Simulizi ya Kijasusi: Salamu Kutoka Kuzimu

Simulizi ya Kijasusi: Salamu Kutoka Kuzimu

SEHEMU YA MWISHO

COUNT-DOWN PART 5


nilikatwa uume wangu. Nataka ujuwe mimi ni nani".

Nuru akabaki ameduwaa. Alitamani kupiga kelele lakini sauti ilikuwa kama iliyouhama mwili wake.

"Vua nguo zako zote".

Bado Nuru alikuwa ameduwaa.

"Nasema vua nguo zako. Au utapenda nizivue mimi? Usitegemee kuvuliwa nguo kistaarabu", Proper alisema akimsogelea Nuru pole pole. Macho yake yalidhihirisha kila dalili ya unyama na yalimfanya Nuru ashikwe na hofu kubwa hivyo akabaki amekodoa macho.

"Utavua au nikuvue?" Proper alihoji tena mikono yake ikiliendea koo la Nuru na kuanza kuliminya.

"Hatazivua na wala hatavua nguo", ilisema sauti nyepesi kutoka nyuma yao. Wote wakagauka kutazama. Msemaji alikuwa akitokea bafuni, akawasogelea taratibu sigala ikiwa mkono mmoja, bastola mkono wa pili. Aliwaangalia akitabasamu.

"Heko Bi. Nuru, U msichana shujaa kuliko nilivyotegemea. Umenifurahisha sana kwa kutobabaishwa kwako na huyu mwehu. Poa moyo. Hataweza kufanya lolote la kinyama tena kwako".

Sauti haikuwa ngeni masikioni mwa Nuru. Ilikuwa sauti ambayo aliizowea sana. Sauti ambayo aliondokea kuihusudu hata akaipenda. Lakini sura na umbile lilikuwa la mtu mwingine asiyemfahamu kabisa. Umbo zuri lenye dalili zote za afya na sura ya kuvutia yenye kila dalili ya ushujaa. Sura ambayo ilioana sana na sauti yake. Kwa Nuru hii ilikuwa enzi yake ya miujiza. Hivyo, kwa kuzingatia alivyoifahamu sauti hiyo alisema pole pole, "Wewe ni Duncan".

Mgeni huyo akacheka. U msichana shujaa na mwenye hekima sana. Umewezaje kunifahamu kwa urahisi kiasi hicho? Kisha akamgeukia Proper na kusema: "Hata hivyo rafiki yangu huyu ananifahamu kwa jina lingine kabisa. Nililazimika kujigeuza sura na umbile kuwa Duncan ili kumthibitishia jamaa huyu kuwa utaalamu wa binadamu kujibadili si jambo geni katika nchi hii. Kila mtu anaweza. Au sivyo Proper, ambaye wakati mwingine ulijiita Profesa Kimara".

Proper alijikuta katika wakati mgumu mno katika maisha yake. Mshangao aliokuwa nao ulikuwa mkubwa kiasi cha kutawala hofu na hasira ambayo ilikuwa imeanza kujitokeza. Proper hakupenda kuyaamini macho yake, kuwa
 
SEHEMU YA MWISHO

COUNT-DOWN PART 4


kijana huyo mwenye bastola mkononi, mwenye tabasamu la dhihaka usoni, alikuwa Joram Kiango mtu ambaye aliamini kuwa alikufa kitambo. Hivyo, aliondoa mikono yake kutoka shingoni mwa Nuru na kukirudia kiti chake alichokuwa amekalia.

"Haiwezekani. Huwezi kuwa Joram. Yeye alikufa kitambo kwa mkono wangu".

"Alaa! Basi lazima ukubali kuwa amerudi kutoka kuzimu ili akupe salamu zako kutoka huko".

Proper hakujibu. Wala hakuwa mtu wa kupoteza muda kuwaza kitu kimemfanya Joram kuwa hai hadi sasa. Bila shaka lilifanyika kosa fulani katika mauaji yale ya bomu. Na ni kosa hilo ambalo limempa Joram fursa ya kumshinda na kuharibu mipango yake yote kwa kufikiriwa kuwa hayuko tena duniani. Kwa kadri anavyomfahamu, ni yeye aliyekuwa ameingilia kati baini yake Nuru. Ni yeye aliyefanikiwa kuiba ile poda yake ya sumu na kuweka hii ya kawaida. Huo ndio mtindo wake. Kuharibu mipango madhubuti kwa namna ya dhihaka, kama mzaha. Hasira aliyokuwa nayo Proper kwa Nuru zikamgeukia Joram. Alitamani ainuke na kumrukia. Amuue kinyama kuliko historia ya mauaji ya kinyama duniani inavyoweza kukadiriwa. Amtafune mzima mzima! Alisita kwa kuiona bastola ya Joram ikimchungulia usoni.

Joram alikuwa akiyasoma mawazo ya Proper. Akacheka kidogo kabla hajasema.

"Ndiyo. Nililazimika kufuata mtindo wako wa uoga, kujificha katika sura za bandia ili niweze kupambana nawe vizuri. Dawa ya moto ni moto. Hata hivyo sina budi kukiri kuwa karibu nikate tamaa baada ya kuona siku zinakwisha kabla hujajitokeza kuanza harakati zako za kinyama. Kidogo nihadaike kama Inspekta Kombora na wasaidizi wake kuwa umekimbilia nje ya nchi. Hata hivyo sikukata tamaa. Niliijua njia ambayo ungeitumia kujaribu kuwaua viongozi kama wale ingekuwa kwa sumu ile ile ambayo ulithubutu kuitumia kwangu ukashindwa, lakini ukafaulu kumuua mpenzi Neema", Joram alinyamaza kidogo kwa huzuni, akakumbuka jinsi Neema alivyokubali kuyapoteza maisha yake kwa ajili yake. "Ndiyo, ulimuua Neema pamoja na watu wengi wasio na hatia", alieleza Joram.
 
SEHEMU YA MWISHO

COUNT-DOWN PART 3



Akaeleza jinsi alivyolazimika kukaa hotelini, akajifanya mtoto wa tajiri aliyeko Ulaya na kuzungumza na kila mtu, ingawa alizungumza mambo ya kawaida tu bila kutia dalili za upelelezi, lakini alikuwa kazini akimchunguza kila mfanyakazi. Akitazama kwa makini nani angekuwa na dalili yoyote ya kukutana na mtu mwenye tabia za Proper. Hasa nilitegemea kuwa ungewatumia wasichana wazuri", alisita kidogo kisha akaendea. "Na kwa kuwa Maunt Meru hakukuwa na msichana mzuri zaidi ya dada yangu Nuru, ilinibidi nimtazame yeye kwa makini zaidi. Kidogo nikate tamaa hadi jana nilipomuoa Nuru akiwa katika hali isiyokuwa ya kawaida nikapata matumaini. Kisha nikakiona kidani ambacho ulimpa kama zawadi. Kidani ambacho kina mitambo ya kunasa sauti na kuisafirisha hadi ulipo. Nia yako ilikuwa kusikiliza anazungumza nini na akina nani. Hivyo nilipomshawishi akivue na kumhoji mengi bila ya yeye kujua uliamua kumtisha. Msaada ulionipa haukuwa mdogo. Uliniwezesha kuwa mmoja wenu katika mkutano wenu wa jana wakati ukimpa ile sumu na laki mbili baada ya kumtisha sana. Nilisubiri hadi ulipokuwa umeondoka na binti huyu amelala ndipo niliingia na kuichukua poda ile ya hatari na badala yake nikaweka hiyo ya kawaida ambayo nilinunua kutoka katika duka la jirani".

Joram akamgeukia Nuru, "Laki mbili zako pia nilizichukua mimi. Ninavyomfahamu huyu nilijua alikuwa akisubiri usafiri pamoja na viongozi kisha arudi hapa na kuzichukua pesa zake. Hivyo, nimezihifadhi mahala ili baada ya shughuli hii iliyobaki uje uzichukue. Ni haki yako kabisa Nuru kwa usumbufu aliokufanyia", Joram akamgeukia Proper.

"Wewe mshinzi pengine utafurahi kusikia kuwa sumu yako iko katika mikono ya vyombo vya usalama yaani polisi. Niliipeleka huko ili ichunguzwe. Baada ya uchunguzi ikijulikana nchi na kiwanda gani kinatengeneza sumu hatari kama hiyo, suala hili litapelekwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Lazima anayehusika kutengenezwa kwa sumu hiyo aadhibiwe vikali. Wakati huu ambao viongozi wa Baraza la kutunga sheria la Umoja huo wanafanya kila
 
SEHEMU YA MWISHO

COUNT-DOWN PART 2


juhudi kupunguza utengenezaji wa silaha za hatari lakini kiwanda hicho bado kinatengeneza sumu hatari kama uliyokuwa nayo wewe, kazi unayo ndugu", alisema Joram.

Joram alisita kidogo akatoa sigara nyingine akaiwasha. Macho yake yalikuwa yakimtazama Proper kwa umakini wa hali ya juu. Tabasamu lilikuwa limetoweka na hasira kali kupokonya nafasi yake. Hata hivyo, Joram akaongea kwa utulivu, "Dunia haijapata kumwona mwendawazimu mshenzi kama wewe. mtu mwenye roho chafu zaidi ya mnyama. Ni ajabu kuwa huna mkia. Unyama wako umewazidi akina Adolf Hitler na Musoline. Umewazidi hata Nduli Iddy Amin wa Uganda na Bokasa. Hata Voster na Smith hawakufikii. kwa kweli ulistahili kufikishwa mahakamani ili dunia nzima ikuone. Inspekta Kombora na wasaidizi wake watafika hapa baada ya dakika chache. Watapenda kukuchukua mzima na kukufikisha mahakamani. Lakini nimelazimika kuwachelewesha kidogo ili wakifika hapa waikute maiti yako. Ni jukumu lao wao wenyewe kuamua kama watakutupa maiti yako vichochoroni iliwe na mbwa koko au kuifikisha mahakamani. Lakini lazima waikute maiti yako. Niliahidi nitakuua kwa mkono wangu mwenyewe ili kulipa kisasi kwa wote uliowaua kikatili, hasa mpenzi wangu Neema Iddy".

Proper alianza kutetemeka kidogo, hofu ikamwingia. Ni rahisi sana kuua mtu. Lakini si rahisi kuuawa huku ukitazama. Akailaani bahati yake kwa kutochukua silaha yoyote siku hiyo. Kwa kweli alikuwa hazihitaji. Aliamini marais wangekufa kwa sumu. Na mwishowe binti huyo angekufa kwa mikono mitupu. kidole chake kimoja kingetosha kumwua.

Joram akamgeukia Nuru. "Bibie. Tafadhali toka nje ili nimalize kazi hii. Sipendi ushuhudie mwendawazimu huyu anavyokufa. Kesho jioni utapokea furushi lenye pesa zako zote. Mimi nitakuwa nimeondoka kurejea Dar es Salaam. Hivyo nadhani hii ni kwa heri ya kuonana".

Nuru hakuinuka. Alikuwa akimtazama Joram kama mtu atazamaye mchezo wa kuigiza katika sinema. Yawezekana huu ukawa mwisho? Mwisho wa ndoto zake zote juu ya Duncan ambaye ametokea kuwa Joram Kiango? Joram ambaye alizisikia sifa zake mara nyingi na kumhusudu kupindukia?
 
SEHEMU YA MWISHO

Asingependa uwe mwisho. Asingekubali. Mara akaangua kilio. Hakujua kinachomliza.

"Nuru", Joram alitamka kwa mshangao.

Mtutu wa bunduki yenye nguvu ulikuwa ukiwachungulia kutoka nje kupitia dirishani. Bastola ilikuwa mikononi mwa mtu aliyeufunika uso wake kwa tambara jeusi. Bastola hiyo ilimwelekea Proper. Lakini ingeweza kumpata Joram vizuri zaidi. Aliyeshika bastola hiyo alisikitika kwa kuwa hakuwa amepewa amri ya kumwua Joram. La sivyo, ingekuwa kazi ndogo sana kwake. Hakujua lini ingetokea tena nafasi nyingine nzuri kama hii. Akailekeza vizuri katika paji la uso wa Proper.

*************

VII
"Nuru"... Joram alikuwa akisema tena wakati mlio wa kawaida ulipolipuka chumbani humo. Joram alijirusha chini akampitia Nuru na kuanguka nae sakafuni. Bastola yake ikaelekea mlangoni! Usingizi ambao hakuutegemea ulimpitia papo hapo.

Dakika chache baadaye alizinduka. Alishangaa kujiona akiwa kamkumbatia Nuru kama walivyoanguka. Alipotupa macho katika kiti alichokuwa amekalia Proper alishangaa kuona kitu kama uji ulichanganywa na damu nzito. Baada ya kutazama kwa makini ndipo alipofahamu ni kipi alichokuwa akikishuhudia. Ulikuwa ubongo wa binadamu uliotoka katika kichwa cha binadamu kilichofumuliwa kwa risasi. Yeyote aliyefyatua risasi hiyo alikuwa ameifanya kazi yake kikamilifu. Na hakusahau kuuchukua wa aliyekuwa Proper. Kwanini hakuuchukua ubongo wake pia? Joram alijiuliza. Au waliuacha ili uwe ushahidi kuwa adui yake amekufa? Hakuona kama ingemsaidia. Alikuwa ameapa angemuua kwa mkono wake. Yeyote angemuua alikuwa amemsaliti.

Hasira mpya zikampanda Joram. Akainua bastola yake na kuielekeza katika kifua chake. Akafumba macho. akajiuliza, kwanini apokonywe kazi kulipa kisasi kwa kumuua Proper, mtu aliyemuua mpenzi wake Neema.

"Joram", sauti ndogo ya kike ikapenya masikioni mwake ikimwonya.

Akafumbua macho na kukutana na macho ya Nuru, yenya machozi na huzuni, ambayo yalikuwa yakimtazama kwa namna ya kusihi na kumbembeleza kama yanavyosema. "Huwezi kufanya hivyo", Ingawa kwa mdomo hakusema lolote, Joram akajua kuwa asingeweza kujiua. Hakuwa mtu wa kujiua. Akaitupa bastola hiyo chini na kuinuka akitoka zake nje.

"Joram", Nuru aliita akimfuata.

"Unataka nini zaidi?".

Nuru alipomfikia alimshika mkono na kumwambia, "Huwezi kuondoka katika hali hiyo Joram. Nataka nikusaidie kukufariji umsahau Neema. Niko tayari kufanya chochote na kupoteza kila kitu mradi uusahau msiba wa ulionao moyoni. Tafadhali nipokee Joram".

Ilikuwa sauti ile ile ya Nuru. Sauti isiyoweza kupingika. Na alimtazama kwa macho yale yale laini yanayosihi na kubembeleza. Macho ambayo hayangepuuzwa. Nuru alisema huku vidole vyake laini vikiuchezea mkono wa Joram katika hali inayoshawishi na kuchokoza kwa kiwango kisichostahimilika. Umbo lake lilikuwa lile lie lenye kila chemaambacho macho ya binadamu hustarehe kutazama na mikono ikiburudika kuligusa.

"Ndiyo, Joram ni shujaa. Lakini nani aliyesema kuwa ana moyo wa chuma?

TAMATI


BURE SERIES
 
TUPIA COMMENT YAKO, TUANZE NA SIMULIZI IPI... SIMULIZI IKICHAGULIWA MARA 5 TUNAANZA NAYO.

KIGUU NA NJIA ✅

SALAMU KUTOKA KUZIMU✅

MIKONONI MWA NUNDA✅

MALAIKA WA SHETANI

MTAMBO WA MAUTI

ZAWADI YA USHINDI

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

NAJISIKIA KUUA TENA

ROHO YA PAKA

NOTI BANDIA
 
TUPIA COMMENT YAKO, TUANZE NA SIMULIZI IPI... SIMULIZI IKICHAGULIWA MARA 5 TUNAANZA NAYO.

KIGUU NA NJIA ✅

SALAMU KUTOKA KUZIMU✅

MIKONONI MWA NUNDA✅

MALAIKA WA SHETANI

MTAMBO WA MAUTI

ZAWADI YA USHINDI

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

NAJISIKIA KUUA TENA

ROHO YA PAKA

NOTI BANDIA
Jamani tuchagueni hii NOTI BANDIA.. fanyeni hivyo ndugu zangu watu jamani chagueni hii jamani walahi walahi..😅
 
Back
Top Bottom