Simulizi ya Kijasusi: Salamu Kutoka Kuzimu

Simulizi ya Kijasusi: Salamu Kutoka Kuzimu

SEHEMU YA 34

"Najua kitakachotokea. Sinywi pombe hiyo. Acha nijifanye kama nakunywa ili nimpumbaze huyu anayetaka kuniua. Nitakuomba wewe uwe msiri wangu. Mwache aamini kuwa ameniua. Mwache kila mtu aamini kuwa nimekufa. Nataka kufahamu hawa waliokusudia kuniua jambo gani wanakusudia kutenda".

waridi aliduaa. "Ume... umewezaje kujua? aliuliza kwa kunong'ona.

"Niliwahi kufika eneo hili mapema na kumsikia alivyokuwa akikuamru. Nawe pia lazima ufahamu kuwa uko hatarini. Huyu ni mtu hatari. Mara tuu utakapotoka hapa, toroka uende kokote asikoweza kukufikia. Sasa acha nijifanye nainywa pombe yake". Joram akaongeza sauti kusema. "Glasi? Acha ninywe kihuni".

Joram aliifungua chumpa moja na kuingia nayo msalani ambako aliimimina nusu kwenye tundu la choo, Akarudi na kuitua mezani huku akiendelea kuongea na Warid, mazungumzo yao yalifanyika taratibu kwa sauti ya chini. Mara kadhaa Joram alimshika waridi na kumtomasa hapa na pale kwa ajili ya kumtoa hofu.

"sasa mpenzi sikia", aliongeza. "Ninaye mgeni ambaye atakuja ofisini kwangu baada ya nusu saa kuanzia sasa. Baada ya kumalizana na mgeni huyo, leo kutwa nzima nitakuwa huru. Waonaje niende ofisini mara moja na kurudi sasa hivi? Naamini leo tutashinda pamoja kwa furaha sana. Naamini itakuwa siku njema twetu".

"Sawa", Waridi alijikongoja kujibu.

"Tafadhali nikukute, ukiwa kama ulivyozaliwa. Ikiwezekana, kitandani, sawa?"

"Bila shaka".

Mara tu Joram alipotoweka machoni mwake, Waridi alijikuta akirejewa na hofu. Ile hakika na ushujaa ambao alikuwa ameuhisi kwa kusikia sauti ya Joram na kuyaona macho yake yang'aavyo sasa ilikuwa kama ndoto tu. Ndoto ya kale. Hakujua lipi afanye. Akaendelea kuduwaa kimya, akitazama huku na huku kama aliyetegemea kumwona Zibril akimjia kwa lengo ka kutwa roho yake.

Waridi angetimua mbio Proper alivyoingia ghafla huku akimtazama Waridi kwa macho ya kutisha. Waridi angeweza kukimbia kama ukuta usingekuwa umemtenga na dunia ya nje. Alichofanya ni kurudi nyuma hatua kadhaa hadi alipoegemea ukuta, macho yenye hofu kayatoa kama kondoo aliyekuwa juu ya madhabahu, akisubiri kutolewa kafara.
 
SEHEMU YA 35


"Mwanakharamu... malaya mkubwa, mwana wa malaya mkubwa...", Proper alifoka. "Umekosa walau ushujaa wa kunidanganya kuwa hawara yako amekunywa pombe niliyomwandalia? Mara hii umesahau kuwa mmekubaliana naye adai kuwa ameinywa ili asingizie kuwa kafa. Nakusikitikia Bi. mdogo. Namsikitikia pia huyo hawara yako. Hajui afanyalo. Anadhani kuwa anacheza na watoto wadogo kama alivyozowea. Nilikuwa nimemfanyia hisani kubwa ili afe kistaarabu hakutaka. Kajitia ujanja. Sasa atakufa kifo cha kusikitisha zaidi".

Jodor Proper aligeuka kama anataka kutoka. Mara kama aliyekumbuka jambo alimgeukia tena Waridi na kusema. "Nawe malaya mwovu hufai kuishi zaidi. Huna faida duniani wala haki ya kuishi tena. Utamfuata mpenzi wako Bomba akhera. Mpe salamu zangu, mwambie hongera kwa hila zake zisizo na ila". Akageuka na kutoka.

Machozi yalikuwa yamenyauka machoni mwa Waridi. Sasa aliiona dunia kama kitu ambacho kilikuwa kando yake. Naam, maisha yake yalikuwa ukingoni. Asingeweza kutilia mashaka sauti ile ya Proper yenye uhakika. Sauti ambayo masikioni mwake ilikuwa kama saut ya mauti yenyewe.

Kwanini aendelee kusubiri? alijiuliza. Kwanini asubiri kifo cha mateso na kashfa? Akajiuliza kwanini asitangulie? Sasa macho yake yalikuwa yakitambaa kila mahali kutafuta silaha yoyote ambayo ingefaa kumtoa roho. Mara macho ya waridi yakatua kwenye ile chupa yenye pombe yenye sumu iliyoandaliwa kwa ajili ya Joram, bila kufikiri kwa mara ya pili aliiendea ile chupa yenye pombe akajimiminia tumboni mwake.

Mara Waridi akapata faraja kubwa ambayo ilimfanya asahau hofu na kudharau vitisho vyote vilivyokuwa mbele yake. Alijiona yu njiani hatua chache tu kufika katika milki mpya. Milki ambayo itampa uhuru kamili.

Furaha hiyo ikamuongoza Waridi, alitoka ndani ya chumba hicho na kuiendea lifti. Akatelemka hadi chini. Aliiacha hoteli na kuanza safari ya kuelekea kituo cha mabasi. Mavazi yake yakiwa kama yalivyokuwa, umbo lake likiwa kama lilivyo, na sura yake nzuri ikiwa imepambwa na tabasamu, viliyafanya macho ya wanaume kumtazama kwa mshangao wenye tamaa. Baadhi waliguna walipomuona, wawili walimkonyeza na mmoja alidiriki hata kumfuata. Wote
 
SEHEMU YA 36

walipata tuzo kwa tamaa zao. Tuzo ambalo lilikuwa tabasamu pana zaidi ambalo liliwafanya wabaki wameduwaa nyuma yake hoi bin taabani.

Waridi akaendelea na safari yake. Mwendo wake ukiwa nyongeza nyingine ya maneno kwa watazamaji. Akiwa kajaza nyuma, kakatika kati na kunyooka alivyonyokeana, ilikuwa kana kwamba hatembei bali anafanya maonyesho ya miondoko kama wanavyofanya warembo katika mashindano ya miss. Mwenyewe akiwa hana habari hizo, aliendelea na msafara wake hadi alipokifikia kituo na kujiunga na umati wa watu waliokuwa wakisubiri usafiri wa umma.

"Gari hii hapa dada", mtu mmoja alimwambia Waridi. Ilikuwa teksi. Waridi hakufanya hiana, akajitosa ndani ya teksi hiyo huku akisema. "Nipeleke Mburahati",

"Vizuri, lakini waonaje kama tukipitia hapa Embassy Hoteli tukapate walau bia mbili mbili baridi?", dereva alitupa ndoano yake.

"Samahani, leo nina haraka, nitafute siku nyingine".

"Kesho".

"Sawa..." waridi alilaghai. Rohoni akiamini kuwa kesho hatakuwa Dar es Salaam. Hatakuwepo hapa nchini, wala popote Afrika. Atakuwa nje. Nje ya dunia. Aliendelea kuwaza kwa furaha huku akimwitikia dereva huyo, "Ndio", kwa kila dereva huyo alilosema wakati hata hamsikii. Walipofika mbele yavijumba vayo, Waridi alimtaka dereva asimame. "Ni hapa, asante kaka", dereva hakuyaamini masikio yake, "Yaani uaishi hapa. Katika vijumba hivi? Na unaishi hapa dada?", dereva alishawishika kuuliza.

"Hapa ndio kwangu", Waridi alijibu wakati akitelemka kutoka ndani ya gari.

"Hapa?", dereva aliuliza tena kwa mshangao. Hakutia neno lingine. Badala yake aligeuza gari lake na kurudi alikotoka kwa mwendo wa kasi.

Walidi akapokelewa na wenzake waliojawa na mshangao. "Iwe", alisema mmoja wao. "Ulikuwa wapi".

"Na ilitokea nini hata ukaondoka bila kuaga?", alihiji mwingine. Maswali yalikuwa mengi mno. Waridi hakuwa na muda wa kuyajibu yote. Wala hakukumbuka ajibu maswali gani. Alichokumbuka ni jinsi alivyoingia chumbani kwake na kujilaza kitandani akisubiri kifo. Usingizi mzito ukamchukua.

Alipoamka ilikuwa usiku wa saa tatu. Chumba cha pili kitanda cha mwenzake kilikuwa kikilalamika kwa uzito wa viumbe waliokuwa wakikitumia. Naye
 
SEHEMU YA 37

alikuwa akigongewa mlango. Mteja akainuka na kumwendea. Alikuwa mtu mwenye umbo la mwili wa mtoto na uso wa mzee. Alikuwa na pesa zake mkononi tayari. "Leo sifanyi kazi", Waridi alimwambia mteja huyo na kufunga mlango wake. Hakujali malalamiko ya mteja huyo. Alikuja mwingine. Na mwingine tena. Wote Waridi aliwakatalia. Nao wakaondoka shingo upande.

Halafu akaja huyu mteja ambaye hakukubali kuondoka. Alikuwa kavaa kofia kubwa iliyofunika uso wake na koti kubwa lililofunika hadi miguuni. Aliingia kwa kujlazimisha na kufunga mlango nyuma yake huku akisema, "Lazima".

"Leo sitaki".

"Hata kwa bei kubwa?".

"Hata ukitoa milioni".

Mtu huyo alicheka kidogo. "Mimi wanitaka. Umekuwa ukinisumbua muda wote huu", Alitupa koti lake chini na kubaki katika suruali na shati. Akaivua kofia yake na kuitupa juu ya koti. Ni hapo Waridi alipomtambua. Macho yenye hofu kubwa yakamtoka.

"Bila shaka utakuwa umenikumbuka ", alisema polepole. "Unadhani nilikusudia ufe kistaarabu kwa ile sumu?, Ile ilikuwa maalumu kwa ajili ya Joram Kiango peke yake. Wewe ni mwovu mwenye dhambi nyingi. Unastahili kufa kishenzi".

Kabla Waridi hajafahamu kama ilimpasa kufanya nini, alijikuta tayari kadakwa ghafla kwa mkono kwa mkono wenye nguvu, ambao uliibana mikono yake yote miwili. Haraka kamba zikapita mikononi mwake. Alipotanabahi kupiga kelele, alijikuta katupiwa dude fulani kinywani ambalo lilimziba kinywa. Mara akatupwa chini na kudungwa sindano ambayo ilimlegeza hata asiweze kutapatapa.

Kisha kisu kikali kilichomolewa kutoka ubavuni na kuanza kupita juu ya mwili wake. Maumivu yalikuwa makali ajabu, lakini hakuwa na uwezo wa kulalamika. Alichoweza kufanya ni kuendeleo kukodoa macho yenye dalili zote za hofu na maumivu. Macho hayo yalishuhudia mikono yake ikikatwa mmoja baada ya mwingine na kuwekwa juu ya kitanda. Kisha tumbo la waridi likafumuliwa na utumbo kumiminika katika sinia lililokuwa mezani. Baada ya sekunde kadhaa alikuwa tayari amekata roho pindi kichwa chake kilipokatwa na kuwekwa juu ya debe, kando ya kitanda.

Baada ya kuridhika na kazi yake. Proper alizivua nguo zake zenye damu na kuzifunika katika mifuko ya koti lake ambalo alilivaa na kisha kutoroka zake
 
SEHEMU YA 38

nje polepole kama wateja wengine. Hapo nje aliwakuta wateja kadhaa ambao walisimama kwa namna ya mstari wakisubiri zamu zao. Akafanya haraka kuiendea sehemu aliyoficha gari yake.

Mteja aliyeingia baada ya Proper aliduwaa kwa kutokumuona Waridi. Kisha alishangaa kuiona mikono ya mwanamke huyo iliyolala peke yake juu ya kitanda. Halafu akakiona kichwa kilicholowa damu, kimelala chali. Hakuyaamini macho yake. Na ilipomtokea kuamini alihisi akili yake ikipaa. Alipiga kelele kwa nguvu na kuanza mbio akielekea barabarani, Alianguuka, akainuka na kuendelea kukimbia.

Mtewa mwingine alichungulia tu na kugeuka akianza safari ya kurudi zake alikotoka kimya kimya.


Ni mteja wa tatu aliyetoa taarifa kwa majirani na wenzake kuhusu kilichomtokea Waridi. Yeye pia alitoweka. Majirani walichanganyikiwa kwa muda mrefu. Mmoja wao alitapika. Wawili wakalia kwa nguvu. Umati mkubwa wa watu ulifika. Polisi pia hawakuchelewa.

"Umesema u nani wewe?".

"Naitwa Joram Kiango".

Inspekta Mkwaju Kombora hakuyaamini masikio yake. Jina la Joram Kiango lilikuwa maarufu kichwani mwake kama mbwa anavyoifahamu harufu ya chui. Mzee huyu alimfahamu vyema Joram. Yule kijana machachari aliyefanya mengi dhidi ya wahujumu uchumi na majasusi hatari ambao jeshi la polisi lilielekea kukata tamaa. Yule kijana nadhifu sana, mpole sana, mwenye nguvu na akili. Si huyu mzee aliyesimama mbele yake katika vazi la Kiarabu, akiwa amevaa kanzu nyeupe, kapiga kilemba, mwenye ndevu nyingi, uso uliofunikwa na miwani na mkononi kashika fimbo ambayo ilimsaidia katika mwendo wake wenye dalili zote za udhaifu wa kizee,

"Joram?", Inspekta Kombora akauliza tena.

"Naona huniamini kwa vile hujanifahamu Inspekita", ilisema sauti ambayo Kombora alielekea kuifahamu kwa mbali,lakini sura haikuwa ya Joram.

"Pengine niondoe miwani na haya madevu ya bandia ili uweze kunitambua". Madevu yakatolewa na miwani ikavuliwa, Uso ulisimama mbele yake ukitabasamu, Alikuwa ni Joram Kiango halisi ambaye Inspekta Kombora alimfahamu vyema.

"Nini sasa unafanya Joram?", alishangaa Inspekta Kombora. "Mchezo huu una lengo gani?".

"Siyo mchezo inspekta. Niko kazini. Unionavyo hapa mimi ni marehemu.
 
SEHEMU YA 39

wapo watu wameniua. Nataka niendelee kuwa marehemu ili...

Inspekta Kombora alimkatisha na kumwekea mkono begani huku akisema, "Sikia Joram. Kama ni mzaha subiri nitakapokuwa huru ndipo utakapoufanya tena mchezo wako, tucheke pamoja. Kwa sasa niko katika mkasa mzito ambao unaweza kuhatarisha usalama wa jiji endapo mtu huyo mwenye roho ya kinyama hatapatikana".

Habari hiyo ikamvutia Joram. "Mtu gani?", Joram alihoji mara moja.

"Hujasikia tu? Nadhani wewe hupitwi na neno".

"Kusikia?".

"Kuhusu msichana huyo aliyeuawa kikatili kuliko ilivyowahi kutokea. Polisi wamefanya kuokota viungo vyake kimoja baada ya kingine ndipo ukapatikana mwili mzima wa marehemu. Mtu aliyefanya mauaji hayo ni mnyama zaidi ya wanyama wengine wa kawaida. Mtu mwenye kumchinja msichana mrembo kama yule".

"Sijakupata Inspekta, yaani..." kisha Joram akapunguza kasi kuhoji kuhusu tukio hilo kwa kituo. Inspekta Kombora akamweleza yote kuhusu tukio zima lilivyotokea usiku huo huko Mburahati.

Hakukuwa na sababun za kuupeleka mwili huo hospitali", Inspekta Kombora aliongeza. "Viongo vyote vya marehemu vimeletwa hapa katika chumba cha maabara. Kama utapenda kutazama vitu vya kutisha unaweza kwenda maabara, inatisha sana".

"Nitapenda kumwona tafadhali".

Inspeta Kombora akaiacha ofisi yake na kumuongoza Joram kuelekea maabara ambako alifungua friji na kutoa kichwa cha msichana mrembo. Joram alikitambua kichwa hicho kuwa cha Waridi. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, alihisi machozi yakimdondoka. Aliyafukuza macho hayo kwa tabasamu huku akinong'ona kama mtu anayesali. "Ni Waridi! Mungu akurehemu. Naamini ni mapenzi yako kwangu ambayo yamekufanya ustahili adhabu hiyo ya kinyama. Naahidi nitakulipia kisasi".

Sala hiyo ilimfikia Inspekta Kombora. Akamgeukia Joram kwa mshangao na kusema, "Kumbe unamfahamu msichana huyu? Tafadhali turejee ofisini ili unisimulie kuhusu mkasa mzima ulivyotokea".

"Sijawa na cha kusimulia", Joram alijitetea. Hata hivyo alilazimika kusimsimulia Inspekta Kombora yote aliyoyajua. Alieleza jinsi alipomwona Waridi kwa mara ya kwanza pale baa akiwa ametegwa kwa sumu iliyokusudiwa kumwua yeye. Akaeleza pia yaliyotokea katika chumba ambacho waridi aliandaliwa kwa sumu ile ile ili amnyweshe Joram kwa hila.
 
SEHEMU YA 40

Ambacho Joram hakueleza ni jinsi alipofika hapo kabla ya wakati na kubahatisha, ingawa kwa taabu, kumwona mwuaji yule akitoa maelezo kwa Waridi. Hilo aliliacha ili apambane nalo binafsi. Hakupenda kuwaachia polisi ambao aliamini wangeweza kuharibu mapngo wake wa kumtia mikononi mwuaji.

"Ina maana binti huyu marehemu ndiye yule msichana aliyetoroka hospitali baada ya kuokotwa kando ya baa", Joram akatikisa kichwa kukubaliana na swali la Inspekta Kombora.

"Ndiye. Basi anastahili kifo cha aina hiyo. Kwa nini hakutoa taarifa polisi, tungeweza kumsaidia. Alishirikiana na wahalifu kuandaa njama za kufanya uhalifu".

"Inawezekana au isiwezekane", Joram alijibu kwa mkato. "Aweza kuwa alilazimika au kulazimishwa. La muhimu sasa ni kumpata huyo mwuaji".

"Ndio... apatikane haraka. Wewe humjui?".

Joram alikanusha. "Angalia bwana mdogo. Ninavyookufahamu mimi bila shaka wajua mwengi zaidi ya haya uliyonieleza. Nawe kama uonavyo hawa ni watu hatari kuliko unavyofikiri. Usiwachukulie mzaha, Ucheze nao kama ilivyo kawaida yako".

"Kawaida yangu sina mzaha wa mwuaji Inspekta", Joram alijibu. "Tena naamini kuwa nitawafikisha mikononi mwako mapema zaidi. Ninayo nafasi nzuri sana. Sasa hivi wao wanadhani kuwa nilikunywa ile dawa na sasa niko mahututi au marehemu tayari. Imani hiyo itawafanya wapate jeuri ya kuendelea na mipango yao kama walivyokusudia. Nataja kujua lengo lao, wanakusudia kufanya nini, na watu hawa ni akina nani, baada ya kufahamu hivyo nitawaleta mikononi mwako.

"Kazi hiyo ndiyo iliyonifanya nijibadili kuwa katika hali hii Inspekta. Nimeona nitoweke machoni mwao. Kusudi langu kwako ni kukuomba uitangazie dunia kuwa nimefariki ghafla. Nadhani watafurahi na kuendeleza mipango yao. Ndipo nitakapofufuka na kuwashangaza kwa kuwatia mikononi.

Walijadiliana kwa muda ofisini. Kombora akawa ameafikiana kwa taabu sana na Joram. Nia ya Joram ilikuwa awaachie polisi kufanya kazi yao kwa makini. Lakini maelezo ya Joram yalimtua Inspekta Kombora hata akakubali japo kwa shingo upande. "Kumbuka ninavunja sheria zote za kushiriki katika uongo mkubwa kama huu. Hivyo. usiniangushe kwa kushindwa kutimiza ahadi yako
 
SEHEMU YA 41
ya kuwatia watu hawa mikononi mwa sheria", Inspekta Kombora alimwambia Joram.

"Wanifahamu vizuri Inspekta. nakuhakikishia kuwa Siwezi kushindwa kamwe", Joram alimjibu akiweka vyema ndevu zake za bandia na kuvaa miwani yake. Akautwaa mkongojo wake na kuiacha ofisi ya Inspekta Kombora kwa mwendo ambao ulimfanya Inspekta huyo ambaye hucheka kwa nadra sana aangue kicheko kipana.

Usiku huo taarifa ya habari ya Radio Tanzania Dar es Salaam ilibeba habari ambazo ziliwashitua wasikilizaji wengi kote nchini.

"...Joram Kiango yule mpelelezi mashuhuri wa kujitegemea amefariki ghafla akiwa nyumbani kwake kwa maladhi ambayo bado hayajathibitishwa. Madaktari wanaendelea na uchunguzi watatoa taarifa za kifo hicho hivi karibuni baada ya uchunguzi,,,"

Haikuwa habari njema hata kidogo. Wala hakuna aliyetarajia kuisikia. Kila aliyemfahamu Joram alitegemea kuwa kijana huyo angeuawa au kufa kwa risasi au madhara mengine kutoka kwa adui zake. Kufa kwa maradhi! haiwezekani!.

Taarifa za habari za sauti ya Kenya na Ujerumani ziliidaka habari hiyo haraka na kuitagaza kwa mapana zaidi... "Yule kijana machachari"... Walisema wakenya, "The Iron boy..." walimwita hivyo wajerumani... "Amefariki leo ghafla. Yawezekana na njama za wahujumu ambao walimuogopa sana kijana huyu kama moto".

Ndipo watu walipolazimika kuamini. Wengi walisikitishwa na kifo hiki. Wengine walitoa machozi. lakini Wachache walishangilia.


Nyumba hii iliyobomolewa kwa bomu ilikuwa katika mtaa wa Manda Magomeni Mikumi. Ilikuwa nyumba ambayo kwa muda mrefu haikutumiwa kutokana na kutokamilika kwake tu. Joram alikuwa ameichagua nyumba hii kwa ajili ya kujificha baada ya kuitazama mara kwa mara kila alipopita katika mtaa huu na kuona ilivyokaa vizuri kwa siri. Ilikuwa imezungukwa na kichaka cha miti ambayo awali ilikusudiwa kuwa bustani. Haikuwa rahisi kwa mtu wa nyumba jirani kufahamu yanayotokea katika nyumba hii kwa jinsi zilivyotengana.

Zaidi, ilikuwa na njia nyingine ya uwani ambayo ilipitia katika uchochoro hadi mitaa ya nje kabisa. Kuhamia hapa ilikuwa siri yake binafsi ingawa Inspekta Kombara alimsihi sana amfahamishe wapi amejificha, Alikuwa amehamia
 
SEHEMU YA 42

hapa usiku wa manane baada ya kujipitishapitisha ili kuhakikisha kuwa hafuatwi au kuonekana na mtu. Mzigo wake pekee ulikuwa ni Suitcase yake ambayo ilichukuwa vifaa vyake muhimu ikiwa pamoja na silaha ndogo,

Usiku huo wa kwanza alilala vyema. Alfajiri aliamka na kujiandaa kwa kuvua ujana na kuvaa uzee. Baada ya kukamilisha taratibu za uzee alilificha vizuri begi lake na kutoka hadi polisi ambako alikamilisha mipango yake na kurejea mafichoni akisubiri muda alioupanga ili aanze harakati zake.

Joram alikuwa na hakika kuwa kazi hii isingemchukua muda kuimaliza. Jambo lililomtia matumaini ni kule kujua kuwa adui zake walikuwa wakisubiri kifo chake ili waanze shughuli zao. Kadharika, mmoja kati ya adui hawa hakuwa mgeni kwake. Alichungulia alipokuwa akitoa amri kwa marehemu Waridi na kuipata picha yake. Insingemchukua muda mrefu kumfahamu kikailifu.

Kitu kimoja Joram hakujua. Hakujua kuwa makazi haya ya siri aiyohamia hayakuwa yake binafsi. Yalikuwa malazi ya Luta Magambe, mmoja kati ya mamia ya vijana wazurulao katika Jiji la Dar es Salaam. Luta alikuwa ameingia Jijini miaka zaidi ya kumi iliyopita, akitokea kwao kijijini katika moja wapo ya Wilaya za mkoa wa Kagera. Alikuja Dar es Salaam kwa nia njema ya kutafuta kazi baada ya elimu yake ya msingi. Jiji likamlaki kijeuri kama linavyowalaki wote. Kazi haikupatikana kwani hakuwa na mtu wa kumfanyia "mpango" wala pesa za "motisha".

Akaambulia kuangukia katika vibarua vya kutwa. Pesa alizopata zikawa ndogo mno kulingana na mahitaji ya Jiji. Kila siku akawa mtu wa "Kuchacha". Hilo likamtuma kutumia muda wake wa ziada kuwachomolea wasafiri wa Uda na Daladala. Tabia hiyo haikuchelewa kumfikisha Keko akiwa na majeraha mengi usoni. Alipotoka Keko hakuwa luta mwenye nia njema tena, bali mtu ambaye yuko tayari kufanya lolote mradi apate chochote.

Msimamo huo mpya ulimanya apoteze chumba na kukosa marafiki wa haja. Rafiki zake pekee walikuwa wahuni wenzake na walikutania "kazini". Baada ya "kazi' kila mmoja alijua lake.
 
SEHEMU YA 43


Siku alizopata, alistarehe kwa kulewa, kujipatia wasichana wazuri na kulala vizuri katika majumba ya wageni ama kwenye nyumba za wasichana hao. Alipokosa alijutia na kujisahaurisha kwa kuvuta bhandi na kujilaza katika jumba hilo bovu.

Hivyo kwenye alfajiri hiyo aliona kama mwujiza kuona 'mzee' huyu mwenye dalili ya pesa na sura ya Kialhaji akitokea ndani ya moja ya vyumba vya jumba hili akiitumia njia yake ya siri! Mara moja wazo likamjia Luta?. Kwamba mzee huyu alikuja katika ghofu hili kwa sababu maalumu. Sababu ambayo Luta aliamini kuwa haikuwa nyingine zadi ya kuficha pesa au vitu vya thamani, Wazo hilo likamtuma kuanza upekuzi akitafuta chochote ambacho mzee huyo alikificha. Hakupata kitu. Hata hivyo alikuwa bado akiendelea na upekuzi wake 'mzee' aliporejea. Hima akajipenyeza katika chumba cha pili ambamo alijificha vizuri. Joram hakumuona. Darubini ya adui yake Joram kutoka nyumba ya pili pia haikuweza kumuona. Alitulia akimchungulia Joram ambaye aliketi akifanya mambo yake.

Kisha Bagambe alimuona mtu mwigine akinyatia nyumba hii mkononi kashika vitu ambavyo alivificha kwa hadhari chini ya mlango, Baada ya mtu huyo kushika hapa na pale aliondoka eneo hilo kwa hadhari na ukimya ule ule.

Kitu gani kitatokea?, Bagambe alijiuliza, Hakika moja alikuwa nayo. kuwa hii ilikuwa nafasi yake pekee ya 'kuukata'. Kwamba leo lazima ungekuwa mwisho wake wa maisha ya kubahatisha na mwanzo wa maisha mapya. Ingekuwaje vngine na eti bahati zinamfuata hadi huku badala ya yeye kuzifuata kwenye vituo vya basi? Hakuona sababu ya kuendelea kusubiri.

Kwa hadhari mfano wa paka anayemnyemelea panya, aliiendea sehemu hiyo aliyoona kitu kikifichwa. alipofika alipekua taratibu. Kisha aligusa waya fulani ambao hakutarajia kuuona hapo. Aliutazama waya huo kwa mshangao. Mshangao ambao ulikatizwa na mlipuko mkali uliomfanya apae juu na kutua chini akiwa tayari ametawanyika vipande mfano wa nyama za kopo, zinazoandaliwa kwa ajili ya kusindikwa.

****************************

Mlipiko huo ulimkuta Joram Kiango akiwa amesimama wima, fimbo mkononi. Aliduwaa alipoona ghafla mtu akizuka mbele yake na kupaa angani
 
SEHEMU YA 44

ambako alitawanyika vipande vipande. Lakini hakupata muda wa kuendelea kuduwaa, kwani wakati huo huo kila kitu kilikuwa kikipaa na kutua huku na huko kwa kishindo cha kutisha.

Kila kitu pamoja na Joram mwenyewe. Alijikuta angani kisha akajibwaga chini akifuatwa na lundo kubwa la vitu vizito ambavyo vilimfunika juu.

Joram hakuwa na muda wa kusikia maumivu pia. Alihisi kama mtu aliyepoteza kichwa au ubongo. Fahamu zikamtoka na nafsi yake kuchukuliwa na kiza kinachotisha.


******************************

Kifo cha kusikitisha! Joram aliwaza hivyo, karibu kila mtu kati ya umati mkubwa uliosimama kando kuizingira nyumba hiyo. Macho yenye hofu na huzuni yalikuwa yakiwatazama askari ambao walikuwa wakiviokota viungo vya marehemu kimoja baada ya kingine na kuvitia katika sanduku. Ni watu wachache sana walioweza kutazama tukio hili kwa muda mrefu. Wengi walitupa jicho kwa sekunde kadhaa na kisha kugeuza nyuso zao upande mwingine huku wakiguna na kufuta machozi. Mama mmoja alisikika akilia kwa sauti.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa wengi wao kushuhudia tukio la mtu aliyepoteza maisha kwa njia hii ya kutisha.

Miongoni mwa walioshuhudia tukio hilo alikuwwepo Jodor Proper. Alikuwa mmoja wa watu waliofika mapema katika eneo hilo. Lakini alimkuta mtu wake aliyetega bomu hilo akijifuta vumbi baada ya ule mweleka alioupata kutokana na tofali lililomponda kichwani. Yeye alikuwa mmoja kati ya 'wapita njia' wanne waliojeruhiwa katika ajali hii. Proper alimsaidia mtu huyu kama asiyemfahamu. Walipopata mwanya walinong'onezana: "Kazi nzuri sana, Sasa nenda zako..."

Mtu huyo alipoondoka. Proper aliendelea kutazama 'ajali' huku akijitia kunung'unika. Lakini ndani ya moyo wake alikuwa akisherehekea na kushangilia sana tukio hilo. 'Kifo kinachomstahili kabisa' Aliwaza kwa furaha. "Mnofu mmoja mmoja! Na ajiunge basi tuuone huo ushujaa wake".

Wazo la kwamba huenda huyu akawa si adui yake mkubwa Joram Kiango halikumjia akilini. Ingawa haikuwa njia rahisi ya kuthibitisha mabaki hayo ya marehemu, lakini katika uchunguzi wake Proper alifanikiwa kuiona ile fimbo
 
SEHEMU YA 45
ya Joram na madevu yake ya bandia ambayo yaliokotwa na askari mmoja na kumwonyesha Inspekta wao ambaye alibabaika kama mtu aliyeguswa na simba. Kitendo hicho kilimfanya Proper ajisikie kucheka huku akijituliza. Wangetangaza nini tena wakati dunia nzima imefahamishwa zamani kuwa Joram Kiago amefariki dunia?.

Proper alipotoka katika eneo hilo kwa tabasamu, alikuwa na wazo moja tu la kuendelea na mipango yao bila kuwa na hofu yoyote. Kikwazo pekee alichoogopa yaani Joram Kiango kilikuwa tayari kimeingia kuzimu, kikiwasalimia babu zake huko.

Mmoja wa maofisa wa polisi alipendekeza wafanye uchunguzi wa kina ili kuhakiki kama eneo hili lilikuwa na maiti ama mareruhi wengine zaidi waliokandamizwa na kifusi. Lakini majirani wa eneo hilo waliwahakikishia polisi kuwa nyumba hiyo haikuwa na watu. Wakaondoka haraka haraka kwani kazi ya kufukua vifudi ilikuwa nzito, ambayo hakika ingewatoa jasho. Wakaondoka na mwili wa marehemu wakiuacha umati wa watu ukiendelea kufika katika eneo hilo kutazama kilichotokea.

Usiku ulipoingia, giza liliwaondoa watu katika eneo hilo likabaki katika hali yake ya kawaida.


Unono, huyu alikuwa mwanamke wa makamo, mfupi kiasi, mnene wa kutosha, mweusi kupindukia, mama huyu alikuwa mmoja kati ya watu wengi walioshuhudia ajali hii ya mtu kuuawa kwa bomu. Mama huyu alikuwa miongoni mwa umati huo, kama wananchi wengine alisema hili na kusikiliza lile, macho yake yakifanya kazi ya kutazama kwa hofu tukio hilo pamoja na polisi kadhaa, ambao walikuwa katika pilika pilika za kukusanya mabaki ya marehemu huyo.

Kichwani Unono alikuwa na mawazo tofauti, nje kabisa ya tukio la msiba huo uliotokea eneo hilo. Alikuwa na mawazo mchanganyiko wa matatizo ya kiuchumi na mapenzi. Mama huyu alihisi kuwa sehemu hiyo ingeweza kumfanya apate ufumbuzi wa tatizo lake moja ama yote mawili yanayomtatiza.

"Usiku..." aliwaza moyoni mwake.

Kimaumbile, Unono hakuwa na umbo la kuridhisha wala hakuwahi kujidanganya kuwa ana sura nzuri. Ukweli huo alikuwa ameubaini tangu enzi za usichana wake alipojiona akikua miongoni mwa vijana wa kiume ambao

ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 46


walionekana kumwepuka kama jini na kumtazama kama jinamizi. Wakati huo huo aliambulia kuwaona wenzake wakifuatwa na vijana wa kiume na kubembelezwa kama malaika, wakipewa lugha tamu na matendo ya kimapenzi. Ndipo alipoanza kujitathimini katika kioo.

Akagundua kuwa pamoja na kuwa na sura mbaya, Alitisha na kuchukiza kwa jinsi alivyojengeka kama kilema ingawa hakuwa na kasoro yoyote kimaumbile. Hivyo maisha yake yaliyofuata aliishi akifahamu kabisa kuwa tunu ya kuzaliwa mwanamke yeye isingemsaidia kama wanawake wengine. Aliamini kuwa katika maisha yake lazima atoe jasho ili aweze kuishi.

Jasho lake alilitoa kwenye vilabu akiwauzia wanywaji makongoro ya ng'ombe ambayo aliyanunua machinjioni na kuyachemsha kwa maji na chumvi. Sura yake haikumtendea wema katika biashara yake. Mwanamke huyo aliyekuwa na tama zote za kike, alipata mume wa kufariji kwa kwa bahati. Na alipompata, ilikuwa mhali mwanaume huyo kumrudia. Naye Unono hilo halikumshangaza kamwe kwani hilo lilikuwa jambo la kawaida katika maisha yake. Hayo yalimtokea kwa nadra sana. Hivyo siku nyingi Unono alikuwa mhitaji. Ndipo akabuni mbinu za kutembea sehemu fulani fulani usiku, sehemu ambazo alikuwa na matumaoni ya kukutana na wanaume ambao nafsi na hali zisingewaruhusu kuchunguza. Walevi wachelewao kurejea majumbani kwao usiku, wazururaji wasio na makazi maalumu, na walinzi wanaokesha wakilinda nje usiku, hawa ni miongoni mwa wateja ambao Unono aliwahi kuwapata ili kutimiza haja zake. Baadhi waliwahi hata kumpatia pesa.

Kwa hivyo Unono akakusudia kujaribu bahati yake kwenye eneo hili lililolipuliwa na bomu. Hangekosa kufua dafu pale. Askari mmoja ama wawili wasingekosa kuwekwa hapa kwa ajili ya kulinda mazingira. mmoja wao asingekosa kumtupia maneno iwapo angecheza vema karata yake. Na hata wawe wote wawili angebabaishwa na nini angestahimili. Eti kakosa mapenzi ya mume kwa muda mrefu sasa. Ni mawazo hayo yaliyomfanya Unono afunge biashara mapema na kurejea nyumbani. Aliogaa, akajipaka mafuta yake yenye harufu nzuri, mafuta ambayo aliyanunua kwa shingo upande. Alivaa baibui lake jeusi bila vazi lingine lolote mwilini.
 
Back
Top Bottom