Simulizi ya Kijasusi: Salamu Kutoka Kuzimu

Simulizi ya Kijasusi: Salamu Kutoka Kuzimu

SEHEMU YA 47


Alijikuta akiingiwa na wasiwasi. Alikuwa peke yake, katikati ya kiza katika eneo ambalo mchana huo lilikuwa la maafa. Akawaza kurudi, lakini alijikongoja hadi alipofika kando ya vifusi vya jumba hilo. Alitupa macho kila upande, hakuonana dalili yoyote ya mlinzi. Baada ya mizunguko kadhaa, aliamini kuwa sehemu hiyo haikuwa ikilindwa. Akasononeka moyoni.

Mara likamjia wazo jingine. Yawezekana katika jumba hili mlikuwa na vitu vya thamani ambavyo angevichukua na kuviuza! Wazo hili likamtuma Unono kuanza kuchungulia, akashika kile na kujipenyeza pale. Alipata mwanya ambao ulimwingiza ndani ya kifusi hicho. Mikono yake iliendelea kupeleleza kwa makini, macho yakifanya juhudi kutazama.

Ghafla Unono aligusa kitu ambacho kilimshitua. Kitu chenye dalili ya uhai. Nyoka? alijiuliza baada ya kuutoa haraka mkono wake. Baada ya kutulia kwa makini, aligundua kuwa alichogusa ni mwili wa binadamu. Ugunduzi wake ulimshitua zaidi. Maiti nyingine! aliwaza akiinuka na kuanza kuondoka.


Kisha ushujaa ukamwingia na kumfanya ahairishe safari yake na kuuinamia mwili huo kwa uchunguzi zaidi.


Inspekta Kombora alikuwa mgonjwa mahututi, ingawa hakuwa tayari kumweleza daktari wake kuhusu kuumwa kwake wala hakutaka kujieleza mwenyewe ni maradhi gani yanamsumbua. Alijiona tu yu hoi bin taaban, hali ambayo ilimtokea ghafla baada ya kuviona vile vipande vya mwili wa binadamu vilivyotawanywa kwa bomu. Lakini kilichomuuguza zaidi ni kuokotwa zile ndevu za bandia alizokuwa amevaa Joram Kiango.

Joram kafa! lilikuwa wazo lililomtesa zaidi ya ukweli Inspekta Kombora. Joram ambaye jina lake lilikuwa tishio kwa waovu wote wenye nia mbaya kwa nchi na wananchi wake! Joram ambaye alikubali kuiweka roho yake hatarini mara kwa mara kwa lengo la kuwakabiri maadui wenye nguvu na uwezo wa kutisha! Joram, kijana mwenye moyo wa jiwe na mwili wa chuma! Joram amekufa?...

Miaka mingi ilikuwa imepita, kiasi kwamba Inspekta Kombora hakumbuki siku gani aliyotokwa na machozi. Leo hii, akiwa peke yake ofidini, akiitazama meza yake, alihisi chozi likipenya kwenye vipingamizi vyote na kuelea juu ya
 
SEHEMU YA 48

mashavu yake, jambo ambalo lilimshangaza zaidi. Mshangao ambao ulimezwa na hasira kali za ghafla. Akaupiga mkono wake mezani kwa nguvu nyingi na kuvifanya vifaa kadhaa vilivyokuwa mezani hapo vidondoke sakafuni. Hakujishughulisha kuviokota.

"Joeam kafa!... aliendelea kuwaza kwa machungu.

Mara swali la kutisha likamjia akilini, Ataitangazia nini dunia iliyoamini kuwa Joram alikufa siku nyingi, atasema nini badala ya ule uongo wa kifo kilichosababishwa na sumu. Dunia ingemwelewa vipi mzee huyu mwenye dhamana kubwa serikalini.

Halafu akajikuta akitetemeka ghafla lilipomjia swali la kutisha zaidi. Nani hawa wauaji na wanakusudia kufanya nini? Kwamba, hawa si adui wa mzaha, Hakuwa na shaka na swali lake hilo. Yeyote aliyehusika kumwua Joram na hasa aliyemwua kikatili kiasi kile, hawezi kuwa mtu wa mzaha hata chembe. Wala hakuwa mtu anayecheza isipokuwa aliyedhamiria kufanya jambo baya mno ambalo hakutaka Joram Kiango aliingilie kama walivyofanya majuzi kwa kuwavunja uti wa mgongo wale waroho waliokuwa katika hatua za mwisho za kupindua nchi na kuiuza kwa mabepari. Hawa ambao wameshawishika kumwua Joram kwa bei yoyote ile wanakusudia kufanya nini?.

Ilimuumiza zaidi kujiona yeye kama mkuu wa usalama akae kimya wakati akijua kuwa kuna uovu uliojificha kando ukinyemelea, wakati huo huo akiwa hajui ni uovu gani na utatokea upande gani. Alikuwa amekwisha fanya mengi. Tangu jana wakati akitazama mabaki ya marehemu wakati yakikusanywa, alikwisha chukua hatua zote za upelelezi dhidi ya mauaji hayo. Kikosi cha askari kilikwisha teuliwa kitambo, kikifuatilia kila kichochoro ambacho kingeweza kuwafikisha mbele ya adui, Maswali mengi pia yalikuwa yakiulizwa. Lakini yawezekana kabisa maswali hayo yangeweza kuulizwa kwa miaka bila majibu kupatikana. Mtu pekee ambaye ama alikuwa na jibu tayari, ama angeweza kulipata mapema zaidi, sasa alikuwa marehemu.

Hata hivyo afanye nini? Aendelee kusubiri mtu au watu hawa wafanye yote waliyokusudia wakati yeye akiendelea kustarehe juu ya kiti hiki kama Ofisa wa Polisi alijiuliza. Afanye nini kuongeza nguvu ya mkono kuwatafuta maadui
 
SEHEMU YA 49

hao? Nani anaweza kuwa na walau fununu ya kinachotokea?.

Ni katika kujiuliza maswali hayo alipomkumbuka Katibu Mahsusi ya Joram Kiango, yule msichana mzuri, Neema Iddy. Akajilaumu kwa uamzi wake wa kumpinga msaidizi wake mmoja ambaye alipendekeza Neema aletwe ili amthibitishie marehemu.

"Ataonyeshwa nini? Huone kama tunaweza kumpata msichana wa watu ndoto za kutisha katika maisha yake yote au hata wazimu kwa kumuonyesha haya mabaki ya mtu aliyekuwa mwenzi na mpenzi wake?". Kombora alikuwa amemjibu hivyo askari huyo. "Hapana", aliongeza. "Mwacheni".

Zaidi ya hayo, nadhani mnakumbuka kuwa hii ni siri ya watu wachache sana, watakaowajibika kufahamu aliyefariki ni Joram Kiango. Wengine wote lazima waendelee kuamini kuwa alifariki ghafla kabla ya kifo hiki.

"Sasa aliuona umuhimu mkubwa wa kumuona Neema. Hivyo bila ya kuaga wapi aendako, alipanda gari na kuielekeza iliko ofisi ya Joram.

Aliikuta ofisi hii imefungwa. Akajielekeza Temeke, ambako alifahamu jina, mtaa na namba ya nyumba ya Neema.

******************************

Ilikuwa siku ndefu kwa Neema Iddy. Ingawa kila siku ni kama siku nyingine lakini siku hii aliiona hivyo kutokana na ile harara kubwa iliyomkaria rohoni ikimtia shauku ya kumwona Joram Kiango na kutaka kufahamu hicho alichokuwa akikishughulikia safari hii, hata akaweza kujibadili na kuwa mkongwe kiasi kile, na kutangazwa uongo kuwa amekufa. Neema alihisi kuwa mkasa huu bila shaka ni wa kutisha na wa hatari kuliko yote iliyotangulia, au sivyo, Joram asingechukua hashari kiasi kile, wala polisi wasingeafiki kutangaza uongo. Ilimsikitisha Neema alipomkumbuka Joram alivyomnyima siri hiyo kwa madai ya kwamba, ni "Hatari" kumhusisha.

Siku ya jana nzima, Neema alikuwa ameshinda katika hali hiyo. Akihesabu dakika na masaa, akisubiri wakati ambao ingetanagzwa upya redioni: "Joram yu hai... Na amesababisha kukamatwa kwa wahujumu ambao..." Ni hapo alipokuwa akiishia Neema. Na ni swali hilo ambalo lilikuwa likimweka roho juu. Hamu ya kujua safari hii adui ni nani na walikusudia kufanya nini.

Neema alitabasamu, akakumbuka sifa ambayo Joram aliipata kwa
 
SEHEMU YA 50

kusuluhisha mambo magumu magumu. Mara hii, akawaza atailetea nchi yake gani? Wazo kuwa angetokea mtu, amshinde Joram, hasa baada ya kutangazwa kuwa amekufa, kama walivyotaka wao, swali hili halikuwa na nafasi katika fikra za Neema. Akawa mtu ambaye anasikia sifa za wapelelezi hodari duniani, pamoja na kusoma hadithi za kubuni juu ya upelelezi, Bado Neema alikuwa hakumbuki kama alikwisha tokea yeyote mwingine ambaye alikuwa na mtindo wa aina ya Joram Kiango. Mtu asiyeogopa wala kutishiwa, mtu asiyekata tamaa, mtu anayejua kila anachofanya! Neema alihisi furaha na faraja kubwa kuona kuwa yeye ni msichana pekee ambaye amepata fursa ya kushirikiana na mtu huyu shujaa. Hadhi iliyoje!.

Ni mawazo hayo yaliyokuwa yakimfanya Neema atabasamu. Lakini alihitahidi kuificha tabasamu hilo kwa huzuni ya uongo kila alipotokea mtu wa kumpa pole kwa kifo cha 'mwajiri' wake. Ilikuwa ni wajibu wake kujifanya yumo katika msiba.

"AMekufa kijana yule mzuri? Siamini" angesema kijana mmoja. Neema bila ya kumtazama ya kumtazama usoni angemjibu kwa masikitiko.

"Amekufa... ndiyo hali ya dunia.

Kifo cha ghafla! Wamempa sumu.

"Haijajulikana".

"Ama kweli ndege mjanja hunasa kwenye tundu bovu".

Angeondoka huyo, aje mwingine. Kila mmoja alisema hili au lile.

Neema aliwasikiliza wote na kuwafanya waondoke wakiwa wameamini kile ambacho hawakutaka kukiamini, kuwa Joram Kiango amefariki.

Neema akiwa katika hali hiyo, tabasamu rohoni, huzuni moyoni, alisikia gari likisimama mlangoni mwao na baadaye mlango wa chumba chake ukagongwa. Aliingia Inspekta Mkwaju Kombora.

Macho ya Inspekta Kombora yalimfanya Neema ahisi jambo mara moja kuwa hakukuwa na habari njema. Neema akiwa si mgeni kwa Inspekta Kombora baada ya kuzungumza naye mara kwa mara kuhusu harakati na mipango ya Joram, Neema alimjua Inspekta huyu vizuri, alifahamu wakati gani yuko katika hali mbaya kimawazo na wakati gani anajisingizia hali mbaya. Leo ilikuwa dhahiri kuwa kuna kitu kikubwa kimemkaria rohoni.

"Kuna nini Inspekta?", Neema alihoji baada ya kumaribisha kiti.

"Joram amekufa!" Inspekta Kombora alimwambia.
 
SEHEMU YA 51

"Najua", Neema alijibu kwa tabasamu.

"Nadhani bado hujanielewa. A-me-ku-fa", alisisitiza,

Kidogo Neema akashangaa. "Ndiyo mzee! Nadhani hata wewe unajua. Imebidi ujifanye hivyo kwa ajili ya watu hawa ambao wanamtafuta Joram. Muda si mrefu atafufuka na jambo ambalo naamini litakusisimua Inspekta".

Kombora akamkatisha kwa kumweleza kuhusu tukio zima la bomu lililosababisha kutawanyika kwa viungo vya marehemu. "Nimeona nitakutia katika msiba na simanzi iwapo nitakuonyesha mabaki hayo ya Joram. Ama kweli kilikuwa kifo cha kusikitisha sana dada yangu. Sikuona kama ungestahili kumwona mtu uliyempenda sana akiwa katika hali kama ile".

Ndipo Neema alipopata ukweli wa mambo ulivyo. Aliduwaa kwa muda, Macho kayatoa akimtazama Kombora wakati hamuoni. Neema alihisi damu yake imesimama kabisa na fikra kukwama. Joram kufa! Fahamu zilipomrejea, alinong'ona maneno fulani ambayo Kombora hakuyasikia. Kisha akaondoka mbio hadi chumbani kwake. Alifunua mto na kutoa bastola yake ndogo aliyozawadiwa na Joram katika moja ya sherehe zake za kuzaliwa. Akaishika imara na kuitingisha huku akipiga kelele: "Nitamwua yeyote aliyekuua Joram..." alifoka Neema, lakini sauti ilitoka ikinong'ona hata isiyafikie masikio yake mwenyewe. Alipokumbuka kuwa alikuwa hamjui mwuaji huyo, aliirejesha silaha hiy katika maficho yake ya siri na kubaki ameduwaa katikati ya chumba chake. Kisha akarejea ukumbini na kuketi chini.

"Samahani Inspekta", Neema alisema polepole, "Kwa muda mrefu sijapata habari mbaya ya kuumiza kama hii",

"Si habari ya kupendeza hata kidogo. Mimi pia imenitia homa. Pole sana".

Baada ya kutafakari kwa muda, Inspekta Kombora akayarejesha maongezi yake kikazi. Alimsihi Neema kumweleza chochote anachofahamu ambacho kingeweza kupatikana kwa mwuaji au wauaji hao mapema iwezekanavyo. Hata hivyo Inspekta Kombora alivunjika moyo baada ya kugundua kuwa Neema hajui lolote la maana. Hivyo akaondoka kimya kimya kurejea ofisini kwake baada ya kumkumbusha Neema kuwa kifo cha Joram kiendelee kuaminika kuwa alifariki ghafla kwa maradhi ambayo hayajafahamika.

Neema alibaki katika hali ile ile ya butwaa, moyo ukiwa kama uliokufa ganzi
 
SEHEMU YA 52

na ubongo kudumaa. Alihisi kama mtu aliyefika ukingoni katika safari yake ya maisha. Kwake Joram alikuwa kila kitu. Alikuwa furaha na faraja katika maisha yake, heri na neema yake. Hakuona vipi angeweza kuyahimili maisha bila tabasam la Koram mbele yake. Hakujua vipi ataweza kusisimukwa bila harakati za Joram dhidi ya adui zake.

Mapenzi ya Neema na Joram hayakuwa yale ya kimwili kati ya msichana na mvulana. Lakini Neema aliyaona kuwa ni makubwa zaidi ya uhusiano wa aina hiyo. Makubwa yaliyojengeka katika misingi mikubwa zaidi. Ni kweli kuwa zipo nyakati ambazo Neema alijikuta akimhitaji Joram kimwili kwa tamaa kali kuliko alivyowahi kuhitaji kitu chochote. Siku kama hizo alikesha kitandani akisali kuomba Joram atokee, amkumbatie. Ni kweli pia kuwa kuna siku ambazo aliwahi kuona tamaa hiyo ikiwaka katika macho ya Joram kwa nguvu kiasi kwamba ilitokea kama mwujiza alipofaulu kutotamka kile ambacho alitamani kukitamka. Kitu ambacho jibu la Neema lisingekuwa zaidi. "Sawa tu".

Wote walifanikiwa kuzitawala nafsi zao. Kama alivyowahi kusema Joram: "Akili isipoutawala mwili ni sawa na gari kuacha barabara na matokeo yake hakuna asiyefahamu", Joram! ambaye sasa ni marehemu!

Bado haikukubalika kichwani mwa Neema kuwa Joram amekufa. Ilimrudia akilini siku ile ambayo alimwona Joram kwa mara ya kwanza.

Wakati huo Neema akiwa mwandishi wa habari katika gazeti moja hapa nchini. Siku hiyo alipata barua kutoka kwa mtu asiyejulikana, ikimdokeza kuwa mtu mmoja mkubwa serikalini alikuwa amehusishwa katika mauaji ya watu watatu ambao maitiza zao ziliokotwa huko Manzese. Habari hii ilikuwa imeishitua sana nchi. Neema akiwa mwandishi anayependa kuripoti habari kubwa kama hii, aliamua kwenda kutafuta ukweli na kuandika habari hii kwa undani ili kuligusa kila jicho la msomaji.

Ilibidi Neema ajifanye kuwa mwanamke kahaba ili aweze kuingia ndani ya jumba la kigogo huyo. Huko ndani Neema alifanya kila mbinu hadi kuteka mawazo ya mtumishi wa mkubwa huyo wa serikali, ambaye bila kufahamu
 
SEHEMU YA 53

aliweza kueleza habari zote za siri zinazofanywa na kigogo huyo. Neema alipofanikiwa kuujua udani wa mauaji hayo alitumia mlango wa uwani kutoka katika jumba hilo na kurejea ofisini kuwahi nafasi katika gazeti la kesho. Lakini hakuweza kufika mbali baada ya kujikuta akiwa katikati ya watu wanne wenye bastola ambao walimpiga na kitako kichwani Neema akapoteza fahamu. Fahamu zilipomrejea alijikuta yuko baharini, katika jahazi, mmoja wa majambazi hao akiwa amemshika kichwani na mwingine miguuni wakijiandaa wakijiandaa kumtosa majini. Alilia kwa nguvu zake zote lakini majambazi hayakuonyesha dalili yoyote ya kumuonea huruma. Mmoja wao alikuwa akisema kwa kebehi.

"Kamlilie mama aliyekuzaa na hao bwana zako waliokutuma kuchunguza mambo yasiyokuhusu".

"Sikieni, mimi si mpelelezi..." alijaribu kusema. hakuna aliyemsikia. Wakamwinua juu na kumchezesha bembea ili wamtupe kwa urahisi. Neema alikoma kulia. Badala yake akayafumba macho yake akisubiri kifo. Ni hapo lilipotokea jambo ambalo hakuna aliyelitegemea. Mtu aliibuka ghafla kutoka mahali fulani katika jahazi hilo na kuwashambulia watu hao kwa mtindo wa upiganaji ambao Neema aliwahi kuuona katika michezo ya sinema tu. Dakika chache baadaye maadui wote walikuwa wamelala chini wakigalagala kwa maumivu. Mtu huyo alimwunua Neema na kuanza kumkumbatia huku akimtazama kwa tabasamu.

"Pole sana mpenzi", alitamka mtu huyo baada ya kuona mshangao hauyaachi macho ya Neema.

"Umeyaokoa maisha yangu... Asante sana", Neema alisema kwa sauti ya unyenyekevu. "U nani wewe?".

"Naitwa Joram Kiango".

"Joram!", Neema alifoka kwa mshangao. Alikuwa amepata kusikia jina jilo likihusishwa sana katika kuwakabiri majambazi, wahaini na wahalifu wengine. Alikuwa amelisoma mara kadhaa magazetini. Lakini hakupata kumtia machoni. Ndio kwanza akaona hawakukosea sana wale walioandika kuwa yu kijana mzuri. Walichosahau ni kutoweka neno 'sana' katika sifa zake. Kwa keli Neema hakutegemea kama mtu mwenye tabia zile za kupambana na maadui wengi ana kwa ana bila hofu angeweza kuwa hivi; mzuri sana, mtaratibu sana, macho yenye upole, sauti... "Joram Kiango!" akaita tena. "Umeniokoa lakini sijui namna ya kukushukuru".
 
SEHEMU YA 54


"Huna haja", Joram alimjibu. "Ni mimi mwenye haki ya kukushukuru. Siku zote nilimshuku mkubwa yule kuhusika katika yale mauaji lakini sikuwa na ushahidi wa kutosha. Wewe umefanya kazi nzuri Neema. Umeniwezesha kupata ushahidi mzuri. Hawa wauaji watasema ukweli watakapofika mahakamani..."

"Ni wewe uliyeandika ile barua?", Neema aliropoka ghafla.

"Ndio", Joram alijibu baada ya kutabasamu. Nadhani utaniwia radhi kwa kukufanya chambo. Nilikufahamu siku nyingi na kujua kuwa u msichana shujaa. Nilijua kuwa ungefanya vizuri, na umefanya vizuri... vitu vyote viwili ambavyo nilivihitaji unavyo, ushujaa na uzuri..."

Neema alijikuta akimkumbatia Joram. Walitulia kwa muda na tena kwa faraja. walipoachana Joram aliiwasha mashine ya jahazi na kuiendesha hadi pwani ya bahari ambapo aliwakabidhi majambazi hao kwa polisi. Siku chache baadaye mahakama ilitoa adhabu kali kwa 'mkubwa' huyo kitanzi na majamazi kufungwa kifungo cha maisha jela. Neema alipotoka mahakamani alimsaka Joram bila mafanikio. Ilikuwa baada ya wiki kadhaa walipokutana bila kutegemea. Hawakutengana tena.

Na sasa Joram amekufa, Neema aliwaza. "Yeyote aliyemwua nitahakikisha anamfuata", Neema alifoka kimya kimya. "Naapa".

Usiku ulipoingia ulimkuta Neema akiwa bado kaduwaa pale pale alipokuwa. Alikuwa hajatia chochote mdomoni ingawa jirani zake walimfuata mara kadhaa wakimshawishi kula. Aliinuka na kuwasha taa ya umeme. Wakati wa kulala ulipowadia, alijilaza kitandani kama kawaida na kuyafumba macho yake, lakini usingizi haukumjia. Hadi asubuhi alikuwa hajatongoa walao lepe.

Kisha mlango uligongwa na kufunguliwa polepole. Neema alikuwa amesahau kuufunga kutokana na kuzongwa na mawazo. Aliyeingia ni mtu ambaye Neema hakupata kumwona katika maisha yake yote. Mtu huyu aliyarejesha mawazo ya Neema katika ulimwengu wa kawaida, Dunia ya mtu kushutuka, kushangaa, kucheka na kukasirika. Mtu huyu angeweza kumfanya yeyote amtazamaye afanye lolote kati ya hayo. Lakini Neema alishangaa tu.

Hiyo ilitokana na umbo la mtu huyo. Neema alifahamu kuwa yu mwanamke kutokana na mavazi na matiti yake manene, ambayo badala ya kukaa kama ilivyo kawaida ya matiti katika kifua cha mwanamke haya yalikuwa kama
 
SEHEMU YA 55

matuta yaliyolimwa shambani pasi na mpangilio maalumu. Sura yake haikuwa na chochote kinachofaa kuitwa 'uzuri' Macho yake hayakupendeza kutazamwa! Pua lake! Midomo!... Neema akajikuta anatokwa na mshangao na kujikuta akiingiwa na mshituko. "Mwenzetu huyu kweli aliumbika", Neema akajisemea.

"Naitwa Unono", mgeni alianza kujieleza akisimama kando ya kitanda. Hakujishughulisha kujaribu kutabasamu. Wala Neema hakuona kitu kinachoitwa tabasamu kiliwahi kuupitia uso huo, Wala hakuona kama tabasamu lingewezekana kwa hali ipi. "Wewe ndiye Neema Iddy?", aliuliza.

"Ndiyo", Neema alijibu.

"Unamfahamu Joram Kiango?".

Neema alibadilika na kuonekana mnyonge zaidi. "Wewe ni nani?", Neema akahoji. Unono hakujishughulisha kujibu. Badala yake akasukuma swali lingine.

"Unajua kuwa Joram amekufa?".

"Na... Najua. Wewe ni nani? Neema aliendelea kuhoji.

"Huna haja ya kunifahamu. Naona dhahiri kuwa u mpenzi wake. Au siyo?" Neema alipochelewa kujibu Unono akaendelea, "Unampenda kweli?"

Mbali na ubaya wa sauti ya mwanamke huyu, na ubaya wa macho yake. Neema aliona kitu kingine pia. Naam, aliona wivu. Naam, mkabala wa mwanamke huyu ulionyesha hisia fulani, wivu. Mwanamke huyu wa ajabu anamwonea wivu kwa Joram Kiango.

|Ni mpenzi wangu", Neema akajikuta akifoka. "Ndiyo nampenda. Hata kwa kifo chake nitaendelea kumpenda. Wewe u nani na unahusika vipi baina yangu na mwandani wangu?".

Unono hakujibu upesi. Aliutia mkono kifuani mwake na kuutoa ukiwa umeshika picha ndogo. "Kama kweli unampenda. Kama kweli utaendelea kumpenda, jitahidi umjue huyu ni nani, na anaishi wapi ili leo jioni nikija hapa uniambie wapi anapatikana".

"Umepata wapi picha hii?" Neema aliuliza baada ya kuipokea na kuitazama kidogo, "Na picha hii inahusikaje na kifo cha Joram?".

"Inahusika... Niliipata kwenye mifuko ya marehemu dakika chache baada ya kifo chake . Naamini mwenye picha hii anahusika. Pata maelezo kamili ya picha hiyo. Nikirudi hapa nitakueleza nini zaidi cha kufanya. "Baada ya maelezo hayo Unono aligeuka na kuanza kuondoka zake kwa mwendo wa kuchekesha.

Neema aliitazama tena picha hiyo. Ilikuwa sura ya mwanaume mwenye dalili
 
SEHEMU YA 56

ya heri kimaisha na kimadaraka. Lakini picha hii ilionekana kama muhusika hakujiandaa kupigwa picha hiyo. Ilikuwa sura ambayo haikuonekana ngeni sana machoni mwa Neema. "Huyu anahusika vipi na kifo cha Joram?", Neema alijiuliza. Na mwanamke yule, Unono analijua asemalo? Akajiuliza kwanza amewezaje kumpata yeye (Neema) kirahisi hivyo katika jiji kubwa kama hili? Lazima kuna jambo hapa. Mawazo haya yakamfanya Neema aamue kufuata maelekezo ya Unono. Kwa kuwa alikuwa bado msichana tena aliyepitia taaluma ya uandishi wa habari, alifahamu wapi angeweza kupata habari za mtu huyu.

Muda mfupi baadaye Neema alikuwa njiani akielekea kituo cha mabasi. Alipanda UDA ambalo lilimfikisha mjini, Akatelemka na kuiendea ofisi yake ya awali, katika shirika moja la habari. Baada ya kupewa pole nyingi na rafiki zake kufuatia kifo cha Joram, aliomba ruhusa ya kutumia maktaba ya picha. Humo alitafuta picha ambayo inafanana na ile aliyokuwa nayo mikononi. Hakuipata, Alipokaribia kukata tamaa akawauliza wengine kijanja kama wanamfahamu mtu huyo.

Mtu wa kwanza kuitazama picha hiyo alicheka na kisha kumtazama Neema kwa mshangao. "Umeipata wapi picha hii Neema?".

"Unamfahamu?", Neema aliuliza kwa msisitizo akiwa na matumaini.

"Wewe Neema, yaani humfahamu huyu?" Alijibiwa kwa swali lingine. "Huyu siyo Profesa Kimara? Karibu kila mtu anamfahamu".

"Kimara yupi?".

"Chain Kimara. Yule Profesa ambaye anaandika kitabu juu ya uwezekano kuifanya mimea aina ya wanga inayolimwa hapa nchini iweze kukua na kukomaa haraka katika kipindi cha nusu ya muda wake wa kawaida. Huwa anakuja hapa ofisini mara kwa mara kueleza jinsi anavyoendelea na utafiti wake",

Ilikuwa habari njema kwa Neema, Anapatikana wapi?", aliuliza Neema.

"Nani anajua?" alijibiwa. Kwani unamhitaji kwa ajili gani Neema?"

Neema alijitahidi kumlaghai alivyoweza. Kisha akachukua kitabu cha orodha za simu na kulitafuta jina la Profesa Kimara. Haikumchukua muda kulipata, Anuani ilionyesha kuwa anapatikana katika mtaa wa India katika nyumba za msajili wa majumba namba 107. Taarifa hizo Neema akazinakiri nyuma ya picha hiyo na kisha kuanza safari ya kutoka akimshukuru mkutubi. Moyoni Neema alijaa furaha. Ilikuwa rahisi kuliko alivyotegemea.

ITAENDELEA
 
Back
Top Bottom