SEHEMU YA 62 & 63
"Wanajisumbua, hakuna watakalogundua kuhusu kifo cha Joram", Mwenyekiti aliwajibu. Kisha alicheka kidogo na kusema, "Pia napenda kutumia fursa hii kuwafahamisha kuwa Joram hakufa kwa sumu. Walipanga hila ili watulaghai tu baada ya kunusurika kwake. Nililazimika kumteketeza kwa bomu".
Hii ilikuwa taarifa ngeni kwa wajumbe. "Si lazima watazidisha mashaka? Nazungumzia polisi. Walipoona amepona kufa kwa sumu na hatimaye kuuawa kwa bomu nadhani watakuwa macho sana, wakipeleleza kwa makini zaidi hadi..." akasita kidogo baada ya kuona ameongea muda mrefu zaidi ya anavyotakiwa kuongea.
"Hadi nini?", Mwenyekiti alihoji. "Hakuna lolote watakalogundua. Watakuwa wakibabaika tu kama mfamaji asiye na msaada wowote. Hawatafahamu iwapo ubaya utatoka mashariki au magharibi. Hawatajua ni kitu gani kinatokea. Watakapofahamu, mambo yatakuwa yamekamilika. Watakachofanya ni kuteremsha bendera zote nusu mlingoti na kuanza maomboleza ambayo hayajawahi kutokea katika historia ya dunia.
Wajumbe waliduwaa. Mioyo yao ikadunda kwa hofu. Ingawaje walikuwepo mkutanoni kama washiriki kamili katika njama hii, lakini hawakuelewa barabara kilichokusudiwa. Tamaa ya pesa nyingi zaidi, madaraka makubwa zaidi, ndio sababu zilizowafanya wakubali kushiriki katika mkutano huo wa siri. Lakini hayo hayakuwafanya watokwe na mashaka. Hawakujua kama mambo yalikuwa heri kama alivyodai Mwenyekiti wao au shari kama miayo yao ilivyokuwa ikinong'ona. Hasa mashaka hayo yalitokana na kuteuliwa kwao. Hakuna mjumbe aliyefahamu wajibu wake. Hakuna aliyekuwa na fununu sababu ya kuteuliwa kuhusika katika mkutano huo. Ni kweli kwamba wajumbe hao walikuwa watu wenye nafasi nyeti katika chama na serikali. Ni kweli pia wote walikuwa pamoja kwa nafsi zao: wote wangependa cheo zaidi na pesa. Lakini umoja huo haukuwafanya washindwe kujiuliza vipi mtu huyu anayejificha nyuma ya mwanga, mbele yao aliwezaje kuisoma mioyo yao, hata akawateua katika jumuia hii. Vipi aliweza, japo katika nchi na ulimwengu mzima? Watu wenye njaa kama zao ni wengi mno, endapo si wengi. Sheria na katiba zisingekuwepo, kulinda haki na usawa, ingethihirika ni jinsi gani wengi walivyo na tamaa ya madaraka na kiu ya kupata pesa.
Ingawa kuna sheria zinazotisha, pamoja na katiba zinazoadili, wengi huzikiuka kwa siri na kulinda nafasi ya kufanya mengi kinyume cha mwelekeo. Wako wachache walio 'jaaliwa' wakafaulu kufanya mengi kwa siri wakati wao ndio wanaongoza kulinda katiba na sheria za nchi. Baadhi ya watu hao ni hawa ambao sasa hivi walikuwa mbele ya Proper wakimsikiliza kwa hofu. Walikuwa na mengi ambayo waliamini ni siri zao binafsi, ambayo hawakupenda jamii ifahamu. Hata hivyo tamaa yao haikuwa kubwa kiasi cha kuwafanya wafurahie jambo la kutisha wasilolifahamu eti kwa ahadi ya pesa na vyeo zaidi.
"Unakusudia kufanya nini?", mmoja wa wajumbe alifoka ghafla.
"Ndiyo... Tufahamishe ni jambo gani unataka kufanya?", mwingine alidakia na kuuliza.
Proper kama mtu aliyekuwa akiyasoma mawazo yao kitambo, alicheka kidogo, kisha akawaambia. "Sikilizeni. Kazi iliyo mbele yenu ni ndogo kuliko kazi zote mlizowahi kufanya... Hamna haja ya kuwa na hofu yoyote".
Alipoona wametulia kumsikiliza aliendelea, "Nimepata fununu kuwa hivi karibuni utafanyika mkutano wa viongozi kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanaojiita wenye msimamo wa kimapinduzi wamealikwa pia. Nitakachohitaji kwenu ni ratiba kamili ya mkutano huo, wapi kiongozi fulani analala, wapi anakula, jumba lipi wanakutana na kadhalika. Nataka taarifa kamili, ya siri, si ile ambayo hutangazwa katika magazeti yanayouzwa mitaani. Kulingana na nafasi zenu najua kazi hiyo ni ndogo mno. Kitakachofauata niachieni mimi.
"Nini kitafuata?", mjumbe mmoja aliropoka kwa shauku.
"Mara ngapi nimewaambia kuwa bendera kadhaa zitapepea nusu mlingoti kwa siku kadhaa katika nchi kadhaa wa kadha?. Nataka kufanya jambo fulani ambalo halijawahi kutokea sasa kifanyike. Kitu ambacho bado hakijafikirika. Kitu ambacho historia haitakisahau. Kwa muda mrefu amekufa kiogozi mmoja. Safari hii nataka kuona viogozi wengi wamekufa wote kwa wakati mmoja. Tena nitafarijika kama watakufa pamoja katika viti na meza zao. Huenda wataanguka mmoja baada ya mwingine, wakati wakiagana. Ama kweli litakuwa jambo la kusisimua sana..."
"Kusisimua!" Mmoja wa wajumbe aliropoka na kufoka baada ya kupatwa na mshangao. ""Kusisimua!", alirudia tena, "Sikuwa na hakika. Sasa nimeamini kuwa una wazimu. Hata hivyo, wazimu wako unakudanyanya sana kukutuma udhani kuwa mimi naweza kushiriki kuinua mikono yangu katika kuwaangamiza watu ambao licha ya kwamba, hawana hatia, wanajitesa kutwa kucha kuwasaidia wanyonge wanaonyimwa haki zao?".
Mjumbe huyo ambaye sasa alikuwa amesimama wima, akitetemeka kwa hasira huku akitokwa na jasho aliwatazama wajumbe wenzake. Alipoona wote wana dalili ya kumuunga mkono aliongeza. "Huna budi kulionea aibu wazo lako la kipumbavu..."
"Keti", Proper alimwamru. "Hujui unalosema. Maneno yako yamejaa ndoto au nyimbo ambazo hao unaowaita viongozi, sijui watetezi wa wanyonge gani, wamekuwa wakizijaza katika vichwa vyenu. Nani anayemtetea nani katika dunia hii? Mnyonge hujitetea mwenyewe. wale wanachofanya ni kutetea matumbo yao. maisha na vyeo vyao tu kwa visingizio vingi. Wamehitimu katika taaluma ya kusema maneno mazuri na kutoa ahadi tamu katika masikio ya wanyonge kiasi cha kuwafanya waonekane kama miungu ambayo wanadamu wanaitegemea!",
"Hata hivyo", mjumbe huyo alidakia, "Siwezi kushiriki upumbavu kuangamiza damu za watu wasiokuwa na hatia".
"Bado hujajua usemalo", Proper alimjibu kwa mara nyingine. "Naweza kuwa mwema kukukaribisha katika mpango huu ambao utasaidia kuyabadili maisha yenu kuwa ya heti na utajiri mkubwa. Lakini siwezi kuwa mpole kiasi hicho kiasi cha kuacha mpango huu ambao nimeuandaa kwa miaka mingi uharibike kwa ajili ya woga na ujinga wa yeyote kati yenu. Nadhani sasa nimeeleweka?".
Proper akanyamaza kidogo ili kutoa nafasi kwa wajumbe waweze kuyatafakari maneno yake.
Ulikuwa ujumbe wa kutisha kwa wajumbe walioshiriki mkutano huo, Kilichofuata yalikuwa maafa na ukatili mkubwa kwao au yeyote ambaye angethubutu kukanusha au kutoa siri hii. Ukweli huo uliwatia hofu wajumbe hata wakatazamana kwa dalili ya kukata tamaa ya maisha.
Kama anayesoma mawazo yao. Proper akarudia kuongea kwa sauti ile ile ambayo japokuwa haikuwa kali, wala yenye hasira, lakini sauti hiyo iliubeba ujumbe kamili, alieleza jinsi alivyodhamilia kutenda yote aliyosema. "Najua kwamba majalada yenu kazini hayaonyeshi doa lolote, Na raia wengi nchini wanayo picha nzuri juu yenu. Picha iliyowawezesha mkachaguliwa kushika nyadhifa katika sehemu mbali mvali muhimu za uongozi. Lakini kuna upande wa pili wa picha hizo. Upande wenye kila aina ya uovu, ukatili, na kukiuka taratibu za nchi. Nyie mnadhani upande huo wa pili ni siri zenu binafsi ambazo hakuna anayefahamu. Kwa bahati mbaya au nzuri, mimi nafahamu kila jambo. Namfahamu kila mmoja wenu vilivyo. Pia ninao ushahidi mzuri ambao ukiwekwa hadharani utayafanya majina yenu yanuke kama takataka".
ITAENDELEA