SEHEMU YA MWISHO
COUNT-DOWN PART 24
Chombo kilizimwa na kurejeshwa katika hifadhi yake. Msemaji alikuwa akifikiri kwa muda. Kigogo mikono yake ilikuwa ikitetemeka. Sio kazi rahisi, kupewa jukumu la kuua. Hasa kumuua mtu hatari ambaye yu macho zaidi ya Simba aliyejeruhiwa. Isitoshe, mtu huyo akiwa rafiki mkubwa, kama ndugu umpendae, mtu uliyeshirikiana pamoja katika maovu na unyama wa kila aina. Mtu kama huyo, kumwelekezea bastola na kumuua, kwa kuwa tu karopoka na kuamua jambo ambalo wakuu hawajaliamua! Aibu ilioje!.
Kwa hivyo, aliposikia habari ya kutorokea Mwanza kwa mwenzake, aliona kama bahati njema imemwangukia. Iwapo huyu aliyeamuriwa kumuua ametorokea huko na kuvuka mpaka, hatabeba jukumu la kumuua tena. Jukumu hili litawahusu wengine walioko huko aendako. Lakini mara wapelelezi wakaleta habari kwamba amerejea na yuko Arusha tayari kwa kusudio lake la kikatili. Ndipo alipowaarifu wakubwa. Nao wakamwamru kumuua. Hakuwa na la kufanya zaidi ya kutekeleza amri. Akainua simu na kuzungusha namba fulani. Ilipopokelewa aliuliza, "Mmempata alipo?".
"Bado, mzee..."
"Bado! Kwa nini?" alifoka.
"Ametoweka kidogo. Nadhani amejibadili tena. Unajua anavyoipenda tabia ya kinyonga. Mara ya mwisho tulimpata alipokuwa kajifanya chongo na mguu mbovu. Sasa haonekani. Bila shaka ame..."
"Hata kama atajigeuza kinyonga kabisa, lazima apatikane haraka, sawa?".
"Sawa mzee".
"Na mara mtakapomuona niiteni mara moja. Sawa?".
"Sawa".
"Au hamuifahamu adhabu ya kushindwa kutimiza wajibu?" Alikata simu na kuliendea kasha lake la silaha. Akachunguza silaha mbalimbali zilizokuwemo; bastola aina aina, viwambo vya kuzuia sauti na mabomu kadhaa. Akaviweka katika mifuko yake ya siri.
Kisha aliiunua simu na kulipigia shirika moja la ndege za kukodi.
"Tafadhali andaa ndege itakayonifikisha Arusha mara moja", aliagiza.
"Umepata", alijibiwa. "Ungependa kuanza safari ya kuondoka saa ngapi?".
**************************
II
"Inspekta Kombora hapa naongea kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi..."
"Ndiyo, afande".
"Nifahamishe, taarifa bado ni ile ile hakuna fununu yoyote ya yule mwenda wazimu Proper?"