulikuwa ukielekea nyuma ya baa, sehemu ambayo ilikuwa na kivuli chenye giza kilichotokana na msitu wa maua yaliyoizunguka baa hiyo.

Japo ndipo sauti ya msichana huyo ilisikika akilia.

Alikuwa kalala chali, nusu uchi, vazi lake pekee ilikuwa kipande kidogo cha kanga ambacho kilifunika sehemu ya kati na kuruhusu sehemu kubwa
 
SEHEMU YA 22

isiyostahili kuonekana hovyo, itazamwe na watazamaji.

"Nakufa jamani, nakufa..." binti huyo aliendelea kulia huku akitupa miguu huku na kule.

Mtu mmoja alikuwa na tochi. Akamulika. Mwanga wake ulinisa kitu cha kutisha zaidi. Damu. Damu nzito ilikuwa imetapakaa kando na juu ya mwili wa msichana huyo. Mara kitu cha kutisha zaidi kikaonekana. Kisu! Kisu kirefu chenye damu. Kilikuwa kando ya mwili wa msichana huyo.

"Kisu jamani", mtu mmoja alilalamika.

"Nakufa... nisaidieni..." msichana huyu aliendelea kulalamika.

Kiasi Joram akaanza kuvutiwa. Hata hivyo Joram hakuvutiwa na kisu wala damu tu. Alikuwa akiutazama uso wa msichana huyo. Aliyaona macho yake. Alikuwa msichana mzuri sana isipokuwa macho yake tu. Yalikuwa macho yale yale aliyoyategemea kitambo. Macho ya msichana mlevi na malaya ambaye amekula vya watu na sasa vinamtokea puani. Hivyo aliushika mkono wa Neema na kumwambia. "Inatosha twende zetu".

"Joram! Tumwache msichana huyu katika hali hii kweli?" Neema alilalamika.

"Ni kazi ya polisi. Haonyeshi kama atakufa".

"Nakufa", binti huyo aliendelea kulia. "Upo hapo Joram? Tafadhali nisaidie. Inama usnishike japo mkono. Naogopa wataniua. Tafadhali Joram".

Kutajwa kwa jina la Joram kilisababisha watu waliokuwa hapo wamsahau msichana huyo mahututi, wakagauka kumtazama Joram, kijana mzuri wa sura, mrefu, nadhifu kwa mwili na mavazi, alionekana mpole tofauti na ilivyofikiriwa. "Kumbe huyu ndiye Joram Kiango!", walinongona watazamaji.
 
SEHEMU YA 23

Mara kadha wamesoma habari zake magazetini na kutegemewa kuwa labda lilikuwa pandikizi la mwanaume linaloweza kuwatisha majambazi. Kumbe.

"Nisaidie Joram..." msichana akaendelea kulalamika.

Joram ni mtu anayechukia kutazamwatazamwa na kushangiliwa, basi aliondoka polepole huku akifuatwa na Neema. Alipofika ndani akakiendea kibanda cha simu na kuzungusha 999. Sauti ilipomjibu alisema. "Hapa ni Forest of Flowers Bar... ndiyo Kinondoni. Njooni kuna mtu wenu anavuja damu..."

Polisi waliotummwa kuja kumchukuwa 'majeruhi' huyo walikuwa vijana wawili wenye imani moja dhidi ya wanawake malaya; kwamba malaya ni mwizi wa mchana. Hivyo, inapotokea akapigwa hata kuuawa ni haki yake kabisa.

Wakiwa na imani hiyo, polisi hao walimzoa Waridi bila huruma wala kujali malalamiko yake. Kama kuna jambo liliwasikitisha ni kule kuona kuwa kipigo alichopata hakikumsitahili kabisa. Majeraha machache yaliyokuwa usoni mwake na damu kidogo iliyokuwa ikivuja polisi hawa hawakuona kama ni adhabu iliyomtosha malaya kama huyu. Kama kuna jambo liliwashangaza polisi hawa, ni kuona kuwa kisu hicho kikali kilicholala kando yake hakikutimiza wajibu. Yawezekana washambuliaji wake walikuwa waoga, au hawakudhamilia lingine zaidi ya kumtisha tu.

Gari lilipoanza kuondoka, polisi hawakuchelewa kumtupia maswali kadha wa kadha, maswali ambayo hawakujali kusikiliza majibu yake. Na kwanini wapoteze muda kusikiliza uongo ulioandaliwa kitambo? Mmoja wa vijana hawa akajikuta kavutiwa na uzuri wa Waridi. Kwa kisingizio cha kumfuta damu, akanyoosha mkono wake na kumgusa titi lililokuwa wazi likiwatazama
 
SEHEMU YA 24

kama linawadhihaki. Mkono ukanogewa na kutelemshwa hadi kwenye paja lake jekundu lililonona. Mkono huo ukaanza ziara nyingine ya kupanda juu. Ulipoelekea kuvuka mipaka, Waridi akashindwa kustahamii zaidi. Akainua mkono wake na kuunasa mkono wa askari huyo na kuutoa juu ya paja lake. Baada ya kitendo hicho, Ndipo alipotanabahi kuwa kamgusa askari huyo kwa mkono ulioandaliwa maalumu
kwa ajili ya mtu mmoja tu, Joram Kiango. Waridi alijua kitakachomtokea askari huyo. Mara akaangua kilio kwa sauti kubwa. Kilio ambacho kiliwashagaza askari hao.

Walifanikiwa kumfikisha katika hospitali ya Mwananyamala ambapo alipokelewa na wauguzi wa zamu. Askari hao wakaaga na kuahidi kurudi hospitalini hapo kesho yake ili kuanza upelelezi wao.

Waridi aliwaomba wauguzi kumpeleka moja kwa moja bafuni. Huko alitupa dawa zote alizohifadhi mkononi, akanawa vizuri kwa dawa kama alivyoelekezwa na Proper. Ndipo aliporudi kwa wauguzi ambao hawakuonyesha nia ya kumhudumia kutokana na hali yake alikuwa hajambo. Walimuonyesha kitanda cha kulala katikati ya wagonjwa wawili, mmoja aliyelala fofofo kama maiti, wa pili alionekana akitapatapa kama mtu aliyekaribia kukata roho.

Waridi alilala kitandani hapo kwa dakika tano tu. Alikuwa akiwaza kwa makini. Hakuona anachofanya hapo hospitali. Wala hakuona sababu ya kuendelea kusubiri hadi atokee yule mtu ambaye aliamini angemwua na kushindwa kutimiza jukumu alilotumwa kulifanya. Wazo hilo likamfanya Waridi aamue kutoroka mara moja hospitalini hapo mara moja. Bila kufikiri
 
SEHEMU YA 25

mara ya pili aliinuka na kutoka kama anaelekea msalaani huku akipitia kanga moja ya yle mgonjwa aliyelala fofofo, akayafunika mavazi ya hospitali aliyovishwa na wauguzi ili ajisitiri. Alipotoka nje, akajitanda kanga hiyo na kufuata njia ya kutokea. Alijiingiza kwenye kundi la watu wengine waliokuwa wakitoka hospitalini hapo. Hakuna aliyemshuku kwa lolote. Dhamira yake ilikuwa kwenda Mburahati, akachukue chochote alichonacho, na senti kadhaa alizoficha chini ya godoro, kisha atoweke Dar na kwenda kokote mbali iwezekanavyo ambako mkono wa Prosper... usingemfikia kwa urahisi.

Lakini hakwenda zaidi ya hatua nne nje ya geti kabla ya kuisikia sauti ya mtu ikimwita kutoka nyuma. Akageuka kwa mshituko na kukutana ana kwa ana na Proper, ambaye alimjia akimchekea huku akisema kwa sauti ya dhihaka.

"Msichana mzuri... Umefanya vizuri... Nilitaka nije nikutoe mimi mwenyewe lakini kumbe umewahi kutoka. Pole kwa yote yaliyokukuta, ok usijali twende zetu, gari ile pale..."

Kesho yake ilikuwa asubuhi yenye mawingu kiasu cha kuvunja nguvu ya jua kali ambalo lilikuwa likitishia kutawala. Mmoja kati ya wale askari waliomchukua Waridi pale baa alikuwa tayari kawasili kazini kwake. Mkuu wake wa kazi alihitaji ripoti kamili ya "Kushambuliwa kwa yule msichana malaya" Akamtaka pia kujitahidi waliotenda tukio hilo watafutwe na kupatikaba haraka iwezekanavyo kwani mchezo wao wa kubaka wasichana si mzuri kimaadili hususan mchezo wa hatari.

Askari huyo akalazimika kumsubiri mwenzake kwa muda mrefu, hakutokea.
 
SEHEMU YA 26

Ikamshangaza. Kwa kuwa makazi yake hayakuwa mbali na kituo cha polisi cha Magomeni, askari huyo aliamua kumfuata nyumbani, Alimkuta! Lakini alimkuta katika hali ambayo haikuwa ya kawaida, Kwani haikuwa jambo la kawaida mtu aanze kuvaa suruali kabla haijafunika matako, aache kazi hiyo ba kuanza kuinamia sakafu hadi kichwa kigonge chini mfano wa mtu anayeswali. Na zaidi ya hayo mgeni aingie baada ya kupiga hodi mara kadhaa bila kuitikiwa, lakini akukute ukiendelea kuinama kimya kimya. Dakika mbili, tatu hadi tano.

"Bobi", askari huyo alimwita mwenzake kwa mshangao, akijiuliza huu ni mzaha wa aina gani, na umeanza lini! "Bobi", aliita tena askari huyo huku akimtazama tena kwa makini zaidi askari huyo. Ndipo alipoanza kuona povu lenye damu damu likimdondoka mwenzake mdomoni na puani. Akaruka nyuma, kisha akakusanya nguvu na kumsogelea ili amchunguze vizuri zaidi. Akayaona macho yake yalivyoduaa, akauona ulimi ulivyotoka na kutembea nje ya meno, akaona... Hofu ikamkumbuka ghafla. alikuwa akitazama maiti ya askari mwenzake. Hima akarudi kituo cha polisi kutoa taarifa.

Marehemu alipelekwa hosptali ambako daktari hakuchelewa kutoa taarifa kuhusu ugonjwa uliosababisha kifo hicho. "Ugonjwa wa moyo", daktari alidai. Kwamba alikutwa na ugonjwa huo ghafla wakati akivaa nguo zake, ikabainishwa kuwa kifo cha askari huyo kilitokana na shinikizo la damu.

Hakuna aliyeshuku kuwa asakri huyo amekufa kwa sumu ile, ya aina yake, ambayo aliigusa kutoka kwa Waridi, na kuifikisha sehemu iliyokusudiwa
 
SEHEMU YA 27

kufika, mwilini mwake, bila askari huyo kujua.

Sumu hiyo iliandawaliwa kwa ajili ya Joram Kiango peke yake

Wakati huo huo Joram Kiango alikuwa akipokea simu iliyopigwa ofisini mwake.

"Sauti yako i tamu mno masikioni sister, yaelekea nawe u kiumbe mzuri sana. Siwezi kuukataa kamwe mwaliko wa mtu mwenye sauti nzuri kama hiyo, Baada ya saa moja nadhani nitafika... Haya... Ahsante... Umesema wapi vile... Heh... Light Lodge?... Hapo siyo?. Nitafika baada ya saa moja...", akaweka simu chini na kuukunja uso wake akimtazama Neema Iddy, katibu wake ambaye pia alikuwa akumtazama.

"Nani?", Neema alihoji kwa shauku.

"Anajiita waridi".

"Waridi? Anataka nini?" Joram alipochelewa kujibu. Neema aliongeza. "Sikujua Joram kama nawe u mroho wa wanawake kiasi hicho. Sauti tu unaridhika na kuahidi kumfuata? Angalia Joram. Utaingia katika mtego. Una maadui wengi katika nchi hii".

"Nalijua hilo", Joram alisema. "Siendi kwa sababu ya sura wala sauti yake kama nilivyosema. Kilichonivutia ni maelezo yake. Anasema yeye ni yule msichana ambaye alipigwa pale baa ya Forest of Flowers. Anadai kuwa nia yake ni kunishukru pamoja na kunipa habari fulani ambayo inasisimua".

"Malaya kama yule! Hana habari yoyote. Anachotaka ni kukupata wewe tu".

"Hapana", Joram alimkatisha. Sauti yake ndiyo iliyonifanya nivutiwe hata kumwahidi kuwa nitakwenda. Inavyoonyesha kuna kitu zaidi ya anachosema. Nahitaji kujua ni nini. Zaidi ya sauti, nadhani utakumbuka kuwa jana binti
 
SEHEMU YA 28

huyo alilia sana akilitaja jina langu. Sijui alivyonijua".

"Ni mimi niliyekutaja kwanza".

"Ni kweli, lakini hiyo siyo sababu ya kumfanya aniite jina langu mara nyigi tena kwa ufasaha kiasi kile. Ni kama mtu aliyekuwa akinifahamu kitambo".

"Wewe si mtu unayefafamika Joram?".

"Pamoja na hilo", Joram aliongeza. "Ni wapi alikopata namba yangu ya simu? Tuseme kwenye vitabu vya simu. Kwa nini ahangaike kiasi hicho? Na kwa nini iwe mapema hivyo? Neema, huoni ni mwujiza huu? Jana tu alikuwa hoi. Leo anazungumza kwa uchangamfu kabisa na yuko logi badala ya hospitali! Huoni kama kuna jambo hapo? Yaonyesha kuwa ananitafuta. Yawezekana hata jana alikuwa akinihitaji mimi tu hakuwa majeruhi wala mgonjwa!" Akasita kidogo kabla hajaongeza kwa sauti ya chini akisema: Na atanipata. Kwa muda mrefu nimekuwa sina kazi ya kufanya".

Wakati huo Joram alikuwa wima akivuta droo hii na ile, akiweka hiki mifukoni na hiki kiunoni. Mara akaanza hatua za haraka kuelekea mlangoni.

"Yaani unakwenda Joram, mara hii!", Neema aliuliza kwa mshangao.

"Naam".

"Mapema namna hiyo? Si umemwambia baada ya saa moja?".

"Niliamua kumdanganya. Siamini kama yeye ananieleza ukweli mtupu, hivyo nami sioni ubaya wa kumweleza uongo kidogo. Nataka kufika mapema kidogo nione anachofanya".

"Lakini ujihadhari", Neema alimwambia wakati akivuka kizingiti cha mlango.

"Usijali Neema", Joram akamjibu bila kugeuka nyuma.


"Anakuja! Na atakufa!" Proper alimwambia Waridi.

"Ondoa hiyo mikunjo ya hofu usoni uvae suruali yako nzuri kama ilivyo.
 
SEHEMU YA 29

Akifika mpe tabasamu, mpe mapenzi, kisha mkaribibishe pombe. Usisahau chupa hilo hapo ni kwa ajii yake, akionja tu yamekwisha, asipoinywa mpake hii kwa hila".

Walikuwa katika chumba fulani, ghorofa fulani, katika jumba hili la light ambalo liko katika mtaa wa Lumumba, jijini Dar es Salaam. Proper alikodi chumba hiki kwa ajili ya kazi hii tangu jana alipomtoa Waridi kule hospitali. Usiku mzima aliutmia kumtisha Waridi kwa kila namna pale alipojaribu kuleta ubishi. Kisha alikuwa amemlazimisha kufanya naye mapenzi kwa njia zake za kinyama. Ilipofika alfajiri ndipo wakaanza kupanga mikakati ya mauaji.

Waridi alivishwa vazi jeupe la hariri, vazi hili lilifichua kila kitu kilichofaa kifichwa katika mwili wake. Kila jicho liliweza kuona mwili mzuri wa msichana huyo, ulikuwa ukimelelemeta kwa wekundu ndani ya mavazi hayo. Uso wake pia ulikuwa "kioo" kwa uzuri wake wa asili ulioshinikizwa kwa vipodozi murua vilivyotumiwa kistaarabu. Nywele zake zilitengenezwa kwa ile mitindo ya kisasa. Kwa kila hali, msichana huyu alionekana mtu tofauti kabisa na yule binti ambaye usiku wa jana tu alilala chini pale baa akiwa nusu uchi, akilia. Huyu alikuwa katika hali ambayo ilikusudiwa na ilitosha kuushinda ukaidi wa Joram Kiango dhidi ya wasichana warembo.

"Uwe msichana hodari. Ni kazi ndogo tu. Baada ya hapo utakuwa huru. Nitakulipa pesa za kutosha ukanisubiri Nairobi. Kutoka hapo tutakwenda zetu London au New York, tukatumie. Unasemaje?".

Waridi hakujibu.
 
SEHEMU YA 30


"Mbona husemi neno?" Proper alimwuliza Waridi. "Hofu ya nini? Hii ni kazi ndogo mno kuliko ile uliyoifanya kwa Bomba. Na bado itakulipa pesa nyingi zaidi ya ule uchafu uliochukua. Jitie furaha na ucheke kidogo".

Kikcheko kilikuwa mbali na Waridi. Aliendelea kuduaa kama mzoga akisubiri lolote aliloelekezwa kulifanya. Hilo likamchukiza sana Proper.

Akasema. "Sikia wewe, endapo utavuruga tena mpango huu, sitasita kukuua papa hapa. Sasa hivi bado dakika ishirini Joram ataingia hapa. Nitakuwa chumba cha pili nikiangalia kila kitu. Ukishindwa au kuvuruga mpango huu nitakuua wewe na huyo Joram papa hapa. Nitakuua wewe kwanza na kisha Joram kwa hili hapa", akatoa bastola ndogo kutoka kwenye mfuko wa koti lake.

"Sipendi kukuua", Proper aliongeza. "Lakini ukinilazimisha nitaitumia kuwaua". Akaitazama tena saa yake. "JOram anaweza kuwa anakuja sasa. Natoka. Kumbuka kuwa niko karibu na tayari kukuua endapo utavuruga mpango huu. Sawa? Proper alitoka na kumwacha Waridi ameduwaa kama alivyokuwa.

Baada ya dakika kadhaa mlango wa chumba hiki uligogwa, kisha ukafunguliwa. Joram Kiango alichungulia ndani na kisha kuingia polepole macho yake yakiwa yamepumbazwa na uzuri wa Waridi. Hakutegemea.

"Sisiter... mimi ni mgeni wako nadhani. Naitwa Joram Kiango", alieleza Joram huku akiandaa tabasamu ambalo alijua linamfaa binti mzuri kama huyu.

Ndipo Waridi alipogeuka kumtazama.


Kama kuna wanawake ambao husimbua mioyo ya wanaume mara tu watokeapo mbele yao hata wanaume hao wakajisahau na kuzisahau shughuli
 
SEHEMU YA 31

zao, basi ni dhahiri pia wapo wanaume ambao huisumbua mioyo ya wanawake kwa kiwango kile kile. Na kama kweli wapo, miongoni mwao yumo Joram Kiango. Hayo yalijidhihirisha baada ya Waridi kumtia machoni Joram alipoingia chumbani.

Moyo wake ulipoteza mapigo kwa sekunde kadhaa. Roho yake ilihisi kupaa nje ya mwili wake. Kadhalika, damu ilimsisimka kiasi cha kumfanya ahisi ganzi mwili mzima. Hivyo, hakuweza kuyaondoa macho yake juu ya umbo la Joram ambaye alimsogelea polepole. Nusura wazimu umpande Waridi alipoona uso na tabasamu la Joram, lililotosha kuwa tiba kwa maradhi yake. Maradhi aliyoamini kuwa hayangeweza kutibika.

Kwa bahati mbaya, Waridi hakuwahi kupenda mwanaume katika maisha yake. Hivyo hakujua mapenzi ni nini. Hakuwahi kuyaonja. Kama angejua, angefahamu nini kitatokea. Badala yake alihisi maumivu moyoni na huzuni kubwa akilini mwake. Akanusurika kutokwa na machozi. Hakujua nini kinamtokea. Isipokuwa kitu kimoja tu alikifahamu, Joram hakuwa mtu wa kufa, Hakuona sababu ya kumwua, Asingeweza...

Tazama alivyosimama mbele yake kwa upendo na utulivu kama malaika asiye na hatia. Tazama anavyochekelea kwa furaha kama nuru, Mtazame. La, huyu kijana si mtu wa kufa. Waridi akawa ameamua hivyo.

"Nadhani mimi ni mgeni wako, mpenzi, Joram alisema tena, akinyoosha mkono wake kumgusa Waridi kwenye bega lake la kuume.

Joram alikuwa ameshangazwa na uzuri wa msicha huyu. Vipi wengine waumbwe kwa upendeleo kiasi hiki wakati wengine wasitofautiane sana na vinyago? alijiuliza. Mavazi mazuri ya msichana huyu pia yalimchanganya
 
SEHEMU YA 32

Joram; yalikuwa mavazi mapya ya thamani kubwa, kisha ya kihuni kama yalivyondaliwa mahususi kwa ajili ya kumtongoza! Hicho hakikumshangaza Joram, Lakini alishangazwa na uso mzuri wa msichana huyu ukiwa katika dimbwi la majonzi, mashaka, hofu na msiba. Hilo halikumshangaza hata kidogo.

"Ndio...ka... karibu kaka", waridi alianza kusema huku akibabaika,

Joram alimvuta mkono na kumwongoza hadi kitandani, ambako alimketisha kisha naye akaketi kando yake huku akiendelea kuushika mkono wa Waridi.

"Nilikwambia kuwa sauti yako ni tamu kama ilivyo sura yako? Naamini sikukosea. Ama kweli umeumbika bibie. Ulimhonga nini muumba hata akakupendelea?"

Sauti ya Joram, tabasamu lake likasindikiza kila neno, hali hiyo ikamfanya Waridi aanze kuchangamka. Akasahau yote yaliyokuwa mbele yake na kujikuta kazama katika maongezi na Joram. Katika kipindi hicho kifupi bila kujifahamu Waridi alijikuta tayari akiwa ameufunua moyo wake wote kwa Joram, akimsimulia matatizo yake yote. Alipotanabahi alikuwa akisema: "Najisikia kutoweka nje ya nchi hii".

"Kwanini?".

Swahili hilo lilimzindia Waridi. Hakujua yapi alikuwa tayari kuyatamka ambayo hayakustahili kuiacha milki ya kinywa chake, Hofu ikamrejea. Akalikumbua jukumu lililokuwa mbele yake: kumfanya kijana huyu kuwa marehemu. Ama ni yeye atajayefanywa marehemu.

Hofu hiyo, ilizidi baada ya Joram kuinuka na kuiendea meza iliyokuwa na chupa mbili za pombe huku akisema: "Bia hii? Unaonaje nikianza kuimimina tumboni mwangu ili kupoza joto la Dar es Salaam kabla hujanieleza sababu za
 
SEHEMU YA 33
kuniita hapa? Siamini kwama kweli umeniita kwa ajili ya kunishukuru tu, yaani hilo likusukume kunitafuta..."

"Usinywe hiyo pombe", Waridi alifoka.

"Kwanini mpenzi? Nilidhani umeiandaa kwa ajili yangu", Joram alifuatwa na tabasamu la kukata na shoka.

Waridi alikuwa akitetemeka. Lakini asingeweza kusahau maneno ya yule mtu katili Proper alipomwambia: "Nitakuwa chumba cha pili... Ukishindwa tena nitakuua papa hapa..." Waridi hakupenda kufa, lakini pia hakuwa tayari kumuona kijana huyu asiye na hatia, afe. Afanye nini? Kwa kutojua la kufanya akaanza kulia. Mikono ya Joram ilitua tena mabegani kwa Waridi akimfariji na kumkumbatia huku akisema.

"Kama hutaki ninywe hii bia ni wazi kwamba kuna zawadi kubwa na tamu zaidi ya bia uliyoiandaa kwa ajili yangu. Kwa bahati mbaya nina mazoea ya kunywa pombe kabla ya yote. Kwa maana hiyo niruhusu ninywe bia moja tafadhali".

"Usi..." Waridi alijaribu kufoka tena. Joram alimzuia kwa kuuziba mdomo wake kwa kiganja cha mkono wake huku akiweka kinywa chakr karibu na sikio la Waridi, akamnong'oneza.

ITAENDELEA
 
Back
Top Bottom